Sunday, November 26, 2023

BOHARI YA DAWA (MSD) YATWAA TUZO YA MLIPA KODI BORA 2023

 Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai (kushoto) akipokea tuzo ya mlipa kodi bora.

MSD Yatwaa Tuzo Ya Mlipakodi Bora 2023

..............................................

 

Na Mwandishi Wetu


BOHARI ya Dawa (MSD), imetwaa tuzo ya Mlipakodi Bora kwa mwaka 2023 ya Mamlaka ya Kodi Tanzania.

Tuzo hizo zimetolewa  usiku wa Novemba 24, 2023 katika hafla maalum ya wiki ya Mlipakodi zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijiini Dar es Salaam ambako Bohari hiyo imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha WalipakodiWalipakodi wa Kati kwa Mkoa wa Kikodi wa Temeke.

Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema ushindi huo una maana kubwa kwa Bohari hiyo na Watanzania.

Amesema MSD ambayo ni moja ya Taasisi za kimkakati za Serikali inayohusika na kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali nchini inafuata taratibu, sheria na miongozose ikiwa ni pamoja na kulipa kodi stahiki.

"Maendeleo yoyote ya nchi yanategemea kodi zinazolipwa hivyo ni vyema kila mlipa kodi akalipa kodi stahiki ili kuwezesha muendelezo wa biashara na  kuimarisha maendeleo kwa mustakali wa ustawi wa jamii, " ameongeza Tukai katika hafla hiyo ambako mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Tukai, MSD sasa iko katika mkakati wa kujiendesha kibiashara hivyo hatua ya kulipa kodi kwa utaratibu uliowekwa hadi kutambuliwa ni fursa ya kuaminika kwa wadau wetu katika huduma tunazotoa.

Awali Mkurugenzi wa Elimu wa Mlipakodi na Mawasiliano, Richard Kayombo alisema vigezo vilivyotumika kupata washindi ni kulipa kiasi kikubwa cha kodi na hiari pamoja na kutunza kumbukumbu vizuri

Tuzo hiyo ya mlipa kodi bora ikioneshwa.
 

Tuesday, November 21, 2023

SERIKALI YAMWAGA VIFAA TIBA VYA SH. MILIONI 222.472 SINGIDA

 

  Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida, Mashariki, Miraji Mtaturu  ikiwa ni ishara ya kumkabidhi jenereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwenye hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

.................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

SERIKALI  ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imekabidhi vifaa tiba Mkoa wa Singida vyenye jumla ya takribani Sh.Milioni 222.472.

Vifaa hivyo ni pamoja na majenereta, sambamba na vifaa vitakavyotumika kuhudumia watoto wanaozaliwa kabla ya muda na huduma nyinginezo ambavyo vimekabidhiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kituo cha Afya Sepuka na Hospitali ya Wilaya ya Singida, Ilongero.

Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ambayo ilishuhudiwa na wabunge, watendaji wa idara mbalimbali za sekta ya afya, wananchi pamoja na Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) , Meneja  wa MSD Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa alisema kazi hiyo ya usambazaji wa vifaa hivyo ni jukumu lao walilopewa na Serikali.

" Kazi yetu kubwa sisi MSD ni Uzalishaji, Ununuzi,  Uhifadhi na Usambazaji wa  bidhaa za afya na vitendanishi hapa nchini ambayo tunaifanya kwa mamlaka ya kisheria," alisema Jumaa.

“MSD leo tupo hapa Ikungi kwa ajili ya kukabidhi jenereta, kitanda cha kufanyia upasuaji, Ultra-Sound mashine pamoja na mashine ya kuasaidia kuwapatia joto watoto wachanga na waliozaliwa kabla ya wakati.(njiti-Infant Radlant warmer) vyenye thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 72

Jumaa alisema lengo kubwa la kupelekwa kwa vifaa hivyo ni kuhakikisha huduma za uzazi zinaboreshwa na kuwa katika wilaya hiyo MSD ilikuwa inakamilisha vifaa ambavyo ilikuwa imepokea fedha zaidi ya Sh. Milioni 300 ili kukamilisha usambaji wake.

Alisema MSD Kanda ya Dodoma imepokea maombi  ya vifaa  tiba zaidi ya  700  Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa ajili ya vituo  vya Afya  na Zahanati.

"Ukiangalia muda tuliopokea fedha hizi na utekelezaji wa kupeleka vifaa hivyo ni muda mfupi sana na hiyo imetokana na Serikali kuboresha huduma za MSD na kufikia hatua hii ya kukamilisha vifaa ambavyo hatukuvipeleka awali na kuvipeleka sasa baada ya fedha zake kuzipokea muda mfupi uliopita," alisema Jumaa.

Alisema Serikali imekuwa ikitoa fedha na MSD imekuwa ikinunua na kusambaza vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya kote nchini ambapo aliishukuru kwa hatua hiyo na kueleza kuwa inajenga morali kwa watumishi wa sekta ya afya na kuipenda kazi wanayoifanya.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu  aliishuru Serikali na MSD kwa kupeleka vifaa hivyo na kueleza kuwa sekta ya afya ni uhai na kuwa watu wakiwa na afya njema ndipo wataweza kufanya kazi zao vizuri.

"Leo hii tunashuhudia vifaa hivi vilivyo letwa na Serikali kupitia MSD na kukabidhi hospitali yetu ya Ikungi maana yake ni utekelezaji wetu wa kujenga Hospitali ya Wilaya ambayo tuliiomba kwa muda mrefu," alisema Mtaturu.

Alisema kujenga majengo tu ya hospitali haitoshi na kuwa inahitaji na vitu vya ziada vikiwemo vifaa na kuwa madaktari na wataalamu wengine wamesomeshwa kwa lengo la kuwasaidia watu kutibu maradhi mbalimbali na kwa kuvitumia vifaa hivyo ndio wanaweza kufanya kazi yao kwa urahisi iwe kwa kupima na kufanya upasuaji.

Mtaturu alisema Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya afya hapa nchini hivyo kila mtu mpenda maendeleo anapaswa kumshukuru kwa jinsi anavyo iendesha nchi kwenye sekta mbalimbali.

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu akipokea vifaa hivyo kwa ajili ya Kituo cha Afya cha  Sepuka alisema miongoni mwa vifaa alivyo pokea kutoka MSD ni jenereta lenye ukubwa wa KVA 60 na vifaa vingine 11 ambavyo baadhi ni toroli la kuwekea vifaa wakati madaktari na wauguzi wanapokwenda kutoa huduma, vifaa vinavyotumika kumsaidia mtoto baada ya kuzaliwa aweze kupumua vizuri na kuwa vifaa vyote alivyovipokea vinatumika kupingana na uzazi pingamizi na lengo lake ni kumuokoa mama wala mtoto wasife wakati wa kujifungua.

Alitaja vifaa vingine alivyopokea ni mashine kwa ajili ya hewa, mashine ya kupimia uzito, kifaa cha kutundikia dripu ya maji, kifaa cha kuwapa joto watoto waliozaliwa kabla ya muda, kifaa cha kuvuta uchafu kwenye njia ya hewa baada ya mtoto kuzaliwa, saa ya ukutani, kifaa kinachobeba vifaa vya kumuhudumia mtu aliyepata majeraha na pampu inayotumika kumnyonya mtoto kwa ajili ya kuondoa kitu kilichokwama kooni au kupoteza fahamu baada ya kupaliwa na kuwa vifaa hivyo vyote vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 82.

Kingu aliishukuru Serikali kwa kutoa fedha na akapongeza maboresho makubwa yaliyofanywa ndani ya MSD na kueleza kuwa MSD ya leo ni ya kisasa na mkombozi kwa wananchi katika kazi ya kutoa huduma za afya si kwa Mkoa wa Singida pekee bali kwa nchi nzima kazi ambazo zimekuwa zikionekana kupitia vyombo vya habari.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo aliishukuru Serikali kwa kuwapelekea jenereta na gari la kuwabebea wagonjwa na wajawazito ambao wengi wao walikuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa umeme wa uhakika wakati wakipata huduma hasa za upasuaji na kukosekana kwa gari la kuwapeleka hosptali wanapokuwa wagonjwa.

Ighondo alisema pamoja na kupelekewa gari hilo pia Serikali kupitia MSD imewapelekea kifaa kinachotumika kwa ajili ya kuwaongezea joto watoto wanaozaliwa chini ya muda.

Alisema mbali ya gari hilo la wagonjwa vifaa walivyopokea vina thamani ya zaidi ya Sh.Milioni 62.7

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dorisila Mlenga, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu pamoja na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel waliishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vinakwenda kuwarahisishia utendaji wa kazi za kutoa huduma kwa wananchi ambapo walisema watavisimamia na kuvitunza ili viweze kudumu kwa muda mrefu wakizingatia Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.

Wananchi Elesisia Mlenga, Asha Salim, Asha Musa, Mwalimu Tatu Njoka, Ashura Iddi na Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Seketoure, Getruda Yona waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapekea jenereta na gari la wagonjwa na kueleza kuwa vifaa hivyo vinakwenda kuwasaidia katika kupata huduma bora za afya.

Mwanafunzi Getruda Yona alimshukuru Rais Samia kwa kuwajengea shule na kuwapunguzia umbali mrefu ambapo walikuwa wakitembea zaidi ya kilomita 10 kwenda shuleni kabla ya kujengewa kwa shule hiyo ya Seketoure.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu  ikiwa ni ishara ya kumkabidhi jenereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwenye hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Kituo cha Afya cha Sepuka Wilaya ya Ikungi. Kutoka kushoto ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Sepuka, Kesia Daniel , Diwani wa Kata ya Sepuka Halima Ng'imba, Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja MSD Kanda ya Kati, Juliana Mbogo na  Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.


Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kushoto) akipeana mkono na Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, Ramadhani Ighondo ikiwa ni ishara ya kumkabidhi jenereta na vifaa tiba vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD kwenye hafla iliyofanyika Novemba 20,2023 katika Hospitali ya Wilaya ya Singida.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati kulia) akisisitiza jambo wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa Mbunge wa Jimbo la Singida, Magharibi Elibariki Kingu (kushoto) Kulia ni Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi wa MSD Kanda ya Kati, Juliana Mbogo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akipeana mkono na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Sepuka Kesia Daniel baada ya kukabidhi vifaa hivyo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa MSD na wakituo cha Afya cha Sepuka baada ya kukabidhi vifaa tiba hivyo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akizungumza na wakazi wa Wilaya ya Singida wakati wa kukabidhi vifaa hivyo
Mbunge Ramadhani Ighondo akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.

Mganga wa Wilaya ya Singida, Grace Ntogwisangu, akizungumza na wananchi kwenye hafla hiyo.
Gari la MSD , likiwa tayari kushusha vifaa hivyo.
Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa (katikati) na Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja wa NSD, Juliana Mbogo wakiwajibika wakati wa kukabidhi vifaa hivyo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu, akizungumza na wananchi wa Kata ya Sepuka wakati wa kupokea vifaa hivyo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Elibariki Kingu,Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa na Afisa Huduma Mwandamizi kwa Wateja wa MSD, Juliana Mbogo wakiwa na zawadi zao za kuku walizopewa na Wanawake wa Kata ya Sepuka.
Wananchi wa Kata ya Sepuka wakiwa kwenye hafla ya kupokea vifaa hivyo.

Meneja  wa  Bohari ya Dawa  (MSD) Kanda ya Dodoma Mwanashehe Jumaa, akiwa katika picha ya pamoja na wanawake waliohudhuria kliniki wakati wa makabidhiano ya vifaa hvyo Kata ya Sepuka.

Muonekana wa moja ya magenereta yaliyo kabidhiwa na MSD katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Singida na Kituo cha Afya cha Sepuka.
Wanawake wakiwa kwenye hafla ya kukabidhiwa vifaa hivyo Hospitali ya Wilaya ya Singida, Ilongero. 


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Seketoure wakiwa kwenye hafla hiyo.

Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru akizungumza na wananchi wakati wa hafla hiyo.

Gari la wagonjwa lililotolewa na SAerikali kwa ajili ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida likioneshwa kwa wananchi (hawapo pichani) wakati wa hafla hiyo ya kupokea vifaa tiba.

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Ilongero, Mwanamoshi Bakari, akizungumza kwenye hafla hiyo.

Muonekano wa baadhi ya majengo ya Hosptali ya Wilaya ya Ikungi.

Muonekano wa moja la jengo la Kituo cha Afya cha Sepuka.

Muonekano wa moja ya jengo la Hospitali ya Wilaya ya Singida Ilongero.
Jenereta likiwa limebebwa kwa jeki tayari ya kuhifadhi katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi wakati ikisubiriwa kujenga kibanda litakalo wekwa.


Sunday, November 19, 2023

WAHITIMU WANAWAKE WANG'ARA MAHAFALI YA 21 TAASISI YA UHASIBU SINGIDA

 

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda (katikati) akiongoza maandamano ya wahitimu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakati wakiwasili kwenye mahafali ya 21 ya taasisi hiyo yaliyofanyika Novemba 17, 2023. Kulia kwake ni Wakili Said Chuguma ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHEREHE za Mahafali ya 21 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida imemalizika huku idadi kubwa ya wanawake  ikizidi kuongezeka mara dufu ikilinganishwa na idadi ya wanaume.

Kwa mujibu wa taarifa ya taasisi hiyo jumla ya wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 wamehitimu katika mahafali hayo Kampasi ya Singida ikilinganishwa na idadi ya wanaume 762 sawa na asilimia 44.8.

Akizungumza kwenye mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 17, 2023 Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo alisema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 1,700 katika kampasi hiyo kati yao wanawake 938 sawa na asilimia 55.2 na wanaume 762 sawa na asilimia 44.8, wamepata tunuku zao kwenye fani mbalimbali.

Alisema jumla ya Wahitimu ngazi ya Cheti cha Awali ni 567, Astashahada 452, Stashahada 491, na Shahada 190.

Profesa Pallangyo alisema idadi hiyo kubwa ya wahitimu wanawake inadhihirisha kwamba TIA inanaunga mkono jitihada za Serikali, kwa kutoa fursa ya mafunzo pasipo ubaguzi.

Alisema idadi ya wahitimu wote wa TIA kwa mwaka wa masomo 2022/2023 kwa Kampasi za Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Singida ni 13,218 ambapo wanawake ni 7,139 sawa na asilimia 54 na wanaume ni 6,079 sawa na asilimia 46.

Alisema wanaposherehekea mahafali hayo ya Ishirini na moja TIA imepiga hatua kubwa katika uendeshaji wa mafunzo, huduma ya ushauri wa kitaalam, rasilimali watu, pamoja na miundombinu ya kusomea na kufundishia katika kampasi hii ya Singida.

Alisema idadi ya wanachuo wanaodahiliwa katika Kampasi ya Singida imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Mathalani, katika mwaka huu wa masomo 2023/2024, ulioanza Mwezi Oktoba, 2023, jumla ya wanachuo 1,443 wamedahiliwa katika kampasi ya Singida.

Aliongeza kuwa hata hivyo, zoezi la usajili bado linaendelea na lengo ni kudahili wanachuo wapya 2,600 ukilinganisha na udahili wa wanachuo 1,556 katika mwaka wa masomo 2022/2023. 

Alisema ongezeko hilo la wanafunzi kwa kiasi kikubwa linatokana na mambo makubwa matatu ambayo ni  ubora wa elimu itolewayo inayotokana na mitaala inayowajengea wanachuo wa ngazi zote msingi wa umahiri hivyo kumwezesha mhitimu kuajiriwa na hata kujiajiri pindi anapohitimu masomo yake. Hatua hii huwafanya wazazi na wanafunzi kuichagua TIA.

Utaratibu mzuri wa Serikali wa kuwapangia vyuo moja kwa moja wahitimu wa kidato cha nne waliofaulu na kukidhi vigezo (kupitia TAMISEMI). Mathalan, katika mwaka wa masomo 2023/2024 jumla ya wanafunzi 1,170.

"Ongezeko la mikopo kwa wanafunzi wa kozi za shahada hatua ambayo imewezesha watanzania wengi wenye sifa kumudu gharama za masomo.  Kwa mfano, katika mwaka huu 2023/2024 Serikali imepanga kuwafadhili wanachuo 810 wa shahada katika kampasi hii ya Singida na hili ni ongezeko la asilimia 15.9 ukilinganisha na wanachuo 699 waliofadhiliwa mwaka 2022/2023," alisema Pallangyo.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleimani Mwenda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo alisema amefurahishwa sana na mpango wa ukuzaji na uendelezaji wa wanafunzi kitaaluma na kitaalamu yaani (Career Development Program) wanaoufanya kwa wanafunzi wa taasisi hiyo kwa kujitengenezea fursa muhimu za kibiashara kwa kuendeleza

ubunifu wao ambao ni fursa adhimu kwa wanafunzi hao.

“ Mmedhihirisha umahiri wenu, na kutupa wasaa wa kushuhudia matunda ya juhudi zenu. Hivyo, sina budi kwa niaba ya Serikali, kutoa pongezi zangu za dhati kwa Uongozi, Wahadhiri na wafanyakazi Waendeshaji, kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kipindi chote cha mafunzo yenu. 

Safari yenu ya mafunzo haikuwa nyepesi; safari yenu ilihitaji uvumilivu, ushirikiano, nidhamu, kujituma na zaidi ya yote kumtegemea Mungu. Kwa pamoja, haya ndiyo yamewawezesha kufikia hatua hii muhimu,” Mwenda alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Serikali.

Aidha, Mwenda aliwaasa wahitimu hao kwamba, hatua

waliyoifikia iwe ni chachu ya kujiimarisha zaidi kitaaluma ili kuweza kushindana katika soko la ajira na kujiajiri na kuwa  Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inahimiza sana Taasisi zote kuhakikisha elimu inayotolewa kwa wanafunzi iwe elimu, ujuzi na maarifa ya kukidhi mahitaji ya soko ili itumike kuleta tija na maendeleo yanayoendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

 Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Pallangyo, akizungumza kwenye mahafali hayo.

Mkurugenzi wa TIA Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema akiwatambulisha wageni waalikwa.


 Mhitimu wa Shahada ya Uhasibu kutoka kampasi ya Singida, Patrick Edward  akipokea cheti kutoka kwa mgeni rasmi 


Viongozi wa TIA wakiwa kwenye mahafali hayo. Kutoka kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa TIA, Dkt. Momole Kasambala, Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala TIA, Dkt. Issaya Hassanal na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko TIA, Lilian Rugaitika.

Mratibu wa Taaluma, Flora Lemnge akizungumza. 

Viongozi wakiwa meza kuu. Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha, Thabiti Dokodoko, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara, Wakili Said Chiguma, Mgeni rasmi wa Mahafali hayo, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Afisa Mtendaji wa TIA, Profesa, William Pallangyo na Mkurugenzi wa TIA, Kampasi ya Singida, Dkt. James Mrema.

Wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wakiwa kwenye maandamano kuelekea kwenye viwanja vya mahafali hayo.



Wahitimu wa Shahada ya Uhasibu wakionesha furaha yao kabla ya kutunukiwa vyeti vyao.

Viongozi mbalimbali na Waadhiri wa TIA wakiwa wamejipanga foleni tayari kwa kumpokea mgeni rasmi wa mahafali hayo.

Mkuu wa Idara ya Mpango wa ukuzaji na Uendelezaji wa Wanafunzi Kitaaluma na Kitaalamu yaani(Career Development Program) wa taasisi hiyo, Imani Matonya (mwenye suti katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajasiriamali wanafunzi wa TIA Kampasi ya Singida wakati wakimsubiri mgeni rasmi kuona bidhaa zao na kuzungumza nao.

Taswira ya mahafali hayo.

Mratibu wa Ujasiriamali na Kituo Atamizi wa Kampasi ya Singida, Mohamed Kaluse, akizungumza kwenye mahafali hayo ya 21.

Wahitimu wa Shahada ya Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala wakionesha furaha zao baada ya kutunukiwa vyeti vyao.

Waadhiri wa TIA wakiwa kwenye mahafali hayo.


Thursday, November 9, 2023

COTUL YATOA OMBI KWA SERIKALI KUSAIDIA MANUNUZI MACHAPISHO YA KIELEKITRONIKI

Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua kongamano la kisayansi ambalo limeandaliwa na Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL) kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi 

.................................................... 

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKISHO la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL) limeiomba Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kusaidia kununua machapisho ya kielekitroniki  yanayotumika kufundishia vyuoni kwa kuwa yanauzwa bei ghali ambayo shirikisho hilo haliwezi kumudu kuyanunua.

Mwenyekiti wa Shirikisho hilo , Dkt. Sydney Msonde alitoa ombi hilo Novemba 9, 2023 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi ambalo limewakutanisha wanataaluma mbalimbali katika ngazi ya wakutubi, walimu wafundishaji kutoka  vyuo vikuu Tanzania Bara na Visiwani, watafiti pamoja na watu wanaoshughulika na masuala ya teknolojia (IT)

Alisema pamoja na kwamba lengo la COTUL ni kuhakikisha kwamba machapisho ya kielekitroniki yanapatikana kwa walimu na wanafunzi ili waweze kufanya shughuli zao za msingi za kujifunza, kufundisha na kufanya utafiti hapa nchini lakini kununua machapisho hayo imekuwa changamoto kutokana na kuuzwa bei ghali. 

Dkt. Msonde alitoa mfano uchapishaji wa kanzi data inayoitwa 'Sience Direct' ambayo inauzwa dola za Marekani 250,000 hivyo sio rahisi kwa taasisi moja za hapa nchini kuweza kumudu kununua chapisho kama hilo. 

“COTUL kazi yetu kubwa ni kuhamasisha na kuzileta pamoja taasisi zote za umma na za watu binafsi ili ziweze kuchangia kwa sehemu rasilimali fedha zitakazo wezesha kununua machapisho hayo ya msingi katika kukidhi haja ya kufanya ufundishaji na utafiti nchini,” alisema Dkt. Msonde.

Dkt. Msonde alisema uhaulishaji na upatikanaji wa machapisho hayo unaweza usiwe na tija kama walimu na wanafunzi watakao kuwa wanayatumia hawatajengewa uwezo bora wa kuyatumia jambo ambalo ndilo la msingi. 

Alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili mustakabari wa fani ya ukutubi na namna gani walimu katika taasisi za umma na watu binafsi wanaweza kutumia machapisho ya kielekitroniki katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu, alipongeza COTUL kwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 15 tangu shirikisho hilo lilipoanzishwa mwaka 2008.

Alisema shirikisho hilo limekuwa msaada mkubwa kwa serikali kwa kuisaidia kupata taarifa na maarifa mbalimbali ambayo kwa njia ya kawaida ingekuwa ni gharama kubwa kuyapata.

"Uwepo wa COTUL ni fursa hata kwa sisi tunaohusika na kufanya tathmini mbalimbali zikiwemo za utafiti hakika ni jukwaa muhimu sana," alisema Mwinyimkuu.

Mwinyimkuu alisema Serikali itaendelea kuunga mkono kazi zinayofanywa na COTUL na kuliomba shirikisho hilo kukutana na wadau wa elimu ndani ya Serikali ili waone namna ya kushirikiana nao na kuwa kazi zao zinazihitaji na hazikwepeki hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inahitaji teknolojia kwa ajili kukuza uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa  Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inafanya maboresho makubwa ya maktaba kutoka katika mfumo wa kuhifadhi vitabu na machapisho mengine kwa njia ya kizamani ya karatasi na kwenda kwenye mfumo wa kidijitali.

Mmoja wa wafadhili wa kongamano hilo Mkurugenzi wa Kampuni ya Totoo Ltd yenye makao yake makuu mkoani Kilimanjaro, Dkt. Elvis Silayo alisema changamoto kubwa inayowafanya watu wengi washindwe kuitumia maktaba kwanza wanakuwa hawajui taarifa ambazo wanaweza kuzipata  na imekuwa ikichukuliwa kama sehemu ya taaluma na inatakiwa kuwa mashuleni.

Alisema watu wengi hawapendi kusoma mambo ya taaluma lakini maktaba kuna taarifa nyingi ambazo wanaweza kuzipata na kuwasaidia kupata maarifa yanayoweza kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Alisema maktaba za sasa zinavitabu vilivyochapishwa kwenye miaka ya 70 na 80 hivyo taarifa zake haziwezi kuwa na msaada kwa mtu anayehitaji kufanya chochote kwa kipindi hiki na kueleza kuwa maktaba za sasa zinapaswa kwenda mbele zaidi kwa kuwa na taarifa ambazo zinakwenda na wakati.

Silayo alisema ile dhana iliyozoeleka kuwa maktaba zipo kwa ajili ya kumuandaa mwanafunzi afaulu mtihani sasa iachwe badala yake zitumike kuwaandaa kimaisha.

 Naye Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Valeria Kyumana, alisema mafunzo hayo yamewajenga kwasababu hivi sasa teknolojia inakuwa na maktaba na huduma wanazotoa haziwezi kuendelea kwa kutumia mfumo wa zamani waliokuwa wakiutoa.

“Ni lazima tuangalie teknolojia inavyokwenda tukue nayo na kama sisi wakutubi tuweze kuichukua na kuitoa kwa wateja wetu tunaowahudumia ambao ni wanafunzi na watu wengine,” alisema Kyumana.

Baadhi ya wadhamini wa kongamano hilo ni Totoo Company Ltd, Ebsco, Elsevier,  Jove, Buku,Eclat, Bookstore, emerad insight, TCC na  LexisNexis.

Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mwenyekiti wa  Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL), Dkt. Sydney Msonde akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Katibu Mkuu Chama cha Wakutubi Tanzania (TLA), Dkt  Rhodes Mwageni akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.

Katibu Mkuu   wa  Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL), Dkt. Vincent Msonge akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo. 
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Totoo Ltd yenye makao yake makuu mkoani Kilimanjaro, Dk. Elvis Silayo akizungumza kwenye kongamano hilo.
Keki ya kutimiza miaka 15 tangu kuzaliwa kwa COTUL mwaka 2008 ikikatwa
Makamu Mwenyekiti COTUL, Profesa Kelefa Mwamtimwa, akitoa neno la shukurani kwa mgeni rasmi na wadau wengine wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Wakutubi wakiwa kwenye kongamano hilo.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Kongamano likiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Wakutubi wakiwa kwenye kongamano hilo.
Viongozi meza kuu wakishiriki kuimba wimbo wa Taifa kabla ya ufunguzi wa kongamano hilo.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Wakutubi wakionesha moja ya ishara ya mshikamano.
Viongozi wa COTUL wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu (katikati waliokaa) baada ya kufungua kongamano hilo Novemba 9, 2023.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamaja ba mgeni rasmi
Picha ya pamoja.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini wa kongamano hilo.

Picha ya pamoja mgeni rasmi na washiriki wa kongamano hilo.