Wednesday, August 16, 2023

SHILINGI BILIONI 5 ZATENGWA NA MFUKO WA KUWAWEZESHA WASANII NA WAIGIZAJI MKOANI MBEYA

 Afisa Utamaduni Mkoa wa Mbeya Victoria Shao akizungumza katika kikao maalumu kilichowahusisha Wasanii, Waigizaji na waimbaji kilicho andaliwa na Wizara ya Utamadunim Sanaa na Michezo.

............................................................

Na Mwandishi Wetu Mbeya

 

KIASI cha Shilingi Bilioni 5 kimetengwa na mfuko wa wizara ya sanaa na utamaduni ili kuwawezesha wasanii na waigizaji wa "Bongo Movie" wa mkoa wa Mbeya.

Akizungumza katika kikao maalumu kilichowahusisha Wasanii, Waigizaji na waimbaji wa mkoa wa Mbeya na Songwe Afisa Mtendaji Mkuu [CEO] wa mfuko huo Nyakaho Mahemba amesema Wizara imeanza kutoa fedha hizo kwa wasanii kuanzia Desemba 2022 ambapo  imelenga kukuza na kuendeleza kazi za wasanii kujiendesha kibiashara badala ya burudani pekee.

Mahemba amesema katika mpango wa serikali ni kuongeza ajira na kuongeza mitaji kwa wasanii kupitia mafunzo na kuongeza ubora  wenye lengo la kukidhi soko la ndani na nje ya nchi.

Amefafanua kuwa wasanii wana uwezo wa kukopa mtaji kuanzia Shilingi laki 2 hadi Shilingi Mil 100 ili kufikia malengo na kwamba mfuko wa Utamaduni unashirikiana na mabenki ili kuwezesha mikopo ya Wasanii.

Afisa mtendaji Mkuu huyo ameendelea kusema kuwa tayari imeshatolewa mikopo kwa awamu mbili, mwezi Desemba 2022 na mkopo wa pili umetolewa Mwezi Februari ambapo tayari  jumla ya Shilingi Bil 1.077 kwa miradi 45 na hivyo kuzalisha ajira 88,750.

Kwa upande wake Afisa Utamaduni wa mkoa wa Victoria Shao amesema mikopo hiyo ya wasanii itachangia ajira na kuwasaidia kuwainua kiuchumi ambapo wasanii,waimbaji,wabunifu wa kazi za mikono,Waandishi wa kazi za kifasihi na wachoraji wanapaswa kuchangamkia fursa hiyo.

Shao amesema serikali itakuwa karibu na wasanii kwa maelekezo na elimu ya mikopo ili waweze kukopa kurejesha ili iweze kuwanufaisha wasanii wengine.

 Afisa Mtendaji Mkuu [CEO] wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa, Nyakaho Mahemba akitoa taarifa ya mfuko huo kwenye kikao hicho.

Wasanii wa Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye kikao hicho
Wasanii wa Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye kikao hicho
Wasanii wa Mkoa wa Mbeya wakiwa kwenye kikao hicho
Picha ya pamoja.

Picha ya pamoja

Tuesday, August 8, 2023

WANANCHI WAFURIKA BANDA LA TARI, KUJIFUNZA TEKNOLOJIA ZA KILIMO MAONYESHO YA NANENANE NGONGO LINDI

 Wananchi wakiwa wamefurika katika Banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo kwenye Maonyesho ya Nanenane 2023 yanayofikia tamati leo Agosti 8, 2023 viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

........................................................... 

Na Dotto Mwaibale, Lindi 

WANANCHI kutoka Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma wakiwa wamefurika katika Banda la Taasisi ya Utafiti kwa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele mkoani Mtwara kwenye Maonyesho ya Nanenane 2023 Kanda ya Kusini yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi kujionea na kujifunza teknolojia mbalimbali za kilimo.

Katika Maonesho hayo watafiti wa kilimo wa TARI wanaonesha na kutoa elimu za teknolojia za kilimo za kuvutia jambo lililosababisha banda hilo kufurika wakulima na wananchi kwa lengo la kujifunza.

Akizungumza na waandishi wa habari katika banda hilo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga kuhusu maonesho hayo Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano alitaja baadhi ya teknolojia  ambazo zinaoneshwa na kutolewa kwa wakulima ni za mazao ya korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi, mahindi na uwele.

Kidunda alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wakulima kuwa katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu bali  wameweka teknolojia ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu,  shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa magonjwa na uvunaji wake.

          Mkulima Mathayo Milanzi kutoka Wilaya ya Nanyumbu alisena amevutiwa na teknolojia zinazofundishwa na TARI na kuwa moja ya teknolojia hizo ni kilimo cha ndizi aina ya Mtwike ambapo awali alipokuwa akilima kwa kutumia kilimo cha mazoea alikuwa akipata mazao kiduchu.

"Zamani ndizi nilizokuwa nikivuna nilikuwa nikizibeba kichwani lakini baada ya kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa nimekuwa nikivuna ndizi nyingi hadi nalazimika kukodi pikipiki kwa ajili ya kuzisafirisha kwenda kwenye soko," alisema Milanzi.

Milanzi alisema TARI wamekuwa mkombozi kwa wakulima wa Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kuwafanya kukielewa kilimo chenye tija.

Mkulima mwingine, kutoka Kijiji cha Chemchem Wilaya na Nachingwea, Issa Bakari amesema TARI imekuwa mkombozi kwa wakulima wengi katika kandahiyo kwani imesabisha uzalishaji wa  mazo yao kuongezeka hususani maeneo ya vijijini.

Mimi natoka Kijiji cha Chemchem wilayani Nachingwea mkoani Lindi nimekuja mahususi katika Banda la TARI ili niongeze uzoefu kutoka kwa wataalam wabobezi ambao wamekuwa ni msaada mkubwa sana kwetu hasa sisi wakulima wa vijijini,” alisema Bakari.


Mtafiti wa mbegu bora za korosho kutoka TARI Naliendele, Joackim Madeni (kushoto) akitoa elimu kwa mkulima kutoka Wilaya ya Nachingwea ambaye alitembelea banda la Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele katika Maonyesho ya Wakulima Nanenane ambayo yanafikia tamati leo katika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Mtafiti wa mbegu bora ya mihogo, Ndwasi Gambo (kushoto) akiwaelekeza wananchi kuhusu kilimo chenye tija za zao hilo.


Muonekano wa mikorosho kwenye maonyesho hayo

Mtafiti Msaidizi wa zao la Karanga na alizeti, Said Ally, akielekeza kuhusu kilimo cha zao hilo.

Mtafiti Msaidizi na Msimamizi wa Kituo Kidogo cha Manyoni mkoani Singida, Eunice Kachungwa (wa pili kushoto), akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la TARI. Kulia ni Mtafiti Msaidizi wa zao la korosho, Nora Manfield.
Mtafiti Msaidizi wa zao la korosho,  Kelvin Kawonga (kulia) akitoa maelezo kwa wananchi waliotembelea banda la TARI kwenye Maonyesho hayo.
Mtafiti wa mbegu bora ya mihogo, Ndwasi Gambo (wa pili kulia) akiwaelekeza wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Mtwara kuhusu kilimo chenye tija za zao hilo. Kulia ni Mtafiti wa zao hilo, Benedetha Kimata kutoka TARI Naliendele.


Wananchi wakipata maelezo ya kilimo bora cha zao la ufuta.
Mtafiti wa Hali ya Udongo na Agronomia ya korosho, Zawadi Kilingala, akielezea kuhusu kilimo hicho.
Mtafiti Msaidizi wa zao la korosho, Dantish Leonard (kulia) akielezea kilimo hicho.
Muonekano wa shamba la ufuta kwenye maonesho hayo.
Muonekano wa shamba la alizeti kwenye maonesho hayo
Muonekano wa shamba la Mtama kwenye maonesho hayo.
Mtafiti wa zao la Korosho, Kasiga Ngiha (kulia) akiwaelekeza wakulima kutoka Wilaya ya Nachingwea, Joackim Lihundi (kushoto) na Bakari Pilipili (katikati) kuhusu mbegu bora za zao hilo.
Muonekano wa kitalu cha mbegu bora za korosho.
Wananchi wakiwa ndani ya banda la TARI Naliendele kwenye maonesho hayo.
 

Saturday, August 5, 2023

DC LINDI AWATAKA WASANII KUCHANGAMKIA BILIONI 20 ZA MFUKO WA UTAMADUNI ZILIZOTOLEWA NA RAIS

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga akizungumza wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo  wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo mkoani humo jana.

............................................

Na Dotto Mwaibale, Lindi 

WASANII mkoani Lindi wametakiwa kuchangamkia fedha Sh.Bilioni 20 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kama ruzuku za kuwawezesha kukopa ili kuwasaidia kuinua vipato vyao kupitia kazi zao za sanaa.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo  wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

"Hizi fedha zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili yenu hivyo changamkieni fursa hiyo kwa kuboreha shughuli zenu ili muweze kujikwamua kiuchumi," alisema Ndemanga.

Alisema wadau wa Sanaa watakaokidhi vigezo vilivyoweka ndio watakaokopeshwa fedha hizo kupitia mfuko ulioanzishwa na Rais Samia ambapo aliwahimiza wasanii hao kuhakikisha wanakithi vigezo hivyo ili waweze kukopesheka na kuwa fedha hizo sio zawadi bali zinatakiwa kurejeshwa ili ziweze kukopeshwa kwa wengine.

Shahibu aliwataka wasanii hao na wadau wa utamaduni kujiendeleza kielimu ili kwenda na dunia ya sasa ya sayansi na teknolojia huku wakianzisha miradi mbalimbali kama ufugaji,kilimo, na mingine badala ya kutegemea sanaa peke yake.

Aidha, aliwataka wasanii hao  kujenga tabia ya kushirikiana na taasisi zingine wakati wa kufanya shughuli zao jambo ambalo litawaongezea uzoefu wa masuala mengine ya maendele na sanaa kwa ujumla.

Alisema Serikali inatambua mchango wa wasanii na kuwa kwa siku za hivi karibuni imeonekana kazi nyingi za wasanii kama filamu na tamthilia zikioneshwa zaidi na vyombo vya habari vya watu binafsi hivyo watawasiliana na wahusika wa vyombo vya Serikali kuona namna ya kuanza kutumia kazi za wasanii hasa chipukizi katika vyombo hivyo.

"Changamoto kubwa iliyopo ni uzingatiaji wa maadili katika kazi zetu nawaombeni mkawe mabalozi wazuri wa kusimamia maadili ya kitanzania na si vinginevyo na kuacha kutengana kwa sababu ya migogoro yakugombea fedha na sisi kama Serikali hatutakuwa tayari kuona mambo hayo yakitokea," alisema Ndemanga.

Awali akitoa taarifa ya mfuko huo Afisa Mtendaji Mkuu  (CEO) wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tazania Nyakaho Mahemba alisema mfuko huo unatoa huduma katika maeneo ya urithi wa utamaduni , lugha  na fasihi, sanaa  za maonyesho, ufundi , filamu, muziki na fani nyingine  zenye mlengo  wa utamaduni na sanaa kwa watu binafsi, vikundi au makundi.

Alitaja huduma zinazotolewa na mfuko huo kuwa ni mikopo ya uendeshaji  yenye lengo  la kuwezesha  shughuli za  kiutendaji wa kila siku za uzalishaji wa kazi za utamaduni au sanaa.

Alitaja kazi nyingine ni utoaji wa mikopo ya vifaa yenye  lengo la kuwezesha  ununuzi  wa vitendea kazi  vya uzalishaji za utamaduni au sanaa na mikopo ya kujikimu/ dharura ambayo ni mikopo ya muda mfupi inayotolewa kwa lengo la kujikimu wakati  wa safari za kuandaa au kufanikisha  kazi za utamaduni au sanaa.

Alisema lengo la mafunzo ni kuongeza ujuzi na thamani  ya kazi za utamaduni na sanaa ili ziwe na ubora unaoendana na mahitaji ya  soko.

Mahemba alisema kulingana na kuingia makubaliano na Benki ya CRDB  na Serikali kupitia  mfuko huo walengwa wa mfuko watakaohitaji huduma za mikopo  watatakiwa kuwasilisha  maombi yao  kwa njia ya posta, barua pepe au  moja kwa moja katika ofisi za  mfuko huo kwa ajili ya mapitio ya awali ya kitaalamu kisha  maombi hayo kufikishwa katika Benki ya CRDB kwa hatua zao.

Msanii wa ngoma za asili Salum Namtitili akizungumza kwa niaba ya wenzake alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa fedha hizo kwa lengo la kuwainua kiuchumi.

“Tunaishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kwa kusikia kilio cha muda mrefu cha wasanii kwani tulikuwa na changamoto kubwa ya kuendeleza sanaa zetu lakini kwa fedha hizi tutasonga mbele kwani tutaweza kutoka sehemo moja kwenda nyingine na kurekodi kazi zetu tofauti na ilivyokuwa zamani tukiangaika kutafuta fedha huku na kule bila ya mafanikio,” alisema Namtitili.

Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shahibu Ndemanga (katikati) akiwasili Hoteli ya Sea View Hotel and Resort kwa ajili ya kufungua warsha ya kuwajengea uwezo  wadau wa utamaduni na sanaa Mkoa wa Lindi iliyoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.
 Afisa Mtendaji Mkuu  (CEO) wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tazania Nyakaho Mahemba akitoa taarifa ya mfuko huo.
Afisa Utamaduni Mkoa wa Lindi,  Makalaghe Nkinda, akizungumza kwenye warsha hiyo.
Afisa Mwandamizi wa  Mkopo wa Benki ya CRDB kutoka Makao Makuu, Alpha  Mgubila, akizungumza kuhusu mikopo itakayokopeshwa kwa wasanii kupitia benki hiyo.
Mwenyekiti wa Wasanii Mkoa wa Lindi, Athuman Mohamed akizungumza kwenye warsha hiyo.
Msanii wa ngoma za asili, Salum Namtitili, akitoa shukurani kwa Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.
Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa warsha hiyo.
Wasanii wakiwa kwenye warsha hiyo.
Viongozi wakiimba wimbo wa kumshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha hizo.

Wasanii wakiimba wimbo wa kumshukuru Rais Samia.
Wasanii wakiwa kwenye warsha hiyo.

 Warsha ikiendelea.


Wasanii wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi


Thursday, August 3, 2023

TARI NALIENDELE KIVUTIO MAONESHO YA NANENANE 2023 NGONGO LINDI

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Naliendele Programu ya Korosho,Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Bobnoel Assenga (kushoto) akitoa maelezo ya Wadudu waharibifu na Magonjwa kwa mkulima Cathbert Richard (kulia) aliyetembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya NaneNane 2023 yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi. Katikati ni Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano wa taasisi hiyo.

..................................................... 

Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Lindi 

KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele kilichopo  mkoani Mtwara kimekuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya Nanenane 2023 Kanda ya Kusini yanayofanyika Viwanja vya Ngongo mkoani Lindi.

Katika Maonesho hayo kituo hicho kinatarajia kuonesha teknolojia za kilimo za kuvutia wakulima kutoka Mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi ambao wameombwa kujitokeza kwa wingi kufika katika viwanja hivyo kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kituo hicho Dk. Fortunus Kapinga kuhusu maonesho hayo Mtafiti wa Kilimo Bakari Kidunda ambaye pia ni Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano alisema wamejipanga vizuri na kuwa wakulima wategemee kupata ujuzi mkubwa wa masuala ya kilimo katika maonesho hayo.

Alisema TARI Naliendele ni miongoni mwa vituo 17 vilivyopo chini ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania ambapo pia wanavituo vingine kama hivyo katika kanda zingine nchini na kueleza kuwa jukumu lao kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima.

    Alisema TARI Naliendele wamepewa jukumu la kitaifa la kutafiti zao la korosho, ufuta na karanga na kuwa changamoto zote zinazojitokeza kwenye mazao hayo wao ndio wanaowajibika kutoa majibu.

Kidunda alisema pia wamekuwa wakifanya utafiti wa mazao mengine kwa kushirikiana na vituo vingine vilivyopewa mamlaka kitaifa na kuwa katika maonesho hayo wana programu ya utafiti wa mazao ya nafaka, mikunde, jamii ya mizizi, mbogamboga na matunda.

 Alisema mwaka huu wamejipanga vilivyo kuonesha teknolojia zote za kilimo na litakuwa ni tukio la aina yake kwani kwa wale waliozoea kufika kwenye siku za nanenane sasa wataona shughuli endelevu za kituo hicho na kuwa wamefanya maboresho lukuki ya kisayansi katika kila idara.

" Kituo cha Ngongo sio kwa ajili ya Nanenane tu bali kipo kwa mwaka mzima kueneza teknolojia za kilimo na wataweza kuangalia teknolojia mbalimbali za korosho, mbegu za mafuta, mikungu ya ndizi ya aina Mtwike , jamii ya mikunde na nafaka. Mbali ya hayo pia kutakuwa na shughuli ya kuangalia jinsi ya kuongeza thamani ya zao la korosho, ufuta na zao la karanga ambapo katika zao la korosho watu walizoea kuja na kutafuna korosho lakini sasa watakuja kula na kunywa korosho kwani watakuwa na juisi, jamu na mvinyo zilizotokana na zao hilo" alisema Kidunda.

Alisema katika maonesho hayo watakuwa na kituo chao cha kanda ambacho kitatumika kutoa mafunzo kwa wakulima hivyo wadau mbalimbali wameombwa wafike kwani wataona mengi kwenye zao la korosho, ufuta, karanga, mihogo, viazi vitamu, kunde, choroko, mbaazi, mahindi, uwele na mengineyo.

Alisema mazao yote ambayo yanalimwa kwenye mikoa ya Mtwara, Ruvuma na Lindi na hata yale ambayo hayalimwi katika mikoa hiyo lakini yanaweza kustawi maeneo hayo yatakuwepo katika maonesho hayo.

Kidunda alisema katika kituo chao cha Naliendele wamekuwa hawana msimu pale wameweka teknolojia ambazo zinaonekana kwa mwaka mzima kwa ajili ya wakulima kujifunza hatua mbalimbali za ukuaji wa zao husika kuanzia likiwa kwenye kitalu,  shambani, utumiaji wa viatilifu, udhibiti wa magonjwa na uvunaji wake.

" Tukisema mkulima au mdau aje wakati wa wiki ya Nanenane tu kuna hatua nyingi hawezi kuzielewa na ndio maana tunasema hatufungi maonesho haya tupo kipindi chote cha mwaka mzima." alisema Kidunda.

Alisema TARI imekuwa ikisogeza huduma zake kwa wananchi nchi nzima ili ziwafikie walengwa.

Alisema zamani zao la korosho lilikuwa likilimwa katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani lakini sasa linalimwa karibu mikoa zaidi ya 20 kama Morogoro, Dodoma, Singida, Kigoma, Tabora, Shinyanga, Katavi, Mbeya, Rukwa, Iringa, Njombe,  Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya Same.

Alisema kinachosemwa korosho ilimwe wapi sio mipaka ya kiutawala bali ni mahitaji ya kiikolojia.

Kidunda alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima na wadau mbalimbali kufika kwenye maonesho hayo ya Kanda ya Kusini yanayofanyika Ngongo mkoani Lindi kuanzia Agosti 1,2023 kwenda kujifunza teknolojia za kilimo ambayo yatafikia tamati Agosti 8, 2023.

Kidunda alisema akiwa kama Mratibu wa Uhalishaji Teknolojia na Mahusiano jukumu lake kubwa ni kuhakikisha teknolojia zinawafikia wakulima.

"TARI Naliendele tunafanya utafiti na ukishafanywa kazi yetu ni kutoa matokeo ya utafiti huo na idara yangu kazi yake kubwa ni kuuchambua na kuchakata taarifa za utafiti huo na kuziweka katika lugha nyepesi ambayo inaweza kuwa rahisi kwa wakulima na wadau wengine kuielewa" alisema Kidunda.

Kidunda alisema kauli mbiu ya maonesho hayo mwaka huu ni Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula.

Mtafiti kutoka TARI Naliendele Programu ya Korosho,
Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Bobnoel Assenga alisema wamekuwa wakitoa mafunzo kwa wakulima
namna ya kudhibiti visumbufu vya wadudu waharibifu na magonjwa, ikiwemo ugonjwa wa Ubwiriunga, ugonjwa wa Blaiti na Debeki ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni changamoto kwa ustawi wa zao la korosho ndani ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na kwingineko
nchini.

Alisema  Tari Naliendele imekuwa ikikabiliana na kukithiri kwa wadudu waharibifu wa zao hilo wakiwemo Mbu wa Mikorosho, Mbu wa Minazi na Vidung’ata ambao ni kikwazo kikubwa cha ukuaji mzuri wa zao la Korosho ambalo linatajwa kuwa ni zao lenye uchumi mkubwa na soko la uhakika. 

Assenga alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakulima kufika katika banda la TARI kwa ajili ya kujifunza mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo.

Maelezo yakitolewa kwa wakulima waliotembelea banda la TARI.
Afisa Kilimi Msadizi wa TARI Naliendele, Justina Misungwi, akiwapa watoto juisi iliyotengenezwa kwa zao la korosho walipotembelea banda la taasisi hiyo.
Wakulima  Ahmadi Mnenele (kushoto) na Mathayo Milanzi (kulia) wakiangalia ndizi aina ya Mtwike ambayo imetokana na utafiti uliofanywa na TARI na kuleta tija. Katika ni Mtafiti wa Kilimo kutoka TARI, Zamira Matumbo.
Muonekano wa Jengo la TARI katika Maonesho hayo.
Afisa Kilimo Msaidizi, Noel Mwigune (kulia) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi, Jitulize ambao walitembelea kuona mazao ya nafaka yaliyofanyiwa utafiti na TARI.
Muonekano wa shamba la mbogamboga katika maonesho hayo.

Mtafiti Msaidizi wa Kilimo kutoka TARI, Dickson Malulu (kulia) akitoa maelezo ya kilimo cha kebichi kwa wakulima Calvin Michael (kushoto) na Evarist Eprahim waliotembelea shamba hilo

Mtafiti wa zao la ufuta kutoka TARI, Mohamed Fadhil, akitoa maelekezo lwa wakulima kutoka Wilaya ya Nachingwea kuhusu kilimo cha zao hilo.
Muonekano wa zao la ufuta aina ya Ziada katika maonesho hayo.
Muonekano wa zao la Muhogo aina ya Kiloba katika maonesho hayo.