Saturday, September 23, 2023

WILAYA YA MKALAMA WAPOKEA MWENGE WA UHURU 2023 KUTOKA IRAMBA, WAPONGEZWA UTEKELEZAJI MIRADI

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali (kulia) akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda baada ya kumaliza mbio zake wilayani humo Septemba 23, 20223 katika makabidhiano yaliyofanyika Viwanja vya Chuo cha Ufundi cha FDC kilichopo Kata ya Msingi wilayani humo.

..............................................................................


Na Dotto Mwaibale, Mkalama

WILAYA ya Mkalama mkoani Singida imepokea Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 kutoka Wilaya ya Iramba  mapokezi yaliyofanyika Septemba 23, 2023 Kata ya Msingi wilayani humo na kupongezwa kwa utekelezaji wa miradi ambapo kesho alfajiri Septemba 24, 2023 utakabidhi mbio hizo Wilaya ya Singida DC.

Akizungumza wakati akiupokea Mwenge wa Uhuru, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali  alisema ukiwa wilayani humo utatembelea, utakukagua, kufungua, kuzindua na kuweka jiwe la msingi kwenye miradi mbalimbali yenye thamani ya Sh. Bilioni 1.7.

" Mwenge wa Uhuru ukiwa katika wilaya yetu utakimbia umbali wa kilometa 150.8  na kupitia miradi ya elimu, afya, maji,barabara, programu za vijana, utunzaji wa mazingira, masuala ya ujasiriamali na mambo mengine," alisema Machali.

Alisema ukiwa katika wilaya hiyo Mwenge huo utakimbizwa katika tarafa tatu na kwenye kata mbalimbali ambapo wananchi watapata fursa ya kuushangilia na kuwaweka pamoja na kupitia kauli mbiu ya Mwenge wa Uhuru ya mwaka huu isemayo Tunza Mazingira, Okoa Vyanzo vya maji kwa Ustawi wa Viumbe Hai na Uchumi wa Taifa watazindua programu ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti zaidi ya 500 katika Shule ya Msingi Mayelu.

"Niwakaribisheni wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika wilaya yetu ya Mkalama tumejiandaa vizuri na tutashirikiana kuukimbiza katika maeneo yote na nichukue nafasi hii kuwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kupokea Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu 2023” alisema Machali.

Akizungumza na wananchi kwa nyakati tofauti wakati  akitembelea miradi hiyo kiongozi wa mbio hizo , Abdalla Shaib Kaim amesisitiza kuwepo na uaminifu, uzalendo na usimamizi wa kina kwenye miradi ya maendeleo kwa kuzingatia kuwa fedha nyingi zimetolewa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hivyo ni vizuri miradi hiyo ikakamilika kwa thamani halisi na si vinginevyo.

Mkimbiza mwenge huyo aliipongeza wilaya hiyo kwa kukamilisha miradi kwa kiwango cha juu na akaomba zile kasoro ndogondogo zilizojitokeza katika baadhi ya miradi kuzirekebisha.

Aidha, Kaim akishiriki kupanda miti katika Shule ya Msingi Mayelu alihimiza suala zima la utunzaji wa  mazingira katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Akitoa neno la shukrani Mbunge wa Jimbo la Iramba Mashariki, Francis Isack alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuijali Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali na akawaomba wananchi kumpa zawadi ya kipekee kwa kumpa kura nyingi wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025.

Baadhi ya miradi iliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru Mwaka 2023 ni Matengenezo ya barabara za Mwando-Mng'anda- Mwanga (Km 12.39) na Ishenga- Iambi (Km 4.12) mradi ambao upo Tarafa ya Nduguti, Kata ya Nduguti na Ilunda ambao umegharimu Sh.314,986,600.82 fedha zilizotolewa na Serikali kuu kupitia tozo.

Miradi mingine ni wa vijana wa kilimo cha nyanya, ujenzi wa miundombinu ya mradi wa maji katika Kijiji cha Malaja ambao umegharimu Sh.565,000,000 ambao utawapunguzia adha wananchi wapatao 6,611 kwa kufuata maji umbali mrefu, Programu ya mapambano dhidi ya malaria ambapo wilaya hiyo imeweza kutoa vyandarua 22,098 kwa walengwa ambao ni wajawazito 8,116 na watoto chini ya umri wa mwaka mmoja, 9,782.

Miradi mingine iliyotembelewa ni ujenzi wa Shule ya Msingi Nkindiko, uzinduzi wa daraja la Iambi na uzinduzi wa Klabu ya kupinga rushwa katika Shule ya Nduguti Pre And Primary English Medium School.

Vijana wa Skauti, Wansinguya Edward (kushoto) na Elia Kamata wakifanya itifaki kwa kumvika Skafu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim kabla ya kuanza mbio za mwenge huo wilayani Mkalama.
Vijana wa Skauti, wakifanya itifaki kwa kumvika Skafu Mkimbiza Mwenge wa Uhuru 2023, Tupokigwe Elia kabla ya kuanza mbio za mwenge huo wilayani Mkalama.
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mkalama (SSP) Richard Mwaisemba, akiwa ameushika Mwenge wa Uhuru kabla ya kuanza kukimbizwa wilayani humo.
Watoto wakionesha furaha zao wakati wa kuupokea mwenge huo.
Hamasa zikifanyika wakati wa mapokezi ya mwenge huo.
Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Wilaya ya Mkalama wakiwa tayari kwa kukimbiza mwenge huo. Kutoka kushoto ni Emilian Masheyo, Iddi Juma, Abdul Said, Plasido William, Karoline Remiji na Maria Sekidava.
Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha FDC Wilaya ya Mkalama wakiwa kwenye mapokezi hayo.
Vijana wa Skauti wakiwatayari kwa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Viongozi, wakuu wa idara na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo wakiwa kwenye mapokezi ya mwenge huo.
Vijana wa  Halaiki wakiwajibika wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2023..
Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda (wa pili kulia) akiongoza kukimbiza Mwenge wa Uhuru 2023 kabla ya kuukabidhi kwa Wilaya ya Mkalama.,
Mwenge wa Uhuru 2023 ukikimbizwa baada ya kuwasili wilayani Mkalama.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim, akizungumza na viongozi wa Wilaya ya Iramba wakati alipokuwa akiwaaga kabla ya kuanza kuukimbiza mwenge huo wilayani Mkalama.
Muonekano wa shamba la nyanya la vijana wa Mkalama ambalo lilikaguliwa na viongozi wa mbio za mwenge.
Nyaraka za mradi wa shamba la nyanya la vijana hao zikikaguliwa na viongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023.
Mwonekano wa shamba darasa la Programu ya Lishe lililopo Shule ya Msingi Mayelu.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mayelu wakiwa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wakati ulipofika kukagua miradi mitatu inayotekelezwa shuleni hapo ambayo ni programu ya lishe, Utunzaji mazingira na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa. 
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim, akivuta pazia kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa darasa katika shule hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali.

Muonekano wa moja ya darasa lililojengwa katika shule hiyo.
Ukaguzi na uwekaji wa jiwe la mradi wa maji wa Kijiji cha Malaja ukifanyika.
Wananchi wakiwa katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa  barabara za Mwando-Mng'anda- Mwanga (Km 12.39) na Ishenga- Iambi (Km 4.12).
Ukaguzi wa daraja la Iambi ukifanyika.
Wananchi wa Kijiji cha Iambi wakiserebuka wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa barabara hiyo.
Muonekano wa jengo la Utawala  la Shule ya Msingi, Nkindiko iliyokaguliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru 2023. iliyopo Kata ya Ishenga wilayani humo.
Wananchi wa Kata ya Ishenga wakiwa kwenye hafla ya kuupokea Mwenge wa Uhuru baada ya kuwasili kutembelea na kuikagua shule hiyo.
Muonekano wa baadhi ya madarasa ya shule hiyo.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim, akigawa vyandarua kwa wajawazito kupitia mradi wa kupambana na malaria kwa wajawazito na watoto walio na umri chini ya mwaka mmoja unaoendeshwa na Hospitali ya Wilaya ya Mkalama.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim, akishirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali wakiteketeza pombe haramu aina ya Gongo ambayo ilikamatwa na jeshi la polisi wilayani humo. Anayeshuhudia kulia ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mkalama, SSP Richard Mwaisemba.
Wanafunzi wa Shule ya Nduguti Pre And Primary English Medium School wakiimba nyimbo baada ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim, kuzindua Klabu ya Kupinga vitendo vya rushwa.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim, akikabidhiwa taarifa ya uanzishwaji wa klabu hiyo ya kupinga rushwa iliyoanzishwa katika shule hiyo.
Askari wa Jeshi la Akiba wakihimarisha ulizi katika mkutano baada ya Mwenge wa Uhuru 2023 kuwasili eneo ambalo utakesha.
 

Friday, September 15, 2023

SATF YAIPIGA JEKI WILAYA YA IKUNGI KUUNDA KAMATI ZA MTAKUWWA KATIKA KATA KUMI

Meneja Miradi wa Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa (kulia) akizungumza na wajumbe wa kamati za Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku nne yaliyoanza Septemba 12, 2023 Wilaya ya Ikungi mkoani Singida na kufikia tamati Septemba 15, 2023. 

..................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida 

TAASISI ya Social Action Trust Fund (SATF) iliyoanzishwa kwa udhamini wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Serikali ya Marekani (USAID) na kuratibiwa na Serikali ya Tanzania kwa lengo la kusaidia juhudi za Serikali katika kutoa huduma kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu waweze kuzifikia ndoto zao limeiwezesha Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida kuunda kamati za Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) katika kata kumi..

Uundwaji wa kamati hizo katika kata hizo ulienda sanjari na wajumbe walioteuliwa kupata mafunzo ya namna ya kuziendesha kamati hizo na kujua utekelezaji wa Mpango Kazi huo wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ambapo wajumbe hao ni ni viongozi kutoka idara mbalimbali za serikali, Asasi za Kiraia,viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu, wanafunzi na wanawake chini ya mwenyekiti wake Afisa Mtendaji wa Kata.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Meneja Miradi wa taasisi hiyo Nelson Rutabanzibwa alisema taasisi hiyo imekuwa ikiwawezesha watoto hao kwa kuwapeleka shuleni, ikiwa hilo halitoshi na kuhakikisha afya zao zinakuwa sawa kwa kuwapatia bima ya afya.

Alisema pamoja na hayo kutokana na watoto hao kutoka katika kaya zenye utete wana hakikisha wanakuwa katika ulinzi na usalama na ndio shabaha kubwa ya kukutana katika kikao hicho cha mafunzo ya kamati hizo za MTAKUWWA zenye lengo la kumlinda mtoto dhidi ya masuala yote ya ukatili.

Alisema kamati hizo zinawasaidia katika miradi yao kuhakikisha watoto wanabaki shuleni kwa sababu vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto vinawafanya washindwe kutimiza ndoto zao kwa kupewa mimba, ndoa za utotoni huku wengine wakiingizwa kwenye ajira wakiwa na umri mdogo na wale wengine ambao -+-+kwa uzembe wao wanaacha tu kwenda shuleni.

Alisema kwa Mkoa wa Singida ipo changamoto kubwa ya watoto kuacha shule kwani walianza na watoto 80 lakini hadi sasa wamebaki na watoto 78 baada ya watoto wawili kutoka kwenye mradi kutokana na sababu mbalimbali kama, mimba, utoro na masuala ya nidhamu.

“Kupitia kamati hizi tunategemea zitaweza kutusaidia kutokana na wajumbe wake kuwa ni polisi ngazi ya kata, maafisa maendeleo, waratibu wa elimu, watendaji wa kata na wengine wote wenye majukumu mbalimbali ngazi ya jamii ambao kwa namna moja yanaweza kusaidia kuwaondolea vikwazo watoto hao washindwe kuendelea na masomo yao,” alisema Rutabanzibwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki kuyatendea kazi hasa kutokana na unyeti wa masuala hayo ya ukatili ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa kwenye jamii.

“Niwaombe sana mafunzo mnayopata hapa baada ya kwenda huko kwenye jamii mkayafanyie kazi kwa kuwafichua wanayotenda na kuhakikisha yanafikishwa kwenye vyombo vya dola na kuepuka kupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa kwa lengo la kuwasaidia,” alisema Myula.

Myula alitumia nafasi hiyo kulishukuru shirika hilo la SATF kwa kuiwezesha halmashauri hiyo kwa kuunda kamati hizo katika kata hizo kumi ambazo zinakwenda kuongeza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake.

Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi ambao wanafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi hiyo alisema kwa ushirika wao wameweza kufanya kazi katika Kata nne za Ihanja, Lighwa, Isunna na Kituntu ambapo waliwabaini watoto 80 ambao walikuwa katika mazingira magumu ambao wamepata ufadhili wa masomo kupitia Taasisi hiyo ya SATF.

Alisema kati ya watoto hao wawili waliondoka kwenye mradi na kuwa hao wengine wanaendelea na masomo katika shule mbalimbali za sekondari ambazo amezitaja kuwa ni Isuna, Masinde, Lighwa, Utaho, Miandi na wengine wapo Chuo cha Ufundi Stadi cha FDC kilichopo Manispaa ya Singida.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Mariam Mwandekile alisema mafunzo hayo yamelenga kuzifikia kamati za MTAKUWWA katika kata 10 ambazo  ni Puma, Kituntu, Ihanja, Issuna, Dung’unyi, Mtunduru, Sepuka, Makiungu, Mungaa na Lighwa.

Alisema anaamini kabisa kuwa kamati hizo zitakapoanza kutekeleza majukumu na mikakati yao zinakwenda kumaliza kama sio kupunguza kabisa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwenye maeneo yao.

Alisema baada ya mafunzo hayo watakwenda kutengeneza mpango kazi na kuanza kuutekeleza ambapo kila baada ya miezi mitatu watakuwa wakitoa taarifa ambayo itaunganishwa na ya wilaya hiyo na kuwa kila mmoja wao atakuwa ni balozi wa kutoa elimu ya kupinga vitendo vyote vya ukatili katika sehemu zao.

Afisa wa Dawati la Jinsia Kituo cha Polisi Wilaya ya Ikungi, Musa Musa alisema katika wilaya hiyo bado kunachangamoto ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vikiwamo vipigo kwa watoto na wanawake, mimba za utotoni, ubakaji, ulawiti na kurithiwa wajane baada ya waume zao kufariki na baadae wakijikuta wakifukuzwa na kunyang’anywa mali walizozichuma na wenza wao.

Alisema kesi nyingi za matukio hayo zimekuwa hazipati ushindi kutokana na mashahidi kushindwa kufika mahakamani kwa sababu mbalimbali zikiwamo za wahusika kupatana na watuhumiwa kwa kupewa fedha hivyo jamuhuri kushindwa kuendelea na kesi hizo kwa kukosa ushahidi.

Alisema desturi ya wajane kurithiwa na ndugu au mdogo wa mume wake baada ya kufariki bado ipo katika wilaya hiyo na inafanyika kwa mtindo wa aina yake kwa familia husika kumchagua mmoja wanafamilia kuwa mwangalizi wa familia ya marehemu ambapo utakuta mjane huyo akiendelea kuzalishwa na endapo atakataa kufanya hivyo atajikuta akifukuzwa huku akinyang’anywa mali alizochuma na mume wake.

Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Flora Temba alisema kuna aina nyingi za ukatili wa kijinsia ambao watu wamekuwa wakifanyiwa hasa watoto na wanawake ambao ameutaja kuwa ni wa kingono, kiuchumi, kisaikolojia, vipigo, kunyang’anywa ardhi.

Temba alisema iwapo atatokea mtu kufanyiwa ukatili huo anaweza kutoa taarifa, kituo cha polisi dawati la jinsia, kwa wajumbe wa kamati ya MTAKUWWA, ofisi za Kata, maafisa wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii na Huduma ya Mkono kwa Mkono (One Stop Centre) na maeneo mengine ambayo ataona anaweza kupata msaada.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo ya MTAKUWWA, Mwinjilisti Isaya Jibu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) akiliwakilisha kundi la viongozi wa dini na mwakilishi wa wanafunzi Salima Juma kutoka Shule ya Msingi ya Damankia walisema kamati hizo zinakwenda kuwa mwiba kwa wale wote wanaoendelea kufanya vitendo hivyo.

Mwinjilisti Jibu ametoa mwito kwa wananchi wa maeneo yote ya kata hizo kutoa taarifa za matukio yote ya ukati kwa wajumbe hao ili watuhumiwa waweze kuchukuliwa hatua na vyombo husika

Meneja Miradi wa Taasisi ya Social Action Trust Fund (SATF) Nelson Rutabanzibwa, akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo. 
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Mariam Mwandekile, akitoa mada kuhusu MTAKUWWA.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Flora Temba, akizungumzia kuhusu aina za ukatili wa kijinsia na namna ya utoaji wa taarifa kwa mtu aliyefanyiwa vitendo hivyo. 
Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi, akiwa kwenye mafunzo hayo.
Wajumbe wa MTAKUWWA wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Taswira ya mafunzo hayo.

 Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi.

Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja. Aliye chuchumaa ni Mratibu wa Shirika la Oblige for Valnerable Children Tanzania (OVCT) lenye Makao Makuu Puma wilayani Ikungi mkoani hapa, Benard Sungi.

Wednesday, September 13, 2023

VETA KANDA YA KATI YATOA MAFUNZO YA UFUGAJI WA MBUZI, KONDOO WILAYA YA IKUNGI BAADA YA KUBAINI SOKO LA UHAKIKA

Afisa Masoko na Utafiti Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati, Sadan Komungoma (katikati) akizungumza na wajasiriamali wakati wa mafunzo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo yaliyoandaliwa na VETA kwa wananchi wa Kata ya Unyahati wilayani Ikungi yaliyofanyika Septemba 13, 2023 Chuo cha VETA Ikungi mkoani Singida. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula na kushoto ni Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ladslous William Mwalimu kutoka VETA Singida.

..........................................................................


 Na Dotto Mwaibale, Ikungi 

MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kanda ya Kati inaendelea kutoa mafunzo ya ufugaji wenye tija wa mbuzi na kondoo kwa wajasiriamali wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida ili waondokane na ufugaji wa mazoea kwenda kwenye ufugaji wa kibiashara ambao utawakwamua kiuchumi.

 Afisa Masoko na Utafiti VETA Kanda ya Kati, Sadan Komungoma, akizungumza leo Septemba 13, 2023  wakati wa mafunzo hayo kwa wajasiriamali wa Kata za Unyahati Kijiji cha Muungano wilayani Ikungi mkoani Singida alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wananchi kufanya ufugaji wenye tija na kuwapatia masoko ambayo yatawaongezea kipato.

"Mafunzo haya ni ya awamu ya pili kutolewa katika Chuo cha VETA Ikungi tangu kilipozinduliwa mwaka jana yanalenga kuboresha biashara za wananchi ili wafuge mbuzi, kondoo na kuku kwa ubora ambao utaongeza thamani ya nyama na mayai," alisema.

 Komungoma,alisema VETA imeanza kutoa mafunzo hayo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo kutokana na Mkoa wa Singida kuwa na soko kubwa la wanyama hao hasa wakati wa Sikukuu ya Eid al-Adha  ya kuchinja ambapo maelufu ya wanyama hao uchinjwa lakini wakinunuliwa kutoka mikoa mingine baada ya Singida kutokuwa nao wa kutosha.

" Mkoa wa Singida unawaumini wengi wa dini ya kiislam ambao moja ya nguzo yao kuu ni kutimiza ibada ya chinja ya wanyama kama ng' ombe, mbuzi na kondoo ambao kama wangekuwa wanapatikana kwa wingi wasingekuwa wanakwenda kununuliwa mikoa mingine bali wangepatikana hapahapa na kuwa fursa kwa wakazi wa Singida," alisema Komungoma.

Alisema baada ya VETA kufanya utafiti na kubaini kuwepo kwa soko la wanyama hao ndipo wakaja na mpango wa kutoa mafunzo hayo yenye lengo la kubadilisha uchumi wa wana Singida kwa kupitia ufugaji wa wanyama hao ambao hawashambuliwi na magonjwa ya mara kwa mara kama ilivyo kwa wanyama wengine.

Alisema VETA inatoa mafunzo ya muda mfupi  kwa wajasiriamali kwenye mikoa ya kanda ya kati ambayo ni Dodoma,Singida na Manyara ili kuwawezesha wananchi kunufaika na uwepo wa vyuo vya VETA vilivyoanzishwa kila wilaya ili wajikwamue kiuchumi kupitia ujasiriamali na ufugaji.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo aliwataka washiriki kuzingatia yale ambayo watafundishwa kwani ni mafunzo yenye tija na yana kwenda kuinua maisha ya familia na taifa kwa ujumla.

"Hivi sasa ufugaji unafaida sana ukienda Mnadani kule njia Panda mbuzi mmoja anauzwa hadi Sh.200,000 tofauti na bei waliyokuwa wakiuzwa zamani nawaombeni zingatieni mafunzo haya kwani ni ya muhimu sana," alisema Myula.

Aidha, Myula alisema mafunzo hayo ni fursa kwao kwani baada ya kuyapata kutapanua wigo wa utafutaji kwa kuuza mifugo yao, mayai na mazao mengine yanayotokana na wanyama hao na watakuwa wamepata ajira ya kudumu tofauti na ile ya kuajiriwa kwa mtu au Serikalini.

Myula alitumia nafasi hiyo kuwashukuru VETA kwa kutoa mafunzo hayo na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha  fedha kwa ajili ya kuwasaidia watanzania kukuza uchumi wao.

 Washiriki  wamafunzo hayo Mwanahamisi Hamisi, Gangala Nsunaluga, Saida Juma na Sauli Mayele walisema licha ya kuanza ufugaji tangu siku nyingi lakini walikuwa hawajui mbinu za ufugaji wa kisasa wenye tija na kuwa wanaishukuru VETA kwa kuwapa mafunzo hayo.

Mfugaji na mkulima Mariam Ntandu kutoka Kijiji cha Muungano Kata ya Unyahati, Ikungi anasema anamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea Chuo cha Ufundi cha  VETA katika wilaya hiyo na kuwezesha fedha za mafunzo hayo na kuwa shukurani za pekee ziende kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA Kanda ya Kati John Mwanja na watendaji wenzake kwa kuwapelekea mafunzo hayo ambayo yanakwenda kubadilisha maisha yao kupitia fursa za ufugaji wa kisasa.

Alisema shukurani nyingine zimuendee Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi kwa kuwapelekea wataalam ambao wamekuwa wakiwafundisha mbinu za kilimo na ufugaji bora wa kuku, mbuzi na kondoo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Eva Myula  akifungua mafunzo hayo.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Ladsilous William Mwalimu kutoka VETA Singida.akitoa mafunzo ya ufugaji wa mbuzi na kondoo kwa washiriki wa mafunzo hayo.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Elisha Kitisho akitoa mafunzo ya ufugaji bora wa wanyama hao.
Afisa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Penveli Raphaely akitoa mafunzo ya ufugaji bora wa wanyama hao.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wajasiriamali hao, Sauli Mayele akizungumza wakati wa mafunzo hayo.
Mshiriki wa mafunzo hayo Mzee Gangala Nsunaluga akichangia jambo wakati wa mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Mshiriki wa mafunzo hayo Mwanahamisi Hamisi akiuliza swali kuhusu ufugaji wa mbuzi na kondoo.

 Mafunzo yakiendelea.

Picha ya pamoja