Thursday, November 9, 2023

COTUL YATOA OMBI KWA SERIKALI KUSAIDIA MANUNUZI MACHAPISHO YA KIELEKITRONIKI

Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua kongamano la kisayansi ambalo limeandaliwa na Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL) kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi 

.................................................... 

Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKISHO la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL) limeiomba Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kusaidia kununua machapisho ya kielekitroniki  yanayotumika kufundishia vyuoni kwa kuwa yanauzwa bei ghali ambayo shirikisho hilo haliwezi kumudu kuyanunua.

Mwenyekiti wa Shirikisho hilo , Dkt. Sydney Msonde alitoa ombi hilo Novemba 9, 2023 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi ambalo limewakutanisha wanataaluma mbalimbali katika ngazi ya wakutubi, walimu wafundishaji kutoka  vyuo vikuu Tanzania Bara na Visiwani, watafiti pamoja na watu wanaoshughulika na masuala ya teknolojia (IT)

Alisema pamoja na kwamba lengo la COTUL ni kuhakikisha kwamba machapisho ya kielekitroniki yanapatikana kwa walimu na wanafunzi ili waweze kufanya shughuli zao za msingi za kujifunza, kufundisha na kufanya utafiti hapa nchini lakini kununua machapisho hayo imekuwa changamoto kutokana na kuuzwa bei ghali. 

Dkt. Msonde alitoa mfano uchapishaji wa kanzi data inayoitwa 'Sience Direct' ambayo inauzwa dola za Marekani 250,000 hivyo sio rahisi kwa taasisi moja za hapa nchini kuweza kumudu kununua chapisho kama hilo. 

“COTUL kazi yetu kubwa ni kuhamasisha na kuzileta pamoja taasisi zote za umma na za watu binafsi ili ziweze kuchangia kwa sehemu rasilimali fedha zitakazo wezesha kununua machapisho hayo ya msingi katika kukidhi haja ya kufanya ufundishaji na utafiti nchini,” alisema Dkt. Msonde.

Dkt. Msonde alisema uhaulishaji na upatikanaji wa machapisho hayo unaweza usiwe na tija kama walimu na wanafunzi watakao kuwa wanayatumia hawatajengewa uwezo bora wa kuyatumia jambo ambalo ndilo la msingi. 

Alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili mustakabari wa fani ya ukutubi na namna gani walimu katika taasisi za umma na watu binafsi wanaweza kutumia machapisho ya kielekitroniki katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa wanafunzi Tanzania.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu, alipongeza COTUL kwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha miaka 15 tangu shirikisho hilo lilipoanzishwa mwaka 2008.

Alisema shirikisho hilo limekuwa msaada mkubwa kwa serikali kwa kuisaidia kupata taarifa na maarifa mbalimbali ambayo kwa njia ya kawaida ingekuwa ni gharama kubwa kuyapata.

"Uwepo wa COTUL ni fursa hata kwa sisi tunaohusika na kufanya tathmini mbalimbali zikiwemo za utafiti hakika ni jukwaa muhimu sana," alisema Mwinyimkuu.

Mwinyimkuu alisema Serikali itaendelea kuunga mkono kazi zinayofanywa na COTUL na kuliomba shirikisho hilo kukutana na wadau wa elimu ndani ya Serikali ili waone namna ya kushirikiana nao na kuwa kazi zao zinazihitaji na hazikwepeki hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inahitaji teknolojia kwa ajili kukuza uchumi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa  Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inafanya maboresho makubwa ya maktaba kutoka katika mfumo wa kuhifadhi vitabu na machapisho mengine kwa njia ya kizamani ya karatasi na kwenda kwenye mfumo wa kidijitali.

Mmoja wa wafadhili wa kongamano hilo Mkurugenzi wa Kampuni ya Totoo Ltd yenye makao yake makuu mkoani Kilimanjaro, Dkt. Elvis Silayo alisema changamoto kubwa inayowafanya watu wengi washindwe kuitumia maktaba kwanza wanakuwa hawajui taarifa ambazo wanaweza kuzipata  na imekuwa ikichukuliwa kama sehemu ya taaluma na inatakiwa kuwa mashuleni.

Alisema watu wengi hawapendi kusoma mambo ya taaluma lakini maktaba kuna taarifa nyingi ambazo wanaweza kuzipata na kuwasaidia kupata maarifa yanayoweza kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.

Alisema maktaba za sasa zinavitabu vilivyochapishwa kwenye miaka ya 70 na 80 hivyo taarifa zake haziwezi kuwa na msaada kwa mtu anayehitaji kufanya chochote kwa kipindi hiki na kueleza kuwa maktaba za sasa zinapaswa kwenda mbele zaidi kwa kuwa na taarifa ambazo zinakwenda na wakati.

Silayo alisema ile dhana iliyozoeleka kuwa maktaba zipo kwa ajili ya kumuandaa mwanafunzi afaulu mtihani sasa iachwe badala yake zitumike kuwaandaa kimaisha.

 Naye Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Valeria Kyumana, alisema mafunzo hayo yamewajenga kwasababu hivi sasa teknolojia inakuwa na maktaba na huduma wanazotoa haziwezi kuendelea kwa kutumia mfumo wa zamani waliokuwa wakiutoa.

“Ni lazima tuangalie teknolojia inavyokwenda tukue nayo na kama sisi wakutubi tuweze kuichukua na kuitoa kwa wateja wetu tunaowahudumia ambao ni wanafunzi na watu wengine,” alisema Kyumana.

Baadhi ya wadhamini wa kongamano hilo ni Totoo Company Ltd, Ebsco, Elsevier,  Jove, Buku,Eclat, Bookstore, emerad insight, TCC na  LexisNexis.

Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dkt. Mboni Ruzegea, akizungumza kwenye kongamano hilo.
Mwenyekiti wa  Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL), Dkt. Sydney Msonde akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Katibu Mkuu Chama cha Wakutubi Tanzania (TLA), Dkt  Rhodes Mwageni akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.

Katibu Mkuu   wa  Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL), Dkt. Vincent Msonge akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo. 
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Totoo Ltd yenye makao yake makuu mkoani Kilimanjaro, Dk. Elvis Silayo akizungumza kwenye kongamano hilo.
Keki ya kutimiza miaka 15 tangu kuzaliwa kwa COTUL mwaka 2008 ikikatwa
Makamu Mwenyekiti COTUL, Profesa Kelefa Mwamtimwa, akitoa neno la shukurani kwa mgeni rasmi na wadau wengine wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Wakutubi wakiwa kwenye kongamano hilo.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Kongamano likiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
Washiriki wakiwa kwenye kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Wakutubi wakiwa kwenye kongamano hilo.
Viongozi meza kuu wakishiriki kuimba wimbo wa Taifa kabla ya ufunguzi wa kongamano hilo.
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Wakutubi wakionesha moja ya ishara ya mshikamano.
Viongozi wa COTUL wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu, Sakina Mwinyimkuu (katikati waliokaa) baada ya kufungua kongamano hilo Novemba 9, 2023.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamaja ba mgeni rasmi
Picha ya pamoja.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na wadhamini wa kongamano hilo.

Picha ya pamoja mgeni rasmi na washiriki wa kongamano hilo.


Wednesday, November 8, 2023

SEMA, STROMME FOUNDATION WAJIVUNIA MAFANIKIO MIAKA MIWILI MRADI WA ELCAP MKOANI SINGIDA

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga, akifunga kikao kazi cha kutathimini utekelezaji wa mradi wa ELCAP wa  miaka mitano ulioanza Septemba 20, 2021 ambao unatarajia kumalizika Mwezi Juni, 2026/ unao tekelezwa na Shirika la SEMA kwa kushirikiana na Shirika la Stromme Foundation Tanzania.

............................................................................


Na Dotto Mwaibale, Singida

SHIRIKA lisilo la Kiserikali la Sustainable Environment Management Action (SEMA) lenye makao yake makuu mkoani Singida kwa kushirikiana na Shirika la Stromme Foundation Tanzania kupitia mradi wa Kilimo Biashara wa ELCAP katika kipindi cha miaka miwili ya utekelezaji wa mradi huo wamepata mafanikio makubwa ya uongezaji uzalishaji wa mazao kwa kutoa elimu za teknolojia mbalimbali za kilimo.

 

Mkurugenzi wa SEMA, Ivo Manyaku akizungumza Novemba 7, 2023 kwenye kikao kazi cha kutathimini utekelezaji wa mradi huo wa  miaka mitano ulioanza Septemba 20, 2021 ambao unatarajia kumalizika Mwezi Juni, 2026 umekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima.

 

Alisema lengo la mradi huo ni kuwawezesha wakulima wadogo kuzalisha kwa ubora zaidi na kupata mazao mengi katika eneo dogo.

 

Manyaku alisema mradi huo ni mahususi kwa vijana na wanawake na ni muendelezo wa vikundi vilivyokuwa vikitumika katika mradi wa awali wa kuweka na kukopa na sasa wanawatoa katika eneo hilo na kuwaingiza kwenye uzalishaji wenye tija na kuongeza thamani kupitia mazao ya kilimo ambayo ni mahindi, alizeti, mtama na mbaazi.

Aidha, Manyaku alisema kupitia mradi huo wamefanikiwa kuwatafutia wakulima masoko kwa kuwaunganisha na wadau mbalimbali na wafanyabiashara .

Akitaja mafanikio mengine kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo wakulima walikuwa wakipata magunia ya mahindi kati ya sita hadi saba kwa heka moja lakini sasa wanapata magunia 15 hadi 20 na akamtaja mmoja wa wakulima hao kutoka Wilaya ya Ikungi kuwa alipata magunia 10 katika nusu heka.

Alisema lengo la mradi huo ni kuwafikia wakulima 6000 na kati ya hao asilimia 40 wawe vijana na asilimia mbili watu wenye ulemavu na kuwa umejikita kuhakikisha kuwa teknolojia wanazo wapa zinaendelea kuwasaidia wakulima hata baada ya mradi huo kumalizika.

Alisema pamoja na kuwa na lengo la kuwafikia wakulima 6000 lakini kwa kupitia mnyororo wa thamani wanatamani kuwafikia wakulima 10,000 katika wilaya ambazo unafanyika mradi huo ambazo ni Iramba, Ikungi na Manyoni na kuwa gharama ya mradi huo ni Sh.Bilioni 4.5.

Alisema mradi huo unatekelezwa na SEMA kwa kushirikiana na  Stromme Foundation na nchi ya Norway pamoja na washirika wao wa  kimkakati, NGI, CSFS na NMBU ambao wanawawezesha kuwapa teknolojia.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga ambaye alikuwa mgeni rasmi alishiriki kikao hicho na alitoa maoni yake namna ya kuboresha zaidi mradi huo ambapo alipongeza mashirika hayo kwa kuusaidia Mkoa wa Singida katika sekta ya kilimo.

“Katika mradi huu ni Singida peke yake ndiyo inasaidiwa kuhakikisha inaboresha kilimo ili kuongeza uzalishaji na hasa kwa kutumia teknolojia inayokwenda kuhifadhi maji katika mashamba yetu na kurutubisha ardhi na kuboresha maisha ya familia zetu,” alisema Mganga.

Alisema kwa kuwa mradi huo una walenga wakulima wadogo hasa wanawake na vijana katika wilaya za Ikungi, Iramba na Manyoni anaamini kutokana na kuwa wepesi wa kuelewa watakwenda kuleta mabadiliko chanya kwenye familia zao kwani wakiwezeshwa kupata mikopo na mbegu bora mashamba yao yanakwenda kuwa dhahabu katika Mkoa wa Singida.

Pamoja na mambo mengine  alishauri mradi huo uweze kufika mpaka shule za msingi na sekondari.kwa ajili ya lishe kwa wanafunzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Wizara ya Kilimo, Mohammed Chikawe aliyashukuru mashirika hayo kwa kuungamkono jitihada za Serikali katika sekta ya kilimo mkoani hapa na kueleza mradi huo unatekelezwa vizuri ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wadau hao wa maendeleo kuusambaza na kwenye mikoa mingine ili nayo iweze kupata teknolojia hiyo ya uzalishaji wa mazao na kuongeza thamani pamoja na kuwatafutia masoko kama ilivyofanya katika Mkoa wa Singida.

Wajasiriamali na wanufaika wa mradi huo Anna Ntandu kutoka Wilaya ya Ikungi na Rehema Mwaliwa kutoka Kata ya Iseke wilayani Ikungi waliyashukuru mashirika hayo kwa kuwapa mafunzo ya kilimo biashara ambayo yamewakomboa kiuchumi na kuweza kujikimu kimaisha na kusomesha watoto wao.

“Changamoto kubwa tuliyonayo ni vifaa vya kufanyia kazi, mtaji na masoko ya uhakika kwa mfano mimi nalazimika kutumia sufuria kwa ajili ya kuoka mkate badala ya oveni naomba tunapo hitimu mafunzo tuwe tunawezeshwa vifaa hivyo hata kwa kukopeshwa,” alisema Mwaliwa.

Mkurugenzi wa SEMA, Ivo Manyaku akitoa taarifa ya mradi huo.

Mkurugenzi Msaidizi wa Mipango na Bajeti Wizara ya Kilimo, Mohammed Chikawe, akizungumza kwenye kikao hicho. 
Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa SEMA, Daniel Chacha, akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwakilishi wa Shirika la CSFS kutoka Zambia, Gibson Simusokwe, akitoa mada kwenye kikao hicho.
Mwakilishi kutoka Shirika la NGI la , Nchini Norway Profesa Gerard Cornelissen, akizungumza kwenye kikao hicho.
Mwakilishi wa Shirika la NMBU kutoka Nchini Norway, Profesa. Jan Mulder, akizungumza kwenye kikao kazi hicho.
Mratibu wa miradi wa ELCAP, Alunas Maxwell, akiongoza kikao kazi hicho.
Meneja wa Miradi ya Stromme Foundation Tanzania , Doreen Matekele, akizungumza kwenye kikao hicho.
Mjasiriamali mnufaika na mradi huo, Anna Ntandu akiyashukuru mashirika hayo kwa kuwapa mafunzo ya kilimo biashara.
Mnufaika na mafunzo ya kilimo biashara, kutoka Kata ya Iseke wilayani Ikungi, Rehema Mwaliwa akitoa shukurani baada ya kupata mafunzo hayo.
Washiriki kutoka Stromme  Foundation  Kampala Uganda wakiwa kwenye kikao kazi hicho.
Kikao kikiendelea.
Kikao kazi kikiendelea..
Taswira ya kikao kazi hixmafunzo hicho.
Mgeni rasmi wa kufunga kikao hicho, Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dkt. Fatma Mganga, akikagua bidhaa za wajasiriamali walionufaika na mradi huo.
Picha ya pamoja na wadau wa mradi huo kutoka Norway.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Mgeni rasmi akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa Shirika la SEMA.


Thursday, November 2, 2023

RAIS SAMIA AMWAGA BIL 1.6/- KUTEKELEZA MIRADI ITIGI


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, Hussein Simba, jana Oktoba 31, 2023 akiongoza kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Leila Sewa, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, John Mgalula na Naibu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo.

.......................................................................

NA DOTTO MWAIBALE , SINGIDA

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan amekabidhi takribani Sh.Bilioni 1.6 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya sekta ya afya na elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mkoani Singida.

Hayo yamebainishwa Oktoba 31, 2023 kupitia kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la madiwani cha kujadili mambo mbalimbali ambacho kilikuwa na ajenda nane.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo. Hussein Simba alisema kati ya fedha hizo Sh. Milioni 700 zitatumika kununua vifaa tiba.

Alisema fedha nyingine Sh.Milioni 100 zinakwenda kujenga zahanati mbili na hivyo kuongeza idadi ya ujenzi wa zahanati hizo kufikia nane na kuwa Sh.Milioni 500 zitatumika kujenga jengo la kufulia, jengo la mionzi na dawa katika Hospitali ya Wilaya.

Simba aliongeza kuwa Sh.Milioni 180 zitatumika kwa ajili ya kuziboresha shule 10 kongwe na Sh.Milioni 128 zinakwenda kujenga bweni kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu.

Alisema Sh.Milioni 544 zinakwenda kujenga Shule ya Sekondari ya Majengo na zitakazosalia zitatumika kwa ajili ya ujenzi wa matundu 20 ya vyoo. 

Aidha, Simba alisisitiza kwamba halmashauri hiyo imekuwa ikikusanya mara dufu zaidi ya mapato ikilinganishwa na awali ambapo mpaka sasa kiasi kilicho kusanywa kinafikia asilimia 54 na kuwa matarajio yao hadi itakapofikia robo ya tatu watafikisha asilimia 100.

Simba alipongeza juhudi za Serikali kupitia Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan namna ambayo imeonesha ushirikiano uliotukuka kwa halmashauri hiyo katika muktadha chanya wa ustawi wa maendeleo ya watu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Leila Sawe na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Jumanne Ismail walisisitiza halmashauri hiyo kusimamia ipasavyo matumizi ya fedha zote zinazotolewa na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

 Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, John Mgalula akizungumza kwenye kikao hicho alipokea ombi la Diwani wa Kata ya Rungwa, Said Yahaya ambaye aliomba asilimia 40 ya mapato yanayokusanywa katika halmashauri hiyo yawe yanapelekwa kwenye kata kwa ajili ya kutekeleza miradi anayoibuliwa na wananchi.

Yahaya alitolea mfano wa stendi ya mabasi ya kata hiyo ambapo Mgalula alisema jambo hilo litapitiwa kwenye kamati ya fedha kuona namna ya kufanya na kueleza kuwa kabla ya kamti hiyo kukaa atawatuma madiwani wa viti maalumu kwenda kuangalia mradi huo. 

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, John Mgalula akizungumza.

Naibu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Jonathan Dule akifutailia jambo kwa makini 

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Leila Sewa, akizungumza.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manyoni, Jumanne Ismail, akizungumza.

Katibu wa CCM Wilaya ya Manyoni Maimuna Likunguni, akichangia jambo.

Waratibu wa vikao wa Halmashauri hiyo wakiwajibika. Kushoto ni Constantine Mihambo na kulia ni Makandaga Magabe.

Diwani wa Kata ya Mgandu, Martin Kapona,akisoma taarifa ya Kamati ya Fedha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili, William Masaka, akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo.

Diwani wa Viti Maalumu, Utukufu Gwimile na Diwani wa Kata ya Mgandu, Martin Kapona wakipitia taarifa za kikao hicho.

               Viongozi wakiwa meza kuu wakati wa kikao hicho

            Kikao kikiendelea.

Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wakiwa kwenye kikao hicho.

Wakuu wa idara na wataalamu wakiwa kwenye kikao hicho.

       Diwani wa Kata ya Rungwa, Said Yahaya, akichangia jambo kwenye kikao hicho.

Diwani wa Kata ya Majengo, Magreth Mwalwayo, akishukuru kwa miradi mbalimbali iliyotekelezwa katika kata hiyo.