Saturday, November 14, 2020

MICHEZO YA WAFANYAKAZI WA SUA YAFUNGWA RASMI

Afisa Tawala Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Bw. Peter Mwakiluma akitambulisha wageni mbalimbali waliofika kwenye ufungaji wa michezo hiyo ya Chibunda Cup 2020 kwa niaba ya naibu makamu mkuu wa chuo utawala na fedha.
Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la SUA Bi. Isabela Kitila akitoa salamu za CRDB ambao ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo.
Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Wami Bwana Harold Lambikile akizungumza neno kwa wanamichezo na wadau waliofika kwenye ufungaji rasmi wa michuano hiyo ya Chibubda Cup.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo  Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Utawala na Fedha, Profesa. Amandusi Muhairwa akitoa salamu za Chuo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Profesa. Raphael Chibunda kuhusu michezo hiyo na umuhimuwake kwa wanajumuiya wa SUA.
Mgeni rasmi kwenye kufunga mashindano hayo ya Wafanyakazi wa SUA Bi. Asteria Mwang'ombe  ambaye ni Afisa Michezo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akitoa neno kabla ya washiriki na wadau wa michezo hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya michezo vya SUA kwenye kampasi ya Edward Moringe.

Mgeni rasmi kwenye kufunga mashindano hayo ya Wafanyakazi wa SUA Bi. Asteria Mwang'ombe  ambaye ni Afisa Michezo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akipata maelekezo kwa waamuzi wa mchezo huo wa mpira wa miguu.


 Mgeni rasmi kwenye kufunga mashindano hayo ya Wafanyakazi wa SUA Bi. Asteria Mwang'ombe  ambaye ni Afisa Michezo wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro akikagua timu za mpira wa miguu zilizoshiriki kwenye kucheza mechi ya ufungaji katika ya SUA  na Don Bosco.
Wachezaji wa mpira wa wavu kati ya timu ya wafanyakazi wa SUA na DON BOSCO wakichuana vikali kwenye mchezo wa kufunga michuano hiyo.


Na; Calvin Edward Gwabara.


WATANZANIA wametakiwa kuhakikisha wanatenga muda kwa ajili ya kushiriki kwenye michezo na mazoezi mbalimbali ya mwili ili kusaidia kujenga mwili na taifa la watu wenye afya watakaoleta  maendeleo.

Wito huo umetolewa na Afisa Michezo Manispaa ya Morogoro Bi Asteria Mwang’ombe kwa niaba ya mkurugenzi wa manispaa hiyo wakati akizungumza na wanamichezo na wanajumuiya wa SUA, Benki ya CRDB na NMB wakati akifunga rasmi michezo kwa ya wafanyakazi wa SUA ya Chibunda CUP.

Bi. Asteria ameupongeza uongozi wa SUA kwa kuamua kuanzisha michezo hiyo ambayo inawakutanisha wafanyakazi wote wa SUA kwenye michezo 20 mbalimbali na kuipongeza benk ya NMB kwa kuamua kufadhili mashinano hayo kila mwaka toka kuanza kwake.

‘’ Naupongeza sana uongozi wa SUA kwa kulipatia kipaumbele swala la michezo kwa wafanyakazi na wanafunzi hasa kwa kuamua kuanzisha idara maalumu kwaajili ya michezo Chuoni hii ni hatua nzuri kwani itaongeza ufanisi na ari ya wanajumuiya wa SUA kushiriki kwenye michezo” Alisistiza Bi. Asteria.

Afisa michezo huyo ameahidi kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika katika kufanikisha michezo chuoni hapo ikiwemo swala la walimu wamichezo pale watakapohitajika na kwamba changamoto mbalimbali zilizobainishwa atazifikisha kwa uongozi wa manispaa ili kuona namna ya kuzitatua.

Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi kufunga maichezo hiyo Naibu makamu mkuu wa chou upande wa taaluma Prof. Amandus Muhairwa kwa niaba ya makamu mkuu wa chou Prof. Rapgael Chibubda amesema michezo hiyo ni sehemu ya Chuo kupata wanamichezo ambao watakiwakilisha chou kwenye michezo mbalimbali ndani nan je ya nchi.

Prof. Muhairwa amesema Uongozi wa chou unathamini sana umuhimu wa michezo ndio maana imeweka mikakati mbalimbali ya kuboresha viwanja na kununua vifaa mbalimbali vya michezo kwenye kampasi zake zote ili wafanyakazi na wanafunzi washiriki vyema michezo.

‘’ Kutokana na idadi kuwa ya wanafunzi na wafanyakazi Chuo kinaendelea na jitihada za kuongeza viwanja vipya na vya kisasa ili kukidhi mahitaji na tayari kiwanja kipya cha mchezo wa kikapu cha kisasa Mkoani Morogoro tumemaliza kukijenga na sasa kinatumika hat ana watu wan je ya Chuo” alifafanua Prof. Mhairwa.

Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa benki ya NMB kwa kufadhili mashindano hayo ya wafanyakazi kwa miaka minne mfululizo lakini akaomba wadau kuwaunga mkono kwa kujitokeza kufadhili mashindano ya wanafunzi ili ambayo ni mikubwa na yenye mvuto sana.

Kwa upande wake Muwakilishi wa banki ya CRDB Bi. Isabela Kitila ambaye ni meneja wa tawi la CRDB SUA ameshukuru uongozi wa SUA kwa kuendelea kuwashirikisha katika michezo hii kwa miaka minne mfululizo kama wadhamini wakuu na kuahidi kuendelea kudhamini kila mwaka.

Isabela amesema kuwa michezo hiyo imewafanya wana CRDB na wanajumuiya wa SUA kuishi kama ndugu na familia kwakuwa michezo imekuwa ikiwaunganisha kwa njia mbalimbali na kufahamiana ikizingatiwa idadi kubwa ya wafanyakazi wa SUA waliopo bila michezo isingekuwa rahisi.

“Niwahakikishie kuwa sisi kama CRDB mlipo tupo na tutaendelea kuwepo katikati yenu kwenye kushiriki michezo hii na mambo mengine hivyo karibuni sana kwenye benki yetu muweze kupata huduma pia za kibenki mbalimbali kulingana na mahitaji yenu maana sisi na nyinyi ni familia moja” alisistiza Isabela.

Nae Menejea wa Benki ya CRDB Tawi la Wami Bw. Harold Lambileki amesema ndio mara ya kwanza kushiriki kwenye michezo hiyo hivyo wamekuja kujifunza kuona kinachofanyika ili na wao waweze kushiriki kikamilifu kama wadau muhimu wa michezo nchini.

Amesema Wanamichezo ndio wateja wa huduma za benki hiyo watahakikisha kwenye michezo ijayo nao wanakuwa sehemu ya wadhamini wa michezo hiyo muhimu ya wafanyakazi lakini pia kwenye michezo mingine ili kusaidia kuboresha afya na kuimarisha undug una ushirkiano.

Michezo hiyo ya wafanyakazi wa SUA ilianza miaka minne iliyopita na imekuwa ikishidanisha wafanyakazi wote kwenye michezo mbalimbali 20 na mwisho wa michezo hiyuo zawadi mbalimbali zinatolewa ikiwemo vikombe,medali na fedha taslimu wa washindi.

Thursday, November 12, 2020

MTATURU AANZA AWAMU YA PILI KWA KISHINDO AUZA VITABU VYA SH.MILIONI 28 NA KUTOA PIKIPIKI SITA

Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu, akimkabidhi  Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi Kitabu cha Misemo na Methali za Wanyaturu katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika mjini hapa jana. 
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Singida, Alex Mkumbo, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Uzinduzi ukiendelea.
Mbunge wa Iramba  Mwigulu Nchemba,  akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Ni furaha tupu wakati wa uzinduzi wa kitabu hicho.
Mbunge wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu,akinunua moja ya kitabu hicho kwa sh.milioni moja.
Burudani ikitolewa kwenye uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida.


MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu ameanza kazi kwa kishindo  katika kipindi chake cha awamu ya pili  kwa kuzindua kitabu na kufanikisha kununuliwa kwa thamani ya sh.milioni 28.

Kitabu hicho kinachoitwa Misemo na Methali za Wanyaturu kilichoandikwa na Mchungaji Dkt.Syprian Yohana Hilinti (PhD) kilizinduliwa jana katika Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Singida mjini na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwepo Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi huku mshereheshaji wa hafla ya  uzinduzi wa kitabu hicho akiwa ni Mbunge wa Iramba,  Mwigulu Nchemba.

Katika uzinduzi huo Mtaturu ambaye alikuwa mgeni rasmi alinunua kitabu kimoja kwa sh.milioni moja jambo lililoongeza ari ya watu waliokuwepo kwenye hafla hiyo kujitokeza na kununua vitabu hivyo kwa fedha taslimu.

Katika hatua nyingine Mtaturu alinunua pikipiki sita kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za kanisa hilo mkoani humo ambapo pia Mbunge wa Iramba Mwigulu Nchemba alichangia pikipiki tatu jumla zikiwa tisa.

Askofu wa kanisa hilo Mkoa wa Singida, Alex Mkumbo aliwashukuru wabunge hao kwa msaada huo.

Tuesday, November 10, 2020

TAKWIMU ZAIPAISHA TANZANIA UCHUMI WA KATI -SERIKALI

 


 A

A     Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi (aliyesimama) akitoa ufafanuzi kwenye mkutano wa uelimishajiwa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata ya Muhamo, Mkoani Singida hivi karibuni(Pichana John Mapepele).

B

A.      Bibi Salma Mkumbo akiuliza swali kwa wataalamu kwenye mkutano wa uelimishaji wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata yaMuhamo, Mkoani Singida hivi karibuni (Pichana John Mapepele).

c

A.      Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (aliyesimama) akitoa ufafanuzikwenye mkutano wa uelimishaji wa zoezi la ukusanyaji wa takwimu za mifugo,kilimo na uvuvi katika Kijiji cha  Msikii, Kata yaMuhamo, Mkoani Singida hivi karibuni(Pichana John Mapepele).

DMeneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo( aliyesimama) akitoa maelezo kwa  katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi (mwenye miwani) na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa (hayupo pichani) kwenye ofisi ya Serikali ya kijiji cha Msikii, Kata yaMuhamo, MkoaniSingidaHivikaribuni(Pichana John Mapepele).
E
Elibariki Musa, Mkazi wa kijiji cha Msikii Kata ya Muhamo, Mkoani Singida akiuliza swali kwa wataalamu  (Pichana John Mapepele)


Na John Mapepele, Singida 

Serikali imesema takwimu sahihi zilizokusanywa kutoka kwenye sekta mbalimbali za kimkakati za Mifugo, Kilimo na Uvuvi nchini zimeifanya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuingia kwenye Nchi za Uchumi wa Kati duniani.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na ujumbe maalum wa kitaifa ulioongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Anjelina Lutambi wakati  walipokuwa wanakagua zoezi la kitaifa ya ukusanyaji taarifa za kina za Kilimo, Mifugo, ufugaji wa samaki Mkoani Singida ambalo  limekamilika  hivi karibuni kwa mafanikio makubwa.

“Madhumuni makuu ya Sensa hii ni kupata taarifa muhimu za kilimo, mifugo na uvuvi zitakazotumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ya sekta katika taifa la Tanzania, na endapo ukusanywaji wa takwimu utakuwa kwenye ubora unaositahili utasaidia kulifanya taifa kupea kwenye uchumi wa juu kabisa katika kipindi kifupi kijacho” ameongeza Dkt. Chuwa

 

Akifafanua amesema taarifa  kwa mfano za magonjwa ya mifugo na mazao zitaisaidia Serikali kuainisha maeneo yanayokabiliwa na visumbufu/magonjwa  ili kuchukua hatua stahiki na kupanga mipango ya kudhibiti.Pia taarifa kuhusu uzalishaji wa mazao zitasaidia kujua kiasi cha uzalishaji kwa maeneo husika na kuiwezesha Serikali kupanga upatikanaji wa masoko na uwezekano wa kuanzisha viwanda vya kusindika mazao hayo.

 

Aidha amesema taarifa kuhusu upatikanaji na matumizi ya ardhi zitatumika kupanga mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini  hivyo zitatumika kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji hapa nchini.

 

Dkt. Chuwa ameongeza kuwa matokeo ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi yanatarajiwa kuweka msingi imara wa sekta hii kwa miaka mingi iyajo, kwa  kuwa Sekta ya Kilimo ina umuhimu mkubwa  kwenye mustakabali wa maisha ya binadamu kwa kuwa ndiyo chanzo cha chakula na malighafi zinazohitajika katika viwanda hususani katika awamu hii inayoongozwa na dira ya uchumi wa viwanda.

 

“Kutokana na umuhimu huo, na kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia ya Mwaka 2030, Sekta ya Kilimo ilipewa Lengo la Pili  la Kutokomeza Njaa, Kuwa na Uhakika wa Chakula, Lishe Bora na Kukuza Kilimo Endelevu. Aidha, lengo hilo limesisitiza umuhimu wa kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao na pia kusisitiza matumizi bora ya ardhi na kurutubisha udongo, ili kuongeza uwezo wa binadamu kukabiliana na kuhimili mabadiliko ya tabianchi na athari zake yakiwemo majanga mbalimbali kama mafuriko na ukame pamoja na majanga mengine ikiwemo ndege waharibifu” ameeleza Dkt. Chuwa

   

Dkt. Lutambi amesisitiza kuwa pamoja na faida za jumla ambazo mkulima atakazozipata Sensa hii itamsaidia mtu mmoja mmoja kutatua changamoto mbalimbali katika kilimo,mifugo na uvuvi hasa upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani, upatikanaji wa masoko kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Ameongeza kuwa takwimu ni kitu cha msingi katika kupanga maendeleo kuanzia kwenye ngazi ya kijiji hadi taifa kwa kuwa zinasaidia kuonyesha changamoto na mafanikio na hivyo kusaidia kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto hizo.

“Ni muhimu tukafahamu kuwa takwimu sahihi za mifugo, mazao na uvuvi zitasaidia  uchangiaji wa malighafi za  viwanda  vyetu hivyo kukuza uchumi wetu ambao tunautaka wa viwanda” amesisitiza Dkt. Lutambi

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe, kwenye hotuba yake, wakati  wa ufunguzi wa mafunzo ya wadadisi wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, iliyofanyika katika Ukumbi wa TMDA,Mwanza Julai, 25 mwaka huu alisisitiza Mwaka huu 2020, Benki ya Dunia imeitangaza Tanzania kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa kipato cha kati, ambapo alisema Taarifa hizi zimeleta faraja kubwa kwa sekta ya kilimo  kwa kuwa ndiyo iliyotoa mchango mkubwa zaidi katika Pato la Taifa wa asilimia 26.6 mwaka 2019 na pia inatoa ajira kwa takribani asilimia 66 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi.

 

“Sekta ya kilimo ilichangia asilimia 24.3 ya mapato ya mauzo nje ya nchi mwaka 2019. Fedha hizi kwa kiasi kikubwa zinatumika nchini katika mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi ya barabara, reli, maji, usambazaji umeme na kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za jamii kama vile afya na Elimu kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya wananchi” alifafanua Dkt. Bashe

 

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa Ripoti ya Tathmini ya Umasikini Tanzania Bara ya Mwaka 2018, sekta hii ikiendelezwa vyema ndio pekee yenye uwezo wa kuleta maendeleo jumuishi nchini, hivyo  kuna umuhimu mkubwa wa zoezi la sensa ya mifugo, mazao na uvuvi likafanyika kwa ubora na kwa umakini  unaositahili.

 

Pia wakati wa tukio la uzinduzi wa mafunzo ya wadadisi wa Sensa hii, Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Amina Msengwa amesisitiza kuwa takwimu zina mchango mkubwa katika maandalizi na utekelezaji wa sera na mipango, na vile vile katika kufanya maamuzi sahihi yanayotakiwa kufikiwa kwa kutumia ushahidi stahiki (evidence based decision making).

 Amesema Sensa ya Mwaka wa Kilimo 2019/20, ni ya tano kufanyika hapa nchini tangu nchi ipate uhuru na inafanyika kwenye jumla ya maeneo yaliyochaguliwa ya kuhesabia2,820 ambapo kutokana na maeneo hayo kaya 33,807 kutoka Tanzania bara na Zanzibar.

Kwa upande wake, Meneja Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Mkoa wa Singida, Naing’oya Kipuyo ameishukuru Serikali ya Mkoa wa Singida kwa kusaidia kufanikisha zoezi hili ambalo  limefanyika kwa takribani siku 50 ambapo pia amewapongeza wananchi kwa kutoa ushirikiano wa  kutosha.

 

 Kipuyo amesema taarifa zilizokusanywa kwenye Sensa hii ni za kipindi cha kuanzia tarehe 1 Oktoba, 2019 hadi tarehe 30 Septemba, 2020 na kuongeza kuwa Mkoa wa Singida umekamilisha zoezi hilo kwa maeneo yote ambapo maeneo madogo ya kuhesabia watu yaani Enumaration Areas (EA) 90 yenye kaya 1087 zilizochaguliwa kwa ajili ya kufanyiwa sensa hii zilifikiwa

Monday, November 9, 2020

WAFANYAKAZI WA BENKI YA I&M WAMEJITOLEA KUELIMISHA JAMII JUU YA MAMBO YA FEDHA NA UWEKAJI AKIBA KWA WANAWAKE NA VIJANA WAJASIRIAMALI

 

Timu ya wafanyakazi wa benki ya I&M waliovalia t-shirt za blue wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha wanawake wajasiriamali kilichopo Yombo vituka walipoenda kutoa elimu ya bure kuhusu usimamizi wa fedha na ujasiriamali

Peter Joseph meneja msaidizi idara ya rasilimali watu akitoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake walioudhuria katika mafunzo hayo, Yombo jijini daresalaam.

Timu ya wafanyakazi wa benki ya I&M waliovalia t-shirt za blue wakiwa katika picha ya pamoja na kikundi cha wanawake wajasiriamali kilichopo Yombo vituka walipoenda kutoa elimu ya bure kuhusu usimamizi wa fedha na ujasiriamali

Mmoja wa wanawake walioudhuria katika mafunzo hayo, Bi. Eva Tumaini akizungumza na waandishi kuipongeza benki ya I&M kwa kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali kwa jamii


Baadhi ya wafanyakazi wa benki ya I&M wakishirikiana na mmoja wa wanawake katika kufundisha mbinu za biashara ili kujikwamua kiuchumi kupitia mapishi.
 
                                                  ..................................................................
 


 Dar es salaam.

Benki ya I&M Tanzania yaanzisha mpango wa ‘IM FOR YOU’ ambao ni moja ya njia ya wafanyakazi wa benki hiyo kurudisha kwa jamii kwa kujitolea elimu bure kuhusu mambo mbalimbali ya kibenki ikiwemo maswala ya matumizi ya fedha, uwekaji akiba na ujasiriamali.

Siku ya Ijumaa Novemba 6, wafanyakazi wa Benki ya I&M wakiongozwa na Meneja Masoko na Mawasiliano ya Benki, Bi. Anitha Pallangyo, Meneja Msaidizi wa idara ya Rasilimali watu, Elimu na Maendeleo Bw. Peter Joseph, Bi. Hellen Mbwana kutoka idara ya ukaguzi wa ndani na wafanyakazi wengine waliotoka katika matawi ya hapa Dar es Salaam na idara nyingine mbalimbali ndani ya benki hiyo, walitembelea vikundi vya kina mama wajasiriamali wadogowadogo waliopo maeneo ya Yombo vituka jijini Dar es salaam, na kutoa elimu ya kuhusu mambo ya fedha, uwekaji akiba na ujasiriamali kwa wakina mama hao waliokusanyika kujipatia elimu hiyo.

Akielezea lengo la kuanzisha mpango huu wa ‘IM FOR YOU’ unaomaanisha ‘I&M Kwaajili yako’, wa kutoa elimu bure kwa jamii na lengo la kutembelea vikundi hivyo vya wakina mama vilivyopo maeneo ya Yombo Vituka, Bi. Anitha Pallangyo alisema, “Tumeazisha mpango huu kama moja ya njia ya kurudisha kwa jamii kile ambacho timu yetu ya rasilimali watu imekipata kutoka kwenye kazi zetu za kila siku, na kama tunavyojua kuwa elimu ni ufunguo wa maisha, hivyo tumeona ni vyema kukutana na vikundi mbalimbali vya wakina mama na vijana hasa ambao wanajishughulisha na biashara ndogondogo kujikwamua kiuchumi, ili kuwaongezea ujuzi na mbinu za kuongeza kipato. Mpango huu utasaidia hata serikali kupunguza idadi ya watu ambao hawajaajiriwa kwani unalenga kumfungua kijana na watanzania kwa ujumla kubuni mbinu mbalimbali za kibiashara ili kuweza kujiajiri.

Bw. Peter Joseph, Meneja Msaidizi idara ya rasilimali watu akiongea na waandishi katika tukio hilo alisema Benki ya I&M inajitahidi kuajiri wafanyakazi wenye uwezo mkubwa na ufanisi wa kazi, pamoja na kuwawezesha kuongeza ujuzi kupitia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya ofisi hivyo imezalisha vijana wanaoweza kutoa elimu bora kwa jamii hasa kwa mambo ya fedha, umuhimu wa kujiwekea akiba na ujasiriamali.

Pamoja na kutoa elimu kwa jamii, timu hiyo ya wafanyakazi wa benki ya I&M ambayo ilienda kuwakilisha wafanyakazi wote kutoka idara mbalimbali, ilipeleka vitu mbalimbali ambavyo wafanyakazi walijitolea kwaajili ya kina mama wanaoishi kwenye mazingira magumu kama vile wajane, wamama wanaolea watoto yatima, na walemavu kwenye jamii hiyo, vitu hivyo ni pamoja na nguo, viatu, vyakula, sabuni, dawa za mswaki nakadhalka.

Benki ya I&M imekua mstari wa mbele katika kujitolea kwa jamii kupitia mikakati mbalimbali ya elimu, afya na mazingira. Benki hiyo inatoa huduma mbalimbali za kibenki kwa wananchi wote kwa ujumla ikiwemo akaunti za akiba za watoto, wanafunzi, wafanyabiashara, wanawake, mikopo, huduma za kuhamisha fedha, huduma za kubadili fedha za kigeni nakadhalika.  Benki hiyo inatarajia kuanzisha huduma za WAKALA hivi karibuni ambapo inategemea kuwa na  mawakala walioenea Dar es salaam na mikoani, pia ina matawi yanaoendelea kutoa huduma bora ambayo ni;Tawi la maktaba, tawi kuu linalo patikana mtaa wa Indira Gandhi, Kariakoo, Nyerere, Oysterbay, Moshi, Arusha na Mwanza. Pia kupitia huduma zake za benki kwa njia ya simu (Mobile Banking) *150*32#, kwa njia ya mtandao (Internet Banking) na App, wateja wake wanaweza kupata huduma za kibenki  saa 24 mahali popote wowote

Friday, November 6, 2020

WoLaOTa: MAGUFULI TUKUMBUKE KWENYE NAFASI ZA UWAKILISHI BUNGE LIJALO


Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Kuimarisha Maadili na Usaidizi kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi (WoLaoTa), Samwel Olesaitabau Lukumay , akizungumza na waandishi wa habari jana (hawapo pichani) kuhusu Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwakumbuka wastaafu walau kwa nafasi 2 za uwakilishi kwenye Bunge lijalo.


Na Godwin Myovela, Singida


TAASISI ya Kuimarisha Maadili katika Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi Tanzania (WoLaOTa) imemsihi Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwakumbuka wastaafu walau kwa nafasi 2 za uwakilishi kwenye Bunge lijalo.

Akizungumza na vyombo vya habari  mkoani hapa jana, Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo, Samwel Olesaitabau  alisema kwa kufanya hivyo ni dhahiri atakuwa ameonyesha ishara ya kutambua mchango mkubwa uliotolewa, na unaoendelea kutolewa na wastaafu kama hazina katika ujenzi wa Taifa. 

"Kwanza itakuwa ni asante kwa wastaafu, lakini itapendeza zaidi sauti ya kundi hili muhimu ikawakilishwa pale bungeni kwa ustawi na maslahi mapana ya wastaafu wote," alisema Olesaitabau.

Akizungumzia hali ya uchaguzi mkuu uliopita, aliwapongeza watanzania kwa utulivu na ukomavu wa kisiasa walioonyesha katika kipindi chote cha mchakato wa zoezi hilo.

Aidha, kwa namna ya pekee alivipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi kwa namna walivyoonesha weledi wa hali ya juu kwenye kuimarisha amani na utulivu, wakati wakitekeleza majukumu yao.

Alisema kama Taasisi isiyo ya kiserikali inayoshughulikia maadili kwa watumishi, inatoa pongezi za dhati kwa ushindi wa kishindo na heshima alioupata Rais Magufuli na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kipindi kingine cha awamu ya pili.

Olesaitabau aliwakumbusha viongozi hao wakuu, akiwemo Rais wa Zanzibar Dkt. Ally Hussein Mwinyi kwamba ushindi walioupata ni deni ambalo malipo yake ni kuonyesha kwa vitendo utumishi uliotukuka kwa mustakabali chanya wa 'Maendeleo ya Tanzania'.

Aidha, kwa upande wa vyama vya upinzani, Taasisi hiyo imevitaka kutafakari kwa kina na hatimaye kuutambua ushindi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

"Sio vema na wala haina afya kuanza kutunishiana misuli na vyombo vya dola. Hata uwanjani Refarii akishatoa ushindi kwa timu A, basi ile timu B kama haikuridhika wanaenda kwenye vyombo vya kutoa haki ili wapewe haki hiyo".

Pia viongozi wetu wakuu kama wazazi na walezi ifike mahali wakubali kukaa meza moja na wapinzani ili kuchambua na kurekebisha changamoto zilizojitokeza ili kuleta ustawi na tija kwa mwendelezo wa amani iliyopo, lakini pia kutoa fursa kwa vyama vyote kujipanga vema kwa chaguzi zijazo." alishauri Olesaitabau


Thursday, November 5, 2020

TAMUFO YAMPONGEZA RAIS DKT. JOHN MAGUFULI KWA KUCHAGULIWA TENA

  
Rais mpya wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) Erick Kisanga akizungunza na waandishi wa habari jijini Arusha muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuapishwa rasmi kuongoza tena kipindi cha miaka mitano katika sherehe iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. Kushoto ni Katibu wa Umoja huo, Stellah Joel.
Katibu wa Umoja huo, Stellah Joel (kushot), akizungumza katika mkutano huo.
 


Na Dotto Mwaibale

UMOJA WA Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) umempongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuongoza nchi kwa kipindi cha miaka mingine mitano kuanzia leo baada ya kuapishwa.

Pongezi hizo zimetolewa na Rais mpya wa umoja huo Erick Kisanga wakati akizungunza na waandishi wa habari jijini Arusha muda mfupi baada ya Rais Magufuli kuapishwa rasmi katika sherehe iliyofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

"Rais Magufuli amekwisha apishwa kwa ajili ya kuwaongoza watanzania kwa kipindi kingine cha pili sisi wanamuziki tunakila sababu ya kumpongeza" alisema Kisanga.

Kisanga alisema kuchaguliwa kwake kwa kishindo kunatoka na imani ya wananchi waliyokuwa nayo katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano ambayo amefanya mambo makubwa ya mandeleo hapa nchini katika maeneo mbalimbali.

Kisanga alitaja baadhi ya mambo aliyoyafanya kuwa ni  umeme, miundombinu ya barabara, shule, ujenzi wa reli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa vivuko, ujenzi wa zahanati na hospitali pamoja na miradi mingine mingi.

"Kutokana na kazi hiyo kubwa aliyoifanya wananchi wakiwepo wanamuziki walikuwa na kila sababu ya kumchagua kwa kura nyingi" alisema Kisanga.

Kisanga alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wananchi, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na vyombo vya usalama kwa kusimamia uchaguzi huo ambao ulifanyika kwa amani na utulivu. 

Katibu wa Umoja huo, Stellah Joel aliwaomba wanamuziki kuendelea kutunga na kuimba nyimbo za kuhamasisha maendelea ya nchi ikiwa ni kuunga mkono jitihada za maendeleo za Rais Dkt.John Magufuli kuanzia awamu yake ya kwanza na hii ya pili ambayo ameianza leo.

Joel aliwataka wanamuziki kote nchini kubuni miradi mbalimbali kama kilimo, ufugaji, viwanda vidogo vya ushonaji na ujasiriamali wa aina tofauti ili kujiongezea kipato badala ya kutegemea muziki pekee.

"Wanamuziki tumekuwa na changamoto nyingi za maisha na hii inatokana na kujikita katika eneo moja la kufanya muziki tu bila ya kuchanganya na fursa nyingine ebu tuamke sasa tujikomboe serikali yetu sikivu ikiona jitihada zetu itatuunga mkono kwa kutupa maeneo ya kuanzisha kilimo na mtaji pia" alisema Joel.

Monday, November 2, 2020

BODABODA SINGIDA WATOA TAMKO KALI KUELEKEA KUAPISHWA RAIS DKT JOHN MAGUFULI

 

Mwenyekiti wa madereva na wamiliki wa Bajaji na bodaboda Manispaa ya Singida Ahmed Juma akitoa ufafanuzi wa tamko la kulaani vijana wanaotaka kufanya vurugu
Dereva wa Bodaboda Manispaa ya Singida Ramadhani Zuberi akitoka ufafanuzi kwa waandishi ambao hawapo pichani kupinga na kulaani maandamano ya vijana ambao wanataka kutumika kuvuruga amani 
Sehemu ya madereva wa bodaboda Manispaa ya Singida 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Wamiliki na Madereva wote wa Bajaji Mkoa wa Singida wametoa tamko rasmi la kulaani baadhi ya vijana ambao wameanza kutumiwa na baadhi ya vyama vya upinzani kuandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba 28, Mwaka huu.

Akitoa  tamko  kwa  niaba ya wanachama 2000 wa  Mkoa wa Singida  kwenye Kituo cha Bajaji Soko Kuu la Mjini Singida, Mwenyekiti wa Madereva na Wamiliki wa Bajaji na Boda boda Manispaa ya Singida, Ahmed Juma amesema  umoja wao umepinga njama  zinazofanywa na  baadhi ya  vyama  ya kuwatumia madereva  hao na kusisitiza kuwa njama hizo hazitafanikiwa katika Mkoa  wa Singida .

“Tumejipanga kukabiliana na uhuni wowote ambao umepangwa kufanywa kwenye kipindi  hiki na baadhi ya wahuni wachache wasioitakia mema nchi yetu, tunaomba  vyombo vya ulinzi visimamie hili kikamilifu na sisi tupo nyuma yao” aliongeza Juma

Amesema kinachotaka kufanyika sasa baada ya  uchaguzi kukamilika na matokeo kutangazwa  kwa kufuata taratibu zote za uchaguzi na Mamlaka halali ni  vurugu na uvunjifu wa amani jambo ambalo amesema halikubaliki badala yake amewasihi wananchi wafanye kazi  ili  kuiletea nchi yetu maendeleo  zaidi katika awamu ya sasa.

Amemwomba Rais, John Pombe Joseph Magufuli  kuendelea kuiletea maendeleo Tanzania ili itoke kwenye Uchumi wa Kati hadi Uchumi wa juu kabisa  na hatimaye  kuboresha maisha  ya watanzania wote.

Mwenyekiti wa Madereva wa Boda boda  wa  eneo  la Soko Kuu Mjini Singida, Kulwa Moshi ameonya madereva wa Bodaboda ambao kwa namna moja au nyingine  watatumika katika kuvunja Sheria za nchi kwa kupanga  njama za kufanya maandamano  yasiyo ya amani.

Moshi ameongeza kuwa wananchi wameamua kuwachagua viongozi wanao wapenda hivyo hakuna sababu ya watu kuandaa njama za kupinga matokeo ya uchaguzi.

Naye Ramadhani  Zuberi,  Dereva wa  Bajaji kwenye  Kituo Kikuu cha Mabasi  ya Mkoa wa Singida amepongeza Serikali kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu kwa uwazi  ambao umeweza kufuata taratibu zote na kutoa matokoa kwa wakati

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Nchini (NEC), Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuapishwa Novemba 5 Mwaka huu kwenye uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.