Tuesday, January 17, 2023

RC SINGIDA AWATAKA VIONGOZI WILAYA YA IRAMBA KUTEKELEZA WAJIBU WAO KWA WANANCHI

Mkuu wa Mkoa wa Singida. Peter Serukamba (kulia) akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Iramba ikiwa ni siku yake ya pili baada ya kuanzisha utaratibu wa kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja katika kikao kilichofanyika jana Januari 18, 2023. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauriya Wilaya ya Iramba, .Dk. Hussein Sepoko na Mkuuwa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa Singida. Peter Serukamba amewataka viongozi na watumishi wa Serikali Wilaya ya Iramba mkoani hapa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi kwa bidii na si vinginevyo.

Serukamba ameyasema hayo jana Januari 17, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Iramba ikiwa ni siku yake ya pili baada ya kuanzisha utaratibu wa kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.

Alisema jambo kubwa aliloliona baada ya kusililiza kero hizo ni baadhi ya viongozi kushindwa kutekeleza wajibu wao ambapo aliwaomba watekeleze wajibu wao kwa kutoa huduma kwa wananchi ndio kazi yao.

“Kazi yetu ni kuwahudumia wananchi ukiwasikiliza mambo yote waliyoyasema hapa wala hayahitaji bajeti bali ni kusikilizwa na watu wanaojitoa kwa wenzao hivyo nakuomba mkurugenzi na wenzako haya yote tuliyo yabaini nendeni mkayafanyie kazi na jumanne mniletee mrejesho wa utekelezaji wake” alisema Serukamba.

Alisema hakuitisha kikao hicho kwa lengo la kusikiliza kero zao tu bali ni kuwasikiliza na kuzitatua kero hizo na kuwa zile ambazo hawatakuwa na uwezo nazo watazipeleka ngazi nyingine ya juu kwa ajili ya hatua nyingine na zile ambazo zipo ndani ya uwezo wao ni lazima wazitatue.

Serukamba alisema changamoto kubwa iliyojitokeza kutoka kwa wananchi hao ni ya migogoro ya arddhi ambapo alimuomba kamishna wa ardhi na timu yake kujipanga kwa ajili ya kutatua jambo hilo.

Alimwagiza kaimu mkurugenzi wa wilaya hiyo kusimamia haki ya wafanyakazi na alimuomba Afisa Utumishi kusimamia utekelezaji wa kazi kwa kufuata sheria na utaratibu uliowekwa wakati wa kutekeleza wajibu wao.

Alisema wananchi hao wanatarajia kusaidiwa changamoto walizo nazo ambazo sio kubwa lakini wao wamekuwa wakitumia muda mwingi  kwenda kusimamia masuala ya kujenga barabara, madarasa lakini yale yanayowahusu watu hawashughuliki nayo.

“Mimi naamini watu hawa ambao changamoto zao hamzifanyii kazi ndio waliyoiweka Serikali iliyopo madarakani hivyo wangetamani kuona inatatua matatizo yao kupitia sisi tuliopewa dhamana ya kufanya hivyo baada ya kupekwa kufanya kazi ya kuwatumikia” alisema Serukamba.

Serukamba aliwaomba viongozi na watumishi wa wilaya hiyo kubadilisha mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea badala yake uwe mfumo wa kutatua changamoto za wananchi ambapo alimtaka mkuu wa wilaya hiyo kwenda kwenye Tarafa, Kata na maeneo mengine kusikiliza changamoto za wananchi na kuwa ile tabia ya kufanya kazi bora iende wakati wake umepita.

Aliwatka wafanyakazi wa halmashauri hiyo kujiuliza wanapokwenda kazini kuanzia jumatatu hadi ijumaa kujiuliza wamefanya nini na wamewahudumia wakina nani na akaomba wawe na lugha nzuri kwa wanaowatumikia.

Aidha Serukamba aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kuhakikisha inaondoa takataka zote zilizopo kwenye maguba yaliyopo kwenye makazi ya watu na maeneo mengine ambapo alitoa ahadi ya kurudi kukagua maeneo hayo na wasije wakaelewana vibaya pindi atakapozikuta takataka hizo.

Baadhi ya kero zilizotolewa katika kikao hicho ni jinsi gani ya kulipwa fidia kwa mtu aliyeshambuliwa na tembo kero iliyotolewa na Hamphrey Philemon, Walimu wa Wilaya za Mkalama na Iramba ambao wana kidai chama cha akiba na mikopo cha Chamwai fedha zao waliochangia ili ziweze kuwasasidia baada ya kustaafu kero iliyowasilishwa na Mwalimu Zefania Makala, Uharibifu wa mazingira iliyotolewa na Janeth Mwendo, kutolipwa fidia kwa mmiliki wa eneo ilipojengwa Shule ya Sekondari ya New Kiomboi iliyotolewa na Stephano Juma.

Kero zingine ilikuwa ni malalamiko yaliyotolewa na Paul Alphonce aliyedai kulipia kupata huduma ya maji akiwa na wenzake  ambao walitoa Sh.150,000 kila mmoja lakini hadi leo hii bado hawajafkishiwa huduma hiyo, kero nyingine ilitolewa na Mjasiriamali Anna Kizinga ambaye aliomba kupunguzwa kwa ushuru katika minada kutokana na biashara zao kuto nunuliwa, kero nyingine ilikuwa ni kukithiri kwa uchafu katika baadhi ya maguba yaliyopo mjini Kiomboi iliyotolewa na Zabron Malecela, kero ya kupelekewa mbolea ya ruzuku ambayo wakulima hawajaizoea iliyotolewa na Elia Zefania.

Kero nyingine iliyotolewa ni iliyowahusu watu wenye ulemavu wilayani humo ambao wanaidai halmashauri ya wilaya hiyo fedha za kujikimu walipokwenda kwenye maadhimishoya siku ya watu wenye ulemavu.

Kero nyingine iliyotolewa ilitolewa na Frank Nkundi ambaye anadai fidia ya kupata ajali akiwa kazini na Michael Juma ambaye anaidai halmashauri hiyo Sh, Milioni 1.3 kama kiinua mgongo baada ya kustaafu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali mkoani hapa, pamoja na wakuu wa idara ili kuzisikiliza na kuzitafutia ufumbuzi ambapo kikao kama hicho kitafanyika katika wilaya zote ambapo leo Januari 18, 2023  kitafanyika Wilaya ya Mkalama.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba,Suleiman Mwenda, akizungumzia malalamiko ya walimu 162 wanao kidai Chama cha kuweka na kukopa cha Chamwai.
Taswira ya kikao cha kupokea kero za wananchi kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Elizabeth Msengi akitoa kero yake inayohusu ardhi.
Afisa Ardhi Wilaya ya Iramba Bwana Magesa akitoa maelezo baada ya kutolewa kwa kero za migogoro ya ardhi kwa mkuu wa mkoa.
Mwalimu Zefania Makala akielezea kero ya madai ya fedha zao dhidi ya chama cha Chamwai.
Kero za wananchi zikiandikwa.
Baadhi ya walimu wanaokidai chama cha Chamwai wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kueleza kero yao kwa mkuu wa mkoa.
Beatrice Jonathan akitoa kero yake.
Agustino Makute akitoa kero zake mbele ya mkuu wa mkoa.
Paul Alphonce akielezea kero yake ya kutopelekewa huduma ya maji licha ya yeyena wenzake 19 kulipia Sh.150,000.
Philemon Hamphrey akiomba kujua malipo ya fidia kwa mtu aliyejeruhiwa na tembo.
Mjasiriamali Anna Kizinga akiomba ushuru upunguzwe.
Zabron Malecela akizungumzia kero ya kukithiri kwa takataka katika maguba.
Elia Zefania akizungumzia changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Watu wenye ulemavu Wilaya ya Iramba, Athuman Kingu akizungumzia malipo ya fedha zao za kujikimu baada ya kwenda kwenye maadhimisho ya siku ya walemavu duniani.

Friday, January 13, 2023

WAZIRI NAPE: SERIKALI INAFANYA KAZI KUBWA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA MAWASILIANO NCHINI

Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (katikati) akikata utepe kuashia uzinduzi wa Mnara wa Simu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) uliojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika hafla iliyofanyika jana Kijiji cha Misughaa kilichopo Wilaya ya Ikungi  mkoani Singida.  
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Mhandisi Peter Ulanga (kushoto) akitoa taarifa ya ujenzi wa mnara huo mbele ya Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba, akizungumzia mradi huo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye (katikati) Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi wakiserebuka sanjari na wakina mama wa Kijiji cha Misughaa kabla ya uzinduzi wa mnara huo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu akielezea kwa kifupi mradi huo na kutoa shukurani kwa niaba ya wananchi kwa  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha fedha za ujenzi wa mnara huo.

Meneja wa TTCL Mkoa wa Singida, Agustino Mwakyembe akizungumza kwenye uzinduzi huo.

Muonekano wamnara huo.
Viongozi na wananchi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Wanafunzi wa Shule ya Dk. Shein wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto, akizungumza kwenye hafla hiyo.
Wanafunzi wakiwa kwenye hafla hiyo.
Hafla ikiendelea.
Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye, akionesha furaha yake baada ya Wazee wa Kijiji cha Misughaa kumpa heshima ya uchifu kwa kumvika mgolole na kumpa ngao na mkuki ikiwa ni heshima ya kimila kwa kabila la Wanyaturu. Kulia ni Mbunge wa Jimbola Singida Mashariki Miraji Mtaturu akifurahia tukio hilo.

Na Dotto Mwaibale, Singida

WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema kutokana na kasi ya ukuaji wa teknolojia Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya mawasiliano kwa kujenga minara ya simu ili kuwawezesha wananchi kupata mawasiliano kote nchini.

Nape ameyasema hayo jana Januari 11, 2022  wakati akizindua mnara wa simu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) uliojengwa na Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) katika Kijiji cha Misughaa kilichopo Wilaya ya Ikungi  mkoani Singida.

Kuzinduliwa kwa mnara huo kuna kwenda kuondoa adha ya muda mrefu waliokuwa wakiipata wananchi wa vijiji sita kutoka Kata za Kikio na Misughaa ya kukosa huduma ya mawasiliano ambapo katika Kata ya Misughaa ni  Kijiji cha Msule, Sakaa na Misughaa na Kata ya Kikio ni Mkunguwakihendo, Munane na Nkundi .

Nape alisema katika Mkoa wa Singida kuna miradi 31 ya ujenzi wa minara, miradi 27 ikiwa imekwisha kamilika huku minne kati ya hiyo ikiendelea na yote ikiwa na thamani ya Sh.5 Bilioni na kuwa maeneo mengine itakapo jengwa minara hiyo ni Kata ya Mang’onyi na Makiungu,kama alivyoomba Mbunge wa jimbo hilo Miraji Mtaturu.

Alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua changamoto hiyo ametoa kiasi hicho cha fedha na kuwa kuna miradi zaidi 33 imekwisha tangazwa na tenda yake itafunguliwa mwishoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kuongeza minara mingi zaidi.

Nape aliomba inapojengwa minara hiyo kuwepo na miundombinu wezeshi kama umeme na barabara ili kupunguza gharama za kuiendesha.

Katika hatua nyingine Nape aliahidi kutoa saruji mifuko 400 kwa ajili ya Shule ya Sekondari ya Dk.Shein saruji ambayo ataipata kwa kushirikiana na makampuni ya simu mbalimbali na kabla ya kutaoa ahadi hiyo wazee wa kijiji hicho walimpa heshima ya uchifu kwa kumpa ngao, mkuki na kuvikwa mgolole.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Mhandisi Peter Ulanga alisema ujenzi wa mnara huo ulikamilika tangu mwaka jana na kazi iliyobakia ni ujenzi wa nyumba ya mlinzi na choo na kuwa mnara huo unafanya kazi vizuri na huduma kwa wananchi inapatikana.

Mkuu wa Mkoa wa Singida alimwakikishia Waziri Nape kuwa umeme na miundombinu ya barabara itafikishwa kwenye eneo hilo la mnara na kuwa kilichofanyika kinakwenda sanjari na mageuzi manne ya teknolojia na akaomba uwekezaji zaidi uwe kwenye mawasiliano na akatoa ombi kwa TTCL kuruhusu makampuni mengine kwenda kufunga mitambo yao kwenye eneo hilo pamoja na kushusha bei ya upangaji.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba alisema  walitoa Sh. 160 Milioni kwa ajili ya kujenga mnara huo na kuongeza kuwa kila alipokuwa akikutana na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu alikuwa akisistiza kupata mnara huo kwa ajili ya wananchi wa Misughaa.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro alisema mnara huo utasaidia sana katika kuimarisha suala zima la ulizi na usalama na kukuza uchumi wa eneo hilo kwani wananchi wataweza kufungua vibanda kwa M-Pesa na kujiongezea kipata tofauti na kabla ya hapo ambapo walikuwa wakisafiri kwenda Kata za Makiungu na Kikio kufuata huduma hiyo.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu aliishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kujenga mnara huo ambapo tangu nchi hii ipate uhuru wananchi wa eneo hilo la Bonde la Ufa walikuwa hawajawahi kuwa na mawasiliano.

“Serikali inafanya kazi kubwa katika sekta mbalimbali kuanzia ya afya, elimu, barabarao na  mawasiliano hakika kila mpenda maendeleo anapaswa kumuunga mkono Rais wetu na serikali yake kwa kazi hii kubwa inayofanyika” alisema Mtaturu.

Alisema mnara  huo una kwenda kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Dk.Shein kwani watatumia intaneti kujifunza mambo mbalimbali yahusuo masomo pamoja na kukuza uchumi wa wananchi wa eneo hilo.

Mtaturu alitoa sola tatu, vifaa vya kuunganishia umeme kama nyaya na vingine kwa ajili ya kusaidia umeme kufungwa kwenye shule hiyo.


Saturday, January 7, 2023

SHIRIKA LA TREES FOR THE FUTURE LAPANDA MITI ZAIDI YA 3000 KWENYE UZINDUZI WA KAMPENI YA UPANDAJI MITI SINGIDA

Mratibu wa Miradi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Trees for the Future Tanzania Mkoa wa Singida Ibrahim Mghama, akizungumza  na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji miti ili kulinda vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira mkoani hapa ulioongozwa na Mkuu wa Mkoa, Peter Serukamba uliofanyika jana katika Halmashauri ya Wilaya ya  Singida Ilongero.

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Trees for the Future Tanzania linalojishughulisha na kilimo mseto, kilimo endelevu kwa wakulima wenye kipato cha chini vijiji ili kutokomeza njaa, Umaskini na Ukataji wa miti lenye makao yake makuu mkoani Singida limetoa miche 3,000 kwa ajili ya kampeni ya kupanda miti ili kulinda vyanzo vya maji na kutunza mazingira iliyozinduliwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba.

 Akizungumza katika hafla ya uzinduzi  wa kampeni hiyo iliyofanyika makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Singida Ilongero Mratibu wa Miradi wa shirika hilo Ibrahim Hassan Mghama alisema miche hiyo ikiwemo ile wanayoigawa kwa wakulima imetolewa na shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wao  Taasisi za kiraia za Adese na Waendelee zote za Singida.

Mghama alisema tangu shirika hilo lianze kufanya kazi mkoani hapa mwaka 2016 limeshiriki katika matukio kadhaa likiwemo la upandaji wa miti Msitu wa Mughola mwaka jana huku mwaka 2019 lilifanikiwa kupanda miti 2.5 milioni, mwaka 2020 miti milioni 3.2.

” Tangu shirika hili lianze kufanya kazi limepanda miti zaidi ya 8 milioni ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Bustani Msitu ndani ya Mkoa wa Singida,” alisema Mghama.

Alisema katika miti hiyo iliyopandwa ipo miti ya matunda, mbao, uzio, miti ya kurutubisha ardhi na malisho kwa ajili ya mifugo.

Mghama  alisema mwaka huu wamejipanga kupanda miti milioni 3 na kuwa mpaka sasa wana miche takribani Milioni mbili na laki tisa iliyopo kwenye vitalu 211 na kuwa lengo lao ni kupunguza umaskini wa kipato kwa kufanya shughuli endelevu za upandaji wa miti ili kukomesha njaa, umaskini wa kipato na kuboresha afya za wanajamii na uhifadhi wa mazingira.

Alisema kati ya miche hiyo 570 itapandwa kando ya barabara ya Singida kwenda Mwanza, mingine itapandwa maeneo ya Karakana na kwenye chanzo cha maji cha Mwankoko jumla ikiwa ni 1500.

Mghama alitumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuitunza miti hiyo inayopandwa kwenye maeneo yao na kuacha tabia ya kuacha mifugo kwenda kuiharibu..

Kwa upande wake Msimamizi Msaidizi wa Miradi wa Shirika hilo, Nurudin Kambulage alisema mkakati wa shirika hilo kwa mwaka huu ni kupanda miche mingi zaidi ambapo kwa wadau wao wana zaidi ya miche milioni moja  hivyo wakulima watapata ya kutosha na kuweza kuhifadhi mazingira na ardhi katika mashamba yao.

Msimamizi wa Miradi Msaidizi wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Nurudin Kambulage akizungumza kwenye uzinduzi huo.
Miche ya miti ikipandwa.
Miche ya miti ikipandwa.
Mtaalam wa Shirika hilo, Abisai Malela akishiriki upandaji wa miche katika uzinduzi huo.
Mratibu wa Miradi wa shirika hilo, Ibrahim Mghama  akishiriki zoezi la upandaji wa miche ya miti.

 Wafanyakazi wa Shirika la Tree for the Future lenye makao yake makuu mkoani Singida na wadau wao kutoka mashirika ya Adese na Waendelee wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kushiriki zoezi la upandaji miche ya miti. 

Thursday, January 5, 2023

CCM SINGIDA WAMPONGEZA RAIS SAMIA KURUHUSU MIKUTANO YA HADHARA KWA VYAMA VYA SIASA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  Mkoa wa Singida,  Martha Mlata akizungumza na waandishi wa habari, viongozi wa dini, wazee na makada wa chama hicho mkoani hapa Januari 5, 2023 wakati akitoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara. Katikati ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida, Yohana Msita na kulia ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Singida, William Nyalandu.

 Na Dotto Mwaibale, Singida

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kinampongeza Rais Dkt. Samia  Suluhu Hassan  na Mwenyekiti wa CCM Taifa  kwa kukubali kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya Siasa.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Martha Mlata akizungumza Januari 5, 2023 na waandishi wa habari, viongozi wa dini, wazee na makada wa chama hicho mkoani hapa alisema kwa hatua hiyo Rais amekuza Demokrasia nchini.

"Tunampongeza  Rais kwa falsafa ya 4R ambayo imemuongoza katika kujadiliana na viongozi wa vyama vya kisiasa ili kuimarisha Umoja, Utulivu na Amani ili Serikali iendelee kutekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo Wananchi" alisema Mlata.

Mlata alisema  CCM Mkoa wa Singida wameona ni moyo wa kishujaa alionao Rais Samia na anastahili kupongezwa na wanaona njia hiyo aliyoitumia inakiimarisha chama hicho na kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.

Alisema kitendo alichofanya  Rais cha kukaa na  viongozi wa vyama vyote meza moja kitawafanya na wananchi pia kuwa wamoja na kwamba  ameiheshimisha nchi na jambo hilo la kuruhusu shughuli za vyama ziendelee ametimiza matakwa ya utawala bora unaoheshimu katiba.

"Tunampongeza Rais kwani ameamsha na kuchochea maendeleo kwa kuwa kwenye mikutano watu watatoa maoni yao kuhusu maendeleo ya nchi na sisi CCM Mkoa wa Singida tunakaribisha kwa mikono miwili uamuzi huo" alisema Mlata.

Alisema CCM Mkoa wa Singida wapo tayari kwa hoja za vyama vingine katika majukwaa kwa kuzingatia utekelezaji mzuri wa Ilani unaoendelea mkoani humo ambapo wanaviomba vyama vingine kutumia vizuri fursa hiyo kwa manufaa ya nchi yetu na maendeleo ya mkoa kwa ujumla.

Mlata alitumia nafasi hiyo kuwaomba wana Singida kuendelee kumuombea Rais wetu, Mungu azidi kumpa afya njema, hekima, maono na umri mrefu.

Mwenyekiti wa CCM  Wilaya ya Singida mjini, Lusia Mwiru akizungumza kwenye mkutano huo.

Katibu Mwenezi wa CCM  Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu akizungumza kwenye mkutano huo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa mkutano huo.
Mkutano ukiendelea. Kulia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Singida, Yagi Kiaratu na kushoto ni Katibu Mwenezi CCM  Wilaya ya Singida, Comrade Mang'ola
Mkutano ukiendelea.
Makada wa CCM wakiwa kwenye mkutano huo.
Makada wa CCM na viongozi wa dini wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Mkutano ukiendelea

Wednesday, January 4, 2023

UWT YAMPONGEZA DKT.SAMIA KUONDOA ZUIO MIKUTANO YA HADHARA KWA VYAMA VYA SIASA

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda. 

Na Mashaka Kibaya, Tanga.

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania  (UWT) Taifa,  Mary  Chatanda amepongeza hatua ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kuondosha zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya Siasa akisema,imerejesha faraja kwa wananchi na wapenda amani.

Akiwa katika mkutano wake na wanahabari jana Jijini Tanga, Chatanda alisema, UWT inampongeza Dkt Samia kwa kufanya maamuzi yaliyoleta furaha isiyo na kifani kwa wananchi na wapenda amani.

Chatanda alisema kwamba, hatua hiyo imetoa majawabu kwa demokrasia ya nchi akitaja uondolewaji mikutano ya hadhara, kukwamua mchakato katiba mpya,kufanya marekebisho sheria mbalimbali ili kupanua wigo wa demokrasia.

"Maamuzi ya Rais Dkt Samia yameleta faraja kwa vyama vya siasa na hatawapenda amani wote, ameonesha uthabiti wa kauli zake kwa matendo"alisema Chatanda.

Aidha Chatanda amesisitiza umuhimu wa vyama vya siasa kufanya mikutano yake bila lugha za matusi kwa maelezo kuwa ni muelekeo mpya wa nchi katika kuihami demokrasia.

"Mama Samia ni neema kutoka kwa Mungu matumaini mapya yamerejea katika kujenga demokrasia,UWT inaungana naye, kilio cha UWT ni kuona amani inatawala" alisema Chatanda.

Mwenyekiti huyo wa UWT amesisitiza umuhimu wa amani na utulivu kuendelea kutawala ili kutoa fursa kwa Rais Dkt Samia kuendelea kushughulika na kero za wananchi.

Amewataka viongozi wa UWT kufanya mikutano ya hadhara kwa kufuata taratibu zote akiwahimiza kusikiliza kero zote kwa lugha ya kistaarabu.

Katika mkutano huo pia Mary Pius Chatanda alitumia wasaa huo akiahidi kutoa shilingi Milioni moja kwa ajili ya kikundi cha hamasa kinachotoa mchango mkubwa kuhamasisha maendeleo.

Alisema amewiwa kutoa mchango wake huo baada ya wahamasishaji hao kuwa na mchango mkubwa kwa shughuli za chama na Serikali.

"Hata kipindi cha Mwalimu alikuwepo bibi Titi aliyekuwa akitangulia kwakuimba na kuzungumza kidogo halafu ndipo akawa anamkaribisha Nyerere"alisema Chatanda.

Chatanda amebainisha kuwa fedha hizo kwa kikundi hicho cha hamasazitawasaidia kujianzishia shughuli za kiuchumi na kuweza kujikwamua.

Tuesday, January 3, 2023

SUA WAANDAA SERA YA KUDHIBITI UNYANYASAJI WA KINGONO

   Kiongozi wa Masuala ya Jinsia kwenye mradi wa wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) Prof. John Jeckoniah akieleza malengo ya Kikao kazi hicho cha kupitia Rasimu hiyo.

     Mtafiti nguli wa masuala ya Jinsia Prof. Fatihiya Masawe akiwasilisha rasimu hiyo ya sera ya chuo ya masuala ya ukat na unyanyasaji wa kijinsia na muongozo wa utekelezaji wake kabla ya kuanza kujadiliwa.

 Picha ya pamoja ya Baadhi ya washiriki wa kikosi kazi hicho cha kupitia rasimu ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na muongozo wa utekelezaji wake.

Wajumbe wa kikosi kazi hicho wakifuatilia uwasilishwaji wa Rasimu na kusikia malengo yake.

Kikao kazi hicho kikiendelea.

Wajumbe wa kikosi kazi hicho wakifuatilia uwasilishwaji wa Rasimu na kusikia malengo yake. 

Na Calvin Gwabara, Kibaha Pwani.                                                                

WATAALAMU na wadau wabobevu wa masuala Jinsia wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wamekutana kukamilisharasimu ya  Sera ya chuo ya masuala ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na muongozo wa utekelezaji wake katika kuelekea uanzishwaji wa  kitengo cha jinsia na hatimaye Dawati la Jinsia.

 Akieleza malengo ya kikao kazi hicho cha siku mbili Kiongozi wa Masuala ya Jinsia kwenye mradi wa wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) Prof. John Jeckoniah amesema kuwa ni kupitia rasimu hiyo ya Sera na Muongozo wake ili baadae uweze kuwasilishwa kwa uongozi wa Chuo kwa kuidhinishwa kupitia kwenye vikao vya maamuzi ya Chuo kupata Baraka na kuanza kutumika.

“Tumeona tuwakutanishe wataalamu hawa wa masuala ya Jinsia kutokana kuwa na uzoefu kutoka kwenye taasisi mbalimbali na Idara za Chuo chetu tuweze kuungalia na kuuboresha vizuri ili uweze kufaa na kutekelezeka kwenye chuo chetu na hivyo SUA kuwa na mazingira salama kwa kila mmoja anayetoa na kupata huduma wakiwemo Wahadhiri,Wafanyakazi waendeshaji,Wanafunzi pamoja na watoa huduma wengine chuoni kwetu” Alieleza Prof. Jeckoniah.

Kiongozi wa masuala ya Jinsia kwenye mradi wa HEET amesema kazi ya utengenezaji wa rasimu ya  Sera ya Unyanyasaji na ukatili wa kijinsia (ikiwa ni pamoja na masuala ya ukatili wa Kingono) na muongozo wa utekelezaji wake ni sehemu ya utekelezaji wa muongozo wa Wizara Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kutaka kila Chuo kuwa na dawati la jinsia.

Aidha amesema kuwa kutokana na umuhimuwa wa jambo hilo wamefanikiwa kupata fedha kupitia mradi wa HEET na hivyo kusaidia kukamilisha kazi hiyo,Ununuzi wa vifaa kwaajili ya uanzishwaji wa kitengo cha jinsia na dawati la jinsia, kutoa elimu kwa wanajumuiya kwenye kampasi zote ili masuala hayo yaweze kueleweka vizuri kwa Chuo kizima na endapo  uongozi utaipitisha na kuanza kutumika  ili kuweka na kuwezesha mazingira salama kwa kujifunza na kufanya kazi kwa wadau wote wa chuo.

Prof. Jeckoniah amewataka wajumbe wa kikosi kazi hicho kushiriki kikamilifu kutoa mchango chanya na mapendekezo ambayo yatasaidia SUA kupata Sera nzuri zaidi ambayo itasaidia Chuo kuwa na mazingira salama kwa kila mmoja anapotoa na kupokea huduma.

Akizungumzia safari toka mwanzo hadi kupatikana kwa rasimu ya sera hiyo na muongozo wake wa utekelezaji mtafiti na nguli wa masuala ya Jinsia Prof. Fatihiya Masawe amesema ilichochewa na Mradi mdogo wa maswala ya Unyanyasaji wa kingono ambao matokeo yake ilikuwa ni kupatikana kwa rasimu hiyo.

Amesema wakati wa uandaaji wa Sera hiyo walitembea kujifunza kwenye vyuo mbalimbali nchini kama vile Chuo kikuu cha Dar es salaam, Chuo Kikuu cha Ardhi,DUCE, Chuo Kikuu cha Muhimbili na vyuo vingine  kuona namna wanavyoshughulika na masuala hayo na kukabiliana nayo.

Prof. Fatihiya amebainisha kuwa pamoja na mambo mengi mazuri waliyojifunza kwenye maeneo waliyotembelea changamoto kubwa imekuwa ni utayari wa viongozi katika kutoa rasilimali ili kutekeleza Sera hiyo na hii inatokana na sera yenyewe kuwa mwiba mchungu kwa wanajumuiya wake wasiofuata maadili bora ya utendaji kazi kwa kutoa adhabu ambazo zinagusa maisha na ajira za wahusika.

“Ukiona wenye madaraka wanapata kigugumizi kuwepo kwa sera ya masuala hayo utajua kuwa kweli kuna changamoto lakini sera hii ni kifaa muhimu ambacho pia kinamsaidia kiongozi kuchukua hatua stahiki dhidi ya watenda makossa hayo na wanaotendewa na hii itawezekana kama utajengwa uelewa na kuwapa watu nafasi ya  kutoa taarifa za matendo hayo ili yakomeshwe” Alieleza Prof. Fatihiya.

Mbobevu huyo wa masuala ya Jinsia amesema Kuwepo kwa Sera hiyo sio tuu kutasaidia kuweka mazingira bora ya kazi na kujifunzia kwa wote kwenye taasisi bali kunawezesha kupatikana kwa miradi mbalimbali ya utafiti na maendeleo kwenye taasisi kwakuwa kuna baadhi ya wafadhili hawakubali kutoa ufadhili kwenye miradi inayotekelezwa na taasisi ambazo hazina sera ya kudhibiti masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinisa ikiwa pamoja na ukatili wa kingono.

Changamoto na matukio ya unyanyasaji wa kingono yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara kutoka kwenye vyuo mbalimbali na taasisi zingine na uwepo wa Sera na dawati mahususi kwaajili ya kushughulikia masula hayo kutasaidia kuongeza elimu na kupunguza matendo hayo na waathirika na kuleta usawa na usalama kwa jamii.