Thursday, March 11, 2021

TAHA YAANZA KUWAPA AFUENI YA KIUCHUMI WANAWAKE WA WILAYA YA IKUNGI SINGIDA



Meneja wa Miradi  TAHA, Elianchea Shang'a, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika mwanzoni mwa wiki wilayani humo, mkoani Singida.
Mnufaika wa mafunzo hayo, Rehema Kulungu, akizungumzia faida ya mafunzo hayo.
Mnufaika wa mafunzo hayo, Neema Martin, akizungumzia faida ya mafunzo hayo jinsi yatakavyo zinufaisha familia.
Wanufaika wa mafunzo hayo wakiwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.


Na  Dotto Mwaibale, Singida 

WANAWAKE wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wameanza kupata afueni ya kiuchumi baada ya kupatiwa mafunzo ya kilimo cha mboga mboga na  matunda na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.

 Akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani  Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a alisema wametoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa ni kuwakomboa wanawake hao kiuchumi.

Alisema TAHA inaendesha kazi zake katika mikoa 23 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja ( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba 

( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini ) na kuwa sasa wameongeza wilaya mbili moja, Ikungi-Singida na  Msalala-Shinyanga na kufikisha mikoa 25 ambayo wanatekeleza mradi huo.

Alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi. 

Shang'a aliwataja wadau wanao wawezesha katika mnyororo huo wa thamani kuwa ni wasambazaji wa pembejeo, wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na makampuni yanayofanya usafirishaji nje ya nchi na wanawawezesha kwa vitendo.

"  Katika uwezeshaji wetu kazi kubwa tunazozifanya naweza nikasema ni tatu lakini nitaongeza ya nne ya kwanza ikiwa ni kuwaunganisha wakulima na masoko, kuwawezesha wakulima katika suala zima la kilimo na kuwaonesha teknolojia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kulingana na uwezo na mazingira waliopo." alisema Shang'a.

Alitaja kazi ya tatu kuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kuwa wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kwa maana ya kushawishi na kutetea sera zile ambazo zinamuumiza mzalishaji, mfanyabiasha na mdau yeyote katika mnyororo wa thamani.

Shang'a alitaja kazi ya nne na ya mwisho kuwa ni kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na vyombo vya fedha baada ya kuwafundisha elimu ya fedha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi aliipongeza Asasi hiyo  ya TAHA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN WOMEN) kwa kutoa mafunzo hayo na akaahidi kushirikiana na asasi hiyo na wadau wote. 

Kwa upande wake Mariam Rashid akizungumza kwa niaba ya wanawake wenzake waliopata mafunzo hayo alisema yanaenda kuwapunguzia mzigo katika familia zao kwani yatawasaidia kuwainua kiuchumi na kuacha kuwategemea wanaume wao kwa kila kitu.

Wednesday, March 10, 2021

WILAYA YA IKUNGI WATUMIA MILIONI 200 KUTOA MIKOPO, WANAWAKE WANUFAIKA WAKUBWA.

Wanawake wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakiserebuka katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika juzi   wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akimkabidhi zawadi diwani pekee mwanamke wa kuchaguliwa wa Kata ya Sepuka, Halima Nyimba katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika juzi.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Massawe, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Justice Kijazi akizungumza na wanawake katika kilele cha maadhimisho hayo.
Wanawake wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakiserebuka katika kilele cha maadhimisho hayo.
Diwani wa Kata ya Ikungi, Abel Nkuwi, akizungumza katika maadhimisho hayo.
Wanawake wakiwa  kwenye maadhimisho hayo.
Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Katibu  wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Mkoa wa Singida, Edina Kuhulu, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Wanawake wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, wakiserebuka katika kilele cha maadhimisho hayo.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Martha Gwau, akitoa mada kwenye maadhimisho hayo.
Watoa mada wakiwa  kwenye maadhimisho hayo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida.


HALMASHAURI  ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida katika kipindi cha miaka miwili na nusu imefanikiwa kutoa mikopo zaidi ya sh. milioni 200 huku wanawake wakiwa ni wanufaika wakubwa.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Justice Kijazi wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika juzi.

Alisema katika fedha hizo nyingi zilikopwa na wanawake hivyo alitoa rai kuwa wanawake ni warejeshaji wazuri wa mikopo kuliko  makundi mengine lakini hata katika makundi hayo ndani yake kuna wakina mama.

" Nipende kusema kuwa mikopo mingi katika halmashauri inaenda kwenye  kundi ili la wakina mama." alisema Kijazi.

Kijazi alisema lengo la mikopo hiyo ni kutaka izalishwe hivyo aliwaomba wakina  mama hao pindi wakikopeshwa waizalishe.

Aidha Kijazi alisema kwa kutambua kuwa mama yeye ni   mtunzaji wa familia na ukimuelimisha utakuwa umeelimisha familia nzima.

" Natambua kazi kubwa wanayoifanya  wakina mama kwenye kuendeleza taifa letu kwani wao ni nguzo ya jamii inayotuzunguka ni jambo moja tu tunalotakiwa kulifanya sio kuwawezesha bali ni kuwaonesha fursa za maendeleo kwa sababu wanaweza." alisema Kijazi.

Kijazi alitoa ahadi kuwa iwapo Rais Dkt.John Magufuli ataona aendelee kukaa Ikungi atakuwa nao bega kwa bega.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akinukuu baadhi ya maneno yaliyopo kwenye biblia alisema mwanamke ni mzazi, mlezi, mlinzi, muombezi na msaidizi kama ilivyo andikwa katika kitabu cha Mwanzo 2:18 hivyo anapaswa kuthaminiwa.

Aidha Mpogolo alisema wanawake wana nguvu na uwezo mkubwa ndio maana wanaweza kugombea nafasi mbalimbali  lakini akatoa angalizo kuwa katika siasa wanavutana wenyewe mmoja akipanda ngazi na kufika juu mwingine anamvuta ashuke chini badala ya kupeana mkono.

Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Massawe alisema jitihada za halmashauri hiyo za kumwezesha mwanamke zinaungwa mkono na wadau wa maendeleo ambapo mashirika ya kimataifa na Asasi za kiraia zimeendelea kuwawezesha wanawake.

Alisema UN Women na watekelezaji wa miradi hiyo  (Farm Africa, TAHA, Kiwohede na C-Sema) wanatekeleza mradi wa kuimarisha usawa wa kijamii kwa kuwajengea uwezo wanawake katika kilimo, umiliki wa rasilimali na kupinga ukatili wa kijinsia.

Massawe aliyataja mashirika mengine yanayounga juhudi hizo za Serikali kwa kundi hilo kuwa ni SEMA- Singida, SPRF-Singida, NODIP, OVCCT na SMCCT.

Tuesday, March 9, 2021

WANAWAKE WILAYA YA IKUNGI WATAKIWA KUTUMIA FURSA WALIZONAZO

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akiwahutubia wanawake katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika jana wilayani humo, mkoani Singida. Kutoka kushoto ni Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a na  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi.

Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a, akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo, akikabidhi zawadi kwa mshindi wa michezo, Mariam Rashid.
Zawadi ikitolewa kwa mshindi, Neema Martin.
Washindi wakionesha zawadi zao.
Wanawake wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo (wa pili kushoto waliokaa). Kutoka kushoto waliokaa ni Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi na Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Aika Masawe.


Picha ya pamoja ya ishara ya upendo.
Mshindi wa mapishi Rehema Kulungu (kulia) akiwa na zawadi ya jiko baada ya kukabiddhiwa. Kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Aika Masawe.
Maadhimisho yakiendelea.
 

Na  Dotto Mwaibale,  Singida


WANAWAKE wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametakiwa kutumia fursa walizonazo ili kuinuka kiuchumi. 

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogolo wakati akiwahutubia wanawake hao katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika juzi wilayani humo. 

Wanawake  hao wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha mboga mboga na  matunda na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA. 

" Wilaya yetu ya Ikungi ina fursa mama zangu tuzitumie ..sisi tuna fursa ya kuuza kuku Dodoma ambako wananunua kwa sh.15, 000 wakati sisi tunanunua kuanzia sh.9, 000, 8,000, 7, 000 hadi 5,000." alisema Mpogolo. 

Mpogolo aliwataka  wanawake hao kujiunga katika makundi ili waweze kuanzisha ufugaji wa mbuzi ambao soko lake lipo Dodoma na Arusha ambako kuna kiwanda na uwezo wake ni asilimia 100 lakini kinapata mbuzi asilimia 50 hadi 40 tu. 

Katika hatua nyingine aliwapongeza wanawake hao kwa kuwa waaminifu kwa kurejesha mikopo wanayokopeshwa na halmashauri ukilinganisha na wanaume ambao wanachangamoto ya urejeshaji. 

Aidha Mpogolo amewataka wanawake hao kuacha kujiingiza kukopa mikopo umiza yenye riba kubwa ambayo inawarudisha nyuma kiuchumi. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alisema wilaya hiyo inatekeleza agizo la Serikali la kuwawezesha wanawake kiuchumi na akatumia nafasi hiyo kuipongeza Asasi ya TAHA na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN WOMEN) kwa kutoa mafunzo hayo na akaahidi kushirikiana nao. 

Meneja wa Miradi wa TAHA, Elianchea Shang'a alisema kwa kuwa mradi huo wanaoshirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi unaohusu kuwakomboa wanawake kiuchumi kupitia kilimo cha mboga mboga na matunda na unatekelezwa katika Wilaya mbili moja, Ikungi-Singida na  Msalala-Shinyanga. 

Alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi. 

Katika maadhimisho hayo wilayani humo asasi hiyo ilitoa mafunzo ya ujasiriamali na utawala wa fedha pamoja na lishe ambapo washindi walipewa  zawadi mbalimbali.

Monday, March 8, 2021

BOHARI YA DAWA (MSD) NA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2021



Wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD), wakiwa na bidhaa mbalimbali walizokwenda kutoa msaada kwa wanawake wenzao waliolazwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road walipowatembelea jana katika kuadhimisha Siku ya Wanwake Duniani kwa mwaka 2021, Jijini Dar es Salaam. 


Wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD), wakiwa na bidhaa mbalimbali mbele ya jengo la Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD), wakiwa katika picha ya pamoja.


 Wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD), wakikabidhi msaada huo.

Wanawake wa Bohari ya Dawa (MSD), wakielekea kukabidhi msaada huo.

 Msaada huo ukikabidhiwa.




Na Mwandishi Wetu

WANAWAKE wa Bohari ya Dawa (MSD) wameungana na wanawake wengine duniani kuadhimisha siku ya wanwake Duniani kwa mwaka 2021 kwa  kuwametembelea wanawake waliolazwa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali.

Aidha wanawake hao wameketi pamoja kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili maeneo yao ya kazi na kwenye jamii ili kuweza kuyapatia utatuzi.

TAMKO LA THBUB, SIKU YA WANAWAKE 2021



 

Sunday, March 7, 2021

THBUB YAIASA JAMII KUTOFUMBIA MACHO VITENDO VINAVYOTWEZA UTU WA MWANAMKE

Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu.
 


Na Mwandishi Wetu,


TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeitaka jamii kuendelea kubeba jukumu la kutokuyafumbia macho matukio yote yenye kutweza utu wa mwanamke na kutoa taarifa katika mamlaka husika pindi wanaposhuhudia matukio hayo.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu, Mathew Mwaimu katika taarifa yake kwa Vyombo vya Habari ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Jaji Mwaimu alisema  kuwa ni vyema jamii ikaendelea kuhamasishana kuacha mitazamo potofu ya kumchukulia mwanamke kama chombo dhaifu kisichoweza kuleta matokeo chanya ya uongozi ili kujenga jamii yenye usawa. 

“Kupitia jitihada mbalimbali za uhamasishaji zilizofanyika nchini kumekuwepo na ushiriki wa wanawake katika masuala ya uongozi kwenye vyama vya siasa, Serikali, Bunge, Mahakama na katika nafasi nyingine za uongozi katika jamii,’” alisema Mwaimu

Aliongeza kuwa pamoja na jitihada mbalimbali za Serikali za kukemea vitendo vya ukatili kwa wanawake bado kumekuwepo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake katika kuwania nafasi za uongozi zikiwemo mila na desturi zinazominya haki za wanawake, elimu na kipato duni kwa wanawake wenye nia ya kugombea uongozi na kutojiamini.

Mwaimu aliendelea kusema kwa kuwa Serikali  imeridhia mikataba na matamko mbalimbali ya Kimataifa inayotoa haki kwa kila mtu kushiriki katika nafasi ya uongozi na utawala wa nchi kwa usawa wa kijinsia, Tume inaunga mkono dhamira hiyo ya Serikali  na kuwahamasisha wanawake kuwania nafasi mbalimbali za uongozi. 

“Tume kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikiwahimiza wanawake kuendelea kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kuanzia ngazi za kijiji/mtaa hadi taifa na kuwajengea uwezo wa namna ya kudai haki zao kisheria pale wanapohisi haki hizo kuvunjwa,” alifafanua Mwaimu.

“Hivyo katika maadhimisho ya siku hii muhimu, Tume inaungana na jamii na wadau mbalimbali duniani kutambua mchango wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo,” aliongeza.

 Jaji Mwaimu alisema kuwa kupitia Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu 2021 ambayo  ni ‘Wanawake katika Uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye Usawa’,  Tume inaihamasisha jamii yote kuendelea kuchukua hatua madhubuti katika kuhakikisha kwamba ushiriki wa wanawake katika uongozi unaongezeka ili kufikia dunia yenye usawa.

Wednesday, March 3, 2021

UVCCM SINGIDA YAMPONGEZA DKT. BASHIRU ALLY KAKURWA KUWA BALOZI NA KATIBU MKUU KIONGOZI


Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Dkt. Denis Nyiraha 

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Dkt. John Pombe Magufuli  akimuapisha Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi.


Na Dotto Mwaibale, Singida

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida umempongeza Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kwa kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Balozi na Katibu Mkuu Kiongozi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Singida Dkt. Denis Nyiraha alisema uteuzi  huo  wa Bashiru ni sahihi kutokana na kazi nzuri alizozifanya  ndani ya chama kwa nafasi ya Katibu Mkuu.

Nyiraha alisema Bashiru akiwa Katibu Mkuu wa CCM alifanikiwa kurejesha mali za chama zilizokuwa mikononi mwa watu wengine kinyume na utaratibu.

" Pamoja na kuzirejesha  mali  hizo Bashiru alifanikisha chama hicho kupata ushindi katika uchaguzi wa Serikali za mtaa uliofanyika mwaka juzi ." alisema Nyiraha.

Aidha Nyiraha alisema katika kukiongoza chama hicho kwa  nafasi hiyo ya Katibu Mkuu  CCM ilipata  ushindi mkubwa kwenye uchaguzi mkuu 2020.

Nyiraha alitaja mafanikio mengine ya Dkt.Bashiru kuwa ni kusimamia nidhamu ya utumishi ndani ya chama na nje ya chama.

" Hakika tunayo imani  Dkt. Bashiru ataisimamia Serikali ipasavyo kutimiza majukumu yake kama alivyofanya akiwa katika nafasi hiyo kubwa ndani ya chama." alisema Nyiraha.