Tuesday, October 31, 2023

WANAFUNZI WAPYA TAASISI YA UHASIBU MKOA SINGIDA WATAHADHARISHWA KUTOJIHUSISHA MAPENZI NA WALIMU

  

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, ambaye pia ni Mratibu wa taaluma,  Flora Lemnge, akizungumza na wanafunzi wapya wa kampasi hiyo katika  semina elekezi kwa wanafunzi hao iliyofanyika Oktoba 30, 2023. Kutoka kushoto ni Mlezi wa Wanafunzi, Asia Hansy, Mshauri wa wanafunzi, Ambwene Kajula, Mratibu wa Mipango na Dawati la Malalamiko wa taasisi hiyo, Magreth Emmanuel.  

....................................................................

NA DOTTO MWAIBALE, SINGIDA

WANAFUNZI wapya waliochaguliwa kujiunga na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida kwa msimu wa masomo wa 2023/2024 wametakiwa kutojihusisha na uhusiano wa kimapenzi na walimu.

Kaimu Mkurugenzi wa kampasi hiyo ambaye pia ni Mratibu wa taaluma,  Flora Lemnge, ameyasema hayo jana Oktoba 30, 2023 katika semina elekezi kwa wanafunzi hao na kueleza kuwa mwanafunzi atakayejihusisha na uhusiano  wa kimapenzi   kwa lengo la kujaziwa matokeo mazuri kwenye mitihani yake  atakuwa amejivua utu wake bure.

Akizungumzia namna ya usahihishaji wa mitihani hiyo, alisema ukusanywa na kusahihishwa sehemu moja na hakuna mwalimu anayesahihisha darasa alilofundisha anapangiwa darasa lingine na kila swali husahihishwa na mwalimu mmoja  hivyo mtihani wenye maswali matano husahihishwa na walimu watano tofauti.

"Sasa hivi nasimama kama mama nafasi yangu ya kitaaluma naiacha kwa muda 'ewe binti usivue nguo zako kisa upate mtihani itakula kwako' kuna baadhi yenu mmekuja hapa na kuanza kujipangia walimu baada ya kuona anamshara na yupo ‘smati’ atakukula bure kwani mtihani huo ni uleule utashindanishwa na kampasi zingine za TIA na unasahihishwa na walimu wa ndani na wa nje na si vinginevyo," alisema Lemnge.

Lemnge, aliwataka wanafunzi hao kuzingatia sheria zote za taasisi hiyo na nchi na kuhudhuria masomo kwani hilo ndilo jambo walilolikusudia wakizingatia kuwa wazazi wao wamekuwa wakitoa fedha nyingi kwa ajili yao.

Alisema lengo la semina hiyo ni kuwafanya wazijue taratibu zote za taasisi hiyo ukizingatia kuwa wanafunzi hao wametoka katika mikoa mbalimbali na kuwa na tabia tofauti.

Naye Mshauri wa wanafunzi katika Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Ambwene Kajula aliwapongeza wanafunzi kwa kuchagua chuo hicho na akawashuru wazazi kwa jinsi wanavyojitoa kuwasomesha watoto wao.

Alisema baadhi ya mambo yanayofundishwa katika semina hiyo elekezi ni kutaka kuwaonesha wanafunzi hao mazingira watakayokuwa nayo na jinsi ya kuishi  na kufikia malengo waliyoyakusudia hivyo watafundishwa mambo ya aina mbalimbali kama miongozo, sheria na kanuni ambazo wanatakiwa kuzifuata wakiwa katika taasisi hiyo.

Aidha, Kajula alisema pia watawakutanisha na wadau kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) watu wa dawati la jinsia, NSSF, NHIF na Taasisi za kifedha kama mabenki,vyombo vya mawasiliano ya simu na kuwafundisha mbinu mbalimbali za kimaendeleo.

Kwa upande wake Mratibu wa Mipango na Dawati la Malalamiko wa taasisi hiyo, Magreth Emmanuel aliwataka wanafunzi hao wanapokuwa na changamoto mbalimbali kuziwasilisha kwa Serikali ya wanafunzi wa chuo hicho.

“Kunatabia baadhi ya wanafunzi wakipata changamoto wanazipeleka kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, TAKUKURU na maeneo mengine hiyo sio sahihi inatakiwa uanzie chini kwa viongozi wa Serikali ya wanafunzi (TIASO) ambao wakishindwa kutatua tatizo lako wanatuletea sisi viongozi wa chuo,” alisema Emmanuel.

Rais wa Serikali ya wanafunzi (TIASO) wa chuo hicho, Godfrey Mbuya alisema moja ya jukumu lao ni kutatua changamoto mbalimbali za wanafunzi na pale zinapowazidi uwezo wanazipeleka ngazi ya juu.

Mbuya alisema semina hiyo ni ya muhimu sana kwao  kutokana na mwingiliano wa wanafunzi kutoka maeneo na makuzi tofauti ikiwa ni pamoja na kuyajua mazingira ya chuo na kufuata sheria kanuni na taratibu za chuo.

Japhet Maximilian mwanafunzi wa Shahada ya kwanza katika Rasilimali Watu na Utawala akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake aliushukuru uongozi mzima wa taasisi hiyo kwa semina hiyo elekezi yenye lengo la kuwajenga na kupata miongozo mbalimbali na kuwa mambo yote waliyoelekezwa ni wajibu wao kuyatekeleza.

Maximilian alitumia nafasi hiyo kumshuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali na kuwaongeza bumu na hela ya kujikimu kutoka Sh.8,500 hadi Sh.10,000 ni jambo la kuendelea kumshuru kwa kuwa anataka tuwe na taifa la watu walioelimika.

  Baadhi ya mambo wanayotakiwa kuyafanya wakati wakiwa chuoni ni kuzingatia uvaaji wenye staha, utunzaji wa mazingira na vifaa vya chuo, heshima kwa kila mtu, lugha nzuri, kushiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo michezo na kutojihusisha na vitendo vya wizi na mapenzi ya jinsia moja (ushoga na usagaji)

Kesho Oktoba 31, 2023 wanafunzi hao wataendelea na semina hiyo kwa kukutana na taasisi zingine kama TAKUKURU na za kifedha kwa ajili ya kujifunza jinsi zinavyofanya kazi.

Mshauri wa wanafunzi wa taasisi hiyo, Ambwene Kajula, akizungumza.   

       Mlezi wa Wanafunzi, Asia Hansy, akizungumza.

Rais wa Serikali ya wanafunzi (TIASO) wa chuo hicho, Godfrey Mbuya akizungumza.

   Mratibu wa Michezo wa taasisi hiyo, Alen Mwanga, akizungumza.

 Waziri wa Sheria na Katiba wa taasisi hiyo, Nurbeti Kabatanye, akizungumza.

Semina ikiendelea

               Wanafunzi wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa.

Saturday, October 28, 2023

TAKUKURU MKOA WA SINGIDA YAOKOA SH.MILIONI 54

 Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU ) Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa kipindi cha Julai-Septemba 2023 katika kikao kilichofanyika Oktoba 27, 2023.
Kikao na waandishi wa habari na maofisa wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, kikifanyika.

Kikao kikiendelea.

.........................................................


Na Dotto Mwaibale, Singida

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),Mkoa wa Singida imeokoa Sh. 54,087,750.58 zilizotokana na wazabuni kutowasilisha kodi ya zuio Mamlaka ya Mapato,Tanzania (TRA) na kupeleka vifaa pungufu katika miradi mbalimbali.

Hayo yamebainishwa Oktoba 27, 2023 na Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida Sipha Mwanjala wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kwa kipindi cha Julai-Septemba 2023.

Alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida kwa kipindi cha Julai –Septemba 2023 kwa upande wa uzuiaji rushwa walifuatilia utekelezaji wa miradi kumi na tatu yenye thamani ya zaidi Sh.Bilioni 5 katika sekta ya Elimu na Barabara na kuwa ilijumuisha miradi ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa
Taifa kwa fedha zilizotolewa na Serikali Kuu.

Alisema miradi mitatu iliyofuatiliwa yenye thamani ya Sh. Bilioni1.4 ilikutwa na mapungufu mbalimbali ambapo walitoa ushauri ili kukabiliana na mapungufu hayo. Alitaja baadhi ya mapungufu hayo ni kupeleka vifaa pungufu katika miradi tofauti na madai aliyowasilisha au fedha alizolipwa.

Akizungumzia kuhusu chambuzi za mifumo alisema katika kipindi tajwa TAKUKURU ilifanya chambuzi saba za mifumo ili kubaini mianya ya rushwa iliyopo katika maeneo hayo na kisha
kushauri namna ya kuiziba na kuwa Warsha saba zilifanyika kwa ajili ya kujadili mianya ya rushwa
iliyobainika katika chambuzi zilizofanyika na kuweka mikakati ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Aidha, Mwanjala alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida iliendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kufanya vikao 18 na wadau katika kata 18 ambapo wadau waliibua kero 175.

Alisema kero zilizotatuliwa mpaka sasa ni 125 na kero 50 zinaendelea kupatiwa ufumbuzi.
Akielezea upande wa elimu kwa umma alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida iliwaongezea wananchi uelewa wa masuala ya rushwa kwa kufanya Semina 34 kwenye makundi mbalimbali
wakiwemo watumishi wa umma.

Alisema pia walifanya mikutano ya hadhara 17,maonesho 7, kutembelea na kuimarisha klabu za wapingarushwa 43 katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Akizungumzia suala la uchunguzi na mashitaka alisema malalamiko 76 yalipokelewa, ambapo malalamiko 52 yalihusu
vitendo vya rushwa na malalamiko 24 hayakuhusu rushwa.

Alisema malalamiko 52 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na
malalamiko 24 ambayo hayahusiani na rushwa walalamikajiushauri.

Alisema katika kipindi hicho kesi 10 zilifunguliwa mahakamani,kesi 13 ziliamuliwa, kesi 8zilishinda.

Akizungumzia mikakati ya utendaji kazi waliojiwekea kwa robo ya pili ya mwaka 2023/2024 ya kuanzia mwezi ni kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Kuendelea kuwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa ili wananchi washiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo
hivyo hasa katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao, Kuendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU – Rafiki.

Mwanjala alitoa wito kwa kusema kuwa TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa RAI kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu kuzuia vitendo vya rushwa vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii. Pia, kuzuia vitendo hivyo hasa
katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao,na kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kufika Ofisi za TAKUKURU Mkoa wa Singida na Wilaya za Iramba,Ikungi,Mkalama na Manyoni.

Mwanjala alitaja njia nyingine ya kutoa taarifa hizo ni kupiga simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa na wakuu wa TAKUKURU wa Wilaya kwa namba RBC –Singida 0738150208, DBC -Mkalama 0738150 212, DBC - Ikungi 0738150213, DBC -Iramba 0738150 210 na DBC - Manyoni 0738150 211 na
akaomba wananchi kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani.

Saturday, October 14, 2023

DC WILAYA YA KALIUA AWATAKA VIJANA KUTUMIA VYAKULA VYENYE LISHE KUKABILIANA CHANGAMOTO YA NGUVU ZA KIUME

Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dk. Rashid ChuaChua akigawa vyandarua vyenye dawa vilivyotolewa na Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kwa ajili kukabiliana na ugonjwa wa malaria wilayani humo.

Na Mwandishi Wetu, Kaliua

 

MKUU wa Wilaya ya Kaliua Dk. Rashid ChuaChua amewataka wananchi wa Wilaya hiyo hususani vijana kutafuta mbadala wa tatizo la nguvu za kiume ikiwemo kuzingatia vyakula vya lishe na kuacha kisingizio kuwa matumizi ya vyandarua vyenye dawa ndio chanzo.

Amesema upendo hekima na huruma ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kunusuru wananchi wake kwa kusambaza vyandarua katika wilaya hiyo ni juhudi ambazo haziwezi kufifishwa na imani potofu.

Akizungumza jana mkoani Tabora wilayani Kaliua Dk. Rashidi amewataka wananchi hao hususani vijana kutafuta mbadala wa tatizo la nguvu za kiume, ikiwemo kuzingatia vyakula vya lishe na kuacha kisingizio kuwa matumizi ya vyandarua vyenye dawa ndio chanzo.

“Kama mashine haifanyi kazi haifanyi tu sio kwa sababu ya kutumia vyandarua vyenye dawa, tutafute chanzo cha wanaume wengi kuwa na changamoto ya nguvu za kiume, sisi  wengine tumetumia hivyo vyandarua miaka na miaka na hadi watoto zetu wanatumia na hatuna hiyo shida,”alisema.

Alieleza, ujio wa vyandarua hivyo ni muhimu hivyo wananchi wanatakiwa kuunga mkono jitihada hizo lengo ni kujilinda dhidi ya malaria ambayo ni tishio.

Alithibitisha ya kwamba Tabora ikiwa ni ya kwanza kitaifa kwa maambukizi ya malaria, Kalihua ni miongoni mwa wilaya zinazoongoza mkoani humo kutokana na maambukizi ya ugonjwa huo.

Alisema,  uchunguzi wa afya unaonyesha kati ya watoto 10 saba wana maambukizi ya malaria hatua ambayo serikali imeona ipo haja kuongeza nguvu katika mapambano hayo ili kuwa na watu wenye afya njema.

“ Wapo watu hawana uelewa wanapotosha jamii na kusema vyandarua hivyo vinapunguza nguvu za kiume, hakuna ukweli wa dawa zinazotumika kuzuia mbu katik vyandarua kupunguza  nguvu naomba mjue kuwa malaria ni hatari hivyo, nawasihi wananchi tumieni vyandarua hivi ipasavyo,”alisisitiza.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa MSD Kanda ya Tabora Adonizedeck Tefurukwa,  alisema, MSD itahakikisha vyandarua 245, 777 vinasambazwa katika vituo 246 sawa na kaya 59,154 za wilaya ya Kaliua kama ilivyokusudiwa.

“Tutasambaza vyandarua kutoka katika ghala letu la MSD Kaliua kwa kutumia magari yetu zaidi ya 13 makubwa na madogo, lengo ni kuhakikisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria yanafikiwa,”alisema.

Aliongeza kuwa, MSD ikiwa ndio msambazaji mkuu wa bidhaa za afya kwa vituo 7, 000 vya umma na binafsi vilivyoidhinishwa na serikali itahakikisha inasambaza vyandarua hivyo hadi vituoni bila kujali kupanda kwa gharama za usafirishaji ikiwemo bei ya mafuta na kupanda kwa dola.

Naye Mwakikishi wa Wizara ya afya Wilfred Mwaifongo alisema, wananchi wa wilaya hiyo wapokee vyandarua na kutumia kwa lengo lililokusudiwa ikiwemo kujikinga dhidi ya malaria.

Alisema, hatua hiyo itaimarisha afya zao na kuchochea ukuaji wa uchumi katika Wilaya ya Kalihua.

Pia Diwani wa kata ya Uyumbu Ramadhani Mrisho,  alieleza kuwa watahakikisha wanatekeleza maelekezo ya Rais hususani katika maboresho sekta ya afya.

Alisisitiza kuwa, viongozi wa kijiji na halmashauri hiyo hawatakuwa tayari kuona ugawaji wa vyandarua hivyo, unakwama kwa kuwa changamoto ya ugonjwa wa malaria wilayani humo  inahitaji ufumbuzi wa pamoja.

Vyandarua vikiendelea kugaiwa.
Maafisa wa MSD wakijadiliana wakati wa ugawaji wa vyandarua hivyo.
 

Thursday, October 12, 2023

TRA YAFAFANUA MADAI YA MFANYABIASHARA EMMANUEL GADI

Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Stephen Kauzeni akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam wakati akitoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Bw. Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha (Picha na Mpiga picha wetu).

........................................ 

Na: Mwandishi Wetu

 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) haina mfumo wowote mwingine inaouendesha wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo wa Forodha wa TANCIS ambao unatumika kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi wa TRA Bw. Stephen Kauzeni kwa waandishi wa habari wakati akitoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu malalamiko ya Bw. Emmanuel Gadi ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Wintech Tanzania Ltd anayedai kuwa, TRA imetengeneza mfumo wa kuingiza mizigo nchini nje ya mfumo halali wa Serikali kinyume na Sheria ya Forodha.

“Bw. Emmanuel Gadi alifikisha malalamiko yake kwa njia ya barua tarehe 27 Februari, 2023 akidai kupewa uthibitisho na TRA wa kuingiza mzigo wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kampuni ya Tosh Logistics Ltd.

TRA ilifanya Uchunguzi wa kutosha na kuthibitisha kwamba hapakuwa na mzigo wowote ulioingizwa nchini kwa jina la Wintech Tanzania Ltd wa vifurushi 471 vya Toner Cartridges kupitia kadhia yenye namba TZDL – 22-1382193 ya tarehe 18 Agosti 2022 kama anavyodai,” amesema Bw. Kauzeni.

Ameongeza kuwa, TRA ilimjibu mhusika kupitia barua yenye kumbukumbu namba CF 8/92/01 ya tarehe 25 Julai 2023 ikimjulisha kuwa, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa House Bill of Lading na kutoonekana kwa mzigo huo kwenye kadhia iliyowasilishwa na kampuni ya Tosh Logistics Ltd, TRA isingeweza kuthibitisha kuingizwa kwa mzigo huo nchini.

“Kupitia taarifa ya Bw. Emmanuel Gadi aliyoitoa kwenye vyombo vya habari, tumebaini kuwepo kwa viashiria vya ukwepaji kodi kwani ni dhahiri kuwa mzigo wake uliingizwa kwa njia za magendo,” ameeleza Meneja Kauzeni. 

Meneja huyo wa Elimu kwa Mlipakodi amemtaka mlalamikaji kuwasilisha nyaraka na uthibitisho wa Kampuni yake kuingiza mzigo huo nchini mara moja ili hatua stahiki zichukuliwe.

 

MSD YAFANYA MABORESHO MAKUBWA SEKTA AFYA SINGIDA, YATOA VIFAA TIBA, DAWA ZA MILIONI 532.4


Mhandisi wa vifaa tiba wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kati Dodoma , Jumanne Mapesa  (kulia) akimkabidhi boksi la dawa Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki mjini Singida Oktoba 11, 2023. Wengine ni wafanyakazi wa hospitali hiyo.

.........................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

BOHARI ya Dawa (MSD) imetoa vifaa tiba na dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh. Milioni 532.4 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Hospitali ya Wilaya ya Singida, Hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi, Hosptali ya Wilaya ya Ikungi na Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu mkoani hapa.

Akizungumza Oktoba 11, 2023 wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwenye hospitali hizo, Meneja wa MSD Kanda ya kati Dodoma, Bi. Mwanashehe Jumaa alivitaja vifaa tiba na dawa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kuwa ni vitanda 9 (ICU  Beds) vya kisasa pamoja na  dawa..

Alisema kwa Hospitali ya Wilaya ya Singida vifaa vilivyotolewa ni vitanda viwili wakati kwa Kituo cha Kituo cha Afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ni pasi ya kunyoshea nguo, vitanda vya wagonjwa, vitanda vya kujifungulia, mashuka, magodoro na viti mwendo..

Jumaa alisema utoaji wa vifaa hivyo ni muendelezo wa uboreshaji wa huduma za sekta ya afya mkoani Singida kwani Machi 15, 2023 MSD ilitoa  mashine za kufulia, vifaa vya kinywa na  meno, usingizi na vitanda  Hosptali ya Wilaya ya Singida Ilongero.

Baada ya kukabidhi vifaa hivyo, Wataalam kutoka MSD walitoa maelekezo na mafunzo kwa wataalam  ambao hospitali zao zimenufaika na vifaa hivyo wavitunze ili vidumu muda mrefu kwani Serikali chini ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua.

"Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kununua vifaa hivi hivyo ni wajibu wa watumishi wa sekta ya afya kuhakikisha vinatunzwa vizuri," alisema .Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.

Viongozi wa Hospitali hizo wameishukuru serikali kupitia MSD kwa kuendelea kuwapatia dawa na vifaa tiba kwa wakati jambo ambalo limeongeza tija na ufanisi wa kazi katika utoaji huduma za afya

Nao Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Paul Ndeki,  Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida, Yusuph Kitinya, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itigi, Emmanuel Mallange, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sapoko waliahidi kuvitunza na kumshukuru Rais Samia  kwa kuendelea kuboresha huduma za afya nchini.

 “Vifaa tulivyopatiwa vitatusaidia kutoa huduma zetu tunawashukuru Serikali kwa kufanikisha upatikanaji wa vifaa tiba kupitia MSD  hivyo kuhimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.,.” alisema Kitinya.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli alisema wamepokea vitanda 16 na kufikisha idadi ya vitanda 80 na kueleza kuwa mbali ya vifaa hivyo pia walipokea baadhi ya vifaa vingine vingi kama magodoro, mashuka, taa za kufanyia uchunguzi, taa ya chumba cha upasuaji na sasa wapo kwenye mchakato wa kupelekewa mashine itakayosaidia kufanya operesheni ya mama na mtoto katika jengo ambalo lipo mbioni kukamilika.

."Kwa ujumla ni idadi kubwa ya vifaa tulivyoletewa na Serikali chini ya mama yetu kipenzi  Rais Samia kupitia MSD." alisema Dk.Kimotoli..

Kwa upande wake Mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Hussein Sepoko alisema Rais Samia amewapelekea vifaa tiba vingi vya kisasa na akaishukuru MSD kwa ushirikiano inayowapa wa kuwapelekea vifaa tiba na dawa kwa wakati.

Nao Diwani wa Kata ya Ilongero Issa Mwiru na Diwani wa Kata ya Itigi Mjini, Ally Minja  walipongeza Serikali na MSD kwa kusambaza vifaa tiba na dawa.

“Kwa nafasi ya kipekee tunaishukuru MSD  wamekuwa na ushirikiano mkubwa tunapohitaji vifaa tiba na dawa wanatuletea kwa wakati hakika wameendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya afya ," alisema Mwiru.

Aidha, Mwiru aliishukuru Serikali kwa kuwaletea watumishi katika hospitali mpya ya Wilaya ya Singida na kusifia utendaji kazi wao kwa masaa yote wanapokuwa kazini.

Leo Oktoba 12, 2023 MSD wamemaliza kufanya kazi ya kusambaza  vifaa tiba na dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba Kiomboi na Ikungi hata hivyo wataendelea kufanya hivyo kulingana na mahitaji ya vifaa tiba na dawa mkoani Singida..

Makabidhiano ya vitanda (ICU Bed) na magodoro yakifanyika Hosptali ya Rufaa Mkoa wa Singida..
Moja ya kitanda kati ya tisa vilivyotolewa na MSD vikishushwa kwenye gari.
Vitanda vikishushwa.
Wafanyakazi wa Sekta ya Afya wa Hospitali ya Wilaya ya Singida wakionesha furaha yao wakati wakipokea vitanda viwili ( ICU Bed) kutoka MSD.
Muonekano wa mashine ya kukaushia nguo iliyopelekwa na MSD Katika Hospitali ya Wilaya ya Singida.

Mashine ya kufulia nguo iliyotolewa na MSD ukiwa Hospitali ya Wilaya ya Singida

Mapokezi ya vitanda (ICU Bed) yakifanyika Hospitali ya Wilaya ya Singida.Katikati ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Singida, Yusuph Kitinyi.
Diwani wa Kata ya Ilongero, Issa Mwiru (mwenye fulana rangi ya njano( akiwa na viongozi wengine baada ya kupokea vitanda hivyo.
Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna.(wa pili kulia) akimkabidhi vifaa tiba Diwani wa Kata ya Itigi Mjini, Ally Minja na viongozi wengine. 

Gari la MSD likishusha vifaa tiba Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida.

Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma , Jumanne Mapesa (wa pili kushoto) akipeana mkono na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Kahabi Kimotoli baada ya kumkabidhi vitanda 25 vya kawaida vya wagonjwa leo Oktoba 12, 2023.
Vitanda vya kawaida vya wagonjwa vikishushwa kutoka kwenye gari la MSD tayari kwa makabidhiano wilayani Ikungi.

Muonekano wa moja ya kitanda cha kawaida cha wagonjwa kati ya vitanda 80 vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD vilivyopo Hospitali ya Wilaya ya Ikungi.

Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma , Jumanne Mapesa (kushoto) akishiriki kubeba vifaa tiba wakati wa makabidhiano wilayani Iramba.


Mhandisi wa vifaa tiba wa MSD Kanda ya Kati Dodoma , Jumanne Mapesa, akipeana mkono na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Hussein Sepoko baada ya kumkabidhi vitanda viwili (ICU Bed) vilivyotolewa na Serikali kupitia MSD.
Dereva wa MSD, Kanda ya Kati Dodoma, Mrisho Gyumi (kushoto( akiwajibika kubeba moja ya boksi la vifaa tiba kabla ya makabidhiano wilayani Iramba

Friday, October 6, 2023

MAADHIMISHO YA WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA NSSF SINGIDA YATAMBUA VINARA WA MICHANGO YA WANACHAMA

Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa (katikati)Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM), (kulia) na Mwakilishi wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT)  Kiomboi Iramba John Leonard wakikata keki maalumu kwa ajili ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yaliyoandaliwa na NSSF Oktoba 6, 2023, 

...........................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

WAKATI maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yakiadhimishwa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Singida limezitambua taasisi na kuwashukuru waajiri wanaojitolea kwa hali na mali kuhakikisha michango ya wanachama wake inawasilishwa kwa wakati.

Hata hivyo shirika hilo pamoja na mambo mengine limezitaja taasisi takribani tano zilizoongoza kwa uwasilishaji wa michango hiyo kwa mwaka huu mkoani hapa zikiwemo Mount Meru Miller na Tree for the Future.

Nyingine ni Makiungu Hospital,  Srs Medical Missionaries of Mary (MMM), na Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT)  Kiomboi Iramba ambazo zimetunukiwa vyeti vya kutambua mchango huo.

Hata hivyo akizungumza wakati wa utoaji wa vyeti hivyo Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa alianisha sababu za utoaji wa tuzo hizo kuwa taasisi hizo zimekuwa zikitekeleza sheria za NSSF kwa kupeleka michango na kuandikisha wanachama kwa wakati.

"Wapo waajiri wakubwa na wadogo wenye michango mikubwa kabisa na wenye michango midogo lakini hawa wamefanya vizuri zaidi," alisema Kalimilwa.

Kalimilwa alihimiza waajiri kufuata sheria za NSSF na kuwataka kutekeleza takwa hilo la kisheria kwa mustakabari wa maslahi bora ya wafanyakazi wao pindi wanapo staafu.

Baadhi ya waajiri waliopata vyeti hivyo, Otomali Haule kutoka Hospitali ya Makiungu, Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM), waliishukuru NSSF kwa kutambua mchango na kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano uliopo baina ya pande zote mbili ambapo walitoa wito kwa taasisi zingine kujenga tabia ya kupeleka michango yao katika mfuko huo.

Tukio hilo la kuzitunuku vyeti vya heshima taasisi hizo limeambatana na kilele cha maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja kwa mwaka 2023 ambayo yamebeba ujumbe usemao ‘Ushirikiano kwa Huduma Bora, ‘Team work for service Excellency’ .

Wawakilishi wa taasisi zilizofanya vizuri wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Mwakilishi wa Shirika la Tree for the Future. Frank Marley akilishwa keki.
Keki ikiliwa.
Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM) akilishwa keki.
Keki ikiliwa.
Maadhimisho hayo yakiendelea.
Mfanyakazi wa NSSF, Hakimu Mbagga kutoka Mkoa wa Kagera, akilishwa keki.
Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM) akimlisha keki Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa.
Maadhimisho yakiendelea.
Meneja Rasilimali Watu na Utawala (HR)_wa Kiwanda cha Mount Meru Miller, Sara Baltazari akikabidhiwa cheti cha mwajiri bora katika kupeleka michango ya wafanyakazi wao NSSF.
Mwakilishi wa Shirika la Tree for the Future. Frank Marley akikabidhiwa cheti.
Otomali Haule kutoka Hospitali ya Makiungu, akikabidhiwa cheti.
Sr Franca Ogbunuju kutoka Shirika la Srs Medical Missionaries of Mary (MMM) akikabidhiwa cheti.
Mwakilishi wa Kanisa la Evangelist Assemblies of God Tanzania (EAGT)  Kiomboi Iramba, John Leonard akikabidhiwa cheti.
Wawakilishi wa taasisi zilizofanya vizuri wakiwa na Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida wakionesha vyeti vyao walivyotunukiwa.
Mstaafu wa NSSF Mkoa wa Singida, Joseph Gidatu akikabidhiwa zawadi. 
Picha ya pamoja na mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Meneja wa NSSF Mkoa wa Singida, Oscar Kalimilwa (katikati mbele)

Thursday, October 5, 2023

MBUNGE MATTEMBE AUNGA MKONO JITIHADA ZA RAIS DKT.SAMIA AZINDUA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI MKOA WA SINGIDA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe akizungumza na wajasiriamali wakati akizindua mafunzo ya ujasiriamali Wilaya ya Mkalama mkoani hapa Oktoba 3, 2023ambayo yatafanyika katika wilaya zote.

......................................................

 

Na Dotto Mwaibale, Singida

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe ameunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha wananchi wanajikomboa kiuchumi kwa kuzindua Mafunzo ya Ujasiriamali  Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, mafunzo yenye kaulimbiu isemayo "SINGIDA YA UJASIRIAMALI NA SAMIA INAWEZEKANA"

Akizungumza wakati akizindua mfunzo hayo Mattembe alisema yamelenga  kuwawezesha wajasiriamali kujiamini na kuweza kutoka hatua moja kwenda nyingine kiuchumi.

"Mafunzo haya ambayo yatatolewa na wawezeshaji wabobezi ni muhimu sana kwa wananchi wetu na wajasiriamali kwani yanakwenda kuchochea uukuaji wa uchumi wao na kujikwamua kiuchumi," alisema Mbunge Mattembe.

Mafunzo hayo ambayo yatafanyika katika wilaya zote za Mkoa wa Singida yatahusisha usindikaji nafaka, matunda, ufugaji bora wa kuku, kilimo, pamoja na usimamizi wa fedha yameandaliwa na ofisi ya mbunge na yanatarajiwa kumalizika   November 10, 2023.

Aidha, Mattembe amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kupata mafunzo hayo na washiriki wayazingatie kikamilifu na kuwa mabalozi wazuri kwa wengine ili tija iweze kupatikana maana ni mkombozi kwao na jamii kwa ujumla.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walimshukuru Mbunge Mattembe kwa kuwajali wananchi na wajasiriamali kwa kuwapelekea mafunzo hayo yenye lengo la kuwakomboa kiuchumi na kuacha kuwa tegemezi.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe akionesha namna  ya kupika wakati akizindua mafunzo hayo.
Mbunge Mattembe akiwa na Wajasiriamali wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.
Mbunge Mattembe akionesha furaha yake wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida Aysharose Mattembe (wa pili kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo wa Wilaya ya Mkalama.