Kansela wa kilimo wa Ubalozi wa Uholanzi nchini , Bw Bart Pauwels (mwanzo kulia)pamoja na anayemfuata mwenye miwani ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Dr Patrick Ngwediagi na Balozi wa Uholanzi hapa nchini , Wiebede Boer katikati na kulia kwa Balozi ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) Bw , Geoffrey Kirenga na mwisho Bw Bob Shuma mdau wa kilimo wakionyesha kitabu cha mwongozo wa kilimo cha viazi ambacho kilizunduliwa.
......................................
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANZANIA kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi wamezindua kitabu cha
mwongozo wa usajili wa aina za mbegu za viazi kwa lengo la kuimarisha ustawi wa
kilimo cha viazi na usalama wa chakula hapa nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho wiki iliyopita
jijini Dar es Salaam,Balozi wa Ufalme wa Uholanzi hapa nchini, Wiebe de Boer
aliwaambia viongozi waalikwa na wageni mbalimbali kuwa hiyo ilikuwa hatua kubwa
katika safari yao ya kuimarisha sekta na kilimo cha viazi hapa nchini.
"Safari ambayo imechangiwa na ushirikiano wa miaka kumi kati ya
Tanzania na Uholanzi,katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ushirikiano huu
umewavutia wakulima wa viazi wa Uholanzi kusajili aina zao za viazi nchini
Tanzania," aliongeza.
Alisisitiza kwamba si hivyo tu bali pia kuvutia uwekezaji kuongeza na
kupanua mnyororo wa thamani wa viazi na sasa wanatambua kwamba viazi kama
chakula kikuu cha kuhakikisha usalama wa chakula, kuzalisha kipato kwa wakulima
na kutengeneza fursa za ajira.
Balozi Boer alisema kuwa ufanisi na tija katika kilimo cha viazi unahitaji
matumizi ya mbegubora sambamba na kanuni bora za kilimo zilizochochea ukuaji wa
sekta ya kilimo.
Alisema nchini Uholanzi kuna aina zaidi ya 250 za viazi zinazolimwa kwa
matumizi mbalimbali,ikiwa ni pamoja na kuchemsha, kukaanga, krisps, kuoka,
kuzalisha mbegu na usindikaji wa wanga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu
Tanzania(TOSCI), Dk Patrick Ngwediagi alisema kitabu hicho kitatumika kama
mwongozo kwa wagunduzi wa mbegu za viazi , wakulima na wawekezaji wa ndani na
nje ya nchini wanaovutiwa kuwekeza kwenye sekta ya viazi hapa nchini.
"Kwa kweli leo ni hatua muhimu kwa sababu kitabu hiki kitasaidia
wakulima kuwa na taarifa za kutosha kuhusu sera, sheria zinazosimamia sekta ya
kilimo pamoja na kuangalia changamoto na fursa zilizopo nchini kwenye kilimo
cha viazi," alisistiza Dr Ngwediagi.
Dk Ngwediagi alisema kuwa kitabu hicho kitawapa wakulima na wagunduzi hatua
kwa hatuajinsi ya kusajili mbegu zao nchini na mchakato wa kuzalisha mbegu bora
ili kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo.
“Jinsi hizi zote ni taratibu za hapa nchini katika kuimarisha ukuaji wa
sekta na mbegu zote lazima zisajiliwe kwenye Daftari la Taifa la mbegu katika
juhudi za serikali kuimarisha usalama wa vyakula kwa watanzania,” aliongeza.
Mshauri wa Kilimo wa Ubalozi wa Uholanzi, Bart Pauwels alisema kuwa Ubalozi
wa Uholanzi hpa nchini utaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya
Tanzania, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na sekta binafsi kwa ujumla ili
kuhakikisha inakuza ukuaji wa sekta ya viazi.
“Kilimo bora ni injini ya ukuaji wa sekta, Ubalozi wa Uholanzi utaendelea
kutoa msaada wasekta hii kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika
kuboresha kilimo kwa kuleta piateknoloji na ujuzi mwingine wa kitaalamu,”
aliongeza.
Kwa miaka 10 sasa, Tanzania na Uholanzi zimekuwa na ushirikiano mzuri
katika sekta ya viazi.Kupitia ushirikiano huu, jumla ya aina 16 za viazi
zilisajiliwa na kati ya hizo 12 ni aina za Kiholanzi zinazotoa mavuno mengi,
kustahimili ukame na wadudu.
Maendeleo haya yalivutia biashara zaidi kwenye mnyororo wa viazi kutoka kwa
ufugaji, kukua hadi usindikaji. Ili kusaidia sekta hii zaidi, Ubalozi
uliiwezesha TOSCI kutoa mwongozo wa hatua kwa hatua kuhusu taratibu za kuchukua
iwapo mwekezaji anataka kusajili aina ya viazi nchini Tanzania kwa ajili ya
biashara. Kitabu hiki kimeidhinishwa na TOSCI kwa matumizi ya Tanzania.
ujumbe wa wafugaji 30 wa viazi vya Uholanzi, watafiti, wakulima
wanaojihusisha na uendelezaji wa aina za viazi hivyo wametembelea Tanzania.
Lengo ni kufahamiana na mahitaji ya soko, upendeleo na kupokea maoni kutoka kwa
wakulima. Taarifa hizi zitatumika katikautafiti na ukuzaji wa aina mpya kwa
Tanzania.