Thursday, October 28, 2021

SlNGIDA NA DHAMIRA YA KUONDOA VIFO VYA KINA MAMA NA WATOTO WACHANGA

Mkuu wa Wilaya ya Singida  Mhandisi Paskasi Muragili akihutubia wataalamu wa afya katika kikao kilichofanyika jana  Halmashauri ya Singida vijijini. 
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Singida Vijijini Ester Chaula  akizungumza kwenye kikao hicho.

SERIKALI YAIPONGEZA SUA KWA TAFITI ZA KILIMO ZENYE TIJA NCHINI

Mkurugenziwa Sera na MipangoWizara ya Kilimo  Bwana Obadiah Nyagiro akiwasilisha hotuba yake kwa wadau wa APRA

Mtafiti kutoka katika Chuo Kikuu Cha Sokoine cha KilimoSUA  Profesa John Jeckonia akitoa ufafanuzi kwa wanahabari kuhusiana na matokeo ya utafiti huo.
Mkuu wa Mradi wa APRA na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo SUA  Profesa Aida Isinika akiwasilisha matokeo ya tafiti kwa wadau.

Wednesday, October 27, 2021

RAIS SAMIA AIPONGEZA WIZARA YA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO KWA UBINIFU

 Na. John Mapepele, WSUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ameipongeza  Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa ubunifu wa kuandaa mikakati mbalimbali ya kuendeleza sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo ikiwa ni pamoja na kuandaa Tamasha kubwa la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo linaoanza kesho oktoba 28 hadi 30  mjini Bagamoyo.

Rais Samia ameyasema hayo leo Oktoba 27, 2021 Ikulu  jijini Dar es Salaam kwenye  hafla maalum aliyoiandaa kwa ajili ya  kuipongeza Timu ya Taifa ya Soka  ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kutwa Kombe la COSAFA hivi karibuni.

“Ili kufanikisha ushindi naomba nitambue TFF, Wizara na Wadau wengine hongereni kwa umoja wenu, najisikia  fahari Twiga Stars  kushinda ugenini na kuleta  kombe  nyumbani” amefafanua Mhe. Rais

Tamasha la kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lenye kauli mbiu isemayo “Sanaa ni Ajira” lina lengo la kukuza na kuendeleza sanaa na utamaduni wa mtanzania pia kukutanisha  watu wa tamaduni tofauti kutoka  sehemu mbalimbali duniani ili kuonyesha utajiri wao wa  sanaa na utamaduni.

Rais Samia pia amepongeza ubunifu na uratibu uliofanywa wa kuandaa Tamasha la Michezo kwa Wanawake la Tanzanite  lililofanyika hivi karibuni  jijini Dares Salaam.

Amesema wakati akikabidhiwa uchifu hivi karibuni na Umoja wa Machifu nchini  mkoani Mwanza aliiagiza Wizara  kuwa na Tamasha  la Uchifu ambalo litakuwa likizunguka kila mkoa  na kuwataka machifu washirikishwe kikamilifu ili kukuza utamaduni  ndani ya nchi yetu.

Ameongeza kuwa mafanikio makubwa yaliyopatika kwenye sekta za Sanaa, Utamaduni na Michezo katika kipindi hiki ni kutokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali ambapo amesema Serikali ilitenga 1.5 bilioni na kiasi kingine   kimetoka kwenye  michezo ya  kubashiri.

Ameipongeza Wizara kwa kuratibu Tamasha kubwa la Bara la Afrika la warembo, mitindo na watanashati ambalo  limetoa  washindi sita kwenda kwenye  mashindano hayo kidunia nchini Brazil Aprili 2022 na kuitaka Wizara  ianze  maandalizi kwa ajili ya washiriki hao mapema ili waende wakiwa  wanajiamini.

Mhe. Rais ametumia tukio hilo kuzipongeza Timu za Kriketi za wanaume na wanawake zilizoshika nafasi ya tatu katika shindano la Bara la Afrika na  kuitaka Wizara kuupa kipaumbele mchezo huo ili uweze kufika kwenye ngazi ya kimataifa.

Pia ameipongeza Timu ya Soka ya Wanawake ya Taifa chini ya umri wa miaka 20 kwa kuendelea  kufanya vizuri kwenye  mashindano  ya kuelekea kombe la dunia na kusisitiza kuwa  yeye kama Rais yupo bega kwa bega  na timu hiyo ambapo ameitaka Wizara  kuwaibua  makocha wengine wa kike na kiume  na kuwapatia mafunzo ili wawe wa kimataifa watakaosaidia kuinua kiwango cha soka nchini.

Amesema  kutokana na kufanya vizuri kwenye  michezo, mataifa  makubwa  duniani  yameanza  kufuatilia  wachezaji nchini.

“Macho ya Timu kubwa wanafuatilia dumisheni nidhamu” amesisitiza  Mhe Rais

Kwa upande mwingine Mhe. Rais amesema anatambua  taasisi za Wizara kama BASATA, COSOTA na Bodi ya Filamu zina bajeti  ndogo ambapo amesema baada ya miezi  sita zitakwenda kupitiwa na kuelekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kukaa na Wizara ya Fedha kupeleka hoja  na amesisitiza  kuwa atasaidia  suala hili ili zipatiwe bajeti ya kutosha ziweze kufanya vizuri.

“Naomba Wizara mkae na Wizara ya Fedha mjieleze vizuri nami nitaweka  nguvu huko”. Amefafanua Mhe.Rais Samia 

Ameitaka Wizara kuwa  wabunifu na kuvutia vijana  katika  michezo  ili kuwandaa kwenye ajira ambapo ameagiza kupata mrejesho wa suala hili katika miezi mitatu ijayo.

Ameitaka  pia Wizara kuangalia na kujadili vyanzo  vipya vya fedha kufadhili Sanaa, Utamaduni na Michezo ambapo ametaka kuangalia  maeneo  ya kuwapunguzia tozo na kodi wasanii na wanamichezo pia kuwapa vivutio vya kikodi ili wawekezaji waweze kuwekeza kwenye maeneo hayo.

Kwa upande mwingine ameitaka Wizara  kuja na  mpango madhubuti wa kufadhili mchezo wa soka kwa wanaume na wanawake  na ameitaka  Wizara ya Utamaduni kushirikiana na TAMISEMI kuibua  vipaji  katika michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA na kuvikuza.

Amefafanua kuwa wanamichezo wana nafasi kubwa  ya kutambulisha utalii wa nchi yetu duniani.

Akizungumzia kuhusu Muundo wa Wizara amesema  amefanya mabadiliko ya Wizara kwa kuiondoa Idara  ya Habari kuipeleka mahali inakohusika ili  viongozi wa Wizara  wajielekeze zaidi kwenye sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Amewapongeza  Mawaziri kwa  kuaminiwa na kuendelea kutumikia kwenye nafasi zao na kuwataka kwenda kushirikiana na kuchapa kazi siyo kugombana.

Ameeleza kuwa sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ni  sekta za kipaombele ambazo pia zimeainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi 2020-2025 na zinatoa ajira kwa wananchi.


Tuesday, October 26, 2021

ASILIMIA 90 WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI MANISPAA YA SINGIDA HAWAPATI CHAKULA CHA MCHANA


Watoto wa Chekechekea wanavyokuwa makini darasani wakiwa katika hali ya kushiba. 

Siku ya Chakula Duniani (World Food Day) kila ifikapo Oktoba  kila mwaka.


Na Abby Nkungu, Singida


ZAIDI ya asilimia 90 ya shule za Msingi za Serikali Manispaa ya Singida hazitoi chakula cha mchana kwa wanafunzi wake hali inayoathiri usikivu, umakini, uelewa na ufaulu hasa kwa watoto chini ya miaka minane ambao bado wanahitaji lishe bora kwa ajili ya ukuaji ubongo ili waweze kufanya  vyema darasani.

Taarifa ya Ofisa elimu Msingi  Manispaa ya Singida, Eugene Shayo inaonesha kuwa kati ya shule 50 za Serikali, nne tu zinazotoa chakula kwa wanafunzi wake wakati kwa binafsi shule zote 16 zinatoa huduma hiyo.

Taarifa hiyo imekuja wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani kote kuadhimisha Siku ya chakula Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Oktoba 16, ambapo kwa mwaka huu ilifanyika Kitaifa mkoani Kilimanjaro kauli mbiu ikiwa ni “Uzalishaji na mazingira endelevu kwa lishe na maisha bora”

Hata hivyo, kwa Manispaa ya Singida hakuna matumaini mema juu ya mustakabali wa wanafunzi wa shule za msingi kutokana na kutopata chakula shuleni hivyo kuathiri kiwango cha taaluma.

“Sababu ya shule nyingi za Serikali kutowapatia chakula wanafunzi ni wazazi kukataa kuchangia wakati hizo nne zinatoa chakula kwa sababu zina wanafunzi wenye mahitaji maalum; hivyo Serikali hubeba mzigo huo”  alisema Shayo na  kuongeza  kuwa  shule binafsi ni lazima zitoe chakula kwa kuwa Wazazi wanalipa ada.

Alikiri kuwa kiwango cha ufaulu darasani kwa Wanafunzi wanaopata chakula cha mchana ni kizuri zaidi ikilinganishwa na wale wasiopata chakula.

“Kwa ujumla, mitihani ya kuhitimu darasa la saba  ni kielelezo tosha kwani wanafunzi kutoka shule binafsi wanafanya vizuri kuliko shule za Serikali; ingawa pia kuna sababu nyingine zinazochangia” alisema.

Mmoja wa walimu wanaofundisha chekechea ambaye hakupenda jina lake litajwe anasema hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wadogo walio chini ya miaka minane ambao licha ya kuwahi kutoka shuleni, mara nyingi ikifika saa 4:00 tu asubuhi huwa wanaanza kusinzia kwa njaa na uchovu hivyo kukosa usikivu.

“Kwa hivi vitoto vya chekechea vilivyopo shule za Serikali hali ndio mbaya zaidi kwani ikifika mchana utavihurumia; vyote utakuta vinasinzia na kupiga miayo  kwa njaa na uchovu” alisema na kuongeza kuwa  kuna haja kwa Serikali kuchukua hatua katika suala hilo  ili watoto wote wapate lishe  shuleni.

Mmoja wa wazazi, Hatibu Ismail mkazi wa Ipembe Singida mjini  alisema kuwa tatizo sio  wao kugoma kuchangia bali  viongozi na watendaji kushindwa kutimiza vyema  wajibu wao wa kuhamasisha juu ya  umuhimu wa suala hilo kwa maendeleo ya mwanafunzi shuleni.

Mtaalamu wa lishe Mkoa wa Singida, Teda Sinde alisema kuwa ulaji duni au ulaji usiozingatia makundi matano ya chakula huathiri ukuaji wa ubongo hivyo kusababisha mtu kutokufundishika kirahisi na kuwa mzito kwenye kufikiria na kutoa uamuzi, pia husababisha upungufu wa damu mwilini.

Alisema  kuwa lishe duni kadhalika huathiri mfumo wa kinga ya mwili katika  kupambana na magonjwa, mtoto kupata utapiamlo na magonjwa mengine hivyo kuweza kusababisha vifo.

Takwimu za utafiti wa Kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo.

Aidha, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora. 

Monday, October 25, 2021

JAJI WARIOBA AFURAHISHWA NA MAFUNZO YANAYOTOLEWA SUA KUSAIDIA VIJANA NCHINI

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu  Joseph SindeWarioba akiangalia baadhi ya bidhaa wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea chuo hicho jana.
Ziara ya kutembelea miradi mbalimbali ikifanyika.
Hapa akipata maelezo wakati wa ziara hiyo.
Ziara ikiendelea,
Ziara ikiendelea,


Na Mwandishi Wetu, SUA Morogoro


MKUU wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Jaji Mstaafu  Joseph SindeWarioba amefurahishwa na mafunzo yanayotolewa SUA kwa kushirikiana na PASS (Private Agricultural Support Sector) yanayosaidia vijana kujiajiri na jamii kwa ujumla.

Jaji Warioba ametoa pongezi hizo jana katika ziara yake ya siku mbili Chuoni hapo, akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa baraza la Chuo Jaji Othman Chande na makamu mwenyekiti wake Doroth Mwanyika.

“Hawa vijana akitoka hapa watasaidia kuwa walimu kwa j amii inayowazunguka na tayari wanakitu cha kufanya ukweli nimefurahi sana kuona vijana kutoka Mikoa mbalimbali kama Tabora, Mwanza, Kigoma, Rukwa wakipata mafunzo haya” alisema Warioba.

“Mafunzo hayo yatasaidia Taifa letu kwa kiasi kikubwa hususani miaka ijayo katika kukidhi mahitaji ya chakula nakuepukana na balaa la njaa kutokana na ongezeko la watu kwani wakati nchi inapata uhuru tulikuwa Watanzania milioni 9 lakini sasa wamefika milioni 60 hivyo tutarajie ongezeko kubwa la watu na uhitaji mkubwa wa Chakula”. 

Pia amewataka SUA kuongeza elimu kwa upana ili kuwafikia vijana wengi zaidi kwa ni mafunzo hayo tayari yameshaleta mafanikio kwa jamii kupitia vijana waliopita ambao wamepata mafunzo hayo.

Kwaupande wa Makamu Mkuuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Prof. Raphael Chibunda alimshukuru Mkuu wa chuo hicho kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne na mafanikio yaliyopatikana.

Profesa Chibunda alisema kuwa wamefanya maboresho makubwa chuoni hapo kwa kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi hususani mashamba ya kujifunzia kwa vitendo ili kujifunza kwa vitendo ikiwemo ujenzi wa maabara na ununuzi wa vifaa vya kisasa vya maabara pamoja na ujenzi wa maabara ikiwemo maabara mtambuka ambayo inweza kuchukua wanafunzi 3200 kwa wakati mmoja.

Makamu mkuu wa chuo pia alisema kuwa chuo kimetenga fedha zaidi ya milioni 450 kwa ajili ya kujenga vitalu 100 katika kipindi cha miaka mitatu, ambapo kwa mwaka huu wataanza na vitalu 30 natayari wamepeleka maombi mahususi kwa Tume yaTaifa ya Sayansi naTeknolojia(COSTECH) kwa lengo la kushirikiana kuendeleza wabunifu kwa kujenga vitalu vingi zaidi.

Aidha, ameongeza kuwa tayari milioni 200 imetumika kwa ajili ya upanuzi wa sehemu ya upasuaji na manunuzi ya vifaa vipya kama mashine ya X- Ray Digital, Ultra Sound ya kisasa yenye kuwezesha kuona kama mnyama amepata tatizo kubwa zaidi kwa ndani lakini pia chuo kipo mbioni kununua gari litakalotumika kama kliniki inayotembea ili kuwafikia wafugaji wanaoshindwa kufika kwenye hospital hiyo yaTaifa ya rufaa ya wanyama ili kupatiwa matibabu.

“Nitoe wito kwa wafugaji wa Wanyama katika nchi hii pale wanapoona wamekosa msaada sehemu nyingine basi waitazame Hospitali yetu ya Rufaa ya Taifa ya wanyama kama sehemu ya kupata msaada” alisema Profesa. Chibunda.

Katika ziara hiyo Warioba alitembelea miradi mbalimbali ikiwemo yaTiba ya wanyama na sayansi za afya, miradi ya kilimo kwenye Shamba la mafunzo, maabara mtambuka, Kituoatamizi cha Vijana kilichopo chini ya Shule kuu ya uchumi kilimo na taaluma za biashara, kitengo cha mifugo Magadu, kitengo cha Samaki Magadu na maabara ya sayansi na teknolojia ya chakula.


Saturday, October 23, 2021

KILIMO IKOLOJIA KITAKUWA MSAADA KWA WAKULIMA WASIOMUDU KUNUNUA PEMBEJEO ZA KILIMO NCHINI

Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji na mifugo  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Soud Hassan akifunga Kongamano hilo la Kitaifa la Pili la Kilimo Hai.

Profesa. Benard Chove akitoa salamu za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kwa niaba ya Makamu Mkuu wa chou hicho Profesa. Raphael Chibunda.

Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji na mifugo  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Soud Hassan (katikati) akimkabidhi cheti cha pongezi kwa kufanisha mkutano huo mkubwa Profesa. Benard Chove kwa niaba ya SUA.

Picha ya pamoja ya washiriki kutoka SUA wakiwa wameambatana na wakulima kutoka maeneo mbalimbali ambao wanafanya tafiti na kushiriki kwenye miradi mbalimbali ya Kilimo Hai inayotekelezwa na SUA.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai.


Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai.

Mkutano ukiendelea.

Washiriki wa mkutano huo wakifuatilia hotuba za ufungaji wa mkutano huo wa pili wa kitaifa wa Kilimo Hai. 


Na Calvin Gwabara, Dodoma


IMEBAINISHWA kuwa wakulima wengi nchini hawana uwezo wa kumudu gharama za kununua madawa na mbolea kwa ajili ya kustawisha mashamba na kuua wadudu na magonjwa kwenye mazao yao hivyo kilimo Ikolojia kinaweza kuwa msaada mkubwa kwao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo,Umwagiliaji na mifugo  wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Soud Hassan kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Profesa  Adolf Mkenda wakati akifunga Kongamano la Pili la kitaifa la Kilimo Hai lililofanyika kwa siku mbili Jijini Dodoma na kuwakutanisha wadau wote wa Kilimo Hai kutoka nani nan je ya Tanzania.

“Niwatake wadau wote wa kilimo Hai nchini kuhakikisha malighafi zinazozalishwa za kuulia wadudu na magonjwa pamoja na mbolea ziweze kupatikana kwa wingi, kwa urahisi na kwa bei nzuri kwenye maeneo mbalimbali nchini ili ziweze kuwafanya wakulima wetu waachane na matumizi makubwa ya madawa na mbolea za viwandani” alisema.

Amewahakikishia kuwa Serikali ya Tanzania iko pamoja na wadau wote wa kilimo Hai na imeiweka katika mipango yake na ili kuendana na mabadiliko ya tabia nchi mbegu stahimilivukwa uhakikika wa chakula lishe na kuongeza kipato zinahitajika.

Waziri huyo wa Kilimo Zanzibar alisema serikali sikivu ya Tanzania imetengeneza mazingira rafiki ya Kilimo Hai kupitia sera yake ya kilimo ya mwaka 2013 na inatambua mchango wa utafiti wa kilimo Hai kupitia wanafunzi wa Shahada za Uzamili na uzamivu wa Chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA.

“Malengo makubwa ya Wizara ya kilimo ni Utafiti,Tija ya uzalishaji,Upatikanaji wa Pembejeo husasani mbolea viutilifu,mbegu bora na zana za kilimo,Masoko ya mazao,Uongezaji thamani wa mazao na Miundombinu ya umwagiliaji”alisisitiza Hassan.

Aidha amesema Tanzania ina wakulima wa Kilimo Hai waliosajiliwa wanafikia wakulima 600,000 na kwa idadi hiyo kubwa ni vyema TOAM kuendelea kuwatambua na kuwasjili ili kuendelea kuwatumia kwa lengo la kuzalisha chakula.

Akitoa salamu za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Benard Chove kwa niaba ya Makamu Mkuu wa chou hicho Jukumu la SUA Prof. Raphael Chibunda amesema jukumu la SUA ni kuchangia katika maendeleo ya nchi kwa kufanya mafunzo, utafiti na kutoa huduma kwa jamii.

”Ni matumaini yangu washiriki kutoka SUA wameweza kutoa maelezo kuhusu shughuli mbalimbali zilizofanyika na zinazoendea kufanyika katika kuhakikisha Chou kinatoa mchango wake katika kuendeleza Kilimo ikolojia kupitia mafunzo utafiti na ushauri, alibainisha Profesa Chove.

Prof. Chove amesema kuwa chuo kimeendelea kuyaishi maono na malengo na maagizo ya Baba wa Taifa ya kuanzisha chuo hicho na kusema kuwa maza yao ni Wanafunzi wanzalishwa chuoni hapo na humu ndani nikisema wote waliopita SUA wasimame naamini itakuwa vurugu kubwa sidhani kama kuna watakaobaki kwenye kiti hivyo tumeendelea kuishi kwenye maono yake.

Ameedelea kusema kuwa yote ambayo SUA imeyatekeleza kwa kipindi chote hicho toka kuanzishwa kwake juu ya mafunzo na kuchangia katika maendeleo ya Kilimo Ikolojia yasingeweza kufanyika bila ushirikiano ambao wameupata kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau mbalimbali wa maendeeo.

“Hivo napenda kuwashukuru wadau wetu wa maendeleo kama vile Serikali ya Denmark kupitia mradi wa BSU,SWISSAID,Wakfu wa MACKNIGHT kutoka Marekani,Shirika la Maendeleo la Ubelgiji na Asasi zingine zisizo za Kiserikali na wengine wengi.

 “Napenda kuchukua nafasi hii kuwahakikishia kwamba chuo kitaendelea kutoa ushirikiano na kufanya kila linalowezekana kuhakikisha malengo ya ushirikiano wetu yanafanikiwa kwa manufaa ya watanzania wote na Taifa”. alisema.

Profesa Chove amesema miongoni mwa mafanikio ya ushirikiano na wadau hao ni kaunzisha Shahada ya Uzamivu Kilimo Ikolojia ambayo imeingia mwaka wa pili lakini mandalizi ya kuanzisha Shahada ya umahili ya Kilimo Ikolojia yanaendelea na hii itasaidia kuboresha na kujenga uwezo zaidi kwa chuo katika kutoa huduma kwa jamii.                                                         

MAAGIZO YA RC SINGIDA YATEKELEZWA NI KUHUSU KILIMO CHA UMWAGILIAJI ITAGATA ITIGI


Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge  akizunguza na Wananchi wa Kijiji wa Itagata hivi karibuni kuhusu umuhimu wa kilimo cha umwagiliji  na mikakati ya kurejesha skimu ya Umwagiliaji ya Itagata ambayo imegharimu kiasi sh shilingi Bilioni 2.2.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni   Rahabu Mwagisa (aliyesimama) akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Itagata hivi karibu. Mkutano huo ulihusu uhuishaji wa skimu ya umwagiliaji ya Itagata  ambayo serikali imetumia fedha nyingi lakini haitumuiki ipasavyo.


Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Itagata wakisikiliza maagizo ya mkuu wa mkoa kuhusu uboreshaji wa skimu ya Itagata.
Mkuu wa mkoa akisikiliza kero mbalimba kutoka kwa wakulima wanaotumia skimu ya Itagata mara baada ya kumaliza mkutano wa hadhara.



Na Bashiri Salum, Itigi.


MATUMAINI ya kurejea kwa kilimo cha umwagiliaji katika skimu ya Itagata iliyopo Wilayani Itigi Mkoani Singida yameanza kujitokeza  kwa Wakulima baada ya kuanza kutekelezwa kwa  maagizo ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge ya kuvunja uongozi uliokuwepo na  kuchukuliwa kwa mashamba ambayo hayaendelezwi katika skimu hiyo.

Ikiwa ni mwezi mmoja umepita  baada ya mkuu wa mkoa kutembelea skimu hiyo na kuwataka wakulima kuchagua uongozi mpya ambao  utashirikiana na viongozi mbalimbali kufanya tathmini ya ugawaji na uendelezaji wa mashamaba, jana Oktober 23, 2021 kwa mara nyingine ametembelea skimu hiyo na kukuta wamechagua viongozi wapya  na tathmini ya mashamba  imefanyika.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara na wakulima hao Mahenge amemshukuru mkuu wa  wilaya hiyo Rahabu Magesa na viongozi wengine kwa kuanza kutekeleza maagizo yake na kuwaeleza kwamba  hatua hiyo  iwe endelevu na kuhakikisha wakulima wanafuata sheria na taratibu za skimu hiyo.

“Skimu hiyo iligharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.2 tokea ilipoanza kujengwa mpaka mwaka 2019 ilipokabidhiwa kwa kijiji husika, ni lazima lazima usimamizi ufanyike ili uzalishaji uongeze iweze kutoa mchango kwa taifa” alikaririwa Dkt. Mahenge.

Aidha Dkt. Mahenge akiwa kijijini hapa akatoa wito kwa wakulima wote  wenye umiliki wa mashamba katika skimu hiyo kulipa ada zinazotakiwa ambazo zitatumika kukarabati miuondombinu ya skimu pale itakapo hitajika.

Hata hivyo Rc huyo alisema ulinzi wa miundombinu ya  skimu ni jukumu la kila mwananchi hivyo akawakumbusha watu wenye makazi ndani ya Skimu kuhakikisha wanafuata sheria zilizowekwa kwenye skimu hiyo kama wakishindwa watalazimika kuhama.

Aidha maagizo hayo yametokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Afisa Kilimo kwamba wakazi hao wamekuwa wakiwatishia wakulima wengine wakidai eneo hilo lipo chini yao jambo ambalo limeleta kero kwa wakulima wengine.

Akijibu maswali ya wananchi ambao wametakiwa kulipia ada wakati mashamba yao hayajafikiwa na miundombinu ya umwagiliaji na kufanya kilimo chao kutengemea mvua za msimu Mahenge akaendelea kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha miundombinu inatengenezwa maeneo yenye changamoto ya kufikisha maji ili wakulima waweze kumwagilia .

“Nataka tuelewane kwamba kila mkulima ndani ya skimu anahaki sawa na mkulima mwingine hivyo kila mtu anatakiwa kufikiwa na maji na kutoa ada kulingana na ukubwa wa anachokimiliki”.aliendelea kufafanua Mahenge.

DC wa wilaya hiyo Rahabu Mwagisa alisma kwa sasa wakulima hao wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji ila serikali inaendelea kuwaunganisha na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kifeza ili kupata mikopo  

Rahabu akawashauri  wakulima hao kulima mpunga kwa kuwa soko lake ni la uhakika na watakao amua kulima matunda au mbogamboga wahakikishe wanalima kwa wingi kwa ajili ya kulitosheleza soko.

Awali Afisa kilimo wa kijiji cha Itagata  Bi. Halima Issingo alibainisha kwamba skimu hiyo ina ukubwa wa ekari 400 zinazofaa kwa kilimo na inauwezo wa kulisha wilaya nzima endapo itafanya kazi kwa viwango vyake vyote.

Afisa kilimo huyo alisema  jumla ya ekari 209 kati ya 400 zimegawiwa kwa wanachama  na kati hizo ekari 115 ndizo zililzolimwa mpunga  na kutoa tani 120.75 wakati ekari 26 zililimwa mahindi na kutoa tani 14.4

Alisema moja ya mipango ndani ya skimu ni kufikisha miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo ambayo hayana ili kuifanya skimu nzima iweze kuzalisha vya kutosha.

Wakulima nao wakapata nafasi ya kutoa maoni baada ya mkutano ambapo Musa Saidi mkulima wa skimu hiyo wameishukuru serikali kwa hatua walioichukua ya kuhuisha skimu hiyo na kuomba wataalamu waendelee kutoa elimu kwa wakulima ili kubadilisha mazingira ya uzalishaji na kulima ki biashara.

Michaeli Simuli Ngawe mkulima wa mpunga naye akiomba  serikali kuwaletea mbolea na mbegu za kisasa za mpunga  kwa kuwa wengi wao hawatumii mbolea na mbegu bora kwa kuwa dhamiara ya serikali na wakulima kwa sasa ni kubadilisha kilimo kiwe chenye tija.

Friday, October 22, 2021

GUGU KONGWA LATISHIA USTAWI WA MALISHO YA MIFUGO KANDA YA KATI

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah (wa pili kutoka kulia waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Washiriki wa Mkutano wa uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika jijini Dodoma jana.
Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Prof. Antony Sangeda akiwasilisha sehemu ya utafiti wa Gugu Kongwa kwa Wadau wa Sekta ya Mifugo katika Mkutano wa uwasilishaji wa Utafiti huo uliofanyika jijini Dodoma jana.
Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Prof. Erick Komba akitoa maoni yake  katika Mkutano wa uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika jijini Dodoma jana.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri  Gillah (kulia) akiwa na wadau wengine wakifuatilia uwasilishaji wa utafiti wa awali kuhusu Gugu Kongwa uliofanyika  jijini Dodoma jana.



Na Mbaraka Kambona,


WATAFITI kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kwa kushirikiana na Serikali wamesema kuna haja ya kuchukua hatua za haraka za kudhibiti kusambaa kwa mmea wa Gugu Kongwa ambao umeonesha kuathiri kwa kiasi kikubwa maeneo ya malisho  yaliyopo wilayani Kongwa na mkoani Singida.

Hayo yalibainishwa na Wataalamu hao walipokutana na wadau wengine wa Sekta ya mifugo jijini Dodoma Oktoba 22, 2021 kuwasilisha  matokeo ya awali ya utafiti waliofanya kujua tabia za ukuaji na usambaaji wa mmea huo ili kutafuta njia fungamanishi za kupunguza au kutokomeza kabisa mmea huo ujulikanao Gugu Kongwa.

Akizungumza katika mkutano huo, Mtafiti Kiongozi kutoka SUA, Dkt. Selemani Ismail alisema utafiti wa Gugu Kongwa ulilenga kujua tabia ya ukuaji wake na  kwa kiasi gani mmea huo unaoathiri malisho ya Mifugo umesambaa.

"Utafiti wa awali tulioufanya kwa miaka miwili (2)  ulilenga kutafuta njia shirikishi za kupunguza au kuangamiza kabisa mmea huo wa Gugu Kongwa ambao usambaaji wake umekuawa na athari kubwa katika maeneo mengi ya malisho hususan katika maeneo ya Kanda ya Kati na Mkoa wa Manyara," alisema Dkt. Ismail

Dkt. Ismail aliendelea kusema kuwa katika kutafuta njia ya kudhibiti Gugu Kongwa walifanya utafiti na kupata mmea unaoitwa Melia ambao umeonesha ufanisi katika kutokomeza usambaaji wa Gugu Kongwa.

"Utafiti wetu tuliufanya Wilayani Kongwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI) na Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ili kutokomeza mmea huo na kulinda malisho kwani likiachwa liendelee kusambaa athari zake ni kubwa sana kwa malisho ya mifugo," aliongeza

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Kejeri Gillah alisema kuwa Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine inajipanga kuhakikisha matokeo hayo ya utafiti yanakwenda kufanyiwa kazi.

"Tumeona athari kubwa za gugu hili vamizi katika maeneo yetu ya malisho na hivyo ni muhimu kulidhibiti mapema ili lisisababishe uhaba wa malisho na kupunguza tija katika uzalishaji," alisema Dkt. Gillah

Meneja wa Mfuko wa Kuendeleza Sayansi na Teknolojia kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Ntufye Mwakigonja alisema anaimani kuwa utafiti huo utatatua changamoto hiyo inayokabili malisho nchini huku akiongeza kuwa  wao kama COSTECH wataendelea kushirikiana na watafiti hao ili kuhakikisha matokeo hayo yanafanyiwa kazi kwa manufaa ya sekta ya mifugo nchini.

Aidha, Wadau wa Sekta ya Mifugo waliohudhuria mkutano huo walisema kuwa pamoja na kuwepo  changamoto zinazosababishwa na mmea huo katika malisho ya mifugo, watafiti hao waendelee kufanya utafiti kuangalia mtizamo chanya ambao unaweza kusaidia jamii kutumia faida zinazoweza kupatikana zitokanazo na Gugu Kongwa.

WAZEE WA CCM MANGUANJUKI SINGIDA WACHARUKA WATAKA MABADILIKO YA VIONGOZI

Mmoja wa wazee wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Manguanjuki, Kata ya Mandewa mkoani Singida kwa niaba ya wenzake akiwasilisha malalamiko mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya chama hicho Kata ya Mandewa, (hawapo pichani) dhidi ya viongozi wao wa chama ambao pamoja na mambo mengine, wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ikiwemo kushindwa kuitisha mikutano halali ya chama kwa mfululizo wa miaka minne tangu walipochaguliwa.

Wazee wakisikiliza kwa makini maamuzi ya chama baada ya kupokea malalamiko hayo.

Katibu wa CCM Kata ya Mandewa, Yusuph Makera Kijanga akizungumza na wazee hao kwenye mkutano huo.

 


Na Mwandishi Wetu Singida


WAZEE wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Manguanjuki Kata ya Mandewa Manispaa ya Singida wameiomba Kamati ya Siasa ya CCM ndani ya kata hiyo kuwaondoa mara moja viongozi wa chama hicho ndani ya tawi hilo-Mwenyekiti Abdalah Kitiku na Katibu wake Jasta Kiwigah ambao pamoja na mambo mengine, wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya uongozi kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ikiwemo kushindwa kuitisha mikutano halali ya chama kwa mfululizo wa miaka minne tangu walipochaguliwa.

Wakizungumza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM ya kata hiyo, wazee hao wameomba maamuzi ya haraka yachukuliwe ili kunusuru uhai wa chama kwenye maeneo hayo kutokana na viongozi hao kuonesha dhahiri ukiukwaji mkubwa wa kanuni na taratibu za chama, sanjari na kutokuwa na mahusiano mazuri baina yao na viongozi wa serikali ya kijiji na wananchi

Akizungumza baada ya kupokea malalamiko hayo, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mandewa Hamis Ireme kwa niaba ya kamati hiyo, alisema amepokea malalamiko ya wazee hao na kuahidi kuitisha mkutano wa wanachama ili kuangalia uwezekano wa kukaimisha nafasi hizo.

“Kamati ya siasa ya kata baada ya kupokea malalamiko ya wazee na kujiridhisha tumekubaliana kukutana na wanachama ili kujadiliana juu ya jambo hilo kwa kuangalia uwezekano wa kukaimisha nafasi za Mwenyekiti na Katibu, lengo ni kuleta ustawi na kuchagiza maslahi mapana ya chama na wanachama wetu ndani ya tawi la Manguanjuki,” alisema Ireme.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Kata ya Mandewa, Yusuph Makera Kijanga alisema kamati hiyo inatarajia kuitisha mkutano mkuu wa wanachama mapema mwezi Novemba mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine, jambo hilo lililojitokeza litatolewa taarifa ili kupata baraka juu ya mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika.

Aidha, Kijanga aliwataka viongozi wengine wa matawi ndani ya kata hiyo kuwajali, kuwapenda, kuwasikiliza na kuwa karibu na wanachama na wananchi wote kwa kuonesha mshikamano ili kwa umoja na pamoja kuwezesha CCM kutekeleza Ilani yake kikamilifu.

“Hii Kata ya Mandewa ni kubwa sasa kama hatutashikamana pamoja tutachelewesha maendeleo. Na nisisitize hakuna aliye juu ya chama, yeyote mwenye dhamana ya chama ndani ya kata yetu atakayekwenda kinyume ajue ataharibikiwa yeye kabla hajakiharibu chama chetu,” alisema Kijanga.

SUA VINARA KATIKA WABOBEZI KWENYE KILIMO IKOLOJIA NA KILIMO HAI NCHINI

1.      Mtafiti Mbobezi kwenye Tafiti za Kilimo Hai kutoka SUA Prof. Kalunde Sibuga akiwasilisha maelezo yake kuhusu mchango wa SUA katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa kwanza wa Kitaifa wa Kilimo Hai wa mwaka 2019.

1.      Mratibu wa Mradi Kitovu cha kilimo Ikolojia Tanzania Prof. Dismas Mwaseba kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo akitoa mrejesho wa mjadala wa mifumo wa chakula.

1.      Prof. Anthony Zozimus kutoka Chou Kikuu cha Kilimo akichangia kwenye moja ya mijadala katika Kongamano hilo la pili la Kilimo Hai.

John Csotantine Mwanafunzi wa shada ya uzamili kutoka SUA akiwasilisha matokeo ya utafiti wake kwenye Kongamano hilo la Kitaifa la pili la Kilimo Hai unaohusu Uboreshaji wa mazao ya mahindi na mihogo kwa kutumia mbinu za kilimo Ikolojia katika wilaya za Mvomero na Masasi nchini Tanzania

1.      Mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili kutoka SUA anyefanya utafiti wa kuongeza uzalishaji wa mpunga kwa kutumia mbinu mbalimbali za kiikolojia za kudhibiti magugu na kuongeza rutuba kwenye udongo katika skimu ya Makwele Wilayani Kyela Mkoani Mbeya akiwasilisha matoke ohayo mbele ya wadau.

 

1.      Wadau wa kilimo Hai kutoka ndani na nje ya Tanzania wakifuatilia kongamano hilo.

Kongamano likiendelea,

1.      Wadau wa Kilimo Hai kutoka ndani na nje ya Tanzania wakifuatilia kongamano hilo.

Kongamano likiendelea, 



Na Calvin Gwabara - Dodoma


CHUO  Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuwa kinara katika kufanya tafiti na  uzalishaji wa wataalamu wa masuala ya kilimo Hai  hata kabla  ya kuaizishwa kwa taasisi na mashirika mbalimbali ambayo yanahamasisha na kusisitiza matumizi na faida za kilimo hai nchini.

Hayo yamesemwa na Mtafiti Mbobezi kwenye tafiti za Kilimo Hai kutoka SUA Prof. Kalunde Sibuga wakati akiwasilisha maelezo yake kuhusu mchango wa SUA katika kutekeleza maazimio ya Mkutano wa kwanza wa kitaifa wa Kilimo hai wa mwaka 2019 kwenye mkutano wa pili unaoendelea Jijini Dodoma.

“Katika shahada ya kwanza tumekuwa na mtaala wa kilimo Hai Hata kabla ya Mkutano wa mwaka 2019 na mataala ulilenga wanafunzi wanaochukua shahada ya kilimo pamoja na ile ya Bustani na Mbongamboga, na huu mtaala bado upo kwahiyo tulianza zamani” alifafanua Prof. Sibuga.

Alisema kila mwaka Nchini Uganda kumekuwa kukiendshwa mafunzo ya muda mfupi ya kilimo Hai na Chuo kwa kutambua umuhimu wake kimekuwa kikiwapatia wanafunzi wake ruhusa ya kwenda kuhudhuria na kuonea ujuzi na kisha kurejea kuendelea na masomo na mitihani yao.

Prof. Sibuga amesema kuwa kupitia pia Mradi wa kujenga Vyuo imara (BSU) wamefanikiwa kuwezesha kupatikana kwa mtaala kwa Wanafunzi wa Shahada ya Uzamivu mtaala ambao wadau mbalimbali walishirikishwa katika kuuboresha na kuwezesha kuwapa nafasi ya kusoma darasani lakini pia kuwepo kwa sehemu ya utafiti .

Sambamba na hilo pia tayari wanao mtaala mwingine wa Shahada ya Uzamili ambao umeshatengenezwa na sasa upo kwenye hatua mbalimbali za kuboreshwa na wadau ili uweze pia kupitishwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kabla ya kuanza kutumika.

Pia Mtafiti huyo amesema pamoja na mambo hayo lakini SUA na watafiti wake wamekuwa na miradi kadhaa ya kilimo hai na kilimo ikolojia kama mradi wa uzalishaji na ukuaji wa mnyororo wa thamani za mazao ya kilimo Hai ambao walikuwa wanshurikiana na watafiti wengine wa afrika mashariki ambapo vijana wawili walipata shahda za Uzamili na wengine wawili walipata shahada zao za uzamivu.

Prof. Sibuga amesema kutokana na umuhimu huo hivi sasa SUA ina takribani miradi minne ya kilimo Hai ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mratibu wa Mradi Kitovu cha Kilimo Ikolojia Tanzania Prof. Dismas Mwaseba kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo akitoa mrejesho wa mjadala wa mifumo wa chakula amesema kuwa walifanikiwa kufanya mkutano ambao wadau mbalimbali walishiriki katika kuongeza mapokeo ya kilimo Ikolojia na kilimo Hai nchini.

Prof.Mwaseba amesema mambo mbalimbali yalijadiliwa lakini hasa ni katika Utafiti,Sera, Uenezwaji wa matokeo na ushawishi ambapo amesema katika sera yalijadiliwa mambo mengi lakini ilibainika kuwa Sera za kilimo nchini hazijazungumzia maswala ya kilimo Ikolojia na kilimo Hai.

“Wadau wamependekeza kwenye mkutano huo kuwa kwenye swala la utafiti na mafunzo iwepo mitaala kwenye taasisi za elimu hasa vyuo vy akilimo ambayo itafundisha maswala ya kilimo Ikolojia na Kilimo hai kwa mapana yake na kuwa kuna haja ya kufanya utafiti kubainisha mahitaji ya wadau mbalimbali kwakuwa sasa tafiti zilizopo zimegusa wadau maalumu tu hasa wa kilimo cha mboga” alieleza Prof. Mwaseba.

Mratibu huyo wa Mradi wa Kitovu cha Kilimo Ikolojia amesema pia kuwa wadau wanapendekeza kuwepo na ushawishi ambao utatokana na Ushahidi wa Kiutafiti na hasa zile teknolojia mbazo zimethibitika kwa ubora wake na utangazaji wa bidhaa za Kilimo ikolojia uzingatie mahitaji ya soko.

Ameongeza kuwa uratibu wa kilimo ikolojia ufanisi uongezeke ili kusaidia wadau wa kilimo ikolojia ili kuhakikisha wadau wa kilimo hicho wakuwa karibu katika kuendeleza lakini pia wakushauri Kitovu cha kilimo ikolojia kipewe kazi ya kuratibu maswala hayo.

Prof. Mwaseba alibainisha kuwa wadau wa mkutano huo walisema Kitovu cha kilimo ikolojia kinaweza kufanikisha maswala mbalimbali ya sera,uwezeshaji pamoja na utafiti ambapo katika kikao hicho wadau walipendekeza sasa kwakuwa mradi unaisha basi kianzishwe kitovu cha kilimo Ikolojia na wadau wote waweze kujiunga na kuchangia katika kushughulikia maswala mbalimbali ambayo yanakigusa kilimo hicho nchini.

Katika Kongamano hilo la pili la kitaifa la kilimo Hai nchini Wanafunzi mbalimbali wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wanaofanya Tafiti zao katika maswala ya Kilimo Ikolojia na Kilimo Hai wamepata nafasi ya kuwasilisha matokeo ya Tafiti zao na kujadiliwa na wadau hao lakini pia watafiti wa SUA nao wamewasilisha na kushiriki kwenye mijadala mbalimbali kuonesha ushiriki wao katika kuchangia ukuaji wa kilimo Hai nchini.

RC SINGIDA ARIDHISHWA UKUSANYAJI , UDHIBITI MAPATO WILAYA YA SINGIDA DC

Mkuu wa Mkoa Singida Dk. Binilith Mahenge. 



Na Mwandishi Wetu, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge ameridhishwa na hatua kadhaa zinazoendelea kuchukuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Singida katika nyanja za udhibiti, kasi ya ukusanyaji na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato ambavyo vimewezesha kupaisha mapato kutoka 60.9 milioni mwezi Julai mwaka huu hadi kufikia milioni 139.3 mwezi Agosti.

Aidha, Dk. Mahenge amepongeza uamuzi wa halmashauri hiyo kutoa eneo la ekari 50 kwa Amcos ya wazalishaji zao la Mkonge iliyopo Kata ya Mudida Kijiji cha Mpipiti, ambapo pamoja na mambo mengine, ameahidi kuhakikisha anawaunganisha kikamilifu na Bodi ya Mkonge nchini ili kuwawezesha kuanza kunufaika na bei ya soko.

Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanaainisha vyanzo vyote vya mapato na kuvifanyia tathmini ili kubaini kila chanzo kihaulisia kinapaswa kukusanya kiasi gani gani cha fedha, kuweka usimamizi na udhibiti madhabuti, lengo ni kuwezesha vyanzo husika kuanza kukusanya mapato kwa asilimia 100.

“Nimeridhika na taarifa yenu hasa ya mapato, kikubwa hapa kaeni tengenezeni timu fanyeni analysis ya uhalisia wa kila kinachofanyika na kukusanywa kwenye vyanzo vyote rasmi na visivyo rasmi…tuwe na shabaha kwa kila tunachokifanya,” alisema.

Kuhusu uzalishaji wa zao la mkonge ambalo baada ya kuoteshwa limeonesha kutoa matokeo chanya na ubora wa hali ya juu kwenye ardhi ya Mkoa wa Singida, hususani ndani ya halmashauri hiyo, Mkuu wa Mkoa aliwahamasisha wana-singida na watakaohitaji kuwekeza kuchangamkia fursa ya zao hilo ambalo uwekezaji wake hauhitaji nguvu kubwa lakini faida yake ni kubwa.

“Uzuri wa mkonge hauna changamoto yoyote ukishapanda basi wewe unasubiri kuvuna tu…hivyo unaweza kulima mkonge na wakati huohuo ukaendelea na kilimo chako cha mazao mengine. Na mkonge wetu wa singida umeonekana kuwa bora zaidi na kimbilio kuliko maeneo mengine nchini,” alisema.

Katika hilo, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri alimweleza Mkuu wa Mkoa kwamba kwa sasa wakulima wa wilaya hiyo wanaozalisha mkonge wanapata tabu kubwa kutokana kulazimika kuuza kwa madalali ambao huwalangua, hivyo alipendekeza waanze kuuza kwa bodi ili kupata bei ya soko sambamba na halmashauri kupata mapato halisi na hatimaye wawekezaji wengi waweze kuja.

Pia katika hatua nyingine kupitia ziara hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Elia Digha alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa namna alivyoonesha kuipenda na kuijali halmashauri kwa kuipatia shilingi bilioni cha 1.6 kwa ajili ya maboresho ya miundombinu ya elimu, afya na maji sanjari na fedha nyingine ambazo zimekuwa zikitolewa kwa kipindi tofauti kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.

Awali akizungumzia fedha hizo, pamoja na kumpongeza Rais Samia, Dk. Mahenge aliwaasa watendaji wa halmashauri hiyo kuhakikisha wanazitumia fedha hizo kwa malengo kusudiwa.

“Niwasihi sana fedha hizo ni za moto…hazina posho wala urafiki. Hakikisheni kila kitu kinafanyika kama kilivyopangwa na kwa viwango na ubora stahiki,” alisema Mahenge.