Friday, June 4, 2021

WANAWAKE ZAIDI 2300 WILAYANI IKUNGI KUNUFAIKA NA MRADI WA UN WOMEN

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa  Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, akitoa maelezo kwa Maafisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA),  Shirika la Umoja wa Mataifa la  Maendeleo la Japani (KOICA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na usawa wa kijinsia na wanawake (UN Women) wakati wa ziara yao ya siku moja ya kukagua mradi walioufadhili uliopo katika Kata za Dung'unyi, Sepuka na Irisya wilayani Ikungi mkoani Singida ili kuona utekelezaji wake na matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Koica
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki (kushoto) akitoa maelezo  ya kilimo chenye tija cha zao la alizeti kwa maofisa hao.
Maofisa hao wakiwa kwenye kikao na wakulima (hawapo pichani) wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka. Kutoka Kulia ni Kaimu Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Julia Broussaud, Kaimu Mkurugenzi Mkazi kutoka Koica, Jieun Mo na Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia kutoka Shirika la UNFPA,  Maja Wanach. .
Mtaalamu wa Kitengo cha kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kutoka UN Women, Lillian Madanga, akizungumzia mradi huo kwa ujumla wake.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumzia mradi huo jinsi utakavyo wanufaisha.
Mkuu wa Idara ya Uzalishaji wa TAHA, Gilliard Mollel, akitoa maelezo  ya kilimo cha mbogamboga na matunda kwa maofisa hao.
Ziara ya ukaguzi wa mradi huo ikiendelea.
Ukaguzi wa mradi huo ukiendelea.
Kaimu Mwakilishi Mkazi wa UN Women, Julia Broussaud, akiwaelekeza jambo maofisa wa shirika la TAHA. Kutoka kulia ni Mkuu wa Idara ya Uzalishaji wa TAHA, Gilliard Mollel, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi na Mratibu wa Mradi wa TAHA, Glory Prosper.
Wanawake wa Kipumbwiko wakiwa shambani wakati wa ukaguzi wa mradi huo.


Maofisa hao wakiwa kwenye kikao na wakulima (hawapo pichani) wa Kijiji cha Mnang'ana Kata ya Sepuka.
Wakulima wa zao la Alizeti wa Kata ya Sepuka, Fatuma Said na Zainabu Hussein (kulia) wakionesha moja ya alizeti iliyostawi vizuri baada ya kuzingatia kilimo bora 
Meneja Mwandamizi wa mradi kutoka Shirika la Farm Africa, Tumaini Elibariki (kushoto) akitoa maelezo  ya kilimo chenye tija cha zao la alizeti kwa maofisa hao.
Wakulimawa Kata ya Irisya wakiimba nyimbo wakati wakiwakaribisha maofisa hao.
Shamba la mfano la mbogamboga la Kata ya Irisya.
Msaidizi wa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa  TAHA, Simon Mlay (kushoto) akitoa maelezo  ya kilimo cha mbogamboga na matunda kwa maofisa hao katika shamba la mfano la Kata ya Irisya.
Msimamizi wa Mashamba ya TAHA Mkoa wa Singida, Mohamed Bakari,  akitoa maelezo  ya kilimo cha mbogamboga na matunda kwa maofisa hao.
Wananchi wa Kata ya Irisya wakiwa shambani wakati wa ukaguzi huo.
Wananchi wa Kata ya Irisya wakiwa shambani wakati wa ukaguzi huo.. Kulia mwenye shati jeupe ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ally Mwanga na Diwani wa kata hiyo.

Mkulima wa Kijiji cha Kipumbwiko kutoka Kikundi cha Upendo, Rachel John, akizungumzia faida ya mradi huo.
Mkulima wa Kijiji cha Kipumbwiko kutoka Kikundi cha Jimudu, Elizabeth Myumbi, akiyashukutu mashirika hayo kwa kuwapelekea mradi huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


ZAIDI ya Wanawake  2300 wilayani Ikungi mkoani Singida wanatarajiwa kunufaika na mradi wa kilimo cha alizeti na mbogamboga kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA),  Shirika la Umoja wa Mataifa la  Maendeleo la Japani (KOICA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na usawa wa kijinsia na wanawake (UN Women)

Hayo yalibainika jana wakati wa ziara ya siku moja ya maofisa wa mashirika hayo ya kukagua mradi uliopo katika Kata ya Dung'unyi, Sepuka na Irisya wilayani hapa ili kuona utekelezaji wake na matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa na Koica ambapo wameridhishwa na utekelwezaji wa awamu ya kwanza wa mradi huo.

Mradi huo wa miaka mitatu ulioanza mwaka jana mkoani hapa unatekelezwa na mashirika hayo,  Serikali ya Tanzania,  Farm Africa na Asasi kilele ya sekta binafsi inayojihusisha na kuendeleza tasnia ya horticulture hapa nchini ijulikanayo kama TAHA katika mikoa ya Singida na Shinyanga.

Akizungumza katika ziara hiyo Mtaalamu wa Kitengo cha Kuwawezesha Wanawake Kiuchumi kutoka UN Women, Lillian Madanga alisema wanafanya kazi hiyo kisera kwa kushirikiana na Serikali, Sekta binafsi na Halmashauri ambazo wana miradi hiyo yenye lengo la kuwainua wanawake kiuchumi kupitia kilimo cha mbogamboga matunda na alizeti.

Alisema katika kilimo cha mbogamboga na matunda wanafanya kazi na TAHA ambao wanauzoefu mkubwa na kilimo hicho hapa nchini kwa ufadhili wa Koica ambao wametoa fedha na kuwa kwa siku za mbeleni wananchi wa Ikungi watabadilika kimaendeleo kupitia kilimo hicho.

"Lengo letu kubwa la kuanzisha kilimo hiki na kuwapa teknolojia na kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi,"  alisema Madanga.

Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akizungumza katika ziara hiyo aliishuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha hizo katika wilaya hiyo na kuwa watafanya kila liwezekanalo na kuona kilimo hicho kinanakuwa endelevu na kinawapeleka mbele.

Aidha Kijazi alisema kuwa mradi huo  utagharimu zaidi ya Sh.Bilioni 5.2 na kuwa umegawanyika katika aina kuu tatu, kilimo cha alizeti ambacho kinaongozwa na Farm Africa, Kilimo cha mbogamboga kinachoongozwa na TAHA na Mradi wa kuwawezesha wanawake kijinsia.

Alisema kwa mwaka huu wa mradi takribani dola 900,000 zimeruhusiwa na Koica na zinaendelea kufanya kazi katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi.

Alisema mradi huo utakuwa kichocheo cha maendeleo katika halmashauri hiyo na kioo ambapo watatarajia kupata wawekezaji wengi baada ya kuona ardhi ya wilaya hiyo kuwa na rutuba ambayo kila aina ya mazao yanastawi.

Alisema jambo kubwa wanalolifanya hivi sasa ni upimaji wa ardhi katika vijiji vinne ambavyo wanavipima kupitia fedha za mradi huo ambavyo ni Kipumbwiko, Irisya, Munyu na Mnang'ana.

"Katika vijiji hivyo tunatenga maeneo mbalimbali  kwa ajili ya matumizi ya kilimo, makazi, misitu na ufugaji jambo litakalotusaidia kujua iwapo akitokea mwekezaji wa eneo husika kati ya haya yaliyotajwa tujue kwa kumpeleka," alisema Kijazi.

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi alisema asasi hiyo yenye makao makuu yake jijini Arusha inafanya mradi huo Msalala mkoani Shinyanga na Ikungi mkoani Singida na imejikita zaidi kuwawezesha wadau katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mboga mboga, matunda, maua, viungo na mazao ya mizizi ambapo katika wilaya hiyo wameweza kuanzisha mashamba darasa . 

Alisema katika wilaya hiyo wameweza kuwapa wakulima teknolojia za kisasa za kilimo cha mbogamboga, matunda, maembe,vitunguu, pilipili kichaa, matumzi ya mbegu bora na kuwa wamepata soko nje ya nchi na mnunuzi wa mazao hayo zikiwemo pilipili atakazo zinunua kwa Sh.6000 kwa kilo.

Aliwataja wadau wanao wawezesha katika mnyororo huo wa thamani kuwa ni wasambazaji wa pembejeo, wakulima, wasindikaji, wafanyabiashara, wasafirishaji na makampuni yanayofanya usafirishaji nje ya nchi na wanawawezesha kwa vitendo.

"  Katika uwezeshaji wetu kazi kubwa tunazozifanya ni kuwaunganisha wakulima na masoko, kuwawezesha wakulima katika suala zima la kilimo na kuwaonesha teknolojia mbalimbali ambazo wanaweza kuzitumia kulingana na uwezo na mazingira waliopo." alisema Mkindi.

Alitaja kazi ya nyingine kuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara na kuwa wanafanya kazi hiyo kwa kushirikiana kwa karibu na serikali kuu kwa maana ya kushawishi na kutetea sera zile ambazo zinamuumiza mzalishaji, mfanyabiasha na mdau yeyote katika mnyororo wa thamani.

Aidha Mkindi alitaja kazi nyingine kuwa ni kuwaunganisha wadau katika mnyororo wa thamani na vyombo vya fedha baada ya kuwafundisha elimu ya fedha.

RAS MPYA SINGIDA AJIPANGA KUPIGANIA ELIMU YA MTOTO WA KIKE.

Aliyekuwa  Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi (kulia ), akimkabidhi kabrasha,  Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Singida, Doroth Mwaluko katika hafla  ya makabidhiano iliyofanyika jana mkoani hapa. , 
Aliyekuwa  Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi akizungumza katika hafla ya kukabidhi ofisi iliyofanyika jana mkoani hapa.
 Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Singida, Doroth Mwaluko akizungumza wakati akikabidhiwa ofisi mjini hapa jana
 Katibu Tawala Mpya wa Mkoa wa Singida, Doroth Mwaluko (kushoto) na Aliyekuwa  Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Angelina Lutambi ambaye ameamishiwa Jijini Mbeya wakisaini nyaraka za makabidhiano ya ofisi jana.

Wakuu wa  Idara mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo ya makabidhiano ya ofisi .
makabidhiano ya ofisi  yakiendelea.
Wakuu wa  Idara mbalimbali wakiwa kwenye hafla hiyo ya makabidhiano ya ofisi .
 




Na Mwandishi Wetu, Singida,
  
 Katibu Tawala mpya  wa Mkoa wa Singida  Dorothy Mwaluko  amekabidhiwa rasmi ofisi na mtangulizi wake Dkt Angelina Lutambi huku akiahidi kusimamia kidete  elimu ya  mtoto wa kike .  

Akizungumza jana kwenye hafla ya makabidhiano hayo Mwaluko pamoja na mambo mengine ameomba ushirikiano kutoka kwa watendaji wote mkoani hapa ili kusukuma kasi ya maendeleo lakini zaidi kuleta ustawi kwenye eneo la elimu na maboresho ndani ya sekta ya afya.

"Kitaaluma mimi ni mwalimu,na kipaumbele changu hasa ni masomo ya sayansi natamani na nitasimamia kuhakikisha watoto wa kike wanasoma masomo haya kwa mafanikio makubwa,alisema katibu Tawala na akaongeza;

"Kwenye elimu msitarajie kunidanganya na atakaye kwenda kinyume hatutaelewana," alisema 

Aidha kwenye eneo la afya ameomba kila mtendaji kuwajibika ipasavyo ili matarajio ya wanasingida yazidi kudhihirika kupitia serikali yao inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Lutambi ambaye kwa sasa amehamishiwa Mkoa wa Mbeya, pamoja na mambo mengine amemueleza Mwaluko kuwa hali ya uchumi wa Mkoa inaenaendelea kuimarika siku hadi siku.

Hata hivyo ameshauri kuwepo kwa msukumo mkubwa na usimamizi kwenye utekelezaji wa sheria ya fedha za serikali za mitaa hasa kupitia tangazo la serikali namba 286 la April 5, 2019 ambalo lilielekeza asilimia 10 ya fedha za mfuko wa Wanawake,Vijana na wenye ulemavu zitolewe ipavyo.

TRAFIKI SINGIDA WAZINDUA KAMPENI YA USALAMA BARABARANI

 Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa Mrakibu wa Polisi (SP) Nestory Didi akikagua matairi ya Basi la Kampuni ya Ally' Star wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Safiri Salama Usalama Wetu Kwanza walioianzisha yenye lengo la kupunguza au kumaliza kabisa changamoto za ajali mkoani hapa.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Singida, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Robert Sewando, akiwaelekeza jambo SP Didi wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo. 

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa, Mrakibu wa Pilisi (SP) Nestory  Didi akizungumza na baadhi ya wajumbe wa kamati ya usalama barabarani mkoani hapa kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa, SP Didi akiwaelekeza jambo askari wa usalama barabarani wakati wa kampeni hiyo.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa, SP Didi akisalimiana na dereva wa Basi la Nyahunge Simon Mtakune wakati wa Kampeni hiyo.

Ukaguzi wa mabasi ukiendelea.

Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoani hapa wakiingia ndani ya moja ya mabasi yaliyokuwepo kituoni kutoa elimu kwa abiri ya usalama barabarani. Kulia ni Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa, SP Didi.

Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa, SP Didi, akizungumza na waandishi wa habari na wadau wa usafirishaji.

Mjumbe wa Kamati ya Usalama Barabarani mkoani hapa Fatuma Malenga akizungumza kwenye uzinduzi huo kuhusu matumizi ya barabara kwa watu wenye ulemavu..

Dereva Musa Shikobe akizungumzia  na waandishi wa habari kwenye  uzinduzi huo.

Wakala wa Mabasi ya NBS Daffi Nyandekwa akizungumzia umuhimu wa madereva kufuata sheria na kanuni zilizowekwa za usalama barabarani.


Na Dotto Mwaibale. Singida


JESHI la Polisi mkoani hapa kupitia kikosi cha Usalama Barabarani  (TRAFFIC) limeanzisha kampeni kambande ya utoaji wa elimu ili kumaliza kabisa changammoto za ajali mkoani hapa.

Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo Kituo Kikuu cha Mabasi  Misuna,  Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa Mrakibu wa Polisi (SP) Nestory Didi alisema wameianzisha kampeni hiyo yenye lengo la kupunguza ajali au kuzimaliza kabisa.

Alisema kampeni hiyo ambayo itakuwa endelevu wameipa jina la Safiri Salama Usalama Wetu Kwanza ambapo watakuwa wakiyakagua mabasi na magari yote na kutoa elimu kwa watumiaji wa wakiwamo abiria.

" Kama mnavyoshuhudia ninyi wenyewe haya matukio ya ajali yanayoendelea kutokea sisi kama jeshi la polisi jukumu letu ni kulinda maisha ya raia na mali zao hivyo tumeamua kutoa elimu na kuhamasisha abiria na makundi mengine yanayotumia barabara wakiwepo watembea kwa miguu, waendeshaji wa bajaj, wanafunzi, bodaboda na walemavu," alisema Didi.

Didi alisema makundi hayo yote yanatumia vyombo vya moto hivyo wanachotaka ni kuona wanakuwa salama pale wanapotumia barabara za umma.

Leo tumeongea na abiria vile vile na madereva kuhusu wajibu wao wanapokuwa wanaendesha magari na tumewaeleza wanatakiwa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa za usalama barabarani lengo likiwa wanahakikisha wanawafikisha abiria wao salama wanakokwenda.

Aidha Didi alisema abiria nao wanajukumu la kuwasaidia jeshi la polisi kukemea yale maovu yanayofanyika pindi wanapokuwa kwenye safari akitolea dereva anayelipita gari jingine kwenye kona au anayeyapita magari sita kwa wakati mmoja huyo asipokemewa ni lazima ajali zitaendelea kutokea.

Alisema baada ya kuongea na madereva hao wamesema kuanzia leo hii ajali zitabaki kuwa ni historia kwa kuwa watazingatia sheria na kuwa abiria nao watakuwa mabalozi wao wa kutoa taarifa pindi watakapo kuwa wanaona mambo yanaenda tofauti.

Didi alisema wametoa namba za simu popote watakapo kuwa wanaweza kupiga simu au kutuma ujumbe na wao watachukua hatua ya kumkamata dereva husika.

Dereva Musa Shikobe na wakala wa mabasi ya Kampuni ya NBS, Daffi Nyandekwa walisema madereva wanatakiwa wajenge tabia ya kujisimamia wenyewe kwani abiria wanao wabeba ni ndugu zao hivyo wanaposabaisha ajali wanapoteza nguvu za taifa na familia.

Tuesday, June 1, 2021

SINGiDA YAANZA RASMI KUKUSANYA USHURU WA MAEGESHO KWA MFUMO WA KIELEKRONIKI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt,Binilith Mahenge akizungumza kabla ya kuzindua mfumo mpya  wa kielektoniki wa ukusanyaji mapato kupitia maegesho ya  vyombo vya moto.
Baadhi ya watendaji wakuu wa chama na serikali wakifuatilia matukio ya hafla ya uzinduzi  wa mfumo huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida Alhaj Juma Kilimba akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mratibu wa Tarura, Mkoa wa Singida Mhandisi, William Boniphace. akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mchambuzi wa Mifumo kutoka makao makuu ya TARURA, Joseph Chigalula  akieleza jinsi ya kufanya malipo ya ushuru wa maegesho kwa kutumia mfumo huo mpya .
Mkutano ukiendelea .
Mkutano ukiendelea .
Mkutano ukiendelea .
Mkutano ukiendelea .
Mrakibu wa Polisi (SP) Nyangi Choma akichangia jambo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida Yagi Kyaratu akichangia jambo.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Singida, Ally Mwendo, akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Mkaguzi wa Polisi Geofrey Karia akizungumza.
Katibu CCM Mkoa wa Singida  Lucy Shee akichangia maboresho ya mfumo huo.
Mtaaramu  wa Kitengo cha Mapato  kutoka TARURA Makao Makuu, Osward  Mobily akifafanua jinsi ya kufanya malipo kwa mfumo wa TeRMIS.


 

Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida.

 

MKOA wa Singinda umefanya uzinduzi rasmi wa mfumo wa kielekroniki wa ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya vyombo vya moto (Parking Fees) unaojulikana kama TeRMIS. 

TeRMIS yaani 'Tarura e-Revenue Management Information System' ni mfumo mpya unaolenga kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali ili kusaidia matengenezo na maboresho ya miundombinu ya barabara. 

Akizindua mfumo huo mkoani hapa Mkuu wa Mkoa Dkt.Binilith Mahenge amewasihi wananchi kuukubali na kuupokea mfumo huo ambao una nia njema. 

Alisema lengo hasa ni kuleta ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, lakini una nia ya kumpunguzia mtumiaji wa maegesho kero ya kudaiwa ushuru. 

Imeelezwa kuwa baada ya kujisajili  mtumiaji ataanza kulipa mwenyewe ada za ushuru stahiki kwa siku, wiki au mwezi kulingana na mahitaji kwa kutumia mtandao wowote wa simu au tawi la Benki ya NMB, CRDB na wakala wa huduma hizo. 

Dkt. Mahenge alisema unafuu mwingine wa mfumo huo ni kumsaidia mteja kufanya maombi ya kulipia huduma mahali popote alipo bila kulazimika kufika ofisi za Tarura. 

Hata hivyo mkuu wa mkoa amewataka Tarura kuwa makini kwa kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa kina kwa waliopewa dhamana ya kukusanya mapato hayo ili kuhakikisha hakuna udanganyifu.

" Nitoe wito kwa wananchi kuyapokea mabadiliko haya na kulipa wenyewe ushuru wa maegesho ili kuepuka tozo za faini zisizokuwa za lazima," alisema Dkt. Mahenge huku akiwataka Tarura kuhakikisha elimu juu ya matumizi ya mfumo huo mpya inawafikia wananchi ili kuwa na uelewa wa pamoja. 

Akifafanua jinsi ya kufanya malipo kwa mfumo wa Termis Mtaalamu kutoka Kitengo cha Mapato Makao Makuu Tarura, Osward Mobily alisema mteja anaweza kulipia ushuru wa maegesho kwa Saa, Siku, Wiki au Mwezi. 

Alieleza kwamba jinsi ya kufanya malipo mteja atalazimika kuomba mwenyewe kumbukumbu namba ya malipo kwa ajili ya kufanya malipo ya kabla kupitia namba *152*00#. 

Alivitaja vyombo vya usafiri vitakavyohusika na ushuru wa maegesho hayo kuwa ni pamoja na pikipiki ya miguu mitatu kwa ushuru wa sh.300 kwa siku, Sh.1500 kwa wiki na Sh.6000 kwa mwezi. 

Pia gari isiyozidi tani 2 kwa ushuru wa Sh.500 kwa siku, 2500 kwa wiki na 10,000 kwa mwezi, huku  gari inayozidi tani 2 lakini isiyozidi tani 3 itatozwa Sh.200 kwa saa, Sh.1000 kwa siku, Sh.5000 kwa wiki na Sh.20,000 kwa mwezi. 

Kwa mujibu wa Tarura gari inayozidi tani 3 itatozwa Sh.400 kwa saa, Sh.2000 kwa siku, Sh.10,000 kwa wiki na Sh.40,000 kwa mwezi, huku gharama ya Maombi ya Maegesho Maalumu yatatozwa kwa gharama ya Sh 20,000 kwa mwezi baada ya mteja kujaza fomu ya maombi au kupitia App ya TeRMI. 

"Mmiliki wa chombo cha moto anatakiwa kulipa Ushuru wa Maegesho ndani ya siku 7 endapo atashindwa kulipa ndani ya muda atapaswa kulipa mara mbili ya kiasi anachodaiwa," alisema Mchambuzi wa Mifumo kutoka Tarura, Joseph Chigalula na akaongeza; 

" Endapo atashindwa kulipa tozo hiyo pamoja na deni analodaiwa kwa muda unaozidi siku 14, atafikishwa mahakamani na akitiwa hatiani atalipa faini ya Sh.laki tatu au kifungo miezi 12 au vyote kwa pamoja," alisema Chigalula.