Sunday, January 31, 2021

STARA THOMAS, HAFSA KAZINJA KUKABIDHIWA KADI ZA MATIBABU NA WAZIRI BASHUNGWA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.

 Wanamuziki Stara Thomas na Hafsa Kazinja wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Eric Kisanga (kushoto) na Katibu Mkuu wa umoja huo, Stella Joel  (kulia) baada ya kufanya mazungumzo jijini Arusha juzi kuhusu Kongamano la Fursa kwa wanamuziki litakalofanyika Februari  20, 2021 Jijini humo.  



Na Dotto Mwaibale.


WANAMUZIKI Maarufu  Nchini Stara Thomas na Hafsa Kazinja ni miongoni mwa baadhi ya wanamuziki watakao pata kadi za bima ya afya ya Taifa (NHIF) zitakazotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.

Bashungwa ambaye atakuwa mgeni rasmi atatoa kadi hizo katika Kongamano la Fursa kwa wanamuziki litakalofanyika Februari  20, 2021 Jijini Arusha.  

"Mastaa hawa Stara Thomas na Hafsa Kazinja tayari wametimiza vigezo vya kupata kadi hizo za bima ya afya baada ya  kukutana na Rais wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Eric Kisanga na Katibu Mkuu wa umoja huo, Stella Joel ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo.

Akiwazungumzia Wanamuziki hao Katibu Mkuu wa TAMiUFO Stella Joel alisema wanaishukuru Serikali kwa kuwakumbuka kuwapatia kadi hizo ambazo zitawasaidia kupata vipimo na matibabu katika hospitali za Serikali na binafsi.

Joel alisema kabla ya hapo wanamuziki wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za vipimo na matibabu.

" Kwa hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano hakika wanamuziki wote tunakila sababu ya kuipongeza  kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo ya kutusaidia wasanii" alisema Joel.

Rais wa TAMUFO,  Eric Kisanga alisema kongamano hilo ni la kipekee kwani litawahusisha wanamuziki wa kada zote  na kuwa maandalizi yote yamekwisha kamilika.

" Maandalizi yote ya kongamano letu ili la fursa kwa wanamuziki yamekwisha kamilika kwa asilimia kubwa na sasa tupo kumalizia mambo madogo yaliyosalia" alisema Kisanga.


Friday, January 29, 2021

WAZIRI BASHUNGWA KUPOKELEWA KWA WIMBO MAALUMU KONGAMANO LA WANAMUZIKI

Wasanii wa Kikundi cha Sanaa cha Dofa kilichopo Karatu mkoani Arusha wakifanya mazoezi ya  wimbo maalumu watakao muimbia Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa  wakati wa kumpokea katika  kongamano la wanamuziki.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Stella Joel.
 


Na Dotto Mwaibale


WASANII wa Kikundi cha Sanaa cha Dofa kilichopo Karatu mkoani Arusha wanatarajia kumpokea Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa kwa wimbo maalumu katika kongamano la wanamuziki.

Bashungwa atakuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo la Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) litakalofanyika Februari 20, 2021 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema hivi sasa kikundi hicho kipo katika mazoezi ya wimbo huo maalumu kwa ajili ya kumpokea Waziri Bashungwa.

" Waziri Bashungwa anakuja kwenye kongamano letu wanamuziki hivyo tumeona ni lazima tumpokee kwa wimbo maalumu kwa ajili ya kumpa heshima." alisema Joel.

Joel alisema katika kongamano hilo  pamoja na mambo mengine Bashungwa atatoa  kadi za Bima ya Afya ya NHIF kwa Wanamuziki wa kada zote na kusikiliza changamoto zao mbalimbali.

Alisema kadi hizo zitawasaidia kupata vipimo na matibabu katika hospitali za Serikali na binafsi.

"Serikali imetukumbuka wanamuziki kwa kutupatia kadi za bima ya afya ya Taifa kwa gharama nafuu kupitia Tanzania Music Foundation (TAMUFO) jambo litakalo tusaidia wanamuziki kupata matibabu." alisema Joel. 

Joel aliwataja baadhi ya wanamuziki watakao kabidhiwa kadi hizo kuwa ni wa muziki wa Injili, bongo fleva, dansi, taarabu na ngoma za asili. 

Aidha Joel alisema kitendo cha Serikali kutoa kadi hizo za bima ya afya kwa wanamuzikini utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuwasaidia wasanii hapa nchini.

Katibu mkuu huyo wa TAMUFO alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuelezea kuwa wamepata ari na nguvu mpya  ya kutekeleza shughuli zao kwa vitendo kwa ajili ya maendeleo ya sanaa hapa nchini.

Alisema maandalizi yote ya kongamano hilo yamekwisha kamilika ikiwa na taratibu  za kuwapata wanamuziki. 

Joel aliongeza kuwa katika kongamano hilo maafisa kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na Maafisa Utamaduni na wadau wengine watakuwepo.

Thursday, January 28, 2021

KAMISHNA WA SKAUTI MKOA WA MBEYA AFANYA ZIARA WILAYANI

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Skauta Sadock Ntole  (wa pili kulia) akisalimiana na  Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Claudia Kitta alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo. Kutoka kushoto ni Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Godfrey Kawacha, Kamishna wa Skauti Wilaya ya Kyela, Skauta Scholastica Msigwa. na kulia ni Kamishna Msaidizi wa Skauti Wilaya ya Kyela, Skauta Ayubu Mwambete.

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Skauta Sadock Ntole, akisalimiana na  Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyasa English Medium, Mika Alinanuswe.
Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Skauta Sadock Ntole, akisalimiana na  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Keneth  Nsilano.
Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Skauta Sadock Ntole, akisalimiana na Kaimu Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Kyela, Leah  Katamba. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Skauti Wilaya ya Kyela, Skauta Ayubu Mwambete.

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Skauta Sadock Ntole, akisalimiana na Mkuu wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji wa Wilaya ya Mbarali, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Musa Nyagalu.
Kamishna wa Skauti Wilaya ya Kyela, Skauta Scholastica Msigwa, akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Keneth  Nsilano.
Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Skauta Sadock Ntole, akiwa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Kyela.


Na Dotto Mwaibale


KAMISHNA wa Chama cha Skauti Tanzania Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole amefanya ziara ya kikazi ya kutembelea wilaya zote za mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Ntole alisema lengo la ziara hiyo ilikuwa kukusanya takwimu za skauti kupitia kwa makamishna wa wilaya hizo pamoja na kujionea shughuli mbalimbali za kimaendeleo zinazo fanywa na skauti.

" Hii ni ziara ya kawaida ya kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na skauti katika maeneo yao kuanzia ngazi ya kundi" alisema Ntole.

Alisema katika ziara hiyo aliweza kukutana na viongozi mbalimbali wa wilaya hizo wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi na maafisa elimu kwani wamekuwa wakishirikiana na Skauti katika kutekeleza majukumu yao.

Kamishna Ntole aliwataja baadhi ya viongozi aliyokutana nao na kufanya nao mazungumzo ya kiutendaji kuwa  ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Afisa Elimu wa Shule za Msingi na Sekondari ambao walimuomba  kuendesha mafunzo kwa walimu, walezi  ili kuwajengea uwezo katika kusimamia miongozo na shughuli za kiutendaji katika skauti.

Alisema baada ya kuonana na viongozi hao alifanya ziara katika shule za msingi za Kyela na Nyasa na kuendelea na ziara  wilayani Mbarali.

Wednesday, January 27, 2021

TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 270

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda (katikati) akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha miezi mitatu Oktoba hadi Disemba 2020 mkoani hapa juzi.



 Na Dotto Mwaibale, Singida


TAASISI ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imeokoa zaidi ya shilingi 270.7 kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo mikopo umiza.

Akitoa taarifa ya utekelezaji kwa kipindi cha miezi mitatu Oktoba hadi Disemba 2020 Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Adili Elinipenda alisema Takukuru imeokoa shilingi milioni 270,079,600 ndani ya kipindi hicho kutoka maeneo mbalimbali.

Elinipenda alisema shilingi milioni 154,416,000 pekee zimeokolewa kutoka mikopo umiza, shilingi milioni 28,000,000 ziliokolewa kutokana na fidia ya maeneo ya wananchi yaliyotwaliwa kufanya shughuli za uchimbaji madini Wilayani Mkalama,wakati kiasi kingine kikiokolewa kutoka maeneo mengine ikiwemo mahakama ya Manyoni.

"Fedha hizi tulizikabidhi kwa wahusika baada ya kuokolewa ambapo fedha tulizoziokoa kutoka mikopo umiza, Mkuu wa Mkoa Dk Nchimbi aliwakabidhi wananchi hao wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani Manispaa ya Singida." alisema Elinipenda.

Alisema katika kuhakikisha Vitendo vya Rushwa vinaisha Takukuru kwa kushirikiana na wadau wengine imeendelea kutoa Elimu kwa jamii kwa kushirikisha makundi mbalimbali ikiwemo Vijana wa shule za msingi, Sekondari na Vyuo.

Aidha Elinipenda alisema Taasisi hiyo imeanzisha utaratibu wa Takukuru inayotembea (MOBILE PCCB) ambapo itatenga siku moja ndani ya mwezi ili kuwatembelea wananchi kwenye maeneo yao lengo la kufanya hivyo ni kusikiliza na kutatua kero zao.

Hata hivyo Taasisi hiyo inazidi kutoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Singida kujiepusha na Vitendo vya Rushwa huku ikiwataka kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa za Vitendo hivyo pamoja na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kutoa ushahidi mahakamani

Tuesday, January 26, 2021

RC NCHIMBI AWATAFAKARISHA WATENDAJI WA MAHAKAMA YA MIAKA 100, AAGIZA TAKUKURU KUANZA KUWAMULIKA “BUSH LAWYERS”

Mkuu waMkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akihutubia kwenye sherehe zamaadhimisho ya uzinduzi wa wiki ya sheria, kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Kiomboi juzi.
Nchimbi akiwa na viongozi mbalimbali w amahakama na serikali kwenye maadhimisho hayo
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Luhaula akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Dkt Rehema Nchimbi akihutubia kwenye sherehe za maadhimisho ya uzinduzi wa wiki ya sheria mwaka huu, kwenye viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida.
Mkuu wa Mkoa akitembelea moja ya banda la wadau wa mahakama linalojishughulisha na kazi za usaidizi wa msaada wa kisheria wilaya ya Singida.
Akiwa kwenyebanda la Jeshi la Magereza.
Akiwa kwenye banda la Watumishi wa Mahakama.
Baadhi ya Watumishi na Mahakimu wa Wilaya ya Iramba wakifuatilia matukio mbalimbali kwenye uzinduzihuo
Wananchi kutoka Taasisi na Asasi mbalimbali wakishiriki maadhimisho hayo
Mada mbalimbali zikiwasilishwa.

Sherehe zauzinduzi zikiendelea.

 



Na Godwin Myovela, Singida


MKUU waMkoawaSingida Dk. Rehema Nchimbi ameiagizaTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuanza mara moja msako wa kuwabaini na kuwachukulia hatua Mawakili na Mahakimu Umiza walioko mitaani maarufu‘Bush Lawyers’ ambao wamekuwa kikwazo kwa kushawishi, kuwatoza tozo kubwa na kuwavuruga raia ili wakatae, wakinzane au kutokukubaliana na mienendo halali ya kesi zinazoamriwa na mahakama kwa mujibu washeria.

Nchimbi alitoa agizo hilo kwa nyakati tofauti wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya sheria kwa Wilaya za Iramba na Singida juzi, huku akisisitiza kwa kuwataka Takukuru kuanza kuwatafuta na kuwashughulikia watu hao kwa mujibu wa sheria kama walivyofanikiwa kudhibiti Wakopeshaji Haramu.

“Haiwezekani hata kidogo tukaendelea kufumbia macho jambo hili. Hawa mawakili umizana mahakimu uchwara huko mtaani wanaumiza sanawatu…wanawadanganya na wakati mwingine kusababisha mienendo ya kesi kubadilika mara kwa mara, hawa ni wavurugaji wakubwa wa mashauri!” alisema Mkuu wa Mkoa.

Akitoa tafakuri na tathmini juu ya maadhimisho hayo kuelekea kilele cha siku ya sheria mwaka huu, na mantiki ya umri wa miaka 100 ya mahakama katika muktadha wa uwiano wa haki nchini, Nchimbi alianza kwa kusema miaka hiyo ni faraja, ni sherehe na ni kitu cha kujivunia.

Alisema kwenye michezo ya  burudani siku zote mashabiki wananafasi kubwa ya kucheza wakiwa nje ya uwanja kuliko hata wachezaji wenyewe, na wakati mwingine mashabiki hao hao wanasahau kwamba jukumu la timu linawahusu na wao pia, wanafikiri wapo nje ya uwanja hapana!..na wao wapo ndani.

Nchimbi alisema asili ya sheria ni Mungu mwenyewe. Au kwa maana nyingine Mungu ni Sheria. Kama mwanadamu atamtii Mungu basi atazitii, atazifahamu, atazipenda, atazienzi, ataziheshimu na kuziishi sheria.

Alisema kila kilichoumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu hapa duniani kimeumbwa kwa kufuata sheria. 

Mkulima hawezi kustawisha mazao na kupata mavuno mengi kama atavunjasheria. 

Mfugaji hawezi kumudu kufuga ipasavyo bila kufuata sheria, mvuvi vile vile na kadhalika. 

Viungo vyote vya mwili macho, moyo, utumbo, masikio, miguu na kila kitu kimewekwa na kipo pale kwa mujibu washeria.

Aliwahamasisha Watendaji wa Mahakama kuongeza kasi ya kutoa elimu ili jamii ijue na kuzingatia sheria kwa ustawi wa haki na wajibu. 

“Pia watu wafahamishwe kuwa haya mambo ya kesi hayana shortcut (njiazamkato) nilazima jamii izingatie utii wa sheria bila shuruti kwa faida ya wewe, yule na mimi-kiusalama na kwa ustawi wa maendeleo.”

“Ikiwezekana hata Jeshi la Magereza nalo natamani siku moja livunje ule ukuta wa gereza kwa kuwachukua na kuwapeleka wafungwa hao wakiwa hivyo hivyo na sare zao kuchanganyikana na raia kwenye makanisa, misikiti na mashuleni ili watu na jamii ione kwa macho, iguswe na kujifunza madhara ya kubaka, kulawiti, kuiba, rushwa na aina nyingine ya makosa endapo mtu atavunja sheria,” alisema

 

Nchimbi alisema mahakama au kutimiza miaka 100 bado haitoshi kama watu hawatazipenda, hawata zingatia na kuziishi sheria. 

Ifike mahali tujiulize mathalani hata unapoajiriwa au kujiajiri ili kila jambo liende sawa sawa na kwa utaratibu mzuri ni lazima mahali hapo pawekwe sheria. Miaka hii100 itutafakarishe na kutuongoza kutathmini  kama taifa kwanini sheria? inamhusunani? na kwanini miaka 100 ya kutafsiri sheria? 

Na kwa muktadha huo, mchango wa mahakama katika Ustawi wa Tanzania ya amani, uhuru, udugu, demokrasia bora, utawala wa sheria, ustawi wa uchumi utaonekana kudhihirika…na mashabiki walio nje ya uwanja wataunga na nawachezaji, sote tutajiona tupo ndani ya uwanja, tutajiona ni sehemu ya mchezo husika, na tutazingatia.

Maadhimisho ya wiki ya sheria mpaka sasa yanaendelea kwenye maeneo mbalimbali katika wilaya mbalimbali za mkoa wa Singida kwa kwa watumishi na wadau mbalimbali wa mahakama kutoa elimu na huduma za msaada wa kisheria, sambamba na kutathmini kwa pamoja dhima kuu ya mwaka huu isemayo“Miaka 100 ya Mahakama Kuu: Mchango wa Mahakama katika kujenga nchi inayozingatia uhuru, udugu, amani na ustawi wa wananchi.”

WAZIRI BASHUNGWA KUTOA KADI ZA MATIBABU KWA WANAMUZIKI

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Stella Joel.
 


Na Dotto Mwaibale


WAZIRIa wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) litakalofanyika Februari 13, 2021 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stella Joel alisema pamoja na mambo mengine Bashungwa atatoa  kadi za Bima ya Afya ya NHIF kwa Wanamuziki pamoja na kusikiliza changamoto zao mbalimbali ili kuzipatia ufumbuzi.

"Serikali imetukumbuka wanamuziki kwa kutupatia kadi za bima ya afya ya Taifa kwa gharama nafuu kupitia Tanzania Music Foundation (TAMUFO) jambo litakalo tusaidia wanamuziki kupata matibabu." alisema Joel. 

Joel aliwataja baadhi ya wanamuziki watakao kabidhiwa kadi hizo kuwa ni wa muziki wa Injili, bongo fleva, dansi, taarabu na ngoma za asili. 

Aidha Joel alisema kitendo cha Serikali kutoa kadi hizo za bima ya afya kwa wanamuziki ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. John Magufuli ya kuwasaidia wasanii hapa nchini.

Katibu mkuu huyo wa TAMUFO alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuelezea kuwa wamepata ari na nguvu mpya  ya kutekeleza shughuli zao kwa vitendo kwa ajili ya maendeleo ya sanaa hapa nchini.

Alisema maandalizi yote ya kongamano hilo yamekwisha kamilika ikiwa na taratibu  za kuwapata wanamuziki. 

Joel aliongeza kuwa katika kongamano hilo maafisa kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na maafisa utamaduni na wadau wengine watakuwepo.

SKAUTI JIJINI MBEYA WAKARABATI MAENEO YALIYO ATHIRIWA NA MAFURIKO

Vijana wa Chama cha Skauti Mkoa wa Mbeya wakikarabati kivuko cha watembea kwa miguu  katika Mtaa wa Mayombo Kata ya Iwambi baada ya kuharibiwa na mafuriko.

Vijana wa Chama cha Skauti Mkoa wa Mbeya wakiwajibika.



Vijana wa Chama cha Skauti Mkoa wa Mbeya wakisafisha mitaro

Kazi ikiendelea.
Kazi ikiendelea.
 



Na Dotto Mwaibale


 KUTOKANA  na mvua zinazo endelea kunyesha Mkoa  wa Mbeya na kuharibu miundombinu ya barabara Chama cha Skauti mkoani humo kimeendelea kutoa huduma ya kukarabati miundombinu hiyo kwa wathirika wa mafuriko.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Kamishna wa Skauti  Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole alisema  mvua iliyonyesha Januari 23 mwaka huu ilileta athari kubwa kSatika Kata ya Iwambi na kuharibu miundombinu mbalimbali.


Alisema kufuata hali hiyo walikaa na kuratibu namna ya kufika katika maeneo hayo kutoa msaada ambapo kikosi cha uokoaji cha skauti wapatao 16 walikwenda kutoa huduma ya kusafisha  mitaro na makaravati. 

 " Mafuriko hayo yalisababisha athari za kubomoa kuta za nyumba za wakazi wa tatu wa eneo hilo na kuharibu vivuko vya watembea kwa miguu na kuleta changamoto ya matumizi ya barabara kwa wakazi  na wanafunzi waishio mtaa wa Mayombo na mitaa jirani ambao wanasoma katika Shule ya Sekondari Sinai, Nsenga, Maziwa, Stella Farm na Shule ya mmMsingi ya Iwambi."  alisema Ntole. 

Mratibu wa Majanga, Uokoaji  na Hali hatarishi wa chama hicho mkoani humo, Lusajo Sanga alisema kazi hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na ushirikiano kutoka kwa viongozi wao.

Alisema kazi kubwa walioifanya ilikuwa ni kurekebisha miundombinu ya kupitisha maji ambayo ilijaa taka na kusababisha maji kutoka nje ya mkondo wake na kuingia kwenye makazi ya watu na kujenga  vivuko vya waenda kwa miguu. 

Alisema kazi hiyo walifanya kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Mayombo akiwepo Mwenyekiti  Philipo Mbembati, Mjumbe wa mtaa huo, James Ngungula pamoja na wakazi wa eneo hilo.

Sanga aliwataja skauti walioshiriki kazi hiyo kuwa ni Kamishna wa Skauti Mkoa Mbeya, Sadock Ntole, Mratibu wa Habari na Mawasiliano Mkoa Mbeya Barnaba Moses, Waratibu wa Skauti Wilaya ya Mbeya, Baraka Martin, Emanuel Mwasikili na Stephano Mwangosi.

Aidha Sanga aliwataja kwa majina  skauti waliounda kikosi kilichoshiriki kufanya kazi hiyo kuwa ni Evaristo Sanga, Glory Augustino, Beckam Frank, Elika Mwakabana, Skauta Macklin Lamsi, Elisha, Ckelvi Ekela, Bambo Ekela na Ali.

Sanga alitumia fursa hiyo kusema kwamba Skauti mkoani humo wapo tayari kutoa huduma kwa jamii pamoja na elimu ya jinsi ya kuepukana na athari zitakazotokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa  huo.

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock  Ntole alitoa rai kwa wananchi na wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya kuchukua tahadhari na kuhakikisha miundombinu ya mitaro na makaravati inayopitisha maji inakuwa Safi na salama wakati wote ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi katika mkondo wake ambapo pia aliwasisitiza wanaozalisha taka wazipeleke kwenye maghuba  sahihi ya kuhifadhia ili kurahisisha ubebaji wa taka hizo na kuzipeleka kwenye dampo kuu.

Monday, January 25, 2021

NAIBU WAZIRI SILINDE AAGIZA TSC IPEWE OFISI ZENYE HADHI

 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), mjini Morogoro, Januari 25, 2021. Wengine kutoka kulia ni Mwenyekiti wa TSC Profesa Willy Komba, Kaimu Katibu wa TSC Moses Chitama na Katibu wa Baraza husika, Lawrence Chankani.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde (kushoto), akisalimiana na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Profesa Willy Komba, muda mfupi baada ya Naibu Waziri kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TSC, mjini Morogoro, Januari 25, 2021. Katikati ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Willy Komba (kulia), akitoa hotuba ya ukaribisho wa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde (katikati), wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo, Januari 25, 2021 mjini Morogoro. Kushoto ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume hiyo, uliofanyika Jaunuari 25, 2021 mjini Morogoro. Katikati ni Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde na kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Profesa Willy Komba.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde (wa tatu – kulia), akiungana na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kuimba wimbo maarufu wa ‘Solidarity Forever’. Naibu Waziri alifungua Mkutano huo mjini Morogoro, Januari 25, 2021. Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba na kulia kwake ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde (hayupo pichani) wakati akifungua Mkutano huo mjini Morogoro, Januari 25, 2021.

Mjumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Abihudi Hemba akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Baraza hilo kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde (hayupo pichani) baada ya kufungua Mkutano huo mjini Morogoro, Januari 25, 2021.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde (katikati-waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), muda mfupi baada ya kufungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakzi wa Tume hiyo Januari 25, 2021 mjini Morogoro. Kushoto kwa Naibu Waziri ni Mwenyekiti wa TSC, Profesa Willy Komba na kushoto kwake ni Kaimu Katibu wa TSC, Moses Chitama.

************************************************

 

Na Veronica Simba – TSC

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde amewaagiza Wakurugenzi wa Wilaya kote nchini, kuhakikisha wanawapatia ofisi zenye hadhi, watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) katika maeneo yao.

Ametoa maagizo hayo leo, Januari 25, 2021 mjini Morogoro wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume.

Naibu Waziri ametoa maagizo hayo baada ya kuelezwa changamoto mbalimbali zinazoikabili Tume husika, ambapo mojawapo ni ya ukosefu wa ofisi zenye hadhi kwa watumishi wa TSC hususani zilizoko katika baadhi ya Wilaya nchini.

“Nitumie fursa hii kuagiza Wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanawapatia Makatibu Wasaidizi wa Tume, ofisi ambazo zinaendana na hadhi ya utumishi wa umma.”

Aidha, ameitaka Tume kuhakikisha inawawezesha Walimu kujitambua na kuelewa sheria, kanuni, taratibu, haki na wajibu wao.

Vilevile, ameipongeza Tume kwa kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kwa moyo wa uzalendo, pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili. Pamoja na kutoa pongezi, ameitaka Tume kuendelea kutoa huduma bora kwa Walimu.

“Sote tunafahamu kuwa tunapotoa huduma bora kwa Mwalimu inamwezesha kutekeleza majukumu yake shuleni kwa ufanisi hatimaye kuinua kiwango cha elimu nchini.”

Naibu Waziri ameihakikishia Tume kuwa ushirikiano uliopo katika utendaji kazi kati ya Tume na Ofisi ya Rais – TAMISEMI ni endelevu. Aidha, ameongeza kuwa Ofisi yake itaendelea kusisitiza kila Wilaya kuhakikisha kazi za kushughulikia masuala ya kiutumishi ya Walimu zinatekelezwa kwa ushirikiano ili kuleta tija na ufanisi katika suala zima la kuwahudumia walimu.

Awali, akiwasilisha hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Tume, Profesa Willy Komba alibainisha changamoto kadhaa zinazoikabili, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na jengo la Ofisi za Tume Makao Makuu na Wilaya.

Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya waajiri kutokuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kushughulikia masuala ya kinidhamu ya Walimu.

“Mfano kuchelewa kuwasilisha mashtaka kwa Mamlaka ya Nidhamu, kuchukua jukumu la kutoa adhabu kinyume cha utaratibu na kuwaondoa Walimu kwenye mfumo wa malipo kabla ya mchakato wa mashauri kuanza na kukamilika,” amefafanua Profesa Komba.

Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa pia na Kaimu Katibu wa Tume, Moses Chitama, Menejimenti ya Tume pamoja na wawakilishi mbalimbali kutoka wilaya zote nchini.

Tume ya Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari za Serikali, Tanzania Bara. Naibu Waziri David Silinde ndiye amepewa wajibu wa kusimamia Taasisi hii pamoja na nyingine zilizo chini ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI.

KAIMU AFISA VIJANA MKOA WA SINGIDA FREDERICK NDAHANI AISHAURI SERIKALI KUFUFUA SHULE ZA UFUNDI

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (wa pili kushoto) akizungumza na Walimu wa Ufundi  wa Shule ya Msingi Makiungua iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida alipoitembelea juzi kwa lengo la kukagua uwezeshwaji mafunzo na ujuzi kwa vijana.

Madawati yakitengenezwa. na Shule ya Msingi Makiungu iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Madawati yaliyotengenezwa.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (kulia) akikagua utengenezaji wa madawati.
Madawati yaliyotengenezwa.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida.


KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa,  Frederick Ndahani ameishauri Serikali kufufua Shule za Msingi za ufundi Nchini. 

Ndahani alitoa ushauri huo juzi alipotembelea  Shule ya Msingi Makiungu iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kwa lengo la kukagua uwezeshwaji mafunzo na ujuzi kwa vijana.

Ndahani alisema Shule ya Msingi Makiungu ni moja ya shule zilizofanya  vizuri katika mradi waliopewa wa kutengeneza madawati 1000  ya shule za msingi zilizopo wilayani humo.

Ndahani alisema shule hiyo ya mchepuo wa ufundi   ni moja ya shule inayoifanya vizuri na kusababisha ofisi ya mkurugenzi wa wilaya ya  Ikungi kuwapa kazi ya kutengeneza madawati hayo.

" Shule hizi za mchepuo wa ufundi hapa nchini zikiboreshwa zinaweza kusawaidia vijana wa kitanzania kupata ujuzi wa ufundi mbalimbali." alisema Ndahani.

Alisema  wanafunzi wanaojiunga katika shule hiyo hapa ni wale ambao wamekosa nafasi ya kuendelea na elimu ya sekondari na vyuo na kuwa faida wanayoipata ni kupata mafunzo hayo ya ufundi bure  kama ilivyo elimu ya msingi.

Alisema  kuboreshwa kwa shule  hizo kutasaidia kupata mafundi ambao watatumika kukarabati samani mbalimbali zilizopo mashuleni badala ya kuwapa mafundi kutoka nje ambao watahitaji kulipwa fedha nyingi.

Kwa upande wao  Walimu wa Ufundi katika shule hiyo Cosmas Uhiku na  Haji Kidabu Wameiomba Serikali kuwapatia vifaa vya kutosha kwani wanao uwezo wa kuwapatia vijana mafunzo ya kisasa  sanjari na vyeti baada ya kumaliza mafunzo kwa muda wa miaka miwili.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo  Hashimu Ntandu amemshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa kuwapatia mradi huo mkubwa wa kutengeneza madawati ambapo wanatengeneza kwa gharama nafuu.


WADAU WA TIBA ASILI WATAKIWA KUCHANGAMKIA SOKO LA DAWA ZAO KIMATAIFA

  Mkurugenzi msaidizi wa tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt. Paul Mhame akitoa hotuba ya uzinduzi wa jukwaa hili.

Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa utawala na fedha Prof. Amandus Mhairwa akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzindua rasmi jukwaa.

Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko akitia neno kwa wagana hao wa tiba asili na wadau wengine wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo.

Mkuu wa mradi huo wa GRILI Dkt. Faitha Mabiki akieleza kwa kifupia majukumua na malengo ya mradi huo wa GRILI na yale ambayo yamefanyika toka mradi uanzishwe.

  

Wadau wa tiba sili na tiba mbadala kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania wakifuatilia hotuba na maneno ya uzunduzi wa Jukwaa lao kutoka kwa viongozi.


Na Calvin Gwabara,   Morogoro.

Wataalamu wa chuo kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wametakiwa kushirikiana na wataalamu wa tiba asili na taasisi zingine katika kufanya tafiti za dawa ambazo zitasaidia dunia katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa COVID 19 na magonjwa mengine hatari kwa afya ya binadamu,Wanyama na hata mimea kwani  takwimu nchini Tanzania zinaonyesha tiba asili  inatoa mchango wa zaidi ya asilimia 45 katika unga wa matibabu.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi msaidizi wa tiba asili na tiba mbadala kutoka wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dkt. Paul Mhame kwa niaba ya Katibu mkuu wa wizara hiyo wakati wa ufunguzi wa jukwaa la ubunifu la wadau wa tiba asili Tanzania uliofanyika SUA mkoani Morogoro.

Dkt.Mhame amesema kuwa Tiba asili inayo nafasi kubwa katika kukabiliana na magonjwa hayo ikiwa ni pamoja na kutafuta namna ya kuzuaia na kutibu na ndio maana kuna sheria ya tiba asili na tiba mbadala Na.23 2002.

“Upatikanaji a tiba asili na tiba mbadala inayotokana na mimea dawa itasaidia sana kufikia wananchi wengi hasa wanaoishi vijijini hivyo nimefurahishwa na malengo ya jukwaa hili kwani yanaendana na malengo ya serikali kupitia wizara yetu hii ya afya ya kuhakikisha tunaboresha afya za wananchi wetu kupitia za kisasa na tiba asili” Alisema Dkt. Mhame.

Amefafanua kuwa biashara ya tiba asili duniani inakuwa kwa kasi sana kwani kwa takwimu za shirika la fya duniani WHO zinasema mwaka 2000 mauzo yake yalikuwa dola za kimarekani bilioni 20,mwaka 2012 ilipanda na kufikia dola za kimarekani bilioni 60,Mwaka 2018 ikafikia dola bilioni 80 na sasa inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 mauzo ya tiba asili yatafikia dola za kimarekani trilioni 3.

“Kwahiyo niwaombe sana ndugu zangu watafiti wa SUA na waganga wa tiba asili nchini kushirikiana ili kusaidia kujipanga vizuri ili Tanzania nayo inufaike kama China na nchi zingine duniani kwenye mauzo ya dawa za tiba asili wakati yakielekea kufikia Trilioni 3” Alisistiza Dkt. Mhame.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi huyo kuzindua jukwaa hilo Naibu Mkamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa utawala na fedha Prof. Amandus Mhairwa kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda amesema lengo la jukwaa hilo ni kuibua ubunifu nna kutatua changamoto zilizoko kwenye mnyaroro wa thamani wa biashara ya bidhaa za miti mimea dawa Tanzania ili iweze kuwa endelevu na kutoa mchango mkubwa kwenye kipato cha Wananchi na Tanzania kwa ujumla.

“Malengo ya Chuo chetu pia yanahusisha uendelezaji wa maarifa na ujuzi,bunifu,busaraza kitaalamu na uelewa kupitia mafunzo,matokeo ya tafiti,huduma za ugani  na ushauri wa kitaalamu na katika uzalishajiu  hivyo tunaamini kuwa uratibu wetu wa kuanzisha jukwaa hili uko kwenye mojawapo ya majukumu yetu na malengo ya uanzishwaji wa chuo chetu” Alifafanua Prof. Mhaurwa.

Aliongeza kuwa SUA kupitia watafiti wake kwenye mradi huu wamefanya tafiti nyingi ambazo zimeonesha kuwa kuna changamoto nyingi kwenye mnyororo mzima wa thamani wa biashara ya tiba asili na mimea dawa hasa ubunifu mchache unaoibuliwa kwenye biashara hii,SUA imeona ni vyema kutumia uzoefu wake wa ndani kwa kushirikiana na wadau wengine kuratibu uanzishwaji wa jukwaa hili.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko amewataka waganga hao wa tiba asili kuendelea kushirikiana na ofisi yake katika kupima viambata mbalimbali vinavyopatikana kwenye dawa zao ili kusaidia kuepusha madhara yoyote yanayoweza kutokea kwa wateja wao endapo dawa itakuwa na viambata ambavyo sio salama.

“Kazi ya ofisi yangu sio kuzuaia nyinyi kupata usajili wa dawa zenu bali tunataka kuona kila dawa mnayoitoa kwa wagonjwa iwe na viambata sahihi ili iweze kutibu vizuri na isilete madhara kwa wateja wenu lakini pia upimaji wetu ndio wa mwisho ili muweze kupata usajili wadawa tukiweka sahihi yetu kuwa dawa iko salama hakuna wa kupinga hivyo msiogope tushirikiane” Alisema Dkt. Mafumiko.

Mkemia mkuu huyo wa serikali alisema kuwa malengo ya waganga wa tiba asili na malengo ya ofisi yake ni moja tuu kuhakikisha usalama wa wananchi na watumiaji wa dawa hizo na ofisi yake inavyo vifaa na wataalamu wa kutosha kubaini kila kilicho kwenye dawa hivyo wale wachache wanaofanya udanganyifu waache maana watabainika.

Pia Dkt. Mafumiko ameipongeza SUA na watalaamu wake kwa jitihada kuwa wanazozichukua katika kuwasaidia waganga hao wa tiba asili kuweza kuboresha huduma ya tiba wanayoitoa kwa Jamii ili iweze kuwa bora na yenye viwango vinavyohitajika.

Mkemia mkuu huyo wa Serikali iliahidi kushirkiana na SUA kwenye mpango huo ili uweze kuleta tija inayokusudiwa kwa jamii na taifa kupitia wataalamu wa ofisi yake muda wowote watakapohitajika.

Kwa upande wake Mkuu wa mradi huo wa GRILI Dkt. Faitha Mabiki alisema kuwa toka mradi huo uanze mwaka 2018 umekuwa na mafanikio makubwa kwa wadau wa tiba asili Tanzania nab ado unaendelea kushirikiana nao kuhakikisha biashara ya tiba asili na mimea dawa inachangia uchumi wa wadau hao na taifa.

“ Wakati tunaanza mradi huu mwaka 2018 waganga wengi hapa wa tiba asili walikuwa wanauza dawa zao kwenye mkifuko ya Rambo,magunia na vifungashio vingine visovyo na ubora lakini tunafurahi leo wakati tunazindua jukwaa hili tunaona wote wameweka dawa kwenye vifungashio bora na vye viwango vinavyokubalika kitaalamu.”Alisema Alifafanua Dkt. Mabiki.

Aliongeza “Lengo letu ni kutaka kuona biashara ya mimea dawa na uuzaji wa dawa za asili haufanyiki tuu hapa nchini bali wataalamu hawa wa tiba asili waweze kufungasha vizuri na kuuza hadi nje ya nchi na kupata mapato wao wenyewe lakini pia na taifa kama ambavyo ilivyo kwa nchi nyingine duniani kama China na India”.

Dkt. Mabiki alisema ili hilo lifanikiwe pia lazima kuwe na uendelevu wa upatikanaji wa mimea dawa hiyo ili pale inapohitajika kwa wingi iweze kupatikana na ndio maana mradi unawafundisha namna ya kuanzisha mashamba ya mimea dawa ili waweze kulima na kuipata kwa wingi na kirahisi pale inapohitajika.