Saturday, October 24, 2020

SERIKALI YAKABIDHI BAISKELI 103 KWA WAHUDUMU WA AFYA IKUNGI

 Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akikabidhi usafiri wa Baiskeli na Vipaza sauti kwa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii wilayani hapo juzi kama nyenzo muhimu zitakazowasaidia. kurahisisha utekelezaji wa majukumu yao.

Hafla ya makabidhiano ikiendelea.
Afisa Lishe na Mratibu wa Huduma za Jamii wilayani hapo, Agnes John akisoma taarifa fupi ya Mradi wa Boresha Lishe kwenye Halmashauri ya Ikungi.

Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wakiwa na baiskeli na vipaza sauti muda mfupi baada ya kukabidhiwa.
Mwonekano wa Baiskeli hizo.

Mkuu wa Wilaya Mpogolo akiendesha hafla hiyo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi (DAS), Winfrida Funto (katikati) akifuatilia kwa makini makabidhiano hayo, kulia ni Afisa Tarafa, Josephine Kadaso na DC Mpogolo.

Hafla ikiendelea.

Afisa Mradi wa Boresha Lishe kutoka shirika la SEMA, Hudson Kazonte akizungumzia tija ya mradi huo na namna usafiri huo wa baiskeli utakavyopunguza changamoto ya utoaji huduma.


Na Godwin Myovela, Ikungi

SERIKALI kwa kushirikina na Umoja wa Nchi za Ulaya na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imetoa jumla ya baiskeli 103 kwa wahudumu wote wa afya ngazi ya jamii sambamba na ‘vipaza sauti’ vyenye idadi kama hiyo wilayani hapa, lengo ni kuwapunguzia changamoto ya usafiri wakati wakitekeleza majukumu yao.

Katika kuboresha afya ya uzazi na lishe, kupitia mradi wa ‘Boresha Lishe’ serikali kupitia halmashauri ya Ikungi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali ya ‘SEMA’ na ‘RECODA’ imeazimia kupunguza udumavu wa siku 1000 za mtoto-yaani tangu kutungwa kwa mimba hadi anapofikisha miaka 2.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi baiskeli hizo ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo aliwataka waliokabidhiwa baiskeli hizo kuhakikisha wanazitunza na zinatumika kwa malengo kusudiwa.

“Niwasihi muwe waangalifu na mzitunze baiskeli hizi, serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwenye sekta ya afya hususani kwenye eneo hili la afya ya uzazi na lishe, azma ikiwa ni kuhakikisha tunaondoa kabisa kiwango cha utapiamlo wa udumavu kutoka asilimia 7 mpaka 0,” alisema Mpogolo.

Aidha, aliyashukuru mashirika na nchi wahisani wanaoendelea kushirikiana na serikali katika kutekeleza mradi wa Boresha Lishe kwa vijiji 43 kuzunguka Ikungi huku akisisitiza ni mradi wenye tija kwa makundi yote ya jamii wilayani hapo, na hasa akinamama wajawazito, wanaonyonyesha na watoto chini ya miaka miwili.

Naye Afisa Lishe na Mratibu wa Huduma za Jamii wilayani hapo, Agnes John, alisema Halmashauri ya Ikungi ina jumla ya Kata 28 na Vijiji 101 vyote vina wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii, na wote wamepatiwa mafunzo ya msingi ya awali ya afya ya uzazi na lishe.

Halmashauri ya Ikungi ina jumla ya wakazi 329,520, ambapo watoto chini ya miaka mitano ni 58,707, na wanawake wenye umri wa kuzaa (miaka 15-49) wanafikia 22,884.

“Mafanikio tuliyoyapata mpaka sasa ni kujikwamua mapema kwenye rangi nyekundu, kwa miaka miwili mfululizo mpaka sasa viashiria vyote vinavyohusiana na huduma za wahudumu wa afya ngazi ya jamii vina alama ya kijani kuashiria tunafanya vizuri,” alisema John.

Aidha, mratibu huyo alisema hata kiwango cha utapiamlo wa udumavu kimepungua kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 5, wakati kimkoa ni asilimia 29.8. Alisema ukondefu umepungua kutoka asilimia 1 hadi kufikia 0.4, wakati kimkoa ni asilimia 4.7.

 

Thursday, October 22, 2020

VIONGOZI WA DINI MKOANI SINGIDA WAJA NA MAAZIMIO SABA UCHAGUZI MKUU

 


  Mwenyekiti wa Kamati ya  Amani ya Viongozi wa Dini  na Madhehebu mbalimbali Mkoa wa Singida,(aliyesimama)Hamis Muhamed Kisuke akiongoza kikao ambapo walizungumzia  hali ya amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu na kuja na maazimo saba. (Picha na Rose Nyangasa).

Mkuu wa Mkoa  wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi  akizungumza na Kamati  ya Amani ya Viongozi wa Dini na Madhehebu  mbalimbali Mkoa wa Singida ambapo ameipongeza Kamati hiyo kwa kuamua  kuhamasisha amani na utulivu kwenye  kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu (Picha na Rose Nyangasa)

 Wajumbe wa Kamati ya Amani Mkoa wa Singida wakimsikiliza kwa makini Kamanda wa Polisi wa MKoa wa Singida, Sweetbert Njewike (hayupo pichani) wakati akielezea majukumu ya jeshi hilo kwenye siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Rose Nyangasa).

      Kamanda wa Polisi wa MKoa wa Singida, Sweetbert Njewike majukumu ya jeshi hilo kwenye siku ya upigaji kura Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Rose Nyangasa).

 

John Mapepele na Rose Nyangasa, Singida

Kamati ya Amani na Dini mbalimbali  Mkoa wa Singida inayojumuisha viongozi wa madhehebu na dini zote  imetoa tamko lenye maazimio saba kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba  28, mwaka  huu huku  ikiwaomba waumini wao kumtanguliza Mungu na Serikali kusimamia  amani na utulivu ili kuwapata viongozi bora watakaoingoza  nchi katika miaka mitano ijayo 2020 hadi 2025.

Akisoma maazimio hayo, Mwenyekiti wa  Kamati hiyo Shehe, Hamis Muhamed Kisuke amesema  miongoni mwa maazimio hayo ni  kuwaomba waumini wao kutenga siku tatu kuanzia Ijumaa hadi Jumapili ya juma hili kwa ajili ya  kufunga na kuomba ili kuombea  uchaguzi upite  kwa  amani na usalama.

Maazimio mengine  yaliyofikiwa kwenye kikao hicho ni pamoja na viongozi wa dini katika kipindi hiki kudumisha  Amani, kutotumika  kwenye majukwaani ya siasa kushabikia  viongozi wa vyama vya siasa, kuhubiri Amani,

kuhimiza waumini wao kushiriki kupiga kura na kuhimiza kufuata na kutii sheria za  nchi ambapo  pia wamesisitiza kuviacha vyombo  halali vilivyopewa dhamana  ya kusimamia uchaguzi huo vifanye kazi yake.

Mwakilishi wa dini ya Kiislam (Baraza la Kiislam Tanzania) katika  Mkoa wa Singida Shehe, Issa Nassor amesema Amani  ikitoweka  watakaoumia  zaidi ni  watoto, wanawake, wajawazito, wazee na watu wenye  mahitaji maalum kwa kuwa  hawana  uwezo wa  kukimbia  na kujitetea.

Aidha,  wamewataka wazazi  na walezi wa kila familia  kuwaasa  vijana kujiepusha  na kushawishiwa na watu wanaoitakia  mabaya  nchi ya Tanzania ambapo ameongeza kwamba   baada ya  kupiga kura vijana warejee  nyumbani  kwa  kuwa tayari Serikali imeshaweka  vyombo maalum kwa ajili  kuhesabu na kutangaza matokeo hayo.

“Historia inaonyesha kuwa nchi zote duniani zilizopoteza amani ni nchi ambazo walilewa amani, vilevile tukumbuke kupata amani ni mchakao wakati  kuvunja amani  ni jambo rahisi  kabisa. Nawaomba watanzania wenzangu  kutumia  vipande  vyetu vya kupigia kura  kuwachagua Viongozi bora” aliongeza  Shehe, Nassor

Mwakilishi kwa upande wa wakristo, Askofu wa Kanisa la TAG mkoani Singida, Gasper Mdimi amesema amani  ya nchi ni jambo nyeti ambalo linatakiwa  kuchukuliwa  kwa uangalifu mkubwa kwa kuwa  lina athari   pana  kuanzia  kwenye  ngazi ya  kaya  hadi taifa kwa ujumla  na kwamba  Bibilia imefafanua  kuwa chanzo cha Amani  ni  Mungu mwenyewe, Haki na Watu wanaomcha  Mungu.

Amefafanua kuwa  vitabu vyote vitakatifu  vinasisitiza kutafuta  kuwa na amani  na watu wote ambapo   na kwamba watanzania  wanatakiwa kupendana  katika kipindi hiki bila kuangalia   vyama vyao  vya  Siasa   na kuiombea  nchi yao  ipate  viongozi ambao  watailinda amani.

Pia amesema   wakati  wananchi wanakwenda  katika siku za mwisho wa kuhitimisha zoezi la kuwachagua viongozi   ni  muhimu  kuzingatia kuacha kuongea  maneno ambayo yatasababisha machafuko na  uvunjifu wa amani.

Mwakilishi wa Mhashamu Baba Askofu wa  Jimbo  Katoliki la Singida, Padre Padri Elia Mnyakanka amesema Uongozi Bora ni tunu na zao  la amani na kwamba  ili kuwa na maendeleo na ustawi  kuanzia ngazi ya familia na taifa ni muhimu kwa wananchi kutafakari kwa kina  na kuwachagua viongozi wanaoweza kuilinda amani.

Akitoa mfano amesema katika taifa la Israel uongozi bora ulikuwa ni nyenzo ya kuwafikisha  kwenye nchi ya ahadi kupitia manabii mbalimbali ambapo kwa kufanya hivyo amani ilipatikana.

Amesema  viongozi wa dini wanapaswa  kuwapa elimu ya uraia waumini wao  ili kuwapa  uwezo  wa kuwachagua wagombea makini kupitia ilani zao ambapo amesisitiza kwamba uchaguzi wa haki na amani ndiyo njia pekee ya kujitawala na kuleta amani katika nchi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida,  Sweetbert Njewike  amesema kwenye kipindi hiki  cha uchaguzi majukumu yao  ni pamoja na  kutunza na kudumisha Amani, kusimamia utekelezaji wa sheria, kuzuia na kubaini makosa ya jinai, kuwakamata wahalifu wanaohatarisha amani na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, kulinda  mali za raia, kutoa ulinzi kwa maafisa na vituo, pia kuhakikisha hakuna mtu anaye watishia wapiga kura na kuhakikisha usalama wa vifaa vya kupigia kura. 

Mkuu wa Mkoa Singida Dkt.Rehema Nchimbi amewashukuru viongozi hao kwa kuandaa mkutano  huu ambao umelenga kudumisha amani na kuwahimiza wananchi washiriki kikamilifu kupiga kura  ili kuwa chagua viongozi bora.

Aidha Dkt.Nchimbi amewataka Viongozi wa Dini kutotumika kuharibu amani na mshikamano ambao  upo kwa kipindi kirefu sasa hapa nchini kutokana na kazi nzuri  ya kusimamia amani hiyo iliyofanywa na Serikali

WATAFITI: MAENDELEO YA KIUCHUMI SINGIDA HAYATOKANI NA KILIMO CHA ALIZETI PEKEE

Mkuu wa Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Tanzani (APRA) Profesa. Aida Isinika akifafanua jambo baada ya kuulizwa maswali na waandishi wa habari kwenye warsha ya siku moja iliyofanyika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro juzi.
Mtafiti wa mradi huo, Profesa Ntengua Mdoe akifafanua kuhusu kilimo biashara cha mpunga, mifugo na hali maisha ya wakulima wadogo katika Bonde la Kilombero kwenye warsha hiyo.
Mtafiti wa mradi huo, Dk.Devotha Kilave akitoa mada kuhusu wanawake wanavyoshiriki shughuli za kilimo.
Mtafiti wa Mradi huo,Dk.Christopher Magomba akifafanua jambo kwenye warsha hiyo.

Mtafiti wa Mradi huo,Profesa Gilead Mlay akishiriki kufafanua mambo kwenye warsha hiyo.
Mwanahabari Gerald Kitabu akishiriki mjadala kwenye warsha hiyo. 
Waandishi wa habari wakiwa kwenye warsha hiyo.
Warsha ikiendelea.
Waandishi wa habari wakifuatilia wakifuatilia mada zilizokuwa zikitolewa na watafiti wa mradi huo..
Warsha ikiendelea.

 Warsha ikiendelea.


Mtafiti Msaidizi wa mradi wa mradi huo, Gideon Boniface akitoa mada kuhusu athari walizopata wakulima kipindi cha ugonjwa wa  Covid-19.  

Picha ya pamoja waandishi wa habari na watafiti wa mradi huo kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) 



Na Dotto Mwaibale,  Morogoro


MABADILIKO ya Maisha na Uchumi wa Mkoa wa Singida imeelezwa hayatokani na kilimo cha alizeti pekee bali na mazao mengine pamoja na shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Hayo yameelezwa na watafiti ambao walifanya utafiti katika Mkoa wa Singida kubaini ukweli wa nini kilichoufanya mkoa huo kuwa na maendeleo ya kiuchumi baada ya kuwepo kwa dhana ya wananchi kwamba kilimo cha alizeti ndicho kimeupaisha mkoa huo kimaendeleo.

Mtafiti Dk. Christopher Magomba akiwasilisha mada mkoani hapa juzi ya utafiti huo kwa  waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwenye warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Mradi wa Utafiti wa Sera za Kilimo Barani afrika (APRA) iliyolenga kutoa matokea ya utafiti wao kwa jamii alisema kilimo cha mazao mengine na shunguli zingine za kiuchumi, vyanzo mbadala na miradi midogo midogo inayofanywa na kaya nayo imechangia kuinua uchumi wa mkoa huo.

Akitolea mfano kilimo cha mahindi ambacho ni asilimia 83.86 ni moja ya zao ambalo linaonesha kuchangia maendeleo mkoani humo ukilinganisha na alizeti ambalo katika utafiti wao walioufanya Wilaya ya Iramba na Mkalama lilionesha kuwa na asilimia 71 tu.

Magomba alitaja mazao mengine ambayo yameonesha kufanya vizuri na kuongeza kipato katika mkoa huo kuwa ni vitunguu, nyanya, mtama pamoja na pamba.

Katika hatua nyingine Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo  (SUA ) ambao wapo kwenye mradi wa APRA katika utafiti wao wamebaini kuwa vijana hasa wa kiume ndio wanaonufaika zaidi na Kilimo Biashara cha Mpunga  Bonde la Kilombero ijapokuwa wanachangamoto ya mitaji na kukosa mashamba binafsi.

Akiwasilisha mada kuhusu matokeo ya utafiti wake uliohusu ushiriki wa vijana kwenye kilimo biashara cha mpunga kwenye Bonde la Kilombero  Profesa Ntengua Mdoe alisema vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 ambao ni sawa na asilimia 35.5% ya watu ndio wenye kunufaika zaidi katika bonde hilo ukilinganisha na makundi mengine.  

"Utafiti wetu umebaini sio kweli vijana hawashiriki kwenye shughuli za kilimo  wanashiriki na wanafanya vizuri kwenye kilimo biashara cha mpunga pamoja na kwenye mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo katika maeneo mbalimbali."alisema.

Alisema kwenye Utafiti huo wamebaini kuwa kipato wanachokiota vijana kwenye nguvu wanayowekeza kwenye kilimo ni kikubwa kuliko nguvu inayowekezwa na vijana wanaofanya kazi zingine hapa nchini.

“Ukiangalia kwenye Utafiti tumebaini kuwa nyumba nyingi zinazoongozwa na vijana zina uhakika mkubwa wa chakula kuliko kaya ambazo zinaongozwa na wazee na watu wenye umri mkubwa na hii ni kutokana na mafanikio makubwa wanayoyapata kutoka kwenye kilimo.” alisema Mdoe.

Katika mapendekezo ya utafiti huo wametoa ushauri kwa  Halmashauri na Serikali za Mitaa kutenga ardhi ya kilimo kwa ajili ya vijana kama ambavyo imeelekezwa kwenye sheria ya Ardhi ya Mwaka 1999 lakini pia kuwasaidia mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana wa asilimia 4%  kwenye mapato ya halmashauri.

Mdoe alisema wanatoa ushauri kwa Halmashauri za Wilaya kwa kushirikiana na wadau wengine wa kilimo kuwawezesha vijana kupata elimu ya kilimo bora kupitia mafunzo ili kuongeza tija zaidi na kuachana na kilimo cha mazoea.

Akitoa ufafanuzi wa maswali mbalimbali ya wanahabari Mkuu wa Mradi huo wa APRA upande wa Tanzania Profesa Aida Isinika alisema vijana wengi wanapenda kilimo chenye tija na soko kama vile kilimo cha mpunga, vitunguu, nyanya na mazao mengine.

“ Vijana hawataki mazao ya muda mrefu maana sio wavumilivu sana wao wanahitaji matokeo ya muda mfupi ndio maana unaona wengi wanakimbilia mazao hayo ambayo wanatumia muda mfupi kupata fedha.” alisema Isinika.

Aidha Isinika alisema mitaji wanayohitaji vijana ni midogo midogo na sio mikubwa hivyo wakiwezeshwa kupata itawasaidia katika kufanya shughuli za kilimo kwa urahisi na kuongeza tija huku wakiboresha maisha yao.

Akizungumzia utoaji wa ajira katika mashamba hayo alisema kundi la wakulima wa kati ndio waliotoa ajira nyingi kwa vibarua ukilinganisha na wawekezaji wakubwa na kusema kuwepo kwa nishati ya umeme katika maeneo yalipo mashamba hayo kumechochea maendeleo. 

Wednesday, October 21, 2020

QUEEN SENDIGA: WATANZANIA NAOMBA RIDHAA URAIS 2020, SINTAWAANGUSHA

 

Mgombea Urais kupitia ADC, Queen Sendiga akihutubia mamia ya wananchi wa Singida Mjini, waliofika kumsikiliza kwenye uwanja wa stendi ya zamani jana.
Queen Sendiga akionyesha mfano wa Karatasi ya Kupigia Kura na sehemu kilipo chama chake na jina lake, ili kuwarahisishia wapiga kura kumtambua kirahisi na kumchagua ifikapo Oktoba 28 .
wa Singida mjini wakisikiliza Sera na Ilani ya ADC kupitia mgombea wake wa nafasi ya Rais.
Wananchi wakifuatilia mkutano huo wa Kampeni.
Queen Sendiga akizungumza kwenye mkutano huo.

Wananchi wakifuatilia mkutano huo wa Kampeni.
Mkutano ukiendelea.


Na Mwandishi Wetu, Singida

MGOMBEA Urais kupitia Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Madam Queen Sendiga, amesema anaomba ridhaa ya kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama Rais wa kwanza mwanamke, lengo hasa ni kutatua kero sugu hususani kwenye la afya, maji, elimu na ajira ambazo zimeshindwa kutatuliwa na mamlaka zilizopo kwa takribani miaka 59 tangu uhuru.  

Sendiga aliyasema hayo, wakati akinadi Sera na Ilani ya ADC kwenye mkutano wa Kampeni za kuwania nafasi ya Rais kwa mwaka 2020, alipohutubia mamia ya wananchi waliokusanyika viwanja vya stendi ya zamani mkoani hapa jana.

“Nimesukumwa kwa dhati ya moyo wangu kama mwanamke…na kama mama kulitumikia Taifa hili kwa nafasi ya Rais, kwa sababu CCM kwa miaka 59 tangu tupate Uhuru imeshindwa kufanya mageuzi stahiki kwa mtanzania katika muktadha wa kimaendeleo licha ya kujaliwa rasilimali zote muhimu,” alisema.

Alisema kitendo cha yeye kutokata tamaa, licha ya idadi ya wagombea hai wa kinyanganyiro cha nafasi ya Rais toka 15 mpaka kubakia wanne kwa sasa, ni dalili tosha na kiashiria cha wazi kwamba ana mapenzi ya dhati-na ya ‘kimama’ ya kutaka kulitumikia Taifa kwa upendo na matarajio chanya kwa kila mwananchi.

Akizungumzia sekta ya afya alisema suala la bima kwa kila mwananchi bila ya masharti yoyote halikwepeki, na kwamba nchi zote zilizoendelea zimewekeza na kutoa msukumo kwenye huduma za afya kwa kuamini kwamba huduma bora za afya ndio msingi wa ustawi wa afya ya raia kwa matokeo chanya ya mageuzi ya kiuchumi.

Aidha, katika elimu mwanamke huyo ambaye kama atapewa ridhaa na watanzania atakuwa Rais wa kwanza Mwanamke tangu Uhuru na wa 3 kwa Bara la Afrika, alisema anaamini maisha duni ni matokeo ya elimu duni.

“Elimu ni kila kitu, elimu ndio ufunguo wa maisha. Mtu akikunyima elimu bora ujue amekunyima maisha, tusisahau pia ndugu zangu elimu bora sambamba na maarifa yenye tija, ni matokeo chanya ya umahiri na ufanisi kwenye taaluma nyingine mbalimbali,” alisisitiza Sendiga.

Katika suala la elimu, alisema ADC kwanza watahakikisha wanatoa elimu bure kweli kweli, pia watajikita katika kutoa maarifa na sio kukaririsha kama ilivyo kwa sasa, na zaidi watabadili mtaala uliopo ili kumfanya mwanafunzi afundishwe ‘elimu maarifa’ kwa kuzingatia elimu bila maarifa ni kazi bure.

Hata hivyo, Sendiga akizungumzia suala la ajira, alisema mkakati wa chama hicho chini ya serikali yake ni kuhakikisha wanakwenda kuzalisha ajira milioni 10, kwa kuhakikisha wanatengeneza miundombinu rafiki kwenye sekta zote mtambuka, ikiwemo kilimo, uvuvi, elimu maarifa na nyinginezo.

“Chama chetu kitashughulikia kwa nguvu zote changamoto zote zilizopo sekta ya kilimo kwa kuhakikisha kunakuwepo na pembejeo za kutosha, masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima, maboresho ya miundombinu kwenye sekta mbalimbali vijijini, ikiwemo maji safi na salama, na ubora wa elimu,” alisema.

Katika kuthibitisha hali ya ukomavu wa kisiasa, uzalendo wa kipekee na nia yake ya dhati ya kuendelea kuwa miongoni mwa wapigania maslahi ya amani ya Tanzania, kama jina lake lilivyo maarufu “Mama wa Taifa” Sendiga aliwasihi wananchi kuhakikisha ifikapo Oktoba 28 wakichapiga kura ya kumchagua yeye na wabunge wa chama chake basi warudi nyumbani kusubiri matokeo.

“Ukipiga kura rudi nyumbani..tunza amani. Ukifanya vurugu yoyote utakamatwa na kushtakiwa kwa jinai kama mhalifu mwingine yeyote na utajikuta ukiishia kuozea jela. Hutahukumiwa kama mwanachama wa chama fulani bali kama mhalifu,” alionya Sendiga, ambaye Singida ni mkoa wake wa 16, tangu aanze kampeni hizo.

Sunday, October 18, 2020

SEKONDARI YA MKWESE MANYONI MKOANI SINGIDA KUANZA KUTOA ELIMU YA STADI ZA UFUNDI



Wahitimu wa Kidato cha  Nne wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Mkwese inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria mahafali ya 42  yaliyofanyika jana shuleni hapo.

Wahitimu Wasichana wa Kidato cha  Nne wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Mkwese inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja.

Wahitimu Wavulana wa Kidato cha  Nne wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Mkwese inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja.

Mwekezaji wa Shule ya Sekondari ya Bweni ya Mkwese inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Askofu Williams Yindi  akitoa dira ya shule hiyo katika mahafali ya 42 ya kidato cha Nne yaliyofanyika jana shuleni hapo wilayani Manyoni mkoani Singida.



Mchungaji Robert Paul wa Kanisa ka Pentekoste la Kijiji cha Mkwese akiomba kabla ya kuanza mahafali hayo.
Burudani ikitolewa na wahitimu hao.
Mkuu wa Shule hiyo, Hamisi Yindi akizungumza katika mahafali hayo.
Wahitimu wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wazazi, walezi, ndugu Jamaa na marafiki wa wahitimu hao wakiwa kwenye mahafali hayo.

Walimu wa shule  hiyo, wakiwa kwenye mahafali hayo. 
Wanafunzi wa kidato cha pili wakitoa burudani kwenye mahafali hayo.
Mahafali yakiendelea.
Viongozi wa dini wakiwa kwenye mahafali hayo.


Kaka Mkuu wa shule hiyo, Kelvine Alex (kushoto) na Dada Mkuu, Jacqueline Samson wakiwa kwenye mahafali hayo.
Wahitimu wakisoma risala. Kushoto ni Olivery Vedasto na Pili John.
Wahitimu hao wakionesha maonesho ya kisayansi jinsi ya kutumia adibini. Kutoka kushoto ni Elibariki Boniface, Grace Peter na Teryson Shillar.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Manyoni,  Robert Chalamaganza, akizungumza  kwenye mahafali hayo.
Vyeti vikitolewa.

Mzee Romani Kanyaulega kutoka Dodoma akitoa nasaha kwa wahitimu hao.

Mama Joyce Kisuda, akitoa nasaha kwa wahitimu hao.



Na Dotto Mwaibale, Manyoni.


SHULE ya Sekondari ya Bweni ya Mkwese inayomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Manyoni mkoani Singida inatarajia kuanza kutoa  elimu ya stadi za ufundi ifikapo Januari 2021.

Hayo yalisema jana na Mwekezaji wa shule hiyo,  Askofu Williams Yindi wakati akitoa dira ya shule hiyo katika mahafali ya 42 ya kidato cha Nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975 lakini tangu aanze kuiendesha yakiwa ni ya pili.

Alisema baada ya kufanya utafiti wa kutosha kwa kusoma nyakati amebaini kuwa wahitimu wa kidato cha nne cha sita na vyuo vikuu iwapo hawataweza kuyashika kwa akili zote yale wanayo fundishwa watajuta hasa katika kipindi hiki ambacho ni cha kizazi cha sayansi na teknolojia.

Alisema baada ya kufanya utafiti huo alibaini kuwa kuna mambo manne ambayo kijana aliyehitimu na kushindwa kuyashika vizuri masomo yake tangu mwanzo atakuwa katika changamoto kubwa katika safari yake ya maisha hivyo nguzo ya kwanza kwa vijana hao ni kuijua lugha ya kiingereza.

Alitaja nguzo ya pili ni kuwa vijana wapate elimu ya ufundi stadi kama uselemara, umeme, magari na kufundishwa stadi za michezo mbalimbali jambo litakalo saidia wahitimu hao wakiwa nyumbani kuwa na kitu cha kufanya baada ya kutoka shuleni.

Alisema tayari amekwisha wapata walimu wanne na januari mwakani wataanza rasmi kufundisha  masomo hayo.

Aliwataja walimu  ambao wataanza kufundisha kwa mkataba masomo hayo kuwa ni Mwalimu  Salum ambaye atafundisha lugha ya kiingereza ili wanafunzi hao waweze kuzungumza na kuandika, Mwalimu wa pili ni Gwamaka Chidodo ambaye ni mbobezi wa ufundi Selemara na watatu ni Mhandisi Godwin Gunda ambaye atafundisha ufundi magari na  Mwalimu wa nne ni Salumu Simba  yeye ni Mhandisi na mtaalamu wa masuala ya  umeme.

Yindi alisema  walimu hao ni wale waliostaafu toka serikalini na maeneo mengine na kuwa shule hiyo itaingia nao mkataba wa kufundisha shuleni hapo.

Alisema shule hiyo imejipanga vizuri kitaaluma kwani wanasafu nzuri ya walimu ambao wanapimwa kwa utendaji wao wa kazi ambapo aliwaondoa hofu wazazi na walezi  kutosita kuwapeleka watoto wao katika shule hiyo na wasitegemee kupokea vijana waliofeli.

Akizungumzia maendeleo ya shule hiyo tangu aanze kufanya uwekezaji alisema ameboresha miundombinu ya majengo, barabara, vyoo, madarasa, maji na umeme na kuwafanya wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha kuomba udhuru wa mara kwa mara kutoka nje ya shule.

"Ninasimamia taaluma kwa kuliangalia kwa macho manne kama mtaendelea kuniletea vijana wenu hapa wategemee kupata daraja la kwanza, la pili na la tatu na si vinginevyo." alisema Yindi.

Wahitimu hao katika risala yao kwa mgeni rasmi ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Manyoni,  Robert Chalamaganza walisema  shule hiyo chini ya mwekezaji huyo imekuwa na maendeleo mazuri kitaaluma kwani ameweza kusimamia kikamilifu suala la elimu tofauti na miaka ya nyuma, wameweza kufanya mitihani mbalimbali ndani na nje ya shule ikiwa ni pamoja na mitihani ya utimilifu ya wilaya na kimkoa.

Mail Delivery Subsystem