Saturday, March 20, 2021

RAIS SAMIA AANZA NA WAANDISHI WA HABARI

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha uaminifu
 

Na John Mapepele, Dodoma

Tanzania imeandika historia ya kuwa na Rais mwanamke wa kwanza kwenye nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameapishwa rasmi tarehe 19 Machi, 2021 kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Mhe, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea tarehe 17 Machi, 2021.

 

Kwa Mujibu wa ibara ya 37(5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano, endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kijiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana namaradhi ya mwili au  kushindwa  kutekeleza kazi za rais, basi  Makamu wa Rais ataapishwa  na atakuwa Rais kwa muda  uliobaki katika kipindi cha miaka mitano.

 

Mara baada ya kula kiapo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na majonzi mazito amezungumza kwa kifupi na kuanza kwa kutoa ratiba ya mazishi ya mwili wa aliyekuwa Rais, Mhe. John Pombe ambapo amesema kutakuwa na vituo vinne (Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza na Chato) vitakavyotumika kwa ajili ya kuagia ili wananchi wengi waweze kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao katika kipindi hiki kabla  ya mazishi rasmi tarehe 25 Machi 2021.

 

“Leo si siku nzuri ya kwangu kusema, kutokana na kidonda kikubwa moyoni na mzigo mzito nilionao. Nimekula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika mazingira tofauti, nimezoea kula kiapo katika hali ya nderemo na furaha lakini leo nimekula kiapo katika hali ya huzuni na masikitiko” amesisitiza Rais Samia Suluhu Hassan

 

Kama ilivyotarajiwa na watanzania wengi  kuhitaji faraja na matumaini kutoka kwa Rais huyu mpya baada ya  wimbi jeusi lililotanda ghafla baada ya jemedari na shujaa  mwanamapinduzi Dkt JPM  kuanguka, ndivyo ilivyokuwa baada ya Rais Samia kusoma hotuba yake fupi iliyosheheni mwanga wa matumaini mapya kwa Taifa iliyosisitiza  upendo, mshikamano na umoja kwenye kipindi hiki cha maombolezo.

 

“Katika kipindi hiki cha maombolezo, ni kipindi cha kuzika tofauti zetu, huu ni wakati wa kuwa wamoja, huu si wakati wa kutazama yaliyopita, huu si wakati wa kunyosheana vidole bali huu ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kuweka mbele nguvu kwa pamoja ili kujenga Tanzania ambayo Mheshimiwa Magufuli aliitamani, na zaidi sana tuungane kumwombea (hayati John Pombe Joseph Magufuli) alale pema peponi.” Amefafanua

  

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Samwel Malecela  amesema Taifa linapitia katika kipindi kigumu jambo la muhimu  ni kuendelea kushikamana  kama watanzania ili kupita kwenye kipindi hiki kwa umoja na upendo.

 

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Julius Mtatiro anaona kuwa pamoja na kuondokewa na Jemedari Mkuu hayati Dkt. John Pombe Magufuli Mungu ataivusha nchi yetu itaendelea kuwa imara.

 

“Taifa hili ni imara,Mungu amelipendelea sana, halikuwahi kuyumba wala kutetereka katika nyakati zote za changamoto; yalipotokea maasi ya kijeshi mwaka 1964, alipofariki Mzee Karume mwaka 1972, nyakati mbaya za njaa, nzige na vita ya Uganda miaka ya 1970 na 1980, alipofariki Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine mwaka 1984 na alipong’atuka madarakani na kufariki Muasisi na Baba wa taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tusiogope na tusitetereke, sisi ni taifa imara siku zote,nyakati zote” anaongeza Mtaturu.

 

Rais Samia ameyashukuru makundi ya watu mbalimbali kwa  kuendelea  kushikamana na Serikali yake, makundi hayo  ni pamoja na Chama cha Mapinduzi,viongozi wakuu wastaafu, vyombo vyote vya ulinzi na usalama na viongozi wa dini.  

 

Pia kwa namna ya pekee amewashukuru Wasanii na Waandishi wa Habari kwa kuendelea kutumia taaluma zao katika kuwaunganisha watanzania kuwa kitu kimmoja wakati wote. Baadhi ya Wasanii wakongwe wa muziki na Waandishi wameonekana kuguswa sana na hotuba hii na kutoa ya moyoni:

 

“OOOh, No. ungekuwepo wakati tunaangalia hii hotuba ilibidi tukae tuangalie kwenye luninga, mimi binafsi nilikuwa ninanena kwa lugha nakumbuka nilikuwa nimezungukwa na vijana nikawamuru watulie kwa sababu  huu ndiyo wakati wa bwana, nikawambia Mungu alipotaka kuwakomboa Taifa la Israel toka kwenye nchi ya utumwa alimtumia mwanamke na kwamba aliweka hekima ndani ya mwanamke na wakati huu Mungu ameweka mwanamke kwa maana kuna jambo ambalo Mungu anataka kutuingiza” amesema Christina Shusho, mmoja wa waimbaji wakongwe wa nyimbo za Injili hapa nchini.

 

“Mimi napenda kwenda na neno la kinabii Mheshimiwa Rais Samia ametuheshimisha sana wasanii wa Tanzania maana kuna makundi mengi lakini sisi wasanii tumependelewa tumetajwa katika hotuba ya kwanza natambua makundi mengine yataendelea kutajwa” ameongeza Shusho.

 

Kuhusu kifo cha Dkt. Magufuli Shusho amesema hayati Rais Magufuli  hakuona haya kumtambulisha Mungu wake katika kila hatua aliyopita pamoja na nafasi aliyokuwa nayo:

 ” kuna watu ambao tunampenda Mungu tunamjua Mungu tunapokuwa chini, tukiinuliwa hivi kama  mimi wa bwana Yesu asifiwe unakuta vinapungua kwa sababu ya position niliyoipata lakini Mheshimiwa Rais JPM hakumwacha kumsema Mungu wake wakati yeye ndiye alikuwa kiongozi Mkuu namba moja katika nchi yetu”.

 

Mwanamuziki Nguli nchni, Mrisho Mpoto amesema Wasanii na Wanamuziki wataendelea kumkumbuka Dkt. Magufuli kwa kuwa hakuwabagua, kila msanii alimfanya sawa na mwingine kiasi cha kumfanya kila msanii ajione anapendwa na Rais JPM.

 

“Utakumbuka  mtindo wake wa kuwavisha kofia yake alijitahidi sana kwa kadiri alivyoweza kufanya hivyo kwa kila msanii, mimi binafsi aliwahi hata kunitambulisha kuwa ni mwanamuziki  bora kabisa na  yeye ni shabiki wangu na kwenda mbali zaidi kwa kuimba  baadhi ya nyimbo zangu mbele ya umati wa  watu” amesema Mpoto kwa furaha

 

Mwandishi wa Habari wa kujitegemea Dotto Mwaibale amesema falsafa ya Dkt. Magufuli ya kuenzi lugha ya Kiswahili duniani umewafanya hata Viongozi wakuu barani afrika kufikiria kuanza Kiswahili kama lugha rasmi katika nchi hizo.

 

Mwandishi wa Makala haya ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kwenye Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo anapatikana katika: jmapepele1@ gmail.com au 0784441180

Friday, March 19, 2021

KANISA LA ABC LAMPONGEZA MAMA SAMIA, LAMLILIA JPM

Askofu Kiongozi wa Kanisa la ABC, Flaston Ndabila


Na Dotto Mwaibale


ASKOFU Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Center (ABC) la Tabata  Mandela jijini Dar es Salaam, Flaston Ndabila kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo wamempongeza  Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Tanzania.

Mbali na pongezi hizo Askofu Ndabila ametumia nafasi hiyo kumpa pole Rais Samia Suluhu Hassani kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli kilichotokea jana Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

Wengine waliyopewa pole ni mjane wa marehemu Janeth Magufuli, viongozi mbalimbali na watanzania wote kwa ujumla.

Ndabila akimzungumzia Hayati Rais John Magufuli alisema watanzania watamkumbuka kwa mambo yote ya maendeleo aliyofanya.

"Kila ninapofikiria mambo ambayo Mungu alimpa neema Rais wetu Magufuli kuyatenda nakumbuka vile Bwana yetu Kristo alivyo kuwa akifanya kazi zake hapa duniani." alisema Ndabila.

Ndabila akimtolea mfano Yesu  wakati akifanya kazi zake za kitume yalitokea mabishano mengi kati yake na waandishi , wanasheria, mafarisayo na masadukayo. 

" Kwa kuwa mtindo wake Yesu  wa kufanya kazi ulitofautiana kabisa na mazoea yao wengine walimtuhumu hafuati taratibu na desturi zao ambazo zilikuwa ni kinyume na mazoea yao ambapo aliokota fimbo na kuwapa mkong'oto na kupindua meza zao walipokuwa wakifanya biashara haramu hekaluni wakati alisaidia watu siku ya sabato na kuponya huku akiwaambia wale aliowaponya wabebe magodoro waende zao kumbe walikuwa  wakikwazika." alisema.

Ndabila alisema Yesu aliwajibu watu hao waliokuwa wakishindana naye kuwa kazi za mtu humshuhudia, kazi za mtu humsadikisha kwa watu. kazi za mtu humuaminisha mtu.

Alisema Rais wetu Magufuli ambaye Mungu amemtwaa alituaminisha ya kwamba kazi anazozifanya anazifanya kwa kumtanguliza Mungu na kuwa mafanikio yake yanatokana na  kumuweka  Mungu mbele.

" Magufuli aliwaaminisha watanzania kumwamini Mungu kwa kila kazi wazifanyazo na kuwa wakati wote alikuwa upande wake" alisema Ndabila.

 Alisema kitendo hicho cha kuwaaminisha kiliwapa wepesi wa kufundisha neno la Mungu na kuwa kazi hizo zilipokuwa zikifanyika alimrudishia Mungu utukufu.

Alisema maaskofu watamkumbuka  Magufuli kwa kuwapa  ari ya  kazi  baada ya kuona kiongozi wao ambaye ni mkuu wa nchi akimtanguliza Mungu kwa vitendo na ameondoka huku kazi zake zikiwa zinahubiri na kushuhudia.

Ndabila   alisema Rais Magufuli atakumbukwa kwa kazi kubwa alizozifanya katika kipindi chake kifupi cha uongozi wake.

" Kazi  aliyofanya   ni ya kutukuka ukiangalia hapa Dar es Salaam na mikoani ni mahali  gani utaenda usione mabadiliko kuanzia barabara, madaraja ya juu kuanzia Tazara na Ubungo" alisema.

Ndabila alisema mbali ya kazi hizo amejenga stendi kuu za mabasi za kisasa katika ya mikoa ya Simiyu,Morogoro, Korogwe Tanga, Kibaha na Dodoma pamoja na vituo vya afya, Hospitali na shule ukiachilia mbali miradi mikubwa kama  Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere, Reli, ununuzi wa vivuko kwa ajili ya usafiri wa majini, ndege na mingine. 

Thursday, March 18, 2021

VIJANA SINGIDA WAMLILIA RAIS DR. JOHN MAGUFULI

Kaimu Afisa Vijana  Mkoa wa Singida Frederick Ndahani.
Mwanaharakati wa masuala ya kijamii  Mkoa  wa Singida, Stella Mwagowa
Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi  wilayani  Ikungi mkoani hapa, Yahaya Njiku.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida


 VIJANA mkoani hapa wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za  kifo cha Rais Dkt. John Magufuli kilichotokea Jana. 

Akizungumza na waandishi  wa habari mkoani hapa jana kwa niaba ya vijana hao Kaimu Afisa Vijana  Mkoa wa Singida Frederick Ndahani alisema   watamkumbuka  Rais Magufuli kwa kuwafundisha  kuwa wazalendo wa Taifa letu.

"  Vijana na  baadhi ya watanzania tulikosa uzalendo lakini Magufuli akatuhasa na kutusihi tuwe wazalendo."  alisema Ndahani.

Ndahani alisema kuonesha jinsi  alivyo  kuwa akiwapenda  vijana  alitoa  nafasi nyingi za uongozi  wakiwemo wakuu wa wilaya, mikoa na baadhi  yao  aliwateua  kuwa  mawaziri.

Alisema aliwateua vijana kwa sababu aliamini wanao uwezo wa kusimamia mambo kwa uchungu kwa kuwa wao ni nguvu ya Taifa.

Aidha Ndahhani  alisema  Rais Magufuli  amefariki akiwa ametujengea uchumi wa viwanda na kutufikisha katika uchumi wa kati sambamba na elimu bure kwa wanafunzi wa shule ya msingi na Sekondari.

Alisema kwa niaba  ya  vijana wa  mkoa  huu wanatoa pole kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu, Rais wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Wabunge, viongozi wote na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa na kuwa  wanamuomba mrithi wake  Mungu amjalie aendeleze yale yote mazuri aliyoyacha.

Mwanaharakati wa masuala ya kijamii kwa ujumla mkoani hapa Stellah Mwagowa alisema  Rais Magufuli aliwaaminisha  vijana kuwa wanaweza kwani  hapo awali hawakuweza kudhubutu kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika chaguzi mbalimbali.

"Magufuli alijenga misingi kwa vijana kugombea nafasi mbalimbali  ambapo katika Bunge la 12 wapo wengi  tofauti na miaka mingine"alisema Mwagowa.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Dung'unyi  wilayani  Ikungi mkoani hapa, Yahaya Njiku alisema Rais Magufuli ametuachia alama na vitu ambavyo tutakapo kuwa tunaviangalia hatutaweza kumsahau kutokana na kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ambao utawasaidia vijana kupata ajira na wananchi kupata umeme wa uhakika.

Njiku alitaja miradi mingine aliyoianzisha kuwa ni reli ya kisasa,  madaraja makubwa jijini Mwanza na Dar-es-saalamu, kununua vivuko kwa ajili  ya  usafiri wa majini  pamoja  na usafiri wa anga

Wednesday, March 17, 2021

UPATIKANA WA MAJI SAFI NA SALAMA WILAYANI MKALAMA SINGIDA KUONGEZEKA

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama (katikati kulia)  Mhandisi Jackson Masaka na Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji,  Rosemary Rwebugisa ( katikati kushoto) wakifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Maji uliopo Kata ya Nduguti Wilayani humo jana kwenye maadhimisho ya wiki ya Maji.

Wananchi na viongozi wakishangilia wa uzinduzi wa mradi huo wa maji.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Lucy Boniphace akimtwisha ndoo mkazi wa Kata ya Nduguti baada ya kuzinduliwa kwa mradi huo.
Maadhimisho hayo yakiendelea.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara Kata ya Nduguti yalipo fanyika maadhimisho hayo.
 


Na Mwandishi Wetu, Singida.


HALI ya upatikanaji wa Maji safi na salama katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama mkoani Singida inatarajiwa kuongezeka hadi kufikia 76.8% kutoka 65.8% ya sasa baada ya Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kuchimba na kukarabati visima katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Meneja wa wakala huo (RUWASA) Wilaya Mhandisi Antidius Muchunguzi alitoa taarifa hiyo jana kwenye maadhimisho ya wiki ya maji wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji uliopo Kata ya Nduguti ukiwa ni miongoni mwa miradi inayoendelea na iliyotekelezwa katika Vijiji mbalimbali wilayani humo.

Mhandisi Muchunguzi alisema kwa sasa hali ya upatikanaji wa Maji katika Wilaya hiyo ni 65.8% lakini baada ya kukamilika Miradi ya Vijiji vya Kinyangiri,Ibaga,Kinyambuli,Mpambala,Ikolo,Lyelembo,Nkungi,Ipuli na Malaja hali ya upatikanaji wa Maji utafikia 76.8%

"RUWASA Wilaya ya Mkalama inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali vijiji, mingine tunakarabati na mingine tunachimba visima katika vijiji vya Nkungi,Ipuli na Malaja." alisema  Muchunguzi.

Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mara baada ya kuzindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka aliziagiza kamati za Maji na wananchi kwa ujumla kuitunza miradi hiyo ili iwe endelevu.

"Miradi hii ili iwe endelevu inahitaji usimamizi wa karibu.Wananchi mshiriki katika ulinzi wa miundombinu ya Miradi ya Maji na kushiriki kupanda Miti kwenye Vyanzo vya Maji." alisema Masaka.

Aidha ameagiza RUWASA na kamati za maji za vijiji kuhakikisha maji hayapotei huku fedha zinazotokana na ankara za maji akitaka zitumike katika kukarabati miundombinu.

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Maji Rosemary Rwebugisa,  aliwaagiza wananchi pamoja na kutunza miradi hiyo na vyanzo vyote vya maji ili kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji,kulipa Ankara kwa wakati ili huduma ziendelee kutolewa.

Rwebugisa alisema Wizara haitafikia malengo yake ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji na salama kama miundombinu ya miradi iliyotekelezwa haitatunzwa.

WANUFAIKA WA TASAF IRAMBA MKOANI SINGIDA WAOMBA WATAALAMU WA KILIMO NA MIFUGO

Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) wilayani Iramba mkoani Singida, Magreth  Peter akiswaga ng'ombe wake aliowapata baada ya kuwezeshwa na mpango huo..
Mnufaika wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF)  Magreth  Peter (kushoto) mkazi wa Kijiji cha Kengege akizungumza na viongozi wa kijiji hicho pamoja na maafisa habari kutoka TASAF makao makuu waliomtembelea kujua mafanikio yake na changamoto alizo nazo.
Mnufaika wa mpango huo, Ukende  Kidyusi akiwa na wajukuu zake mbele ya nyumba yake ya kisasa aliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF.
Mnufaika wa mpango huo, Joyce Mpugi akiwa na mume wake mbele ya nyumba yao ya kisasa waliyoijenga baada ya kuwezeshwa na TASAF huku wakiwa na kuku ambao ni zao lililotokana na mpango huo..
Nyumba ya tembe iliyo kuwa ikitumiwa na Mariam Danford na wazazi wake kabla ya kujengwa nyumba yao ya kisasa.
Hii ni nyumba ya kisasa ya wazazi wake  Mariam Danford baada ya kuwezeshwa ma TASAF.
 Mariam Danford (kulia) akizungumzia mafanikio waliyopata kutoka TASAF.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kijiji cha Kengege, Edward Mdende akizungumzia jinsi TASAF ilivyo wawezesha kulifanyia matengezo  lambo la maji ambalo linawasaidia katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Betha Simon akizungumzia faida za lambo hilo.
Mratibu wa TASAF wilayani humo, Adamu Msangi akizungumzia utekeleza wa mpango huo. 



Na Dotto Mwaibale, Iramba


WANUFAIKA wa mpango wa kunusuru Kaya Masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  (TASAF) wilayani Iramba mkoani hapa wameomba kutembelewa mara kwa mara na wataalamu wa kilimo, mifugo na biashara ili waweze kuwasaidia  kupata faida badala ya  hasara.

Maombi hayo yametolewa jana kwa nyakati tofauti na wanufaika hao wa Kijiji cha Kengege wakati wakizungumza na waandishi wa habari na maofisa wa mfuko huo ambao wapo katika ziara ya kuwatembelea ili kujua mafanikio na changamoto walizo nazo.

Mnufaika wa mpango huo Magreth Peter ambaye hujishughulisha na kilimo pamoja na ufugaji wa nguruwe na ng"ombe alisema changamoto kubwa waliyonayo ni kukosa wataalamu wa kuwapa elimu ya ufugaji na kilimo pamoja na  biashara.

"Tunashindwa kupiga hatua kutokana na kupata matunda kidogo yatokanayo na kazi zetu kwa sababu ya kukosa wataalamu hao ambao hapa kwangu walifika mwaka juzi na hawajarudi tena" alisema Peter.

Aidha Peter alisema kutokuwa na elimu ya biashara kumechangia kwa kiwango kikubwa kuuza mifugo yao kwa bei ya chini kupitia walanguzi na madalali akitolea mfano alipouza nguruwe wake 11 kwa sh.milioni 1.8 tu.

Mnufaika mwingine Ukende Kidyusi anaye jishughulisha  na kilimo na ufugaji kazi zilizo msaidia kujenga nyumba ya kisasa baada ya kuwezeshwa na TASAF anasema elimu ndogo wanayopata kutoka kwa wataalamu hao wanayoitoa kwenye mikutano ya hadhara bila ya kufika zilipo shughuli hizo zina warudisha nyuma licha ya TASAF kuwa na maono mazuri ya kuziinua kaya Masikini.

Mratibu wa TASAF wilaya hiyo Adamu Msangi alisema mara kwa mara wanapokutana na  wataalamu hao katika mikutano ya kiutendaji  wamekuwa wakihimiza kuwatembelea walengwa wa mradi huo kwa ajili ya kujua changamoto zao za kilimo na ufugaji ili kuzipatia ufumbuzi haraka.

Akizungumzia utekeleza wa mpango huo alisema halmashauri hiyo ilipokea kiasi cha sh. 7,716,971,481 kutoka Serikali kuu ambapo kwa  mwaka 2014/ 2020 wametumia sh.5,049,115,890 kwa ajili ya uhaulishaji fedha za ruzuku na utimizaji wa masharti ya afya na elimu. 

Alisema kwa mwaka 2016/2020 walitumia sh.2,032,809,000 kwa  ajira  ya muda mfupi.

Aidha Msangi aliongeza kuwa mwaka 2018/2020 walitumia sh.300,750,000 kwa ajili ya kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ulimi na athari za ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana walio ndani ya mfumo wa shule  (Timiza malengo)

Alisema mwaka  2018/2020 walitumia sh.23,963,500 kwa ajili ya kuwawesha wananchi kiuchumi na kuwa mwaka huo huo walitumia sh.170,304,091 kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa vijana walio nje ya mfumo wa shule (Timiza male ngo)

Wanufaika wengine wa mpango huo ni Joyce Mpugi ambaye anajishughulisha na kilimo, ufugaji wa kuku, mbuzi na ng'ombe, Ukende  Kidyusi na Mariam Danford ambapo wote kwa pamoja wamefanikiwa kuondoka kwenye nyumba za matembe walizokuwa wakiishi  baada ya kujenga za kisasa.

Tuesday, March 16, 2021

WAFANYABIASHARA WAPEWA SIKU 5 KUONDOA MIFUGO KATIKA MNADA WA KIZOTA

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Kizota wakati alipotembelea mnada huo kukagua shughuli zinazofanyika ambapo amewapa siku tano kuhakikisha wanaiondoa mifugo yao wanayoitunza kwenye mnada huo ikisubiri kwenda kuchinjwa. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akizungumza na watendaji wa mnada wa kizota, viongozi wa halmashauri ya Jiji la Dodoma na viongozi kutoka WMUV wakati alipotembelea mnada Kizota kukagua shughuli zinazofanyika ambapo ameagiza ujenzi wa ukuta katika mnada huo uanze haraka. 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul akikagua miundombinu iliyopo katika Mnada wa Kizota wakati alipotembelea mnada huo kukagua shughuli zinazofanyika jana. 

 

Mwandishi Wetu, Dodoma

Wafanyabiashara wa mifugo katika Mnada wa Kizota Jijini Dodoma wametakiwa kuacha kuhifadhi mifugo yao inayokwenda machinjioni katika eneo la mnada kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul leo (16.03.2021) wakati alipotembelea mnada huo kwa lengo la kukagua shughuli zinazofanyika ambapo pia alikutana na baadhi ya wafanyabiashara wa mifugo.

Gekul amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa zipo taratibu za uendeshaji wa Minada ya Upili ambapo mifugo ikishanunuliwa inatakiwa kuchukuliwa na sio kutuzwa hapo ikisubiri kupelekwa machinjioni.

“Hivyo natoa siku tano kwa wafanyabiashara wote ambao mnatunza mifugo yenu hapa mkisubiri kuipeleka machinjioni kuhakikisha mnaitoa na kuitafutia eneo jingine kwa ajili ya kuitunza,” alisema Naibu Waziri Gekul.

Aidha, Naibu Waziri Gekul aliwaeleza wafanyabiashara hao kuwa wizara imeshatenga fedha zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kuanza kuboresha miundombinu ya mnada huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa ukuta unaozunguka mnada huo.

Vilevile ametoa rai kwa wananchi kutovamia eneo la mnada, kwani moja ya sababu iliyochelewesha kuanza kwa ujenzi wa ukuta huo ni migogoro iliyotokana na uvamizi wa ardhi. Pia amewataka viongozi katika ngazi ya Kata, Mitaa na Vijiji kuhakikisha wanasimamia na kuchukua hatua mapema pale wanapoona mtu anavamia maeneo haya ya minada.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Joseph Mafuru amesema kuwa timu ya wataalam inayofanya uhakiki wa eneo hilo kutokana na uvamizi itakapomaliza kazi yake watahakikisha wanalipima eneo hilo kwa haraka

WABUNGE WAPATIWA KIKOMBE CHA DAWA YA CORONA, MTATURU AIPELEKA SINGIDA

Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo akimkabidhi Mkuu wa Mkoa huo Dkt.Rehema Nchimbi dawa yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A . baada ya kumalizika kwa kikao maalumu cha ushauri cha mkoa (RCC)  kilicho keti mwishoni mwa wiki. Dawa hiyo  imetengenezwa   na Mbunge  wa Jimbo la Lushoto, Shabaan Shekilindi wa Mkoa wa Tanga.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi akionesha dawa hiyo yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A . baada ya kukabidhiwa..
Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo, akizungumza kwenye kikao hicho. Kutoka kushoto n Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi na Mkuu wa Mkoa huo, Dkt.Rehema Nchimbi.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
Wajumbe wakibadilishana mawazo katika kikao kikao hicho.
Kikao kikiendelea.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida


WABUNGE wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamepata kikombe cha dawa ya Corona yenye uwezo wa kukinga na kutibu ugonjwa wa virusi vya corona iitwayo Shekilindi BOSN. A. iliyotengenezwa   na Mbunge  wa Jimbo la Lushoto, Shabaan Shekilindi wa Mkoa wa Tanga.

Katika hatua nyingine kwa mapenzi dhidi ya wananchi na watumishi wa umma wa Mkoa wa Singida, Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ambaye ni Mwenyekiti wa wabunge wote wa mkoa huo amemkabidhi dawa hiyo mkuu wa mkoa Dkt.Rehema Nchimbi ili waitumie kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo.

Mtaturu akimkabidhi dawa hiyo Dkt.Nchimbi baada ya kumalizika kwa kikao maalumu cha ushauri cha mkoa (RCC)  kilicho keti mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh. Bilioni 222,188,872,239  ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambayo ni zaidi ya bajeti ya Sh. Bilioni 175,619,858, 500 iliyotengwa mwaka wa fedha wa 2020/2021 alisema dawa hiyo imewasaidia wabunge kwa kiasi kikubwa kujikinga na maambukizi ya Covid 19.

"Mheshimiwa mkuu wa mkoa  hivi sasa tupo katika mapambano ya ugonjwa wa Covid 19 ambapo tunatakiwa tuchukue tahadhari zote za kujikinga nao kama tulivyo sisitizwa na Rais wetu Dkt.John Magufuli na wataalamu wa afya," alisema Mtaturu.

Alisema baada ya Mbunge mwenzao huyo kuitengeneza dawa hiyo walipata kikombe kama kile alichokuwa akikitoa Babu wa Loliondo Ambilikile Mwasapile.

" Kusema kweli kikombe cha dawa hiyo kimetusaidia sana ndio maana hamjasikia wabunge tukisumbuliwa na changamoto hiyo. Mheshimiwa mkuu wa mkoa nakukabidhi dawa hii ambayo kichupa kimoja kinauzwa sh.30,000 nawe uone namna ya kufanya utaratibu kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wetu na watumishi wa umma mkoani hapa." alisema Mtaturu.

Alisema watawasiliana na mtengenezaji wa dawa hiyo kuona namna ya kuisafirisha hadi Singida kwa ajili ya wale watakao ihitaji kwani suala la afya ni la muhimu kwa kila mmoja wetu kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mtaturu alisema dawa hiyo imeonekana inafaa kwa matumizi na inauwezo wa kujikinga na maambukizi ya ugonjwa huo baada ya kuidhinishwa na vyombo husika vya Serikali ikiwemo Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) na kukabidhiwa vyeti vya udhibitisho.