Thursday, August 31, 2023

BENKI YA CRDB YAJA NA HATIFUNGANI YA KIJANI

Na Selemani Msuya 

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ametoa rai kwa wananchi, kampuni za sekta binafsi na umma, taasisi za serikali kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza katika hatifungani ya kijani au “Green Bond” ya Benki ya CRDB.

Profesa Kitila ametoa raia hiyo leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Hatifungani ya Kijani uliofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu wa kada mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.

Amesema uamuzi wa Benki ya CRDB kuja na hatifungani hiyo ya kijani na kutoa fursa kwa wananchi na taasisi mbalimbali kununua hisa na fedha zitakazopatikana kuelekezwa kwenye miradi ya mazingira ni wa kuigwa na taasisi nyingine kwani unaenda kusaidia serikali kutekeleza miradi mingi.

Kitila amesema serikali ina mipango mingi ya kuhakikisha miradi ya kuzuia uharibifu wa mazingira unaosababishwa mabadiliko ya tabianchi kutokea, hivyo ujio wa Kijani Bond ni wazi kuwa lengo hilo litaweza kutumia.

"Kijani Bond inaenda kugusa miradi ya mazingira, afya, elimu, maji na mingine mingi, hivyo nichukue nafasi hizi kuziomba taasisi zingine za kifedha na zisizo za kifedha kuunga mkono juhudi hizo za CRDB," amesema.

Waziri huyo amesema ujio wa hatifungani hiyo ya kijani sio tu kwamba unanufaisha miradi tajwa, ila hata wawekezaji wenyewe ambapo benki imeweka bayana kuwa itatoa riba ya zaidi ya asilimia 10.2 kwa kila mwekezaji ambaye atawekeza kuanzia shilingi 500,000 ndani ya siku 37 kuanzia leo.

Amesema Serikali itatoa ushirikiano na taasisi yoyote ambayo itajikita kwenye uwekezaji ambao unagusa jamii, kwa kuwa lengo lake ni kuongeza ajira na kipato kwa wananchi na nchi kwa ujumla.

"CRDB inafanya kile ambacho sisi tunakipigania kuongeza ajira, kipato na kuitangaza nchi, leo hii wapo hadi Burundi, DR Congo na hili la hatifungani ya kijani linaenda kugusa dunia kwa ujumla," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Mkuu wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema fedha ambazo zitapatikana kupitia hatifungani ya kijani zitatumika kufanikisha miradi yenye mrengo wa kuhifadhi mazingira hali ambayo itaifanya Tanzania iendane na mikakati ya dunia ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

"Agosti 18, 2023 ilikuwa siku moja ya siku za furaha sana kwa Benki ya CRDB baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kutupa idhini ya kuuza hatifungani ya kwanza ya kijani Tanzania na kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Lakini naweza kusema leo tupo katika kilele cha furaha kwa kuwa sasa tunakwenda kuaza kuunza hatifungani za kijani nawaomba Watanzania na wasio watanzania kuchangamkia fursa hii," amesema.

Nsekela amesema kamilika kwa mchakato huu ulioanza mapema mwaka jana ni mafanikio makubwa kwao kwani wataalamu wao wa ndani na nje ya Benki yetu walilazimika kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha taratibu za kikanuni na kisheria.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema jitihada hizi zisingefaa kitu kama si ushirikiano ambao tulipata kutoka CMSA ambao hawakuchoka kuwapa miongozo mpaka leo hii wanaanza kuiuza hatifungani yao.

"Kufanikiwa kuanza kuuza hatifungani hii kubwa zaidi kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni heshima kwa nchi yetu kwa kuwa Benki ya CRDB ni benki ya kizalendo inayomilikwa na Mtanzania mmoja mmoja, Serikali pamoja na taasisi zake. Na hili linaendelea kudhihirisha kuwa taasisi zetu zina uwezo wa kufanya mambo makubwa katika ulingo wa kimataifa,"amesisitiza.

Nsekela amesema msukumo wa benki hiyo kuuza hatifungani ya kijani umejikita katika ushiriki wao wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambayo yameleta athari duniani kote.

"Kwa kutambua umuhimu na mahitaji yaliyopo, Benki ya CRDB iliona ni muhimu kutafuta vyanzo vipya vya fedha ili kuwezesha miradi hii ndipo lilipopatikana wazo la hatifungani ya kijani.

Hatifungani hii ambayo CMSA imetupa idhini ya kuiuza ina thamani ya dola milioni 300 za Marekani sawa na takribani shilingi bilioni 780 za Tanzania ambayo kama nilivyosema awali hii ni kubwa zaidi kuwahi kutolewa katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara," amesema.

Amesema hatifungani hii itakayoorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Soko la Hisa London yaani London Stock Exchange (LSE), wanatarajia kuiuza kwa awamu na katika awamu hii ya kwanza mauzo yanaanza leo, Agosti 31, 2023 na yatadumu kwa siku 37 mpaka Septemba 6 na matarajio ni kukusanya Shilingi Bilioni 55.

Nsekela amesema kufanikiwa kuuzwa kwa hatifungani hiyo kutakwenda kuiongezea uwezo mkubwa Benki  kuwezesha wawekezaji ambao miradi yao katika namna moja au nyingine inasaidia katika utunzaji wa mazingira.

Amesema hili ni eneo ambalo wameshuhudia mataifa mengi duniani yanawekeza huko ambapo hapa Afrika tayari nchi kama Afrika Kusini, Ghana, Nigeria na Kenya tayari wamepiga hatua kubwa.

Akizungumzia umuhimu wa Watanzania kuwekeza katika hatifungani ya kijani Nsekela amesema ambapo kiwango cha chini ni shilingi 500,000.

"Sambamba na hilo, hatifungani hii ya kijani ni uwekezaji ambao una uhakika wa kukulipa au kwa lugha ya kigeni wanasema “risk free investment”. Kupitia uwekezaji wa hatifungani ya kijani ya Benki ya CRDB, muwekezaji atakua na uhakika wa kupata riba ya asilimia 10.25 ambayo ni biashara chache sana ambazo unaweza kuzifanya na ukawa na uhakika wa kupata kiasi hiki tena bila kujali mazingira ya biashara yatakuaje," amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB, Alhaj Ali Lawi amesema benki hiyo itaendelea kuboresha huduma zake, ili kuhakikisha kila anayepata huduma ananufaika.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama amesema kinachofanywa na CRDB ni cha kuigwa na kila taasisi ya kifedha kwani kina faida kwa jamii kwa ujumla.

Mkama amesema ili Tanzania iweze kuendelea ni jukumu la kila taasisi kuja na bunifu mbalimbali za kuwezesha jamii nzima inashiriki kwenye uchumi.

"CMSA tupo tayari kushirikiana na taasisi yoyote ambayo itakuja na wazo ambalo linataka kuwakwamua wananchi na nchi kwa ujumla, CRDB imeonesha njia tuiunge mkono benki yetu kwa kununua hisa za hatifungani ya kijani,"amesema.

Monday, August 28, 2023

MSD KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA VIWANGO VYA KIMATAIFA

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa  (MSD), Mavere Tukai

.........................................................


Na Mwandishi wetu- Dodoma 

 

BOHARI ya Dawa (MSD) imewahakikishia wananchi huduma bora   zinazokidhi  viwango vya Kimataifa kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utendaji wake.

Akieleza hatua hizo  Agosti 24, 2023 jijini Dodoma wakati wa mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO), Mkurugenzi Mkuu wa Bohari hiyo Bw. Mavere Tukai amesema, MSD inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa maghala  ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya katika mikoa  mitano ikiwemo  Dodoma na Mtwara ambapo mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi.

“Mradi huu hapa jijini Dodoma na kule mkoani Mtwara inagharimu shilingi Bilioni 39 ikiwa ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa maghala matano tuliyopanga kujenga katika Ofisi za Kanda katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha huduma zetu kwa kuzisogeza zaidi kwa wananchi, kupanua uwezo wa miundombinu yetu hali itakayopunguza umbali wa kufuata bidhaa za afya Dar es Salaam”, amesisitiza Bw. Tukai.

Akieleza zaidi, Bw.Tukai  amesema, maghala hayo yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kutoa huduma kama ilivyo ghala la Dar es Salaam, hivyo uwekezaji huu utakuwa na faida nyingi ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji, kusogeza zaidi huduma kwa wananchi, kupunguza muda wa kufikisha bidhaa za afya kwa watoa huduma, kuwepo kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA na kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa za afya kwa kuzingatia viwango vya kimatifa.

Sanjari na faida za uwekezaji huo, Bw. Tukai ameongeza kuwa, MSD imejipanga kujiendesha kibiashara hivyo kutimiza azma ya kunzishwa kwake kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuzalisha faida itakayosaidia kuimarisha zaidi huduma zake kwa wananchi.

“Hatua hizi zitaenda sambamba na kujiimarisha katika utoaji wa huduma Kimataifa hasa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo tuna jukumu la kuzihudumia”, alisisitiza Bw. Tukai.

Aidha, Bw. Tukai amesema kuwa MSD imechukua hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija.

Ujenzi wa Maghala yote matano utakapokamilika unakadiriwa  kugharimu Serikali kati ya Shilingi Bilioni 90 hadi 95 za Kitanzania hali itakayoiwezesha MSD kuimarisha zaidi utendaji wake  kwa kutumia mifumo ya kisasa zaidi katika utoaji wa huduma zake..


Sunday, August 27, 2023

LATRA YAIAHIDI KAMATI YA BUNGE KUBORESHA SHUGHULI ZA USAFIRISHAJI, YATOZA FAINI MABASI SH. MIL.1, 250,000/-

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo.

........................................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

 

MKURUGENZI Mkuu  Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo, ameihakikishia Kamati ya Bunge ya Miundombinu kuwa mamlaka hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kikamilifu kwa kuboresha shughuli za usafirishaji nchini na kuwapima madereva ili waendeshe vyombo vya moto kwa usalama zaidi.

Suluo aliyasema hayo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Miraji Mtaturu, kuipongeza LATRA kwa kusimamia mfumo utoaji wa tiketi kwa mtandao ambao umeanza kupunguza kero kwa abiria.

'' Tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa ukamilifu na kuufanyia kazi ushauri uliotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa lengo la kuboresha shughuli za usafirishaji ikiwemo kuendelea kuwatahini madereva ili kuhakikisha abiria wanasafiri kwa usalama,''. alisema Suluo wakati akiwasilisha taarifa ya mamlaka hiyo kwa wabunge wa kamati hiyo Agosti 25, 2023. 

LATRA katika kuhakikisha inadhibiti mawakala wa mabasi wanaokwepa kukata tiketi kwa mfumo wa mtandao,  LATRA Mkoa wa Singida juzi iliyatoza faini ya Sh. 250,000 kila basi kwa mabasi matano na kuvuna jumla ya Sh. 1, 250,000.

Mabasi yaliyotozwa faini hizo ni ya Kampuni ya Nyahunge mabasi manne na basi moja la kampuni ya Supafeo ambapo mabasi hayo yalikumbana na adhabu hiyo kutokana na  kuwakatia abiria tiketi za zamani ambazo sio za kielektroniki  zilizopigwa marufuku.

Hatua ya LATRA Mkoa wa Singida  kuyatoza faini mabasi hayo ilikuja baada ya mmoja wa wasafiri waliokuwa ndani ya mabasi hayo kutoa taarifa kwa Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa kuwepo kwa abiria waliokatiwa tiketi ambazo sio za kielektroniki.

Baada ya Dafa kupewa taarifa hizo, alimtuma Afisa wake aitwaye Kilua Mbezi kuyafutilia  mabasi hayo Stendi Kuu ya Mabasi Mkoa wa Singida ya Misuna na kubaini kosa hilo na kuyatoza faini.

Abiria waliokuwemo kwenye moja ya mabasi hayo walimpongeza Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida kwa kulifanyia kazi suala hilo kwa haraka na waliomba kuendelea na moto huo wa kazi hasa pale wanapopata taarifa kutoka kwa abiria na kuchukua hatua kwa haraka kama walivyofanya kwani mara nyingi katika maeneo mengine maafisa hao huwa hawafiki eneo la tukio jambo linalowakatisha tamaa na kuendelea kukithiri kwa vitendo hivyo. 

Afisa wa LATRA Mkoa wa Singida Kilua Mbezi baada ya kuyatoza faini mabasi hayo alitoa elimu kwa abiria kuhusu umuhimu na faida ya kupatiwa tiketi za mtandao na kuwa kabla ya kupanda gari nilazima wapatiwe tiketi hizo na kama watawakatalia na kuwapa za zamani ambazo zimepigwa marufuku watoe taarifa kwa kupiga namba ya bure 0800110020.

Mbezi pia aliwakumbusha wafanyakazi wa mabasi hayo kuendelea kufuata sheria za usafirishaji ili kuepuka adhabu mara watakapobainika kutenda makosa na kuwa jambo hilo lipo ndani ya uwezo wao na kuwa wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kutoa elimu hiyo. 

Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Miraji Mtaturu akizungumzia baadhi ya faida za mfumo wa ukataji wa tiketi kimtandao (Kielektroniki)  alisema ni pamoja na kupunguza mianya ya uvujaji wa mapato kwani abiria ana uhuru wa kukata tiketi basi analolitaka na  mmiliki wa basi anaona idadi ya siti zilizokatwa tofauti na zamani na kuwa faida hizo zipo kwa wahusika wote, abiria, wafanyakazi wa mabasi hayo  mmiliki na Serikali.

Tunawapongeza sana LATRA sababu kupitia mfumo wa tiketi mtandao abiria anaweza kukata tiketi akiwa popote bila kulanguliwa na mawakala , lakini pia mfumo huu umerahisisha ukusanyaji wa mapato kwa wamiliki na Serikali sababu unaweza kuona idadi za tiketi moja kwa moja kupitia mfumo,’’ alisema Mtaturu.

Mara baada ya mfumo wa Tiketi Mtandao kuanza kufanya kazi rasmi Julai 1, 2022, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) ilifanya mkutano na wadau wa usafirishaji kutathmini utekelezaji wa mfumo huo na kujadili changamoto zinazojitokeza ili kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na ukataji wa tiketi kimtandao.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Miraji Mtaturu akiipongeza Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kwa kusimamia Mfumo wa Tiketi Mtandao kwani umepunguza kero kwa abiria wa usafiri wa ardhini nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Habib Suluo. akizungumza katika kikao kazi na mmoja wa maafisa wa jeshi la Polisi kuhusu masuala ya usafirishaji.

 Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Singida, Layla Dafa, akizungumza katika moja ya mikutano na wananchi, Iguguno  wilayani Mkalama mkoani hapa kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na LATRA.

Tuesday, August 22, 2023

KAMPUNI YA JOSTANO TRANS KINARA SEKTA YA USAFIRISHAJI NCHINI

Mabasi ya Kampuni ya Jostano and General Supplises Limited yakiwa Stendi ya Mabasi ya Mkoa wa Singida Misuna tayari kwa safari zake.

..................................................................................


Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

KAMPUNI ya Jostano and General Supplises Limited licha ya kuanza kufanya kazi  hivi karibuni imekuwa kinara katika sekta ya usafirishaji hapa nchini hususani katika Mikoa ya Singida, Manyara, Morogoro, Dar es Salaam, Dodoma na Mbeya.

Licha ya kuwa na miaka miwili katika sekta hiyo tangu ianze kufanya kazi zake mwaka 2021 kampuni hiyo imejizolea umaarufu mkubwa kutokana na utoaji wa huduma zake kwa viwango vya hali ya  juu na kuwa kimbilio la abiria wengi.

Mfanyabiashara Margaret Ntandu ambaye anasafirisha mchele kati ya Mkoa wa Tabora kupitia Singida anasema amekuwa akisafirisha bidhaa hiyo kupitia mabasi ya kampuni hiyo na haja wahi kupata changamoto yoyote.

'' Nimekuwa nikisafirisha mizigo yangu kutoka Singida kwenda Dodoma sijawahi kupata changamoto ya aina yoyote iwe ya kupotea mzigo na nyingine na hata bei zao ni rafiki ukilinganisha na mabasi ya kampuni zingine,'' alisema Ntandu.

Edina Alex ambaye ni mfanyabiashara wa vitenge anayevitoa Tunduma na kuvipeleka Singida anasema mabasi ya kampuni hiyo ndiyo anayopanda wakati akifuata bidhaa zake hizo na kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wamekuwa na lugha nzuri kwa abiria.

Alex anasema tangu kampuni hiyo ianze kufanya safari zake Mkoa wa Mbeya anatumia mabasi ya kampuni hiyo na akaupongeza uongozi kwa kusimamia vizuri utendaji kazi wa wafanyakazi ambao umewapa mafanikio hayo kwa kipindi kifupi tangu waingie kwenye sekta hiyo.

'' Niwaombe viongozi wa kampuni hii waendelee kuwa wabunifu kwa kujifunza zaidi kutoka kwa makampuni yenye uzoefu naamini ndani ya miaka miwili ijayo Jostano Trans watakuwa wabobezi wakubwa kwenye sekta hii kwani wameanza vizuri,'' alisema Alex.

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ] UDSM }, Amina Seif ambaye alisafiri na basi la kampuni hiyo kutoka Singida kwenda Dar es Salaam alisema muda wanaoambiwa kufika Dar es Salaam kutoka Singida unakuwa ni uleule wa saa 11 na nusu jioni tofauti na mabasi mengine ambayo yanafika kuanzia saa 12 jioni hadi saa mbili na kuendelea.

''Abiria waliowengi hawapendi longolongo wanapenda kufika muda uleule walioambiwa labda tu ziwepochangamoto za kuharibika kwa gari lakini za kukamatwa na trafiki zinaweza kuepukika kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani kama za mwendo kasi, uchakavu wa gari na matairi,'' alisema Seif.

Alisema lugha nzuri wakati wa utoaji huduma kwa abiria ni jambo lingine ambalo limemfanya avutike na kusafiri kwa kutumia mabasi hayo na utaratibu wa kuomba dua wakati wa kuanza safari na baada ya kufika.

Wakala wa mabasi katika Stendi Kuu ya Mabasi Mkoa wa Singida aliyejitambulisha kwa jina la Awadhi Sendoro  alisema amefanya kazi hiyo kwa muda mrefu katika stendi hiyo na kueleza kuwa kampuni hiyo kwa muda mfupi tangu ianze kufanya kazi imekuwa na wateja wengi.

'' Mimi sio wakala wa mabasi hayo lakini kutokana na watu wengi kuwa na namba zangu wamekuwa wakinipigia simu niwashikie nafasi katika mabasi hayo na nimekuwa nikifanya hivyo,'' alisema Sendoro.

Alisema abiria wengi wamekuwa wakipenda kusafiri na magari hayo kwa sababu ya huduma nzuri wanazozipata na kufika muda wanaoambiwa na mwendo mzuri wa mabasi hayo.

Katibu Mkuu Kiongozi wa Kampuni hiyo hiyo, Elias Meko alisema mafanikio hayo waliyoyapata kwa muda mfupi yanatokana na ushirikiano baaina ya viongozi wa kampuni hiyo pamoja na wafanyakazi ambao wakati wote ndio wanaokuwa na abiria.

'' Tumekuwa tukikutana na wafanyakazi wetu wa kada zote wakiwemo makondakta na madereva na kufanyanao vikao kazi kwa ajili ya kukumbushana majukumu ambayo matunda yake ndiyo mafanikio haya yanayoonekana kwa abiria tunao wahudumia,'' alisema Meko. 

Alisema kampuni hiyo ilianza rasmi kufanya kazi zake mwaka 2021 kati ya Singida na Babati Manyara na baadae Singida, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam.

Meko alisema hivi sasa wameanzisha safari ya kutoka Singida kwenda Mbeya na kuwa kampuni yao hivi sasa imekuwa bora na kimbilio kwa wananchi wanaosafiri kwa mabasi yao.

Alisema licha ya kuwepo na ushindani wa kibiashara hali sio mbaya hasa ukizingatia kuwa hawana muda mrefu tangu waingie kwenye sekta hiyo na amewaomba wananchi kuendelea kuwaamini na kuwaunga mkono zaidi na wao wataendelea kuwapa ushirikiano lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha sekta ya usafirishaji inakua na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katibu Mkuu huyo Kiongozi alisema wamekuwa na safari zao kila siku kutoka Singida kwenda Dares Salaam, Dar es Salaam kwenda Singida, Singida kwenda Mbeya na Mbeya kwenda Singida na kuwa tiketi zao zinapatikana kwa njia ya mtandao www.jostano.co.tz na www.busbora.co.tz.

Alisema namna ya kununua tiketi zao kwa njia ya mtandao hatua ya kwanza ni tembelea www.jostano.co.tz au pakua BUSBORA APP kutoka google play Store busbora.co.tz.

Alitaja hatua ya pili ni kuchagua unapotoka na unapotaka kwenda na tarehe ya safari kisha 'TAFUTA'

Meko alitaja hatua ya tatu kuwa Chagua Bus la Jostano Trans kisha '' ONYESHA SITI''  chagua siti uipendayo, chagua kituo cha kushukia na kupandia. Jaza majina kamili, namba ya simu, jinsi kisha endelea.

Alitaja hatua ya nne ni hakikisha taarifa za safari yako na kisha ENDELEA NA MALIPO.

Alitaja hatua ya tano kuwa ni chagua mtandao wa malipo kisha fuata maelekezo yanayojitokjeza kulipia.

Alitaja hatua ya mwisho kuwa mara baada ya malipo utapokea ujumbe wenye uthibitisho wa tiketi na utaweza kupakua nakala ya tiketi katika kifaa chako.

Meko alisema vitu vya kuzingatia kuwa ni vigezo na masharti vilivyowekwa ni nauli iliyowekwa kwenye tiketi haibadilishwi, kuzingatia muda wa safari na abiria afike kwenye kituo cha kupandia bus kabla ya nusu, mzigo wa ziada utakaozidi kilo 20 utatozwa nauli,  mzigo wa mkononi wa abiria sio dhamana yao, abiria akisitisha safari atoe taarifa saa 12 kabla ya safari na atakatwa asilimia 15 ya nauli aliyolipa.

Alitaja vigezo na masharti mengine kuwa ni iwapo abiria atasitisha safari pasipo kutoa taarifa au kuachwa na basi kwa kuchelewa  kufika kituo cha kupanda nauli haitarudishwa.

Alisema viongozi wa kampuni hiyo wapo tayari wakati wote kupokea maoni mbalimbali wanayoletewa na wasafiri wao na kuyafanyia kazi mara moja ikiwa ni ni moja ya njia ya kuboresha huduma zao.

Alisema kila penye mafanikio hapakosi kuwa na changamoto za hapa na pale hivyo aliwaomba wateja wao kuendelea kuwaamini na kwa changamoto zilizojitokeza wakati wa safari zao wanaomba wawasamehe,

Pia Meko ameendelea kuwahimiza wateja wao kukata tiketi kwenye ofisi zao  au kwa njia ya mtandao jambo litakalosaidia kuondoa changamoto za kuzidishiwa nauli na kutapeliwa,

Katika hatua nyingine Meko amesema kampuni hiyo itakuwa na uchoyo wa fadhira iwapo itashindwa kumshuru na kuthamini mchango wa Kampuni ya mabasi ya Happy Nation katika mchango mkubwa wa ukuaji wa kampuni yao ya Jostano Trans na kuwa wanashirikiana viziri na Mkurugenzi wa kampuni hiyo ndugu Issa ambaye amekuwa hachoki kushiriukiana nao katika kila jambo la kuboresha utendaji kazi ambao umewaletea mafanikio hayo.  

Aidha, alitaja namba za mawakala wao kuwa ni 0683-712030 Makao Makuu Dar es Salaam, 0765-290928 Singida, 0786-292792 na 0759-500010 Dar es Salaam, 0785-776402 Dodoma , 0655-900909 Morogoro na Mbeya ni 0752-397910.

Wafanyakazi wa  Basi namba T 133 DEA wakiwa mbele ya basi hilo tayari kwa safari ya Dar es Salaam kwenda Singida.Kushoto ni Dereva Hamad Athuman na kulia ni Kondakta Martha William.
Abiria wakiingia katika basi Stendi kuu ya mabasi Singida.
Wafanyakazi wa mabasi hayo wakiwa mbele ya moja ya mabasi hayo kabla ya kuanza safari. Kuitoka kushoto ni Kondakta wa mabasi hayo Martha William, Msimamizi wa Usalama na haki za abiria upande wa Dar es Salaam,  Ally Atuman na kulia ni  Ofisa Mwandamizi wa Ofisi ya kampuni hiyo Makao Makuu Dar es Salaam, Vanessa Samwel.
Basi la kampuni hiyo linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Singida likiwa safarini. 

Saturday, August 19, 2023

RAIS DK.SAMIA SULUHU HASSAN AIPA TANO MSD KWA UFANISI WA KAZI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Dk.Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye ufunguzi wa Kikao Kazi kwa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Jukwaa la Wakuu wa Taasisi za Umma, kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa AICC Jijini Arusha tarehe 19 Agosti, 2023.

..................................................

 Na Mwandishi Wetu, Arusha

RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameridhishwa na mabadiliko yanayoendelea Bohari ya Dawa ( MSD) na kuwataka waendeleee kuchapa kazi.

Rais Samia amesema hayo  Jumamosi Agosti 19, 2023 jijini Arusha wakati akifungua kikao kazi cha wenyeviti wa bodi na taasisi za umma.

Rais Dk.Samia akiwa amemsimamisha Mkurugenzi wa MSD, Mavere Tukai alisema taasisi hiyo ni kati ya mashirika yaliyo badilika na matumaini yake itakwenda kufanya vizuri hasa katika mfumo wa  uuzaji wa Dawa Afrika kwa kuwa na soko kubwa hususani kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC).


Wednesday, August 16, 2023

MSD YATAKIWA KUONGEZA SPIDI YA USAMBAZAJI WA BIDHAA ZA DAWA

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu  akijibu maswali ya Wajumbe wa Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI  wakati kamati hiyo ilipokuwa ikipokea taarifa ya usambazaji wa bidhaa za Afya kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai katika kikao cha Kamati kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma. jana.

.....................................................

Na WAF, Dodoma

 

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI imeitaka Bohari ya Dawa (MSD) nchini kuongeza kasi ya usambazaji wa bidhaa za Dawa pamoja na kuwa na maghala ya dawa katika kila Halmashauri.

Wito huo umetolewa leo Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya usambazaji wa bidhaa za Afya kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai katika kikao cha Kamati kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

“Kwanza naipongeza sana Wizara kwa hatua mnazoendelea kuchukua za kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za Dawa na vifaa tiba inaongezeka lakini pia niwatake muongeze jitihada hizo kwakuwa uhitaji wa bidhaa hizo ni mkubwa nchini”, ameeleza Mhe. Nyongo

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akijibu maswali ya Wajumbe wa kamati hiyo amesema Serikali imewapa mtaji Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuhakikisha Dawa na vifaa tiba zinapatikana kwa wakati na kusambazwa nchini.

“Tumepokea mapendekezo yote ya kamati, Serikali tutahakikisha tunaiwezesha MSD ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na kuwafutia madeni waliyonayo”, amesema Waziri Ummy

Pia, Waziri Ummy ameitaka MSD kujipima katika upatikanaji wa Dawa, Vifaa tiba pamoja na vitendanishi kwenye huduma za Afya ngazi ya msingi.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai wakati akiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo amesema usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupitia Mfumo wa Ugavi Shirikishi umefanikiwa kwa asilimia 97.

Pia, amesema kwa Mwaka wa fedha 2022/23, Bohari ya Dawa ilianza usambazaji wa bidhaa za afya mara Sita kwa mwaka badala ya mara Nne kama ilivyokuwa awali.

“Lengo la usambazaji huu ni kupunguzia vituo vya kutolea huduma za afya muda wa kusubiri bidhaa hivyo kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za Afya nchini”, ameeleza Bw. Mavere.

Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.
 Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Mavere Tukai akiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Taarifa ya usambazaji wa bidhaa za afya ikitolewa.
 

SHILINGI BILIONI 5 ZATENGWA NA MFUKO WA KUWAWEZESHA WASANII NA WAIGIZAJI MKOANI MBEYA

 Afisa Utamaduni Mkoa wa Mbeya Victoria Shao akizungumza katika kikao maalumu kilichowahusisha Wasanii, Waigizaji na waimbaji kilicho andaliwa na Wizara ya Utamadunim Sanaa na Michezo.

............................................................

Na Mwandishi Wetu Mbeya

 

KIASI cha Shilingi Bilioni 5 kimetengwa na mfuko wa wizara ya sanaa na utamaduni ili kuwawezesha wasanii na waigizaji wa "Bongo Movie" wa mkoa wa Mbeya.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowahusisha Wasanii, Waigizaji na waimbaji wa mkoa wa Mbeya na Songwe Afisa Mtendaji Mkuu [CEO] wa mfuko huo Nyakaho Mahemba amesema Wizara imeanza kutoa fedha hizo kwa wasanii kuanzia Desemba 2022 ambapo  imelenga kukuza na kuendeleza kazi za wasanii kujiendesha kibiashara badala ya burudani pekee.

Mahemba amesema katika mpango wa serikali ni kuongeza ajira na kuongeza mitaji kwa wasanii kupitia mafunzo na kuongeza ubora  wenye lengo la kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Amefafanua kuwa wasanii wana uwezo wa kukopa mtaji kuanzia Shilingi laki 2 hadi Shilingi Mil 100 ili kufikia malengo na kwamba mfuko wa Utamaduni unashirikiana na mabenki ili kuwezesha mikopo ya Wasanii.

Afisa mtendaji Mkuu huyo ameendelea kusema kuwa tayari imeshatolewa mikopo kwa awamu mbili, mwezi Desemba 2022 na mkopo wa pili umetolewa Mwezi Februari ambapo tayari  jumla ya Shilingi Bil 1.077 kwa miradi 45 na hivyo kuzalisha ajira 88,750.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni wa mkoa wa Victoria Shao amesema mikopo hiyo ya wasanii itachangia ajira na kuwasaidia kuwainua kiuchumi ambapo wasanii,waimbaji,wabunifu wa kazi za mikono,Waandishi wa kazi za kifasihi na wachoraji wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

Shao amesema serikali itakuwa karibu na wasanii kwa maelekezo na elimu ya mikopo ili waweze kukopa kurejesha ili iweze kuwanufaisha wasanii wengine.

 Afisa Mtendaji Mkuu [CEO] wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Nyakaho Mahemba akitoa taarifa ya mfuko huo kwenye kikao hicho.

Wasanii wa Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye kikao hicho
Wasanii wa Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye kikao hicho
Wasanii wa Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye kikao hicho
Picha ya pamoja.

Picha ya pamoja

Tuesday, August 8, 2023

WANANCHI WAFURIKA BANDA LA TARI, KUJIFUNZA TEKNOLOJIA ZA KILIMO MAONYESHO YA NANENANE NGONGO LINDI

 Wananchi wakiwa wamefurika katika Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kwenye Maonyesho ya Nanenane 2023 yanayofikia tamati leo Agosti 8, 2023 viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

........................................................... 

Na Dotto Mwaibale, Lindi 

WANANCHI kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wakiwa wamefurika katika Banda la Taasisi ya Utafiti kwa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele mkoani Mtwara kwenye Maonyesho ya Nanenane 2023 Kanda ya Kusini yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo.

Katika Maonesho hayo watafiti wa kilimo wa TARI wanaonesha na kutoa elimu za teknolojia za kilimo za kuvutia jambo lililosababisha banda hilo kufurika wakulima na wananchi kwa lengo la kujifunza.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga kuhusu maonesho hayo Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano alitaja baadhi ya teknolojia  ambazo zinaoneshwa na kutolewa kwa wakulima ni za mazao ya korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi, mahindi na uwele.

Kidunda alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wakulima kuwa katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu bali  wameweka teknolojia ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu,  shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa magonjwa na uvunaji wake.

          Mkulima Mathayo Milanzi kutoka Wilaya ya Nanyumbu alisena amevutiwa na teknolojia zinazofundishwa na TARI na kuwa moja ya teknolojia hizo ni kilimo cha ndizi aina ya Mtwike ambapo awali alipokuwa akilima kwa kutumia kilimo cha mazoea alikuwa akipata mazao kiduchu.

"Zamani ndizi nilizokuwa nikivuna nilikuwa nikizibeba kichwani lakini baada ya kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa nimekuwa nikivuna ndizi nyingi hadi nalazimika kukodi pikipiki kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda kwenye soko," alisema Milanzi.

Milanzi alisema TARI wamekuwa mkombozi kwa wakulima wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kuwafanya kukielewa kilimo chenye tija.

Mkulima mwingine, kutoka Kijiji cha Chemchem Wilaya na Nachingwea, Issa Bakari amesema TARI imekuwa mkombozi kwa wakulima wengi katika kandahiyo kwani imesabisha uzalishaji wa  mazo yao kuongezeka hususani maeneo ya vijijini.

Mimi natoka Kijiji cha Chemchem wilayani Nachingwea mkoani Lindi nimekuja mahususi katika Banda la TARI ili niongeze uzoefu kutoka kwa wataalam wabobezi ambao wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwetu hasa sisi wakulima wa vijijini,” alisema Bakari.


Mtafiti wa mbegu bora za korosho kutoka TARI Naliendele, Joackim Madeni (kushoto) akitoa elimu kwa mkulima kutoka Wilaya ya Nachingwea ambaye alitembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele katika Maonyesho ya Wakulima Nanenane ambayo yanafikia tamati leo katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Mtafiti wa mbegu bora ya mihogo, Ndwasi Gambo (kushoto) akiwaelekeza wananchi kuhusu kilimo chenye tija za zao hilo.


Muonekano wa mikorosho kwenye maonyesho hayo

Mtafiti Msaidizi wa zao la Karanga na alizeti, Said Ally, akielekeza kuhusu kilimo cha zao hilo.

Mtafiti Msaidizi na Msimamizi wa Kituo Kidogo cha Manyoni mkoani Singida, Eunice Kachungwa (wa pili kushoto), akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la TARI. Kulia ni Mtafiti Msaidizi wa zao la korosho, Nora Manfield.
Mtafiti Msaidizi wa zao la korosho,  Kelvin Kawonga (kulia) akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la TARI kwenye Maonyesho hayo.
Mtafiti wa mbegu bora ya mihogo, Ndwasi Gambo (wa pili kulia) akiwaelekeza wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Mtwara kuhusu kilimo chenye tija za zao hilo. Kulia ni Mtafiti wa zao hilo, Benedetha Kimata kutoka TARI Naliendele.


Wananchi wakipata maelezo ya kilimo bora cha zao la ufuta.
Mtafiti wa Hali ya Udongo na Agronomia ya korosho, Zawadi Kilingala, akielezea kuhusu kilimo hicho.
Mtafiti Msaidizi wa zao la korosho, Dantish Leonard (kulia) akielezea kilimo hicho.
Muonekano wa shamba la ufuta kwenye maonesho hayo.
Muonekano wa shamba la alizeti kwenye maonesho hayo
Muonekano wa shamba la Mtama kwenye maonesho hayo.
Mtafiti wa zao la Korosho, Kasiga Ngiha (kulia) akiwaelekeza wakulima kutoka Wilaya ya Nachingwea, Joackim Lihundi (kushoto) na Bakari Pilipili (katikati) kuhusu mbegu bora za zao hilo.
Muonekano wa kitalu cha mbegu bora za korosho.
Wananchi wakiwa ndani ya banda la TARI Naliendele kwenye maonesho hayo.
 

Saturday, August 5, 2023

DC LINDI AWATAKA WASANII KUCHANGAMKIA BILIONI 20 ZA MFUKO WA UTAMADUNI ZILIZOTOLEWA NA RAIS

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga akizungumza wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo  wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mkoani humo jana.

............................................

Na Dotto Mwaibale, Lindi 

WASANII mkoani Lindi wametakiwa kuchangamkia fedha Sh.Bilioni 20 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kama ruzuku za kuwawezesha kukopa ili kuwasaidia kuinua vipato vyao kupitia kazi zao za sanaa.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo  wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

"Hizi fedha zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili yenu hivyo changamkieni fursa hiyo kwa kuboreha shughuli zenu ili muweze kujikwamua kiuchumi," alisema Ndemanga.

Alisema wadau wa Sanaa watakaokidhi vigezo vilivyoweka ndio watakaokopeshwa fedha hizo kupitia mfuko ulioanzishwa na Rais Samia ambapo aliwahimiza wasanii hao kuhakikisha wanakithi vigezo hivyo ili waweze kukopesheka na kuwa fedha hizo sio zawadi bali zinatakiwa kurejeshwa ili ziweze kukopeshwa kwa wengine.

Shahibu aliwataka wasanii hao na wadau wa utamaduni kujiendeleza kielimu ili kwenda na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia huku wakianzisha miradi mbalimbali kama ufugaji,kilimo, na mingine badala ya kutegemea sanaa peke yake.

Aidha, aliwataka wasanii hao  kujenga tabia ya kushirikiana na taasisi zingine wakati wa kufanya shughuli zao jambo ambalo litawaongezea uzoefu wa masuala mengine ya maendele na sanaa kwa ujumla.

Alisema Serikali inatambua mchango wa wasanii na kuwa kwa siku za hivi karibuni imeonekana kazi nyingi za wasanii kama filamu na tamthilia zikioneshwa zaidi na vyombo vya habari vya watu binafsi hivyo watawasiliana na wahusika wa vyombo vya Serikali kuona namna ya kuanza kutumia kazi za wasanii hasa chipukizi katika vyombo hivyo.

"Changamoto kubwa iliyopo ni uzingatiaji wa maadili katika kazi zetu nawaombeni mkawe mabalozi wazuri wa kusimamia maadili ya kitanzania na si vinginevyo na kuacha kutengana kwa sababu ya migogoro yakugombea fedha na sisi kama Serikali hatutakuwa tayari kuona mambo hayo yakitokea," alisema Ndemanga.

Awali akitoa taarifa ya mfuko huo Afisa Mtendaji Mkuu  (CEO) wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tazania Nyakaho Mahemba alisema mfuko huo unatoa huduma katika maeneo ya urithi wa utamaduni , lugha  na fasihi, sanaa  za maonyesho, ufundi , filamu, muziki na fani nyingine  zenye mlengo  wa utamaduni na sanaa kwa watu binafsi, vikundi au makundi.

Alitaja huduma zinazotolewa na mfuko huo kuwa ni mikopo ya uendeshaji  yenye lengo  la kuwezesha  shughuli za  kiutendaji wa kila siku za uzalishaji wa kazi za utamaduni au sanaa.

Alitaja kazi nyingine ni utoaji wa mikopo ya vifaa yenye  lengo la kuwezesha  ununuzi  wa vitendea kazi  vya uzalishaji za utamaduni au sanaa na mikopo ya kujikimu/ dharura ambayo ni mikopo ya muda mfupi inayotolewa kwa lengo la kujikimu wakati  wa safari za kuandaa au kufanikisha  kazi za utamaduni au sanaa.

Alisema lengo la mafunzo ni kuongeza ujuzi na thamani  ya kazi za utamaduni na sanaa ili ziwe na ubora unaoendana na mahitaji ya  soko.

Mahemba alisema kulingana na kuingia makubaliano na Benki ya CRDB  na Serikali kupitia  mfuko huo walengwa wa mfuko watakaohitaji huduma za mikopo  watatakiwa kuwasilisha  maombi yao  kwa njia ya posta, barua pepe au  moja kwa moja katika ofisi za  mfuko huo kwa ajili ya mapitio ya awali ya kitaalamu kisha  maombi hayo kufikishwa katika Benki ya CRDB kwa hatua zao.

Msanii wa ngoma za asili Salum Namtitili akizungumza kwa niaba ya wenzake alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha hizo kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

“Tunaishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wasanii kwani tulikuwa na changamoto kubwa ya kuendeleza sanaa zetu lakini kwa fedha hizi tutasonga mbele kwani tutaweza kutoka sehemo moja kwenda nyingine na kurekodi kazi zetu tofauti na ilivyokuwa zamani tukiangaika kutafuta fedha huku na kule bila ya mafanikio,” alisema Namtitili.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga (katikati) akiwasili Hoteli ya Sea View Hotel and Resort kwa ajili ya kufungua warsha ya kuwajengea uwezo  wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
 Afisa Mtendaji Mkuu  (CEO) wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tazania Nyakaho Mahemba akitoa taarifa ya mfuko huo.
Afisa Utamaduni Mkoa wa Lindi,  Makalaghe Nkinda, akizungumza kwenye warsha hiyo.
Afisa Mwandamizi wa  Mkopo wa Benki ya CRDB kutoka Makao Makuu, Alpha  Mgubila, akizungumza kuhusu mikopo itakayokopeshwa kwa wasanii kupitia benki hiyo.
Mwenyekiti wa Wasanii Mkoa wa Lindi, Athuman Mohamed akizungumza kwenye warsha hiyo.
Msanii wa ngoma za asili, Salum Namtitili, akitoa shukurani kwa Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa warsha hiyo.
Wasanii wakiwa kwenye warsha hiyo.
Viongozi wakiimba wimbo wa kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.

Wasanii wakiimba wimbo wa kumshukuru Rais Samia.
Wasanii wakiwa kwenye warsha hiyo.

 Warsha ikiendelea.


Wasanii wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi