Tuesday, September 22, 2020

MOROGORO YAJIPANGA KUWA KINARA UZALISHAJI KOROSHO KWA TIJA.

Mratibu wa Kitaifa wa Zao la Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele Mtwara, Dkt.Geradina Mzena (kulia), akiwaelekeza Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Isabella Chilumba (kushoto) na  Afisa Kilimo wa Wilaya ya Gairo, Eunice Kyungai jinsi ugonjwa wa Ubwiriunga unavyoathiri zao la korosho. Mafunzo hayo kwa vitendo yalifanyika jana kwenye shamba la korosho la Shule ya Msingi Mnjilili wilayani Gairo, Morogoro.  

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa Visumbufu vya Wadudu na Magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Mtwara, Dkt.Wilson Nene, akiwaeleza  Maafisa Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali ya zao hilo.
Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya jinsi ya kuandaa shamba, kulipima na upandaji wa zao la korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Gairo.
Maafisa Ugani na Wakulima wakijifunza kwa vitendo namna ya upimaji wa shamba la korosho kabla ya kupanda.
Afisa Kilimo kutoka Kata ya Madege Wilaya ya Gairo, Fideli Ntumo (Aliye chuchumaa akipima shamba kwa kamba katika mafunzo hayo ya vitendo. 
Mkulima Julius Senyagwa kutoka Kijiji cha Majawanga wilayani Kilosa,  akijifunza namna ya kuweka 'mambo' wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Mary Gasper (kulia) na wenzake,  akijifunza namna ya kuweka 'mambo' wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho. Kushoto ni Afisa Kilimo, Lucy Mushi na Jacquline Roland.
Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Laya Abbas,  akijifunza namna ya kuweka mambo wakati wa mafunzo kwa vitendo ya upimaji wa shamba la korosho.
Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Dkt.Wilson Nene, akiwaonesha kwa vitendo Maafisa Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali ya zao hilo.

Afisa Kilimo kutoka Wilaya ya Gairo, Nasibu Said, akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa kuchimba mashimo kabla ya kupanda miche bora ya mikorosho katika shamba hilo lililopo shule ya Msingi Mnjilili, Gairo.


Mkulima  Elizabeth Senyagwa kutoka Gairo,  akishiriki mafunzo kwa vitendo kwa kuchimba mashimo katika shamba hilo la mfano la korosho la Shule ya Msingi Mnjilili.


Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mafunzo ya jinsi ya kupanda mche wa korosho kwa Maafisa Ugani na Wakulima.


Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu,  akitoa mafunzo ya jinsi ya kuchanganya viuatilifu na maji  kwa Maafisa Ugani na Wakulima kabla ya kupulizia kwenye mikorosho. 

Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akionesha namna ya kupulizia viuatilifu kwenye mikorosho.


Afisa Kilimo kutoka Kata ya Magubike wilayani  Kilosa, Iston Kutita, akijifunza kwa vitendo namna ya kupulizia viuatilifu mikorosho.


Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Morogoro.

WAKULIMA wa zao la korosho mkoani hapa wameahidi kufanya mageuzi makubwa ya kilimo cha zao hilo baada ya kuhamasika na programu maalumu ya mafunzo ya nadharia na vitendo inayoendelea kutolewa na Wizara ya Kilimo kupitia Taasisi yake ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI)

Taasisi hiyo kupitia kituo chake cha Naliendele kwa sasa kinaendesha mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa wakulima na maafisa ugani wa Halmashauri zilizo kwenye mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini lengo likiwa kuongeza tija na kuinua kiwango cha uzalishaji wa zao hilo.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo eneo la Shule ya Msingi Mnjilili, Mji Mdogo wa Gairo mkoani hapa wadau hao walisema mafunzo hayo yamekuja wakati mwafaka.

"Mafunzo haya yamenisaidia na kunipa mwanga wa namna ya kuboresha shamba langu la ekari mbili, kwa sasa nina matumaini makubwa ya kulima kitaalam zao hili." alisema mkulima wa korosho kutoka Dumila, Samwel Dede.

Mkulima mwingine Elizabeth Senyangwa kutoka Gairo alisema kabla ya kupata mafunzo hayo miongoni mwetu tulikuwa kwenye mtazamo wa kustawisha zao hilo kimazoea. Lakini kwa sasa nimejifunza mengi hasa kwenye eneo la udhibiti wa wadudu na magonjwa na namna bora ya kuandaa shamba langu.

Naye Afisa Ugani Elina Dastan kutoka Kilosa anaeleza kuwa anaona fahari kwa Taifa la Tanzania kupitia watafiti wake kuzidi kubuni teknolojia mpya kwa ustawi wa sekta ya kilimo nchini.

"Ugunduzi wa teknolojia za aina zote hizi za mbegu bora za korosho kutoka Tari ni fursa kubwa kwa wakulima na watanzania kwa ujumla." alisema Dastan.

Aidha, kutokana na hamasa iliyotawala wakati mafunzo yakiendelea, wadau hao wa zao la korosho walitaka kufahamu kwa kina ni aina ipi ya mbegu za korosho ambazo ni bora zaidi na zinazaa kwa wingi kama mkulima atahitaji kupata mavuno zaidi?.

Lingine lililojitokeza kwenye majadiliano ni je mbegu za zao hilo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo zinachukua muda gani hadi kuanza kuvunwa korosho yake sanjari na umakini wa palizi yake?

Na washiriki wa mafunzo hayo walitaka kufahamishwa endapo wanataka mbegu za Tari kwa haraka watazipataje na kwa utaratibu gani?.

Na zaidi wakionesha mwamko mkubwa walitaka kujua uhakika wa mwenendo wa soko kwa sasa...huku wale wengine waliopatiwa mbegu na Serikali huko nyuma wakitaka kuhakikishiwa ubora na uhalali wa mbegu hizo.

Akijibu maswali hayo Mratibu wa zao hilo kitaifa, Dkt Geradina Mzena alisema mbegu zote zilizogunduliwa na kufanyiwa utafiti na Serikali kupitia taasisi hiyo zina ubora na zinafaa kwa matumizi ya mkulima katika kupata tija inayostahili.

Huku Mtafiti kutoka Kituo cha Tari Naliendele Mtwara, Kasiga Ngiha akibainisha kuwa mbegu za korosho zinazozalishwa na kituo hicho huchukua kati ya miaka miwili mpaka mitatu kabla ya kukomaa na korosho yake kuanza kuvunwa.

Ngiha alisema mkulima anapaswa kuzingatia kanuni bora za kilimo cha zao hilo ili kuleta tija na ustawi, na anapofikia wakati wa kupalilia hupaswa kuwa makini kwa kuhakikisha jembe analotumia lisizame zaidi ya sentimeta 20 kinyume chake anaweza kujikuta akikata mizizi ya mkorosho inayoota kwa kwenda chini na ile inayotambaa.

Akifafanua utaratibu wa kupata mbegu hizo hususan kwa wakulima wa mkoa wa Morogoro, Dkt  Mzena alisema mkulima yeyote anayehitaji mbegu hizo awasiliane na Bwana Shamba aliye karibu naye, na yeye atawasiliana na Tari Naliendele ili kupatiwa huduma hiyo.

Aidha kwa wakazi wa mkoa wa Morogoro wanaweza kutumia kituo cha mauzo ya mbegu cha Tari kilichopo Bagamoyo maarufu 'Cash Development Centre (CDC)'

Akifafanua kuhusu uhakika wa soko la korosho Mzena aliwahakikishia wakulima kuwa zao hilo kwa miaka yote limeendelea kuwa ni 'dhahabu ya kijani' na soko lake halijawahi kuyumba.

Alisema zao hilo linauzwa kwa mfumo kamili unaosimamiwa hatua kwa hatua yaani mfumo wa stakabadhi ghalani sambamba na mkulima wa zao hilo kuendelea kuwa na fursa lukuki za kukopesheka kupitia taasisi za fedha.

Na kuhusu hoja iliyoibuliwa juu ya zile mbegu zilizotolewa na Serikali huko nyuma kipitia mabwana shamba alisema mbegu hizo zipo salama na zinafaa kwa matumizi.

Kwa upande wake Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho mkoani hapa Isabella Chilumba alisema azma ya mkoa huo ni kuzalisha tani 500 za korosho ifikapo 2023, huku msimu ujao 2020/21 wakitarajia kuzalisha tani 300 ya zao hilo.

Hata hivyo Chilumba alibainisha hatua kwa hatua maendeleo kadhaa ya ongezeko la uzalishaji wa zao la korosho kwa misimu 3 iliyopita, ambapo mwaka 2017/18 mkoa ulipata tani 63, na 2018/19 ulipata tani 155, mwaka 2019/20 kiwango hicho kiliongezeka na kufikia tani 181.5, huku shabaha ya taifa ni kufikia tani milioni 1  ifikapo 2023.

"Naamini kwa mafunzo haya yanayotolewa  na taasisi ya utafiti wa  kilimo, pamoja na stratejia zingine tulizonazo kama mkoa yatachochea kwa kiasi kikubwa kasi ya ongezeko la uzalishaji kwa tija na ubora." alisema Chilumba.


Monday, September 21, 2020

TARI YAANZA KWA KASI UTOAJI MAFUNZO KWA VITENDO KUINUA UBORA WA ZAO LA KOROSHO


Mratibu wa Kitaifa wa Zao la Korosho kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele, Dkt.Geradina Mzena, akitoa mada kwenye mafunzo ya kilimo bora cha korosho yaliyotolewa jana kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Gairo kwa Maafisa Ugani na Wakulima kutoka Halmashauri 7 za  Mkoa wa Morogoro. 

 

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Dkt.Wilson Nene, akitoa mada kwenye mafunzo hayo.

Mtafiti  kutoka Tari- Naliendele Programu ya Zao la Korosho, Kasiga Ngiha, akitoa mada kuhusu Agronomia ya korosho.


Washiriki wakiwa katika mafunzo hayo.

Mkuu wa Kituo cha Morogoro kutoka Bodi ya Korosho, Luseshelo Silomba akizungumza kwenye mafunzo hayo.


Mafunzo yakiendelea.

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Gairo, Eunice Kyungai akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Washiriki wakiwa katika mafunzo hayo.

Afisa Kilimo na Mratibu wa Zao la Korosho Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Isabella Chilumba akizungumza. 


Mafunzo yakiendelea.


Mjadala ukiendelea.

Washiriki wakiwa kwenye mafunzo hayo.
Mkulima Elizabeth Senyagwa kutoka Gairo,  akishiriki moja ya mjadala  kwenye mafunzo hayo kwenye mafunzo hayo.

Afisa Kilimo wa Wilaya ya Kilosa, Elina Dastan, akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Afisa Kilimo Abilah Samli kutoka Kilosa akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Mkulima kutoka Dumila, Samwel Dede akishiriki moja ya mjadala  kwenye mafunzo hayo.



Godwin Myovela na Dotto Mwaibale.

TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) kupitia Kituo chake cha Naliendele kimewataka wakulima wote wa zao la korosho kubadilika na kuanza kulima kilimo cha biashara kwa kuzingatia 'agronomia' stahiki ili kuongeza tija na ubora wa zao hilo.

Sambamba na hilo kituo hicho kimetoa angalizo kwa wakulima na wadau wa korosho kuhakikisha wanaepuka udanganyifu wowote wanapohitaji huduma ya mbegu bora ya zao hilo, badala yake wawasiliane na Maafisa Kilimo wa eneo husika ili kupata maelezo ya namna ya upatikanaji wake .

Mratibu wa zao hilo kitaifa kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Tari Naliendele Dkt.Geradina Mzena aliyasema hayo  kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa Gairo jana wakati   akifungua mafunzo ya kilimo bora cha zao la korosho kwa maafisa ugani na wakulima kutoka Halmashauri 7 za Mkoa wa Morogoro.

"Tari Naliendele hatuuzi mbegu kwa fedha taslimu, lazima uwe na namba ya malipo 'control number' na  endapo ukiuziwa mbegu na mtu yeyote kwa fedha taslimu ujue umeibiwa. Korosho ni zao la kudumu, lina mfumo wake na kamwe usijaribu kupanda mbegu usiyoijua." alisema Mzena.

Alisema mbegu bora ya zao hilo na aina zake huzalishwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tari Naliendele pekee na sio kwingineko, hivyo wakulima wanapaswa kuwa makini ili kwa pamoja kuweza kuinua ubora wa zao hilo na kujihakikishia uwepo wa soko lake kitaifa na kimataifa.

Aidha Mtafiti huyo na Mgunduzi wa zao hilo Dkt.Mzena alisema ili kubaini kama mbegu ya korosho husika ina ubora ni sharti idadi ya punje za korosho ziwe chini ya 200 kwa kilo moja na sio zaidi ya hapo.

Mratibu huyo kitaifa alifafanua kwamba kilo moja ya zao hilo inaposheheni punje zaidi ya 200 hudhihirisha wazi kuwa ubora wa mbegu hiyo una mashaka na mkulima husika anapaswa kufika Tari Naliendele ili kupatiwa mbegu mbadala zenye ubora.

Hata hivyo akizungumza mbele ya wakulima na maafisa ugani, Mzena ambaye pia ni Mratibu wa  Utafiti na Ubunifu kutoka Kituo cha Tari Naliendele alibainisha kuwa pamoja na mambo mengine korosho ambayo hulimwa na takribani watanzania laki 283 nchini ina faida kubwa katika kuongeza kipato cha kaya na kuondoa umasikini.

Alisema Mtanzania yeyote atakayelima korosho ndani ya mikoa rafiki takribani 17 inayostawisha zao hilo ni dhahiri atajipatia pesa za kutosha kutokana na ukweli kwamba zao hilo lina nguvu na utajiri mkubwa, tofauti na mazao mengine. Kikubwa ni kuzingatia kanuni bora za kilimo.

"Korosho haijawahi kukosa soko la uhakika, na zaidi inamfumo wa soko linaloeleweka unaoitwa stakabadhi ghalani na kukuwezesha kukopesheka kupitia taasisi za fedha." alisema.

Mzena alisisitiza kwa wale walio mbali na vituo vya Tari wakihitaji huduma ya mbegu bora wamuone Afisa ugani wa eneo lake ili hatimaye awasiliane na Tari Naliendele ili kuepuka hasara ya mkulima kuuziwa mbegu na viuatilifu feki.

"Mbegu za zao hili la kimkakati na aina zake zinazozalishwa na kituo chetu zinavumilia ukame, magonjwa, visumbufu vya wadudu na zinatoa mazao mengi." alisema Mzena.

Kwa upande wake Mtafiti mwingine wa zao hilo wa kituo hicho Kasiga Ngiha alisema kwa sasa wataalamu wa kituo hicho wanapita maeneo mbalimbali nchini kutoa elimu ya kuongeza ubora na uzalishaji wa zao la korosho kwa tija na ustawi.

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa visumbufu vya wadudu na magonjwa kwenye zao hilo, Dkt.Wilson Nene alisema kituo hicho kinatoa mafunzo hayo lengo ni kuwawezesha wakulima na maafisa ugani kuwatambua wadudu waharibifu, magonjwa na namna ya kukabiliana nayo ili kufikia shabaha tarajiwa kutoka tani laki tatu zinazozalishwa kwa sasa kufikia tani milioni 1 ifikapo  2023.

" Korosho inafaida nyingi ikiwemo baada ya kusindika tunazalisha bidhaa kama korosho karanga, na bibo lake hutumika kutengeneza bidhaa ya juisi, mvinyo, ethanol na malisho ya mifugo." alisema Nene.

Alisisitiza kimsingi mafunzo hayo yanalenga kutoa teknolojia ya mbinu bora na za kisasa za uzalishaji wa zao la korosho kwa kuzingatia wapi mkulima atapata mbegu bora, namna ya kuandaa shamba, kuchimba mashimo, kupanda na kupalilia hatimaye mavuno yake.

Kituo  cha Tari Naliendele pamoja na mambo mengine kimepewa majukumu ya kitaifa ya kutafiti, kustawisha na kuongeza tija na thamani kwenye mazao ya korosho na mbegu jamii ya mafuta-ikiwemo ufuta, karanga na alizeti. 

Sunday, September 20, 2020

KANISA LA ABC LAFANYA MAOMBI YA KULIOMBEA TAIFA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 




vlcsnap-2020-09-20-11h48m00s617.png
Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela , jijini Dar e Salaam, Flaston Ndabila, akiongoza maombi kwenye kongamano la maombi ya kuliombea Taifa kuelekea Uchaguzi Mkuu lililofanyika kanisani hapo jana.


IMG_3725.JPG
Maombi yakiendelea kwenye kongamano hilo.
IMG_3686.JPG
Kushono ni Bendera ya Tanzania iliombewa na maaskofu na Katikati ni Bendera Nyeupe ya Taifa la Israel ikiombewa na Kulia ni  Wachungaji wa Madhehebu wa Huduma ya Maombi wakiiombea Bendera ya Africa.
IMG_3661.JPG

 Mchungaji wa Huduma ya Maombi Tanzania, .Alice Kopwe akizungumza kwenye Kongamano hilo.



Na Dotto Mwaibale.

KANISA la Abundant Blessing Centre (ABC) lililopo Tabata Mandela , jijini Dar e Salaam limefanya maombi ya kuliombea Taifa liwe na amani wakati huu wa kampeni hadi utakapofanyika uchaguzi Mkuu Oktoba 28, mwaka huu.

Kongamano la maombi hayo liliongozwa na Askofu Kiongozi wa Kanisa hilo, Flaston Ndabila akishirikiana na wachungaji, maaskofu na waumini kutoka jijini Dar es Salaam na mikoani.

Akifungua kongamano hilo, Ndabila alisema wameamua kufanya maombi hayo kwa sababu unapofanyika uchaguzi kunakuwa na changamoto mbalimbali.

Alisema kufuatia kuwepo kwa changamoto hizo, anahitajika mtu au watu wa kuzitatua kwa kuziombea na kuelimisha wagombea.

Ndabila alisema kanisa lina hekima ya kuvielekeza vyama vya siasa njia iliyonyooka ili viwe na busara ya kufanya uchaguzi bila ya umwagaji damu.

Aliongeza kuwa wao kama kanisa wanamuombea mama Janeth Magufuli Mungu ampe hekima ya kumshauri mumewe azidi kuliongoza taifa letu kwa busara kuepuka umwagikaji wa damu wakati huu wa uchaguzi.

Ndabila aliwapongeza wagombea wa vyama vya siasa kwa kuanza kuimba wimbo wa taifa kwenye kampeni zao huku wakimtanguliza Mungu.

Ndabila alisema vita ikitokea wa kulaumiwa litakuwa kanisa kwa sababu halikumuomba Mungu atuepushe na machafuko wakati wa uchaguzi.

"Wagombea wote ni watoto wa kanisa hivyo wanapaswa kumtii Mungu ili wasilete machafuko katika nchi yetu," alisema Ndabila.

Naye Mchungaji Evelyne Mayengo akizungumza kwenye kongamano hilo alimshukuru Mungu kwa kulilinda taifa letu tangu lilipoanzishwa kwa kulifanya taifa lenye umoja na mshikamano ingawa lina makabila mengi.

“Tumshukuru Mungu kwa viongozi wetu wakuu kubadilishana kijiti cha uongozi kwa amani bila kumwaga damu wala kuligawa taifa,” alisema mchungaji huyo.

Aidha, alimshukuru Mungu kuliponya taifa letu na maradhi ya Corona na kutuwezesha kufanya kampeni na uchaguzi mwaka huu.

Mchungaji Alistidia Modest wa Kanisa la MPC akizungumza kwenye kongamano hilo alimshukuru Mungu kwa kuliwezesha taifa letu kuingia kwenye uchumi wa kati kabla ya Mwaka 2025 uliokadiriwa.

Alimshukuru pia Mungu kwa kuifanya nchi yetu kuwa na rasilimali nyingi kama bahari, maziwa, madini yakiwemo ya Tanzanite yanayopatikana nchini mwetu pekee, gesi, milima, mbuga za wanyama na maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho.

Naye Mchungaji Alice Kopwe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amemuomba Mungu aiwezeshe NEC kusambaza vifaa vya kupigia kura vifike vituoni kwa wakati,  vitosheleze na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Oktoba 28.

Maombi yaliyojiri kwenye kongamano hilo pia yalihusu kuwaombea viongozi wa NEC, vyombo vya dola vitende haki na wote wawe na hofu ya Mungu ili uchaguzi uwe huru na haki. 

Kwa upande wake Bishop Sendrich Ndonde aliliombea baraka taifa la tanzania, taifa la Israel na kuwabariki waombaji waliohudhuria katika  kongamano hilo ambapo naye Mchungaji Dkt.  William Kopwe wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amemuomba Mungu atupe Rais kutoka kwake.

Saturday, September 19, 2020

MTATURU: KUTOICHAGUA CCM NI SAWA NA KUPISHANA NA GARI LA MSHAHARA.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu, akiwasili kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Tarafa ya Makiungu Wilaya ya Ikungi mkoani Singida jana.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu, akihubia kwenye mkutano huo.
Wananchi wa Tarafa ya Makiunga wakimsubiri Mtaturu.
Waendesha boda boda wakiongoza msafara wa mgombea huo.
Wananchi wa Tarafa ya Makiungu wakiwa na mabango yenye picha za mgombea Urais wa CCM wakati wa kumpokea Mtaturu.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano.


Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu, akionesha upendo kwa wapiga kura kwa kusalimiana nao.
Burudani ikiendelea katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Makiungu, Daud Kinjagahi, aakizungu kwenye mkutano huo.
Kada wa CCM, Gerald Mahami akizungumza kwenye mkutano huo.
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu (kulia), akiteta jambo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,  Alhaji Juma Kilimba.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Ikungi, Pius Sanka, akizungumza katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa, akizungumza katika mkutano huo.

Wananchi wakiwa kwenye mkutano.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,  Alhaji Juma Kilimba, akiwanadi wagombea udiwani wa Kata ya Makiungu, John Mathias (kulia) na Gabriel Dule (katikati) wa Kata ya Mngaa.
 



Na Dotto Mwaibale, Singida.


MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Singida Mashariki kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Miraji Mtaturu amesema kutokukichagua chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu ni sawa na kupishana na gari la mshahara.

Mtaturu aliyasema hayo jana wakati akiwahutubia Wananchi na wana CCM wa Tarafa ya Makiungu na Kata ya Mngaa katika mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni ndani ya jimbo hilo.

"CCM tumejipanga sawa sawa kwenye sekta zote hivyo kutokukichagua CCM ni sawa na kupishana na gari la mshahara." alisema Mtaturu.

Katika mkutano huo Mtaturu alikwenda mbali zaidi kwa kuwafananisha wagombea wengine wa nafasi ya Urais wa vyama vingine na mgombea Urais wa CCM kama ni kichuguu na Mlima Kilimanjaro au Mbingu na ardhi kutokana na mambo makubwa aliyoyafanya mgombea wao.

"Hatuwezi kabisa kuwafananisha wagombea hao na Magufuli kwani amewaacha mbali sana." alisema Mtaturu.

Mtaturu alitumia nafasi hiyo kuomba ridhaa ya kuchaguliwa tena kwa kipindi cha Miaka 5 ili aweze kufanya makubwa ndani ya jimbo hilo na pia alimuombea kura mgombea wao wa nafasi ya Urais Dkt John Magufuli,wabunge na madiwani wa chama hicho.

Alisema kugombea ubunge sio kujaza nafasi bali ni uwakilishi wa kuwatumikia Wananchi kwa kuwapelekea maendeleo na kuacha shughuli nyingine binafsi ambazo haziwahusu wananchi.

Aidha alisema kiongozi yeyote anapoaminiwa na wananchi kwa kupewa kazi ni lazima aache alama ya utendaji wake kama alivyofanya yeye katika maeneo mbalimbali alikoaminiwa kufanya kazi na kuhakikisha jimbo hilo linakuwa la mfano kwa maendeleo katika majimbo yote hapa nchini.

Akizungumzia ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 alisema ni kubwa kuliko ile ya 2015-2020 ambayo imebeba matumaini na kuwa na majibu ya kero za watanzania.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,  Alhaji Juma Kilimba alisema uchaguzi wa mwaka huu ni wa muhimu hivyo wananchi wasifanye utani bali wamchague Rais ambaye atawafaa watanzania ambaye ni Dkt. John Pombe Magufuli.

Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi Mika Likapakapa alisema wagombea pekee wanapaswa kuchaguliwa ni wale wanaotoka kwenye chama hicho chenye sera na dira na sio kwa wagombea wengine ambao wamekuwa wakipitisha mabakuli kuomba wachangiwe.