Wednesday, September 29, 2021

SINGIDA DC YAPONGEZWA KWA UELEWA WA UHAMASISHAJI CHANJO YA UVIKO 19

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii  na Lishe, Dinah Atinda, akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Singida DC      katika kikao kilichoketi mkoani hapa jana.    

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskas Muragili, akizungumza kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Picha ya pamoja.

 Picha ya pamoja.


Na Dotto Mwaibale, Singida.


MWAKILISHI kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii  na Lishe, Dinah Atinda amewapongeza wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Wilaya ya Singida DC kwa kuwa na uelewa mpana wa uhamasishaji wa chanjo ya Uviko 19 ambao unaendelea nchini kote.

Atinda alitoa pongezi hizo jana kwa niaba ya wenzake katika semina ya siku moja iliyokuwa ikitolewa kwa wajumbe hao wilayani humo.

" Tunapita katika Halmashauri zote kuangalia namna kinavyofanyankazi hiki kikao cha PHC lakini napenda kusema kikao hiki ni tofauti kidogo na vikao tulivyo vipitia ndugu mwenyekiti wa kikao 'Mkuu wa wilaya' inaonekana wajumbe wa kikao hiki wamepata elimu ya kutosha na wapo vizuri kabisa hivyo tunawapongeza sana,". alisema Atinda.

Alisema Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na TAMISEMI na wadau mbalimbali baada ya kuona hali ya nchi sio nzuri ugonjwa wa Uviko 19 unaendelea na watu wanakufa tukaona kuna haja ya kuanzisha  mpango mkakati shirikishi na harakishi kwa ajili ya kuhamasisha na kuelimisha jamii ili wote waweze kupata chanjo na kupunguza madhara yanayotokana na ugonjwa huo.

Alisema zoezi la mtu kuchanja ni la hiyari hivyo lifuate maagizo yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwa vituo vya chanjo sasa vimeongezwa hadi kufikia zaidi ya 6,500 na vinatoa huduma.

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Paskas Muragili alisema changamoto kubwa iliyopo kwa Watanzania ni kuwa hawajapewa elimu ya kutosha kuhusu chanjo na hawajui umuhimu wa chanjo hiyo lakini wanauelewa mkubwa wa mambo mbalimbali hivyo ni wajibu wa kamati hiyo kwenda kuwaelimisha na wakielewa watachanja.

Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo wajumbe wa kamati hiyo walisema sasa wanakwenda kufanya uhamasishaji wa nguvu wakianzia kwenye familia zao.

Walisema uhamasishaji huo wataufanya kwenye nyumba za ibada, magulio, mashuleni, na kwenye mikusanyiko ya watu.

Wajumbe hao walisema wataenda kutoa elimu hiyo kwa viongozi mbalimbali wa vijiji wakiwemo wa Serikali na vyama vya siasa lengo likiwa ni kuhakikisha wananchi wana elewa na kujitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo hiyo.

Tuesday, September 28, 2021

MSD KUANZISHA KIWANDA CHA DAWA ZA NGOZI NCHINI

Mkurugenzi Mkuu Bohari ya Dawa (MSD), Meja Jenerali Gabriel Mhidze akizungumza na  waandishi wa habari kwenye semina ya  siku moja iliyoandaliwa na MSD iliyokuwa na lengo la kutoa taarifa ya mafanikio na mwelekeo wa MSD,  jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa MSD Erick Mapunda.

Wafanyakazi wa MSD wakiwa kwenye semina hiyo.
Waandishi wa Habari wakiwa kwenye semina hiyo.
Semina ikiendelea.


Na Dotto Mwaibale


MKURUGENZI  Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Meja Jenerali Gabriel(Dkt) Mhidze amesema MSD iko mbioni kuanzisha kiwanda cha dawa za ngozi,ikiwemo mafuta maalumu ya watu wenye ulemavu wa ngozi.

Meja Jenerali Mhidze aliyaeleza hayo jana  mbele ya waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia kuhusu majukumu na maboresho ya MSD.

Alisema kiwanda hicho, ambacho mashine zake zimeshafika kitazalisha pia dawa za meno na dawa za macho.

Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo wa MSD ameeleza kuwa kiwanda cha  MSD cha kuzalisha mipira ya mikono kilichopo imIdofi, Makambako mkoani Njombe kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Novemba mwishoni,huku akisema viwanda vingine vya dawa za rangi mbili, vidonge na dawa za maji maji za watoto mashine zake zimeshaanza kuwasili.

Tayari ina viwanda vya kuzalisha barakoa na dawa Keko jijini Dar es Salaam,ambavyo vinauwezo wa kuzalisha aina 10 za dawa na barakoa.

MAFUNZO YA CHANJO KWA KAMATI ZA AFYA YA MSINGI WILAYA YA MKALAMA YAZAA MATUNDA


Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI) Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe, Dinah Atinda akizungumza jana wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa Wajumbe wa Kamati ya Msingi ya Afya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida yenye mpango harakishi wa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu chanjo ya Uviko 19 na kuchanja.


Richard Magodi kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Idara ya Mpango wa Taifa wa Chanjo akishiriki kutoa mafunzo hayo.
Mkuu wa wilaya hiyo Sophia Kizigo (katikati) akishiriki mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yakiendelea. Nyuma mwenye miwani ni Mchungaji Sefine Kanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT) Usharika wa Dumanga.
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI) Idara ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe, Dinah Atinda na Afisa Msanifu Patrice Makhao kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakifuatilia mafunzo hayo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Afya Wilaya ya Mkalama, Sippi Shabani akichangia jambo kwenye mafunzo hayo.
 Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama     Bosco Charles akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ibrahim Pazia, akipata chanjo hiyo.

     Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Mkalama Hamisi Ramadhani akizungumza kwenye mafunzoh hayo.

Mafunzo hayo yakiendelea.
Mafunzo hayo yakiendelea
Mafunzo hayo yakiendelea.
Mafunzo hayo yakiendelea.
Watoa Huduma wa Afya wilayani Mkalama wakisubiri kupata chanjo.


Na Dotto Mwaibale, Mkalama


MAFUNZO yaliyotolewa kwa Watoa Huduma wa Afya wilayani Mkalama mkoani Singida kwa ajili ya kutoa elimu  dhidi ya Uviko 19 kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo yamezaa matunda baada ya baadhi ya wahudumu hao kuelewa na kuchoma chanjo hiyo hivyo kuwa mabalozi wa kwenda kutoa elimu hiyo kwa wananchi.

Mafunzo hayo yalitolewa jana wilayani hapa kutoka kwa timu ya uhamasishaji wa chanjo kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Maofisa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa  (TAMISEMI)

Akizungumza wakati wa kufungua mafunzo hayo ya chanjo kwa Wajumbe wa Kamati ya Afya ya Msingi Mkuu wa wilaya hiyo Sophia Kizigo alisema changamoto ya wananchi kutojitokeza kwa wingi kwenda kupata chanjo hiyo kwa idadi ya watu 10 inaweza kuwa ni moja ya sababu iliyosababisha wilaya hiyo na zingine hapa nchini kuwa na idadi ndogo ya watu walioitikia mwito wa kupata chanjo.

" Utaratibu wa kutoa chanjo hiyo ilikuwa wapatikane watu 10 ili dawa itakayotumika isiweze kuharibika hivyo watoa huduma walikuwa wakisubiri ifike idadi hiyo ndipo watoe chanjo,". alisema Kizigo.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Jamii  na Lishe, Dinah Atinda alisema uelewa na uhamasishaji mdogo kwa wananchi kuhusu umuhimu wa chanjo hiyo iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan umechangia kwa kiasi kikubwa watu kutojitokeza kwa wingi kwenda kuchanjwa.

" Serikali imetumia fedha nyingi kuagiza chanjo lakini wananchi bado hawaja kwenda kuchanjwa hivyo imetengeneza mpango mkakati harakishi wa kutoa elimu na kuhamasisha jamii kuhusu chanjo ya Uviko 19 na kuchanja" alisema Atinda.

Alisema hatua iliyofikiwa na Serikali ni kuanza kutoa mafunzo kuanzia ngazi ya Taifa hadi kuwafikia walipo wananchi.

Richard Magodi kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Mpango wa Taifa wa Chanjo alisema baada ya kutokea vifo vingi maeneo mbalimbali duniani kutokana na ugonjwa huo sasa hivi vifo hivyo vimeanza kupungua kutokana na kutumia chanjo.

" Na sisi kama nchi na pia Taifa ambalo lipo miongoni mwa mataifa mengine lilikuwa ni jukumu letu kuishauri Serikali na kuanzisha mpango huu wa chanjo," alisema Magodi.

Magodi alisema chanjo hiyo ni salama na haina madhara yoyote baada ya kuhakikiwa na wataalamu na tayari imetolewa nchi mbalimbali duniani.

Wakizungumza baada ya kupata mafunzo hayo Mchungaji Setina Kanga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania  (KKKT) Usharika wa Dumanga alisema sasa anakwenda kuwaeleza waumini wake umuhimu wa kupata chanjo hiyo.

Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Mkalama Hamisi Ramadhani alisema awali alikuwa alielewi zoezi hilo la chanjo kutokana na kuwa na maneno mengi ya kukanganya lakini sasa anakwenda kutoa elimu hiyo kwa wananchi.

Makamu  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bosco Charles aliwataka washiriki wote waliopata mafunzo hayo kwenda kuhamasisha wananchi katika maeneo yao ili wapate chanjo hiyo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliopata chanjo hiyo ni Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Ibrahim Pazia, Afisa Elimu Taaluma Sekondari, Ernest Stephen, Kalisti Faustin ambaye ni Muuguzi, Nyandewa Zabron, Afisa Muuguzi Salum Mputa, Farida  Seleman, Aizack Zabron.

Monday, September 27, 2021

Wadau wa Maendeleo Kutia Nguvu Kwenye Uhamasishaji na Elimu ya Chanjo Mkoa Wa Singida

 


SERIKALI imewapongeza Wadau mbalimbali wa maendeleo waliojitokeza katika kikao kazi cha Sekta ya Afya Mkoani Singida na kujitolea viwezeshi mbalimbali vitakavyosaidia  kuendesha zoezi la  utoaji wa  hamasa, elimu na chanjo kwa jamii .

Baadhi ya wadau hao wameahidi kusaidia upatikanaji wa  magari ya matangazo, mafuta kwa ajili ya safari za vijijini  huku wengine wakiwa tayari kusaidia kupeleka elimu waliyoipata kuhamasisha jamii juu ya  zoezi la uchanjaji lengo likiwa na kufanikisha kwa kiwango kikubwa.

Pongezi hizo zimetolewa leo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida na Mganga Mkuu wa Mkoa Victorina Ludovick wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa  Hoteli ya KBH na kubainisha kwamba  jitihada zinazooneshwa na wadu hao zitasaidia katika kuwafikia watu wengi vijijini na kutoa elimu ya chanjo.

Mganga Mkuu wa Mkoa  Singida Victorina Ludovick akieleza jambo wakati wa mkutano huo.


Pamoja na hayo Mganga mkuu amesema kwamba Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbalia  itaendela kusambaza huduma ya chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 katika maeneo mbalimbali Mkoani Singida kama hatua muhimu ya kupambana  na kudhibiti  ugonjwa huo.

Amesema Chanjo zinaendelea kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma ambapo awali vilikuwa  vituo 21 vilivyoanishwa na  Serikali lakini kupitia Mkakati Shirikishi na Harakishi, Serikali  itawafikia wananchi kupitia vituo 219 vinavyotoa huduma za Chanjo.

Chanjo tayari zipo katika vituo vya kutolea huduma, lakini tunayo changamoto kubwa ya kufikisha elimu na hamasa ili wananchi wakubali kuzitumia” Alikaririrwa Mganga Mkuu

Aidha amebainisha kwamba  jamii imekuwa na mwitikio mdogo katika kupokea  chanjo sababu kubwa ikiwa ni hofu iliyojengeka licha ya jamii kushuhudia wananchi wengine wakiendelea kunufaika  bila kuwepo kwa madhara yoyote.

Kutokana na muingiliano mkubwa uliopo hasa kibiashara na kijamii kati ya Mkoa wa Singida, Mikoa mbalimbali na Nchi nyingine, ni muhimu kuchukua tahadhari za kutosha ili kuukabili ugonjwa, Alibainisha Dkt Ludovick.

Aidha Dkt Ludovick. amesisitiza kwamaba Chanjo zilizoruhusiwa kutumika hapa nchini ni salama hivyo kila mtanzania ana hiari ya kupata chanjo hiyo na kuwataka kutokuwa na hofu .

Aidha amewataka Wadau wote na viongozi wa Dini kusaidia jithada za Serikali ili Chanjo ziweze kuwafikia wananchi wote wenye uhiari wa kupatiwa Chanjo ili  kuiweka jamii salama.

Alimalizia kwa kusema kwamba Jukumu la kinga dhidi ya ugonjwa huu ni la kila mtanzania  hivyo kutoa wito kwa jamii kuendelea kuzingatia afua za kinga.

Hivyo, Wizara ya Afya inawataka Viongozi wote wa serikali, sekta binafsi, Viongozi wa Kijamii na madhehebu ya dini kuwajulisha wananchi wote kuchukua tahadhari zote muhimu, kuelimisha, na kutekeleza afua za kujikinga .

Awali mratibu wa Malaria mkoani Singida Dkt. Abdallah Balla alieleza lengo la mkutano huo kwamba ni kutoa taarifa kuhusu hali ya UVIKO-19 na udhibiti wake katika Mkoa wa huo na  kubadilishana uzoefu pamoja na  kuyatambua  maeneo  Serikali iliyofanya vizuri.

Dkt. Abdallah aliendelea kusema mkutano huo utasaidia kuongeza ufanisi na ubora unaohitajika katika utoaji wa huduma za afya kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa na Serikali na kuwepo kwa mfumo mmoja wa utoaji huduma unaoshirikisha wadau wote ( mfumo wa rufaa – “Vertical and Horizontal referrals”)

Mwenyekiti wa dini mbalimbali Mkoa wa Singida Sheikh Hamisi Mohamedi Kisuke akizungumza wakati wa mkutano

Naye Mwenyekiti wa dini mbalimbali Mkoa wa Singida Sheikh Hamisi Kisuke ameiomba serikali kuendelea kutoa elimu juu ya chanjo hasa kwa vijana kwa kuwa katika kipindi hiki wameonekana kutokujali ugonjwa huku wengi wao wakiwa hawajapata chanjo.

Ameihakikishia serikali kwamba kwa upande wa dini wanazo simamia wanaunga mkono na watashiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya chanjo kwa jamii kwa kuwa vitabu vya mwenyezimungu vinataka jamii kujikinga na mambo yenye kuangamiza. Alifafanua sheikh Kisuke.

Askofu wa Kanisa la Tanzania assemblies of God (TAG) Jimbo la Singida Kati Rev.Gasper Mdimi amesema wamejipanga kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kutoa elimu na hamasa juu ya chanjo ili kuwaepusha  watanzania juu ya  madhara makubwa yanayoweza  kutokana na ugonjwa wa KOVID 19.

Mratibu wa Malaria Mkoa wa Singida Dkt. AbdallaH Balla akieleza lengo la mkutano huo


Sunday, September 26, 2021

SERIKALI YATUMIA SH. BILIONI 52.975 KUTEKELEZA MIRADI MBALIMBALI SINGIDA

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akionesha Jarida la Nchi Yetu wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida leo.
Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa hiyo.
Taarifa ikitolewa.
Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo.
Waandishi wa habari wakisikiliza taarifa hiyo. Kushoto ni Afisa Habari Msaidizi Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mwanahabari Elisante Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mwanahabari Damiano Mkumbo akiuliza swali kwenye mkutano huo.
Mwanahabari  Edina Alex akiangalia   Jarida la Nchi Yetu kwenye mkutano huo. 
Waandishi wa habari wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Kazi ikiendelea,
Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu akiuliza swali kwenye mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


SERIKALI imetoa Sh.Bilioni 52.975  mkoani Singida kwa ajili  ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo barabara, elimu, afya, maji, huduma za utawala na uwezeshaji wa wananchi. 

Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akitoa taarifa ya wiki ya Serikali kwa waandishi wa habari mkoani Singida jana.

Alisema Serikali inaendelea kutoa huduma za kiutawala na maendeleo katika Mkoa wa Singida kama kawaida chini ya Mkuu wa Mkoa Dkt. Binilith Mahenge na kuwa hali ya mkoa ni shwari na wananchi wanaendelea na shughuli zao za uzalishaji mali bila bughudha. 

Alisema katika kuimarisha ustawi wa wananchi wa Singida, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kama ambavyo inafanya katika mikoa mingine hapa nchini na katika kufanikisha utekelezaji huo Serikali inahakikisha inatoa fedha kama ilivyopangwa. 

Msigwa alisema kuanzia Mwezi huu wa tisa, Serikali imeleta Sh. Bilioni 2 na Milioni 275 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vituo vya Afya 8 (Ntuntu-Ikungi, Mitundu-Itigi, Chibungwa/Sasajila-Manyoni, Ilunda-Mkalama, Iglansoni-Ikungi, Tyegelo-Iramba, Kasisiri-Iramba na Makuro-Wilayani Singida) na kukamilisha vyumba vya madarasa 22 katika shule za Sekondari. Hizi ni fedha ambazo zinakusanywa kutokana na tozo katika miamala ya simu. 

Alisema kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa Barabara na Madaraja inayoendelea kutekelezwa na kati ya Machi na Septemba mwaka huu 2021, Serikali imeleta Singida shilingi Bilioni 21 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja. 

"Mfano mmoja wapo ni ujenzi wa Daraja la Msingi (lenye urefu wa mita 100) katika barabara ya Ulemo-Gumanga-Sibiti. Ujenzi wa daraja hili utagharimu Sh. Bilioni 10.933, hadi sasa ujenzi umefikia asilimia 69. Daraja hili pamoja na barabara zake unganishi zitakamilika Juni 2022,".  alisema Msigwa.

Msigwa aliongeza kuwa pamoja na miradi hiyo Serikali imeanza  kufanya upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa barabara ya Sabasaba, Sepuka na Ndago Kizaga yenye km 77.6.

Alitaja barabara nyingine kuwa ni ya mchepuo ya Singida (Singida bypass) ya kilometa 46, Barabara ya Mkalama-Gumanga-Nduguti-Iguguno ambayo ni sehemu ya barabara inayoanzia Bariadi mkoani Simiyu ambayo itaunganisha na Iguguno. 

Akizungumzia miradi ya maji alisema Serikali imeleta sh. Bilioni 5 na Milioni 278 kutekeleza miradi hiyo katika vijiji vya Mughamo, Ibaga, Kipumbuiko na Kintinku/Lusilile. Hii yote nijuhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua ndoo ya Maji Mama na kukabiliana na tatizo la maji. 

 Kuhusu umeme kupitia mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA-III), Serikali imesambaza umeme katika vijiji 274 kati ya vijiji vyote 441 (sawa na asilimia 62.1). Kazi inayoendelea sasa ni kusambaza katika vijiji 167 vilivyobaki. Vijiji hivi vyote vitakuwa vimepata umeme ifikapo Desemba mwakani. 

Pia alisema Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa umeme wa kitaifa unaitwa Backbone Transimission Investment Project (BTIP) na kuwa hapa Singida kuna kituo kikubwa cha kupooza umeme na kinapokea kutoka kituo cha Zuzu – Dodoma umeme wa msongo wa kilovoti 400. Uwezo wake wa juu ni kupokea, kupoooza na kusambaza jumla ya Megawati 600. Kwa sasa tayari kimeanza kuhudumia Mji wa Singida na kazi inayoendelea ni kuunganisha na mitambo ya msongo wa kilovoti 400 na ile ya kilovoti 220 ambayo inatumika kuwapelekea wananchi. 

Alisema mradi huo  ni sehemu ya mradi mkubwa wa kujenga njia kuu ya umeme kutoka Iringa, Dodoma, Singida hadi Shinyanga. Na pia ni sehemu ya mradi wa kuunganisha njia ya umeme kati ya Tanzania na Kenya. Njia hii inakwenda mpaka  Namanga – Arusha hadi kuunganisha na Isinya nchini Kenya. 

Alitaja Gharama za mradi huo kuwa ni  Dola za Marekani Milioni 56 (Bilioni 128.8), hadi sasa umefikia asilimia 99 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba mwaka huu 2021.

Akizungumzia mradi wa kimkakati wa kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini alisema nchi yetu inahitaji kama tani 640,000 za mafuta ya kula, uzalishaji wetu ni tani 240,000 tu. Mafuta yanayobaki kiasi cha tani 400,000 tunalazimika kuagiza kutoka nje ya nchi na tunatumiza zaidi ya shilingi Bilioni 500 kuagiza mafuta hayo. 

Alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inaleta mbegu za alizeti za kupanda tani 1,194 kwa ajili ya wakulima. Hizi ni mbegu bora ambazo zinatoa mafuta mengi. 

Alisema katika juhudi za kuongeza mbegu za alizeti kwa ajili ya kuzalisha mafuta, tunahitaji tani milioni 2 kwa mwaka lakini tunazalisha tani laki 6 tu. 

"Serikali inawapongeza viongozi na wakulima wa Mkoa wa Singida kwa kujiwekea mpango wa kulima ekari 597,000 na kuzalisha tani 581,986 ambazo zitazalisha tani 242,500 za mafuta. Hii itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upungufu wa mafuta ya kula hapa nchini na kupanda kwa bei ya mafuta, alisema Msigwa.

 Msigwa alitumia nafasi hiyo kunatoa wito kwa wakulima wote nchini kuongeza uzalishaji wa alizeti na Serikali itaendelea kutoa huduma za ugani, kutafuta mbegu bora na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kusafisha mafuta. 

Adha Msigwa akizungumzia Mapambano dhidi ya Uviko-19 alisema  janga la ugonjwa  unaosababishwa na Virusi vya Korona (Uviko-19). Serikali kupitia Viongozi wake na Wataalamu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga na ugonjwa huo na kupokea chanjo. 

"Kwa kutambua changamoto ya kuhakikisha elimu dhidi ya ugonjwa huu inawafikia wananchi ipasavyo pamoja na kupata chanjo, Wiki hii Serikali imeanza kutekeleza Awamu ya Pili ya utoaji chanjo kwa kupanua uwigo wa vituo vya kutolea chanjo ya Uviko-19, tulianza na vituo 550 nchi nzima na sasa chanjo zinatolewa katika vituo vyote vinavyotoa chanjo zingine nchini. Kuna vituo zaidi ya 6,784 vinatoa chanjo na pia wataalamu wa kutoa chanjo sasa wanakwenda hadi vijijini na maeneo yote yenye mikusanyiko ya watu. Hata juzi kwenye mtanange wa Yanga na Simba, watu wamepata chanjo pale," alisema Msigwa. 

Alisema kwa tulipofikia sasa, hatutaki Mtanzania aliyetayari kupata chanjo apate shida ya kwenda sehemu ya kuchanjwa. Tunaweka vituo vya chanjo kwenye vituo vya mabasi, kwenye masoko, vituo vya kupima uzito magari, Mwenge wa uhuru, tunakwenda mechi ya watani wa jadi na kila mahali ambapo tunaona pana weza kuwarahisishia watu kupata chanjo. Na hii ni kwa sababu, tumeona Watanzania wengi wapo tayari kupata chanjo lakini changamoto imekuwa kuvifikia vituo vinavyotoa chanjo. 

Alisema utoaji chanjo unakwenda vizuri, mpaka leo Watanzania takribani 400,000 wamechanjwa na wengine wanaendelea kupata chanjo dhidi ya uviko-19. Kasi hii imeongezeka sana baada ya Wizara ya Afya, TAMISEMI na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuzindua Awamu ya Pili ya Uhamasisha na utoaji elimu (Sepetemba 15, 2021) ambapo sasa chanjo zinapelekwa hadi vijijini na Wataalamu wetu sasa wameanza kupita nyumba kwa nyumba ili wale ambao wapo tayari kupata chanjo wapate. 

Aliongeza kuwa Serikali inawapongeza Wataalamu wa Afya wote kwa kazi kubwa wanayoifanya, kwanza kwa wao wenyewe kuonesha mfano kwa kupokea chanjo na pili kupeleka huduma za Mkoba kwa wananchi (yaani mwananchi anapata chanjo pale alipo. 

Msigwa alimpongeza kijana Michael Filbert Nondo ambaye ameamua kusafiri kwa baiskeli kutoka Kigoma hadi Dar es Salaam akipita kuhamasisha wananchi kupokea chanjo. Leo amefika Dodoma na kukutana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,  Jinsia, Wazee na Watoto lakini kwa bahati mbaya hatoweza kumaliza safari yake baada ya kupatwa na msiba wa kufiwa na mwanae huko Kigoma. Nawaomba vijana wote tuungane kuhamasisha jamii kupata chanjo kama anavyofanya kijana huyo. 

Alisema Serikali inahimiza watu kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko-19 na kupata chanjo kwa sababu KINGA NI BORA KULIKO TIBA. Kitengo cha Kinga cha Wizara ya Afya kinachoongozwa na Dkt. Leonard Subi wanafanya kazi kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata elimu na chanjo, na leo hapa nimeongozana na Dkt. Ama Kasangala, yeye ni Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha elimu ya afya kwa Umma cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. 

Alisema  kwa kutambua kuwa Waandishi wa Habari wana umuhimu mkubwa katika jukumu la kuwaelimisha Watanzania kukabiliana na Uviko-19 Serikali imeona iongeze ushirikiano nao ambapo alimtambulisha Rais wa Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari vya Mikoa (UTPC)  Deogratius Nsokolo alikuwa ameongozana naye. 

"Mimi lengo langu Waandishi wa Habari twende pamoja, tufanye kazi zetu kwa kuzingatia weledi, sheria za nchi, kanuni na taratibu lakini muhimu zaidi tuiweke nchi yetu kwanza (Tanzania Kwanza), tuwapiganie Watanzania pamoja. Kwenye hili janga la Korona Watanzania wanakufa kwa sababu ya kutozingatia afua hizi za kukabiliana na virusi vya ugonjwa huu, kutozingatia kuwa KINGA NI BORA KULIKO TIBA," alisema Msigwa. 

Msigwa alihitimisha hutuba yake kwa kuwaomba Waandishi wa Habari kushirikiana na Wataalamu waliopo katika mikoa yote hapa nchini  kuhakikisha elimu kwa wananchi inafika ipasavyo kwa kuwasiliana na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Waganga wa Hospitali zetu, viongozi wa Mikoa na Wilaya ili Watanzania wapate chanjo na wajikinge na balaa hilo. 

Katika mkutano huo Msigwa alipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali ya wananchi waliokuwa wakipiga simu moja kwa moja kwenye mkutano huo.

Friday, September 24, 2021

MKOA WA SINGIDA WABAINIKA KUWA NA ALMASI BORA TANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JICT LTD inayojishughulisha na Utafiti wa Almasi Javan Bidogo ambaye pia ni mmiliki wa mradi wa utafuta wa Almasi katika Kijiji cha Mbereseke kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa, akimuelekeza jambo Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya (wa pili kulia mbele) wakati alipofanya ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea na kukagua mradi huo jana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JICT LTD inayojishughulisha na Utafiti wa Almasi Javan Bidogo ambaye pia ni mmiliki wa mradi wa utafuta wa Almasi katika Kijiji cha Mbereseke kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa, akitoa maelezo kwa  Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya (katikati) wakati alipofanya ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea na kukagua mradi huo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Selemani Mwenda akizungumza wakati wa ziara hiyo. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahaman Mwanga, Kaimu Afisa  Madini Mkazi Mkoa wa Singida,Chone Malembo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JICT LTD inayojishughulisha na Utafiti wa Almasi Javan Bidogo.
Kazi zikiendelea katika mgodi huo.
Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya na ujumbe wake wakiangalia udongo ambao unasubiri kuingizwa kwenye mtambo ili kubaini kama una Almasi. 
Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahaman Mwanga, akiangalia mtambo (karasha) wa kusaga mawe yenye Almasi uliopo katika mgodi huo.
Kazi zikiendelea katika mgodi huo.
Muonekano wa sehemu ya mgodi huo.
 



Na Dotto Mwaibale Iramba


MKOA wa Singida umebainika kuwa na Almasi bora zaidi kuliko maeneo yote Tanzania.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya JICT LTD inayojishughulisha na Utafiti wa Almasi Javan Bidogo ambaye pia ni mmiliki wa mradi wa utafuta wa Almasi katika Kijiji cha Mbereseke kilichopo Wilaya ya Iramba mkoani hapa wakati akitoa taarifa ya mradi huo kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya alipofanya ziara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea mradi huo jana.

Bidogo alisema kampuni yao imejikita kufanya utafiti wa Almasi katika wilaya za Ikungi na Iramba tangu mwezi Machi mwaka jana na hatua wanayoendelea nayo ni ya mwisho.

"Tumefanya uvumbuzi katika baadhi ya miamba inayokuwa na Almasi jumla yake ipo 13 na kati ya hiyo tisa ni mikubwa ambayo tumekuwa tukiifatilia sana,". alisema Bidogo.

Bidogo alisema kwa hivi sasa wamechukua sampuri ya udongo na kuanza kuziosha kwenye mtambo wao uliopo kwenye mradi ili waweze kuziona Almasi zote ambazo zipo kwenye udongo huo ambao wameuchukua kutoka maeneo mbalimbali wilayani Ikungi na Iramba.

Alisema mtambo wao ambao wataufunga kwa ajili ya kuanza kuhutumia kuosha mchanga huo wiki mbili zijazo kuanzia sasa una uwezo wa kuosha tani 10 za mchanga huo kwa muda wa saa moja.

Alisema kwa kuanza wanatarajia kuwa na ajira za wafanyakazi wasio pungua 50 kwa muda huu wa kwanza wa utafiti ambao wanaumalizia lakini kadri Mungu atakavyo wasaidia na kuwa na mchanga wenye Almasi watatarajia kuwa na wachimba 1000 kwa kila mgodi mmoja.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya alisema Serikali kupitia wizara hiyo sasa ni kitu kimoja kwani inafanya kazi kwa umoja kwa kushirikiana na wadau wengine kama wakuu wa mikoa na wilaya katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la madini. 

Alisema jambo hilo ni nzuri na ndilo analolisisitiza wakati wote Rais Samia Suluhu kuwa wao waliopewa dhamana ya uongozi wasaidie kufanya uwekezaji kwenye maeneo yao ili uweze kukua.

" Ninyi wenzetu mliopo kwenye nyadhifa za ngazi ya Tamisemi mnapo wiwa kutekeleza masuala haya ya uwekezaji kwa dhati na dhamira ya mioyo yenu na kuwa kama uwekezaji huo ni wenu binafsi kwa ajili ya kuongeza uzalishaji ni jambo zuri na la kutia moyo.

Alisema uchumi wa madini ni tofauti na uchumi wa mazao ambao unahitaji kilo ngapi za pamba kwa kilo moja ya dhahabu hapo  ndipo utakapoweza kujua uwekezaji katika madini jinsi unavyo kuwa na tija ya mapato hadi kwenye Halmashauri za wilaya mbalimbali.

Alisema mafanikio hayo yatapatikana kwa kuzuia migogoro ambayo haina tija katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya uchimbaji wa madini.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba Selemani Mwenda alisema amemshirikisha Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida kuwa wachimbaji wadogo wenye leseni waalikwe ili kufanya mazungumzo nao lengo likiwa na wao wapate maeneo ya kuchimba na wale ambao hawana uwezo wasaidiwe kuwatafuta wawekezaji ambao watashirikiana nao jambo litakaloongeza uzalishaji.

Baadhi ya wataalamu wa miamba katika mgodi huo wakizungumza na waandishi wa habari walisema katika miamba walioifanyia utafiti imeonesha Mkoa wa Singida kuwa na Almasi bora hapa nchini.

Thursday, September 23, 2021

NAIBU WAZIRI WIZARA YA MADINI AMALIZA MGOGORO WA UMILIKI MGODI KWA DAKIKA 120

Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya akizungumza na wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Kijiji cha Matongo katika mkutano wa hadhara alipokwenda kutatua mgogoro wa umiliki wa mgodi huo jana uliopo wilayani Ikungi mkoani Singida
Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahaman Mwanga akizungumza na wachimbaji wakati wa utatuzi wa mgogoro huo.
Kaimu Afisa  Madini Mkazi Mkoa wa Singida,Chone Malembo akizungumza na wananchi katika mkutano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza na wananchi katika mkutano huo.

Naibu Waziri wa Madini Profesa Shukuru Manya (wa nne kulia)akizungumza na wachimbaji wadogo wa mgodi wa dhahabu wa Kijiji cha Matongo wakati akikagua maduara ya uchimbaji.
Wachimbaji wadogo wa mgodi huo wakiwa mkutanoni.
Mchimbaji Abdulkheri Abdulkadir kutoka Geita, akizungumza kero zinazo wasibu wachimbaji kwenye mgodi huo.
Mchimbaji  kutoka Mkoa wa Iringa Geita, akizungumza kero zinazo wasibu wachimbaji kwenye mgodi huo.
Mmiliki wa mgodi huo Richard Lyamuya akizungumza katika mkutano huo
Mbia wa mgodi huo Helena Mtaturu akizungumza  katika mkutano huo


Na Dotto Mwaibale, Ikungi Singida


NAIBU Waziri  Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya katika hali ambayo haikutegemewa na wengi ametumia masaa mawili sawa na dakika 120 kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa umilikaji mgodi wa uchimbaji dhahabu katika machimbo ya Kijiji cha Matongo yaliyopo wilayani Ikungi mkoani hapa.

Mgogoro huo ambao umemalizwa na Profesa Manya ulikuwa ukimuhusisha mmiliki halali wa mgodi huo Richard Lyamuya na wabia wenzake Israel Njiku na Helena Mtaturu ambaye alikuwa mlalamikaji na mmiliki wa eneo hilo la mgodi lenye ekari 70 ambalo alidai lilichukuliwa na Lyamuya bila ya kufuata taratibu kwa kumuhusisha Mtaturu na ndugu zake.

Kutoka na madai hayo  Mtaturu ambaye ni mjane alimuandikia barua Waziri Wizara ya madini akidai kuwa kwa kificho bila yeye kujua mmiliki wa mgodi huo Richard Lyamuya ambaye ni mkazi wa Singida Mji alikwenda ofisi za madini Mkoa wa Singida ili apewe kibali cha kuchimba dhahabu kwenye eneo lake bila ya kushirikishwa.

Baada ya barua hiyo kufika katika wizara hiyo na kufanyiwa uchunguzi ndipo jana Naibu Waziri Wizara ya Madini Profesa Shukuru Manya alipofika kwenye mgodi huo na kufanya mkutano wa hadhara uliowahusisha wadau wa uchimbaji, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro, Viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi  (CCM) wananchi na wamiliki wa mgodi huo ambao baadhi yao waliweza kuelezea walivyokuwa wakielewa jinsi mmiliki wa mgodi huo alivyopata eneo hilo kwa kufuata sheria za uchimbaji wa madini kwa kumshirikisha Helena Njiku na kuweka kumbukumbu za makubaliano kwa maandishi na kutiliana saini.

Mmoja wa viongozi wa Umoja wa wachimba madini katika wilaya hiyo  (SIREMA) Seleman Omari alisema mbele ya Naibu Waziri Wizara ya Madini kuwa anaujua mchakato mzima wa uanzishwaji wa mgodi huo na kuwa hakukuwa na udanganyifu wowote na wabia hao waliwekeana namna ya kulipana ambapo Mtaturu aliachiwa asilimia 40 huku Richard Lyamuya na Israel Njiku wakichukua asilimia 30 kila mmoja.

Mbali ya Omari kuyasema hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro alisema suala hilo alilikuta ofisini kwake baada ya kusikizwa na mtangulizi wake Edward Mpogolo ambaye amehamishiwa Wilaya ya Same ambapo nyaraka zote zinaonesha umiliki wa mgodi huo ni wa watu hao watatu na tayari Serikali imekwisha wapa leseni ya uchimbaji na si vinginevyo.

Baada ya watu mbalimbali kutoa maelezo yao na kubaini kuwa Mtaturu aliandika barua ya madai ambayo sio ya kweli Naibu Waziri Profesa Manya alimwambia asirudie tena kufanya jambo hilo.

Profesa Manya alitumia nafasi hiyo kuwaomba wachimbaji hao kufanya kazi zao kwa upendo na kufuata sheria za uchimbaji.

Mkuu wa wilaya hiyo Jerry Muro aliwaomba wachimbaji hao kudumisha amani na kujikinga na magonjwa ya Corona na ukimwi kutokana na mwingiliano mkubwa wa watu katika eneo hilo.