Wednesday, January 31, 2024

Wateja Benki ya CRDB kuzawadiwa zawadi za Sh. Milioni 470 kampeni ya Benki ni SimBanking

 
Dar es Salaam. Tarehe 31 Januari 2024:  Katika jitihada zake za kuhamasisha  matumizi ya mifumo ya kidijitali nchini, Benki ya CRDB imezindua msimu wa tatu wa kampeni ya ‘Benki ni SimBanking’ na kutenga jumla ya zawadi zenye thamani ya Shilingi milioni 470 mamilioni kwa wateja wake mwaka huu.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Wateja wadogo na wakati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul amesema lengo la kampeni hiyo ni kujenga utamaduni wa matumizi ya kidijitali katika huduma za kifedha ili kuendana na kasi ya maendeleo na kuondokana na matumizi ya fedha taslimu.
“Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaihamisha dunia kutoka kwenye miamala ya fedha taslimu kwenda ile isiyohusisha fedha taslimu yaani cashless economy. Tanzania hatupaswi kuachwa nyuma, ni lazima twende na mabadiliko hayo tena kwa kasi inayostahili,” amesema Bonaventure.

Kushiriki na kujiwekea nafasi ya ushindi katika kampeni hiyo mteja anatakiwa kutumia SimBanking kufanya miamala yake yote ya kibenki ikiwamo kulipia ankara za maji, umeme au visimbusi vya television, ada, malipo ya manunuzi, kutuma pesa, kulipia kodi, mikopo ya kidijitali, kutoa fedha kwa ATM au CRDB Wakala, kulipia bima ya vyombo vya moto, na huduma nyenginezo.
“Kwa kadri mteja atakavyokuwa akifanya miamala mingi zaidi ndivyo atakavyojiwekea nafasi ya ushindi,” amesema Bonaventure huku akibainisha kuwa katika kampeni hiyo itakayoenda hadi mwisho wa mwaka, kutakuwa na washindi wa gari aina ya Toyota Dualis watakaopatikana kila baada ya miezi mitatu, huku zawadi za  bajaj na pikipiki zikitolewa kwa mshindi wa kwanza na wa pili kila mwezi.

Aidha, katika msimu huu wa tatu wa kampeni ya ‘Benki ya SimBanking’, Benki ya CRDB imetenga zawadi za kompyuta mpakato kufikia 10 kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu, zawadi za simu janja, pamoja na fedha taslimu.

Pamoja na zawadi hizi Benki hiyo pia imetenga kiasi cha Shilingi milioni 200 zitakazotolewa kupitia Tembo Points ambazo mteja atakuwa akikusanya kila anapofanya muamala. Wateja wataweza kubadili Tembo Points zao kuwa fedha na kuzitumia kulipia huduma au bidhaa.
Bonaventure amewakumbusha wateja wa  Benki ya CRDB ambao hawajakamilisha usajili wa huduma za SimBanking kukamilisha mchakato huo ili wakidhi vigezo vya kujishindia moja kati ya zawadi zilizotangazwa na kuwakaribisha wananchi wengine kufungua akaunti kwa vigezo nafuu sana na kuunganishwa na SimBanking ili kufurahia huduma zilizoboreshwa zaidi.

Benki imeendelea kuiboresha huduma yake ya SimBanking ili kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa na uzoefu ulio bora zaidi kwa wateja.  Mwaka jana, tulizindua SimBanking App iliyoboreshwa ambayo inatumia akili mnemba (Artificial intelligence), ianyoiwezesha kuwa na uwezo mkubwa katika utambuzi wa tabia na mahitaji ya mteja pindi anapotumia.

Mapema mwaka huu Benki ya CRDB imeongeza huduma mbili mpya ndani ya SimBanking ikiwamo  huduma ya malipo kupitia Msimbomilia wa Taifa (TANQR) ikimuwezesha mteja kufanya malipo kwa watoa huduma wote wa Benki ya CRDB na hata mitandao ya simu. Huduma nyengine ni ile ya kujitengenezea Tembo Virtual Card mahsusi kufanikisha miamala ya kieletroniki popote pale duniani kwa kushirikiana na Union Pay.











TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SH.MILIONI 156 ZA MIRADI YA MAENDELEO

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Januari 31, 2024 ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023.

............................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imeokoa zaidi ya Sh.Milioni 156 baada ya kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Januari 31, 2024 ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023 alisema miradi iliyofuatiliwa ilikuwa ni 11 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 5 katika sekta za Elimu na Afya.

Mwanjala alisema miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa Shule za Sekondari za Kutwa na za Kata iliyotekelezwa kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambao unahusisha ujenzi na ukarabati wa Shule za Sekondari na kuwa fedha hizo pia zinahusisha ujenzi wa vituo vya Afya.

"Katika ufuatiliaji huo, fedha kiasi cha Sh. 10,220,000/= ziliokolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika ujenzi wa Kituo cha Afya Gumanga na Ilunda kutokana na milango aina ya flash door iliyokuwa imewekwa awali kukosa ubora uliokuwa unatakiwa kwa mujibu wa BOQ, hivyo kulazimika kuiondoa na kuweka milango aina ya Hard wood doors yenye ubora uliotakiwa kwa mujibu wa BOQ," alisema Mwanjala.

Aidha, Mwanjala alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni fedha kiasi cha fedha Sh. Milioni 110.5 ziliokolewa, kutokana na kufanya malipo ya vifaa vilivyoagizwa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Singida Solya kabla ya Mzabuni huyo kupeleka vifaa hivyo ili vikaguliwe, vikubaliwe na kupokelewa.

Alisema baada ya TAKUKURU kufuatilia, mzabuni huyo alipeleka vifaa vyote vilivyokuwa vimeagizwa.

Mwanjala alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi fedha kiasi cha Sh. 1,100,000/= kiliokolewa kutokana na kodi ya zuio ambayo ilikatwa kwa wazabuni waliotoa huduma katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Iyumbu kwa ajili ya kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini hazikupelekwa na baada ya ufuatiliaji uliofanywa TAKUKURU fedha hizo zimepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Katika kipindi hicho Mwanjala alisema TAKUKURU ilifanya  chambuzi sita za mifumo ili kubaini mianya ya rushwa iliyopo katika maeneo mbalimbali na kisha na kushauri namna ya kuiziba mianya hiyo ambapo pia walifanya fanya warsha tano kujadili mianya ya rushwa iliyobainika katika chambuzi zilizofanyika na kuweka mikakati ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Alisema kutokana na uchambuzi wa mfumo wa ulipaji na ukusanyaji kodi ya zuio uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi,fedha kiasi cha Sh. Milioni 25 kiliokolewa Manyoni na fedha kiasi cha Sh. Milioni 9.9 ziliokolewa Itigi kutokana na kodi ya zuio ambayo ilikatwa na Halmashauri hizo kwa watoa huduma mbalimbali muda mrefu kwa ajili ya kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini hazikupelekwa na baada ya uchambuzi huo fedha hizo zimepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA)

Mwanjala alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida iliendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kufanya vikao 23 katika kata 23 na makundi mbalimbali ya wadau na kuwa kupitia vikao hivyo wadau waliibua kero 102 na kueleza kuwa kati ya kero 102 zilizoibuliwa, kero 79 zimetatuliwa na kero 23 zinaendelea kutatuliwa. 

Akizungumzia kuhusu Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Singida iliwaongezea wananchi uelewa kuhusu rushwa ambapo wananchi 13,601 (wanaume 6,971 na wanawake 6,630) walipata elimu hiyo kupitia Semina 61 kwenye makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Umma, mikutano ya hadhara 53, maonesho 7, Kutembelea na kuimarisha Klabu za Wapinga Rushwa 58 katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo. 

Mwanjala akizungumzia uchunguzi na mashtaka alisema malalamiko 69 yalipokelewa kwa kipindi hicho ambapo malalamiko 34 yalihusu vitendo vya rushwa na malalamiko 35 hayakuhusu vitendo vya rushwa.

"Malalamiko 34 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali, malalamiko 35 ambayo hayakuhusu rushwa walalamikaji walishauriwa kadiri malalamiko yenyewe yalivyokuwa yakiendelea," alisema Mwanjala.

Alisema katika kipindi cha miezi hiyo kesi 10 zilifunguliwa mahakamani, kesi 7 ziliamuliwa, kesi 3 zilishinda na kesi 4 zilishindwa na jumla ya kesi 27 zinaendelea Mahakamani.

Akielezea mikakati ya TAKUKURU Mkoa wa Singida ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024 wataendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wataendelea kuwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa ili wananchi washiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo vya Rushwahasa katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao na kuendelea kutekeleza Programu ya TAKUKURU – Rafiki. 

Mwanjala alitoa wito kuwa TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa RAI kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo hivyo vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii na hasa katika utekeleaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Alisema kwa taarifa ya vitendo vya rushwa wasiliana nao kwa njia zifuatazo:

i. Fika Ofisi za TAKUKURU (M) Singida na Wilaya za Iramba, Ikungi, Mkalama na Manyoni.

ii. Kupiga simu ya bure 113 au simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa na Wakuu wa TAKUKURU wa Wilaya kwa namba zifuatazo:

Na Mkoa /Wilaya NAMBA YA SIMU

1 RBC –SINGIDA 0738150208

2 DBC - Mkalama 0738150 212

3 DBC - Ikungi 0738150213

4 DBC - Iramba 0738150 210

5 DBC - Manyoni 0738150 211

iii. Kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani. Maafisa wa Takukuru wakiwa kwenye kikao hicho.Kikao na waandishi wa habari kikiendelea.Mkutano na waandishi wa habari kikiendelea.Taswira ya kikao hicho.Muonekano wa Jesho la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida. 

Monday, January 29, 2024

KIKAO KAZI CHA KUJADILI RASIMU YA TAARIFA YA TATHMINI YA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI NCHINI CHAANZA SINGIDA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa akifungua kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida, tarehe 29 Januari, 2024. 

.....................................................

Na Mwandishi Wetu, Singida 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa, ameongoza kikao kazi cha wataalam kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida Januari 29, 2024. 

Bw. Mutatembwa, alisema  dhana ya Ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati yaani (Local content) ni dhana inayolenga katika kuhakikisha kuwa thamani ya ziada inayopatikana kwenye uchumi kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uwekezaji inabaki nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi pamoja na kunufaisha Watanzania na Taifa kwa ujumla. 

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inatekeleza dhana hii kwa kuhakikisha ajira kwa watanzania zinapatikana, uanzishwaji wa kampuni za ubia,  matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini katika uzalishaji na utoaji wa huduma,  manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa au zinazotolewa na kampuni za Kitanzania na  uhawilishaji wa teknolojia. 

Aidha aliongeza kusema kuwa, dhana hiyo inahakikisha uwepo wa ushiriki wa kampuni za kitanzania, na ushirikishwaji wa jamii zinazoishi katika maeneo ya uwekezaji au miradi inapotekelezwa. 

Akiongea na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Condrad Millinga alisema moja ya eneo linalofanyiwa kazi katika kikao kazi hiki ni kuona watanzania watashiriki vipi hasa katika eneo la ajira za ndani kwa kuwajengea uwezo waweze kushiriki kwa maana ya wenye ujuzi na wasiokuwa na ujuzi, aidha kuangalia eneo la matumizi ya malighafi na rasilimali zilizopo nchini katika miradi mikubwa.

“Tunauzalishaji unaotumika lakini kwa kiwango kidogo sana kulinganisha na mahitaji halisi, kumbe tunahitaji wenyewe kujipanga ndani lakini pia kushirikiana na wenzetu wanaotoka nje ili kuzalisha kulingana na mahitaji katika maeneo ya Uwekezaji,” alisisitiza. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya masoko Nchini Bw. Charles Ogutu alisema mapitio ya rasimu hiyo yatahakikisha kwamba wanatanzania wanashirki kikamilifu na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini. 

“Bila kusahau kwamba hakuna mradi mkubwa ambao hautegemei kilimo kwa hiyo tunakitazama kilimo kama ndiyo sekta mama inayobeba sekta zote kwa hiyo ni vizuri sana mazingira ya kibiashara na mazingira yote katika sekta ya uwekezaji zijumuishe sekta ya Kilimo.” alibainisha. 

Akizungumza katika kikao kazi hicho kilichohusisha wataalam kutoka Serikali kuu,Taasisi, MDA’s na sekta binafsi mtaalam wa uwekezaji wa Kimataifa (FDI) na Uchumi mkubwa Dkt. Juma Makaranga alisema ni muhimu kwa makampuni ya ndani kufanya biashara na makampuni makubwa ya nje kwa kusaidiwa kutengenezwa na kuwainua kiteknolojia, usimamizi na kitaaluma.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa (Kulia) na Mkurugenzi Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Condrad Millinga wakifuatilia jambo, katika kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya Masoko nchini Bw. Charles Ogutu akizungumza katika kikao hicho.
Baadhi ya Watalaam wakipitia machapisho mbalimbali katika kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini.