Saturday, July 8, 2023

VIONGOZI, WATENDAJI WILAYA YA SINGIDA WATAKIWA KUTUMIA MATOKEO YA SENSA KUTATHMINI UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA MAENDELEO

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili akihutubia wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi hao yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida Julai 8, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

...................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida

VIONGOZI  na watendaji wa ngazi mbalimbali za utawala katika Wilaya ya Singida na Halmashauri ya Manispaa ya Singida mkoani hapa wametakiwa kutumia matokeo ya Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 katika kufanya maamuzi na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Muragili wakati akifungua mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi hao yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida leo Julai 8, 2023 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.

"Mafunzo haya yanatekelezwa kwa mujibu wa Mpango kazi wa Usambazaji na Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa unaotokana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhahiri kuwa si kila mdau tukiwemo miongoni mwetu tunafahamu vyema kutumia matokeo ya Sensa katika kufanya maamuzi na kutathmini utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo ambapo Serikali iliona ni vyema kutoa mafunzo haya kwa wadau mbalimbali katika ngazi mbalimbali za kiutawala kuhusu namna ya kutumia matokeo ya Sensa," alisema Mragili.

Alisema mafunzo hayo kwa namna moja au nyingine yatawapa uwezo wa kushiriki katika kufanya maamuzi yanayohusu sera na mipango ya maendeleo ya wananchi kwa kuwa wapo karibu nao, hivyo kutumia matokeo ya Sensa watatekeleza majukumu yao vizuri ya kuwawakilisha wananchi.

Mragili alitumia nafasi hiyo kutoa shukrani zake za dhati kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wa Singida kwa ushirikiano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida na Ofisi ya  Taifa ya Takwimu kwa kuratibu vyema maandalizi ya mafunzo hayo.

Meneja wa Takwimu Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo akizungumza kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dk.Albina Chuwa alisema mafunzo hayo ni mfufulizo wa mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa kwa makundi mbalimbali katika jamii  yanayoendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar na kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpangokazi wa Usambazaji na Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Mwaka 2022

"Hadi sasa, mafunzo kama haya yamefanyika kwa makundi mbalimbali yakiwemo viongozi wa ngazi za chini katika mikoa ya Dar es salaam, Dodoma, Kigoma na Morogoro pamoja na mikoa mitano ya Zanzibar," alisema Kipuyo.

Kipuyo aliyata makundi mengine yaliyopata mafunzo hayo kuwa ni Wakurugenzi wa Sera na Mipango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa mikoa, Kamati za Sensa za Mikoa na wajumbe wa Sekretarieti ya Mikoa ya Lindi, Mtwara,Pwani,Singida na Wilaya ya Iramba.

Alisema mafunzo mengine yamefanyika katika ngazi ya mkoa katika mikoa ya Mbeya na Ruvuma. Hivi sasa tunaendelea na mafunzo ya aina hii katika ngazi ya Halmashauri na majiji katika mikoa ya Dar es salaam na Dodoma.

Alitaja kundi jingine lililofaidika na mafunzo hayo kuwa  ni vyombo vya habari ambapo wahariri wa habari wa redio zaidi ya 120 nchini pamoja na wanachama 25 wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Singida na kuwa yataendelea kufanyika kwa ngazi zote za utawala na kuhusisha makundi kama vile viongozi wa siasa, dini, mila na destruri, Asasi za Kiraia, sekta binafsi, taasisi za elimu ya juu na za kitafiti, Watu Wenye Ulemavu,vyombo vya habari na wananchi wa kawaida.  

Kipuyo alisema  madhumuni ya mafunzo hayo ni kusambaza matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 na kuwajengea uwezo wadau wote wa namna ya kutumia matokeo hayo katika kutekeleza majukumu yao ya uongozi na utendaji katika Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi ikiwemo biashara na uwekezaji, tafiti, utoaji huduma mbalimbali zikiwemo za kijamii na uchumi.

Alisema kufanya hivyo kutasaidia kuongeza uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya Matokeo ya Sensa kwa Serikali, Sekta Binafasi na wananchi kwa ujumla ili kupanga mipango jumuishi kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga alisema kuhusu maelekezo ya Serikali juu ya matumizi ya matokeo ya Sensa, mkoa huo umejipanga kuhakikisha mipango yao  na programu zao zote za maendeleo zinapangwa kwa kuzingatia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi ya Mwaka 2022.

"Nieleze kuwa katika mipango na programu zetu za mwaka wa fedha 2023/24 zimezingatia matokeo ya Sensa na Takwimu nyingine zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu," alisema Dk.Mganga.

Alisema mbali ya kutekeleza maelekezo ya Serikali, mkoa umeweka msisitizo wa matumizi ya matokeo ya Sensa kwa lengo la kuhakikisha kuwa mipango na programu hizo zinajibu changamoto mbalimbali ambazo wananchi wanapambana nazo katika maisha yao ya kila siku.

Aidha, Dk. Mganga alisema matumizi ya matokeo hayo ya sensa ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki kwa wakati na zenye ubora unaozingatia mahitaji halisi kulingana na idadi yao, jinsi yao, kuzingatia mahitaji maalum ya makundi mbalimbali katika jamii na hali ya mazingira wanamoishi.

Alisema mafunzo hayo ni muhimu sana kwa sababu yanawajengea uwezo wa kuyatafsiri na kuyatumia matokeo ya Sensa ipasavyo na hatimae kukuza uchumi wa mkoa, kuongeza na kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi na kuchagiza harakati ya kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Meneja wa Takwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo, akitoa taarifa za takwimu kwa niaba ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk.Albina Chuwa, wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali Watu, Mkoa wa Singida, Stephen Pankras akiwatambulisha viongozimbalimbali wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili wakati wa mafunzo hayo.
Mbunge wa Singida Mjini, Musa Sima akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo
Mbunge wa Singida, Kaskazini, Ramadhan Ighondo, akizungumza kwenye mafunzo hayo ambapo aliomba yapelekwe kwa wananchi waliopo vijijini.
Taswira ya mafunzo hayo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa mafuno hayo
Mtakwimu Mwandamizi, Mdoka Omari, akitoa mada wakati wa mafunzo hayo.


Thursday, July 6, 2023

KAIMU RAS MKOA WA PWANI: MSD ENDELEZENI MIPANGO YA UPATIKANAJI WA BIDHAA ZA AFYA NCHINI




KAIMU Katibu Tawala Mkoa wa Pwani (RAS), Bi. Salvera Salvatory ameishauri Bohari ya Dawa (MSD) kuwa na mikakati endelevu ya kuboresha upatikanaji wa bidhaa za afya ili kuondoa malalamiko kwa wananchi ambayo kwa kiasi kikubwa yameanza kupungua.

Bi Salvatory ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa MSD Kanda ya Dar es Salaam na wadau wake wa Mkoa wa Pwani uliofanyika Kibaha Julai 6, 2023.

“Wananchi wanafarijika sana wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakapatiwa Dawa zote walizoandikiwa”

Kiongozi huyo amekiri kuvutiwa na MSD kuwa na kitengo cha Huduma kwa Wateja, ambao ndio hufanya mawasiliano kwa karibu na wadau na wateja, ambapo amewashauri kuhakikisha wanafuatilia malalamiko ya wateja na namna yanavyoshughulikiwa.

 Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Miradi wa MSD Victor Sungusia ameeleza kuwa usambazaji wa bidhaa za afya mara sita kwa mwaka umesaidia kuongeza hali ya upatikanaji wa bidhaa hizo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Kwa upande wake Meneja wa Kanda ya MSD Betia Kaema ameahidi kufanyia kazi maazimio yote yaliyoazimiwa kwenye kikao hicho huku akisisitiza ushirikiano na mawasiliano ya mara kwa mara na wadau hao.


Wadau wa MSD wakiwa kwenye mkutano huo

Mkutano ukiendelea


Kaimu Mkurugenzi wa Uendeshaji na Miradi wa MSD,  Victor Sungusia  akiwa kwenye mkutano huo

Wadau wakiwa kwenye mkutano huo.

 

DKT. YONAZI: TUTAENDELEA KUELIMISHA UMMA MASUALA YA MAAFA

 Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza na Mkurugenzi Msaidizi Utafiti Idara ya Menejimenti ya Maafa Bw. Charles Msangi (kwanza kushoto) alipotembela banda la ofisi yake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba Julai 6, 2023 Jijini Dar es Salaam. 

..................................................

Na Mwandishi Wetu 

OFISI ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge kupitia Idara ya menejimenti ya maaafa imesema itaendelea kutoa elimu kwa wananchi  juu ya namna ya kujikinga na majanga mbalimbali pindi yanapotokea ili kupunguza athari za majanga hayo.

Akizungumza hii leo Julai 6, 2023 wakati alipotembelea maonesho ya kimataifa ya 47 ya biashara maarufu kama sabasaba Katibu Mkuu wa ofisi hiyo Dkt. Jim Yonazi amesema kuwa Serikali inaendelea Kushirikiana na wadau ili kuhakikisha kuwa uwezo wa nchi katika kukabiliana na majanga mbalimbali pindi yanapotokea unaboreshwa.

Aliongezea kuwa, Serikali itaendelea kuratibu vyema masuala ya menejimenti ya maafa kwa kuzingatia mifumo ya kitehama ili kuwafikia wananchi kwa wakati kuendelea kuleta matokeo yanayokusudiwa.

“Serikali imewekeza katika mifumo mbalimbali ya kiteknolojia inayosaidia kutoa Viashiria vya awali vya majanga na pia kusaidia katika utoaji wa taarifa kwa haraka,”Alieleza Dkt. Yonazi.

Pia akieleza mikakati ya serikali kuratibu masuala ya maafa alisema imejipanga kuufikia umma wa Watanzania kuanzai ngazi ya Kijiji, Kata, Wilaya , Mkoa hadi Taifa na kwa kuzijengea uwezo kamati za maafa kwa ngazi zote na kuwa na jamii stahimilivu ya maafa nchini.

“Katika mwaka huu mpya wa fedha, tumejipanga kuendelea kujenga uwezo kwa wadau wetu ili kuhakikisha uwezo wetu wa kukabiliana na majanga aina mbalimbali unaboreshwa kwa kuzingatia athari zake kiuchumi, kijamii na nyingine nyingi,” Alisisitiza Dkt. Yonazi.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiangalia moja ya kitabu wakati alipotembelea katika banda la Idara ya Menejimenti ya Maafa  lililochini ya ofisi yake katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) JIjini Dar es Salaama
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akiangalia moja ya kitambulisho cha waandishi wa habari (press card) wakati wa ziara yake banda la Idara ya habari maelezo, kulia ni Afisa habari Idara ya Habari maelezo Bi. Lilian Lundo.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (mwenye suti) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa ofisi yake alipotembelea  banda la Idara ya Menejimenti ya Maafa katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
Afisa TEHAMA Kutoka TSN Bw. Prosper Mallya akimuonesha Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi namna mifumo ilivyoboreshwa na taasisi hiyo alipotembelea banda la TSN katika maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) Jijini Dar es Salaam Julai 6, 2023.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akizungumza jambo kuhusu uboreshwaji wa mifumo ya TEHAMA na Afisa TEHAMA wa taasisi hiyo  Bw. Prosper alipotembelea banda la lao Julai 6, 2023  Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Afisa Masoko kutoka TSN Bi. Anitha Shayo akimkabidhi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi nakala ya magazeti yanayochapiswa na taasisi hiyo alipotembelea katika banda lao katika maonesho ya Kimataifa ya biashara ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam. 

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUANDAA MASHINDANO YA UANDISHI WA INSHA KWA WANAFUNZI VYUO VIKUU NCHINI

Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) , Bw. Griffin Mwakapeje    akizungumza wakati wa Kikao cha Menejimenti ya Taasisi hiyo kilichofanyika leo Julai 6, 2023  katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za tume hiyo jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KATIBU Mtendaji wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) , Bw. Griffin Mwakapeje amesema Tume ipo kwenye mchakato wa kutekeleza  Mpango wa kushirikisha vyuo vikuu mbalimbali hapa nchini katika mashindano ya Uandishi wa Insha za masuala mbalimbali ya Kisheria na yenye changamoto katika jamii  ili waweze kushiriki na kuchangia katika utaratibu wa marekebisho ya sheria kwenye maeneo husika.

Maelezo hayo ameyatoa wakati wa Kikao Cha menejimenti ya Taasisi hiyo kilichofanyika leo Katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Tume hiyo ambapo ameeleza kwamba yapo matukio mbalimbali yanayoibuka Katika jamii yenye mueonekano wa kisheria ambapo zikiandikwa Insha zinaweza kuisaidia Tume kupata taarifa za kitafiti.

Amesema kazi hiyo ya Uandishi wa Insha kwa wanafunzi  itasaidia kuwajengea wanafunzi hari ya kufanya utafiti na kuiwezesha Tume kupata  taarifa mbalimbali zitakazofanyiwa kazi Kwa kina na wataalamuwa Taasisi hiyo, Jambo ambalo litaongeza ufanisi wa Tume na maboresho ya sheria.

Aidha ameeleza kwamba washindi wa Insha watapatiwa zawadi mbalimbali zikiwemo  fedha  taslimu, kuchapishwa kwa maandiko yao kwenye jarida la tume, pamoja na vyeti na kwamba zoezi hilo litaongeza  hamasa kwa wanafunzi kuwa wazalendo Katika nchi yao.

"Tutafanya makubaliano na vyuo mbambali hapa nchini kuhusu Uandishi wa Insha ili kuwa na uratibu mzuri wa zoezi hili ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wanafunzi kufanya utafiti wa masuala mbalimbali ya kisheria yanayogusa jamii ili  mwisho wa siku maandiko hayo yasaidie  kufanya maboresho ya Sheria husika.

Katika kikao hicho, Bw. Mwakapeje amewahimiza wataalam na watumishi kuongeza jitahada kwenye utekelezaji wa majukumu  na kuwataka wawe wabunifu ili kuyafikia malengo yao.

Kikao hicho kikiendelea.
Kikao kikifanyika.
Washiriki wakifuatilia kikao hicho.
Mmoja wa washiriki wa kikao hicho akichangia jambo.
 

Wednesday, July 5, 2023

MEJA JENERALI MBUGE: TUTUMIE RASILIMALI ZILIZOPO KUKABILI MAAFA

Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge akimsikiliza Mratibu wa maafa wa ofisi yake Bi.Numpe Mwambenja alipotembelea banda la Ofisi hiyo katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea ndani ya viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Julai 3, 2023. 

............................................................... 

Na Mwandishi Wetu 

MKURUGENZI Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge ameiasa jamii kuendelea kutumia rasilimali zilizopo katika masuala ya menejimenti ya maafa nchini.

Ametoa kauli hiyo alipotembelea na kujionea shughuli zinazoendelea katika banda la Ofisi yake katika maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) katika Viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Meja Jenerali Mbuge alisema kuwa ni muhimu kuendelea kujiandaa na kujilinda na maafa kwa kutumia rasilimali zilipo nchini ili kuwa na mazingira salama na bora katika nchi yetu.

“Tutumia rasilimali tulizonazo katika masuala haya ya maafa kwa kuzingatia masuala ya usimamizi wa maafa ni jukumu la kila mmoja katika eneo lake huku tukizingatia maelekezo ya kitaalam ya usimamizi wa maafa nchini,”alisema.

Aidha alitumia fursa hiyo kuikumbusha jamii kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya majanga na tahadhali zinazotolewa na Mamlaka husika ili kuwa na utaratibu wa kujiandaa, kuzuia, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea.

Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri MMkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza na watendaji wa idara yake alipowatembelea katika banda la ofisi hiyo kwenye maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakiwa katika Banda la Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea ndani ya viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakiwa katika Banda la Idara ya Menejimenti ya maafa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea ndani ya viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Maafa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Khowe Malegeri akitoa maelezo kuhusu masuala ya menejimenti ya maafa katika maonesho ya sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge akiangalia moja ya kiatu katika banda la Jeshi la Polisi kikosi cha Polisi Ufundi alipotembelea banda hilo katika maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.
Mratibu wa Maafa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Numpe Mwambenja akitoa maelezo kwa wadau waliotembelea banda la ofisi hiyo katika maonesho ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba.
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri MMkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge akiuliza jambo kuhusu masuala ya afya za polisi alipotembelea banda la Jeshi la Polisi Tanzania Kikosi cha Afya katika maonesho ya Sabasaba
Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri MMkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge akizungumza jambo kuhusu zao la bangi alipotembelea banda la Jeshi la Polisi katika maonesho ya Sabasaba yanayoendelea Dar es Salaam.

 Mkurugenzi Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri MMkuu Sera, Bunge na Uratibu Meja Jenerali Charles Mbuge akifurahia Muziki wa Bendi ya Polisi alipotembelea banda la Jeshi la Polisi katika maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Tuesday, July 4, 2023

RC SINGIDA ATAKA NGO’s ZINAZO KWENDA KINYUME NA UTAMADUNI WA KITANZANIA ZICHUKULIWE HATUA KALI ZA KINIDHAMU

Mkuu wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO's) Mkoa wa Singida baada ya kufungua kongamano la Jukwaa la mashirika hayo mkoani hapa lililofanyika Ukumbi wa Hoteli ya KBH Julai 3, 2023.

..................................................... 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

MKUU wa Mkoa wa Singida,Peter Serukamba ameagiza Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoani hapa kuzichukulia hatua za kinidhamu Azise ambazo zinafanya mambo ambayo hayaendani na Tamaduni za Kitanzania. 

Serukamba alitoa agizo hilo jana Julai 3, 2023 wakati akifungua kongamano la Jukwaa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO's) Mkoa wa Singida lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya KBH mjini hapa. 

Alisema Azise zipo nyingi ambazo zinafanya vizuri lakini zipo ambazo hazifanyi vizuri na kukiuka taratibu na sheria za nchi. 

" Mchukue hatua za kinidhamu  kulingana na mwongozo wa mashirika kwa baadhi ya mashirika yanayoendesha shughuli zao kinyume na sheria za nchi,". alisema Serukamba. 

Serukamba aliyakumbusha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (AZISE) kufuata misingi ya katiba, sheria na kanuni zilizowekwa katika utekelezaji wa majukumu yao na kuliomba baraza la mashirika hayo kusimamia vema uendeshaji wa mashirika hayo kuanzia ngazi za chini na kufungamanisha taarifa za utekelezaji wa AZISE na taarifa za serikali zinazowasilishwa ngazi zote ili jamii ione tija ya utekelezaji wa AZISE. 

Awali akisoma risala ya jukwaa hilo mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Mkurugenzi wa Shirika la REDO, Hudson Kazonta alisema katika kipindi cha mwaka 2022 mashirika hayo yametoa takribani jumla ya ajira 400 na kuwa ajira hizo ni mojawapo ya njia ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kutengeneza ajira kwa wananchi wake. 

Alisema pamoja na mambo mengine, mashirika hayo (AZAKI) yamekuwa yakiwajengea uwezo wahitimu wanaomaliza vyuo mbalimbali ili kuwawezesha kupata uzoefu katika utendaji kazi ambapo jumla ya vijana takribani 150 wamenufaika na jambo hilo katika nyanja mbalimbali. 

Aidha, Kazonta alisema katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa mwaka 2022 jumla ya takribani Sh. Billioni 8 zimetumika kutekeleza miradi hiyo Mkoa wa Singida katika afua za Afya, Elimu, Msaada wa kisheria, Usawa wa Kijinsia, Vijana, Wanawake na watu wenye Ulemavu, Kilimo, Watoto, Mazingira, Maji na Usafi wa Mazingira, Utawala Bora, Mabadiliko ya Tabia Nchi pamoja na uwezeshaji jamii kiuchumi. 

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa alisema Asasi za kiraia ni kiungo kikubwa sana katika maendeleo ya Taifa na duniani kote kwani historia ya dunia haiwezi kuzungumzwa bila ya kuwepo asasi hizo. 

Alisema duniani kuna sekta tatu ambazo zinaunda taifa lolote lile na kuzitaja kuwa ni Serikali, Wafanyabiashara na sekta za kijamii na kuwa mara jingi sekta ya kijamii imekuwa haieleweki vizuri licha ya kuwa na mchango mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

Alisema changamoto kubwa iliyopo ni suala la kodi na wamekuwa wakiwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuangalia kuwa wao kama sekta au mkono wa pili wa serikali  katika kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii nchini waondolewe zile kodi pingamizi ukiachilia mbali za ajira kwa wafanyakazi wao ambazo ni lazima zilipwe. 

Alitaja msamaha wa kodi ambao wanaomba wasamehewe ni wakiingiza magari kutoka nje ya nchi ambayo yanakwenda kutumika vijijini kwa ajili ya shughuli za maendeleo na vitu vingine vinavyofanana na hivyo.

Mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyokuwa  ya Kiserikali (NACONGO), Peter Lisu alisema lengo kubwa la kukutana ni kujengeana uwezo katika masuala ya kodi na kupeana mbinu mbalimbali za utendaji wa kazi wa mashirika hayo, kuona fursa ambazo zitatoa mchango wa kuendeleza shughuli maendeleo mkoani Singida.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa (katikati) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati alipokuwa akitembelea mabanda kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na mashirika hayo.
Mkurugenzi wa Shirika la Jiokoe na Umaskini yaani Stars of Poverty Rescue Foundation, Tanzania (SPRF) lililopo mkoaniSingida Dk. Suleiman Muttani, akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa (Aliyekaa)baada ya kutembelea banda la shirika hilo.

Fundi wa majiko Sanifu, Musa Nasoro (kulia) akitoa maelezo kwa mkuu wa mkoa alipotembelea banda la fundi huyo.
Wajasiriamali waliowezeshwa na mashirika hayowakionesha bidhaa zao
Mjasiriamali Pendo Samuel aliyenufaika na mashirika hayo akionesha bidhaa zake kwa mkuu wa mkoa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika  lisilokuwa la Kiserikali la Save the Mother and Children of Central Tanzania (SMCCT), Evalyen Lyimo (katikati) akimueleza mkuu wa mkoa kazi zinazofanywa na shirika hilo.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Mjumbe wa Baraza la Mashirika Yasiyokuwa  ya Kiserikali (NACONGO), Peter Lisu, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Singida, Patrick Kasango akiongoza kongamano hilo.
Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Onesmo Ole Ngurumwa, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Singida sehemu ya  Rasilimali Watu, Stephen Pankras akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa mkoa huo, Dk.Fatuma Mganga.
Mkurugenzi wa Shirika la REDO, Hudson Kazonta, akisoma risala ya mashirika hayo kwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mragili akizungumza wakati akimkaribisha mkuu wa mkoa kutoa hutuba yake ya ufunguzi.
Taswira ya kongamano hilo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (katikati) waliokaa.