Saturday, November 21, 2020

USWIS WARIDHISHWA NA KAZI INAYOFANYWA NA TFCG NA MJUMITA KATIKA KUHIFADHI MISITU NCHINI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG ) Charles Meshack akifafanua jambo mbele ya Katibu Tawala  Msaidizi  wa Uchumi na Uzalishaji  wa Mkoa wa Iringa, Elia Luvanda na wadau wengine alipokuwa akieleza lengo la mradi na namna utakavyotekelezwa mkoani humo.
 Muwakilishi wa Balozi wa Uswis nchini Tanzania, Peter Selder ambaye ni Mkuu wa Kitengo  cha ajira na kipato akivishwa nguo ya jamii ya kimasai kama zawadi kwa kufadhili mradi huo.
Wajumbe wa kamati ya ushauri ya Mradi, Wanahabari, Viongozi wa kijiji na wana Kijiji wa Kijiji cha Mahenge wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo kwenye kijiji hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA). Rahma Njaidi  akizungumza na Wajumbe na kamati ya ushauri ya Mradi na wananchi wa Kijiji cha Mahenge Wilayani Kilolo Mkoani Iringa.
Muwakilishi wa Balozi wa Uswis nchini Tanzania bwana Peter Selder ambaye ni Mkuu wa Kitengo  cha ajira na kipato akizungumza na wana Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo alipotembelea kuona maendeleo ya kijiji hicho kipya katika awamu ya tatu ya Mradi alipoambatana wajumbe wa ushauri wa mradi.



Na Calvin  Gwabara, Morogoro.


UBALOZI wa Uswis nchini  kupitia Shirika lake la Maendeleo (SDC) umeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali na wadau wengine  katika uhifadhi shirikishi wa misitu ili kuitoa Tanzania kwenye nchi zinazoongoza kwa uharibifu wa misitu duniani.

Hayo yalisemwa na Muwakilishi wa Balozi wa Uswis nchini Tanzania, Peter Selder wakati wa ziara ya wajumbe wa bodi ya ushauri wa Mradi wa Uhifadhi shirikishi wa Misitu ya vijiji katika Kijiji cha Mahenge wilayani Kilolo mkoani Iringa kuona maendeleo na ushiriki wa wana kijiji katika jitihada hizo ili kilinda misitu na kunufaika na rasilimali zinazotokana na uhifadhi huo.

Selder alisema ameridhishwa mbinu inayotumiwa na  Shirika la Shirika la kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG)  na Mtandao wa jamii wa usimamizi wa Misitu (MJUMITA)  ya kuwajengea uwezo jamii, viongozi na wadau wengine jinsi ya kuilinda, kuihifadhi na kisha kunufaika na mazao ya misitu hiyo moja kwa moja kupitia shughuli mbalimbali.

“ Nimefurahi kuona namna jamii inavyoshiriki na kunufaika moja kwa moja na hii itasaidia sana kwani wanapata motisha ya moja kwa moja kwao binafsi na vijiji na hii inawafanya waone umuhimu wa kuitunza na kuilinda kwa ajili ya vizazi hivi na vizazi vijavyo, alisisitiza.

Aliongeza” Ufadhili tunaoutoa sisi ni mdogo sana lakini kazi kubwa na jukumu kubwa ni la jamii yenyewe na Serikali ya Tanzania ndio maana tunapendekeza mbinu hii nzuri itumike na isambae kwenye vijiji na wilaya nyingine nchi nzima”.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TFCG, Charles Meshack alisema katika kipindi cha miaka sita katika awamu ya kwanza na ya pili Shirika hilo la ushirikiano na maendeleo ya Uswis limetoa zaidi ya shilingi bilioni 12 na sasa awamu hii ya tatu wametoa kiasi cha shilingi bilioni 7 katika kutekeleza miradi Mradi huu awamu itakayoisha mwaka 2023.

Alisema katika awamu hii ya tatu ambayo imejikita katika kujengea uwezo Wilaya zingine kuanzisha usimamizi shirikishi wa Misitu wameongeza wilaya nne ili nazo ziweze kuambukiza wilaya zingine na hivyo kuwezesha mbinu hiyo kusambaa hatua kwa hatu hadi kufikia nchi nzima.

“Tanzania jumla ya hekta milioni 48.1 za misitu ambazo hekta milioni  22 sawa na asilimia 45% za misitu hiyo ipo chini ya ardhi za vijiji lakini iliyohifadhiwa chini ya usimamizi shirikishi wa misitu ni asilimia 5 wakati hekta milioni 17 na zisiposimiwa zinaweza kutoweka” alisema Meshack.

Naye Mkurugenzi wa Mtandao wa Jamii wa usimamizi wa Misitu Tanzania MJUMITA, Rahma Njaidi alisema misitu mingi inaangamia labda ni kwa sababu ya jamii kutojua  thamani na faida za misitu hiyo lakini anaamini baada ya muda mfupi kwa kutumia mbinu hiyo wataona faida na kisha kuwa askari wazuri katika kuilinda na kuitunza Kama ambavyo wanafanya wananchi wa Wilaya ya Kilosa wanaotekeleza mradi huo toka awamu ya kwanza.

“ Kuna vijiji vingi nchi hii ambavyo vina misitu ya miyombo lakini bahati hii imewaangukia nyinyi watu wa Kijiji cha Mahenge wilaya ya Kilolo, hii ni fursa kwenu kuhifadhi na kunufaika na matunda ya uhifadhi shirikishi wa misitu hivyo muwasikilize wataalamu ili muweze kufanikiwa kama wenzenu. “ alisema Njaidi.

Mradi wa Usimamizi shirikishi wa Misitu ya jamiii(USMJ) inatekeezwa chini ya Mradi wa kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) na mradi wa kuhifadhi Misitu kwa kuwezesha biashara endelevu ya Misitu (CoFOREAT) kwa ufadhili wa Shirika la  Maendeleo la Uswis (SDC).

Thursday, November 19, 2020

TARI ILIVYOJIPANGA KUAKISI MAONO YA RAIS MAGUFULI MAZAO YA MKAKATI

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Yohana Budeba akiangalia moja ya mti wa mkorosho uliozalishwa kwa mafanikio makubwa kutokana na mbegu bora zinazozalishwa na Taasisi hiyo kwenye shamba la Kilimo cha Pamoja (Block Farming) eneo la Masigati Wilaya ya Manyoni  jana. Budeba kwa kuongozana na wajumbe wa bodi hiyo walifanya ziara ya kukagua kazi zilizofanywa na taasisi hiyo, tija iliyopatikana na kufanya tathmini ya kuona kama kuna haja ya kufanya maboresho zaidi.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI nchini, Dkt Geofrey Mkamilo (aliyesimama) akizungumzia mambo kadhaa kuhusu ustawi wa zao la korosho nchini na namna taasisi hiyo ilivyojipanga kuinua tija ya zao hilo katika kuhakikisha malighafi yake inakwenda kutosheleza mahitaji kwenye uchumi wa viwanda, alipofanya ziara kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni kwa kuongozana na Bodi ya Taaasisi hiyo jana.

-Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) wakiwa na baadhi ya wadau na wakulima wa korosho kwenye shamba la Kilimo cha Pamoja, eneo la Masigati, Wilaya ya Manyoni jana, muda mfupi baada ya kukamilisha ziara yao.

Afisa Kilimo Wilaya ya Manyoni (DIACO), Fadhil Chimsala, akitoa maelezo mbele ya wajumbe wa Bodi ya TARI ya namna wanavyoshirikisha wadau mbalimbali (wakiwemo Jeshi la Magereza) katika kuzalisha miche ya mbegu bora zinatoka Kituo cha Utafiti TARI-Naliendele na kuzisambaza kwa wakulima wakati wa ziara ya wajumbe wa Bodi hiyo kwenye Gereza la Manyoni jana. 

Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Naliendele, Dkt Fortunatus Kapinga akitoa maelezo kwa wajumbe wa Bodi ya namna taasisi hiyo ilivyojipanga kuzalisha mbegu za korosho za kutosheleza mikoa yote ya Kanda ya Kati, sambamba na kuwaonyesha maandalizi ya awali na ukubwa wa shamba hilo la mfano lenye takribani ekari 30, lililopo Masigati, Manyoni jana.

- Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Naliendele, Dkt Fortunatus Kapinga akiendelea kutoa maelezo ya kitaalamu kuhusu mwendelezo na tija ya shamba hilo litakaloanza kuzalisha mbegu bora za korosho.

Ziara ikiendelea.
Ziara ikiendelea.
Wajumbe wakiendelea na ziara kuzunguka Block Farming hizo.
Ziara ikiendelea.
Vitalu vya miche inayotokana na mbegu zinazozalishwa na Kituo cha TARI Naliendele, kwenye Gereza la Wilaya ya Manyoni.

Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt Mkamilo akieleza namna Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo ilivyojipanga kuongeza tija ya zao la Korosho sambamba na kuchangia ustawi wa viwanda nchini.

Ziara ikiendelea.

Mkurugenzi wa Ward Holdings, Ukanda wa Afrika, Godfrey Simbeye akionyesha ubora wa kipekee wa ‘korosho karanga’ na ‘korosho bibo’ uliotokana mbegu zinazozalishwa na TARI kwenye ‘Block Farming’ za Masigati alipotembelea shamba hilo hivi karibuni.
 


Na Godwin Myovela, Singida


BODI ya Wakurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo nchini (TARI) imetoa wito kwa watafiti wake sambamba na wadau wa taasisi hiyo kuhakikisha wanaongeza kasi zaidi katika kuleta mapinduzi ya kilimo katika muktadha wa shabaha ya kuongeza malighafi ya kutosha kwenye ukuaji wa viwanda vya ndani, na kubadilisha kwa pamoja mfumo mzima wa kilimo kutoka kile cha kujikimu kwenda cha kibiashara

Mkurugenzi wa Bodi hiyo, Dkt Yohana Budeba aliyasema hayo eneo la Masigati, Wilaya ya Manyoni, mkoani hapa jana, eneo unapotekelezwa mradi wa ‘Kilimo cha Pamoja’ cha zao la Korosho, alipotembelea na kuangalia sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya bodi kwa taasisi yake

Budeba mbali ya kupongeza dhamiri ya dhati ya Rais John Magufuli katika mantiki ya kuinua tija ya kilimo nchini kupitia hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge la 12, aliwataka watafiti na wadau wengine wa kilimo kuunga mkono juhudi za serikali ili kuchagiza kasi ya mabadiliko hayo, sanjari na kusukuma ukuaji wa uchumi.

“Kwa mujibu wa Rais Magufuli serikali imedhamiria kuongeza juhudi ili kubadilisha kilimo cha Tanzania kuwa cha kibiashara. Hivyo ni jukumu letu watafiti na wakulima kwenda pamoja na dhamiri hiyo njema ili kuongeza tija,” alisema Budeba

Alisema katika kuhakikisha inasimamia utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na maelekezo ya serikali, Bodi yake imefarijika sana kuona maagizo iliyotoa ya kuhakikisha ugunduzi na teknolojia zote zinawafikia walengwa limezingatiwa na kutekelezwa mpaka sasa kikamilifu

Baadhi ya maagizo yaliyotolewa na bodi hiyo inayoundwa nawajumbe 12 kutoka taasisi na wadau mbalimbali na utekelezaji wake, ilikuwa ni kuitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo kuhakikisha inasambaza kwa kasi teknolojia zake hususani eneo la ugunduzi wa mbegu bora kwa tija ya mkulima na ustawi wa kilimo nchini-jambo ambalo limeendelea kutekelezwa kwa ukamilifu.

Agizo lingine lilikuwa ni kuitaka TARI kufanya tafiti yenye lengo la kupanua wigo wa kilimo cha zao la korosho kutoka mikoa 5 iliyokuwa ikilima zao hilo, jambo ambalo nalo limetekelezwa ipasavyo kwa taasisi hiyo mpaka sasa kufanikisha kwa tija uanzishwaji  wa kilimo cha zao hilo kwa mikoa takribani 20 ikiwemo Singida, ambayo alipongeza kwa kuendelea kufanya vizuri hususan kupitia shamba lake la masigati lenye takribani ekari elfu 22 zinazolimwa zao hilo kwa tija na mafanikio makubwa

Budeba aliwataka wadau wa sekta za umma na binafsi yakiwemo Majeshi na Amcos za kilimo kushirikiana na TARI katika kupanua wigo wa usambazaji wa teknolojia zake kwa kasi na tija ili ziweze kufikia idadi kubwa zaidi ya wakulima kwa haraka

“Kuona ni kuamini..nawasihi watanzania watembelee shamba hili la Masigati ili wajifunze teknolojia hizi tunazozizalisha. Pia tunakaribisha mashirikiano na sekta nyingine, mathalani Jeshi la Magereza wao wamekwishaanza, shabaha yetu ni kuzalisha kwa tija ili kuondokana na kilimo cha kujikimu,” alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI nchini, Dkt Geofrey Mkamilo, alisema hitaji la Taasisi hiyo kwa sasa ni kuona uzalishaji wa teknolojia zake, ubunifu na mbinu bora za kilimo zinakwenda sambamba na ukuaji wa viwanda-huku taasisi ikiahidi kuongeza juhudi katika kuhakikisha kiwango cha asilimia 60 za malighafi ya kilimo kwenye viwanda vya ndani na zaidi ya hapo inafikiwa ipasavyo.

Alisema pamoja na mambo mengine, shabaha iliyopo mbali ya kupanua wigo wa huduma za kiugani kwa kushirikiana na wadau, taasisi imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu za korosho ili kukidhi mahitaji ya mikoa yote 20 inayolima zao hilo, na stratejia iliyopo ni kuzalisha kutoka wastani wa tani takribani laki 3 zinazozalishwa kwa sasa kufikia tani milioni 1 ifikapo 2024.

“Maono ya Rais Magufuli ni kuona tija inaongezeka zaidi kupitia hasa mazao haya ya kimkakati likiwemo zao la korosho. Na katika hili tumejipanga vizuri kuhakikisha tunakwenda kuzalisha mabilionea wa kutosha kupitia takribani mazao yote 85 ikiwemo korosho tunayoshughulika nayo, lengo ni kumtoa mkulima kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kile cha kibiashara” alisema Mkamilo.

DK.MNDOLWA: UCHAGUZI UMEKWISHA TUVUNJE MAKUNDI TUFANYE KAZI NA KUKIJENGA CHAMA CHETU.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa (katikati), akizungumza na wanachama wa jumuiya hiyo na Wana CCM baada ya kuwasili jijini Arusha jana kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Kulia ni Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Arusha,  Hezron Mbise na kushoto ni Mbaraza wa jumuiya hiyo mkoani humo, Victor Mollel.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC),  Elishilia Kaaya, akizungumza katika mkutano huo.


Mkutano ukiendelea.
 Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa, akisalimiana na wanachma wa Jumuiya hiyo baada ya kuwasili jijini Arusha jana kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Salamu zikiendelea.
Mapokezi ya Dk.Mndolwa yakifanyika.

 Mkutano ukiendelea.



Na Mwandishi Wetu, Arusha


MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi  (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa amewataka wanajumuiya hiyo na wanaCCM Mkoa wa Arusha kuacha makundi na kufanya kazi baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Mndolwa alitoa ombi hilo jana wakati akizungumza na wana CCM hao katika ziara yake ya kikazi ya siku moja mkoani humo.

"Hivi sasa tumekwisha maliza uchaguzi tuyaache makundi tuliyokuwa nayo tuungane pamoja tuchape kazi na kukiimalisha chama chetu" alisema Mndolwa.

Mndolwa aliwaambia wana CCM hao kuwa mwisho wa uchaguzi ndio mwanzo wa uchaguzi mwingine hivyo wasibweteke bali waanze kujipanga kwa kutekeleza ilani ya uchaguzi ya 2020-2025 ili waje wapate ushindi mnono kama waliopata mwaka huu.

Aidha Mndolwa akizungumza na Baraza la Wazazi la Mkoa huo alisema kila mmoja wao anapaswa kuyajua majukumu yake jambo litakalosaidia kuijenga jumuiya hiyo.

Pamoja na mambo mengine Dk. Mndolwa alitumia nafasi hiyo kufundisha masuala ya utawala bora na kukagua miradi mbalimbali inayoendeshwa na jumuiya hiyo.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Arusha,  Hezron Mbise akizungumza wakati akimkaribisha Dk. Mndolwa alimuhakikishia kuitunza na kuendeleza miradi yote ya jumuiya hiyo ukiwepo wa mashine ya kufyatulia matofari uliopo Longido mkoani humo.


Wednesday, November 18, 2020

KIKWETE AKANUSHA KUUZA KIWANJA ALICHOPEWA SINGIDA- UVCCM YAJIPANGA KUREJESHA NYUMBA YA CCM

Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na Mzee Andrew (wa pili kulia) ambaye ni mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi wakati akifanyakazi mkoani Singida. Katikati ni mke wa Mzee Andrew. Wengine ni watoto wa Mheshimiwa Kikwete.
Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa na wajumbe wa kamati ya siasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida na wananchi waliojitokeza kumpokea alipowasili kwa ajili ya ziara ya siku moja ya kutembelea nyumba alizokuwa akiishi mkoani humo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha.
Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akipata maelezo katika ziara hiyo. Kulia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha.


Hii ni moja ya nyumba aliyowahi kuishi Mhe. Kikwete mkoani Singida.
Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Mulagiri. Kutoka kulia ni  Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha na Katibu wa Itikadi na Uenezi  na Itikadi wa Chama cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Singida Ahmed Kaburu.


Rais mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akisalimiana Mzee Andrew ambaye ni mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi wakati akifanyakazi mkoani Singida.


 Na Mwandishi Wetu, Singida


RAIS mstaafu wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekanusha taarifa zilizopo Mkoani Singida kwamba kiwanja alichopewa kwa ajili ya makazi amekiuza kwa moja ya waumini wa makanisa yaliyopo mjini Singida.

Dkt. Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti mstaafu wa CCM Taifa, alitoa kauli hiyo mjini Singida alipokuwa katika ziara yake ya siku moja ya kutembelea na kukagua nyumba alizowahi kuishi zaidi ya miaka 40 iliyopita wakati akiwa mtumishi wa chama cha TANU.

Alifafanua kiongozi huyo mstaafu kwamba mwaka 1975 akiwa Katibu Msaidizi wa Chama Cha TANU aliishi katika nyumba tano tofauti tofauti kabla na baada ya kwenda jeshini kwa hali hiyo anazifahamu kikamilifu mali za chama mkoani Singida zilipo.

“Kiwanja changu sijampa mtu yeyote yule kama wamechukua kanisa waulizeni,kama ni kiwanja changu waulize,kama ni kiwanja changu tulipatana wapi mimi na wao? alihoji raisi huyo mstaafu.

Akizungumzia moja ya nyumba alizowahi kuishi wakati akiwa mtumishi wa chama katika kipindi hicho,Dkt. Kikwete alisisitiza kwamba nyumba ile alikuwa akiishi baada ya kurejea kutoka jeshini. 

Kwa upande wake Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Ahmed Kaburu alisema baada ya kupokea maelekezo kutoka kwa rais na mwenyekiti mstaafu wa CCM, Dkt Jakaya Kikwete watayafuatilia ili waweze kujua ukweli kuhusu kiwanja alichokuwa amepewa kiongozi huyo mkuu ya nchi.

“Tumepokea maelekezo na tutayafuatilia na kwa bahati nzuri na kamisaa wetu DC alikuwepo anasikia kwamba kuna kiwanja cha Mheshimiwa rais mstaafu Jakaya Kikwete eneo la Somoku tutafuatilie vile vile hapo alipokuwa akikaa zamani ambako amesema ilikuwa nyumba ya TANU tutaifuatilia na tutatoia matokeo yake.”alisisitiza Kaburu.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Dk. Denis Nyiraha amemuhakikishia Mwenyekiti huyo mstaafu wa chama hicho Dkt.Jakaya Kikwete kuwa kwa kushirikiana na viongozi wa CCM wa mkoa huo watahakikisha moja ya nyumba mali ya TANU aliyokuwa akiishi wakati akifanyakazi mkoani hapa umiliki wake unarudishwa kwenye CCM kwani hivi sasa anaishi mfanyabiashara mmoja.

"Sisi kama vijana wa CCM kwa kushirikiana na viongozi wetu tutafanya uchunguzi ili kujua mfanyabiashara huyo alipateje nyumba hiyo iliyokuwa mali ya TANU na sasa CCM" alisema Nyiraha.

TFCG na MJUMITA WACHOCHEA KUWEPO USAWA WA KIJINSIA KATIKA JAMII KWENYE UHIFADHI SHIRIKISHI WA MISITU

Rasi wa Ndaki ya Misitu Wanyamapori na Utalii  SUA, Prof. Suzan Augustino akiwasilisha matokeo ya utafiti huo wa masuala ya kijinsia kwa wadau wa uhifadhi shirikishi wa misitu  nchini.
Prof. John Jackoniah ambaye ni mmoja wa watafiti kutoka Ndaki ya sayansi za jamii na Insia ya Chuo kikuu cha sokoine cha kilimo SUA  akiwasilisha sehemu ya utafiti huo wa mbele wa wadau hao wa misitu mjini Morogoro.
Mkurugenzi msaidizi wa Shirika la TFCG bwana Emmanuel Lyimo akieleza malengo ya utafiti huo uliofanywa na watafiti kutoka SUA kabla ya kuanza rasmi kusikiliza matokeo hayo ya utafiti.
Baadhi ya wadau kutoka TFCG,MJUMITA, Wizara ya Maliasili na utalii,Waandishi wa habari na maafisa Misitu kutoka halmashauri za wilaya wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo.
Baadhi ya wadau kutoka TFCG,MJUMITA, Wizara ya Maliasili na utalii,Waandishi wa habari na maafisa Misitu kutoka halmashauri za wilaya wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo.
Baadhi ya wadau kutoka TFCG,MJUMITA, Wizara ya Maliasili na utalii,Waandishi wa habari na maafisa Misitu kutoka halmashauri za wilaya wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo.
Baadhi ya wadau kutoka TFCG,MJUMITA, Wizara ya Maliasili na utalii,Waandishi wa habari na maafisa Misitu kutoka halmashauri za wilaya wakifuatilia uwasilishwaji wa matokeo hayo.


Na Calvin Edward Gwabara, Morogoro


UTAFITI uliyofanywa na Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) umebainisha kuwa usawa wa kijinsia unaimarika na kuzingatiwa sana kwenye vijiji vinavyoshiriki miradi ya uhifadhi shirikishi wa Misitu kupitia Shirika la kuhifadhi Misitu ya asili Tanzania -TFCG.

Hayo yamebainika na Rasi wa Ndaki ya Misitu, Wanyama pori na utalii Profesa. Suzan Augustino  wakati wa  uwasilishwaji wa matokeo ya utafiti mbele ya wadau wa misitu mjini Morogoro na kusema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na TFCG na Mtandao wa Jamii wa usimaizi wa Misitu Tanzania MJUMITA kwa kuhakikisha jamii yote inashirikishwa na inanufaika na rasilimali zitokanazo na misitu hiyo.

“ Kuna mabadiliko makubwa chanya kwenye vijiji ambavyo TFCG na MJUMITA wanatekeleza miradi yao hasa wa mkaa endelevu ikilinganishwa na vijiji vilivyo nje ya mradi ingawa wanaume wanaongoza kwenye kazi zinazohitaji nguvu” alibainisha Prof. Suzan.

Prof. Suzan alisema kuwa kwenye Mradi wa Mkaa Endelevu wanawake wanakuja juu katika kushiriki kwenye biashara hiyo ijapokuwa wao wanatumia fedha kulipa watu kufanya kazi zao kama vile kukata magogo, kuyakusanya na kupanga tanuri la mkaa kazi ambazo zinaonekana kuhitaji nguvu zaidi.

Aidha Suzan alisema kuwa baadhi ya vijiji vina ushiriki mdogo wa wanawake na hiyo kwa mujibu wa utafiti wao wamesema inasababishwa mila na  destuli Zao kwamba kazi za maporini hufanywa na wanaume tu na sio wanawake ingawa mitazamo hiyo imeanza kufutika taratibu baada ya jitihada za TFCG na MJUMITA za kutoa elimu.

Prof. Suzan alisema watu wengi wanajua usawa wa kijinsia kwenye ngazi za maamuzi ni kuwa na idadi sawa ya wanawake, wanaume na Makundi mengine lakini ukweli ni kwamba kinachotakiwa kuangaliwa ni nani kawakikisha kundi gani na sauti ya like na mchango wake kwenye kufanya maamuzi maana wanaweza kuwa idadi sawa lakini wote hawana sauti.

Kwa upande wake Prof. John Jackoniah Mtafiti kutoka Ndaki ya Sayansi za jamii na Insia - SUA alisema pamoja na mafanikio hayo ya kuongeza uwiano wa kijinsia kwenye jitihada za usimamizi shirikishi wa Misitu na matumizi ya mapato ya rasilimali hizo lakini wanaume ndio wameonekana kunufaika zaidi.

Alisema kupitia utafiti huo walioufanya kwenye vijiji 10 katika Wilaya za Kilosa, Mvonero na Morogoro wanaume ndio wameonekana kuwa na sauti zaidi kwenye maamuzi na hata kwenye kugawana rasilimali za misitu kwenye maeneo hayo.

“ Lakini utaona wanawake walioolewa ndio wasio na sauti zaidi lakini wale ambao hawajaolewa au waliopewa talaka wananufaika Kama wanaume na Pia wana sauti kwenye kutoa maamuzi na kwenye kugawana mapato ya rasilimali za Misitu” alifafanua Prof. Jackoniah.

Alisema kuwa ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za kibiashara za rasilimali za Misitu umeongeza mzigo kwa wanawake kwakuwa kazi za nyumbani nazo zinawaangalia kwakuwa mgawanyo wa majukumu ya nyumbani haujabadilika umebaki palepale.

Akieleza lengo la Utafiti huo Mkurugenzi Msaidizi wa TFCG, Emmanuel Lyimo alisema masuala ya kijinsia yametengenezewa mkakati mahususi wa kuhakikisha yanazingatiwa kikamilifu kwakuwa ni swala mtambuka kwenye maendeleo.

Alisema baada ya kutekeleza Mradi kwa muda sasa wameona wafanye Utafiti huo ili kuona namna maswala hayo yanavyozingatiwa na kutafuta njia za kuboresha zaidi kama kuna vitu Vinakosekana kupitia mapendekezo ya watafiti hao kutoka SUA.

DK.MNDOLWA AUNGURUMA MKOANI KILIMANJARO KATIKA ZIARA YAKE YA KIKAZI

    Mwenyekiti wa  Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa, akisaini kitabu cha wageni baada ya kuwasili mkoani Kilimanjaro jana kwa ziara ya kikazi ya siku moja. Kulia ni Mwenyekiti wa  Jumuiya hiyo, mkoa humo, Daudi Mrindoko.

 Mwenyekiti wa  Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa, akisalimiana na wanajumuhiya hiyo wa Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kuwasili katika ziara ya kikazi.
Salamu zikiendelea.
Mapokezi yakifanyika.
Salamu zikiendelea.



Na Mwandishi Wetu, Kilimanjaro

MWENYEKITI wa  Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dk.Edmund Mndolwa, jana aliendelea na ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro kwa na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Wazazi la mkoa huo.

Mndolwa aliwapongeza wanachama na viongozi wa jumuiya hiyo kwa ushiriki wao kikamilifu katika kampeni za uchaguzi wa mwaka huu zilizoleta matokeo chanya kwa mkoa huo na kuibuka na ushindi wa kishindo kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge na Madiwani.

Pia aliwasihi watendaji wa jumuiya hiyo kuendelea kufanya kazi na kuisemea jumuiya  kwa ushirikiano mkubwa na CCM.

"Nawapongeza watendaji wa Jumuiya ya Wazazi kwa kazi kubwa mnayoifanya katika kuitetea na kuipaisha jumuiya yetu, ninafahamu changamoto ni nyingi ila endeleeni kupambana;

"Pia nitoe wito kwenu wakuu wa Shule za Sekondari za Jumuiya ya Wazazi kote nchini kuhakikisha walau kila mkoa mchague katika hizo shule mojawapo iwe inafundisha masomo ya sayansi tu, lengo kuisaidia serikali na jamii yetu kupata madaktari na wataalamu wa masuala ya sayansi hata kuongeza walimu wa masomo ya sayansi" alisema Dk.Mndolwa.

Akizungumza kwa niaba ya Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Daudi Mrindoko, alimshukuru Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Dk.Mndolwa, kwa ziara hiyo inayotoa Dira ya wapi jumuiya hiyo inatakiwa ielekee katika kusaidia jamii kote nchini. 

Monday, November 16, 2020

CAMFED YATOA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA WASICHANA SINGIDA

Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Singida, Yasinta Alute akifungua mafunzo ya elimu ya utambuzi juu ya mambo mbalimbali kwa wasichana yanayofadhiliwa na CAMFED, ikiwemo uelewa ya afya ya uzazi, UKIMWI, Ujasiriamali na namna ya kubaini fursa zinazozunguka jamii na njia bora ya kuzifikia mkoani Singida jana. Kulia ni Mjumbe wa shirika hilo Paschal Kichambati, Mkuu wa Miradi Nasikiwa Mwalisu na Mwenyekiti wa CDC Manispaa ya Singida, Omary Kisuda.

- Mkuu wa Miradi Nasikiwa Mwalisu akitoa mada kwenye mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa CDC Manispaa ya Singida, Omary Kisuda akizungumza.
Washiriki kutoka Wilaya za Manyoni na Singida Manispaa wakifuatilia mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Mafunzo yakiendelea.

Mafunzo yakiendelea.

Mwenyekiti wa CAMA wilaya ya Manyoni, Bahati Ismaili akiwasilisha mada kwenye mafunzo hayo.

Mafunzo yakiendelea.

Mafunzo yakiendelea.

Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
 



Na Godwin Myovela, Singida

SHIRIKA lisilo la kiserikali la CAMFED limewataka wasichana mkoani hapa kutobweteka, na badala yake kutazama fursa zinazowazunguka na kuzigeuza kuwa chanzo cha kuinua kipato katika muktadha chanya wa kuibadili jamii kimaendeleo.

Imeelezwa stratejia mojawapo itakayowasaidia wasichana hususani wale waliojifungua katika umri mdogo -ni kuwawezesha kwa kuwajengea pamoja na mambo mengine, misingi ya kutambua haki ya wao kupata elimu juu ya afya ya uzazi na UKIMWI.

Akizungumza mkoani hapa wakati wa mafunzo hayo ya kuwawezesha kujitambua, sambamba na kutambua fursa mbalimbali zinazowazunguka nje ya mfumo rasmi wa elimu, Mkuu wa Miradi kutoka Camfed, Nasikiwa Mwalisu alisema kama mtoto wa kike akijilinda na kuwa na utambuzi wa magonjwa basi atakuwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa na kutimiza ndoto zake za maisha.

“Kundi hili kama lisipoangaliwa kwa makini na kupewa elimu hii ya utambuzi juu ya mambo mbalimbali, ikiwemo elimu ya uzazi na kujikinga na magonjwa linaweza kupoteza mwelekeo, ambao madhara yake huwa ni makubwa...lakini pia athari zake husambaa kwa jamii na taifa kwa ujumla,” alisema Mwalisu.

Aidha, kuhusu sera ya ulinzi na usalama wa mtoto, Mwalisu alisema jamii inapaswa kutambua na kuheshimu takwa hilo la msingi la mtoto kupata elimu, kuheshimiwa, kupendwa na kulindwa kama haki ya msingi na sio hiari, lengo hasa ni kujenga ustawi na taswira chanya ya ukuaji wake kisaikolojia na kiafya.

Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Yasinta Alute alisema afya njema ni matokeo ya kila kitu katika maisha na ustawi wa ukuaji wa mtoto. Alisisitiza kama rika hilo la mtoto wa kile likipatiwa mafunzo ya mara kwa mara juu ya utambuzi kwenye nyanja mbalimbali- mfano wa hayo yanayowezeshwa na ‘Camfed’  ni dhahiri litageuka chachu katika kuleta maendeleo kwenye jamii.

“Ukipata mafunzo ya afya ya uzazi na ukajitambua huwezi kukosea wala kurudia tena makosa…nawaomba ninyi mliobahatika kupata mafunzo hayo mkawe chachu na mabalozi kwa wengine,” alisema Alute huku akiwaomba Camfed Makao Makuu kuangalia namna ya kupanua wigo wa huduma zao kwenye wilaya nyingine mkoani hapa ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika.

Awali, Afisa Elimu Sekondari na Mwenyekiti wa Kamati ya Wilaya ya Camfed Manispaa ya Singida, Omary Kisuda, alisema jumla ya wasichana 60 kutoka Singida Manispaa na wilaya ya Manyoni wanaendelea kupewa mafunzo kupitia programu ya elimu ya utambuzi kwa mtoto wa kike yaani ‘Tanzania Campaign for Female Education’

“Hili ni rika la wao kujiendeleza kielimu, biashara, ujasiriamali, na elimu ya afya ya uzazi na ndio sababu hasa ya kuwakutanisha na kuwapa mafunzo haya muhimu ya utambuzi chini ya ufadhili wa Camfed na Serikali,” alisema Kisuda.