Wednesday, June 30, 2021

WANAFUNZI SINGIDA WADAIWA KUTUPIWA MAPEPO WAACHE SHULE WAKAOZESHWE

Afisa Mtendaji wa Kata ya Msange, Clement Jumbe akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA)  wa kata  hiyo  katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jana Halmashauri ya Wilaya ya Singida  yaliyoandaliwa na Shirika la Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi ambapo aliibua madai ya tukio la Ukatili wa Kijinsia la kuwatupia  kitu kilichodhaniwa ni mapepo wanafunzi wa Sekondari ya Madasenga kwa njia ya ushirikina ili waache masomo waweze kuozeshwa. 
Afisa Miradi wa Shirika la ESTL, Annamaria Mashaka, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa Shirika la ESTL Edna Mtui, akizungumzia aina tano za ukatili wa kijinsia kwenye mafunzo hayo/
Mjumbe wa Kamati hiyo Sheikh Hassan  Ifande akizungumza tukio la wanafunzi kutupiwa mapepo na jinsi walivyo limaliza kwa njia ya maombi./
Mjumbe wa Kamati hiyo PC Christian kutoka Kituo cha Polisi Kata ya Msange alisema matukio hayo ya ukatili hasa kijana akimpenda msichana humkamata kwa nguvu na kumpeleka nyumbani kwake na siku inayofuata hutumwa watu nyumbani kwao kuwaeleza ndugu zake binti yao alipo yameshamiri mno katika kata hiyo.
Mzee maarufu wa kata hiyo Hamisi Kunja, akizungumzia tukio hilo
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangida iliyopo shule hiyo Frank Itambu, akizungumzia tukio hilo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MADAI ya Ukatili wa Kijinsia wa kuwatupia  kitu kilichodhaniwa ni mapepo wanafunzi wa Sekondari ya Madasenga kwa njia ya ushirikina ili waache masomo waweze kuozeshwa katika Kata ya Msange Wilayani Singida yameleta changamoto kubwa katika eneo hilo.

Hayo yalisemwa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Msange, Clement Jumbe katika  kikao kazi kilicho keti juzi ambacho kiliwakutanisha wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya Kata kuangalia namna bora ya kupambana na ukatili.

Kikao hicho kilicho wakutanisha wajumbe hao ambao ni viongozi wa idara mbalimbali za Serikali, Asasi za kiraia, viongozi wa dini, na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu chini ya mwenyeki wake  Afisa Mtendaji wa kata hiyo kiliandaliwa na Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi.

Jumbe alisema hali hiyo ilikuwa ikiwatokea wanafunzi hao wakiwa shuleni lakini wakifika nyumbani hali zao zilikuwa nzuri hapo ndipo walipobaini kuwepo na imani za kishirikina.

Afisa Elimu wa kata hiyo Mwalimu Stephen Haule amethibitisha kutoa kwa tukio hilo na kuwa hali hivi sasa ipo shwari kutokana na jitihada mbalimbali zilizofanyika kukabiliana na changamoto hiyo.

Alisema tukio hilo lilitokea kati ya mwaka 2019/2020 ambapo wanafunzi zaidi ya 10 waliathiriwa na baada ya wataalamu wa afya kushindwa kubaini chanzo chake waliamua kuwashirikisha wazazi, wazee maarufu, viongozi wa dini ilikusaidia kuliondoa jambo hilo.

"Tangu yakutane makundi hayo na kufanya mikutano hali  iliyokuwa ikiwatokea  wanafunzi hao wakiwa kwenye vipindi sasa ipo shwari na kati ya shule 10 zinazofanya vizuri kitaalumu katika halmashauri yetu nayo ni mojawapo," alisema Haule.

Mzee maarufu wa kata hiyo Hamisi Kunja alisema hali hiyo iliyokuwa ikiwatokea watoto hao iliwafedhehesha sana lakini hatua zilizochukuliwa za kufanya mikutano zilisaidia kulimaliza.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mangida iliyopo shule hiyo Frank Itambu alisema baada ya kutokea kwa tukio hilo walifanya mikutano ya kukemea tukio hilo hadi hivi sasa halijatokea tena.

Sheikh wa Kata ya Maghojoa Hassan Ifande alisema baada ya kutokea suala hilo ambalo walilihusisha na imani za ushirikina kwa wanafunzi wakianguka hovyo kama wanamapepo aliwatuma masheikh wenzake kwa kushirikiana na viongozi wa dini ya kikristo kwenda kwenye shule hiyo kufanya maombi na hali imekuwa shwari hadi leo hii.

SHIRIKA LA ESTL LATOA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA KAMATI YA MTAKUWWA KATA YA MSANGE WILAYA YA SINGIDA

 Afisa Miradi wa Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi, Annamaria Mashaka, akizungumza na wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA)  wa Kata ya Msange wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jana Halmashauri ya Wilaya ya Singida.


 Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa shirika hilo Edna Mtui, akizungumza katika mafunzo hayo.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Msange, Clement Jumbe akizungumza katika mafunzo hayo/
Mafunzo yakiendelea.
Mjumbe wa Kamati hiyo Sheikh Hassan  Ipande akizungumza katika mafunzo hayo/
Mjumbe wa Kamati hiyo Felister John akizungumza kwenye mafunzo hayo/
Mjumbe wa Kamati hiyo Theresia Yambi akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
  

 

Na Dotto Mwaibale,Singida.

 

SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uholanzi limewakutanisha kwa pamoja wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya Kata kuangalia namna bora ya kupambana na ukatili.

Wajumbe hao ambao ni viongozi kutoka idara mbalimbali za serikali, Asasi za Kiraia,viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu chini ya mwenyekiti wake Afisa Mtendaji wa Kata wamekutana juzi kwenye kikao cha mafunzo ya kuwajengea uwezo na kujadili mbinu za  kukabiliana na ukatili Kata ya Msange katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida. 

Akizungumza katika kikao hicho Afisa Miradi wa Shirika hilo Annamaria Mashaka alisema baada ya kuzijengea uwezo kamati za Mtakuwwa ngazi ya kata wanaamini zitakwenda kutekeleza mpango huo kupitia majukumu yaliyoainishwa na mwongozo ambayo yamewekwa pia katika lugha rahisi na kamati hiyo ili waendelee na mchakato wa kutokomeza ukatili kwa jamii ya watu wa Msange.

Alisema lengo la kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati hiyo ni kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na mtoto ambao katika halmashauri hiyo unafanyika katika Kata za Msange, Ikhanoda, Mudida na Mukuro.

" Miongoni mwa majukumu waliojipangia kama kamati katika utekelezaji wa mpango huo ni kuendelea kutoa elimu, kuhamasisha jamii kuepukana na vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto," alisema Mashaka.

Aidha Mashaka alisema kamati hiyo ineelekeza nguvu katika kuibua changamoto hama matukio yote yanayotokana na ukatili na si tu kuyaibua na kufanya ufuatiliaji ili haki iweze kupatikana kwa wahanga wa ukatili na watuhumiwa waweze kuhukumiwa kutokana na vitendo wanavyofanya. 

Pia Mashaka alisema sambamba na kutoa elimu na kuibua matukio kamati hiyo imewekeza nguvu katika kuhamasisha jamii kupitia mbinu mbalimbali yakiwemo mabonanza ambayo yatafanywa kwa kushirikiana na Polisi Jamii ngazi ya kata yakiwa na lengo la kutokomeza ukatili huo katika kata hiyo ya Msange.

  Afisa Mwezeshaji wa Mwanamke na Maendeleo wa shirika hilo Edna Mtui alisema wamekutana na kamati hiyo kuongelea ukati huo na aina tano ambazo zinawakumba sana wanawake na watoto wadogo ambao ni ukatili wa kingono, kimwili, kisaikolojia, kiuchumi na ukatili wa kiafya.

Alisema wanakamati hao pia walitamani kujua je mtu akifanyiwa ukatili sehemu husika ya kwenda kutoa taarifa ni wapi ambapo pia walipitia vipengere mbalimbali ili kujua ni sehemu gani wataweza kulisema suala hilo la ukatili.

Alisema katika kata hiyo  bado kunaonesha  kuna ukatili wa ukeketaji ambao ni wa kiafya, kimwili na kingono ambao unafanyika kwa siri kubwa sana ambapo wamegundua mbinu mpya kwa kufanya ukeketaji kwa mtoto mdogo kuanzia anapozaliwa mpaka anapokuwa na miaka mtano.

Alisema ukatili huo wanaufanya kwa kutumia chumvi ya magadi, mazinzi yanayotoka juu kwenye nyumba za tembe na kusugua sehemu za siri kwa kutumia mtula ambapo pia mabibi wanafuga kucha ambazo hutumika kumfinya mtoto kwenye kiungo chake ili kumkeketa jambo ambalo wamekiri kuwa ni baya. 

Kamati hiyo imepanga mkakati wa muda wa miezi mitatu ili kuendelea kutoa elimu kuhusu ukatili huo na kuwa wataitoa makanisani, misikitini, mashuleni, kwenye masoko, sehemu hatarishi na kwenye mikusanyiko ya watu.

Mjumbe wa Kamati hiyo PC Christian kutoka Kituo cha Polisi Kata ya Msange alisema matukio hayo ya ukatili ni muhimu yakatokomezwa na changamoto kubwa iliyopo ni wahusika wa matukio hayo kushindwa kufika kwenye vyombo vinavyotoa haki kutoa ushahidi jambo linalosabisha kesi hizo kuishia njiani bila kutotolewa hukumu.

FAINALI ZA KIHISTORIA UMISSETA 2021 ZAUNGURUMA MTWARA

 

 

Mwandishi Maalum, Mtwara

Michezo inayoendelea kwenye Mashindano ya Taaluma na Michezo kwa Shule za Sekondari (UMISSETA) yanafikia fainali Julai 1, 2021 kwenye viwanja mbalimbali vya mjini Mtwara ambapo mashindano hayo yatafungwa rasmi Julai 2,2021.

Kwa mujibu wa Msemaji wa mashindano hayo, John Mapepele fainali ya soka kwa wavulana itakuwa baina ya timu ya Pemba na Mtwara na itachezwa siku ya kufunga mashindano hayo Julai 2, 2021 katika uwanja wa Nangwanda Sijaona wakati mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu soka utachezwa kesho baina ya timu ya mkoa wa Dodoma na Geita.

Amesema mchezo wa Soka kwa upande wa wasichana utakuwa baina ya timu ya mkoa wa Mwanza na Tabora ambao utachezwa mchana Julai 1,2021 ambapo hadi sasa mshindi wa tatu ni mkoa wa Arusha.  

Pia fainali ya Mpira wa Pete itakuwa dhidi ya timu ya mkoa wa Mwanza na Songwe

Kwa upande wa mpira wa Wavu fainali wasichana itachezwa baina ya mkoa wa Dar es Salaam na Mtwara wakati wavulana itakuwa kati ya Dar es Salaam na Arusha.

Mpira wa mikono fainali wasichana itakuwa baina ya mkoa wa Songwe na Morogoro na kwa upande wa wavulana Unguja watakipiga na Tabora.

Kwa upande wa mpira wa kikapu fainali kwa wanaume itakuwa baina ya Unguja na Dar es Salaam wakati kwa upande wa wanawake itakuwa baina ya Dar es Salaam na Mwanza.

Mechi ya nusu fainali ikiendelea baina ya Dodoma (nyekundu) na Mtwara(nyeupe) ambapo Mtwara imeshida bao 1 dhidi ya Dodoma 0.

A.  Penati ikipigwa na mchezaji wa Pemba (kijani) kwa golikipa wa Geita (nyekundu) ambapo timu ya Pemba imeshinda penati 4 dhidi ya penati 3 za Geita.

  Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na MichezoDkt. Hassan Abbasi (aliyejishika kidevu) akiangalia mechi ya nusu fainali baina ya timu ya Mtwara na Dodoma ambapo Mtwara imeshida bao 1 na Dodoma 0. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya kuchoto ni Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusuph Singo.

Sunday, June 27, 2021

MAAFISA VIJANA NA MAAFISA MAENDELEO NGAZI ZA HALMASHAURI WATAKIWA KUWASAIDIA VIJANA.

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (wa pili kulia) akiwaelekeza jambo  viongozi wa mradi wa kilimo wa vijana  ujulikanao kwa jina la Singida Youth Agricultural Group uliopo Uhamaka Manispaa ya  Singida alipofanya ziara ya kukagua mradi huo juzi.  

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (wa pili kulia) akisisitiza jambo katika ziara hiyo.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (wa pili kulia) na viongozi wa kikundi hicho wakiangalia bwawa la ufugaji wa samaki.
Ukaguzi wa shamba ukifanyika katika ziara hiyo. 


Na Dotto Mwaibale, Singida


KAIMU Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amewataka Maafisa Maendeleo ngazi za Halmshauri na Kata kuwasaidia vijana kuwaweka pamoja na kuunda vikundi.

Ndahani alitoa ombi hilo juzi wakati akikagua mradi wa kilimo wa vijana  ujulikanao kwa jina la Singida Youth Agricultural Group uliopo Uhamaka Manispaa ya  Singida.

Vijana hao kupitia mradi huo wanajishughulisha na kilimo cha matunda,mboga, ufugaji wa kuku na samaki.

Ndahani alisema asilimia 10 ya mkopo unaotolewa na halmashauri kwa ajili ya vijana hauwahusu vijana wa mjini pekee bali ni kwa kila kijana mwenye sifa aliyopo hata kijijini na wanatakiwa kupewa bila ya ubaguzi wowote.

" Jambo linalo nisikitisha kwenu licha ya kuwa na mradi mzuri na wenye tija hamjui kabisa namna ya kusajili vikundi na fursa za kupata mikopo kutoka halmshauri na Taasisi za fedha," alisema Ndahani.

Hivyo aliwaomba maafisa vijana wenzake katika ngazi za halmshauri na maafisa maendeleo wa kata kuwasaidia kuwafundisha michakato yote ya kuanzisha vikundi ,kusajili na namna ya kupata mikopo.

Pia Ndahani aliwataka vijana wanao nufaika na mkopo huo kujenga tabia ya kurejesha haraka fedha hizo ili kutoa fursa kwa vijana wengine kukopeshwa.

Aliwahimiza vijana hao kujikita zaidi katika kilimo cha pilipili 'maarufu mwendo kasi' ambazo soko lake ni kubwa hapa nchini na nje ya nchi ambapo wilaya ya Kahama mkoani Geita ndio ni kinara wa kilimo cha zao hilo.

Mwenyekiti wa kikundi hicho  Ally Hamisi ametoa shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha upendo na imani kubwa kwa vijana wa makundi yote na hilo lilidhihirika wakati alipokuwa akizungumza nao jijini  Mwanza ambapo alisisitiza kuendelea kuwapatia nafasi za uongozi na kuwawezesha kiuchumi.

Naye Katibu wa kikundi hicho Gwanaka Mwakyusa amemshukuru  Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani kwa kazi anayoifanya ya kuwaunga mkono vijana na moyo wa kipekee wa kuwasaidia akitolea mfano alivyo tumia muda mrefu kuwafundisha namna ya kusajili kikundi na jinsi ya kupata mkopo katika Halmshauri na kubwa zaidi anavyotumia gari lake kuwafikia vijana bila kujali gharama.

Naye Diana Gibson amewaomba vijana kujishughukisha na kilimo ambacho kimekuwa mkombozi kwa kwani kwa muda mrefu alikuwa akifanya kazi katika salooni mbalimbali lakini kipato alichokuwa akikipata kilikuwa ni kidogo ukilinganisha na anacho kipata sasa kupitia kilimo.

Saturday, June 26, 2021

MFUMO WA RIPAT CHACHU YA MAGEUZI YA KILIMO NCHINI USAMBAE NCHI NZIMA.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA (Taaluma) Prof. Maulid Mwatawala akitoa nasaha zake kabla ya kufunga mradi huo wa RIPAT - SUA. 

Mratibu wa Mradi upande wa SUA Dkt. Emmanuel Malisa akieleza utekelezaji wa mradi huo hatua kwa hatua toka mwanzo hadi hapo unapofikia tamati.

Zidia Malundo akisoma risala kwa niaba ya vikundi vyote 22 vilivyoshiriki kwenye mradi huo mbele ya mgeni rasmi.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Ugani na utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Charles Mjema akitoa salamu za Wizara kwenye hafla hiyo ya kufunga mradi.

Rasi wa Ndani ya Sayansi za Jamii na Insia ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Samweli Kabote akitoa akizungumza kwenye hafla hiyo kuhusu mashirikiano kati ya SUA na shirika la RECODA.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manispaa ya Morogooro, Michael Waluse akitoa salamu za Manispaa kuhusu mafanikio na mikakati ya kuendeza Mbinu hiyo kwenye kata zote za Manispaa ya Morogoro.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Blandina Marijani akitoa salamu za Wilaya yake kwenye ufungaji wa mradi huo.

Wanavikundi na wadau wakifuatilia Hotuba kwenye hafla hiyo ya ufungaji wa mradi wa RIPAT - SUA.

Hafla ikiendelea.

Wanavikundi na wadau wakifuatilia Hotuba kwenye hafla hiyo ya ufungaji wa mradi wa RIPAT - SUA.

Hafla ikiendelea.
 


Na Calvin Gwabara, Morogoro


WIZARA ya Kilimo na Halmashauri za wilaya nchini zimeshauriwa kujifunza na kutumia Mfumo wa Kilimo wa RIPAT ili mafanikio yaliyoonekana yaendelee si kwa wilaya za mkoa wa Morogoro tu bali nchi nzima ili kufikia mageuzi ya kweli ya kilimo nchini.

Wito huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA upande wa Taalamu Prof. Maulid Mwatawala wakati wa hafla ya kufunga Mradi wa mfumo shirikishi wa kuleta mageuzi katika sekta ya Kilimo (RIPAT-SUA) uliokuwa unatekelezwa kwenye Wilaya ya Kilosa na Mvomero Mkoani Morogoro.

"Nasisitiza; Msiwe wa kuona matatizo au kulalamika bali zingatieni kwa kutendea kazi teknolojia mlizofundishwa kupitia mradi huu kwa bidii na kuhakikisha teknolojia zinasambaa pamoja na mfumo wake wa RIPAT na kuwanufaisha wananchi wengi zaidi ndani na nje ya mkoa wetu," alisisitiza Prof. Mwatawala.

Ameongeza kuwa mradi huu ambao ulikuwa ukisisitiza teknolojia mbalimbali za kilimo kuwafikia wakulima na wafugaji unaenda sambamba na mpango wa Maendeleo Endelevu unaolenga sio tu kuondoa umasikini uliokithiri ifikapo 2030 bali pia kuwa na ushirikishwaji na uwiano katika maeneo matatu ya maendeleo;Uchumi, Jamii na mazingira.

"Kama ilivyoainishwa kwenye muongozo wa RIPAT, Mradi unapofikia mwisho vikundi hukabidhiwa kwa halmashauri husika hivyo nichukue fursa hii kuwashukuru viongozi wa halmashauri za Mvomero na Manispaa ya Morogoro kwa kushirikiana vizuri na SUA na RECODA na sasa nitamke rasmi kuwa sasa vikundi vyote 22 vilivyoanzishwa chini ya mradi wa RIPAT - SUA vimekabidhiwa rasmi kwa Halmashauri ya Mvomero na Manispaa ya Morogoro" . alisema Prof. Mwatawala.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo wa RIPAT- SUA,Mratibu wa mradi kwa upande wa SUA Dkt. Emmanuel Malisa amesema baada ya SUA kujionea mafanikio makubwa ya matumizi ya mfumo wa RIPAT katika kusaidia jamii kukabiliana na njaa na umasikini ilionekana kuwa kuna haja ya kuwa na mradi huo Morogoro maeneo ya jirani na SUA ili kutoa fursa kwa Wananchi wa Morogoro kunufaika na pia jamii ya SUA kujifunza kuhusu mfumo huo na kuuhakiki zaidi kupitia tafiti.

Amesema toka mradi umeanza vikundi 22 vimeundwa ambapo kila kikundi kina was tani wa wanakikundi 25 ambapo mpaka sasa Mradi umefikia wakulima 1,053 moja kwa moja lengo lilikuwa kufikia wakulima 720 ifikapo mwisho wa mradi lakini mradi umevuka lengo.

"Teknolojia zote zilizoletwa na mradi kwa wakulima kupitia vikundi zilikuwa ndani ya kapu la uchaguzi ambalo lilikuwa na Kilimo bora cha migomba,Mihogo,Viazi lishe,Kilimo cha mahindi kwa kutumia teknolojia ya jembe la Mzambia mbegu tisa na matuta funga,Maharage lishe,Ufugaji bora wa Kuku,Mbuzi wa maziwa na Nguruwe hivyo wakulima walichagua teknolojia waliyoitaka ingawa zilijaribiwa zote kwenye shamba darasa la pamoja kabla ya kila mmoja kuchagua aliyoipenda" alifafanua Dkt. Malisa.

Dkt. Malisa ameongeza kuwa mfumo huu wa RIPAT umeweza kufundishwa chuoni kwa nadharia na vitendo ambapo hadi sasa wanafunzi zaidi ya 800 wamejifunza masuala ya Kilimo,Ufugaji na maendeleo vijijini kwa vitendo kupitia mradi wa RIPAT - SUA na kutembelewa pia na wanafunzi wawilli wa shahada ya Uzamivu na watumishi wa SUA wapatao 25 kwa lengo la kufanya utafiti zaidi.

Mratibu huyo wa mradi upande wa SUA amesema mradi umefanikiwa kufikia malengo yake na hii imethibitishwa na matokeo ya awali ya tafiti zilizofanywa na watafiti wa SUA na tathimini zilizofanywa na wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu na zile za awali.

Akisoma risala kwa niaba ya Wanavikundi vyote 22  Zidia Malundo wamesema mradi wa RIPAT- SUA umefanya jambo kubwa katika kuzibua pengo la wataalamu na pengine kuwafanya watalaamu wa kilimo na ufugaji kufuatilia kwa urahisi pale panapohitaji taaluma zaidi.

"Katika kuleta mageuzi katika kilimo mradi umefanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuleta mafanikio ya kuwa na kaya bora nyingi pia kuwa na uhakika wa chakula kwa muda mrefu sambamba na kujifunza namna ya kuongeza thamani mazao wanayozalisha na kupata faida zaidi" alisema Malundo kwa niaba ya Wanavikundi wenzake.

Pia wakaahidi kushirikiana na wakulima wenzao walio nje ya vikundi ili kueneza teknolojia hii ili Tanzania yote iwe na nchi yenye kujitosheleza kwa mazao ya chakula  na biashara na ziada kuuza nje lakini pia kuwa na Wafugaji wenye tija na mwisho wakaahidi kupeleka elimu hiyo ma shuleni na taasisi zingine za dini na mashirika ili isambae kwa haraka.

Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za ugani na utafiti kutoka Wizara ya Kilimo Charles Mjema amepongeza mbinu zilizotumiwa na mradi huo wa RIPAT - SUA na kuahidi kuendelea kushirikiana ili mbinu hizo ziweze kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini.

"Tatizo lenu sio ardhi kuwa ndogo kama mnavyosema kuwa ni changamoto bali tatizo ni tija ndogo na lengo letu kama wizara ni kuhakikisha watu wanalima maeneo madogo na kupata tija kubwa na hii ndio imepelekea mazao kutoka nje ya nchi yanauzwa nchini bei ndogo kuliko mazao yetu ni kwakuwa wanazalisha zaidi kwa tija hivyo wanapata faida kubwa hata kama anauza bei ya chini hivyo tuzingatie tija" alisisitiza Mjema.

Friday, June 25, 2021

RC. MAHENGE AKERWA NA MLUNDIKANO WA TAKA MANISPAA YA SINGIDA ATOA SIKU TATU ZIONDOSHWE

Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhandisi Paskas Muragili akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge alipofika kukagua  Ofisi za Manispaa ya Singida baada ya kuzungumza na watumishi na watendaji wa manispaa hiyo wakati akianza ziara yake ya kwanza ya kikazi kukagua miradi ya maendeleo, kuzungumza na wananchi,  kuhamasisha ukusanyaji wa mapato, ulipaji wa kodi na ushuru.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Singida (hawapo pichani) katika mkutano alioufanya jana  wakati wa ziara hiyo.

Watumishi na watendaji wa Manispaa ya Singida wakimsikiliza mkuu wa mkoa wakati alipokuwa akizungumza nao kwenye mkutano huo.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Deus Luziga akizungumza kwenye mkutano huo.

Mkutano ukiendelea.

Watumishi na watendaji wa Manispaa ya Singida wakimsikiliza mkuu wa mkoa wakati alipokuwa akizungumza nao kwenye mkutano huo.

Katibu Mwenezi na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi (CCMMkoa wa SingidaAhmed Kaburu.akizungumza kwenye mkutano huo.
Naibu Meya wa Manispaa ya Singida Shabani Mkata akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akionesha uchakavu wa dari wakati akikagua ofisi za idara mbalimbali ndani ya Manispaa ya Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akiangalia takataka zilizorundikana katika moja ya maguba yaliyopo ndani ya manispaa hiyo.

Wananchi wakiangalia takataka zilizolundikana katika guba lililopo Soko Kuu la Manispaa ya Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge (katikati mwenye mvi) akiangalia gari la Halmashauri ya Manispaa hiyo ambalo lipo kwenye Karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) kwa ajili ya matengenezo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Kimataifa la Vitunguu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akiangalia tenki maalumu la maji la mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika Kijiji cha Kisasida ambao uligharimu zaidi ya Sh.700 Milioni ambao haufanyi kazi kutokana na sababu mbalimbali.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge ametoa siku tatu kwa Manispaa ya Singida kuhakikisha inatoa takataka zote zilizojaa kwenye maguba ndani ya Manispaa hiyo.

Dkt.Mahenge alitoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara yake ya kwanza ya kikazi ndani ya manispaa hiyo ya kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi baada ya kuhamishiwa mkoani hapa akitokea Dodoma.

Hatua hiyo ya kutoa siku tatu  kuondoa takataka hizo ilifikiwa na Mahenge baada ya kutoridhishwa na usafi wa mazingira ndani ya manispaa hiyo na uchakavu wa miundombinu ya barabara za mitaa hususani za eneo la Sabasaba.

" Kwa hali hii hatuwezi kabisa kufikia ndoto zetu za kuifanya Manispaa ya Singida kuwa jiji, hivyo naagiza kuanzia leo nataka kuona takataka zote hizi zilizo jaa kwenye maguba zinaondolewa" alisema Mahenge.

Alisema ratiba inayotakiwa kuanzia jana ni kufanya kazi ya kutoa takataka hizo kila siku kwa kutumia mapato ya fedha zao za ndani na kuwa usafi ndio unaowafanya wananchi wanaofanya biashara zao katika maeneo hayo kuzalisha zaidi wakiwa kwenye mazingira mazuri. 

Katika hatua nyingine Dkt.Mahenge aliagiza vikundi vyote vilivyokuwa vikifanya usafi ndani ya manispaa vilivyositisha kufanya kazi hiyo kutokana na kutolipwa fedha zao virudishwe mara moja na madeni yao yapangiwe namna ya kulipwa.

"Madeni yao myawekee ratiba ya kuyamaliza kuyalipa kwanza mtakuwa mmetoa ajira kwa vijana na kwa akina mama," alisema Mahenge. 

Aidha Mahenge aliwataka watu wote wanaohusika na usafi ndani ya manispaa hiyo kuhakikisha wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na kila mtu anayezalisha takataka anapaswa kuchangia kama wanavyochangia huduma za matumizi ya maji.

Mahenge aliitaka manispaa hiyo kuandaa mchanganuo na mpango mzima utakaoonesha jinsi ya kufanya usafi ambao watampa mkuu wa wilaya hiyo pamoja na yeye na kuonesha jinsi watakavyokuwa wakikusanya mapato.

Mkuu wa wilaya ya Singida   Mhandisi Paskas Muragili akizungumza katika ziara hiyo alisema wamekuwa wakipanga mikakati ya kufanya usafi lakini imekuwa haitekelezeki kutokana na kukosekana kwa ushirikiano mzuri na Menejimenti ya Manispaa hiyo. 

Dkt. Mahenge katika ziara hiyo alitembelea Soko la Kimataifa la Vitunguu na mradi wa kilimo cha umwagiliaji uliopo Kijiji cha Kisasida ambao uligharimu zaidi ya Sh.700 milioni lakini haufanyi kazi ambapo pia alizungumza na wananchi kujua changamoto zao na akatumia nafasi hiyo kuhamasisha ulipaji wa kodi na ushuru kutokana na biashara wanazozifanya ndani ya manispaa hiyo.

Leo Dkt. Mahenge ataendelea na ziara hiyo kwa kutembelea Kituo cha Afya  Sokoine na Mnada wa Mtamaa kwa lengo la kuona namna ya ukusanyaji mapato.

Thursday, June 24, 2021

TEWW INAVYOWASAIDIA WASICHANA WALIOISHIA NJIANI KUMALIZA MASOMO YAO

Timu ya Viongozi wa Taasisi ya Elimu ya Watu wazima nchini (TEWW) mkoani Iringa wakiwa wamemtembelea mmoja wa wasichana aliyekatisha masomo yake baada ya kupata ujauzito ili arejee shuleni.
Mmoja wa Mabinti (katikati) ambaye ndoto zake zilizima baada ya kupata ujauzito akiwaelekeza wenzake baada ya kurudi shule kupitia mpango wa TEWW.
Baadhi ya walimu na wanafunzi wanaosoma kupitia Taasisi ya Elimu ya Watu wazima nchini (TEWW) mkoani Iringa kupitia Kituo cha Sabasaba wakiwa katika picha ya pamoja.


Na Mwandishi wetu, Iringa


TAASISIi ya Elimu ya Watu wazima nchini (TEWW) inatekeleza mpango wa kuwasaidia wasichana waliokatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwamo mimba, kumaliza elimu ya sekondari.

Taasisi hiyo imebeba jukumu la kuwasaidia wasichana hao wakati ambapo  bado sera ya elimu ikiwa haijaruhusu, kuendelea na masomo kupitia mfumo wa kawaida.

Mkurugenzi Mkuu wa TEWW, Dkt Michael Ng’umbi amesema katika taarifa yake kuwa kwa namna ya pekee mfumo huo umekuwa mkombozi kwa wasichana waliopata changamoto na kulazimika kuacha masomo yao.

“Kuna ushuhuda wa wasichana ambao wamefanya vizuri sana katika masomo yao kwa kupitia vituo vya elimu kwa njia mbadala vinavyosimamiwa na TEWW,” amesema Dk Ng’umbi.

Akitoa mifano, amesema katika mwaka 2020, wasichana kumi kutoka mkoa wa Tanga waliosoma kupitia mfumo huo walifaulu vizuri na kujiunga na vyuo vya elimu ya juu.

“Wasichana hawa ni miongoni mwa wasichana waliosoma katika vituo vinavyosimamiwa na taasisi hii, kupitia ufadhili wa shirika la BRAC Maendeleo,” anasema Dk Ng’umbi.

Alisema katika mkoa huo wa Tanga,  mwaka 2020 wasichana 31 walifaulu mtihani wa kidato cha nne kati ya daraja la kwanza na la tatu. 

“Kati yao, 20 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za serikali na sita  kujiunga na vyuo vya serikali,” alisisitiza.

Akielezea mkoa wa Mwanza, Dk Ng’umbi alisema mwaka 2019, wasichana 37 walifaulu mtihani wa kidato cha nne daraja la kwanza hadi la tatu na kuwa kati yao, tisa walichaguliwa kuendelea kidato cha tano na 12 walijiunga na vyuo. 

Aidha katika mwaka 2020, wasichana 24 wa mkoa wa Mwanza walifaulu mtihani huo kwa daraja la 1 hadi la 3, kati yao 11 wamechaguliwa kuingia kidato cha tano na 12 wanaendelea na mafunzo vyuoni. 

Mwaka 2020 mikoa ya Kigoma na Dodoma kila mmoja ulipata msichana aliyefaulu kiwango cha daraja la kwanza.

Baadhi ya wasichana waliosoma kupitia mfumo huo waliishukuru taasisi hiyo kuwa daraja kwao na kuhakikisha wanatimiza ndoto zao.

Mmoja wa wasichana hao, ambaye anasoma kituo cha sabasaba alisema, ndoto zake zilikufa alipoacha masomo yake kwa sababu ya mimba lakini sasa anauhakika.

Kwa upande wake, Mkufunzi Mkazi wa Mkoa wa Iringa, Camilius Mwila amesema Iringa ni kati ya mikoa inayotekeleza kwa vitendo, elimu hiyo.

Taasisi hiyo ilianza kuendesha masomo ya sekondari kwa njia mbadala mwanzoni mwa miaka ya 1970.