Friday, January 8, 2021

HALMASHAURI ZASHAURIWA KUTUMIA BMU KUKUSANYA MAPATO YA UVUVI

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) inayojengwa katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo jana.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU), Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo, Isihaka Hudi (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Ofisi ya BMU hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akitoa maelekezo kwa Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila ( kulia) alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya Kikundi Cha Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) katika kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo.

 


Na Mbaraka Kambona, Bagamoyo.

 

Mratibu wa Mradi wa Usimamizi wa Rasilimali za Bahari Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFish), Dkt. Nichrous Mlalila ameziomba Halmashauri kuvitambua Vikundi vya Ulinzi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi (BMU) na kuzipa uwezo wa kukusanya mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi ili ziweze kusaidia vikundi hivyo kujiendesha na kuendeleza sekta ya uvuvi nchini. 

Dkt. Mlalila alitoa rai hiyo katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa ofisi ya BMU inayojengwa na Mradi wa SWIOFish katika Kata ya Dunda, Wilayani Bagamoyo jana. 

Kwa mujibu wa Dkt. Mlalila sehemu kubwa ya mapato yanayokusanywa kwa sasa na Halmashauri hayarudishwi kwa Jamii ya wavuvi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za sekta na uchumi wa jamii husika. 

Dkt. Mlalila alisema anatambua kuwa kuna changamoto ya kisheria ambayo baadhi ya Halmashauri zimetumia kuzizuia BMU kukusanya mapato yanayotokana na rasilimali za uvuvi. 

“Tunahamasisha Halmashauri kuwapa uwezo BMU kukusanya mapato ili kuziwezesha kupata kipato cha uhakika cha kuendesha shughuli zao za kulinda rasilimali za Uvuvi lakini pia mapato hayo yatawezesha kuendeleza sekta ya uvuvi tofauti na ilivyo sasa,” alisema Dkt. Mlalila. 

Katika baadhi ya Halmashauri ambazo wamewapa kazi BMU ya kukusanya mapato kama vile Halmashauri ya Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga, Mapato yanayotokana na uvuvi yameongezeka kutoka shilingi milioni 9 kwa robo mwaka hadi milioni 51 na kutoka shilingi milioni 36 hadi milioni 256 kwa mwaka. 

“Nazishauri Halmashauri nyingine zichukue mfano wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani kwa sababu sisi tumezipa mafunzo ya kina hizi BMU katika kusimamia fedha na ukusanyaji wa mapato, hivyo tunaamini hilo ni suala la mchakato na tumewasilisha andiko TAMISEMI ili kuangalia namna ya kuzifanya BMU kuendelea na shughuli zake hata pale ambapo mradi wa SWIOFish utakapokwisha muda wake,” aliongeza Dkt. Mlalila. 

Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alisema kuwa BMU ya kata ya Dunda na zingine zikajifunze Pangani kuona wao wanafanyaje na sisi kama Wizara tutaangalia kama kuna chanzo ambacho wataalam wa Halmashauri wanakusanya na hakifanyi vizuri na kuna BMU mahali inakusanya vizuri basi tutaibua hiyo hoja tuone tutafanyaje. 

“Ukweli ni kwamba kwenye vyanzo hivi vya leseni na ushuru wa rasilimali za uvuvi katika halmashauri zetu nyingi hazifanyi vizuri na hivyo kuna haja ya kuviangalia vizuri hasa wataalam wetu wanaotumika kukusanya hayo mapato kwa sababu kuna baadhi yao wamefanya hapo ndio maeneo yao ya kupatia pesa zao,” alisema Gekul. 

Alisema Wakurugenzi wanaweza kuwa na nia njema kabisa lakini wale wanaotumwa kukusanya hayo mapato wanarudisha maduhuli hayo kama walivyotumwa? Kama kuna watu wanauwezo wa kukusanya zaidi ya wataalam wa Halmashauri sidhani kama kuna haja ya kuwa na kigugumizi cha kuwatoa hao watu ili kazi hiyo apewe anayeweza kukusanya vizuri. 

“Kwa sababu mwisho wa siku sisi wananchi tunachotaka ni maendeleo hivyo nisingependa niseme moja kwa moja hapa kuwa BMU wapewe kazi hiyo isipokuwa Halmashauri ziangalie kama sheria inawaruhusu kuwatumia BMU kukusanya mapato,” aliongeza Gekul. 

Gekul alisema kuwa wao kama Wizara watawasiliana na TAMISEMI kuona maelekezo yakoje kwa sababu anasema kuna vyanzo Halmashauri zenyewe zinakusanya na vingine vinaruhusiwa kukusanywa na wakala na pale ambapo BMU itaonekana inafaa ipewe uwezo wa kukusanya. 

Mradi wa SWIOFish unafadhiliwa na Benki ya Dunia kuhamasisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za bahari na ndio umeimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari (BMU) kwa ajili ya kulinda na kuhamasisha uvunaji endelevu wa rasilimali za bahari katika Wilaya za Mkinga, Pangani, Bagamoyo, Lindi Vijijini na Tanga Jiji.

Wednesday, January 6, 2021

VIJANA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA UFUGAJI SAMAKI KATIKA MABWAWA


Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI), Dkt. Ismael Kimerei (kulia) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam jana. Wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Mradi wa SWIOFish, Dkt. Nichrous Mlalila. 

Mshauri wa Uvuvi kutoka Japan, Koji Hase (kushoto) akimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul(kulia) baadhi ya taarifa kuhusu uvuvi alipotembelea Shirika la Uvuvi la Tanzania (TAFICO) lililopo jijini Dar es Salaam Jana.

Afisa Uzalishaji Vifaranga, Kampuni ya Bigfish, Pastory Aloyce (kushoto) akifafanua jambo kuhusu ufugaji wa samaki kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul alipotembelea eneo la ufugaji wa samaki la kampuni hiyo iliyopo Wilayani Kigamboni, jijini Dar es Salaam Jana. 

 

Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewahimiza vijana kujihusisha na ufugaji wa samaki katika mabwawa huku akisema fursa hiyo itawaokoa vijana wengi kuondokana na kilio cha ukosefu wa ajira nchini. 

Gekul aliyasema hayo alipotembelea Kampuni ya ufugaji wa Samaki inayojulikana kwa jina la Bigfish iliyopo Wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Jana. 

Alisema kuwa muelekeo wa Serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa samaki katika mabwawa kwasababu uvuvi wa kutegemea maji ya asili umekuwa mkubwa na kupelekea kupungua kwa rasilimali za uvuvi, hivyo kimbilio pekee ambalo litawawezesha vijana wengi kupata ajira ni ufugaji wa samaki katika mabwawa. 

Aliongeza kuwa Serikali ipo mbioni kuweka miongozo na kanuni za ufugaji huo ili kuwalinda na kuwawezesha wafugaji waweze kufuga vizuri na kwa kuzingatia taratibu zitakazowekwa. 

“Serikali itawawezesha vijana kwa hali ya juu, kuwajengea mabwawa, kuwapatia mafunzo ya ufugaji bora wa samaki ili vijana wetu waweze kujikwamua na suala la ukosefu wa ajira,” alisema Gekul. 

Aliendelea kusema kuwa Rais, Dkt. John Magufuli aliahidi ajira zaidi ya milioni 8, moja ya sekta ambayo inategemewa kutengeneza ajira hizo ni ya uvuvi hivyo aliwahimiza vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujikomboa kiuchumi. 

Kuhusu uwezeshaji, Gekul aliziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 10 katika mapato yao kwa ajili ya kuwawezesha vijana na watu wenye Ulemavu ili waweze kufanya ufugaji katika mabwawa na kujipatia ajira.

Aidha, Gekul alisema kuwa anafahamu changamoto zinazokabili ufugaji wa samaki wa mabwawa ni pamoja na uhaba wa vifaranga vya samaki na ukosefu wa chakula cha kutosha na cha uhakika kwa ajili ya samaki hivyo alitumia fursa hiyo kuiagiza Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kutafuta muarobaini wa changamoto hizo ili kuwaondolea kero hiyo wafugaji. 

Aliongeza kuwa ufugaji wa samaki katika mabwawa utasaidia kupunguza kilio cha uhaba wa malighafi unaokabili viwanda vingi nchini huku akiongeza kuwa ufugaji huo pia utasaidia kupunguza uvuvi haramu kwa sababu watu watakuwa na chanzo mbadala cha kujipatia kipato.

 


GEKUL ‘AWASHUKIA’ MAAFISA UVUVI WANAOSHIRIKIANA NA WAHALIFU

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akikagua moja ya  nyavu inayozalishwa katika Kiwanda cha kutengeneza nyavu za kuvulia Samaki, Nyamagara kilichopo Chanika, jijini Dar es Salaam alipokitembelea Januari jana.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wakwanza kushoto) akiwaeleza jambo Wanafunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Mifugo (LITA) alipotembelea maabara wanayoitumia wanafunzi hao kuchunguza magonjwa ya mifugo jijini Dar es Salaam Jana. Katikati ni Mtendaji Mkuu, Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene.
Wafanyakazi wa Kiwanda cha kuchakata Samaki, Alpha wakimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa kwanza kulia) Minofu ya Samaki aina ya Pweza ambayo imechakatwa katika Kiwandani hicho kilichopo jijini Dar es Salaam. Naibu Waziri alikitembelea kiwanda hicho Jana.


 

Na Mbaraka Kambona,

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amesema kuwa hakuna haja ya kuendelea kuwa na Maafisa Uvuvi ambao wanashirikiana na wahalifu kufanya vitendo vya hujuma wakati kuna vijana wengi wenye nia njema ya kulitumikia Taifa wanahangaika na ajira. 

Gekul aliyasema hayo alipotembelea Kiwanda cha kuchakata samaki, Alpha kilichopo Vingunguti jijini Dar es Salaam Jana. 

Kwa mujibu wa Gekul sehemu kubwa ya upungufu wa rasilimali za uvuvi unachangiwa na baadhi ya Maafisa Uvuvi ambao sio waaminifu ambao wamekuwa wakishirikiana na wahalifu kufanya uvuvi usioendelevu unaopelekea kupungua kwa samaki. 

“Tulikuwa Kanda ya ziwa, na hapa pia kilio ni hicho hicho malighafi, malighafi zinapungua kwa sababu baadhi ya maafisa uvuvi wanashiriki katika vitendo vya uvuvi haramu, wanashirikiana na wahalifu, hata pale ambapo vyombo vya ulinzi na usalama vinapotaka kufanya operesheni ya kuwakamata wahalifu wamekuwa wakitoa taarifa kwa wahalifu hao kama ambavyo ilitokea hivi karibuni kule Wilayani Babati,”alisema Gekul. 

“Kwa nini tuendelee na watu wa namna hii wakati kuna vijana wengi wenye nia njema na taifa lao wapo huko nje hawana ajira na huku ndani ya serikali kuna baadhi ya watu wanahujumu taifa na uchumi wa nchi, hatuna haja kuendelea kuwa na watu kama hawa,” alisisitiza Gekul. 

Aliendelea kusema kuwa itakuwa aibu wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza hapa nchini halafu washindwe kuendelea na uzalishaji kwa kukosa malighafi kutokana na kushindwa kudhibiti uvuvi haramu.

Aliongeza kuwa wawekezaji ni muhimu kwa uchumi wa taifa kwa sababu wanalipa kodi na tozo mbalimbali ambazo zinasaidia kukuza pato la taifa, uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa vijana. 

Aidha, aliwataka maafisa hao ambao wanaojihusisha na vitendo hivyo kujirekebisha na washirikiane kwa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama ili kwa pamoja waweze kukomesha vitendo hivyo kwa lengo la kunusuru rasilimali za uvuvi. 

“Tutimize wajibu wetu tukijuwa kuwa uvuvi haramu ukiendelea tutaviua hivi viwanda na matokeo yake ajira nazo kwa vijana wetu zitapotea,” alieleza Gekul. 

Gekul aliwataka maafisa uvuvi wote nchini kuendelea kuchukua hatua za haraka kudhibiti hali iliyopo ya upotevu wa rasilimali za uvuvi katika maeneo yote yalipo maji na maziwa. 

Awali, Meneja wa Uzalishaji wa Kiwanda cha Alpha, Sreejish Srinivasan wakati akitoa taarifa ya uzalishaji wa kiwanda hicho alieleza kuwa changamoto kubwa wanayokumbana nayo ni uchache wa malighafi kwa ajili ya kuchakatwa kiwandani hapo na mpaka sasa wanafanya shughuli zao chini ya asilimia 15 ya uwezo wa kiwanda hicho. 


Monday, January 4, 2021

DC MPOGOLO MBIONI KUFUFUA RIADHA IKUNGI MKOANI SINGIDA

Mgeni rasmi wa ‘Kilimo Cup Kata ya Dung’unyi’ na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikagua Timu ya Dung’unyi FC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchuano wa fainali kati ya timu hiyo na Damankia FC jana. Dung’unyi FC ilitwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa kuilaza Damankia FC 2-1.
wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (katikati) akifuatilia fainali hiyo.
Matukio mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kwa mchuano huo.
Matukio mbalimbali yakiendelea kabla ya kuanza kwa mchuano huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikagua Timu ya Damankia FC muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchuano wa fainali kati ya timu hiyo na Dung’unyi FC.

Picha ya pamoja ya wachezaji na viongozi wa ngazi mbalimbali ndani ya Wilaya ya Ikungi , mkoani Singida waliohudhuria kabla ya kuanza kwa fainali hiyo jana.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (wa pili kutoka kushoto) akiwa na baadhi ya viongozi wa Kata ya Dung’unyi, kushoto ni mwanzilishi wa mashindano hayo ambaye pia ni Mtendaji wa Kata ya Dung’unyi, Yahaya Njiku, Mjumbe wa Kamati ya Siasa (CCM)Wilaya ya Ikungi, Salum Chima, na Afisa Kilimo wa Kata ya Dung’unyi Esther Bayda.
Mgeni rasmi akikabidhi zawadi ya fedha kwa mshindi wa pili ambaye ni Damankia FC .
Bingwa wa michuano hiyo Dung’unyi FC wakiondoka na mbuzi wao..
Mtendaji Kata Dung’unyi, Yahaya Njiku akizungumza. Kulia ni DC Mpogolo akifuatilia matukio hayo.

Fainali hizo zikiendelea.



Na Dotto Mwaibale, Singida


HATIMAYE michuano ya kusisimua ya Kombe la Kilimo ‘Kilimo Cup’ kata ya Dung’unyi wilaya ya Ikungi yamemalizika jana huku timu ya Dung’unyi FC ikiibuka mshindi kwa kujinyakulia zawadi ya Mbuzi na fedha taslimu baada ya kuichapa Damankia FC 2-1 kwenye fainali za mashindano hayo.

Kilimo Cup iliyoasisiwa na Mtendaji wa Kata hiyo Yahaya Njiku, ni miongoni mwa ligi za mpira wa miguu zilizokuwa na hamasa na mvuto wa aina yake, zikiambatana na shughuli mbalimbali za uelimishaji jamii kuhusu dhana ya kilimo bora-lengo hasa ni kuhamasisha vijana na watu wazima kushiriki kikamilifu katika shughuli za kilimo katika kipindi hiki cha msimu wa mvua.

Awali, kabla ya kufungua fainali hiyo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo, aliahidi kuboresha zaidi mashindano hayo kwa siku za usoni, na kuahidi kupanua wigo kwa kuyafanya kuwa katika ngazi ya wilaya, azma ikiwa ni kuzidi kutangamanisha wataalamu na jamii katika kuleta ustawi kwenye kilimo na ufugaji.

“Natamani ligi hii tungeianza mapema zaidi kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili kuongeza tija kwenye kilimo, nafahamu mashindano haya yamechagiza sana uelewa wa masuala ya kilimo kutoka kwa wataalamu kwenda kwenye jamii hatua kwa hatua,” alisema Mpogolo.

Aidha, kupitia michuano hiyo, aliagiza Watendaji wa Kata kuanza mara moja mchakato wa kufufua mchezo wa riadha kwenye maeneo yao na kuahidi kusimamia ipasavyo, shabaha kubwa ni kutaka kurudisha mchezo huo kwenye ‘pick’ kutokana na huko nyuma kuwa ni kati ya michezo iliyoipa heshima kubwa wilaya hiyo.

“Naagiza kila Tarafa, shule za Msingi na Sekondari kuwe na kituo cha mchezo wa riadha...nafahamu Ikungi ni mahiri sana kwenye riadha ni lazima tujipange kama wilaya kuhakikisha tunafufua mchezo huu na hatimaye hapo baadaye kuwezesha wachezaji wake kushiriki katika michuano ya kimataifa,” alisema Mpogolo

Katika hatua nyingine, alihamasisha wana-michezo hao kuhakikisha wanajiunga kwenye vikundi ili kunufaika na fursa za mikopo ya halmashauri, sambamba na kuongeza tija ya wingi wa uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo iliyopo, ili kukidhi hitaji kubwa la soko lililopo katika jiji jirani la Dodoma na kwingineko nchini.

Kwa upande wake, mwanzilishi wa mashindano hayo Njiku alisema mashindano hayo ambayo yalianza Desemba 20 mwaka jana, yalihusisha vijiji 5 vya kata hiyo Dung’unyi, Damankia, Samanka, Munkinya na Kipumbuiko kwa minajiri ya kuhamasisha shughuli za maendeleo ndani ya kata hiyo-na hasa kilimo.

“Kwa wiki nzima mfululizo michuano hii imekwenda sambamba na utoaji wa elimu kutoka kwa wataalamu wa kilimo juu ya tija ya kilimo, lakini Jeshi la Polisi nao wamefika na kutoa elimu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu jukumu la raia katika ulinzi wa amani na usalama,” alisema Njiku.

Hata hivyo, Afisa Kilimo wa Kata hiyo, Esther Bayda, alimweleza Mkuu wa Wilaya kuwa kupitia ligi hiyo wamefanikiwa kuhamasisha vijana kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo umuhimu wa matumizi ya mbolea na mbegu bora katika kuinua tija na ustawi.

Bayda kupitia kauli mbiu ya ligi hiyo isemayo ‘kilimo ni kazi kama zilivyo kazi nyingine’ alisema katika kipindi chote cha ligi hiyo wamefanikiwa kuwafikia wakulima 50 na kuwafundisha mbinu bora za kilimo cha zao la mtama kupitia mashamba darasa mawili yaliyopo katika vijiji vya Samanka na Damankia.

“Bado kuna changamoto ya mwamko mdogo kwa kundi la vijana, hususani wale wa kati ya miaka 18 na 25 kutojihusisha na shughuli za kilimo, jitihada za uhamasishaji zinaendelea… na kuanzia jumatatu tutaanza kutoa mafunzo ya kilimo bora kwa wanakijiji takribani 150 wakiwemo vijana, kupitia mashamba darasa 3 kwa vijiji vya kipumbuiko, Damankia na Munkinya,” alisema Bayda. 


Saturday, January 2, 2021

KANISA LA MORAVIAN USHARIKA WA KIJICHI LAFANYA BONANZA KUSHEREHEKEA CHRISMASI NA MWAKA MPYA.

Baadhi ya vijana walioshiriki bonanza hilo lililoandaliwa na Kanisa la Moravian Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam  kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za mwishoni mwa mwaka 2020. Kulia ni Mchungaji wa kanisa hilo Raphael Mwampagatwa.
Timu hii ya vijana walioshiriki bonanza hilo lililoandaliwa na Kanisa la Moravian Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam  kwa ajili ya kusherehekea Sikukuu za mwishoni mwa mwaka ndio iliibuka kidedea katika bonanza hilo.
 


Na Dotto Mwaibale


KANISA la Moravian Usharika wa Kijichi jijini Dar es Salaam limefanya bonanza la  mpira wa miguu kwa ajili ya kusherehekea sikukuu za mwishoni mwa mwaka 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi Mchungaji wa kanisa hilo Raphael Mwampagatwa alisema walifanya hivyo ili kuhubiri neno la Mungu kupitia michezo.

"Michezo mara zote ukusanya watu hivyo tuliona tufanye kitu kama bonanza ili tukikutana na watu mbalimbali tukumbushane neno la Mungu hasa katika sikukuu hizi na mwishoni mwa mwaka yaani chrismasi na mwaka mpya." alisema Mwampagatwa.

Mwampagatwa alisema mbali ya kuhubiri kupitia michezo pia uwajenga kiakili na kiafya na kufahamiana na watu wengine ambao wanaishi jirani na kanisa hilo.

Alisema muitikio wa watu kushiriki mchezo huo ulikuwa mkubwa  hivyo mwaka huu Mungu akiwajaalia wataongeza michezo mingine mingi kama Netball, kukimbiza kuku, riadha, kukimbia huku ukiwa umevaa gunia miguuni, kuvuta kamba na uimbaji.

Friday, January 1, 2021

MLEZI WA SKAUTI MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI AFANYA ZIARA MKOANI MBEYA

Kamishna Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania anayeshughulikia makambi na mazingira ambaye pia ni mlezi wa mikoa ya  Nyanda za Juu Kusini ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, Mary Anyitike.
Kamishna Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania anayeshughulikia makambi na mazingira ambaye pia ni mlezi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, Mary Anyitike akisalimiana na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole baada ya kuwasili mkoani Mbeya.
Kamishna Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania anayeshughulikia makambi na mazingira ambaye pia ni mlezi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, Mary Anyitike akisaini kitabu cha wageni. Kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Skauti Wilaya ya Chunya, Mwalimu Alex Nyangwa na kulia ni Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole.
Kamishna Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania anayeshughulikia makambi na mazingira ambaye pia ni mlezi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, Mary Anyitike (katikati) akiwa na viongozi wa Skauti Mkoa wa Mbeya. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Skauti Wilaya ya Chunya, Mwalimu Alex Nyangwa na kushoto ni Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole.

Kamishna Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania anayeshughulikia makambi na mazingira ambaye pia ni mlezi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, Mary Anyitike (katikati) akiwaelekeza jambo viongozi wa Skauti Mkoa wa Mbeya. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Skauti Wilaya ya Chunya, Mwalimu Alex Nyangwa na kushoto ni Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole

Mjumbe wa Bodi wa Skauti, Christopher Mwasambili (kulia) akizungumza kwenye kikao cha bodi.
Mwenyekiti wa Bodi wa Skauti, Dkt.Julius Kaijage (kushoto) akiwa na Kamishna Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Makambi na Mazingira, Mary Anyitike  (katikati) na Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole.
 Kamishna Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Makambi na Mazingira, Mary Anyitike, akikagua eneo la uwanja wa Skauti mkoani humo.
Kamishna Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Makambi na Mazingira, Mary Anyitike, akizungumza na wananchi na wafanya biashara ndogo ndogo wanaoishi jirani na uwanja huo . 
Wananchi na wafanyabiashara ndogo ndogo wanaoishi jirani na uwanja huo .wakimsikilza Kamishna Mkuu Msaidizi anayeshughulikia Makambi na Mazingira, Mary Anyitike (hayupo pichani)


Na Dotto Mwaibale, Mbeya


KAMISHNA Mkuu Msaidizi wa Skauti Tanzania anayeshughulikia makambi na mazingira ambaye pia ni mlezi wa mikoa ya Mbeya, Ruvuma na Iringa, Mary Anyitike amefanya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa juzi, Anyitike alisema kuwa lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kuangalia utendaji kazi na kutembelea Uwanja wa Skauti  wa Ally Hassan Mwinyi uliopo  mkoani humo.

" Lengo la ziara hii ya siku moja ilikuwa ni kuangalia utendaji kazi na kutembelea uwanja wetu ambapo   pia  nilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya wajumbe wa bodi ya skauti mkoani hapa na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Skauti, Dkt.Julius Kaijage." alisema Anyitike.

Aidha Anyitike alisema kuwa katika ziara hiyo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi wanaoishi jirani na uwanja huo na wafanya biashara ndogo ndogo  kwa lengo la kujua changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi na kudumisha ujirani mwema.

Kamishna wa Skauti Mkoa wa Mbeya, Sadock Ntole alisema ziara hiyo ya kikazi ya Anyitike imewapa mori zaidi wa kazi  na kuwa ujumbe walioupata ataufikisha katika wilaya zote za mkoa huo.

"Tumefarijika sana na ziara ya mlezi wetu na yote aliyotuelekeza tutayafanyia kazi" alisema Ntole.

KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA AWATAKA WAZAZI, MAAFISA USTAWI KUWA KARIBU NA WATOTO WENYE MAHITAJI MAALUM


 Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (aliyevaa miwani) akikabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu, Halmashauri ya Ikungi, mkoani Singida.

Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi wa kituo hicho Padre Tom Ryan, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.


 Dk. Jingu akifurahi kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watoto wa kituo hicho.
 Dk. John Jingu (kushoto) akisalimiana na Diwani wa Siuyu Celestine Yunde, muda mfupi baada ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.
Dk. John Jingu (kulia) akizungumza na watendaji mbalimbali walioshiriki katika hafla hiyo ya kukabidhi bidhaa na chakula kwa viongozi na watoto wa Kituo cha Kulelea Watoto wenye Ulemavu Siuyu mkoani Singida.


Na Dotto Mwaibale,  Singida


KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii) Dk. John Jingu, amewataka wazazi wanaoishi na watoto wenye changamoto za ulemavu wa aina mbalimbali kuwathamini sanjari na kuwapa matunzo stahiki katika malezi na makuzi yao.

Jingu aliyasema hayo alipotembelea na kutoa zawadi za bidhaa mbalimbali na chakula kwa watoto wa Kituo cha Walemavu Siuyu, Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani hapa juzi

“Wazazi wawathamini watoto bila kujali hali zao. Kuna baadhi wanawaleta watoto kwenye vituo na kisha kuwatelekeza…hii haikubaliki ni lazima tuzingatie haki za msingi za malezi na makuzi ya watoto hususani watoto hawa wenye ulemavu,” alisema Jingu.

Aidha, aliwataka Maafisa Ustawi wa Jamii nchini kuongeza kasi ya kuhakikisha wanawatangamanisha watoto na wazazi wao-sambamba na jamii katika muktadha wa kubadili fikra, mtazamo ili kuleta ustawi wa watoto hususan wale wenye aina mbalimbali za ulemavu katika ngazi zote bila kubagua.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, kituo hicho cha Siuyu ni miongoni mwa vituo vyenye sifa stahiki za utoaji wa huduma za malezi kwa watoto, ikiwemo usalama wa kutosha sambamba na walimu waliosomea elimu maalumu ya watoto wenye ulemavu, huku akiwataka viongozi wa vituo vingine nchini kuzingatia matakwa ya kisheria katika uendeshaji wa huduma za usajili wa vituo vyao.

“Moja ya majukumu yetu ni kuvisajili na kuhakikisha vituo hivi vinafanya kazi sawasawa. Hivyo nimekuja hapa kutembelea kituo hiki kwa lengo la kukagua lakini nimeona pia nitoe zawadi kwa watoto hawa ambazo ni bidhaa na chakula,” alisema Jingu.

Hata hivyo, Diwani wa Kata hiyo, Selestine Yunde, alimshukuru Katibu Mkuu kwa kutembelea kituo hicho huku akimsihi kuangalia namna ya uwezekano wa serikali kuanza kutenga bajeti za kuhudumia vituo hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo hicho, Padre Tom Ryan, alisema ziara ya viongozi wa serikali akiwamo Jingu hutafsiri faraja, ustawi na kuchagiza ustawi na furaha kwa watoto hawa. “Tunaona fahari kwa kutiwa moyo na hamasa kupitia zawadi hizi,” alisema.

Huku mmoja wa watoto wanaolelewa katika kituo hicho, Raymond Daudi, mbali ya kushukuru, aliomba mamlaka ndani ya serikali kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wenye ulemavu, hususan wahitimu wa darasa la saba kwa kuwatengenezea mazingira ya kujipatia kipato badala ya kuwaacha bila ya msaada wowote.

Awali, akisoma taarifa ya kituo hicho, Kaimu Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Paul Sangalali, alisema kituo hicho cha Siuyu, kilichopo wilaya ya Ikungi mkoani hapa kilijengwa kwa ufadhili wa watu wa Ulaya na Marekani na kilifunguliwa Februari 2007 na aliyekuwa Mhashamu Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Desderis Rwoma.

Hata hivyo, Sangalali alisema mbali ya mafanikio yaliyopo, kituo kinakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwemo uhitaji wa baiskeli kwa ajili ya watoto wenye ulemavu wa viungo, uhitaji wa chakula, sabuni, mashuka na fedha kwa ajili ya nauli ya kuwarudisha watoto nyumbani wakati wa likizo.

“Pia miundombinu yake sio rafiki sana hasa pale watoto wanapokuwa wakielekea shule ya msingi Siuyu, na kuna ushirikiano hafifu kwa wazazi kuchangia shilingi laki moja za huduma kwa kila mwaka…lakini watoto wanapokuwa likizo nyumbani hawapati mazoezi kwa wazazi hivyo wakirudi kituoni walimu hulazimika kuanza upya kufundisha,” alisema Sangalali.