Sunday, February 4, 2024

KAMATI YA KUDUMU YA AFYA YA BUNGE YARIDHISHWA NA UTENDAJI WA MSD

Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD), Mavere Tukai, akitoa taarifa  ya hali ya utendaji na majukumu ya MSD kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI jijini Dodoma., 

..............................................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI imesema imeridhishwa na hali ya utendaji wa Bohari ya Dawa(MSD) na mipango ya utekelezaji wa majukumu yake ikiwemo uzalishaji wa dawa ili kupunguza kununua dawa nje ya nchi.

Hayo yameelezwa Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya hali ya utendaji na majukumu ya Bohari ya Dawa (MSD), ambapo ameichagiza MSD kuongeza ufanisi, ubunifu wa hali ya juu kwa kuhakikisha bidhaa za afya zinakuwa toshelevu na kusambazwa.

Kwa upande mwingine Mwenyekiti ameshauri MSD kufuatilia na kukusanya madeni ili kuhakikisha inajiendesha vizuri bila kuathiri mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya na kuongeza kuwa wataendelea kuishauri serikali kuiwezesha MSD kupata mtaji ili iweze kujiendesha.

_“Bohari ya dawa sasa imeongezewa jukumu moja la kuzalisha bidhaa za afya na kuifanya sasa kutekeleza majukumu manne ambayo ni kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya katika vituo vya vyote vya umma vya kutolea huduma za afya nchini”_ ameeleza Mhe. Nyongo.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kwa uongozi imara katika taasisi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za afya kuongezeka na kufikisha vituoni kwa wakati.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai ameeleza kuwa tayari wameanzisha kampuni Tanzu ambayo itaingia mikataba na makampuni binafsi ya ndani na nje kuwekeza kwenye viwanda vya kuzalisha bidhaa mbalimbali za afya nchini, na wajumbe wanne wa Bodi wa kampuni hiyo tanzu wameshateuliwa.Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amempongeza Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai kwa uongozi imara katika taasisi hiyo na kuwezesha upatikanaji wa bidhaa za afya kuongezeka na kufikisha vituoni kwa wakati.

Naibu Waziri wa Afya Dkt.Godwin Mollel, akichangia jambo kwenye kikao hicho.Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Maswala ya UKIMWI, Mhe. Stansilaus Nyongo akizungumza kwenye kikao hicho.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo wakiwa kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea

 Mkutano ukiendelea.

Wednesday, January 31, 2024

Wateja Benki ya CRDB kuzawadiwa zawadi za Sh. Milioni 470 kampeni ya Benki ni SimBanking

 
Dar es Salaam. Tarehe 31 Januari 2024:  Katika jitihada zake za kuhamasisha  matumizi ya mifumo ya kidijitali nchini, Benki ya CRDB imezindua msimu wa tatu wa kampeni ya ‘Benki ni SimBanking’ na kutenga jumla ya zawadi zenye thamani ya Shilingi milioni 470 mamilioni kwa wateja wake mwaka huu.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Wateja wadogo na wakati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul amesema lengo la kampeni hiyo ni kujenga utamaduni wa matumizi ya kidijitali katika huduma za kifedha ili kuendana na kasi ya maendeleo na kuondokana na matumizi ya fedha taslimu.
“Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanaihamisha dunia kutoka kwenye miamala ya fedha taslimu kwenda ile isiyohusisha fedha taslimu yaani cashless economy. Tanzania hatupaswi kuachwa nyuma, ni lazima twende na mabadiliko hayo tena kwa kasi inayostahili,” amesema Bonaventure.

Kushiriki na kujiwekea nafasi ya ushindi katika kampeni hiyo mteja anatakiwa kutumia SimBanking kufanya miamala yake yote ya kibenki ikiwamo kulipia ankara za maji, umeme au visimbusi vya television, ada, malipo ya manunuzi, kutuma pesa, kulipia kodi, mikopo ya kidijitali, kutoa fedha kwa ATM au CRDB Wakala, kulipia bima ya vyombo vya moto, na huduma nyenginezo.
“Kwa kadri mteja atakavyokuwa akifanya miamala mingi zaidi ndivyo atakavyojiwekea nafasi ya ushindi,” amesema Bonaventure huku akibainisha kuwa katika kampeni hiyo itakayoenda hadi mwisho wa mwaka, kutakuwa na washindi wa gari aina ya Toyota Dualis watakaopatikana kila baada ya miezi mitatu, huku zawadi za  bajaj na pikipiki zikitolewa kwa mshindi wa kwanza na wa pili kila mwezi.

Aidha, katika msimu huu wa tatu wa kampeni ya ‘Benki ya SimBanking’, Benki ya CRDB imetenga zawadi za kompyuta mpakato kufikia 10 kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo vikuu, zawadi za simu janja, pamoja na fedha taslimu.

Pamoja na zawadi hizi Benki hiyo pia imetenga kiasi cha Shilingi milioni 200 zitakazotolewa kupitia Tembo Points ambazo mteja atakuwa akikusanya kila anapofanya muamala. Wateja wataweza kubadili Tembo Points zao kuwa fedha na kuzitumia kulipia huduma au bidhaa.
Bonaventure amewakumbusha wateja wa  Benki ya CRDB ambao hawajakamilisha usajili wa huduma za SimBanking kukamilisha mchakato huo ili wakidhi vigezo vya kujishindia moja kati ya zawadi zilizotangazwa na kuwakaribisha wananchi wengine kufungua akaunti kwa vigezo nafuu sana na kuunganishwa na SimBanking ili kufurahia huduma zilizoboreshwa zaidi.

Benki imeendelea kuiboresha huduma yake ya SimBanking ili kutoa huduma zenye viwango vya kimataifa na uzoefu ulio bora zaidi kwa wateja.  Mwaka jana, tulizindua SimBanking App iliyoboreshwa ambayo inatumia akili mnemba (Artificial intelligence), ianyoiwezesha kuwa na uwezo mkubwa katika utambuzi wa tabia na mahitaji ya mteja pindi anapotumia.

Mapema mwaka huu Benki ya CRDB imeongeza huduma mbili mpya ndani ya SimBanking ikiwamo  huduma ya malipo kupitia Msimbomilia wa Taifa (TANQR) ikimuwezesha mteja kufanya malipo kwa watoa huduma wote wa Benki ya CRDB na hata mitandao ya simu. Huduma nyengine ni ile ya kujitengenezea Tembo Virtual Card mahsusi kufanikisha miamala ya kieletroniki popote pale duniani kwa kushirikiana na Union Pay.











TAKUKURU SINGIDA YAOKOA ZAIDI YA SH.MILIONI 156 ZA MIRADI YA MAENDELEO

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Januari 31, 2024 ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023.

............................................................

Na Dotto Mwaibale, Singida 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imeokoa zaidi ya Sh.Milioni 156 baada ya kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sipha Mwanjala akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Januari 31, 2024 ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2023 alisema miradi iliyofuatiliwa ilikuwa ni 11 yenye thamani ya zaidi ya Sh.Bilioni 5 katika sekta za Elimu na Afya.

Mwanjala alisema miradi hiyo inajumuisha ujenzi wa Shule za Sekondari za Kutwa na za Kata iliyotekelezwa kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ambao unahusisha ujenzi na ukarabati wa Shule za Sekondari na kuwa fedha hizo pia zinahusisha ujenzi wa vituo vya Afya.

"Katika ufuatiliaji huo, fedha kiasi cha Sh. 10,220,000/= ziliokolewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama katika ujenzi wa Kituo cha Afya Gumanga na Ilunda kutokana na milango aina ya flash door iliyokuwa imewekwa awali kukosa ubora uliokuwa unatakiwa kwa mujibu wa BOQ, hivyo kulazimika kuiondoa na kuweka milango aina ya Hard wood doors yenye ubora uliotakiwa kwa mujibu wa BOQ," alisema Mwanjala.

Aidha, Mwanjala alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni fedha kiasi cha fedha Sh. Milioni 110.5 ziliokolewa, kutokana na kufanya malipo ya vifaa vilivyoagizwa kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Singida Solya kabla ya Mzabuni huyo kupeleka vifaa hivyo ili vikaguliwe, vikubaliwe na kupokelewa.

Alisema baada ya TAKUKURU kufuatilia, mzabuni huyo alipeleka vifaa vyote vilivyokuwa vimeagizwa.

Mwanjala alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi fedha kiasi cha Sh. 1,100,000/= kiliokolewa kutokana na kodi ya zuio ambayo ilikatwa kwa wazabuni waliotoa huduma katika ujenzi wa Shule ya Sekondari Iyumbu kwa ajili ya kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini hazikupelekwa na baada ya ufuatiliaji uliofanywa TAKUKURU fedha hizo zimepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA).

Katika kipindi hicho Mwanjala alisema TAKUKURU ilifanya  chambuzi sita za mifumo ili kubaini mianya ya rushwa iliyopo katika maeneo mbalimbali na kisha na kushauri namna ya kuiziba mianya hiyo ambapo pia walifanya fanya warsha tano kujadili mianya ya rushwa iliyobainika katika chambuzi zilizofanyika na kuweka mikakati ya kuziba mianya ya rushwa iliyobainika.

Alisema kutokana na uchambuzi wa mfumo wa ulipaji na ukusanyaji kodi ya zuio uliofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi,fedha kiasi cha Sh. Milioni 25 kiliokolewa Manyoni na fedha kiasi cha Sh. Milioni 9.9 ziliokolewa Itigi kutokana na kodi ya zuio ambayo ilikatwa na Halmashauri hizo kwa watoa huduma mbalimbali muda mrefu kwa ajili ya kupelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini hazikupelekwa na baada ya uchambuzi huo fedha hizo zimepelekwa Mamlaka ya Mapato (TRA)

Mwanjala alisema TAKUKURU Mkoa wa Singida iliendelea na utekelezaji wa Programu ya TAKUKURU RAFIKI kwa kufanya vikao 23 katika kata 23 na makundi mbalimbali ya wadau na kuwa kupitia vikao hivyo wadau waliibua kero 102 na kueleza kuwa kati ya kero 102 zilizoibuliwa, kero 79 zimetatuliwa na kero 23 zinaendelea kutatuliwa. 

Akizungumzia kuhusu Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Singida iliwaongezea wananchi uelewa kuhusu rushwa ambapo wananchi 13,601 (wanaume 6,971 na wanawake 6,630) walipata elimu hiyo kupitia Semina 61 kwenye makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Umma, mikutano ya hadhara 53, maonesho 7, Kutembelea na kuimarisha Klabu za Wapinga Rushwa 58 katika Shule za Msingi, Sekondari na Vyuo. 

Mwanjala akizungumzia uchunguzi na mashtaka alisema malalamiko 69 yalipokelewa kwa kipindi hicho ambapo malalamiko 34 yalihusu vitendo vya rushwa na malalamiko 35 hayakuhusu vitendo vya rushwa.

"Malalamiko 34 yaliyohusu rushwa uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali, malalamiko 35 ambayo hayakuhusu rushwa walalamikaji walishauriwa kadiri malalamiko yenyewe yalivyokuwa yakiendelea," alisema Mwanjala.

Alisema katika kipindi cha miezi hiyo kesi 10 zilifunguliwa mahakamani, kesi 7 ziliamuliwa, kesi 3 zilishinda na kesi 4 zilishindwa na jumla ya kesi 27 zinaendelea Mahakamani.

Akielezea mikakati ya TAKUKURU Mkoa wa Singida ya utendaji kazi kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Machi 2024 wataendelea kufuatilia matumizi ya fedha za Serikali zinazoelekezwa Mkoa wa Singida kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, wataendelea kuwaongezea uelewa wananchi kuhusiana na masuala ya rushwa ili wananchi washiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo vya Rushwahasa katika miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao na kuendelea kutekeleza Programu ya TAKUKURU – Rafiki. 

Mwanjala alitoa wito kuwa TAKUKURU Mkoa wa Singida inatoa RAI kwa wananchi wote kujiepusha na vitendo vya rushwa na kushiriki kikamilifu katika kuzuia vitendo hivyo vinavyotokea katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za kijamii na hasa katika utekeleaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.

Alisema kwa taarifa ya vitendo vya rushwa wasiliana nao kwa njia zifuatazo:

i. Fika Ofisi za TAKUKURU (M) Singida na Wilaya za Iramba, Ikungi, Mkalama na Manyoni.

ii. Kupiga simu ya bure 113 au simu ya Mkuu wa TAKUKURU Mkoa na Wakuu wa TAKUKURU wa Wilaya kwa namba zifuatazo:

Na Mkoa /Wilaya NAMBA YA SIMU

1 RBC –SINGIDA 0738150208

2 DBC - Mkalama 0738150 212

3 DBC - Ikungi 0738150213

4 DBC - Iramba 0738150 210

5 DBC - Manyoni 0738150 211

iii. Kutoa ushirikiano kwenye uchunguzi na kushiriki kutoa ushahidi Mahakamani. Maafisa wa Takukuru wakiwa kwenye kikao hicho.Kikao na waandishi wa habari kikiendelea.Mkutano na waandishi wa habari kikiendelea.Taswira ya kikao hicho.Muonekano wa Jesho la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida. 

Monday, January 29, 2024

KIKAO KAZI CHA KUJADILI RASIMU YA TAARIFA YA TATHMINI YA USHIRIKI WA WATANZANIA KATIKA MIRADI YA KIMKAKATI NCHINI CHAANZA SINGIDA

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Anderson Mutatembwa akifungua kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida, tarehe 29 Januari, 2024. 

.....................................................

Na Mwandishi Wetu, Singida 

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa, ameongoza kikao kazi cha wataalam kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini kilichofanyika Mkoani Singida Januari 29, 2024. 

Bw. Mutatembwa, alisema  dhana ya Ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati yaani (Local content) ni dhana inayolenga katika kuhakikisha kuwa thamani ya ziada inayopatikana kwenye uchumi kutokana na utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uwekezaji inabaki nchini na kuchangia ukuaji wa uchumi pamoja na kunufaisha Watanzania na Taifa kwa ujumla. 

Aliendelea kusema kuwa, Serikali inatekeleza dhana hii kwa kuhakikisha ajira kwa watanzania zinapatikana, uanzishwaji wa kampuni za ubia,  matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini katika uzalishaji na utoaji wa huduma,  manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa au zinazotolewa na kampuni za Kitanzania na  uhawilishaji wa teknolojia. 

Aidha aliongeza kusema kuwa, dhana hiyo inahakikisha uwepo wa ushiriki wa kampuni za kitanzania, na ushirikishwaji wa jamii zinazoishi katika maeneo ya uwekezaji au miradi inapotekelezwa. 

Akiongea na waandishi wa habari baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Condrad Millinga alisema moja ya eneo linalofanyiwa kazi katika kikao kazi hiki ni kuona watanzania watashiriki vipi hasa katika eneo la ajira za ndani kwa kuwajengea uwezo waweze kushiriki kwa maana ya wenye ujuzi na wasiokuwa na ujuzi, aidha kuangalia eneo la matumizi ya malighafi na rasilimali zilizopo nchini katika miradi mikubwa.

“Tunauzalishaji unaotumika lakini kwa kiwango kidogo sana kulinganisha na mahitaji halisi, kumbe tunahitaji wenyewe kujipanga ndani lakini pia kushirikiana na wenzetu wanaotoka nje ili kuzalisha kulingana na mahitaji katika maeneo ya Uwekezaji,” alisisitiza. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya masoko Nchini Bw. Charles Ogutu alisema mapitio ya rasimu hiyo yatahakikisha kwamba wanatanzania wanashirki kikamilifu na kunufaika na miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa nchini. 

“Bila kusahau kwamba hakuna mradi mkubwa ambao hautegemei kilimo kwa hiyo tunakitazama kilimo kama ndiyo sekta mama inayobeba sekta zote kwa hiyo ni vizuri sana mazingira ya kibiashara na mazingira yote katika sekta ya uwekezaji zijumuishe sekta ya Kilimo.” alibainisha. 

Akizungumza katika kikao kazi hicho kilichohusisha wataalam kutoka Serikali kuu,Taasisi, MDA’s na sekta binafsi mtaalam wa uwekezaji wa Kimataifa (FDI) na Uchumi mkubwa Dkt. Juma Makaranga alisema ni muhimu kwa makampuni ya ndani kufanya biashara na makampuni makubwa ya nje kwa kusaidiwa kutengenezwa na kuwainua kiteknolojia, usimamizi na kitaaluma.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Anderson Mutatembwa (Kulia) na Mkurugenzi Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Condrad Millinga wakifuatilia jambo, katika kikao kazi cha wataalam cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uboreshaji wa Mifumo ya Masoko nchini Bw. Charles Ogutu akizungumza katika kikao hicho.
Baadhi ya Watalaam wakipitia machapisho mbalimbali katika kikao kazi cha kujadili Rasimu ya Taarifa ya Tathmini ya Ushiriki wa Watanzania katika Miradi ya Kimkakati Uwekezaji inayotekelezwa nchini.

Sunday, December 10, 2023

SERIKALI YATOA MIL. 114/- KITUO CHA AFYA MTAE, MSD YAKIKABIDHI VIFAA TIBA

Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango, akimpatia nyaraka mbalimbali, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae kilichopo Lushoto mkoani Tanga, Shafii Makamba (kulia), wakati wa makabidhiano ya vifaa tiba vyenye thamani ya Sh.Milioni 114 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kununulia vifaa hivyo kupitia MSD kwenye tukio la makabidhiano lililofanyika Disemba 9, 2023. Wengine wanaoshuhudia tukio hilo kutoka kushoto ni Dereva wa MSD, Rashidi Msambo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtae, Andrew Kilama. 

.........................................................

Na Dotto Mwaibale, Lushoto

SERIKALI imetoa Sh.Milioni 114 kwa Kituo cha Afya  Mtae kilichopo Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ambazo zimetumika kununulia vifaa tiba kupitia Bohari ya Dawa (MSD) na hivyo kinatarajia kuanza kutoa huduma ya upasuaji mwishoni mwa mwezi Disemba 2023.

Hatua ya kituo hicho kuanza  kutoa huduma hiyo inatokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya kuibadilisha zahanati ya kijiji cha Mtae kuwa Kituo cha  Afya ili wananchi waweze kupata huduma bora na karibu.

Mganga Mfawidhi wa kituo hicho,  Shafii Makamba akizungumza wakati akipokea vifaa hivyo kutoka MSD alianza kwa kuishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassani kupitia MSD kwa kuwezesha kutoa vifaa hivyo vya dharura kwa ajili ya kufanya huduma ya dharura kwa wakina mama na watoto.

"Vifaa hivi tulivyovipokea leo kutoka MSD Kanda ya Tanga  vitasaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwa sababu kabla ya hapo walikuwa wakilazimika kutembea umbali usiopungua kilometa 65 kwenda Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kupata huduma za dharura hasa za upasuaji na kuwa wataachana na adha hiyo na kupata huduma hii hapa hapa katika kituo chetu," alisema Makamba.

Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kanda ya Tanga, Mary Isango akizungumza wakati akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Meneja wa MSD wa kanda hiyo, Sitti Abdulrahman, alisema wamepeleka vifaa hivyo baada ya kituo hicho cha afya kujengwa jengo la upasuaji na kupelekewa vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh.Milioni 114 ambavyo vinaenda kuondoa changamoto waliyokuwa wakiipata wananchi kwenda kupata huduma hiyo mbali.

"Huduma za upasuaji sasa zitafanyika katika kituo hiki baada ya kupata vifaa hivi ambavyo ni muhimu sana sisi kama bohari ya dawa wito wetu kwa watendaji wa kituo hiki ni kuvitunza ili viweze kudumu muda mrefu na kuleta tija kwa wananchi kadri watakavyokuwa wakiendelea kuvitumia kwa kuzingatia kuwa Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuvinunua," alisema Isango.

Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mtae, Beatrice Alphonce, Disifa Mdoe na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Andrew Kilama waliishukuru Serikali kupitia MSD kwa kuwapelekea vifaa hivyo ambavyo vitaondoa kabisa madhira waliyokuwa wakiyapata na wakati mwingine kusababisha vifo.

"Tulikuwa na changamoto kubwa baadhi ya wajawazito walikuwa wakijifungulia njiani kutokana na umbali mrefu wa kwenda Hospitali ya Wilaya ya Lushoto kupata huduma lakini sasa tutakuwa tunaipata hapahapa nyumbani kwa kweli tuna kila sababu ya kumshukuru Rais wetu mama Samia kwa kutuona na kutuonea huruma wanawake wenzake na kama ingewezekana tungemuomba siku moja aje hayaone kwa macho maendeleo haya aliyotuletea," alisema Alphonce.

Alphonce alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia, Mbunge wa jimbo hilo, Rashid Shangazi na viongozi wa wilaya hiyo kwa jitihada kubwa wanayoifanya ya kuwaletea maendeleo hayo ambapo aliwaombea kwa Mungu awape afya na maisha marefu.Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae, Shafii Makamba wakizipitia nyaraka hizo kabla ya kukabidhiana vifaa hivyo.Mapitio ya nyaraka hizo yakifanyika kwa pamoja kabla ya makabidhiano. Kutoka kushoto ni Afisa Huduma kwa Wateja wa Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Tanga, Mary Isango, Dereva wa MSD, Rashidi Msambo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtae, Andrew Kilama na  Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Kijiji cha Mtae, Shafii Makamba,Mwenyekiti wa Kijiji cha Mtae, Andrew Kilama akishukuru Serikali kwa kuwapelekea vifaa hivyo kupitia MSD,Muonekano wa Zahanati ya Kijiji cha Mtae kabla ya kubadilishwa kuwa Kituo cha AfyaMuonekano wa jengo la upasuaji lililojengwa na Serikali na kuipandisha hadhi zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya.Vifaa tiba hivyo vikitolewa kwenye gari tayari kwa makabidhiano.Vifaa tiba vikipelekwa kwenye jengo la upasuaji.Watoto wa Kijiji hicho wakishiriki kubeba vifaa hivyo.Kazi ya ubebaji wa vifaa hivyo ikiendelea.Vifaa vikibebwa.Wananchi wa kijiji hicho wakishiriki kubeba vifaa hivyo.Mkazi wa kijiji hicho, Beatrice Alphonce akiishukuru Serikali na MSD kwa kufanikisha kupatikana kwa vifaa hivyo.Mkazi wa kijiji hicho, Disifa Mdoe akipipongeza Serikali na MSD kwa kuwapelekea vifaa hivyo.Gari la MSD likiwa safarini kupeleka vifaa hivyo.

Monday, December 4, 2023

REA YAWASHA MRADI WA BILIONI 25 KUPOZA, KUSAMBAZA UMEME IFAKARA MOROGORO

Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya, akizungumza baada ya kuwasha  Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara    (Ifakara Substation), Desemba 3, 2023 Ifakara, Morogoro. Kituo kimejengwa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa gharama ya Shilingi bilioni 25.

...........................................................................

Na Mwandishi Wetu, Ifakara-Morogoro

SERIKALI  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) imewasha Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha  Ifakara ambacho kimegharimu shilling bilioni 25.

Akiwasha kituo hicho ambacho kimelenga kuongeza uwekezaji na uanzishaji wa viwanda kwa upatikanaji wa umeme wa uhakika, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero , Mh Dunstan Kyobya ameshauri kituo hicho kiitwe Samia Ifakara Substation.

Ameipongeza REA na EU kwa kuhakikisha kituo kimekamilika na kuwashwa kwani kinaenda kumaliza matatizo ya umeme katika wilaya ya Kilombero, Malinyi na Ulanga ambayo ni maeneo ya kimkakati ya kilimo na viwanda.

“Tunategemea kuongeza uwekezaji kwa kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na vile vya kuchakata madini” amesema Mh Kyobya.

Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza mazingira na vyanzo vya maji ili kujihakikishia umeme wa uhakika katika mabwawa ya kuzalisha umeme ya Kihansi na Kidatu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu amesema kuwashwa kwa kituo hicho kunaongeza upatikanaji wa umeme na hivyo kuwawezesha wananchi  kukuza na kuboresha hali zao za kiuchumi kwa kufungua biashara mbalimbali kwa uwepo wa umeme wa uhakika katika maeneo hayo.

“Wananchi watumie upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujiongezea kipato kwa kuwekeza na kuanzisha viwanda vya mazao ya kilimo na madini ambayo yanapatikana kwa wingi Kilombero, Ifakara, Ulanga na Malinyi,” amesema Mhandisi Olotu.

Naye Mbunge wa Kilombero, Aboubakar Asenga amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuchangamkia fursa ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuzalisha kwa wingi na kuanzisha viwanda vikubwa.

“Tunaishukuru serikali kwa kutimiza ahadi yake, ni wajibu wetu wananchi kutumia fursa hii ya upatikanaji wa umeme mkubwa kwa kuwa na viwanda vya kukausha na kukoboa mpunga, uzalishaji wa matofali kwa kisasa na uongezaji thamani wa madini ili kujiongezea kipato, ” amesema Mh Asenga.

Meneja wa Mradi huo kutoka REA, Mhandisi Romanus Lwena amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza 2020 ambapo kinazalisha kV 220 za umeme baada ya wananchi wa maeneo hayo kuwa wanapata umeme mdogo wa kV 33 uliokuwa unasababisha kukatika mara kwa mara.

Na baada ya kuwashwa kwa kituo hicho, kutawezesha kuwa na umeme wa uhakika kwa ajili ya viwanda na shughuli nyingine za kilimo.

Meneja Miradi ya Nishati wa EU, Mhandisi Francis Songela amesema katika Mradi huo wamechangia shilingi bilioni 18 na Serikali ya Tanzania imetoa shilingi bilioni 7.

Amesema kituo hicho kipo katika eneo la  kimkakati la  Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania , SAGCOT ambapo Mradi huo unaenda kuleta mapinduzi ya kilimo na viwanda.

“Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi ni maeneo ya kimkakati ya SAGCOT kwani yana rutuba kwa kilimo na shughuli nyingi za kiuchumi ambapo umeme wa uhakika ilikuwa changamoto  na kwa kuwashwa kwa kituo hiki tunategemea mapinduzi ya kilimo na viwanda, ” amesema Mhandisi Songela.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu akizungumza.
. Mbunge wa Kilombero, Mhe. Aboubakar Asenga akizungumza.
 Meneja wa Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation) kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Romanus Lwena akitoa maelezo kuhusu Kituo hicho kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya na Viongozi wengine mbalimbali wakati wa tukio la kuwasha Kituo hicho kilichojengwa na Serikali kupitia REA kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU) kwa lengo la kuimarisha huduma ya upatikanaji umeme kwa wananchi wa wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi.
Taswira ya Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation). Taswira hii ilichukuliwa Desemba 3, 2023 wakati wa tukio la kuwasha rasmi Kituo hicho baada ya ujenzi wake kukamilika.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dunstan Kyobya (katikati)  akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali na wataalam kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), TANESCO na Umoja wa Ulaya (EU) wakifurahi baada ya tukio la kuwasha rasmi Kituo cha Kupoza na Kusambaza Umeme cha Ifakara (Ifakara Substation), Desemba 03, 2023.