Tuesday, March 16, 2021

WABUNGE WAPATIWA KIKOMBE CHA DAWA YA CORONA, MTATURU AIPELEKA SINGIDA

Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo akimkabidhi Mkuu wa Mkoa huo Dkt.Rehema Nchimbi dawa yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A . baada ya kumalizika kwa kikao maalumu cha ushauri cha mkoa (RCC)  kilicho keti mwishoni mwa wiki. Dawa hiyo  imetengenezwa   na Mbunge  wa Jimbo la Lushoto, Shabaan Shekilindi wa Mkoa wa Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi akionesha dawa hiyo yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A . baada ya kukabidhiwa..
Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo, akizungumza kwenye kikao hicho. Kutoka kushoto n Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi na Mkuu wa Mkoa huo, Dkt.Rehema Nchimbi.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Wajumbe wakibadilishana mawazo katika kikao kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida


WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepata kikombe cha dawa ya Corona yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A. iliyotengenezwa   na Mbunge  wa Jimbo la Lushoto, Shabaan Shekilindi wa Mkoa wa Tanga.

Katika hatua nyingine kwa mapenzi dhidi ya wananchi na watumishi wa umma wa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo amemkabidhi dawa hiyo mkuu wa mkoa Dkt.Rehema Nchimbi ili waitumie kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Mtaturu akimkabidhi dawa hiyo Dkt.Nchimbi baada ya kumalizika kwa kikao maalumu cha ushauri cha mkoa (RCC)  kilicho keti mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh. Bilioni 222,188,872,239  ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambayo ni zaidi ya bajeti ya Sh. Bilioni 175,619,858, 500 iliyotengwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 alisema dawa hiyo imewasaidia wabunge kwa kiasi kikubwa kujikinga na maambukizi ya Covid 19.

"Mheshimiwa mkuu wa mkoa  hivi sasa tupo katika mapambano ya ugonjwa wa Covid 19 ambapo tunatakiwa tuchukue tahadhari zote za kujikinga nao kama tulivyo sisitizwa na Rais wetu Dkt.John Magufuli na wataalamu wa afya," alisema Mtaturu.

Alisema baada ya Mbunge mwenzao huyo kuitengeneza dawa hiyo walipata kikombe kama kile alichokuwa akikitoa Babu wa Loliondo Ambilikile Mwasapile.

" Kusema kweli kikombe cha dawa hiyo kimetusaidia sana ndio maana hamjasikia wabunge tukisumbuliwa na changamoto hiyo. Mheshimiwa mkuu wa mkoa nakukabidhi dawa hii ambayo kichupa kimoja kinauzwa sh.30,000 nawe uone namna ya kufanya utaratibu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu na watumishi wa umma mkoani hapa." alisema Mtaturu.

Alisema watawasiliana na mtengenezaji wa dawa hiyo kuona namna ya kuisafirisha hadi Singida kwa ajili ya wale watakao ihitaji kwani suala la afya ni la muhimu kwa kila mmoja wetu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mtaturu alisema dawa hiyo imeonekana inafaa kwa matumizi na inauwezo wa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo baada ya kuidhinishwa na vyombo husika vya Serikali ikiwemo Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) na kukabidhiwa vyeti vya udhibitisho.

TASAF YAWAINUA KIUCHUMI WANANCHI 2,212 MANISPAA YA SINGIGA


Mariam Kassim mkazi wa Kata ya Ipembe Manispaa ya Singida akipika vitumbua katika ofisi yake iliyopo Mtaa wa Soko mjini hapa leo,  baada ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)

Wateja wakinunua vitumbua ofisini kwa Mariam Kassim.

Mnufaika wa TASAF, Pili Radhaman ambaye ana mradi wa kuuza kokoto, akiwa mbele ya nyumba yake (Tembe) aliyokuwa akiishi kabla ya kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)



Muonekano wa nyumba ya kisasa aliyoijenga Pili Ramadhan.

Mnufaika wa TASAF, Hassan Ng'imba ambaye ana mradi wa kuuza kokoto, akiwa mbele ya nyumba yake (Tembe) aliyokuwa akiishi kabla ya kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)

Muonekano wa nyumba ya kisasa aliyoijenga  Hassan Ng'imba.

Hassan Ng'imba mkazi wa Mtaa wa Mnung'una Manispaa ya Singida akiponda kokoto katika kiwanda chake kidogo, ambazo lori moja huziuza kati ya sh. 130,000 hadi 140,000 baada  ya kuwezeshwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  TASAF.

Mwanahamisi Athuman mkazi wa Kibaoni ambaye anajishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na ufugaji akielezea mafanikio yake baada ya kuwezeshwa na mpango huo.

Shamba la mahindi la Mwanahamisi Athuman.
Mratibu wa TASAF Manispaa ya Singida, Juma Mkumbo Nzovu, akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF ndani ya Manispaa hiyo.
Mnufaika wa mpango huo, Joyce Lissu ambaye anajishughulisha na ufugaji wa nguruwe akielezea mafanikio yake baada ya kuwezeshwa na TASAF.


Na Dotto Mwaibale, Singida 

WANANCHI 2,212 katika Manispaa ya Singida mkoani hapa wamenufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)

Hayo yamebainishwa na Mratibu wa TASAF Manispaa ya Singida, Juma Mkumbo Nzovu wakati wa ziara ya maofisa wa mpango huo na waandishi wa habari ya kuwatembelea wanufaika hao iliyoanza jana mkoani hapa.

Nzovu  alisema tangu mradi huo uanze manispaa hiyo imepokea takribani sh.bilioni 4.5 kwa ajili ya ruzuku za TASAF ambazo zimegawanyika katika maeneo mbalimbali.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni ruzuku ya msingi na masharti, ajira za muda yaani PWP, shughuli za wasichana balehe na wanawake vijana AGYW ambao wanapata ruzuku ili waweze kutimiza malengo yao wakiwa shuleni na wengine kwa ajili ya kupata mitaji ya kufanyia biashara. 

" Mpango huu wa TASAF umeweza kuwasidia walengwa wengi kwa kujipatia kipato kwa kuwekeza, kujenga nyumba bora na sasa hivi hakuna malalamiko tena ya kuwa na uhaba wa chakula kwani wanajipatia kupitia ruzuku hizo za TASAF." alisema Nzovu.

Aidha Nzovu alisema zipo changamoto chache lakini nyingi ambapo wamezitoa zinaendelea kufanyiwa kazi na TASAF na madu mfupi ujao tutapata majibu.

Alitaja moja ya changamoto kubwa kuwa ni Kaya nyingi ambazo ni duni zaidi katika manispaa hiyo kuwa na uhitaji wa kujiunga kwenye mpango huo wa TASAF ambapo wanaamini watakumbukwa ili nao waingie.

Mariam Kassim mkazi wa Kata ya Ipembe mnufaika wa mpango huo anayejishughulisha na biashara ya kuuza vitumbua alisema TASAF imemsaidia sana kwani hivi sasa anamtaji mkubwa na ana ndoto ya kujenga nyumba kubwa na kununua gari.

" Awali niliogopa kujiunga na TASAF nikidhani walikuwa ni Freemason lakini baadae niliwaelewa kwani walinikuta nikiwa napika kilo mbili tu za vitumbua ambapo baada ya kunipa ruzuku niliendelea hadi nikapata sh.650,000 na hadi leo naendelea na biashara hii ambayo imeniwesha kuwasomesha watoto wangu na mmoja ana malizia shahada yake chuo kikuu.

Alisema mbali ya kufanya biashara hiyo ya vitumbua kupitia mpango huo anafuga kuku na amejiunga katika kikundi cha kukopeshana pesa.

Mnufaika mwingine Hassan Ng'imba anasema hapo awali hata huo mlo mmoja na familia yake  ilikuwa ni changamoto lakini baada ya kujiunga na mpango huo wanapata milo yote mitatu na ameweza kujenga nyumba ya kisasa na kuwa hivi sasa anajishughulisha na mradi wa kuuza kokoto kupitia kiwanda chake kidogo kilichopo mtaa wa Mnung'una pia amejiunga katika kikundi cha kukopeshana fedha.

Wanufaika wengine wa mpango huo ni Mwanahamisi Athuman, mkazi wa Kibaoni ambaye anajishughulisha na kilimo cha umwagiliaji na ufugaji, mwingine ni Pili Radhaman ambaye ana mradi wa kuuza kokoto na Joyce Lissu ambaye anajishughulisha na ufugaji wa nguruwe ambapo wote kwa pamoja wamefanikiwa kujenga nyumba za kisasa na kusomesha watoto wao. 

Monday, March 15, 2021

RC SINGIDA AZINDUA MAJENGO MATATU SHULE YA MSINGI GEZENARETH


Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (kushoto) akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo la Utawala la Shule ya Awali na Msingi ya Genezareth iliyopo Singida DC mwishoni mwa wiki. Kulia ni Meneja wa shule hiyo, Sister Yohana Duwe.

Katibu wa Elimu wa Jimbo Katoliki Singida, Padri Gilbert Mwiru akizungumza katika hafla hiyo.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (kushoto) akitoa zawadi kwa mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Wanafunzi wa shule hiyo wakiimba katika hafla hiyo.
Wanafunzi wa shule hiyo wakiimba katika hafla hiyo.
Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (kushoto) akitoa zawadi.kwa mmoja wa wanafunzi aliyefanya vizuri mtihani wa darasa la nne.
Jengo la chakula lililo zinduliwa.
Jengo la Utawala lililo zinduliwa.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida 

KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa Frederick Ndahani amewataka walimu na walezi kuwa lea watoto katika maadili ya kizalendo.

Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya  Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Rehema Nchimbi alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye hafla ya uzinduzi wa majengo matatu ya Shule ya Awali na Msingi ya Genezareth iliyopo  Singida DC.

" Tukiwa na Taifa la wasomi na wazalendo tutaisogeza nchi yetu kwenye uchumi wa juu hivyo ni jukumu la walimu na walezi kuwafundisha watoto wetu maadili ya uzalendo kuanzia shule za awali na kuendelea." alisema Ndahani.

Ndahani alisema anasikitika kuona vijana waliosomeshwa na Serikali ndio wanakuwa mstari wa mbele kupinga mambo ya maendeleo yanayofanyika hapa nchini kutokana na kukosa uzalendo.

Aidha Ndahani alitumia nafasi hiyo kuomba elimu ya kujitegemea ianze kutolewa mashuleni pamoja na kuanzisha miradi itakayo wajenga wanafunzi kiuchumi kuanzia ngazi ya chini. 

Katibu wa Elimu wa Jimbo Katoliki Singida, Padri Gilbert Mwiru aliishikuru Serikali kwa kushirikiana na mashirika ya dini kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi  na kueleza kuwa katika Mkoa wa Singida jimbo hilo lina taasisi za elimu 23, shule za msingi 10, Sekondari 8 na vyuo vya kati 5.

Meneja wa shule hiyo ambayo inamikiwa na Jimbo Katoliki Singida, Sister Yohana Duwe  alisema  majengo yaliyozinduliwa ni jengo la Utawala, Bweni na Bwalo la chakula na kuwa ujenzi huo umegharimu zaidi ya Sh.milioni 300.

Sister Duwe alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kusaidia kuboresha miundombinu ya umeme na maji ambayo haipo na kueleza kuwa hivi sasa wanatumia umeme wa jua  (sola) pamoja na maji ya mvua ambayo hayakidhi mahitaji. 

Sunday, March 14, 2021

WANAFUNZI FANI YA HRMA TIA SINGIDA WAZINDUA CHAMA CHAO



Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa Chama cha Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) wa Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Meneja wa Viwanda Vidogo  (SIDO) Mkoa wa Singida,  Agness Yesaya akionesha katiba ya chama hicho baada ya kukizindua chama hicho kwenye hafla iliyofanyika jana mkoani hapa. Kushoto kwake ni Meneja wa TIA, Kampasi ya Singida, Dkt. Jmes Mrema.
Meneja wa Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida, Agness Yesaya, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Meneja wa Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Dkt.James Mrema, akitoa taarifa wakati akimkaribisha Meneja wa Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida, Agness Yesaya (kushoto) ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya uzinduzi wa Chama cha Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) wa Taasisi hiyo iliyofanyika jana mkoani hapa. Kutoka kushoto ni Mhadhiri wa Chuo cha Utumishi Mkoa wa Singida, Lameck Sospeter na Mwenyekiti wa EWURA Mkoa wa Singida, Bertha Mlingi.
Mlezi wa Chama cha Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, Jackson Payowela, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Mwenyekiti  wa chama hicho, Janeneema Makulu akizungumza.




Viongozi wa chama hicho wakimsubiri kumpokea mgeni rasmi.
Mratibu wa Taaluma TIA, Kampasi ya Singida, Shisalalyandumi Ulomi, akizungumza.
Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa chama chao.
Hafla ikiendelea.
Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa chama chao.
Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa chama chao.
Hafla ikiendelea.
 Kaimu Mwenyekiti wa  chama hicho, Charity Mbiriti, akisoma hotuba ya wanafunzi mbele ya mgeni rasmi.. 
Wanafunzi wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa chama chao.
Wanafunzi wakiserebuka baada ya kuzindua chama chao.

Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala TIA, Kampasi ya Singida, Mtogo Kagulu, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo.

 Rais wa Serikali ya Wanachuo, TIA, Kampasi ya Singida, Dauda Dauda, akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo.

Picha ya pamoja na mgeni rasmi.



Na Dotto Mwaibale, Singida

WANAFUNZI wa fani ya Usimamizi wa Rasilimali Watu (HRMA) Taasisi ya Uhasibu   Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida wameunda chama chao lengo likiwa ni kuwakutanisha na kuwaweka pamoja.

Mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa chama hicho Meneja wa Viwanda Vidogo  (SIDO) Mkoa wa Singida,  Agness Yesaya akizungumza juzi na wanafunzi hao aliwapongeza kwa kuanzisha chama hicho na kueleza kuwa wanafunzi wa fani hiyo ni watu muhimu sana katika muktadha mzima wa kusimamia na kulinda rasilimali za nchi yetu.

" Ninyi ni watu muhimu sana hapa nchini hasa katika soko la kiuchumi tunawakaribisha Sido mje tuwafundishe mbinu  za kutengeneza mashine na bidhaa mbalimbali tutawapa ushirikiano" alisema Yesaya.

Yesaya aliwaambia wanafunzi hao kuwa baadhi yao wataajiriwa serikalini na sekta binafsi lakini ni muhimu pia kupata mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na Sido ili waweze kujiajiri badala ya kutegemea kuajiiriwa tukizingatia kuwa hivi sasa kuna changamoto ya ajira.

Meneja wa TIA Kampasi ya Singida Dkt.James Mrema akitoa taarifa ya chuo hicho wakati akimkaribisha mgeni rasmi  alisema Kampasi hiyo ya Singida ni miongoni mwa kampasi sita za Taasisi ya Uhasibu Tanzania ambayo makao makuu yake yapo Kurasini jijini Dar es Salaam.

Alitaja kampasi zingine kuwa ni Mbeya, Mwanza, Mtwara, Kigoma na makao makuu Dar es Salaam na kuwa kampasi ya Singida ilianzishwa mnamo mwaka 1974 ikiwa na programu mbili za Uhasibu na Masoko.

Dkt.Mrema alisema tangu kampasi hiyo ilipoanzishwa kumekuwepo na ongezeko la udahili wa wanachuo na kuwa sasa kina idadi ya wanachuo 2,242 kati yao wavulana  ni 1,099 sawa na asilimia 49 na wasichana wakiwa ni 1,143 sawa na asilimia 51.

Meneja huyo wa kampasi hiyo alisema hivi sasa idadi ya programu zimeongezeka hadi kufikia nne ambazo ni Uhasibu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, na Uongozi  wa Rasilimali Watu ambazo zote zinatolewa kuanzia ngazi ya astashahada, stashahada na shahada.

" Pamoja na mafanikio hayo kampasi yetu bado inakabiliwa na changamoto kama vile uhaba wa madrasa, mabweni, mwitikio mdogo wa wakazi wa Mkoa wa Singida kuchangamkia fursa ya elimu na kujiunga na chuo chetu kwani asilimia kubwa ya wanachuo wanatoka mikoa mingine.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa  chama cha wanafunzi wa fani hiyo ya Usimamizi wa Rasilimali Watu  Kampasi ya Singida, Charity Mbiriti alisema  chama hicho kiliundwa  April 12, 2016 ambapo kilianzishwa katika Kampasi ya Dar es Salaam na sasa kimekusudia kuunganisha kampasi zote ili kuwaweka pamoja.

Mbiriti alitaja malengo  ya chama hicho mbali ya kuwaunganisha pia ni kupata warsha na mafunzo ya fani hiyo na yote yanayohusu jamii kwa ujumla, kuhakikisha wanafunzi wanapata uelewa juu ya usimamizi wa rasilimali watu na umuhimu wake katika jamii kwa ujumla, kutengeneza mtandao wa kimasomo kati ya vyuo mbalimbali  ili kuleta tija katika fani yao.

Aidha Mbiriti alitaja malengo mengine ya chama hicho kuwa ni kuleta fursa kwa wanafunzi kujitengenezea uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa pamoja na kuimarisha mahusiano mazuri na vyama vingine vya taaluma.

Saturday, March 13, 2021

SBL YAPANDA MAELFU YA MITI KONGWA MKOANI DODOMA

Spika wa Bunge Job Ndugai akizungumza na wananchi, viongozi wa Wilaya ya Kongwa, na wafanyakazi wa Kampuni ya  Bia ya Serengeti (SBL)  katika Shule ya Sekondari ya Laikala wakati wa shughuli ya upandaji wa miti iliyoandaliwa na SBL jana.  Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya  Bia ya Serengeti (SBL), Mark Ocitti,

Mkurugenzi Mkuu wa SBL, Mark Ocitti, akizungumza  kabla ya kuanza shughuli hiyo ya upandaji wa miti.
Spika wa Bunge Job Ndugai, akishiriki kupanda miti katika Shule ya Sekondari ya Laikala.
Spika wa Bunge Job Ndugai (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa SBL,  Mark Ocitti wakiwa wameshika miti ikiwa ni ishara ya kuhamasisha wadau wengine kushiriki shughuli ya upandaji miti.

Mkurugenzi Mkuu wa SBL Mark Ocitti, akishiriki kupanda miti katika Shule ya Sekondari ya Ndurugumi iliyopo wilayani humo.

Wafanyakazi wa SBL wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo ya upandaji wa miti.

 Spika wa Bunge Job Ndugai (kulia) akizungumza na viongozi wa Kampuni ya  Bia ya Serengeti (SBL) baada ya kukamilika kwa shughuli hiyo ya upandaji miti.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


KAMPUNI ya Bia ya Serengeti (SBL),  imeungana na viongozi pamoja na wananchi wa wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma katika shughuli ya upandaji miti ikiwa ni sehemu ya mpango wa kampuni hiyo wa kutunza mazingira.

Mgeni rasmi aliku wa Spika wa Bunge Job Ndugai, viongozi wa wilayaya Kongwa, na wabunge ni badhi ya wageni walioshiriki katika zoezi hilo la upandaji miti lililoandaliwa na SBL.

Akiongea wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa SBL, Mark Ocitti,  alisema upandaji miti katika wilaya ya Kongwa ni sehemu ya mkakati endelevu wa kampuni hiyo unaolenga kupanda maelfu ya miti sehemu mbalimbali hapa nchini. 

Mkurugenzi huyo alisema mwaka 2019 kampuni ya SBL ilipanda miti katika wilaya za Same Pamoja na Moshi ilikuongeza uoto katika maeneo ya jirani na mlima Kilimanjaro.

“SBL inachukulia miti kama sehemu muhimu sana yamazingira. Miti inasaidia kuhifadhi vyanzo vya maji, ni makazi kwa wanyama na wadudu mbalimbali, ina vutahewa chafu ya kaboni na kuzalisha hewa safi na pia miti ni chanzo cha dawa. 

Biashara yetu na jamii kwa ujumla ni sehemu ya mazingira na hii itunafanya kuwa jukumu letu sote kuyalinda na kuyatunza mazingira,” alisema Ocitti. 

Upandaji miti wa SBL unakuja katika kipindi ambacho dunia inahangaika kupunguza uzalishaji ya hewa ukaa ilikupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na kuyalinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Kwa upande wake Mhe Job Ndugai aliishukuru kampuniya SBL kwa kuunga mkono jitihada za upandaji miti na kuongeza kuwa miti inanafasi ya kipikee kwa maisha ya watu na kusistiza kuwabila miti hakuna maisha.

Mhe Job Ndugai alisema ukataji miti holela ni moja kati ya sababu za mabadiliko ya tabiaya nchi ambayo yamesababisha changamoto nyingi zinazomkabili binadamu ikiwa ni pamoja na athari kwenye uzalishaji wa chakula, upatikanaji wa maji, afya ya viumbe mbalimbali ikiwa ni pamoja na binadamu.

Ni matumaini yangu kuwa zoezi hili la upandaji miti litawavuta wakazi wengi wa Kongwa na maeneo mengine nchini kupanda miti kila wanapopata fursa. Pia napenda kuzikumbusha taasisi na makampuni mbalimbali kufikiria juu ya dunia yetu na kuchukua hatua za kuilinda na kuitunza,” aliongeza Mhe Spika.

Katibu Mkuu Mtendaji wa Taasisi ya Habari Development Association (THDA),  Benard James alisema shughuli hiyo  imeandaliwa na taasisi hiyo na kuwa wamepanda miti 3000 wakiongozwa na Spika wa Bunge Job Ndugai kwa ufadhili wa SBL lengo likiwa ni kuikijanisha Dodoma na kuhamasisha jamii  kupanda miti na kuikuza kwa kuzingatia Dodoma ndio makao makuu ya nchi na ni eneo kame baada ya misitu mingi kuvamiwa na kukatwa kwa ajili ya mkaa, mbao na kuni.

James aliongeza kuwa miti hiyo imepandwa katika shule tatu wilayani humo ambazo amezitaja kuwa ni Shule ya Sekondari ya Ndurugumi, Laikala na Mwang'weta.