Tuesday, April 13, 2021

TAHA YATOA MAFUNZO YA LISHE BORA KWA WANAWAKE WA IKUNGI MKOANI SINGIDA

Mratibu wa Jinsia na Lishe kutoka  Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA, Salome Stephen, akitoa mafunzo ya  lishe bora kwa wanawake na baadhi ya wanaume wa  kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka  wilayani  Ikungi mkoani Singida juzi.

Wanawake na baadhi ya Wanaume wa Kata ya Kipumbwiko  wilayani  Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupatiwa juzi mafunzo ya lishe bora kwa watoto wao kutoka Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.

Baadhi ya Wanaume wa Kata ya Kipumbwiko wakiwa kwenye mafunzo hayo


Wanawake wa Kata ya Kipumbwiko wakiwa kwenye mafunzo hayo.

Wanawake na baadhi ya Wanaume wa Kijiji cha Mnang'ana Kata za Sepuka  wilayani  Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupatiwa mafunzo ya lishe bora kwa watoto wao kutoka Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.


Wanawake  wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka wakiwa kwenye mafunzo hayo.


Mratibu wa Jinsia na Lishe kutoka  Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA, Salome Stephen, akitoa mafunzo ya  lishe bora kwa wanawake na baadhi ya wanaume wa  Kata ya Kipumbwiko.

Wanawake wa Kata ya Kipumbwiko wakiwa kwenye mafunzo hayo.
 



Na  Dotto Mwaibale, Singida 


WANAWAKE zaidi ya 300 wa Kata za Sepuka,  Irisya na Kipumbwiko wilayani  Ikungi mkoani Singida wamepata mafunzo ya lishe bora kwa watoto kutoka   Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.


Mafunzo hayo yametolewa na Asasi hiyo kwa ufadhili wa UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa kuwaepusha watoto na udumavu unaosababishwa na ukosefu wa lishe bora.

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanawake hao wakati akitoa mafunzo hayo Mratibu wa Jinsia na Lishe kutoka TAHA, Salome Stephen alisema lishe bora kwa watoto ni muhimu sana kwa ukuaji wao tangu wakiwa tumboni mwa mama zao.

Stephen alisema mafunzo hayo yalilenga kuangalia mambo mawili moja likiwa ni ulishaji bora wa watoto na pili ni namna bora ya utayarishaji wa mbogamboga na umuhimu wa ulaji wake.

Akizungumzia msingi wa lishe bora alisema unapatikana kutoka katika makundi matano ya chakula la kwanza likiwa ni vyakula vinavyo tokana na nafaka, mizizi pamoja na ndizi za kupika.

Alitaja kundi la pili kuwa ni la vyakula  asili ya wanyama, samaki na jamii ya mikundekunde ambayo ni maharagwe, mbaazi, choroko, njugu, dengu na njegere. 

Alitaja kundi la tatu kuwa ni la mbogamboga na la nne ni la matunda ya aina mbalimbali.

Stephen alitaja kundi la tano kuwa ni la vyakula vya mafuta, sukari na asali ambapo kwenye mafuta ni zile mbegu zote kama karanga, alizeti na za maboga.

Akizungumzia namna bora ya kuwalisha watoto kuanzia chini ya miezi sita, Stephen alisema chakula pekee kinachotakiwa ni maziwa ya mama.

"  Maziwa ya  mama ndio chakula sahihi kinachofaa kwa mtoto chini ya miezi sita kwa ajili ya ukuaji bora kwa mwili na akili" alisema Stephen.

Alitaja sababu nyingine ya mtoto kupata maziwa ya mama yake ndani ya miezi hiyo kuwa yanamsaidia kupata kinga ya mwili na kwamba mama anaweza kumnyonyesha mtoto wake kwa muda huo pasipo kumpa kitu chochote.

Alisema changamoto kubwa waliyonayo wakina mama  ni kukosa ufahamu wa namna gani ya kunyonyesha na wale vyakula gani ili maziwa yaendelee kutoka.

" Ili maziwa ya mama yaendelee kutoka anapaswa kunyonyesha mara nyingi zaidi kwani mwili wa binadamu unavichocheo vya kutengeneza maziwa." alisema Stephen.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni wakina mama kunyonyesha watoto wao haraka haraka na hawana muda wa kutosha wa kunyonyesha kwani mtoto anapaswa kunyonya ziwa moja si chini ya nusu saa au anyonye mpaka atakapo shiba.Na ziwa lingine atanyonya wakati mwingine atakaposikia njaa.

Alisema hakuna mahali ambapo pameelekeza lazima mtoto anyonye maziwa yote mawili kwa wakati mmoja na kuwa mtoto hasipo nyonya kwa muda mrefu maziwa yanatabia ya kujitenga, atakapo anza kunyonyeshwa huanza kutoka maziwa ya maji ambayo utuliza kiu ya mtoto na kufuaata maziwa mazito ambayo umfanya mtoto ashibe, hapo hapo mama bila ya kusubiri kidogo ili yaanze kutoka maziwa mazito yenye virutubisho anamwamishia katika ziwa jingine.

Asasi ya TAHA yenye makao yake makuu jijini Arusha imekuwa ikitoa mafunzo kama hayo katika mikoa 25 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja 

( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba ( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini ) ,Ikungi-Singida na  Shinyanga.

Monday, April 12, 2021

MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA SOKOINE KUFANYIKA SUA MOROGORO

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo (SUA)  Prof. Maulid Mwatawala (Wa kwanza kulia) akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo yatakayofanyika Chuoni hapo mwezi huu mwishoni kulia kwake ni Prof. Samweli Kaboto Mwenyekiti wa kamati ya mandalizi ya maadhimisho hayo.

Mwenyekiti wa kamati ya maadhimisho hayo Prof. Samweli Kabote ( Wa kwanza kushoto)   akizungumzia maandalizi hayo kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kuzungumza na waandishi wa habari. Katikati ni Prof. Maulid Mwatawala Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo na Bi. Mariam Mwayela.Wa kwanza kulia ni Afisa Mahusiano na Masoko wa SUA.


Afisa Mahusiano na Masoko wa SUA, Mariam Mwayela ( kulia) akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki wa mkutano huo wa waandishi wa habari,
Washiriki wa mkutano huo na Wandishi wa habari wakifuatilia taarifa inayotolewa kuhusu maadhimisho hayo ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi ujao
Mkutano ukiendelea.
Washiriki wa mkutano huo na Wandishi wa habari wakifuatilia taarifa inayotolewa kuhusu maadhimisho hayo ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi ujao.


Washiriki wa mkutano huo na Wandishi wa habari wakifuatilia taarifa inayotolewa kuhusu Maadhimisho hayo ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine yatakayofanyika mwishoni mwa mwezi ujao.
Mkutano ukiendelea.
 


Na Calvin Gwabara, Morogoro.


CHUO Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA kimeahidi kunedelea kuenzi mchango wa AliyekuwaWaziri Mkuu Hayati Edward Moringe Sokoine kutokana na ushupavu wake kama kiongozi katika kusimamia uchapakazi, Kilimo vijijini, Uzalendo na kuchukia rushwa.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo ambaye ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Upande wa Taaluma Prof. Maulid Mwatawala wakati akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo juu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Hayati Edward Moringe Sokoine kwa mwaka 2021.

“Chuo kiliamua kutekeleza maamuzi ya kuadhimisha siku hii kuanzia mwaka 1992 kwa kuwa kiongozi huyu alikuwa mchapa kazi na alipigania ,masuala ya kilimo hasa katika mapinduzi vijijini na utoshelevu wa chakula kwa watanzania” Alisisitiza Prof. Mwatawala.

Prof.Mwatawala aliongeza kuwa katika kipindi cha uongozi wake Hayati Sokoine alipiga vita suala la rushwa na kuimarisha uadilifu katika utumishi wa umma ambapo serikali iliyopomadarakani inayazingatia na kuyaenzi kwa ajili ya maendeleo yaTaifa.

Kaimu Makamu huyo wa Mkuu wa Chuo alibainisha kuwa maadhimisho hayo kwa  mwaka huu yatafanyika kuanzia tarehe 24-27 Mei, 2021 chuoni hapo baada ya kuhairishwa hapo awali kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati Dkt. John PombeMagufuli.

Aidha alisema mambo yatakayofanyika katika wiki hiyo ya maonesho yateknolojia na ubunifu katika Kilimo, Ufugaji naUvuvi, kufanya mkutano  wakisayansi kwa wanataaluma, watafiti, wanafunzi na wadau mbalimbalii, mdahalo wa kitaifa wa kumbukizi  yaSokoineutakaofanyika siku ya tarehe 27 Mei 2021, kutoa huduma za afya kwa binadamu hususani magonjwa yasiyo ambukiza, kutoa huduma za tiba ya  mifugo 

kupitia  hospitali ya rufaa ya wanyama bure kwa jamii, kuchangia damu salama na kufanya michezo mbalimbali ambayo itaambatana na zawadi kwawashindi..

Hayati Edward Moringe Sokoine alifariki dunia kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984 akiwa na umri wa miaka 46 katikaMkoa wa Morogoro akitokea Dodoma katika kikao cha Bunge na katika kipindi chake cha uongozi alihudumu kwa vipindi viwili.

“Kwa mwaka huu 2021 itakuwa ni maadhimisho ya 17 kumuenzi Hayati Edward Moringe Sokoine toka kumbukizi ya kwanza mnamo mwaka 1992  ya maadhimisho hayo  ambayo hufanyika kila mwaka Chuoni ” alisema prof. Mwatawala.

Awali akimkaribisha mgeni rasmi mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya kumbukizi ya hayati Edward Sokoine Moringe Prof. Samweli Kabote kutoka SUA alisema kuwa huwezi kuongea historiaya Chuo cha Sokoine cha Kilimo SUA bila kumtaja Hayati Sokoine kwasababu Chuo kimebeba jina lake.

 Wiki ya Kumbukizi ya Hayati Edward Moringe Sokoine mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo, Teknolojia za kilimo, kuzalisha kwa tija na ushindani katika Soko, Kuelekea Nchi ya Uchumi wa juu wa Kati.   

NJIKU AWATAKA WANAFUNZI KUWA WAZALENDO

Kaimu Afisa Tarafa  ya Ikungi mkoani Singida,  Yahaya Njiku , akihutubia kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogolo wakati akizungumza na Vijana Wanafunzi wa Katoliki Tanzania (TYCS) wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Ikungi mkoani Singida  katika sherehe ya kuagana na wanafunzi wenzao wa kidato cha 

5-1 iliyofanyika juzi wilayani humo.


Vijana Wanafunzi wa Katoliki Tanzania (TYCS)  wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Ikungi wakiwa wamejipanga tayari kuingia ukumbini katika sherehe ya kuagana na wanafunzi wenzao wa kidato cha 5-1 iliyofanyika juzi wilayani humo.
Walimu wakiwa kwenye sherehe hiyo.
Wazazi wakiwa kwenye sherehe hiyo.
Vijana Wanafunzi wa Katoliki Tanzania (TYCS)  wahitimu wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Ikungi wakiwa kwenye sherehe hiyo.
Afisa Elimu Kata ya Ikungi, Mghenyi Nkuwi, akizungumza katika hafla hiyo.
Vyeti vikitolewa.
Wazazi wakiwa kwenye sherehe hiyo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Mgeni rasmi akikabidhiwa keki..
Mshereheshaji wa sherehe hiyo (MC) akiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi na walimu.



Na Dotto Mwaibale, Singida.


Kaimu Afisa Tarafa ya Ikungi mkoani hapa Yahaya Njiku amewataka vijana wanafunzi wa Katoliki Tanzania (TYCS) waliohitimu kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Ikungi kuwa wazalendo wa nchi yetu.

Njiku ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa wilaya hiyo Edward Mpogolo aliyasema hayo wakati akizungumza na wanafunzi hao katika sherehe ya kuagana na wanafunzi wenzao wa kidato cha 5-1 iliyofanyika juzi wilayani humo.

"Mnapaswa kuwa wazalendo na uzalendo unatafusiri nyingi kwanza unapaswa kuipenda nchi yetu kuifahamu  kuithamini na kuitunza." alisema Njiku.

Alisema wakiwa kama vijana wanaohitimu kidato cha sita na wale ambao wanaendelea na masomo ni lazima kwanza wawe wazalendo.

Alisema sisi tupo katika Taifa la Tanzania hatuna lingine zaidi ya Tanzania hivyo tunapaswa kulitunza na kulitetea popote pale duniani.  

Njiku aliwaambia vijana hao kuwa uzalendo unatakiwa kuuanza wakiwa na umri mdogo na kuwa hawawezi kuwa wazalendo pasipo kulielewa taifa lao kuanzia historia yake, misingi na jinsi lilivyopatikana.

"Niwaombe ninyi wahitimu na nyie mnaoendelea na masomo ni lazima mfahamu historia ya taifa letu kwani leo hii mpo hapa mna furaha kwa kucheza muziki, michezo mbalimbali na kubadilishana mawazo kuna watu waliteseka kuliangaikia taifa letu akiwepo Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere na wenzake.

Alisema ni muhimu kwa vijana hao kusoma masomo ya uraia ili waweze kulielewa taifa lao kwani wakilielewa wataweza kulitetea.

Katika hatua nyingine Njiku aliwataka vijana hao kuwa mabalozi wa kuhamasisha amani hapa nchini na kuwaombea viongozi wetu hasa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliapishwa hivi karibuni kuongoza nchi baada ya aliyekuwa Rais wetu Dkt.John Magufuli kufariki.

Aliwataka wahitimu hao kuendelea kumuomba Mungu ili waweze kuendelea na masomo yao ya  elimu ya juu kwani kumaliza kidato cha 5-6 sio mwisho wa kusoma.

"Nyinyi wanafunzi mnakila sababu ya kuendelea na masomo kwani Serikali  kupitia Rais wetu Mama Samia Suluhu imeweka mazingira bora ya kusoma kwa kutoa elimu bure." alisema Njiku. 

Aidha Njiku aliwaambia wahitimu hao kuwa nidhamu na uwajibikaji ni jambo jema litakaloweza kuwafanya waishi vizuri wakiwa shuleni, nyumbani na jamii na bila kuacha kumuomba Mungu ambaye siku zote hawezi kumuacha mtu amuombaye.

Njiku aliwataka vijana hao kuto jiingiza katika vitendo visivyo na maadili badala yake watumie muda wao kwa kujisomea na kuendeleza vipaji vyao vya michezo walivyonavyo na kuwapa heshima wazazi wao wanao wasomesha kwa kufanya vizuri mitihani yao.

Wahitimu hao 19 katika risala yao kwa mgeni rasmi walitaja baadhi ya mafanikio waliyopata wakiwa shuleni ni kushiriki katika kuchangia ujenzi wa parokia ya mtakatifu Rita wa Kashia wilayani humo.

Sunday, April 11, 2021

NDAHANI AVISHAURI VYAMA VYA MICHEZO KUTIMIZA AGIZO LA RAIS SAMIA LA KUENDELEZA MICHEZO YA WANAWAKE.

Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (katikati mwenye fulana ya blue) akikabidhi zawadi ya mbuzi kwa wachezaji wa Timu ya Muhanga FC baada ya kuwa washindi wa  michezo mbalimbali iliyofanyika mjini jana  mkoani haa yenye lengo la kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Mkurugenzi wa Shirika ya YUNA,  Ally Mwamzola (kushoto) akizungumzia umuhimu wa michezo. Kulia ni Afisa Michezo wa Manispaa ya Singida, Samweli Mwaikenda na Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani.
Zawadi zikitolewa kwa washindi wa michezo hiyo.
Zawadi zikitolewa
 


Na Dotto Mwaibale, Singida


KAIMU Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amevitaka vyama vya mechezo katika Mkoa wa Singida kuhakisha wanawasaidia vijana wa kike kutimiza ndoto za vipaji vyao kupitia agizo la Rais Samia Suluhu Hasssn alipolitoa kwa Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo wakati akiapisha Baraza jipya la Mawaziri. 

Rais Samia aligiza kuona michezo kwa upande wa wanawake inathaminiwa kama ilivyo  kwa wanaume ,hivyo vyama vya michezo vinawajibu kuweka mikakatika ya kukuza vipaji vya vijana wanawake kuanzia ngazi ya chini,

Ndahani aliyasema hayo wakati akitoa zawadi kwa washindi wa michezo mbalimbali iliyofanyika mjini Singida iliyokuwa na lengo la kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Michezo hiyo ilidhaminiwa na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Men engage,Youth of United Nation Association Tanzania (YUNA),Youth Movement for Change (YMC), Ofisi ya Mkurugenzi Manispaa na Chama cha Mpira wa Miguu Manispaa ya Singida.

Akimkaribisha mgeni Rasmi Mkurugenzi wa Shirika ya YUNA,  Ally Mwamzola amewataka wanaume kuhakikisha kuwa ukatili kwa wanawake na watoto unatoweka nchini kwani wanaume bado wanashiriki katika ukatili wa kijinsia.

Naye Afisa michezo wa Manispaa hiyo Samweli Mwaikenda ameyashukuru mashirika hayo Kwa kuamua kutumia michezo katika kutoa elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia,ameyataka mashirika mengine kuiga mfano kwani kuna faida kubwa kutumia michezo katika kutoa elimu.

Mkurugenzi wa Shirika la YMC Fudelis Lyunde  amemshukuru Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Ndahani kwa kukubali kuja kushiriki na vijana katika michezo na kuomba aendelee na moyo huo wa kuwa karibu na vijana ili wafikie ndoto  zao katika nyanja za michezo na uchumi.

Saturday, April 10, 2021

TAHA YAWAWEZESHA WANAWAKE WILAYA YA IKUNGI KUANZA KILIMO CHA MBOGAMBOGA

Wanawake wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka wilayani Ikungi mkoani Singida kutoka katika vikundi vinne vya Mfuu, Mrumba, Wajifya na Misenga wakitandaza mabomba juzi katika shamba lao la  kilimo cha mbogamboga baada ya kuwezeshwa na Asasi ya TAHA.
Mtaalamu wa Kilimo wa TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari (kulia) akiwaelekeza jambo wanawake hao wakati wa kuandaa shamba hilo.
Wanawake hao wakishiriki kuchimba mifereji kwa ajili ya kutandaza mabomba ya mfumo wa umwagiliaji katika shamba hilo.
Muonekano wa shamba hilo.
Wanawake wakishiriki kubeba mabomba kupeleka shambani.
Wanawake hao wakishiriki kuunganisha mabomba kabla ya kutandazwa shambani.


Na  Dotto Mwaibale, Singida 


WANAWAKE wa Kata za Sepuka na Irisya wilayani  Ikungi mkoani Singida wameanza kuandaa shamba kwa ajili ya kilimo cha mboga mboga na  matunda baada ya kuwezeshwa na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA.

Wamefikia hatua hiyo baada ya kupatiwa mafunzo na Asasi hiyo kwa kushirikiana na UN WOMEN pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi lengo likiwa ni kujikomboa kiuchumi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi wakati wakiandaa shamba hilo lililopo Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka kwa ajili ya kilimo hicho baadhi ya wanawake hao kutoka katika vikundi vinne vya Mfuu, Mrumba, Wajifya na Misenga walitoa pongezi kwa asasi hiyo na halmashauri hiyo kwa kuwathamini kwa kuwapelekea mradi huo.

Katibu wa Kikundi cha Mrumba, Asia Gudo alisema mradi huo wameupokea kwa mikono miwili na kuwa wamefurahi kwani  wanatarajia kunufaika kiuchumi na mazao watakayopata ambayo ameyataja kuwa ni nyanya, pilipili hoho na miche ya miembe watakapoyauza  fedha zitakazo patikana watawasomesha watoto wao, kununua mifugo na kujikimu kimaisha.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Mfuu, Mwahija Njiku alisema kupitia mradi huo waliowezeshwa na UN-WOMEN na TAHA utawakomboa kiuchumi na kuwapunguzia mzigo wanaume katika majukumu ya kulea familia.

Kwa upande wake Mayasa Omari ambaye ni Katibu wa Kikundi cha Wajifya aliipongeza asasi hiyo ya TAHA kwa kuwapelekea mradi huo ambao ni endelevu na kuwa utawakomboa wanawake kwa namna moja hama nyingine.

Mtaalamu wa Kilimo wa TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari alisema hivi sasa kwa kushirikiana na wanawake hao wapo katika hatua ya kufunga mifumo ya umwagiliaji katika mashamba manne na kuwa wamefikia hatua nzuri.

Alitaja mazao watakayoyapanda katika mashamba hayo kuwa ni nyanya maji, pilipili kichaa pamoja na vitunguu.

" Mazao haya yamekuwa zaidi ya moja kwenye eneo moja kwa sababu tutayatumia kama mashamba darasa ambapo wakulima watakuja kujifunza ili nao wapeleke teknolojia hiyo maeneo mengine.  

Bakari alisema kwa kuwa kilimo hicho ni kipya katika wilaya hiyo mwitikio wa wanawake hao ni mkubwa huku wakiwa na hamu ya kuona matokeo yake baada ya kupanda mazao hayo.

Asasi ya TAHA yenye makao yake makuu jijini Arusha inafanya kazi zake na kuendesha mradi kama huo  katika mikoa 25 ya Tanzania ikiwemo Arusha, Mwanza, Manyara, Kilimanjaro,Tanga, Dodoma, Morogoro, Iringa, Njombe, Pwani, Dar es salaam, Lindi, Mtwara, Mara, Simiyu, Mbeya, Songwe, Unguja ( Unguja Kaskazini, Unguja Kusini na mjini Magharibi ) na Pemba ( Pemba Kaskazini na Pemba Kusini ) ,Ikungi-Singida na  Shinyanga.

Thursday, April 8, 2021

MHE GEKUL AOMBA USHIRIKIANO BAINA YA VIONGOZI WAKUU WA WIZARA,WATENDAJI NA WATUMISHI

 

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Innocent Bashungwa (katikati mwenye tai nyekundu) akiwa  na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt Hassan Abbasi (mwenye tai ya bluu) wakimkaribisha Naibu Waziri, Mhe. Pauline Gekul alipowasili rasmi kwenye Ofisi yake mpya iliyopo eneo la Mji wa Serikali –Mtumba jijini Dodoma leo, baada ya kuapishwa  na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 01,2021 Ikulu ya Chamwino  kushika wadhifa huo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul akipokea maua kutoka  kwa wafanyakazi wa Wizara hiyo  kama ishara ya kumkaribisha rasmi kwenye Ofisi yake mpya iliyopo  eneo la Mji wa Serikali –Mtumba jijini Dodoma leo, baada ya kuapishwa  na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 01,2021 Ikulu ya Chamwino  kushika wadhifa huo

a.    Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Pauline Gekul akisaini  kitabu  cha wageni  mara baada ya  kuingia kwenye Ofisi yake mpya iliyopo eneo la Mji wa Serikali –Mtumba jijini Dodoma leo, baada ya kuapishwa  na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 01,2021 Ikulu ya Chamwino  kushika wadhifa huo.

                                     

Na John Mapepele, Dodoma


Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Sanaa na Michezo Mhe. Pauline Philipo Gekul ameomba ushirikiano baina Viongozi Wakuu wa Wizara, Watendaji na Watumishi wote wa Wizara ili kutekeleza majukumu ya Wizara hiyo kimamilifu kulingana na Miongozo ya Serikali, Maelekezo ya Mheshimiwa Rais na Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hatimaye matarajio ya wananchi yaweze kufikiwa.



Mhe. Gekul ameyasema haya alipowasili rasmi leo kwenye Ofisi yake mpya eneo la Mji wa Serikali- Mtumba jijini Dodoma mara baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kwenye nafasi hiyo hivi karibuni akitokea Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambako alikuwa akihudumu kwa nafasi hiyohiyo.



“Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara, madaraka haya tuliyopewa ni sawa na makoti ya kuazima hivyo tuna kila sababu ya kumtanguliza Mungu na kuimarisha ushirikiano ili kuleta matokeo tarajiwa kwa wananchi wetu wakati tunatekeleza majukumu yetu ya kila siku” amesisitiza Mhe. Gekul

Amemshukuru Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumwamini na kumrejesha tena kwenye nafasi hiyo pamoja na viongozi wote Wakuu wa Wizara hiyo ambapo ameongeza kuwa hali hiyo itarahisisha utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa ufanisi kwa kuwa watendaji wote wamerejeshwa na wanauzoefu wa kutosha.

Amemhakikishia Waziri Bashungwa kufanya kazi kwa bidii ya kumshauri na kumsaidia kwa kadiri ya uwezo wake wote kama msaidizi wake.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema Watumishi wote kuwa na mshikamano wa hali ya juu ambapo amesisitiza watumishi wasisubiri kusukumwa na Katibu Mkuu na badala yake wachape kazi ili kukidhi dhamira ya Mhe. Rais ya kuwatumikiwa wananchi kikamilifu.

“Napenda kusema tukigundua mahali popote kwenye Wizara yetu hakuna ushirikiano tutachukua hatua mara moja maana hiyo itakuwa ni hujuma kwa taifa”amefafanua Mhe. Bashungwa

Amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kumwamini na kumteua tena kuendelea kusimamia Sekta zilizo chini ya Wizara hiyo pia kumteua Mhe. Gekul kuja kuongeza nguvu katika kutekeleza na kumuahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutekeleza Ilani ya CCM na hotuba aliyoitoa awali kama mwongozo kwa Watendaji wote wa Serikali.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amemshukuru Mhe.Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini na kumteua kwa mara nyingine kuwa Katibu Mkuu na kumwahidi kushirikiana na Viongozi na Watumishi wote kutekeleza majukumu ya Wizara kwa weledi na kuzingatia taaluma.

Akizungumza kwenye Kikao cha Menejimenti ya Wizara hiyo mara baada ya kupokea maelekezo ya Waziri Bashungwa, Dkt. Abbasi amesisitiza watendaji wa Wizara kutoka na kuwa jirani na wadau wa sekta zilizochini ya Wizara hiyo kwa kuwa wanahitaji kulelewa kwa karibu.

Amesema jukumu la Wizara ni kuzisimamia sekta zilizo chini ya wizara hiyo kikamilifu kwa weledi ili kupata matokeo chanya kwa kuwa nchi yetu imebahatika kuwa na wasanioi wenye vipaji na vipawa vingi kinachotakiwa ni usimamizi madhubuti.

Wednesday, April 7, 2021

VIJANA IKUNGI WAONESHA UZALENDO WACHANGIA MADAWATI SHULE YA MSINGI MWISI


Viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwisi wilayani Ikungi mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja baada ya hafla ya makabidhiano ya madawati Shule ya Msingi Mwisi.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Mwisi kwenye shughuli za kukabidhi madawati.


Afisa Maendeleo Wilaya ya Ikungi  Haika Masawe akizungumza jambo kwenye hafla hiyo.




Afisa Mtendaji Kata ya Ndung'unyi, Yahaya Njiku ambaye pia ni mdau wa maendeleo akizungumza kwenye halfa hiyo ya kukabidhi madawati Shule ya Msingi Mwisi.

Wananchi wa Kijiji cha Mwisi wakiwasikiliza kwa makini viongozi kwenye halfa hiyo.

Madawati yakikabidhiwa. Kushoto ni Diwani wa Kata ya Lighwa Borgius Ntandu.

 Saimon Philipo mmoja wa vijana waliochangia madawati hayo akielezea namna walivyoguswa na kuamua kutoa msaada wao.

Viongozi wakiwa meza kuu.



Na Dotto Mwaibale, Singida.


VIJANA wazalendo kutoka Kijiji cha Mwisi Kata ya Lighwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wametoa Madawati kwenye Shule ya Msingi Mwisi kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha watoto wote wanakaa kwenye madawati wakati wa masomo yao.

Vijana hao ambapo kwa sasa wako maeneo mbalimbali,wameona vema kuunga mkono juhudi za Serikali na wameamua kuanzia nyumbani kwenye Shule walikosomea ambapo wamechangia madawati 37.

Akikabidhi Madawati hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Justice Kijazi amewapongeza Vijana hao ambapo amesema amefarijika kuona wazalendo wanaokumbuka kurudisha fadhila nyumbani.

"Hongereni sana ni watu wachache sana wanaokumbuka kurudisha fadhila,hivyo endeleeni kuchangia mnapoona kuna changamoto katika kijiji chenu.Na mimi nachangia madawati 20." alisema Kijazi na kuongeza.

"Vijana kwenye risala yenu mumesema kuna uhitaji wa kukarabati chumba cha Darasa katika Shule hii ambalo litatumika kama Ukumbi, nachangia mifuko 30 ya Saruji pamoja na kumlipa fundi,hivyo mtakapoanza mipango niambieni." alisema.

Kijazi aliwataka Vijana kubuni Miradi mbalimbali ili kufungua fursa za ajira zitakazopelekea maendeleo ya Elimu na mambo mengine ambapo aliwaahidi kuwa Halmashauri kupitia asilimia 10%  zinazotengwa itatoa mikopo hiyo kwa Vijana watakao anzisha miradi ya maendeleo.

Aidha mmoja wa vijana hao waliounda umoja wa wanadarasa waliohitimu Shule ya Msingi Mwisi Mwaka 2007,Saimon Philipo alisema waliona zawadi pekee ya kulipa nyumbani ni kutengeneza madawati ili wadogo zao wasome kwenye mazingira mazuri.

"Sisi tuliamua kuanzisha umoja wetu ili tuweze kuchangia shughuli za maendeleo,Sio tu hapa tutafanya hata maeneo mengine lakini tuaona tuanzie kwanza nyumbani." alisema Saimon.

Naye Diwani wa Kata hiyo Borgius Ntandu aliwataka Vijana wa Kata hiyo kuwa chachu ya maendeleo kwa kuiga mfano wa Vijana wengine wazalendo wanaunga mkono juhudi za Serikali.

Hata hivyo Diwani huyo aliwapongeza wananchi wa kijiji cha Mwisi kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha inawaletea maendeleo wananchi wake.

Kwa upande wake Mdau wa maendeleo wilayani humo Yahaya Njiku ambaye pia ni Afisa Mtendaji Kata ya Ndung'unyi alisema uzalendo wa vijana utapimwa kwa utendaji kazi wao na sii vingine,hivyo akawaomba vijana wengine kuwa wazalendo kwa kushiriki shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

"Huyu Saimon mmoja waliochangia madawati haya nimesoma naye kidato cha tano na sita na amekuwa rafiki yangu sana,nimeona nimuunge mkono katika hili na hata mengine.Nachangia sh.elfu Hamsini." alisema Njiku.