Monday, November 28, 2022

MILA, DESTURI ,UKOSEFU WA ELIMU VIMETAJWA KUWA NI SABABU YA KUWEPO KWA VITENDO VYA UKATILI MKOANI SINGIDA

p>

Mmoja wa Shujaa kutoka Taasisi ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA)  akitolewa damu kwa ajili ya kuchangia akiba ya damu wakati Mashujaa kutoka SMAUJATA  walipotembelea Hospitali ya Makiungu iliyopo wilayani Ikungi kwa ajili ya kutoa elimu ya kupinga vitendo vya ukatili, pamoja na kuwajulia hali wagonjwa ambapo pia walifanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo katika ziara iliyofanyika jumamosi..


Uchangiaji wa damu ukifanyika.
Mashujaa wakifanya usafi kuzunguka viunga mbalimbali vya Hospitali hiyo.
Usafi ukiendelea.
Mashujaa wa SMAUJATA wakiwafariji wagojwa kwa kufanya maombi pamoja.
Sabuni zikitolewa kwa wagonjwa.
Picha ya pamoja wakati wa ziara hiyo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MILA na desturi na ukosefu wa elimu vimetajwa kuwa sababu ya kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii kwa watoto ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukeketaji kwa watoto wadogo.

Sababu hizo zimetolewa na wananchi wa Wilaya ya Singida na Iikungi wakati Taasisi ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania –( SMAUJATA)  wakito elimu ya kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa akina mama wajawazito katika Hosiptal ya Makiungu wilayani Ikungi..

Wamesema kuwa kuna baadhi ya wananchi bado wanaendelea kufuata mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo bado zinasababisha kufanyika kwa vitendo hivyo vya ukatili.

Wameongeza kuwa hata mangariba wamebadili njia ya kufanya ukeketaji ambapo kwa sasa vitendo vya ukeketaji unafanywa kwa watoto wachanga .

Kutokana na sababu hizo, taasisi ya shujaa wa maendeleo na ustawi wa jamii tanzania - SMAUJATA imeitembelea hospital ya makiungu wilayani ikungi  mkoani singida kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia hasa vitendo vya ukeketaji kwa watoto kwa akina mama wajawazito.

Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Singida Dismas Kombe, alisema wanatoa elimu kwa akina mama wajawazito kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutambua ubaya wa ukatili wa kijinsia ili waweze kuwalinda watoto wao wanaotarajia kuwaza na vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.

Kombe alisema kuwa bado makundi la watoto na wanawake yanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na ukeketaji kwa watoto, vipigo na ubakwaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Kombe ameongeza pia changamoto iliyopo kwa jamii ni kushindwa kuripoti vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyofanyiwa akina mama na watoto, kutokana na vitendo vingi kufanywa na wanandugu.

Katibu idara ya wanaume SMAUJATA - Mkoa Singida, Simon  Mdumah alisema kundi la wanaume nalo ni moja ya kundi linalofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa sasa, changamoto ni namna ya wanaume hao kuripoti vitendo hivyo wanavyofanyiwa.

Mdumah alisema wanaume wengi wanashindwa kuripoti ukatili wanaofanyiwa kutokana na mila na desturi za kiafrika na kuogopa kuonekana wadhaifu kwa wake zao na jamii kwa ujumla.

Pamoja na kutoa elimu, SMAUJATA pia imefanya usafi katika hospitali hiyo na kuchangia damu kwa ajili ya kuwasaidia wale wenye uhitaji wa damu.

TARI UKILIGURU YAELIMISHA MANUFAA KILIMO CHA PAMBA

Mratibu wa zao la Pamba nchini kutoka Kituo cha Utafiti cha Kilimo Ukiliguru Dk. Paul Saidia (wa kwanza kushoto) akifuatilia tukio la utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wa 'Beyond Cotton' unaolenga kuinua thamani ya zao la pamba kwenye mnyororo wa thamani kwa wilaya za Kwimba, Magu na Misungwi jijini Mwanza-unaofadhiliwa na Brazil kwa kushirikiana na Tanzania kwa gharama ya Dola 930,118 (Tsh.Bilioni 2.17) na kutekelezwa na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) na Bodi ya Pamba (TCB). Wengine pichani ni wataalamu mbalimbali watakaoungana na taasisi hizo kutekeleza mradi huo.

.Kaimu Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), David Basley akikagua na kufanya uhakiki wa vifaa mbalimbali vitakavyotumika kufundishia wakulima wa pamba kupitia mradi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Magu Salum kali aliyevaa suti (katikati) akiwa na wataalamu mbalimbali wanaotekeleza mradi wa kuongeza thamani kwenye zao la pamba ndani ya wilaya hiyo

Mkufunzi Mwandamizi wa masuala Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Campina Grande nchini Brazil, Profesa Vannile Penoa, akitoa mafunzo ya lishe bora kupitia mradi huo kwa wakulima wa pamba wilayani Magu.

Mtaalamu wa zao la pamba kutoka WFP, Joelcio Carvalho akiwaelekeza wakulima namna ya kutumia teknolojia ya kupanda mbegu mbalimbali kwa kutumia mashine maalumu.

Mmoja wa wakulima akiwa kwenye mazoezi kwa vitendo ya namna ya kutumia teknolojia ya mashine rahisi ya kupandia (planter) mbegu za pamba na mazao mengine bila ya kuinama.
Mtaalamu Mwandamizi wa masuala ya lishe na virutubishi kutoka TARI Ukiligulu Dk. Calesma Chuwa (wa kwanza kulia) akisimamia utekelezaji wa mafunzo kupitia mradi wa 'Beyond Cotton' kwenye eneo la kuboresha lishe kwa wakulima.

Mmoja wa wataalamu wa mradi huo, Profesa Luderlandio Andrade aliyevaa miwani shimoni akiwaelekeza mafundi na baadhi ya wakulima namna ya kujenga tenki kwa ajili ya teknolojia ya kuvuna maji ya mvua yatakayosaidia kuendesha kilimo cha mbogamboga na matunda hata wakati wa msimu wa kiangazi lakini pia kama kituo cha kujifunzia teknolojia hiyo kwenye eneo la lishe na namna ya kujiongezea kipato.Mratibu wa Lishe kutoka Wizara ya Kilimo Magreth Matai akitoa mafunzo kwa akinama wa wilaya ya Magu kupitia mradi huo.

 Wataalamu wa mradi huo wakitoa mafunzo ya namna bora ya kupima hali ya hewa kwa kutumia kifaa maalumu cha kupima kiasi cha mvua kabla ya kupanda pamba maarufu 'rain gauge'

Mratibu wa zao la Pamba nchini kutoka Kituo cha Utafiti cha Kilimo Ukiliguru ambaye pia ni mkurugenzi wa kituo hicho Dk. Paul Saidia (aliyesimama) akizungumza na wataalamu mbalimbali wa mradi huo muda mfupi kabla ya kuanza utekelezaji wake kwenye wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi mkoani Mwanza.

Mtaalam kutoka Bodi ya Pamba Nchini (TCB) Renatus Luneja akitambulisha wageni mbalimbali wanaotekeleza mradi huo ndani ya Wilaya ya Magu. Bodi hiyo ni miongoni mwa taasisi zinazotekeleza mradi wa Beyond Cotton. 

Na Godwin Myovela, Mwanza 

Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) kupitia kituo chake mahiri cha Ukiliguru kimehamasisha wananchi kutumia fursa ya msimu huu wa kilimo kuzalisha zao la pamba kwa tija, ubora na kwa kuzingatia agronomia stahiki ili kupata matokeo tarajiwa kwa manufaa chanya ya ukuaji uchumi kwenye mnyororo wake wa thamani.

Kwa mujibu wa Tari Ukiliguru, zao hilo la kimkakati ambalo linaongoza kwa kuwa na faida kubwa za kiuchumi ikilinganishwa na mazao mengine, linatajwa kama kiini cha malighafi muhimu kwa uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo, nguo, pamba za hospitali, magodoro, mazulia na mito ya viti.

Mratibu wa zao la pamba nchini Dk. Paul Saidia alitoa hamasa hiyo wakati akishiriki utekelezaji wa mradi wa 'Beyond Cotton' unaofadhiliwa na Brazil kwa kushirikiana na Tanzania chini ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Bodi ya Pamba (TCB) unaolenga kuinua tija ya zao la pamba kwa wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi mkoani hapa.

Saidia ambaye pia ni Mkurugenzi wa kituo cha Tari Ukiliguru alisema hata mbegu za pamba ambazo hazitumiki kwa kupandwa na wakulima bado zina faida; kwani hutumika kwa kusagwa katika viwanda kwa ajili ya kutengeneza mafuta ya kula, margarine na sabuni-huku mashudu yake yakitumika  kama chakula cha mifugo na mboji.

Aidha, alifafanua kwamba kama mkulima atajifunga mkanda na kuzalisha robota moja ya pamba yenye kilogramu 227 ni dhahiri baada ya uchakataji itakwenda kuzalisha suruali za 'jeans' 215, mashati 750, fulana1200, soksi 4300 na kaptula 2100.

Zaidi kwa robota moja hiyo hiyo mtaalamu huyo alisema mkulima atazalisha idadi ya shuka za kitanda za futi 3 zipatazo 250, nepi 3000 na pamba za kuondolea uchafu masikioni kwa idadi ya 680,000 sambamba na mti wake kuchakatwa na kutumika kama mkaa mbadala.

"Ninajaribu kuainisha tija ya kilimo cha pamba na matokeo yake kwenye mnyororo wa thamani na upana huu wa soko ndani na nje ili kila mtanzania aone fursa zilizopo na azichangamkie," alisema Saidia.

Hata hivyo, katika muktadha wa mzunguko wake wa kibiashara alisema Tani moja pekee ya mbegu ina uwezo wa kuzalisha mpaka lita 200 za mafuta ya kula, kilo 500 za mashudu, kilo 300 za pumba na takribani lita 40 za magwanji ambayo hutumika kama malighafi ya kutengenezea sabuni.

Alisema kwa sasa ni mikoa 17 tu nchini inayolima pamba ambayo imeendelea kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa dunia ambapo kila mwaka linakadiriwa kuingiza takribani Dola Milioni 120 (Bilioni 27.6)

"Pamoja na kwamba ni mikoa hii michache inalima bado mchango wake ni mkubwa, sasa kama tutahamasishana na watanzania wakahamasika nadhani hapa tutachangia vizuri ajenda yetu ya 10/30," alisema Saidia na kusisitiza;

Pia kilimo hiki ni mwafaka wa falsafa ya waziri wa sasa wa kilimo, Hussein Bashe ambaye anaamini katika dhana ya 'kilimo cha kibiashara'  kwa maana ya kuuza bidhaa za kilimo zilizochakatwa kwa matokeo chanya kwenye kukuza uchumi, ongezeko la tija na fedha za kigeni kama mkakati wa ajenda 10/30 ifikapo 20/30.  

Sunday, November 27, 2022

WAKULIMA WILAYA YA MAGU WAPATA MAFUNZO YA KILIMO CHA PAMBA CHENYE TIJA KUPITIA MRADI WA BEYOND COTTON

Mkulima wa Kijiji cha Chandulu Wilaya ya Magu mkoani Mwanza akijifunza kupanda mbegu za pamba kwa kutumia teknolojia rahisi inayotumia muda mfupi baada ya kupata mafunzo kupitia mradi wa ‘Beyond Cotton, unaotekelezwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Bodi ya Pamba (TCB) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP)

Saturday, November 26, 2022

KATIBU TAWALA MKOA WA SINGIDA AKABIDHI PAMPU 13 ZA UMWAGILIAJI KWA VIJANA

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko (katikati) akikabidhi pampu 13 za umwagiliaji zinazotumia nishati ya jua kwa vikundi 13 vya  Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya  Manyoni, Itigi, Mkalama, Singida, Manispaa na Iramba zenye thamani ya Sh.Milioni 23.4 katika hafla iliyofanyika jana Shirika la Sema. Wa pili kulia mbele ni Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani..
Vifaa hivyo vikikabidhiwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko (katikati) akikabidhi pampu hizo. Wa pili kutoka kushoto ni Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani.

.............................................................

Na Mwandishi Wetu, Singida 

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko  amekabidhi pampu 13 za umwagiliaji zinazotumia nishati ya jua kwa vikundi 13 vya vijana  Vijana Halmashauri ya Manyoni, Itigi, Mkalama, Singida, Manispaa na Iramba zenye thamani ya Sh.Milioni 23.4.

Akizungumza na vijana hao katika Ukumbi wa Ofisi za Shirika lisilo la Kiserikali la SEMA mkoani hapa Mwaluko alisema mashine hizo zitawasidia kuongeza kipato katika shughuli za kilimo cha bustani na kuwataka wazitunze ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Aidha Mwaluko ametoa wito kwa vijana kuacha kulalamika kwamba hakuna ajira na badala yake wajitume kufanya kazi za kilimo na ufugaji kwa kuwa bidhaa zitokanazo na shughuli hizo zina soko kubwa ndani ya Mkoa na nje.

Aidha Katibu Tawala huyo amelishukuru Shirika la NSV (Nedhalend Development Organization) kupitia Mradi wake wa OYE (Opportunities for youth Employment) kwa msaada wa mashine hizo ambazo zimegharimu kiasi cha Milioni 1.8 kwa kila moja ambapo shirika limechangia asilimia 68 na Kampuni iliyotengeneza ikachangia asilimia 15 wakati vikundi vikachangia asilimia 17 ambao inalipwa kwa miezi  16.

Kwa upande wake Afisa Mwandamizi wa Usimamizi na Tathmini katika Mradi huo wa OYE  Belinda Masawe, amesema  mashine hizo hutumia nishati ya jua ambayo haitawaingizia gharama za uendeshaji Wanakikundi.

Hata hivyo Belinda ameendelea kufafanua kwamba mashine ina uwezo wa kumwagilia shamba lenye ukumbwa wa ekari mbili kwa msimu mmoja na ina uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka kumi (10) ukipata mafunzo.

Aidha ameeleza kwamba vikundi hivyo vimepewa muda wa miaka miwili (2) wa uangalizi na endapo zitaharibika kabla ya hapo vitarudishwa kwa muuzaji.

Akimalizia hotuba yake Belinda ameeleza kwamba mashine hizo zimetafutiwa ubora wake na kubainika kwamba ni nzuri kwa mazingira kwa kuwa hazitoi moshi wala mabaki ya mafuta ambayo yangechafua mazingira.

Awali akitoa maelezo ya ukaribisho Afisa Vijana wa Mkoa wa Singida Fredrick Ndahani, ameeleza kwamba fursa za biashara katika Mkoa huo nikubwa kwa kuwa kuna miradi mingi imeanzishwa ikiwemo bomba la mafuta na miradi ya machimbo ya madini kwamba ni soko kubwa.

KITUO KIPYA CHA AFYA KATA YA NTUNTU IKUNGI MKOANI SINGIDA KUANZA KUTOA HUDUMA

Muonekano wa jengo la Kituo cha Afya cha Kata ya Ntuntu kilichopo wilayani Ikungi mkoani Singida ambacho kimetakiwa kuanza kutoa huduma za utabibu mara moja ifikapo Novemba, 28, 2022 baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 99.
Wajumbe wa kamati ya ujenzi wa kituo hicho wakifanya ukaguzi wakiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) Dkt.Ntuli Kapologwe wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea kituo hicho na kukikagua aliyoifanya wilayani humo hivi karibuni.
Ukaguzi wa kituo hicho ukifanyika.
Picha ya pamoja baada ya kukaguliwa kwa kituo hicho.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WANANCHI wa  Kata ya Ntuntu Walayani Ikungi mkoani hapa wanatarajia kuanza kupata huduma za kitabibu katika Kituo kipya Cha Afya Cha  Ntuntu baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 99.

Akizungumza  hivi karibuni wakati wa ziara yake Mkurugenzi wa Huduma za Afya Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) Dkt.Ntuli Kapologwe  amesema ifikapo jumatatu ya Novemba 28 mwaka huu kituo hicho kiwe kimeanza kazi na kuhudumia wananchi.

Aidha ameeleza kwamba  hatua iliyofikia kituo hicho  inastahili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo wakati vitu vidogo vidogo vilivyobaki vikiendelea kukamilishwa.

Hata Hivyo Dkt.Kapologwe ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida kuendelea na maandalizi ya kupokea vifaa tiba ili ifikapoa Novemba 28,2022 huduma ziwe zimeanza na wananchi wanapata matibabu.

"Tumeambiwa jengo limefikia asilimia 99 kukamilika kwa hatua hii ni lazima huduma zianze  kutolewa hata kama kuna vitu vichache vya kumalizia " alisema.

Hata hivyo ameendelea kueleza kwamba Serikali ipo hatua ya mwisho ya kuleta vifaa tiba katika kituo hicho ambapo amesema kufikia jumatatu vitakuwa vimeshafika.

"Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za uletaji wa vifaa tiba mbalimbali katika kituo cha afya hivyo wananchi waanze kupata huduma"  alisema Dkt. Kapologwe.

Dkt. Kapologwe  ameipongeza  Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na timu nzima ya usimamizi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa ukamilishaji mzuri wa majengo matatu ya awamu ya kwanza (Jengo la Wagonjwa wa Nje OPD, Jengo la Maabara na Kichomea Taka) ambao mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 99% .

Aidha  majengo  matatu mengine  ni pamoja na  Jengo la Wodi ya Wazazi (Maternity), Jengo la Upasuaji (Theatre) na Jengo la Kufulia (Laundry)  ambapo ujenzi huyo umefikia zaidi ya asilimia 60%  huku Dkt.Kapolongwe akiwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili  kufikia Disemba 30 majengo hayo yawe yamekamilika.

Ujenzi wa vituo vya afya ni moja ya mkakati na kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia  kuhakikisha  wananchi wanapata huduma za afya katika maeneo ya karibu na makazi yako.

Thursday, November 24, 2022

TIA SINGIDA YATOA SEMINA YA UJASIRIAMALI KWA WANAFUNZI ILI KUPUNGUZA CHANGAMOTO YA AJIRA

 Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania, (TIA) Profesa William Pallangyo akizungumza wakati akifungua semina ya Ujasiriamali kwa wanafunzi wa taasisi hiyo ambayoitawasaidia kuanziisha biashara mbalimbali watakapomaliza masomo yao.   Semina hiyo ya siku moja ilifanyika leo katika Taasisi hiyo Kampasi ya Singida.

.Mratibu wa Ujasiriliamali , Imani Matonya akizungumzia umuhimu wa semina hiyo kwa wanafunzi hao.
Makamu Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu- Taaluma, Dk. Momole Kasambala akizungumza katika semina hiyo.

Wanafunzi wakishiriki kwenye semina hiyo.

Semina ikiendelea.
Mratibu wa Ujasiriamali na Kituo Atamizi wa Kampasi ya Singida , Mohamed Kaluse (kushoto) akiwa na mratibu mwenzake kutoka Dar e Salaam wakati wa semina hiyo.

Wanafunzi wa Taasisi hiyo wakiwa kwenye semina hiyo.
Semina ikiendelea.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja. 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

TAASISI ya  Uhasibu Tanzaia  (TIA), Kampasi ya  Singida imetoa semina  kwa wanafunzi wa Taasisi hiyo kwa lengo la kupunguza changamoto ya upungufu wa ajira inayowakabili vijana wengi pale wanapomaliza masomo yao ya elimu ya juu.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) , Prof. William Pallangyo  amesema semina hiyo ya Ujasiriamali itawasidai vijana hao kuanziisha biashara mbalimbali watakapomaliza masomo yao.

Pallangyo alisema hayo wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Taasisi hiyo ya Uhasibu Tanzania namna ya kubuni mawazo mbalimbali ya biashara, yatakayowasidia kujiajiri wenyewe na kuacha tabia ya kusubiri kuajiriwa.  

Alisema kumekuwa na ufinyu wa ajira katika sekta mbalimbali hivyo kupitia mfunzo hayo ya ujasiriamali itasaidia kutambua fursa zilizopo.

Makamu Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu- Taaluma, Dk. Momole Kasambala alisema Taasisi ya Uhasibu Tanzania imejipanga kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa ajiliya kuwajengea uwezo wa kupata mawazo ya biashara ambayo yatawasiadia katika kujiajiri.

Aidha Dk.Kasambala alisema wanafunzi wenye mawazo mazuri watashindanishwa na mawazo yatakayoshinda yatapelekwa mbele zaidi kwa kutafutiwa mitaji na kukutanishwa nataasisi za kifedha ili wanafunzi hao waweze kupata mikopo ya kuanzisha biashara.

Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo wamesema mafunzo hayo yatawasidia kuanzisha biashara zitakozowasaidia kuondokana na changamoto ya upatikananji wa ajira.

Wamesema kupitia biashara hizo pia wataweza kuajiri vijana wengine ambao hawana ajira na hivyo kuwasaidia vijana wengi waliomaliza vyuo na hawana ajira kupata ajira nchini.

Hata hivyo wameomba taasisi za kifedha kuweka mikopo yenye riba nafuu ambayo itawasiadia wao kukopa na kuanzisha biashara ambazo zitatoa ajira kwa vijana wengi.


Tuesday, November 22, 2022

TARI, BODI YA PAMBA NA WFP WASAINI RASMI MAKUBALIANO YA KIUTENDAJI KUINUA ZAO LA PAMBA

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini  (TARI) Dkt. Geofrey Mkamilo (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kiutendaji utakaowaongoza kutekeleza programu ya kuinua tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na chakula lishe-ikiwemo mazao ya maharagwe, viazi, mahindi na mbogamboga kwa wilaya za Kwimba, Magu na Misungwi mkoani Mwanza-Novemba 21,2022.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini  (TARI) Dkt. Geofrey Mkamilo (kulia) akipeana mkono na Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson baada ya kusaini mkataba huo.
Mwakilishi wa Bodi ya Pamba nchini (TCB), ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa bodi hiyo, James Shimbe (kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kiutendaji utakaowaongoza kutekeleza programu ya kuinua tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na chakula lishe-ikiwemo mazao ya maharagwe, viazi, mahindi na mbogamboga kwa wilaya za Kwimba, Magu na Misungwi mkoani Mwanza-Novemba 21,2022.

Washiriki wa hafla hiyo wakiwa kwenye picha ya pamoja.

Mwakilishi wa Bodi ya Pamba nchini (TCB) James Shimbe, (kushoto), Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini  (TARI) Dkt. Geofrey Mkamilo kabla ya kusaini mkataba huo.
Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa TARI, Profesa Joseph Ndunguru akizungumzia  manufaa ya mradi wa 'Beyond Cotton'.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI-Ukiruguru mkoani hapa, ambaye pia ni mratibu wa zao la Pamba nchini, Dkt. Paul Saidia, akieleza baadhi ya mambo yatakayotazamwa zaidi katika utafiti kulingana na mkataba, ikiwemo; suala la  kuongeza thamani kwa kuwa na mbegu bora za pamba, kuongeza usalama wa chakula na namna ya kupambana na magugu.

Washiriki wakiwakwenye  hafla hiyo.

Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Mwanza

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI), Bodi ya Pamba (TCB) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wamesaini mkataba wa mashirikiano ya kiutendaji (MoU) katika eneo la mradi wa kuzalisha na kuongeza tija kwenye mnyororo wa thamani wa zao la pamba na mazao mengine ya chakula lishe.

Mradi huo wa mwaka mmoja unaojulikana kama ‘Beyond Cotton,’ unafadhiliwa na Serikali ya Brazil kwa gharama ya Dola za kimarekani 629,000, na kutekelezwa na taasisi hizo, unatarajiwa kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo wa zao la pamba takribani 9,000 kutoka wilaya za Magu, Kwimba na Misungwi mkoani hapa.

Akizungumza muda mfupi baada ya kusaini mkataba huo, Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Geofrey Mkamilo alipongeza serikali ya Brazili na Tanzania kupitia Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono na mtazamo chanya katika kuhakikisha zao la pamba na mazao mengine ya chakula yanaendelezwa na kuongezewa tija kwa manufaa ya wakulima wake na ukuaji wa uchumi.

Mkamilo alisema kwa namna serikali zote mbili zilivyojipanga, chini ya utekelezaji wa wadau mbalimbali, watahakikisha matokeo ya utekelezaji wa mradi huo yanakwenda kuleta ustawi na ongezeko la ubora na uzalishaji kwenye zao la pamba na kilimo mseto.

“Hafla hii ni fursa ya kipekee katika kuendeleza na kuongeza uzalishaji wa mnyororo wa thamani kwa wakulima wa ukanda wa pamba, lakini pia kuwajengea uwezo zaidi maafisa ugani wa zao hilo,” alisema Dkt. Mkamilo.

Pia Mkurugenzi Mkazi wa WFP, Sarah Gordon-Gibson, alisema ndani ya mfumo wa Ushirikiano wa Kusini-Kusini, Mradi wa ‘Beyond Cotton’ unalenga zaidi kubadilishana maarifa kati ya Tanzania na Brazili katika mustakabali chanya unaolenga kuongeza tija katika kilimo cha pamba na mazao mengine ya chakula, pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani, ikiwemo kuwaunganisha wakulima na masoko ya ndani na nje.

“Ni matumaini yetu kuwa mradi huu utabadilisha maisha ya wakulima wadogo, sisi WFP nchini Tanzania na Kituo cha Ubora cha WFP dhidi ya Njaa nchini Brazili-tunathamini ushirikiano thabiti wa TARI na TCB ulioanza tangu 2019, na tunatazamia kuendeleza vilivyo ushirikiano huu,” alisema Gibson na kuongeza;

“Naishukuru Serikali ya Brazil kupitia Shirika la Ushirikiano la Brazili, kwa kufadhili mpango huu, na kwa kuwachukulia wakulima wadogo wa Tanzania kama wadau watarajiwa katika sekta ya pamba. Pia ningependa kushukuru Chuo Kikuu cha Shirikisho cha Campina Grande na Taasisi ya Pamba ya Brazili kwa kusaidia mradi huu.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa TCB, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Usimamizi wa bodi hiyo, James Shimbe, alisema ustawi, tija na ongezeko chanya la uzalishaji wa zao la pamba nchini linategemea zaidi utafiti. Hivyo katika kutekeleza azma ya mradi huo TCB, TARI na WFP wamejipanga kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu na halmashauri zote zitakazofikiwa ili kufikia lengo lililokusudiwa.

Naye, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa TARI, Profesa Joseph Ndunguru alisema pamoja na mambo mengine, mradi huo unakwenda kufanya utafiti na majaribio ya mbegu, kutoa mafunzo ya kilimo cha pamba na mazao lishe mengine, ikiwemo viazi, mahindi na maharagwe lishe.

Kwa mujibu wa Ndunguru, mradi huo unakwenda kuongeza thamani kwenye uchakataji wa pamba kwa AMCOS 9 ndani ya wilaya 3 za Kwimba, Magu na Misungwi-na baadaye matokeo tarajiwa yatasambazwa nje ya wilaya hizo na kwingineko nchini kwa lengo la kueneza teknolojia ya mradi huo.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI-Ukiruguru mkoani hapa, ambaye pia ni mratibu wa zao la Pamba nchini, Dkt. Paul Saidia, aliainisha baadhi ya mambo yatakayotazamwa zaidi katika utafiti kulingana na mkataba huo kuwa ni pamoja na kuongeza thamani kwa kuwa na mbegu bora za pamba, kuongeza usalama wa chakula na namna ya kupambana na magugu.

“Na tunatarajia wakulima takribani 9,000 wa pamba watakaofikiwa wataelimishwa juu ya kilimo cha maharagwe lishe, viazi lishe na mbogamboga, pia mradi huo unatarajia kujenga matanki makubwa yatakayosaidia kuvuna maji ya mvua,” alisema Dkt Saidia. 

Monday, November 21, 2022

RC SINGIDA ASEMA LISHE BORA KWA WATOTO WADOGO NI MUHIMU



Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa wa Singida wakati akitiliana saini mikataba kwa ajili ya huduma ya Lishe kwa watoto mkoani humo

Kaimu Afisa Lishe Mkoa wa Singida, Christowelu Barnabas akiwasilisha mpango huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida , Ester Chaula (kulia)akisaini mkataba huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akisaini Mkataba maalum wa kushughulikia suala la Lishe katika wilaya ya Mkalama huku Mkuu wa Wilaya hiyo, Sophia KIzigo akiwa makini kuangalia utiaji saini huo.


Na Abby Nkungu, Singida

WAKUU wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri zote saba za mkoa wa Singida wamesaini mikataba maalum kwa ajili ya kushughulikia kikamilifu suala la kuboresha lishe katika maeneo yao ikiwa ni utekelezaji wa Agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa hivi karibuni Jijini Dodoma.

Mikataba hiyo inayohusu usimamizi madhubuti wa kuboresha masuala ya lishe katika jamii, imesainiwa na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa halmashauri mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.  

“Hivi karibuni, Rais wetu Mama Samia alituita Dodoma na kutuagiza kuongeza jitihada katika kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za lishe bora." alisema kisha akaendelea;

Nami nimewaita nyie Ma-DC na Ma-DED ili kusaini mikataba hii kwa ajili ya kusimamia lishe bora kwenye maeneo yenu. Nasisitiza, atakayeshindwa jukumu hili atakuwa ametafuta ugomvi na Serikali"

Pamoja na kusimamia huko, Serukamba aliwataka Wakurugenzi wa halmashauri zote kuhakikisha wanatenga 1,000/- kwa kila mtoto kwenye bajeti ya mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa lishe bora.

“Suala la lishe na afua za lishe tulipe kipaumbele cha kwanza. Tukifanikiwa kuifanya jamii yetu kuwa na lishe bora; hasa kwa watoto wa mwaka mmoja hadi mitano, tutakuwa tumeweka jiwe la msingi kwenye kizazi kijacho," alisema kisha akaendelea;

Tunaweza tukawa tunajiuliza kwa nini watoto wetu wanafeli sana mitihani tukadhani walimu hawafundishi kumbe sababu mojawapo ni madhara ya kutopata lishe bora; hasa kutoka kwa mama anapopata mimba," alifafanua.

Wadau mbalimbali wanasema kuwa utiaji saini mikataba hiyo ya kusimamia lishe bora kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri, umekuja wakati muafaka ambapo Serikali inatekeleza Programu Jumuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJ-MMMAM) ya miaka mitano iliyoanza Januari 2021.

Mmoja wa wadau hao, Mganga Mkuu wa mkoa wa Singida, Dk Victorina Ludovick alisema kuwa  chini ya Programu hiyo ya Taifa inayoshughulika na masuala mtambuka; ikiwemo afya bora, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali na ulinzi na usalama ni muhimu kwa maendeleo na makuzi ya mtoto chini ya miaka minane. 

"Ni dhahiri suala la udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa kundi hilo litakuwa historia. Hivi sasa takwimu zinaonesha udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano limepungua kwa asilimia 10 katika kipindi cha miaka minane iliyopita. Naamini chini ya juhudi hizi zilizopewa msisitizo na Rais mwenyewe, changamoto hii inaenda kwisha” alisema.

Hata hivyo, Utafiti wa Kitaifa wa hali ya lishe nchini mwaka 2018, unaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano mkoani Singida wana tatizo la udumavu, asilimia 5 wanakabiliwa na ukondefu na asilimia 15 ya watoto hao wana uzito mdogo.

Daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya Wanawake na Watoto hospitali ya Rufaa mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani anasema pamoja na sababu nyingine, mara nyingi udumavu, ukondefu na uzito pungufu kwa mtoto ni matokeo ya lishe duni na huleta homa za mara kwa mara.

“Lishe duni ni chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo kwa watoto wadogo. Hudumaza ukuaji wa kimwili na kiakili lakini pia hupunguza uwezo wa mtoto kufanya vizuri shuleni na ufanisi wa kazi katika maisha ya utu uzima. 

Ndio maana msisitizo mkubwa wa lishe bora huwekwa kwa mtoto katika siku 1,000 za mwanzo; yaani tangu mimba kutungwa” alifafanua.

Baadhi ya wazazi na walezi  wanasema kuwa cha muhimu ni kwa wataalamu wa afya, lishe na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa jamii; hususan Vijijini juu ya umuhimu wa lishe bora hasa kwa akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na wenye watoto walio na umri chini ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutofikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na viashiria kama vile utapiamlo, umasikini na kukosekana kwa uhakika wa  chakula. 

ORYX ENERGIES YAWAKUMBUKA WANAWAKE WAJAWAZITO SERENGETI KWA KUWAPATIA MITUNGI YA GESI NA MAJIKO YAKE

Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Peter Ndomba (wa tatu kulia) akikabidhi mtungi wa gesi kwa mmoja ya wanawake wajazito wa Kata ya Rubanda kwa niaba ya wanawake wengine wajawazito wa wilaya ya Serengeti.Wa pili kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja akishuhudia utolewaji wa mitungi hiyo ya gesi kwa wanawake wajawazito wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja (watatu kulia) akipokea mtungi wa gesi kutoka kwa Meneja Masoko wa Kampuni ya Oryx Peter Ndomba(wan ne kushoto).Tukio hilo limefanyika jana eneo la Rubanda wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti iliyoratibiwa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation ambayo imejikita katika kusaidia mtoto njiti na lengo la mitungi hiyo ni kuwawezesha wanawake kutumia nishati safi ya kupikia.

Meneja Masoko wa Kampuni Peter Ndomba(kulia) akipokea cheti cha shukrani kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti.Cheti hicho kimeandaliwa na Taasisi ya Doris Mollel Foundation ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa wadau hao katka kusaidia taasisi hiyo.

 

Naibu Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel (kushoto aliyejifunga mgolole) akizungumza umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia baada ya Kampuni ya ORYX Energies kukabidhi mitungi ya gesi na majiko yake kwa wanawake wajawazito wilayani Serengeti kupitia Taasisi ya Doris Mollel Foundation.


 Doris Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Mollel Foundation akisoma jina la mmoja wa wadau walioshiriki kufanikisha Siku ya Mtoto Njiti Duniani wakati wa maadhimisho ya siku hiyo yaliyofanyika wilayani Serengeti mkoani Mara.

Viongozi wakiwa meza kuu.
Muonekano wa mitungi ya gesi kabla ya kukabidhiwa. 

Na Mwandishi Wetu, Serengeti. 

KAMPUNI ya Oryx Energies imekabidhi mitungi ya gesi 200 pamoja na majiko yake kwa kwa Taasisi ya Doris Mollel Foundation inayojishughulisha kusaidia watoto njiti pamoja na malezi ya watoto hao ambapo mitungi hiyo imetolewa kwa wanawake wajawazito katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kuwaondolea adha ya kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia.

Mitungi hiyo ya gesi ikiwa na majiko yake imekabidhiwa leo Novemba 20 mwaka 2022 kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani ilyofanyika Kata Rubanda wilayani Serengeti mkoani Mara na kuhudhuriwa na wananchi pamoja na viongozi wa Serikali akiwemo Naibu Waziri wa Afya Dk.Godwin Mollel, Naibu Waziri wa  Maliasili na Utalii Mary Masanja, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani.

Uamuzi wa kampuni hiyo kutoa mitungi hiyo umepongezwa na viongozi mbalimbali walioshiriki maadhimisho hayo ambao wameeleza kitendo cha mama mjamzito kupewa mtungi wa gesi na jiko lake inakwenda kutoa nafasi mama kulea familia na hasa watoto na kuondokana na adha ya kwenda kukata kuni kwa ajili ya kupikia.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Marry Masanja amesema Oryx imeona umuhimu wa kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti kwa kutoa mitungii ya gesi na hiyo inakwenda kusaidia kutunza mazingira na wamekuwa mfano wa kuigwa kwani ndio kampuni ya mwanzo kabisa kuja na nishati safi ya kupikia.

“Tunawapongeza kwa jitihada zao za kuhakikisha jamii yetu inakuwa na nishati safi ya kupikia ambayo pia inasaidia katika kutunza mazingira.Kutumia nishati safi ya kupikia inasaidia  katika jitihada za Wizara ya Maliasili na Utaliii kulinda na kutunza mazingira, takwimu zinaonesha asilimia 90 ya nishati isiyo safi yaani mkaa na kuni ndio inayotumika kwenye kupikia,”amesema.

Aidha ametoa ombi kwa wadau wanaohusika na kampuni za nishati safi za kupikia kuangalia namna ya kuifanya nishati hiyo kupatikana kwa bei nafuu ambayo kila mwananchi anaweza kumudu kununua jiko la gesi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Dk .Godwin Mollel pamoja na kuzungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha afya ya mama na mtoto ikiwemo afya ya Mtoto Njiti pia anatoa pongezi kwa Taasisi ya Doriss Mollel katika kuokoa maisha ya Watoto Njiti na kuendelea kutoa kila aina ya misaada inayogusa jamii ya watoto njiti.

“Rais siku zote amekuwa akionesha njia lakini kwenye vifo vya mama na mtoto ni eneo ambalo linamgusa sana .Hata kwenye hotuba yake ya kwanza bungeni alionesha msisitizo mkubwa.Katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani Rais wetu ameweka fedha kwenye akaunti ya Doris Mollel Foundation Sh.milioni 20.Pia Rais ametoa Sh.milioni 50 kwa ajili ya kununuliwa vifaa kwa ajili ya Watoto Njiti.Kupitia bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujengwa vituo 100 vitakavyohusika na matibabu ya watoto njiti.

“Aidha nampongeza Dorris Mollel kwa mchango wake wa kusaidia jamii hasa watoto njiti, amekuwa hafanyi semina wala makongamano lakini kila anapoonekana anagusa jamii moja moja.Lakini leo hapa tumeshuhudia mitungi ya gesi 200 inakabidhiwa kwa wamama wajawazito.”Nishati safi ya kupikia inakwenda kupunguza uharibifu wa mazingira na tunafahamu mabadiliko ya kimazingira yanachangia uwepo wa Watoto njiti.”

Awali Meneja Masoko wa Kampuni ya ORYX Energies  Peter Ndomba aliyemwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo, amesema wao wameamua kuonesha njia kwa kuamua kutoa mitungi ya gesi kwa ajili ya kumuwezesha wamama wajawazito kuwa na nishati safi ya kupikia.

 “Tangu tulipoingia Tanzania mwaka 1999 moja ya ajenda yetu kuu ni kutetea mazingira kwa kuhakikisha jamii inakuwa na nishati safi ya kupikia lakini pili kuimarisha  afya ya watanzania hususani ya Mama ambaye amekuwa mstari wa mbele katika familia kwa upande wa mapishi , na Doris Mollel Foundatuion alipotuomba mitungi ya gesi hatukusita kumpatia kwasababu sisi tulimuona mama moja kwa moja., hivyo tuliamua kushiriki bila kusita.

Aidha amesema mitungi ambayo wameitoa kwa wanawake wajawazito ni sehemu ya kuunga mkono  jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na  Rais Samia Suluhu Hassan inayohamasisha Watanzania kutumia zaidi nishati safi ya kupikia badala ya kuendelea kukata kuni ambayo imekuwa ikichangia kuharibu mazingira.

Kwa upande wake wa Doris Mollel ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Dorris Mollel Foundation ameishukuru kampuni ya ORYX  kwa kumpatia mitungi hiyo ambayo aliiomba kwa ajili ya kuwasaidia wanawake wajawazito ambao ndio wamekuwa wakihangaika kutafuta kuni kwa ajili ya kupikia, hivyo kupatikana kwa mitungi hiyo kunakwenda kumuondolea mama mjazito changamoto ya kutafuta kuni.

“Wakati wa mjadala wa nishati safi ya kupikia ambao ulihudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan , ndo siku ambayo nilikutana na Mkurugenzi wa Oryx ambaye alishiriki mjadala huo na hivyo nilitumia nafasi hiyo kumuomba mitungi ya gesi na majiko yake ili nikawapatie wanawake wajawazito.Nashukuru leo nakabidhi mitungi hii na ndoto yangu imetimia ya kuona tunatafuta ufumbuzi wa kumuondolea adha mama mjamzito ya kwenda mbali kutafuta kuni.”

Aidha ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau wengine waljochangia vifaa mbalimbali kwa ajili ya kusaidia watoto njiti lakini kwa upekee anatoa shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amempatia Sh.milioni 20 kufanikisha maadhimisho hayo pamoja na Sh.milioni 50 kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali