Thursday, August 6, 2020

NANENANE DODOMA KUANZISHA MAONESHO YA KIMATAIFA YA UTALII WA MIFUGO

 

Mwakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma  kwenye  Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati, ambaye  pia ni  Mkuu ya Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athuman Mukunda akijaribu  kuendesha Trekta kwenye maonesho hayo  leo, aliye pembeni yake ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel,  walio chini  mwenye miwani ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Injinia Jackson Masaka wakishuhudia tukio hilo. Picha na John Mapepele
Mfugaji wa Mifugo Juma Seleman kutoka  Mpwapwa akipitisha Ng’ombe wake  Mashindano maalum ya Paredi ya mifugo iliyofanyika kwenye maonesho ya nanenane kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Picha na John Mapepele
Viongozi kutoka Mkoa wa Dodoma na Singida  pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwenye picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa  mashindano maalum ya Paredi ya mifugo iliyofanyika kwenye maonesho ya nanenane kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma. Picha na John Mapepele
Wawakilishi wa Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma  kwenye  Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati,ambaye ni  Mkuu ya Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi  Athuman Mukunda(mwenye kilemba) akimuuliza maswali muoneshaji wa kampuni la uzalishaji wa chakula cha mifugo ya Harsho Group, Juma Ally (mwenye Tisheti ya Njano) Kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Anjelina Lutambi. Picha na John Mapepele

Na John mapepele, Dodoma

Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Singida wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii  kuyafanya mashindano maalum ya Paredi ya Mifugo yanayofanyika kila mwaka kwenye  kanda ya kati kwenye viwanja vya Nzuguni  jijini Dodoma kuwa Maonesho ya Kimataifa  ya utalii wa mifugo ili kuongeza pato la taifa na kuleta hamasa kwa wananchi kushiriki.

Katika hotuba iliyotolewa kwenye Paredi la Mifugo leo na Mkuu ya Wilaya ya Bahi Mwanahamisi  Athuman Mukunda kwa niaba ya Wakuu hao wa Mikoa, amesema Tanzania imebarikiwa kuwa nchi ya pili  kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika  hiyo uanzishaji uboreshaji wa Paredi  la mifugo utasaidia  kuinua uchumi wa taifa kwa kuongeza  kipato kutoka kwa watalii  kupitia mifugo.

Ameongeza kuwa jiografia ya Dodoma kuwa katika ya nchi na  hali ya hewa nzuri ya majira ya mwezi Agosti katika eneo la Nzuguni  linafanya watalii wengi kuja kutembelea maonesho hayo.

“Ndugu zangu  niwaambie ukweli  katika nchi yetu miongoni mwa Wizara mama ambazo ni nguzo na tegemeo wa maisha ya wananchi wake na ambayo inaweza kuongeza mapato ya Serikali ni  Wizara ya Mifugo na Uvuvi”  alisisitiza Mhe. Mukunda

Amesema mifugo na uvuvi ni dhahabu inayotembea ambayo kama  itatunzwa  kwa kuzingatia ushauri na utaalam  utaongeza tija na kulifanya taifa lisonge  mbele  kiuchumi

Hata hivyo amesema changamoto inayosababisha kutokuwa na mageuzi ya haraka kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi nchini ni kukosekana kwa wataalam kwenye  ngazi za chini kwa wananchi ambapo amesisitiza kuwa  kuna umuhimu Wizara husika kushusha wataalam hadi kwenye ngazi za vijiji  badala yahali ilivyo sasa ambapo wataalam  wapo kwenye ngazi za juu jambo ambalo linafanya utalaamu usiwafikie wananchi kama ilivyokusudiwa.

Aidha ameongeza kuwa kuna haja ya Wizara husika kuboresha ushirikiano katika utekelezaji  na utoaji wa maelekezo ambapo amesema  kumekuwa na ushahidi kuwa sehemu ambazo wizara zimeshirikiana kikamilifu na Halmashauri husika kumekuwa na matokeo chanya.

 Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi amepongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Sekta mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambapo ameelekeza  Halmashauri za Mkoa wa Singida kutenga maeneo  kwa ajili ya kulima malisho ya  mifugo na ameishukuru Wizara ya Mifugo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Ikungi kuanzisha shamba darasa  bora la malisho ya mifugo ambalo ni la mfano hapa nchini.

“Ukiona Mheshimiwa, Rais Dkt. John Magufuli anawekeza kwenye miradi kama ule wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere Rufiji, Reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam hadi Makutupola ya Singida lengo ni kujenga uchumi jumuishi” ameongeza Dkt. Lutambi

Amesema Mkoa wa Singida umendelea kupiga hatua katika kutekeleza   miradi mbalimbali ambapo amesema licha ya kufanya mapinduzi makubwa kwenye zao la Korosho   pia wamesimamia  vizuri sekta nyingine  kama vile  sekta ya madini ambapo muelekeo wa sekta ya madini ni kuwafanya wananchi wamiliki raslimali hii kwa kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina amesema  Serikali  ya awamu ya Tano imefanya mageuzi makubwa  kwenye sekta ya mifugo ambapo  viwanda vingi vya nyama  vimeanzishwa, kuboresha kwa miundombinu ya mifugo kama majosho na kuimarisha  minada, kuzuia utoroshaji wa  mifugo kwenda nchi jirani na  kuanza  kutengeneza  chanjo za mifugo ambapo hadi sasa chanjo sita zimekamilika na  nyingine saba zinatarajia kukamilika katika kipindi  kifupi kijacho na kufanya  chanjo  dhidi ya magonjwa 13 za kipaombele kukamilika.

Aidha, amesema Wizara  ya Mifugo tayari imeshatangaza  rasmi tarehe 13/5/2020  bei elekezi za chanjo za wanyama dhidi ya magonjwa 13 ya kipaombele  kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 za Mwaka  2020 kifungu cha 3(2)(g) na Kanuni za Chanjo na Uchanjaji Na 180 za Mwaka 2020 Kifungu cha 14(b) na (c)  ambapo bei ya dukani nay a kuchanjia kwa dozi  haitazidi  viwango vilivyoainishwa.

Tuesday, August 4, 2020

MAONYESHO YA NANE NANE KANDA YA KATI DODOMA YAING’ARISHA TANZANIA DUNIANI

Waziri wa TAMISEMI,  Mhe. Seleman Jaffo akipokewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Anjelina Lutambi  mara baada ya kuwasili kwenye viwanja vya maonesho ya Nanenane  kanda ya kati Dodoma leo.kushoto  ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi. (picha na  John mapepele)

   Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo (mwenye suti nyeusi na tai)  akiwa na viongozi wakuu wa Mkoa wa Dodoma na Singida akikata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya Kati Dodoma kwenye viwanja vya Nzuguni leo. (Picha na John Mapepele)
    Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ( mwenye kilemba) akishiriki kucheza Ngoma za Utamaduni za kikundi cha Chuo Kikuu cha Dodoma wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho ya Nanenane kanda ya kati Dodoma wakati Mgeni rasmi Mheshimiwa Seleman Jaffo Waziri wa TAMISEMI (mwenye suti) akikagua vikundi hivyo. (picha na John Mapepele)

1Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo (mwenye suti nyeusi na tai) akiwa  na viongozi wakuu wa Mkoa wa Singida na Dodoma  wakipata maelezo ya kilimo cha mtama kutoka kwa mtaalam wa Wizara ya Kilimo kwenye  viwanja vya Nzuguni -Dodoma wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati.(Picha  na John Mapepele)

       Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Seleman Jaffo (mwenye suti nyeusi na tai) akipata  maelezo ya uhimilishaji wa mifugo kutoka kwa mtaalam wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, nyuma ni Mwnyekiti wa Maonesho ya Nanenane kanda ya kati, Mhe. Dkt Binilithi Mahenge Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, kushoto ni Bi. Aziza Mumba Katibu wa Kamati ya Maandalizi. (Picha na John Mapepele)



Na John Mapepele

Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano ya kuanzisha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati Dodoma yameufanya Mkoa wa Singida kubuni na kuanzisha kilimo cha pamoja cha Korosho, zaidi ya ekari 25000 za pamoja.


Hatua hiyo imelifanya  eneo hilo kuwa miongoni mwa maeneo makubwa ya kilimo hicho duniani ambalo litasaidia kuipaisha Tanzania katika uchumi wa kati wa juu na kuwa eneo maarufu la utalii wa kilimo duniani.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti Mwenza wa Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kati Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Singida kwenye ufunguzi rasmi wa maonesho hayo kwa mwaka huu.


Maonesho hayo ya kanda ya kati katika viwanja vya maonesho vya Nzuguni jijini Dodoma wakati akitoa salamu za Mkoa huo kabla ya kumkaribisha Mwenyekiti wa Kanda ya Kati Mhe, Dkt. Binilith Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ili amkaribishe Mgeni Rasmi wa Maonesho hayo Mhe. Selemani Said Jaffo, Waziri wa TAMISEMI

Dkt. Nchimbi amesema elimu iliyotolewa na taasisi mbalimbali za kilimo kwenye maonesho hayo ziliufanya mkoa uweze kuanzisha mashamba hayo makubwa kwenye Wilaya ya Manyoni, Ikungi na Itigi baada ya kupata msaada wa kitaalamu kutoka Bodi ya Korosho nchini na Watafiti kutoka chuo cha Kilimo cha Naliandele ambao wamefungua ofisi baada ya kuona kuwa kuna uhitaji wa kipekee wa kuwa hapo kutokana na tija kubwa ya zao hilo katika Mkoa wa Singida.

“ Kutokana na Mkoa wa Singida kuwa na mashamba makubwa ya Korosho natoa wito kwa wawekezaji wa viwanda vya kubangua Korosho kuja Singida ili kuwekeza kwani kutakuwa na malighafi ya kutosha na ya uhakika katika kipindi kifupi kijacho” alisisitiza Dkt. Nchimbi.

Ameongeza kuwa utafiti uliofanyika umeonesha Korosho za Singida zinauwezo wa kuzaa mara mbili kwenye msimu mmoja kutokana na hali ya hewa katika eneo hili na kwamba mkulima mmoja tayari amepata kilo 100 kutoka kwenye mkorosho mmoja kwa mwaka mmoja tu hali ambayo inaashiria zao hilo lina tija kubwa kwa wakulima.

Amesema kwa sasa Mkoa wa Singida unahamasisha “Nanenane Kaya” kwa maana ya kuwa kila kaya lazima kuzingatia maarifa yanatolewa na wataalam kwenye maonesho ya nanenane kanda ya katika maeneo ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza kipato.

Ameongeza kuwa kwa sasa mkoa unajipanga kuongeza zao la Parachichi ambapo amesema tafiti zinaonyesha kuwa ardhi ya Mkoa wa Singida inafaa kwa kilimo cha zao hilo na kwamba kinachotakiwa ni kupata maji ya kutosha kwa ajili ya umwagiliaji wa zao hilo.

Ampongeza  Rais John Pombe Magufuli kwa kuiingiza Tanzania kwenye uchumi wa Kati na kuwaomba watanzania kumchagua tena katika kipindi kijacho ili maono yake ya kuhakikisha uchumi wa nchi unakua kwa kasi itimie.


"Kwa mkoa wa Singida tumejipanga kuhakikisha tunaunga mkono jitihada hizo kwa kufanya kazi kwa bidii na kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika mkoa huo"Alisema

Awali akizungumza Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi amezitaja fursa zinazopatikana kwenye Mkoa huo kuwa ni pamoja na viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo,viwanda vya kukamua mafuta ya alizeti na karanga,viwanda vya kusindika asali,ranchi za mifugo na kilimo cha vitunguu. 


Vingine ni viwanda vya kuchakata bidhaa za maziwa,viwanda vya kutengeneza chakula cha samaki na mifugo,viwanda vya kutengeneza mvinyo,viwanda kutengeneza jasi (gypsum),viwanda vya kuchakata korosho na uchimbaji wa madini na mafuta

Aidha Mwenyekiti wa maonesho hayo Kanda ya Kati Dkt. Mahenge alimwomba Mgeni Rasmi Mhe. Jafo kuiomba Serikali katika mwaka ujao kufanyia maonesho ya Nanenane kitaifa katika viwanja vya Nzuguni kwa kuwa ndiyo makao makuu ya nchi na kwamba uwanja huo unakidhi vigezo vyote ambapo Mhe. Jaffo alikubali kuwasilisha ombili hilo Serikalini.

Akifungua maonesho hayo ya Kanda ya Kati Waziri Jaffo amewataka wananchi kutumia maarifa yanayotolewa na wataalam ambapo amesema bado hayajatumika kikamilifu na kuagiza maafisa ugani kote nchini kuhakikisha wanawasaidia wananchi kulima na kufuga kisasa.

“Tuna fursa kubwa ya kujenga nchi yetu kwa kutegemea Kilimo, Mifugo na Uvuvi” amesisitiza Jaffo

Amepongeza kuwa na paredi la mifugo kwenye maonesho ya mwaka huu na kuelekeza kila Halmashauri nchini kuhakikisha inatenga maeneo ya kutosha ya malisho.

Aidha amempongeza Katibu ya Kamati ya maandalizi ya maonesho hayo kanda ya kati Bi Aziza Mumba ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Sekta ya Uchumi Mkoa wa Dodoma, pamoja na Kamati yake kwa maandalizi mazuri ya mwaka huu ambapo ameitaka kamati hiyo kufanya maandalizi mazuri zaidi katika miaka ijayo ili wananchi wanufaike zaidi na maarifa yanayotolewa.

Bi. Mumba amesema Kamati yake imepokea na itahakikisha kuwa inasimamia na kutekeleza maagizo hayo kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuboresha mapungufu yote yaliyojitokeza mwaka huu.

Mwaka 2020 ni mwaka wa kumi na tatu (13) katika kufanyika kwa maonesho ya nanenane katika viwanja vya Nzuguni na ni mara ya Kumi (10) kuendelea kufanya mashindano maalum ya paredi la mifugo ili kushindanisha mifugo bora.