Tuesday, October 27, 2020

CCM SINGIDA KUIBUKA NA USHINDI WA KISHINDO

Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dodoma baada ya kuhitimisha kampeni zake za uchaguzi 

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Hassan Kilimba akiwa katika moja ya mikutano ya kampeni Tarafa ya Makiungu mkoani hapa. 


Na Godwin Myovela, Singida


MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani hapa Alhaji Juma Hassan Kilimba amesema kwa idadi ya kura zote zitakazopigwa kwa nafasi ya Udiwani, Ubunge na Rais, chama hicho kinatarajia kuibuka na ushindi wa asilimia 83.75

Akitoa ufafanuzi mbele ya vyombo vya habari jana, Kilimba alisema kwa kuanza na madiwani CCM ilisimamisha viti vyote 136, na kati ya hivyo viti 35 vilipita bila kupingwa hatua iliyokifanya chama hicho kubaki kikishindania viti 101 vya nafasi hiyo pekee.

Kilimba alisema kwa upande wa Ubunge walifanikiwa kusimamisha wagombea wote 8 kwa idadi ya majimbo yaliyopo, na katika siku zote 60 za Kampeni, kuanzia Septemba walipoanza mpaka sasa wamemaliza salama, hakukuwa na tatizo lolote.

Kada huyo wa CCM alisema katika kipindi chote cha kampeni walifanikiwa kuwa na mikutano mikubwa ya kitaifa 34, ambapo kati yake mgombea wa nafasi ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli alikuja mkoa wa Singida na kufanya mikutano ya hadhara 7, huku Mgombea Mwenza Samia Suluhu Hassan akifanya mikutano ya hadhara mitano.

Mwenyekiti huyo wa CCM alisema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mjumbe wa Kamati Kuu alifanya mikutano ya hadhara 3, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye mkutano 1, Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mikutano 4, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mlezi wa CCM Mkoa Munde Tambwe mikutano 4.

Wengine ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Dk Bashiru Ally mikutano 8, na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Hery James mikutano 2, idadi iliyopelekea jumla ya mikutano yote ya viongozi wa kitaifa kufikia 34, idadi ya mikutano ya wabunge 8,050, huku Mwenyekiti pamoja na Kamati yake ya Siasa ya Mkoa wakifanya jumla ya mikutano ya hadhara 217.

Kilimba akizungumzia takwimu za awali za stratejia za ushindi kwa upande wa Madiwani, alisema katika kata 136 zilizopo ndani ya mkoa wa Singida…madiwani wamefanikiwa kufanya mikutano ya hadhara 560, idadi ambayo ikijumlishwa na ile mikutano ya ndani kimkoa jumla yake kuu inafikia mikutano 13,520.

Alhaji Kilimba akitoa tathmini hiyo alisema baada ya juhudi kubwa za kampeni kufanyika, ikiwemo mabalozi, madiwani na wabunge kutumia njia ya ‘nyumba kwa nyumba’ hatimaye chama hicho kimeweza kufanikiwa kuifikia idadi yote ya watu 36, 300 mkoani hapa waliojiandikisha kupiga kura.

Kulingana na vyanzo vilivyopo kutoka CCM Singida na Tume ya Uchaguzi, mpaka sasa idadi ya waliojiandikisha mkoani hapa imefikia 848, 833, huku idadi ya wanaotarajia kupiga kura ikifikia laki 7, 44,762.

“Sasa ukitazama mkoa wetu wa Singida tuna wanachama wa CCM laki tatu, arobaini na mbili elfu, mia tano sabini na saba (3,42,577) ambao ni zaidi ya nusu ya wapiga kura wote…” alisema Kilimba.

Hata hivyo, aliongeza kwamba kupitia mikutano hiyo ambayo tulifanikiwa kunadi sera na Ilani yetu kwa Mama Ntilie, Machinga, Waendesha Bajaji na Bodaboda, Vijana, Wazee, Wenye Ulemavu na Wachimba Madini, CCM mkoani hapa mpaka kumalizika kwa ngwe ya mbio hizo za uchaguzi 2020, imeweza kuwafikia wapiga kura zaidi ya milioni 1, yaani (1, 234,540).

 “Matarajio kwa ushindi wa ujumla, kura za Rais tutakuwa na uhakika wa kupata asilimia 92.5, ubunge kwa wagombea wote asilimia 100, na Madiwani asilimia 94.375….lakini kwa idadi ya kura zote baada ya kujumlishwa CCM Singida tutakuwa na asilimia 83.75,” alisema Kilimba.

MARAIS WASTAAFU WAOMBWA KUMSHAURI RAIS MAGUFULI KUTUVUSHA SALAMA UCHAGUZI MKUU UTAKAO ANZA KESHO

Askofu Kiongozi wa Kanisa la  Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila (kulia) akiongoza maombi maalumu ya kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho.
Askofu Kiongozi wa Kanisa la  Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila (kulia) akiongoza maombi hayo maalumu.
Muumini wa kanisa hilo, Mariam Luvanda akiombea nchi amani katika maombi hayo.

Maombi yakiendelea.

Muumini wa kanisa hilo Daniel Hezron Mpemba akiomba kwa hisia kali katika maombi hayo.

Mama Askofu, Janeth Ndabila akiomba kwenye maombi hayo. 

Maombi yakiendelea.

Mzee Gerald Enock akiomba huku akililia amani ya nchi isipotee wakati huu wa mchakato wa kupiga kura.

Maombi yakiendelea.
Maombi yakiendelea.
Waumini wa kanisa hilo wakiomba huku wakililia amani isipotee wakati wa kupiga kura.
Maombi yakiendelea.
Katibu wa kanisa hilo, Jane Magigita (kushoto) akiomba katika maombi hayo. Kulia n Muumini wa kanisa hilo, Mariam Luvanda..





 Na Dotto Mwaibale

MARAIS wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu , Masipika, mke  wa Rais Mama Janeth Magufuli, Wazee pamoja na Viongozi wa dini wameombwa kwa busara na hekima walizo nazo kumshauri Rais Dkt. John Magufuli ili aweze kuivusha salama nchi yetu  katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu utakaofanyika kesho.

Ombi hilo linetolewa Jumapili na Askofu Kiongozi wa Kanisa la  Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila wakati wa maombi maalumu ya kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu kesho.

Akihubiri katika maombi hayo Ndabila alisema wameamua kufanya maombi hayo kwa sababu mara nyingi unapofanyika uchaguzi kunakuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuashiria uvunjivu wa amani na utulivu wa nchi yetu.

"Baba pekee tunaye mtegemea kutuvusha salama katika uchaguzi huu ni Rais wetu Dkt. John Magufuli ambaye kikatiba bado ni Rais licha ya kwamba kesho tutapiga ya kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani." alisema Ndabila.

Alisema katika chaguzi nyingi duniani zimekuwepo changamoto kadhaa na ndio maana akawaomba viongozi hao wastaafu kumshauri Rais Magufuli azidi kuwa imara ili atuvushe salama katika uchaguzi huu kama alivyotuvusha katika kipindi kigumu cha ugonjwa wa Covid 19 na ndio maana wao kama kanisa wamefanya maombi hayo ikiwa ni kukumbushana kuitunza amani kuanzia kesho siku ya kupiga kura na siku za kuhesabu kura hadi kumpata Rais, Wabunge na Madiwani.

 "Kanisa lina hekima ya kuvielekeza vyama vya siasa, viongozi wastaafu na makundi mengine kwa njia ya maombi ili viwe na busara ya kulinda amani pasipo kuharibu  utulivu wa nchi uliopo." alisema Ndabila.

Ndabila aliwapongeza wagombea wa vyama vya siasa kwa kuonesha kuilinda amani ya nchi katika kipindi chote cha kampeni licha ya kuwepo changamoto ndogo ndogo na akaviomba vyama hivyo viendelee kufanya hivyo na kesho.

Alisema jambo linalo mpa amani ya kupiga kura kesho kwa amani ni kila mgombea alipokuwa kwenye kampeni jinsi walivyokuwa wakimtangulinza Mungu kabla ya kuanza mikutano yao.

Ndabila alisema amani inapokosekana wa kulaumiwa ni viongozi wa dini kwa sababu ndiyo wenye wajibu wa kuhamasisha waumini wao kumuomba Mungu atuepushe na uvunjifu wa amani wakati wote.

"Wagombea wote ni watoto wa Mungu hivyo wanapaswa kumtii Mungu ili wasilete machafuko katika nchi yetu," alisema Ndabila.

Ndabila aliomba hekima iongoze Tume ya Taifa ya Uchaguzi itende haki, hekima iviongeze vyama vya siasa, hekima iviongoze vyombo vya usalamau na tuazimie kuto watoa watanzania kafara na kupoteza maisha ya mtanzania hata mmoja.

"Niwasihi viongozi wenzangu wa kidini pamoja na maombi mengi tunayoendelea nayo tunajukumu la kuwaondolea hofu watanzania na kusimama kwenye nafasi zetu kama wapatanishi. Imeandikwa her wapatanishi (Mathayo 5:9) na Mungu atatujalia kwa maombi yetu na hekima zetu kwa kushirikiana na Rais wetu aliyepo sasa kuivusha Tanzania kwa amani na salama." alisema Ndabila.

Katibu wa kanisa hilo,  Jane Magigita aliwahimiza waumini wa kanisa hilo na wananchi waliokuwepo kwenye maombi hayo kujitokeza kesho kwenda kupiga kura ya kumchagua Rais, wabunge pamoja na madiwani  na akawaomba watanzania kuombea uchaguzi huo ili Mungu atujalie kuwapata viongozi watakaoliongoza vema Taifa letu la Tanzania. 

"Kila muumini na mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura kesho ajitokeze na kadi yake akapige kura katika kituo alicho jiandikisha ili kutimiza haki yake ya msingi na ya kikatiba." alisema Magigita. 

Aidha Magigita alisisitiza umuhimi wa kila mtanzania kuzingatia misingi ya amani na utulivu wakati mchakato huo wa kupiga kura ukiendelea, ikiwemo kufika mapema kituoni na kuondoka kuelekea kwenye majukumu mengine baada ya kupiga kura kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kuepusha madhara au viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza.

Monday, October 26, 2020

RAIS MAGUFULI AWAFUTA MACHOZI WALIMU NA WASTAAFU WALIONYANG'ANYWA ‘ATM CARD,’ KUTOZWA RIBA BILA HURUMA

Mkuu wa Mkoa wa Singida (RC) Dkt Rehema Nchimbi akimkabidhi Mwalimu Mstaafu kutoka Wilaya ya Singida  Amosi Njoghomi kiasi cha shilingi milioni 18.8 zilizookolewa kutoka kwa mmoja wa wakopeshaji wa ‘Riba Umiza.’ Mwalimu Njoghomi alikopa shilingi milioni 2, lakini mkopeshaji alimtaka arejeshe fedha taslimu shilingi milioni 31 hadi serikali ilipoingilia kati na kumsaidia. 

Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida, Suzan Shesha (kulia) akishuhudia tukio la Mwalimu Njoghomi kukabidhiwa pesa zilizookolewa. Kushoto ni Mwenyekiti Mstaafu wa CWT mkoa wa Singida, Aran Jumbe.
Familia ya Mwalimu Mstaafu Albert Mpahi ikipokea kiasi cha shilingi milioni 2 zilizookolewa kutoka kwa moja ya Kampuni za Mikopo zisizofuata utaratibu. Mwalimu Mpahi alikopa shilingi milioni 7.2 na mkopeshaji wake akamtaka arejeshe fedha taslimu Shilingi Milioni 17 hadi serikali ilipoingilia kati.
RC Nchimbi akimkabidhi Mwalimu Mstaafu kutoka Wilaya ya Ikungi  Gerase Mshumbusi kiasi cha shilingi milioni 13 zilizookolewa kutoka kwa mmoja wa wakopeshaji wa ‘Riba Umiza.’ Mwalimu Mshumbusi alikopa shilingi milioni 3.5, lakini mkopeshaji alimtaka arejeshe fedha taslimu shilingi milioni 17 hadi serikali ilipoingilia kati na kumsaidia.
Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Singida Suzan Shesha (kushoto) akishuhudia tukio la Mwalimu Gerase Mshumbusi kukabidhiwa pesa zilizookolewa. Kulia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CWT mkoa wa Singida, Aran Jumbe.
RC Nchimbi akizungumza na wadau mbalimbali kutoka kwenye mabenki, Taasisi, Maafisa Utumishi, watu binafsi na Kampuni za Mikopo kutoka mkoa wa Singida kabla ya zoezi la kurudisha fedha zilizookolewa.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, akitoa taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba 2020.
Wadau wakifuatilia mkutano huo .
Mkutano ukiendelea.
Maombi na Dua maalumu kupitia mkutano huo vikifanyika kwa lengo la kuliombea Taifa la Tanzania na watu wake.
Maombi yakiendelea.
Familia ya Mwalimu mstaafu Albert Mpahi muda mfupi baada ya kukabidhiwa shilingi milioni 2 zilizookolewa na serikali.


 Na Godwin Myovela, Singida


RAIS John Magufuli amewafuta machozi walimu, wastaafu na baadhi ya wananchi mkoani hapa kwa kuokoa na hatimaye kuwakabidhi mali na fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni 82 walizokuwa wametapeliwa kupitia Kampuni za Mikopo zinazoendesha shughuli zake kinyume na utaratibu.

Mkuu wa Mkoa Dk Rehema Nchimbi, kwa niaba ya Rais, amewakabidhi kiasi hicho cha fedha waathirika wote waliopitiwa na wimbi hilo, maarufu ‘Mikopo Umiza,’ ofisini kwake leo.

“Ni Serikali hii ya Magufuli ndio iliyofanikisha kuwabana hawa wakopeshaji haramu na hatimaye leo walimu wangu na ninyi watumishi wenzangu mnakabidhiwa haki yenu iliyokuwa imeporwa, tuendelee kumshukuru Rais kwa mema haya anayoendelea kutufanyia,” alisema Nchimbi na kuongeza:

“Rais Magufuli mda mrefu alishakampeniwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe kupitia Corona, kama Mungu alipitishia kwake ile neema, maono na uwezo ule wa kusimama bila kutetereka, mimi Rehema Nchimbi ni nani hata nisiendelee kumsifu?” alihoji.

Akiwasilisha taarifa ya fedha zilizookolewa kutokana na Riba Umiza katika kipindi cha Julai hadi Oktoba mwaka huu, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Singida, Adili Elinipenda, alisema takribani shilingi milioni 82.8 pamoja na mali nyingine vimeokolewa na kurejeshwa kwa wahusika. 

Alisema matokeo ya ufuatiliaji na udhibiti huo umebaini kuwa baadhi ya wakopeshaji binafsi wanafanya shughuli hiyo bila ya vibali halali, hali inayosababisha kukwepa kodi na hivyo kuikosesha serikali mapato na kujipatia fedha isivyo halali.

Pamoja na mambo mengine, alisema udhibiti umebaini kuwepo kwa utozaji mkubwa wa riba zisizovumilika za zaidi ya asilimia 100 kinyume na viwango vilivyowekwa na kuainishwa na Benki Kuu, sanjari na wakopeshaji kukaa na kadi za benki za wakopeshwaji kwa lengo la kuchukua fedha kila ifikapo mwisho wa mwezi. 

Aidha, kupitia ripoti hiyo iliyowasilishwa na Takukuru, imeelezwa baadhi ya wakopeshaji hawaandai mikataba ya ukopeshaji, hivyo wakopeshwaji hawana nakala za mikataba, na hata iliyopo kwa baadhi ya kampuni hizo haikidhi sifa na vigezo.

“Baadhi ya kampuni hizi za mikopo hazina hata wataalamu wa mahesabu hali inayowafanya kutoza riba zenye mkanganyiko, na hivyo kujikuta wakimbambikiza riba kubwa mkopeshwaji,” ilieleza sehemu ya ripoti hiyo.

Hata hivyo, Afisa wa Takukuru mkoani hapa, Shemu Mgaya, pamoja na mambo mengine alisema kuna uvujaji mkubwa wa taarifa za watumishi wanaostaafu. Mathalani mafao ya mstaafu yanapokuwa yameingizwa benki wakopeshaji wanakuwa wa kwanza kupata taarifa kabla ya mhusika. 

“Tumebaini kwa baadhi ya mabenki kuna ukiukwaji mkubwa wa taratibu za kibenki kupitia maafisa wao, kwa eneo la kuwezesha kutolewa fedha kutoka akaunti ya mteja kwenda akaunti ya mkopeshaji bila mwenye akaunti kuwepo,” alisema Mgaya na kuongeza: 

“Udhibiti pia umebaini hata Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa ikichelewesha mafao kwa wastaafu hali ambayo inasababisha baadhi ya wastaafu kujikuta wakiingia katika hii mikopo umiza (mikopo yenye riba kubwa).” 

Ofisi hiyo ya Takukuru, hata hivyo inasisistiza kuwa endapo matokeo hayo ya udhibiti na mapendekezo yatatekelezwa basi ni dhahiri yataleta ustawi kwa wazee na wastaafu wa Tanzania ikizingatiwa wastaafu ndio ‘Hazina ya Taifa.’


FUATILIA HAPA CHINI TAARIFA ALIYOPOKEA MKUU WA MKOA KWA NIABA YA RAIS YA KAZI KUBWA YA ILIYOFANYWA NA TAKUKURU KUWABANA WAKOPESHAJI HARAMU NA KULINDA MASLAHI YA WANYONGE KWENYE WILAYA ZA SINGIDA, IRAMBA, IKUNGI NA MANYONI KUFUATIA AGIZO LA HIVI KARIBUNI 

 

26 Oktoba, 2020

 

TAARIFA YA FEDHA ZILIZOOKOLEWA NA TAKUKURU MKOA WA SINGIDA KUTOKANA NA RIBA UMIZA KIPINDI CHA JULAI HADI OKTOBA,2020

MKOA WA SINGIDA.

  1. WILAYA YA SINGIDA

a.       Wilaya ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 18,800,000/= kutoka kwa Mkopeshaji BISEKO MUNGETA KAZUNGU ambaye alimkopesha Mwalimu Mstaafu AMOSI NJOGHOMI fedha kiasi cha Tshs.2,000,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha Tshs. 31,000,000/=.Tunaomba leo Fedha hizi Tshs. 18,800,000/= uzikabidhi kwa  AMOSI NJOGHOMI.

b.      Wilaya ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 700,000/= kutoka kwa Mkopeshaji CHARLES WAWA ambaye alimkopesha Mtumishi Mmoja wa serikali (Jina limehifadhiwa) fedha kiasi cha Tshs.500,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha Tshs.1,900,000/=.Fedha hizi zimekabidhiwa kwa mhusika kupitia Akaunti yake huku tukiendelea kufuatilia fedha iliyosalia.

c.       Wilaya ya Singida tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs. 2,000,000/= kutoka kwa Kampuni ya BOMANG MICROFINANCE ambayo ilimkopesha Mwalimu Mstaafu ALBERT SUNGI MPAHI fedha kiasi cha Tshs.7,200,000/= na kumtaka kurejesha fedha kiasi cha Tshs.17,000,000/=. Tunaomba leo Fedha hizi Tshs. 2,000,000/= uzikabidhi kwa  ALBERT SUNGI MPAHI, TAKUKURU inaendelea kufuatilia fedha zilizosalia.

IKUNGI

a.       Katika  Wilaya ya IKUNGI tumefanikiwa kuokoa kiasi cha Tshs.17,000,000/= kutoka kwa mkopeshaji , kampuni ya MAGIREI COMPANY LTD (MICRO CREDIT) ya Singida mjini. Kampuni hii ilimkopesha Mwalimu Mstaafu GERASE KAJUNA MSHUMBUSI Tsh.3,500,000/= mwaka 2015 na kulipa Tsh.17,000,000/=  mwaka 2017. Baada ya Ofisi ya TAKUKURU kufanya ufuatiliaji iliitaka kampuni hii imrejeshee jumla ya Tshs.17,000,000/=. BWANA GERASE KAJUNA MSHUMBUSI alirejeshewa kupitia kwenye akaunti yake namba 50802500415 iliyopo katika Benki ya NMB kiasi cha Tsh.4,000,000/=  kati ya tarehe 02/07/2020 na tarehe 03/08/2020. Tunaomba leo Fedha iliyosalia kiasi cha Tshs. 13,000,000/= uzikabidhi kwa Mwalimu Mstaafu GERASE KAJUNA MSHUMBUSI .

b.      Kampuni iitwayo WIDOP COMPANY LTD ilimkopesha kiasi cha Tsh.1,700,000/= Bi. LUCIA PETRO NYIKA Muuguzi Mstaafu na kurejesha kiasi cha Tsh.5,100,000/=  .Baada ya TAKUKURU kufuatilia Bi. LUCIA PETRO NYIKA amerejeshewa Tshs.2,400,000/=  tarehe 15/10/2020, na fedha nyingine zilizobaki zipo kwenye utaratibu wa kurejeshwa TAKUKURU Wilaya ya Ikungi na mara tu zitakaporejeshwa atakabidhiwa Bi. LUCIA PETRO NYIKA.

IRAMBA       

a.       TAKUKURU (W) ya  IRAMBA imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.3,500,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na kampuni ya ANGELVA FINANCIAL LTD kinyume na utaratibu wa Kibenki. Ambapo  siku ya  tarehe 26/06/2020 Ofisi ya TAKUKURU (W) IRAMBA ilimkabidhi MAGRETH  BUSONGO fedha  kiasi cha Tsh.3,500,000/=.

Awali ilipokelewa taarifa ya  kulipishwa riba kubwa katika mkopo aliokopa kutoka kwa kampuni ya ANGELVA FINANCIAL LTD ya Kiomboi Iramba kiasi cha Tsh.1,000,000/= mwezi agosti mwaka 2019  na kulipa marejesho ya Tsh.9,250,000/= mwezi February mwaka 2020 sawa na riba ya asilimia 925 baada ya kupata fedha za mafao ya kustaafu.

 

MANYONI

a. TAKUKURU(W) YA  MANYONI imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.360,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na kampuni ya MWITA CREDITORS kinyume na utaratibu wa Kibenki .Mtumishi Mstaafu Bw. CHRISTOPHER MWALUKO KABUDI alizidishiwa riba kwenye mkopo wake na alikuwa amelipa fedha nyingi kuliko alivyotakiwa kurejesha.Baada Takukuru kufuatilia ilibainika kwamba kiasi cha shilingi laki tatu na sitini (360,000/=) zilikua zimerejeshwa na mlalamikaji baada ya mkopo kumalizika.Hivyo wahusika walipohojiwa walikiri kosa na kuzirejesha fedha hizo kiasi cha Tshs. 360,000/=. TAKUKURU(W) ya Manyoni imerejesha fedha hizo kwa CHRISTOPHER MWALUKO KABUDI.

b.      TAKUKURU (W) MANYONI imeweza kuokoa fedha  kiasi cha Tsh.200,000/= zilizokuwa zimechukuliwa na ALPHONCE NJALIKE kinyume na utaratibu wa Kibenki. Bi.PAULINA JOSEPH alikopa kwa ALPHONCE NJALIKE kiasi cha shilingi laki mbili na wakati wa marejesho alishindwa kurejesha waliuza vitu vyake vya ndani yakiwemo makochi.Baada ya ofisi kuingilia kati iligundua kwamba mkopeshaji hakuwa na leseni ya ukopeshaji na pia taratibu za uuzwaji wa makochi yake haukufuatwa.Baada ya mlalamikiwa kuhojiwa na ofisi aliomba kulipa gharama za makochi hayo kiasi cha shilingi laki mbili (200,000/=) na hivyo kufutwa kwa deni husika na mlalamikaji kupata haki yake.

 

c.       TAKUKURU (W) MANYONI ilifanya ufuatiliaji kwa ISSA KIULA BAKARI ni Mwalimu mstaafu na alitozwa riba kubwa na  HAMIS ISSA ambae awali alikuwa mfanyakazi wa MRITHOS CREDITORS. Alikopa kiasi cha shilingi milioni tisa (Tshs. 9,000,000) pamoja na riba na wakati wa marejesho mlalamikiwa alikua na kadi pamoja na namba ya siri ya mlalamikaji.

Kutokana na hivyo mlalamikiwa alichukua kiasi cha shilingi milioni kumi na nane kwenye akaunti ya mlalamikaji. Baada ya mlalamikaji kumfuata alikubali kulipa shilingi milioni tatu.Takukuru ilifanya ufuatiliaji na mlalamikiwa nae alikiri kuwa na kiasi cha shilingi milioni tano na laki tano (Tshs.5,500,000/=) za mlalamikaji. Aliomba kuzilipa fedha hizo ndani ya mwezi mmoja na tayari ameshalipa shilingi milioni nne (Tshs.4,000,000/=) ambazo mlalamikaji ISSA KIULA BAKARI alikabidhiwa na Katibu Tawala wa Wilaya Manyoni. .Fedha zilizobaki zitawasilishwa TAKUKURU na mdaiwa tarehe 29 mwezi huu wa Oktoba 2020.

TAKUKURU (M) inazidi Kutoa rai kwa wananchi wote kwa ujumla kujiepusha na vitendo vya Rushwa na kushiriki kikamilifu kutoa taarifa za vitendo vya Rushwa kwa kufika ofisi zetu za TAKUKURU (M) na Wilaya au kupiga simu namba 113, kwa kutumia TAKUKURU APP wanapobaini kutokea/kutaka kutokea kwa vitendo vya Rushwa na kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.

Imetolewa na:

 

ADILI ELINIPENDA

MKUU WA TAKUKURU (M)

SINGIDA


WANAOISHI MLIMA ULUGURU KUFUNDISHWA MBINU ZA KUENDELEA KUISHI HUKO BILA KUSHUSHWA.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manispaa ya Morogoro, Fikiri Juma  ( kulia) akiwa na Mgombea Udiwani, Juma Kiduka kwenye mkutano wa kampeni wa lalasalama uliofanyika kwenye Mtaa wa Folkland mjini Morogoro juzi
Wananchi wa Kata ya Magadu wakifuatilia mkutano huo wa kampeni wa kumnadi mgombea Udiwani wa Kata hiyo bwana Juma Kiduka.
Wananchi wa Kata ya Magadu wakifuatilia mkutano huo.
Wananchi wa Kata ya Magadu wakifuatilia mkutano huo
Mkutano ukiendelea.
 


Na Calvin Gwabara, Morogoro.


Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Wilaya ya Morogoro Mjini, Fikiri Juma amewahakikishia wananchi wanaoishi kwenye mlima Uluguru kuwa hawatashushwa bali watafundishwa njia na mbinu bora za kuishi milimani kama wanavyofanya watu wa Lushoto na kwingine duniani.

Fikiri aliyasema hayo kwenye mkutano wa kampeni ya udiwani kwenye Kata ya Magadu ambayo sehemu ya jamii ya watu wa kata hiyo wanaishi kwenye mlima Uluguru na kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji.

“ Tumezielekeza Taasisi mbalimbali za misitu kuacha kwenda kupanda miti kwenye mlima huo badala yake miti hiyo ipandwe na wananchi wa maeneo hayo ili waweze kuitunza tofauti na sasa ambapo miti inayopandwa inakauka kwakuwa wananchi hao wanaona sio sehemu yao na hivyo kukauka” alisema  Fikiri.

Akimnadi mgombea udiwani wa kata hiyo Juma Kiduka,  Mwenyekiti huyo wa CCM Manispaa ya Morogoro alisema Serikali ya CCM inajenga viwanda nchi nzima sio tu kutoa ajira bali kuwezesha Wakulima wa Morogoro na nchi nzima kupata Soko la uhakika wa mazao yao.

“ Hapo Mkambarani kwa pembeni kuna kiwanda cha mfano cha kusindika mazao ya mikunde kwenye mkoa wetu kitasaidia sana kuinua maisha ya wakulima wa mazao hayo ya mikunde na ajira kwa vijana na mama zetu” aliongeza Fikiri.

Alisema kitendo cha kwenda kuuza mali ghafi nchi za nje kunapeleka ajira pia kwa watu wa nje lakini viwanda vikiwa hapa nchini vitatoa ajira hizo kwa vijana na watanzania na hivyo kusaidia kuchichea maendeleo ya Taifa hili ambalo asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wale wanategemea kilimo.

Amebainisha kuwa ilani ya CCM ya miaka mitano 2015 hadi 2020 imetekelezwa kwa asilimia 100 ndio maana Chaka kinampa nafasi nyingine ya kusimamia ilani ya CCM kwa miaka mingine mitano na hakuna ubishi kuwa atashinda kwa kishindo.

 Fikiri alisema kazi iliyopo mbele ya Wana Morogoro mjini kesho kutwa ni kumchagua  Azizi Abood kuwa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kiduka kuwa Diwani wa Kata ya Magadu na Rais John Pombe Magufuli kuwa Rais wa awamu ya sita ili amalizie kazi kubwa aliyoianza ya kuleta maendeleo ya Tanzania.

Kwa upande wake Mgombea Udiwani wa Kata ya Magadu Juma Kiduka alisema kuna kazi kubwa inafanywa na serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kuleta maendeleo ya Kata ya Magadu na Jimbo la Morogoro mjini hivyo kama mtumishi wao anakwenda  kusimamia miradi hiyo ili maendeleo yafikiwe.

Akizungumzia changamoto ya maji alisema tayari kuna Mradi Mkubwa wa maji unaendelea kwa sasa na utakapokamilika utatatua changamoto zote za maji kwenye kata na Jimbo la Morogoro mjini hivyo waendelee kuiamini CCM maana sera zake zinatekelezeka.

Awali akizungumza kwenye mkutano huo aliyekuwa Meya wa Zamani wa Manispaa ya Morogoro Profesa. Romanus Ishengoma amewataka wakazi wa kata hiyo kumuamini Rais John Pombe Magufuli na wagombea wa CCM Kwani amefanya kazi kubwa katika Historia ya Tanzania.

“Mimi mnadhani nipo CCM kwa bahati mbaya? Simnajua nina akili kubwa sio? nipo CCM kwakuwa nina uhakika na kazi za CCM, Sera zake na wagombea wake” alisisitiza  Ishengoma.

Kampeni zinaendelea kupambana Moto katika dakika za lala salama zikiwa imebaki siku moja tu kabla ya Wananchi wa Tanzania kupiga kura kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani.

KILIMO SHADIDI CHA MPUNGA KUONGEZA TIJA KWA WAKULIMA NCHINI.

Dkt. Devotha Kilave Mtafiti akiwasilisha matokeo ya utafiti wa Kilimo Shadidi cha Mpunga mbele ya waandishi wa habari.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo ya utafiti ili wayafikishe kwa jamii.
Waandishi wa habari wakochukua vipeperushi na machapisho mbalimbali ya matokeo ya Tafiti zilizofanhwa na Mradi wa APRA Tanzania.

Mkuu wa Mradi wa APRA Tanzania Profesa. Aida Isinika akichangia neno kwenye uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti wa Kilimo Shadidi cha mpunga uliowasioishwa na Dkt. Devotha Kilave.

Waandishi wa habari wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo ya utafiti wa Mradi wa APRA Mkoani Morogoro kwenye ukumbi wa ICE - SUA.
Mwandishi wa habari wa Gazeti ka the Citizen Jacob Mosenda akiuliza swali kwa watafiti ili kupata ufafanuzi zaidi.
Waandishi wa habari wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo ya utafiti wa Mradi wa APRA Mkoani Morogoro kwenye ukumbi wa ICE - SUA.
 


Na Calvin Gwabara, Morogoro


WATAFITI wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)  kupitia Utafiti wao wamependekeza Sera za kilimo kuhimiza mafunzo ya Kilimo Shadidi cha Mpunga nchi nzima ili kuongeza mavuno na kuboresha maisha ya wakulima wa zao hilo nchini.

Mapendekezo hayo yametokewa na Mtafiti kutoka SIA Dkt. Devotha Kilave  kwenye warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali  iliyoandaliwa na Mradi wa kutafsiri Sera za Kilimo Barani Afrika (APRA) kwa lengo la kufikisha matokeo ya utafiti wao kwa jamii.

“ Sambamba na hilo Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inatakiwa kutengeneza mkakati wa nchi nzima wa kutoa mafunzo ya kilimo hicho bora cha mpunga ili kuwafanya wakulima kuipenda teknolojia hiyo na kuifanyia kazi.” alisema Dkt. Devotha.

Ameongeza kuwa jitihada zozote za kupunguza gharama za uzalishaji na za masoko kama voor kuboresha miundombinu na kupeleka umeme zitasaisia sana kukufanya kilimo cha mpunga kuwa na faida kubwa kwa jamii.

“Katika utafiti wetu tumebaini kuwa mafunzo yana mchango mkubwa sana kwenye kuongeza tija kwenye kilimo, mfano wakulima waliopata mafunzo ya kilimo shadidi cha mpunga wamepata asilimia 8.7 zaidi ya wale ambao hawa kupata mafunzo ya Kilimo hicho” alifafanua Dkt. Devotha.

Mtafiti huyo alisema kwenye msimu wa Kilimo wa Mwaka 2016/2017 asilimia 45.8 wakulima  walianza kulima kilimo hicho lakini mbinu hiyo baadae ilisambaa kutoka kwenye vikundi vilivyo pata mafunzo ambao ni asilimia 61.6 na kufikia vikundi vingine 36 ambavyo havikupata mafunzo lakini vikaanza kilimo hicho.

Dkt. Devotha amebainisha kuwa wakulima waliolima kilimo shadidi cha mpunga walipata mavuno mengi ya tano 2.9 kwenye hekta moja wakati ambao hawakutumia mbinu hiyo walipata tani 2.9 kwa hekta moja.

Akizungumzia faida nyingine za kilimo hicho,  mkuu wa mradi huo Professa. Aida Isinika alisema kinasaidia kuokoa  upotevu wa maji na uharibifu wa mazingira ikizingatiwa kuwa Kilimo hicho cha mpunga kinafanyika jirani na ardhi oevu ya RAMSA ambayo inatunzwa.

Profesa. Isinika pia alisema endapo mbinu hiyo inatumika vizuri kwenye eneo hilo itasaidia kutoharibu mazingira kwani sehemu kubwa ya maji yanayotumika kuzalisha umeme kwenye Bwawa la Kidatu yanatoka kwenye bonde hilo.

Kilimo Shadidi cha Mpunga (SRI) ni mbinu unayotumia maji kidogo, mbegu kidogo lakini kwa kufuata kanuni bora za kilimo kama voor kulima kwa wakati, kupandikiza miche ikiwa na siku saba hadi kumi kutoka kwenye kitalu na kupanda kwa nafasi na mistari na kupata mavuno makubwa kuliko kilimo cha mazoea.

Sunday, October 25, 2020

SINGIDA YATAKIWA KUCHUKUA TAHADHARI BIASHARA USAFIRISHAJI BINADAMU

Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, Seperatus Fella, akiweka mkakati wa namna bora ya kukabiliana na biashara hiyo, alipokutana na wadau mbalimbali kwenye mafunzo maalumu mkoani Singida juzi.

Afisa wa Sekretarieti hiyo, Ahmad Said Mwen-dadi, akitoa mada kwenye mafunzo hayo.

wa Sekretarieti hiyo, Alex Lupilya akitoa mada kwenye mafunzo hayo.

Picha ya Pamoja ya baadhi ya wadau walioshiriki mafunzo hayo.

 


Na Godwin Myovela, Singida


WAKAZI mkoani hapa wametakiwa kuwa makini kabla ya kuwaruhusu mabinti kuchukuliwa na kupelekwa maeneo mbalimbali nchini kwa kigezo cha kutafutiwa au kufanya kazi za ndani, badala yake wahakikishe kwanza wanahusisha uongozi wa Serikali ya Mtaa husika ili mchakato huo ufanyike kihalali.

Pia ‘dalali’ au mtu yeyote anayetaka kumchukua binti yako hakikisha anakuwa na mdhamini wa kuwezesha kurahisisha  mawasiliano ya mara kwa mara, lengo hasa ni kuwa na uhakika wa mazingira ya usalama wa mwanao huko aendako.

Katibu wa Sekretarieti ya Kuzuia na Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji wa Binadamu, kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Seperatus Fella aliyasema hayo jana mkoani hapa, wakati akitoa mafunzo kwa wadau mbalimbali ya namna ya kupambana na biashara ya usafirishaji binadamu.

“Singida ikitanguliwa na Wilaya ya Kondoa Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo wasichana wanachukuliwa na kwenda kutumikishwa kwa kufanyishwa biashara za ngono kwenye majiji kama Dar es Salaam na kwingineko,” alisema Fella.

Aliongeza kwamba tangu kuanza kwa mafunzo hayo kwa kushirikiana na mashirika ya kitaifa na kimataifa mwaka 2017, mkoa wa Singida ulikuwa bado haujafikiwa, na kinachofanyika kupitia mafunzo hayo ni kuwaelekeza wadau mbinu bora za kuzuia na kukabiliana kisheria na biashara hiyo haramu.

 Fella pamoja na mambo mengine, alisema kwa muktadha wa kitaifa hali siyo ya kuridhisha sana kutokana na mabinti wengi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa siri, kwa ahadi za kutafutiwa ajira zenye mshahara mnono jambo ambalo sio kweli, na kinyume chake hugeuzwa watumwa kwa kufanyishwa biashara za ngono na madawa ya kulevya kwa maslahi ya waliowasafirisha.

“Tunaendelea na juhudi za kuwaokoa, na hivi karibuni tumewaokoa mabinti wa kitanzania waliokuwa wakitumikishwa kama watumwa kutoka Iraq, Malaysia na India…na wametueleza kuwa bado wamewaacha wenzao wengi wakiendelea kuteseka,” alisema Fella.

Kwa upande wake Afisa wa Sekretarieti hiyo, Ahmad Mwen-Dadi, alisema biashara hiyo ni ya tatu kwa kuingiza fedha nyingi ikitanguliwa na ile ya Madawa ya Kulevya na Uuzaji wa Silaha Haramu, hivyo ni jukumu la kila raia wa Taifa la Tanzania kuchukua tahadhari kwa ulinzi madhubuti wa watoto na mabinti kuanzia kwenye ngazi ya familia.

Alisema madalali wa biashara hiyo wanapokutana na mabinti wamekuwa wakiwahadaa kwenda kufanya kazi kwenye mahoteli makubwa, maduka makubwa (supermarkets), Saluni na kazi nyinginezo zenye maslahi makubwa, jambo ambalo hatimaye huwashawishi mabinti walio wengi kutoroka bila kuaga wazazi.

“Wengi wanasafirishwa kupelekwa nchi za Thailand, China, Malaysia, Bangladesh na hata Iraq na wakifika huko wanajikuta kazi walizohaidiwa sio wanazifanya. Wengi tuliowaokoa wanasema wenzao wapo katika hali mbaya ya kutumikishwa kikatili mpaka pale watakapomaliza kulipa deni la gharama za kuwasafirisha hadi kufika kwenye hizo nchi,” alisema Mwen-Dadi.

Aidha, alitoa tahadhari kwa wana-singida na taifa kwa ujumla kuwa makini kutokana na ukweli kwamba kwa sasa usafirishaji wa ndani kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine hadi Zanzibar umeuzidi ule usafirishaji wa watoto na mabinti wa kitanzania kupelekwa nje.

“Naomba sana tuwe makini, bado hatujafikia umasikini wa kuacha watoto na mabinti zetu kwenda kudhalilishwa na kufanyiwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu. Mapambano dhidi ya biashara hii haramu ni jukumu letu sote kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa,” alisema.

Wadau waliopata fursa ya kushiriki mafunzo hayo ni Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka Singida, Mashirika yasiyo ya kiserikali, kikiwemo Kituo cha Faraja na Jeshi la Wokovu, Jeshi la Polisi, Uhamiaji na Maafisa Serikali za Mitaa.

Mafunzo hayo pamoja na mambo mengine yanalenga kuelimisha na kutoa taswira ya namna bora ya kukabiliana kisheria na biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kuendesha kesi, kupepeleza na kutoa misaada ya utambuzi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

ASKOFU FLASTON NDABILA AOMBA AMANI SIKU YA KUPIGA KURA


Askofu Kiongozi wa Kanisa la  Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila (kulia) akiongoza maombi maalumu ya kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, 2020.
Muumini wa kanisa hilo, Mariam Luvanda akiombea nchi amani katika maombi hayo.
Mama Askofu, Janeth Ndabila akiomba kwenye maombi hayo. 
Maombi yakiendelea.
Mzee Gerald Enock akiomba huku akililia amani ya nchi isipotee wakati huu wa mchakato wa kupiga kura.
Maombi yakiendelea.
Muumini wa kanisa hilo Daniel Hezron Mpemba akiomba kwa hisia kali katika maombi hayo.
Waumini wa kanisa hilo wakiomba huku wakililia amani isipotee wakati wa kupiga kura.
Maombi yakiendelea.
Maombi yakiendelea.
Maombi yakiendelea.


Na Dotto Mwaibale


WANANCHI nchini wametakiwa kuilinda amani siku ya kupiga kura na kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwachagua viongozi wanaowataka.

Ombi hilo linetolewa jana na Askofu Kiongozi wa Kanisa la  Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila wakati wa maombi maalumu ya kuiombea nchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano Oktoba 28, 2020.

Akihubiri katika maombi hayo Ndabila alisema wameamua kufanya maombi hayo kwa sababu mara nyingi unapofanyika uchaguzi kunakuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinaweza kuashiria uvunjivu wa amani na utulivu wa nchi yetu.

Alisema kufuatia kuwepo kwa changamoto hizo ambazo amekuwa akiziona zikifanyika katika nchi kadhaa wanafanya maombi hayo ikiwa ni kukumbushana kuitunza amani katika kipindi hiki kwani baada ya uchaguzi maisha yataendelea.

 "Kanisa lina hekima ya kuvielekeza vyama vya siasa kwa njia ya maombi ili viwe na busara ya kufanya uchaguzi bila ya kuharibu amani na utulivu wa nchi uliopo." alisema Ndabila.

Ndabila aliwapongeza wagombea wa vyama vya siasa kwa kuonesha kuilinda amani ya nchi katika kipindi chote cha kampeni licha ya kuwepo changamoto ndogo ndogo na akaviomba vyama hivyo viendelee kufanya hivyo hata siku ya kupiga kura.

Alisema jambo linalo mpa amani ya kupiga kura kwa amani siku hiyo ni kila mgombea anapokuwa kwenye kampeni kuanza mkutano wake kwa kumtanguliza Mungu.

Ndabila alisema amani inapokosekana wa kulaumiwa ni viongozi wa dini kwa sababu ndiyo wenye wajibu wa kuhamasisha waumini wao kumuomba Mungu atuepushe na uvunjifu wa amani wakati wote na hasa inapofika kipindi cha uchaguzi.

"Wagombea wote ni watoto wa Mungu hivyo wanapaswa kumtii Mungu ili wasilete machafuko katika nchi yetu," alisema Ndabila.

"Nimesikiliza kwa makini sera za wagombea mbalimbali wote wana kiu ya kuona mabadiliko ya kiuchumi, kiafya na kijamii ni vema sana!  napenda kuwakumbusha mabadiliko yalipohitajika yaani ya kujitawala wenyewe Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere alitumia hekima na kumtanguliza Mungu na kwa hekima zake tukawa mojawapo ya nchi iliyopata Uhuru bila kupoteza maisha ya watu wake" aliongeza Ndabila. 

Ndabila aliomba hekima iongoze Tume ya Taifa ya Uchaguzi itende haki, hekima iviongeze vyama vya siasa, hekima iviongoze vyombo vya usalamau na tuazimie kuto watoa watanzania kafara na kupoteza maisha ya mtanzania hata mmoja.

Aidha Askofu Ndabila alisema tusijiharibie CV kwa kuchochea machafuko kibiblia penye machafuko yoyote yale Mungu hayupo haijalishi mwenye kuyasababisha ni nani? kwani hakuna kitu ambacho Mungu anakichukia kama kuharibu nchi ambayo kimsingi alitupa tuitunze na imeandikwa katika zaburi ya 119:119 tukifanya ubaya katika nchi yetu kuna kuondolewa bila heshima yeyote.

Ndabila alitumia maombi hayo kuwaombea kwa Mungu Marais wastaafu, Mawaziri Wakuu wastaafu , Masipika pamoja na mke  wa Rais Mama Janeth Magufuli Mungu awape busara   na hekima za kumshauri Rais wetu ili aweze kuivusha salama nchi yetu  katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Katibu wa kanisa hilo,  Jane Magigita aliwahimiza waumini wa kanisa hilo na wananchi waliokuwepo kwenye maombi hayo kujitokeza kwenda kupiga kura ya kumchagua Rais, wabunge pamoja na madiwani  na akawaomba watanzania kuombea uchaguzi huo ili Mungu atujalie kuwapata viongozi watakaoliongoza vema Taifa letu la Tanzania. 

"Viongozi wa dini ni watu muhimu kwani wananguvu ya kupeleka ujumbe haraka kwa waumini wao kupitia mahubiri yao hivyo niwaombe katika hizi siku mbili zilizosalia wahamasishe kulinda amani ya nchi na waumini wao wenye sifa ya kupiga kura wajitokeze na kadi zao za kupigia kura katika vituo walivyo jiandikisha ili kutimiza haki yao ya msingi na ya kikatiba." alisema Magigita. 

Aidha Magigita alisisitiza umuhimi wa kila mtanzania kuzingatia misingi ya amani na utulivu wakati mchakato huo wa upigaji kura ukiendelea, ikiwemo kufika mapema kituoni kupiga kura na kuondoka kuelekea kwenye majukumu mengine kwa mujibu wa sheria za uchaguzi ili kuepusha madhara au viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyoweza kujitokeza.