Thursday, December 17, 2020

RC NCHIMBI: WAZAZI MSIWE MBALI NA VIJANA KIPINDI HIKI BAADA YA MITIHANI

Kaimu Afisa Vijana wa Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akihutubia mahafali ya 10 ya Shule ya Sekondari Utaho iliyopo wilaya ya Ikungi, mkoani Singida jana.



Mwonekano wa kisima hicho ambacho hakijaanza kufanya kazi kutokana na kukosa mabomba ya kusambazia maji
Mkuu wa shule ya Sekondari Utaho, Mwavita Malagila, akizungumza kwenye mahafali hayo.

Wanafunzi wakiingia kwenye viwanja vya shule hiyo kabla ya kuanza mahafali hayo

Maandamano kuelekea kwenye viwanja kabla ya kuanza kwa sherehe za mahafali hayo. Kulia ni Mkuu wa shule ya Sekondari Utaho, Mwavita Malagila

Meza kuu ikishiriki kuimba wimbo wa Taifa

Wanafunzi wakiimba wimbo wa uzalendo kabla ya mahafali hayo

Wahitimu wakiingia kwenye viwanja vya shule hiyo kabla ya kuanza mahafali hayo.

Ndahani akikagua moja ya visima vilivyochimbwa kwa umahiri mkubwa ndani ya shamba la mwekezaji huyo kwa lengo la kusaidia upatikanaji wa maji kwa jamii inayozunguka maeneo hayo.

Embe zilizotokana na shamba hilo lililopo eneo la Utaho

Mwenyekiti wa Bodi ya shule ya sekondari Utaho, Idd Siph, (kushoto) akimwelekeza jambo mgeni rasmi wa mahafali ya 10 ya shule hiyo Frederick Ndahani (wa pili kulia). Wengine ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Utaho ‘A’ Shaban Daghau, Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Utaho, Yasini Juma, Mwenyekiti wa Kijiji cha Utaho ‘B’ Omari Chima, na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Samamba iliyojengwa kwa nguvu ya wananchi, Japhet Pwiti. 

Sherehe za mahafali hayo zikiendelea.

Ndahani akikagua shamba bora la zao la embe ambalo limelimwa kwa tija kubwa na kuonyesha matokeo makubwa ndani ya muda mfupi, kulia ni mwekezaji mzawa wa shamba hilo, Aqlan Gharib maarufu Turu Best, eneo la Utaho, Ikungi, Singida

Mwonekano wa shamba hilo ambalo kama litatumika kama shamba darasa kwa makundi rika mbalimbali ndani ya jamii litainua tija ya kilimo ndani ya mkoa wa Singida.



Na Godwin Myovela, Singida 


WITO umetolewa kwa wazazi na walezi wote nchini kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika kuwapa uangalizi wa karibu vijana wanaomaliza kidato cha nne ili kuwanusuru kutumbukia kwenye majanga yanayoweza kuhatarisha mustakabali mzuri wa ndoto zao. 

Akihutubia sherehe za mahafali ya 10 ya Shule ya Sekondari Utaho, iliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani hapa jana, Kaimu Afisa Vijana mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Dkt Rehema Nchimbi, alisema ni jukumu la mzazi kupokea kijiti kile kile cha mwendelezo wa maadili mema kutoka kwa walimu wao, pindi vijana wawapo majumbani. 

"Wazazi msiwe mbali na vijana hawa, tushirikiane kuhakikisha kile walichojifunza shuleni hata wakiwa nyumbani wanaendelea kukiishi katika misingi ya uzalendo," alisema Ndahani.

Alisema mustakabali chanya wa maendeleo ya Tanzania katika muktadha wa ustawi wa kiuchumi, amani na usalama wa nchi upo mikononi mwa vijana hao, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwatupia jicho la karibu katika kipindi hiki wanapoandaliwa kimasomo. 

Pamoja na mambo mengine, aliwasisitiza wazazi katika kipindi hiki kuwa makini dhidi ya genge baya la wasafirishaji haramu wa binadamu wanaopita-pita kuwarubuni vijana, hususani watoto wa kike mkoani hapa kwa kigezo cha kwenda kuwatafutia ajira zenye maslahi makubwa jambo ambalo sio la kweli. 

“Katika hili wazazi tuchukue tahadhari kubwa…hali siyo ya kuridhisha kutokana na mabinti wengi kuendelea kusafirishwa nje ya nchi kwa siri, kwa ahadi za kutafutiwa ajira zenye mshahara mnono jambo ambalo sio kweli, na kinyume chake hugeuzwa watumwa kwa kufanyishwa biashara za ngono na madawa ya kulevya kwa maslahi ya waliowasafirisha” alisema Ndahani. 

Aidha, akitoa salamu za Mkuu wa Mkoa Nchimbi kwa vijana hao, Ndahani alisema Rais John Magufuli anaipenda sana Singida, na ndio maana hivi karibuni amekabidhi shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa sekondari hiyo ya Utaho. 

Alisema juhudi za kukabiliana na changamoto nyingine zilizopo, ikiwemo uhaba wa nyumba za walimu na maabara vitaendelea kuzingatiwa na kushughulikiwa ipasavyo, ili kuhakikisha Utaho naendelea kuwa kitovu cha elimu ndani ya mkoa. 

Awali, Ndahani akiwa kwenye eneo hilo la Utaho, alipata fursa ya kutembelea na kukagua mradi wa aina yake wa shamba bora la zao la embe linalomilikiwa na mwekezaji mzawa, Aqlan Gharib maarufu "Turu Best" na aliwasihi wana-singida kwenda kujifunza teknolojia za kilimo hicho chenye tija kwa ustawi wa lishe na ongezeko la kipato.

Mail Delivery Subsystem

MTATURU ATOA MSAADA WA VIFAA VYA UJENZI ASHIRIKI UJENZI WA SHULE YA MSINGI MBWANJIKI.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akishiriki uchimbaji wa msingi wa Shule ya Msingi ya Mbwanjiki  ambapo pia alitoa  msaada wa vifaa vya ujenzi.

Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akikabidhi mifuko ya saruji,
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akiwa na wananchi wakati wa utoaji wa msaada huo.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akisshhiriiki kubeba ma4ofari.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akikabidhi saruji na mabati.
Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu akikagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi ya Mbwanjiki.


Na Dotto Mwaibale, Ikungi


MBUNGE wa Jimbo la Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameshiriki shughuli za maendeleo katika Jimbo hilo ikiwemo utoaji wa msaada wa vifaa vya ujenzi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akishiriki ujenzi huo alisema ameanza kwa  kuchimba msingi,kusogeza tofali na kukabidhi mifuko 30 ya saruji katika Shule ya Msingi ya Mbwanjiki ili kuendeleza ujenzi huo uliokwama kwa takribani miaka 30.

"Kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kutaondoa changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu na msongamano katika shule wanazosoma za Ikungi,Ighuka na Matongo". alisema Mtaturu.

Mtaturu alitumia nafasi hiyo kuwapongeza walimu kwa jitihada zao za kufundisha watoto na kuwaomba wazazi kuendelea kushirikiana na walimu ili kuongeza ufaulu.

“Najua walimu wetu mnapambana ili kuhakikisha watoto wetu wanafaulu na shule yetu inakuwa katika nafasi nzuri,niwatie moyo kuwa nipo pamoja na ninyi, nimejivika joho la kuwa champion wa elimu katika jimbo hili,ahadi hii nitaitekeleza kwa vitendo.”alisema.Mtaturu 

mbali na kutembelea shule hiyo pia alifanikiwa kufika Shule ya Msingi Minyinga kuangalia athari ya mvua zilizoezua paa za madarasa na kuchangia saruji mifuko 20 ,bati 30 na matofali 500.

Akitoa msaada huo Mtaturu ameziomba kamati za shule kuweka mkazo kwenye lishe mashuleni ili kuwafanya watoto wawe watulivu na kuzingatia masomo ikiwa ni jitihada za kukuza taaluma.

Aidha Mtaturu aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli  kwa kuendelea kutoa elimu bila malipo na kuleta fedha za miradi ya maendeleo ikiwemo miundombinu katika shule za msingi na sekondari.

 Alisema kazi hiyo kubwa inayofanywa na Serikali iwe chachu katika kuhakikisha kila mmoja anatimiza jukumu lake ili lengo la Rais Magufuli liweze kufikiwa.

Kwa upande wao Diwani wa Kata ya Ikungi Abely Nkuwi na wa Kata ya Makiungu John Mathias wameunga mkono jitihada za mbunge na kuchangia tofali 200 huku diwani wa viti maalum Zainab Ntui akichangia sh  100,000.

Ziara ya mbunge huyo imemfikisha pia katika ujenzi wa daraja lililopo Kata ya Ntuntu linalojengwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura ) ambalo litasaidia kuondoa kero ya kukatika kwa mawasiliano pindi mvua inaponyesha.

Daraja hilo linajengwa kwa gharama ya zaidi ya sh. milioni 90, madaraja madogo pamoja na matengenezo ya barabara ya Mungaa -Ntuntu hadi Mang'onyi ambapo shughuli zote hizo zinagharimu zaidi ya  sh. milioni 142.

Wednesday, December 16, 2020

WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI YAJA NA MIPANGO SABA YENYE TIJA

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Kejeri Gillah akizungumza katika kikao kazi cha washauri wa mifugo mikoa na wataalamu wa wizara katika kutekeleza mikakati ya sekta ya mifugo kuendana na llani ya Chama Tawala mkoani Singida leo. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mbaraka Stambuli na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Deogratius Yinza. 

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Deogratius Yinza (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi akifungua kikao kazi hicho. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI) Mhandisi Enock Nyanda na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Kejeri Gillah.

Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI) Mhandisi Enock Nyanda, akizungumza katika kikao kazi hicho. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Dkt. Stanford Ndibalema.
Afisa Mifugo Mkuu, Idara ya Uzalishaji wa Mifugo na Uvuvi, Mariam Mkachila akiwasilisha mada katika kikao hicho.
Viongozi wakiwa meza kuu.
Kikao kikiendelea.

Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.

Kikao kikiendelea.
Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mbaraka Stambuli akitoa mada katika kikao kazi hicho.
Afisa Mifugo Mkoa wa Pwani, Elisante Qadwe akiuliza swali katika kikao hicho.
Daktari wa Mifugo Mkoa wa Morogoro, Gasper Msimbe, akiuliza swali katika kikao hicho. Kushoto ni Daktari wa Mifugo kutoka Mkoa wa Mtwara, Subira Simbeye.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Uratibu wa Sekta, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (ORTAMISEMI) Mhandisi Enock Nyanda, akiongoza kikao hicho, Kulia ni Afisa Utafiti wa Mifugo, Grace Masolwa.
Afisa Mifugo Mkoa wa Mara, Denis Ishengoma, akisisitiza jambo kwenye kikao hicho,
 

 


Na Dotto Mwaibale, Singida 


WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imekuja na mipango saba yenye lengo la kuboresha tija ya uzalishaji wa mifugo hapa nchini. 

Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Utafiti, Mafunzo na Ugani Dkt. Kejeri Gillah wakati akizungumza katika  kikao kazi cha washauri wa mifugo mikoa na wataalamu wa wizara katika kutekeleza mikakati ya sekta ya mifugo kuendana na llani ya Chama Tawala mkoani Singida leo. 

Alisema katika mwaka wa fedha 2018/2019, wizara imeandaa na kuanza kutekeleza mikakati saba ili kuendeleza sekta ya mifugo nchini. utekelezaji wa mikakati hiyo utaisadia Wizara kufikia dira na maono iliyojiwekea tangu awali kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Mifugo ya 2006. 

Gillah alitaja malengo ya mikakati hiyo ni kuongeza uzalishaji na tija, kudhibiti utoroshaji na biashara haramu za mifugo na mazao yake, kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na mifugo na mazao yake ili Sekta iweze kuchangia kikamilifu kwenye pato la Taifa, kuepusha migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, kulinda raslimali za mifugo zilizopo na kuhifadhi mazingira. 

Dkt. Gillah alitaja mikakati inayotekelezwa na wizara hiyo kuwa ni kuboresha kosaafu za ng’ombe nchini, kudhibiti magonjwa na matumizi ya dawa, chanjo na viuatilifu vya wanyama nchini, kutafutia ufumbuzi wa kudumu migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji kwa mifugo, kuanzisha na kuwezesha ushirika wa wafugaji, kudhibiti upotevu wa mapato yatokanayo na biashara ya mifugo na mazao yake  na kuboresha uzalishaji na biashara ya ndege wafugwao nchini. 

Alisema tangu kuanza kwa utekelezaji wa mikakati hiyo katika maeneo mbalimbali nchini, wataalamu wa Wizara wanaosimamia utekelezaji wa mikakati hii wamebaini uwepo wa elimu duni ya ufugaji bora na wa kibiashara kwa wafugaji walio wengi, hususan wenye mifugo mingi na wanaohamahama na mifugo yao. 

Awali akifungua kikao kazi hicho Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Deogratius Yinza alisema Sekta ya mifugo ni miongoni mwa Sekta za kiuchumi ambayo ni muhimu katika kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa Taifa kwa ujumla. 

"Sekta hii inachangia katika kuwapatia wananchi ajira, chakula, lishe, kipato na fedha za kigeni: Katika Mwaka 2019/2020 Sekta hii imechangia asilimia 7.4 katika pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 7.2 ya mwaka 2018/2019 na kuwa Sekta hii imekua kwa asilimia 5 kwa mwaka 2019/2020 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2018/2019 na kuwa hiyo imetokana na juhudi zenu maafisa midugo, wafugaji na wadau wengine katika kufanya kazi kwa bidii ili kuzalisha kwa tija. 

Alisema nchi yetu ina rasilimali ya mifugo ambayo Wizara inasimamia na kwa sasa inakadiriwa kufika ng'ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, kondoo milioni 5.65, kuku wa asili milioni 38.77, kuku wa kisasa milioni 44.51, nguruwe milioni 2.14 na punda wapatao  657,389.

WAZIRI DK. DOROTH GWAJIMA AONGOZA KUAGA MIILI YA WATU WALIOKUFA KWENYE AJALI SINGIDA

 

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima (mbele) akitoa heshima za mwisho mbele ya majeneza yenye miili ya watu 15 waliofariki dunia baada ya Hiace waliokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Itigi kwenye harusi kugongana uso kwa uso na lori la mafuta Kijiji cha Mkiwa mkoani Singida. Miili mitatu kati ya hiyo ni abiria walioomba msaada kutokea Ikungi kwenda Manyoni kwa shughuli za msiba.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima, (katikati) akimfariji Heri Mkama manusura wa ajali iliyosababishwa na basi dogo la abiria (Hiace) baada ya kugongana uso kwa uso na lori la mafuta eneo la Kijiji cha Mkiwa mkoani Singida. Mkama ambaye ni Bwana harusi mtarajiwa alipata ajali hiyo wakati akiwa na ndugu zake 13 waliokuwa wakimsindikiza kutoka Mwanza kwenda Itigi kwa ajili ya kuoa, hata hivyo kati ya ndugu hao 12 walipoteza maisha kupitia ajali hiyo. 

Dkt.Suleiman Muttani wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida akimuelekeza jambo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dkt.Doroth Gwajima wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuwafariji majeruhi wa ajali hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alitoa salamu za pole na faraja kutoka kwa Rais John Magufuli kwa wote walioguswa na msiba huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akitoa salamu za rambirambi wakati wa kuaga miili hiyo.

Mmoja wa wafiwa wa ajali hiyo akitoa shukurani kwa Serikali na wananchi kwa msaada waliotoa wakati wa ajali hiyo.
Makatibu Tawala wa Mkoa wa Singida wakiwa katika shughuli ya kuaga miili hiyo. Kutoka kushoto ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Deogratius Yinza,, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto na Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Hassan Ngoma.
Katibu wa Barraza Kuu la Waislam 4anzania (BAKWATA) Sheikh Buruan Mlau akitoa salamu za rambirambi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ASP) Sweetbert Njewike akielezea ajali hiyo na hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi.
Mchungaji Michael Mgandila wa Kanisa la Moravian akiomba wakati wa kuaga miili hiyo.
Sheikh wa Wilaya ya Singida, Iddi Simba akiomba dua wakati wa kuaga miili hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskas Mulagiri akielezea utaratibu waka4i wa kuaga miili hiyo.
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk.Doroth Gwajima (wa pili kulia akiangalia eneo ilipotokea ajali hiyo. Kulia ni Dk.Suleiman Muttani wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.


Godwin Myovela na Dotto Mwaibale, Singida


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Doroth Gwajima, ameongoza kuaga miili ya watu 15 waliofariki kutokana na ajali mbaya iliyosababishwa na basi dogo la abiria (hiace) kugongana uso kwa uso na lori la mafuta eneo la kijiji cha Mkiwa, wilaya ya Ikungi, mkoani hapa juzi.

Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, mbele ya Waziri wa Afya, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Sweetbert Njewike, alisema mnamo Machi 13 mwaka huu, majira ya saa 9.30 alasiri, ndipo ajali hiyo ilitokea kwa kuhusisha basi dogo la abiria lililokuwa likitokea Mwanza kugongana uso kwa uso na lori la mafuta lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenye maeneo yaliyotajwa.

Njewike alisema basi hilo kutoka Mwanza lilikuwa na abiria 14 wanaosemekana kuwa walikuwa wakimsindikiza ndugu yao ambaye ni bwana harusi mtarajiwa kwenda kufunga ndoa na lilipofika eneo la Ikungi mkoani Singida likaongeza abiria wengine 3 ambao waliomba msaada kwenda msibani eneo la uelekeo wa gari hilo, na kufikisha idadi ya abiria 17.

Alisema baada ya kufika kijiji cha Mkiwa ndipo lilipopata ajali hiyo-na abiria 13 walipoteza maisha pale pale, huku majeruhi wengine 2 nao wakifariki kwa nyakati tofauti wakati wakipatiwa matibabu hospitali-idadi iliyofikisha jumla ya vifo 15 vilivyotokana na ajali hiyo mpaka sasa.

“Kwa sasa majeruhi wawili waliotambuliwa kwa majina ya Hema Mkama (Bwana Harusi mtarajiwa aliyekuwa akisindikizwa kwenda kuoa) na mwingine Shakira Hamis wanaendelea kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya St. Gasper iliyopo Itigi, Manyoni,” alieleza Njewike.

Aidha, aliwataja waliofariki kuwa ni Mrisho Swedi (Mabatini Mwanza), Swalala Ibrahimu (Mabatini Mwanza), Zakia Ibrahimu (Mwanza), Lamlati Mkama (Mabatini Mwanza), Rehema Hussein (Mabatini Mwanza), Abdul Mirambo (Mabatini Mwanza) na Christian Sande (Mabatini Mwanza).

Wengine ni Halima Rashida (Mabatini Mwanza), Lukuman Ibrahimu (Mabatini Mwanza), Joseph Ludovick (Damankia Ikungi), William Churi (Damankia Ikungi), Anna Gabriel (Damankia Ikungi), Anjela Phinias, aliyekuwa dereva wa hiace hiyo Majaliwa Paschal, na mwingine aliyetambuliwa kama Mama Mdogo.

Gwajima, kabla ya kuongoza kuaga miili ya marehemu eneo la hospitali ya mkoa mapema jana, alianza kwa kutembelea hospitali ya St. Gasper iliyopo halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, kwa lengo la kuwafariji manusura wawili wa ajali hiyo Heri Mkama (bwana harusi mtarajiwa) na Shakira Hamis.

Aidha, alipata nafasi ya kutembelea eneo la tukio ambalo ajali hiyo ilitokea, na baadaye alitembelea hospitali kadhaa za mkoa wa Singida, ikiwemo ya Rufaa Mandewa na hospitali ya mkoa ili kuhakiki na kujiridhisha juu ya mfumo mzima wa huduma za kitiba pindi ajali zinapotokea.

Akizungumza wakati wa tukio la kuaga miili hiyo, Gwajima pamoja na kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki waliokusanyika eneo hilo, alionyesha kufarijika na salamu na kiitikio ambacho viongozi wa dini na serikali mkoani hapa wakati wote walikitumia kama kauli mbiu-yaani “Upendo na Amani” kiitikio “Dini Mbalimbali” na kinyume chake “Dini Mbalimbali ” kiitikio “Upendo na Amani.”

Alisema salamu hiyo ni ishara ya umoja na mshikamano, ni ishara ya upendo na uzalendo, na kiashiria cha ustawi wa maendeleo yanayotokana na mshikamano wa dhati, uliosheheni kiu ya kufikia malengo kama mkoa na taifa kwa pamoja bila kubaguana kwa namna yoyote inayotokana na itikadi za kidini.

Aidha, Gwajima aliwashukuru wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine, katika kuhakikisha wanaokoa maisha ya majeruhi waliotokana na ajali hiyo lakini pia kwa kuwasitiri wengine waliotangulia mbele za haki

“Nimeona nije hapa sababu toka tu pale ajali ilipotokea mfumo wa afya uliingia katikati. Hivyo nimekuja kuhakiki mfumo mzima na kujiridhisha-na ukweli watendaji wa afya wanajitahidi sana kuokoa maisha ya majeruhi waliopo na kuendelea kuwasitiri wote waliotangulia mbele ya haki,” alisema.

Aliwataka watanzania kuhakikisha wanafuata sheria za barabarani zilizopo, sambamba na kuunga mkono juhudi za maksudi zinazofanywa na majeshi yetu, hususani maelekezo ya mara kwa mara yanayotolewa na kikosi cha usalama barabarani ili kwa pamoja kuweza kutokomeza matukio ya ajali.

“Kwa upande wa serikali kupitia sisi sekta ya afya tunajitahidi kuelekeza rasilimali tunazopewa katika kuboresha miundombinu ya kukabiliana kikamilifu pindi ajali zinapojitokeza. Na kuna mradi unakuja ambao utakwenda kuimarisha miundombinu yetu kuwa imara na ya kisasa zaidi,” alisema Gwajima.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Rehema Nchimbi, alitoa salamu za pole na faraja kutoka kwa Rais John Magufuli kwa wote walioguswa na msiba huo.

“Rais John Magufuli ameniagiza kutoa salamu za pole kwa wafiwa, ndugu, jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huu, anaungana na familia zote katika kipindi hiki kigumu. Mwenyezi Mungu awape uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki-marehemu wote wapumzike kwa amani,” alisema Nchimbi kwa niaba ya Rais

Aidha, akieleza utaratibu wa kusafirisha miili hiyo kuifikisha mahali inapotakiwa, alisema serikali itagharamia kila kitu katika kuhakikisha wote waliofariki kupitia ajali hiyo wanasafirishwa na kupumzishwa kwenye makao yao ya milele.

Imeelezwa, taratibu zote za kusafirisha miili hiyo zimekamilika, na kwamba miongoni mwa waliofariki miili 11 itaelekea Mwanza, mwili mmoja utasafirishwa kwenda Mbeya, na miili 3 itaelekea Ikungi kwa taratibu nyingine za maziko.

Kupitia ajali hiyo, mama mdogo wa ndugu hao amejikuta akipoteza watoto wawili, wajukuu wanne, na kitukuu kimoja-yaani watu 7 kwa mara moja ndani ya familia moja, huku Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Singida Dk .Victorina Ludovick naye akijikuta akipoteza ndugu 3 wa familia moja-ambao walipanda basi hiyo kutokea Ikungi.

NDAHANI AWATAKA WANAFUNZI KUWA WAZALENDO WA NCHI

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi akihutubia wakati akizungumza na  wahitimu wa kidato cha nne na wanaoendelea na masomo ambao ni wanachama wa Klabu ya Fema mkoani hapa wakati wa Tamasha maalumu lililoandaliwa na Fema  hivi karibuni.
Mwenyekiti wa Fema Mkoa wa Singida, Donald Adam, akizungumza katika Tamasha hilo.
Wanafunzi wakiwa katika Tamasha hilo.
Tamasha likiendelea.
Wanafunzi wakiwa katika Tamasha hilo.
Wanafunzi hao wakiserebuka katika Tamasha hilo.
Picha ya pamoja na mgeni rasmi. 
Mgeni rasmi akiwa na viongozi wa Fema mkoani hapa.
Mgeni rasm Ndahani akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanafunzi waliohudhuria tamasha hilo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida.


KAIMU Afisa Vijana mkoani hapa Frederick Ndahani amewataka vijana waliohitimu kidato cha nne kuwa wazalendo wa nchi yetu.

Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wanafunzi wa sekondari mkoani  hapa ambao ni wanachama wa Klabu ya  Fema.

"Tunapaswa kuwa wazalendo wa nchi yetu na uzalendo unatafusiri nyingi kwanza unapaswa kuipenda nchi yetu kuifahamu  kuithamini na kuitunza" alisema Ndahani.

Alisema wakiwa kama vijana waliohitimu kidato cha nne na wale ambao wanaendelea na masomo ni lazima kwanza wawe wazalendo.

Alisema sisi tupo katika Taifa la Tanzania hivyo hatuna Taifa lingine zaidi ya Tanzania hivyo tunapaswa kulitunza.  

Alisema  vijana wengi wamepoteza uzalendo kwani wanaweza kuona miundombinu imeharibika na inaibiwa wakawa hawana mpango wa kuirekebisha na kusema potelea mbali jambo ambalo si nzuri.

Ndahani aliwaambia vijana hao kuwa uzalendo unatakiwa kuuanza wakiwa na umri mdogo na kuwa hawawezi kuwa wazalendo pasipo kulielewa Taifa lao kuanzia historia yake, misingi na jinsi lilivyopatikana.

"Niwaombe ninyi wahitimu na nyie mnaoendelea na masomo ni lazima mfahamu historia ya taifa letu kwani leo hii mpo hapa mna enjoy kwa kucheza mziki na kubadilishana mawazo kuna watu waliteseka kuliangaikia taifa letu akiwepo Baba wa Taifa Hayati Julius Kambarage Nyerere na wenzake.

Alisema ni muhimu kwa vijana hao kusoma masomo ya uraia ili waweze kulielewa taifa lao kwani wakilielewa wataweza kulitetea ndani na nje ya Tanzania.

Alisema kulielewa somo la uraia ndilo litakalowafanya waujue uzalendo wa nchi yetu ulivyo na kuwa Rais wetu Dkt.John Magufuli ni moja ya kiongozi ambao ni wazalendo wa taifa letu ambaye anaonesha uzalendo mkubwa kwa kusimamia rasilimali zetu yakiwemo madini hivyo ni lazima wawe wazalendo wa nchi.

Ndahani aliwataka vijana hao kutii sheria na kuacha kujiingiza katika vitendo vya uvutaji wa bangi, ukahaba, ushoga, wezi na vingine hivyo aliwaomba 

kutumia muda wao kwa kucheza mpira kuliko kufanya vitendo hivyo ambavyo vitaweza kuharibu tabia zao.

Aidha Ndahani aliwaambia vijana hao kuwa wanao uwezo wa kuanzisha na kubuni shughuli ndogo ndogo za kiuchumi ambazo zinaweza kuwaingizia kipato kama ufugaji wa kuku, sungura na kilimo badala ya kukaa vijiweni wamepoteza muda.

Ndahani aliwataka vijana hao kulinda afya zao ili watimize ndoto zao kwani kama viongozi hawa waliopo wasinge linda afya zao tusingekuwa nao leo hii.

Mwenyekiti wa Fema Mkoa wa Singida, Donald Adam alitoa rai  kwa vijana hao  waliohitimu  kidato cha nne kuwa wakawe wabunifu na watafiti katika kujishughulisha na kazi halali zitakazowapatia kipato kwa lengo la kusaidia jamii na Taifa  la Tanzania. 

Alisema vijana hao watumie dhana ya  4H (4Hhead, health, haert, na hands)  wakiwa mashuleni pamoja na akili, utashi kujifunza zaidi kwa vitendo wajali afya zaidi na wasijihusishe na ngono zembe na wawe na moyo wa kujitolea na kusaidia wahitaji ikiwa ni agenda ya sema tenda na kwa mikono yao wajikite kufanya kazi kwa bidii ili kujisaidia wenyewe na jamii kwa ujumla .

Adam aliwataka wahitimu hao Wakawe mabalozi katika kuhakikisha ukatili wa kijinsia unaisha katika jamii wanayotoka na kuwa wao kama Fema wanayo kazi ya kujenga Taifa imara na la kizalendo.