Wednesday, February 17, 2021

AGIZO LA MAGUFULI KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI WA BI ELIZABETH MANYONI LATEKELEZWA 100%

 

Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) (aliyeshika  hati  ya ardhi) akiwa kwenye picha ya pamoja  na  Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi( mwenye msalaba), Viongozi wa  Wilaya ya Manyoni,wataalam wa ardhi  Mkoa  wa Singida na wanafamilia  mara baada ya kukabidhiwa hati hiyo ya eneo lake lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa  kwa Kampuni  mmoja ya simu za mikono ambapo  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza  lirejeshwe mara moja  kwa  bibi huyo ambaye ndiye ataingia  mkataba  wa upangaji na Kampuni  hiyo
Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) akitoa shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  mara baada  ya kukabidhiwa  hati ya eneo lake

                                                          ...........................................................

Na John Mapepele, Manyoni

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Dkt. Rehema Nchimbi ametekeleza agizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alilomtaka kushirikiana na Viongozi wa Wilaya ya Manyoni kumrejeshea umiliki  wa eneo  lililokuwa mali ya  Bibi Elizabeth Msalali Chilingo (90) ambaye lilichukuliwa na Afisa Ardhi aitwaye Leonard Msafiri na kisha kupangishwa  kwa Kampuni  mmoja ya simu za mikono ambayo  imeweka mnara wa mawasiliano lirejeshwe mara moja  kwa mama huyo ambaye ndiye ataingia  mkataba  wa upangaji na Kampuni  hiyo.

Akikabidhi  hati ya umiliki wa ardhi wa miaka 66 wa eneo hilo la Majengo Kiwanja Na 13 hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Singida  Mhe, Dkt. Rehema Nchimbi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano  inayoongozwa na Mhe, Dkt. John Pombe  Magufuli ina dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi wanyonge ili wapate haki zao na kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo ili kuchangia katika uchumi wa kati na hatimaye uchumi wa juu wa Taifa letu.

Amesema Mkoa umejipanga kimkakati kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi inakwisha mara moja  kwenye Mkoa wa Singida na kuagiza Wakuu wote wa Wilaya na Wataalam wa ardhi  kuanzia sasa kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo husika badala ya kufanya mashauri ya migogoro ya ardhi  maofisini.

“Kuanzia leo sitaki kuona shauri na migogoro ya ardhi ikitatuliwa  maofisini, naagiza wakuu wote wa Wilaya katika Mkoa wangu  na wataalam kwenda moja kwa moja  kutatua  migogoro ya ardhi ya wananchi  katika maeneo ya migogoro, hatua kali zitachukuliwa kwa wote ambao hawatatekeleza  agizo hilo” alisisitiza Mhe. Nchimbi

Akizungumzia kuhusu migogoro ya ardhi kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni amesema ni lazima iishe mara moja kwa  kuwa Manyoni  ya sasa ni Sebule ya Makao Makuu ya nchi-Dodoma na kwamba watu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania wanakuja Manyoni kwa kuwa kuna maeneo mazuri yenye fursa za uwekezaji hususan kwenye  viwanda, biashara  na kilimo cha zao la Korosho ambapo kwa sasa Wilaya hii inaongoza siyo tu Tanzania bali katika  Bara la Afrika kwenye kilimo hicho ambapo kumekuwa na shamba la pamoja la Kilimo cha Korosho (Block Farming)lenye takribani ekari 25000.

“Haiwezekani Manyoni hii ambayo ni lango la makao  makuu ya nchi ikaendelea kuwa na migogoro ya ardhi ambapo sasa  ardhi yake imebeba uwekezaji mkubwa katika nchi yetu” aliongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa

 Akipokea hati yake ya umiliki wa eneo hilo, Bibi Elizabeth Msalali  alimshukuru Rais Magufuli kwa kusaidia kupatikana kwa kiwanja chake ambapo amesema Magufuli  ameonyesha kuwa ni Rais anayewapigania  watu masikini na wanyonge kama yeye hivyo anamwombea kwa Mungu azidi kumbariki katika utumishi na maisha yake kwa ujumla.

Aidha Mtoto wa pekee wa Bi Elizabeth ambaye ndiye aliyemwomba Mhe. Rais Magufuli kuingilia kati suala hili Bwana, Adamu Kazimoto alimshukuru na kumpongeza Mkuu wa Mkoa, Dkt. Rehema Nchimbi kwa kuharakisha  kukamilisha  mchakato wa kupata  hati ya umiliki wa kiwanja  hicho kwa mama yake ambapo amesema  mchakato huo umechukua muda mfupi sana.

“Naomba niwe mkweli kama tungekuwa na fedha ya kulipia  hiki kiwanja  nadhani  ingechukua  siku  moja au mbili tu baada ya agizo la Mhe.Rais maana Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Dada Shamimu Hoza alikamilisha  utengenezaji wa hati hiyo mara moja baada ya tamko  hilo la Mhe.Magufuli jambo ambalo limetupa faraja kubwa kwani sasa mama yangu amepata  haki yake” ameongeza Adamu

Akifafanua Adamu amesema suala hili  alianza kufuatilia zaidi ya  miaka tisa iliyopita, na anamshukuru Rais Magufuli  kwa kutoa suluhisho la kudumu ambapo pia ameongeza kwamba mgogoro huo umeifanya familia ya Mzee Kazimoto kuwa kitu kimmoja licha sintofahamu ambazo zilikuwepo hapo awali kwa sababu ya tamaa ya pesa kwa wanafamilia.

Mhe. Rais John Pombe  Magufuli  alilitoa agizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kushughulikia mgogoro  huo tarehe 31Januari 2021 aliposimama kuwasalimu wananchi wa Manyoni wakati akiwa safarini akitokea Tabora kwenda Dodoma.

Rais Magufuli  alisikiliza  kero inayowakabili wananchi hao ambao walilalamikia  kitendo cha Idara ya Ardhi kuchukua maeneo  yao bila kuwalipa fidia  na wengine kuamriwa  kuondoka katika  eneo hilo baada ya kupewa nyaraka  za kupatiwa  radhi(offer) hali iliyozua mgogoro kati ya wamiliki wa asili wa eneo hilo na Idara ya Ardhi.

Rais ameagiza wananchi wenye offer waruhusiwe kuendeleza maeneo waliyopatiwa na wamiliki wa asili wa eneo hilo  kulipwa fidia kwa mujibu wa Sheria.

Awali, kufuatia agizo  la Mheshimiwa Rais, Timu Maalum ya wataalam kutoka Mkoani na Wilaya ya Manyoni iliyoongozwa na Kamishina Msaidizi wa Mkoa wa Singida Shamimu Hoza Shaban ilikutana  familia nzima ya mmiliki wa asili wa eneo hilo marehemu  Salum Kazimoto aliyefariki mwaka 1973  ambayo   ilikuwa  inavutana  kuhusu  umiliki wa eneo  hilo ambapo  baada ya  majadiliano ilikubaliana kwa kauli mmoja kwamba mmliki halali  wa eneo hilo ni Bibi Elizabeth Msalali.

Kutokana  na  Wilaya ya Manyoni kuonekana kuwa na migogoro ya ardhi kadhaa ya ardhi kwa muda mrefu sasa, mkakati maalum wa kusikiliza kero hizo umeandaliwa  ambapo timu ya wataalam na viongozi wa Halmashauri hiyo unazungukia katika maeneo husika ili kuhakikisha migogoro yote inaisha  kama ilivyoamriwa.

Monday, February 15, 2021

WAZIRI BASHUNGWA KUKUTANA NA WANAMUZIKI ZAIDI YA 500 HOTELI YA MOUNT MERU JIJINI ARUSHA

Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa.

Katibu Mkuu wa wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), , Stella Joel.

Wasanii wa Kikundi cha Sanaa cha Dofa kutoka Karatu ambao wataimba wimbo maalumu kwenye kongamano hilo.
 


Na Dotto Mwaibale


WAZIRI wa Habari, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa anatarajiwa kukutana na wanamuziki zaidi 500 katika kongamano la fursa litakalofanyika Jumamosi Hoteli ya  Mount Meru jijini Arusha.

Katika kongamano hilo baadhi ya wanamuziki watakabidhiwa kadi za bima ya afya ya Taifa (NHIF) na Bashungwa ambaye anatarajiwa  kuwa mgeni rasmi.

  "Wanamuziki watakao pata kadi hizo ni wale ambao wametimiza vigezo kama walivyoeleza Rais wa Umoja wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO), Eric Kisanga na Katibu Mkuu wa umoja huo, Stella Joel ambao ndiyo waandaaji wa kongamano hilo.

Baadhi ya wanamuziki watakao kabidhiwa kadi hizo wametajwa kuwa ni mwanamuziki mkongwe hapa nchini, Kida Waziri,  Emmanuel Mbasha, Madamu Flora, Goodluck Gozibeth, Stara Thomas, Hafsa Kazinja Renatha Sedekia na Rehema Tajiri.

Akiwazungumzia Wanamuziki hao Katibu Mkuu wa TAMiUFO Stella Joel alisema wanaishukuru Serikali kwa kuwakumbuka kuwapatia kadi hizo ambazo zitawasaidia kupata vipimo na matibabu katika hospitali za Serikali na binafsi.

Joel alisema kabla ya hapo wanamuziki wengi wamekuwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kumudu gharama za vipimo na matibabu.

" Kwa hatua hii iliyochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano hakika wanamuziki wote tunakila sababu ya kuipongeza  kwa kutekeleza ahadi yake kwa vitendo ya kutusaidia wasanii" alisema Joel.

Rais wa TAMUFO,  Eric Kisanga alisema kongamano hilo ni la kipekee kwani litawahusisha wanamuziki wa kada zote  na kuwa maandalizi yote yamekwisha kamilika.

" Maandalizi yote ya kongamano letu ili la fursa kwa wanamuziki yamekwisha kamilika kwa asilimia kubwa na sasa tupo kumalizia mambo madogo yaliyosalia" alisema Kisanga.

Kisanga alitumia fursa hiyo kuwakaribisha kwenye kongamano hilo wananchi, wasanii  na wadau wengine wa muziki  na kuwa halitakuwa na kiingilio ni bure. 

Sunday, February 14, 2021

UHABA WA WATAALAMU WENYE UJUZI KILIO KWA WAWEKEZAJI

Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.


  1. Mtaalam wa Kuendesha Mitambo katika Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Geofrey Mahende (kulia) akitoa maelezo ya namna anavyofanyakazi yake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto)alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.
  2. Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa Kitanzania wanaofanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza Chanjo cha Hester alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Pwani jana. Wa kwanza kushoto ni Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Tina Towo Sokoine.

    1. Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.

       


      Na Mbaraka Kambona, Pwani

       

      Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Tina Towo Sokoine amesema kuwa lengo la kiwanda hicho ni kutumia Wataalamu wa ndani lakini uhaba wa Wataalam wa masuala ya sayansi wenye ujuzi hasa wa vitendo unaelekea   kukwamisha dhamira yao hiyo. 

      Towo aliyasema hayo alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana. 

      Alisema kuwa kwa sasa wana wataalamu watatu tu kutoka nje nchi ambao wamewaajiri katika Kiwanda hicho lakini   kwa hali ilivyo wanaona watashindwa na labda wanaweza kuomba vibali vingine vya kuajiri wataalamu kutoka nje. 

      “Nia yetu ni kufanyakazi na Watanzania tu lakini bado vijana wengi tunaowafanyia usahili wanakosa ujuzi hasa wa vitendo, tunaiomba Serikali na Vyuo vinavyoandaa hawa Wataalam kuhakikisha wanajikita katika elimu ya vitendo na sio nadharia peke yake ili kukidhi mahitaji ya sasa na kulinda ajira za Watanzania,” alisema Towo 

      Kuhusu uzalishaji, Towo alisema kuwa wanatarajia kuzalisha chanjo ya kwanza mwezi wa nne mwaka huu, huku akiiomba Serikali kuona uwezekano wa taasisi zinazohusika na kusimamia uwekezaji kuunganishwa ziwe na lugha ya pamoja ili kumfanya muwekezaji aweze kupata huduma zote sehemu moja bila kuhangaika kama ilivyosasa. 

      Naye Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel aliutaka Uongozi wa Kiwanda hicho  kuhakikisha wanazalisha chanjo zenye ubora ili nchi iweze kuondokana na utegemezi wa chanjo na bidhaa nyingine za mifugo kutoka nchi za nje. 

      “Lengo la Wizara ni kuhakikisha kuwa nchi inaondokana na uagizaji wa chanjo kutoka nje, tunatamani kuwa na chanjo tunazoweza kudhibiti ubora wake na tuwe na uhakika nayo, hivyo uwepo wa kiwanda hiki kutatusaidia kuzalisha chanjo hapa hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya Wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Ole Gabriel. 

      Aliongeza kwa kusema kuwa Serikali inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili mahitaji ya wafugaji na wananchi yawe yanashughulikiwa ndani ya  nchi. 

      Aidha, Prof. Ole Gabriel aliwaomba Wafugaji na Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa za ndani na waondokane na ile dhana ya kwamba bidhaa bora ni ile inayotoka nje, wakithamini vya ndani wataongeza pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

      Thursday, February 11, 2021

      NARCO YAAGIZWA KUWANYANG'ANYA VITALU WALIOKIUKA MKATABA

      Katibu Tawala, Mkoa wa Kagera, Prof. Faustin Kamuzora (wa kwanza kulia) akimueleza jambo Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wakwanza kushoto) walipokutana katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma juzi. Wa pili kushoto ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel na wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Jeremiah Wambura.

      Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro walipokutana katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma juzi.

      Mmoja wa Wafugaji kutoka Wilayani Kilindi, Mkoani Tanga, Yohana Samwel akieleza jambo katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma juzi. 

      Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kwa baadhi ya wafugaji waliohudhuria kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma. 



      Na Mbaraka Kambona,

       

      Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameiagiza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuwanyang'anya wale wote walioshindwa kuendeleza vitalu walivyokodishwa katika ranchi za kampuni hiyo kwa sababu wamekiuka masharti ya mkataba. 

      Ndaki alitoa agizo hilo alipokutana na Viongozi wa Chama cha Wafugaji katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma juzi. 

      Alisema kuwa kuna watu wengi wamekodishwa maeneo katika ranchi za taifa lakini wamezitelekeza na wengine wamekodisha watu wengine ambao wanatumia maeneo hayo kinyume na makubaliano ya mkataba. 

      "Ikifika tarehe 15 mwezi huu, wale wote waliochukua vitalu na wamekodisha watu wengine wanyang'anywe maeneo hayo na hatutajali mikataba yao kwani wameshakiuka masharti," alisema Ndaki. 

      Aliongeza kwa kusema kuwa baada ya tarehe 15 kupita wataanza kuwasaka wote waliochukua maeneo hayo na kuwanyang'anya ili wapewe wafugaji makini waweze kutumia maeneo hayo kuweka mifugo yao. 

      Kuhusu baadhi ya Wananchi wanaoishi karibu na ranchi kuvamia maeneo hayo, Ndaki alitumia nafasi hiyo pia kuwataka waondoke katika maeneo hayo na wasipofanya hivyo wataondolewa. 

      Aliendelea kusema kuwa wameanza mikakati ya kuiweka vizuri NARCO ili maeneo makubwa iliyonayo ambayo mengine hawayatumii vizuri yagawiwe kwa wafugaji watakaoweza kuyatumia kufanya ufugaji wa kisasa nah atua waliyoanza nayo ni kupunguza bei ya kukodisha vitalu. 

      "Tumekubaliana kuwa bei ya kukodisha kitalu iwe ni shilingi elfu tatu mia tano (3500) kwa Ekari moja na sio zaidi ya hapo," alisema Ndaki. 

      Waziri Ndaki alisema kuwa wameielekeza NARCO kuwa katika yale maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ukodishaji watenge asilimia thelathini (30) kwa ajili ya kuwakodisha wafugaji wanaoishi karibu na maeneo ya ranchi hizo ili kupunguza migogoro na uvamizi wa maeneo hayo. 

      "Hata maeneo yetu yaliyotengwa kwa ajili ya kupumzishia mifugo (holding grounds) tutayapunguza ili nayo tuwape NARCO ili wayakodishe kwa wafugaji wetu, tunaamua kufanya haya ili kutibu tatizo la malisho na wafugaji waondokane na kutangatanga," alifafanua Ndaki. 

      Mapema wiki hii Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NARCO, Paul Kimiti alitangaza kuwa ekari moja ya kitalu katika ranchi hizo itakodishwa kwa shilingi elfu tatu mia tano (3500).

      Tuesday, February 9, 2021

      SERIKALI ZA VIJIJI ZATAKIWA KUWATAMBUA VIJANA WENYE UJUZI MBALIMBALI.

      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani, akiangalia kazi za wahitimu wa mafunzo ya ufundi  katika Kata  ya Kinyangege na Ulemo wilayani  Iramba mkoani Singida.


      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani ( kushoto) akizungumza na  vijana waliohitimu mafunzo ya Ufundi Stadi.  


       Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu na viongozi mbalimbali.

      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akikabidhi vyeti.



      Na Dotto Mwaibale, Singida


      KAIMU Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani amezitaka Serikali za Vijiji, Mitaa na Kata kuwatambua vijana wote wenye ujuzi wa ufundi mbalimbali.

      Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi alitoa kauli hiyo kwenye mahafali ya wahitimu elimu ya ufundi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Kata ya Kinyangege wilayani Iramba mkoani humo.

      Alisema Serikali imekuwa ikituma fedha za ujenzi na shughuli mbalimbali katika maeneo yenye kazi mfano ujenzi wa miundombinu ya shule kama mabweni, madarasa, hospitali na vituo vya afya lakini viongozi badala ya kuwapatia kazi vijana walio katika maeneo yao wao wanachukua mafundi kutoka maeneo mengine.

      Ndahani aliongeza kuwa pia  wakati mwingine fundi mmoja anaweza kuwa na kazi zaidi ya mbili katika vijiji tofauti kuwa utaratibu huo haukubaliki kwani  lengo la Serikali la kutumia Force Account katika kazi hizo ni kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana na wananchi kwa ujumla.

      "Ukisha watambua vijana wenye ujuzi ni rahisi kuwapatia kazi  katika maeneo walipo." alisema Ndahani.

      Aidha  Ndahani aliyataka mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya kazi kwa uzalendo mkubwa na kujali masilahi ya Taifa kwani  mengi yamepata ufadhili kutoka nje ya nchi hivyo wahakikishe kuwa ufadhili huo  usije kuathiri Taifa kwa namna yoyote kupitia masharti yao.

      Alisema kuna taarifa katika nchi za jirani  kuwa mashirika yalitumika kuvuruga amani, mshikamano na usalama wa  nchi ambapo aliliomba  Shirika la SEMA ambalo limetoa ufadhili wa mafunzo hayo kwa vijana kuwa makini ili  heshima walioijenga katika mkoa huo na Taifa isije kutoweka.

      Ndahani aliwataka vijana waliopata ujuzi mbalimbali katika Kata hiyo ya Kinyangege na Ulemo wilayani humo kuonesha kwa vitendo ujuzi wao badala ya kujifungia ndani huku wakilalamika kuwa hawana ajira.

       Katika mahafali hayo jumla ya vijana 157  ikiwa wavulana 98  na wasichana 58 walihitimu mafunzo ya ufundi stadi katika fani ya ushonaji, upishi, uhunzi , kilimo, urembo na ususi , useremala na ujenzi kwa ufadhili wa Shirika la SEMA na SROMME kupitia miradi ya BONGA NA TUNAWEZA.

      Kwa upande wao Vijana wamelishukuru Shirika la SEMA kwa kuwapatia ujuzi na kuahidi kutumia majukwaa ya vijana ili kujikwamwua na umasikini.

      VIJIJI MKOA WA SINGIGA VYATAKIWA KUTENGA MAENEO KWA AJILI YA VIJANA


      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani, akihutubia katika  Mahafali ya vijana waliohitimu mafunzo ya Ufundi Stadi katika fani za ushonaji, uashi, useremala, ufundi pikipiki, ususi ,urembo na uhunzi  yaliyofanyika  Kijiji Cha Iseke wilayani Ikungi kwa ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la SEMA lenye makao yake makuu mkoani Singida kwa ushirikiano wa Shirika la STROMME.


      Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la SEMA Peter Lissu, akiwa kwenye mahafali hayo.


      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani, akiangalia kazi za wahitimu wa mafunzo ya ufundi wa Kata ya Iseke, na Muhintiri, Ikungi mkoani Singida.

      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu na viongozi mbalimbali.
      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akikabidhi vyeti.
      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akiangalia kazi za wahitimu wa mafunzo ya ufundi wa Kata ya Iseke, na Muhintiri, wilayani Ikungi mkoani Singida.
      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akiangalia kazi za wahitimu wa mafunzo ya ufundi wa Kata ya Iseke na Muhintiri wilayani Ikungi mkoani Singida.

      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akikabidhi vyeti kwa wahitimu.

      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akikabidhi vyeti.

      Kaimu Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida  Frederick  Ndahani, akiwa katika picha ya pamoja na wahitimu na viongozi mbalimbali.
       


      Na Dotto Mwaibale, Singida.


      KAIMU Afisa Maendeleo ya Vijana Mkoa wa Singida,  Frederick  Ndahani amezitaka Halmashauri za Vijiji na Mitaa Mkoani Singida kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za Vijana.

      Ndahani ambaye alikuwa mgeni rasmi ameyasema hayo katika  Mahafali ya vijana wa Kata za Iseke na Muhintiri waliohitimu mafunzo ya Ufundi Stadi katika fani za ushonaji, uashi, useremala, ufundi pikipiki, ususi ,urembo na uhunzi  yaliyofanyika  Kijiji cha Iseke wilayani Ikungi kwa ufadhili wa Shirika lisilo la Kiserikali la SEMA lenye makao yake makuu mkoani Singida kwa ushirikiano wa Shirika la STROMME.

      Alisema Serikali ilishatoa mwongozo kwa kila halmashauri kutenga maeneo ya shughuli za vijana lakini unakuta baadhi ya viongozi wanatoa taarifa kuwa maeneo yametengwa lakini ukifuatilia unakuta hakuna hata eneo lilitengwa kwa shughuli za Vijana.

      " Jambo hili siyo sawa tunakuwa hatuwatendei haki vijana wetu nawaomba viongozi wa kamati ya maendeleo ya kata kuhakikisha suala hili la kutenga maeneo hayo linatekelezwa kwa vitendo." alisema Ndahani.

      Aidha Ndahani aliwataka vijana kutumia umeme vijijini ulioletwa na Serikali kwa ajili ya kuendeleza ujuzi na kufungua Shughuli za kimaendeleo katika Vijiji vyao badala ya kukimbilia mjini.

      Kwa upende wao vijana kupitia risala yao wameomba kupatiwa mikopo ili ujuzi walionao waweze kuuendeleza na kuutumia kwa ajili ya kujikwamua na umasikini.

      Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Shirika la SEMA Peter Lissu ameishukuu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuonesha ushirikiano na mashirika yasiyo ya Kiserikali na kuahidi kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo na adhima ya Serikali ya kuondoa umasikini kwa watanzania na kuinua uchumi wa Taifa kwa ujumla.

       Katika mahafali hayo jumla ya vijana 106 wavulana 54 na wasichana 52 walihitimu mafunzo hayo ya ufundi wilayani Ikungi.


      Saturday, February 6, 2021

      SERIKALI KUTUMIA ZAIDI YA SH. MILIONI 100 KUIMARISHA KITUO CHA KUTOTOLESHA VIFARANGA VYA SAMAKI CHA RUHILA

      Afisa Mfawidhi, Kituo cha kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila, Emmanuel Maneno (wa kwanza kushoto) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) alipotembelea Kituo hicho kilichopo Mkoani Ruvuma jana.  Wa kwanza Kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji WMUV), Dkt. Nazael Madalla.

      1. Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kushoto) alipotembelea Kituo cha kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma jana.
      1. Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akinawa maji ya Ziwa Nyasa alipotembelea Kituo cha Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Nyasa kilichopo Mbamba Bay, Wilayani Nyasa, Mkoani Ruvuma jana. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla.
      Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia - aliyevaa koti) akieleza jambo wakati akiangalia moja ya Mabwawa ya kufugia Samaki alipotembelea Kituo cha Kutotolesha Vifanga vya Samaki cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma jana. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazae.


       

      Na Mbaraka Kambona, Ruvuma

       

      Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Serikali imepanga kutumia Shilingi Milioni 110 kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu ya Kituo cha Kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila ili kiweze kuzalisha vifaranga vitakavyokidhi mahitaji yaliyopo sasa. 

      Dkt. Tamatamah aliyasema hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na kituo hicho kilichopo Mkoani Ruvuma jana. 

      Alisema kuwa kwa mwaka huu wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga kuzalisha vifaranga Milioni 22, na kati ya hivyo, vifaranga Milioni 16 vitazalishwa na vituo vya kutotolesha vya watu binafsi na vifaranga Milioni 6 vitazalishwa na vituo vya Serikali. 

      Dkt. Tamatamah aliongeza kuwa hivi karibuni Wizara itatangaza zabuni kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha kituo hicho ili kiweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuzalisha vifaranga utakaowezesha kukidhi mahitaji yaliyopo sasa. 

      “Baada ya kukiimarisha kituo hiki mwaka huu, mwaka ujao wa fedha tutafanya ukarabati mkubwa na ukarabati huo ukikamilika tunatarajia uwezo wa uzalishaji wa kituo hiki kuongezeka mara tatu zaidi ya sasa na hivyo kutaongeza uhakika wa upatikanaji wa vifaranga vya samaki,’’alisema Dkt. Tamatamah. 

      Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla alitoa rai kwa Watanzania hasa wale wanaoishi mbali na vyanzo vikubwa vya maji kama maziwa kujihusisha na shughuli za ufugaji wa samaki kwani kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata kipato na lishe bora. 

      “Naomba Watanzania watembelee kituo hiki ili waweze kujifunza kwa vitendo namna ya kuchimba mabwawa makubwa na kufugaji samaki ili kujiongezea kipato na lishe bora kwa ajili yao na Watoto wao,” alisema Dkt. Madalla. 

      Kaimu Katibu Tawala anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Mkoani Ruvuma Deogratius Sibula alisema kuwa Ruhila kimekuwa kituo muhimu sana kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa sababu wafugaji wengi wanategemea kituo hicho kupata vifaranga vya samaki kwa ajili ya kufuga. 

      “Katika Mkoa wa Ruvuma kuna Wafugaji wa Samaki takriban Elfu nne (4000) na kuna mabwawa ya Samaki zaidi ya Elfu Sita (6000) na wote wamekuwa wakitegemea kituo hiki kwa ajili ya kupata mbegu na kupata elimu ya ugani, hivyo ni kituo muhimu sana katika kuchagiza ongezeko la ufugaji wa samaki na upatikanaji wa lishe bora kwa Wananchi,” alisema Sibula. 

      Naye, Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Ruhila, Emmanuel Maneno alisema kuwa baadhi ya Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakabiliwa na Utapiamlo hivyo fursa ya uhakika ya kuondokana na tatizo hilo ni kufuga samaki ambao watawahakikishia kupata lishe bora na kipato cha kujikimu kimaisha. 

      Maneno aliongeza kuwa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ina mazingira mazuri ya kufuga samaki kwa sababu hali ya hewa ni nzuri, maji yapo ya kutosha lakini pia malighafi kwa ajili ya kutengenezea chakula cha samaki inapatikana kwa urahisi na hivyo kufanya gaharama za ufugaji wa samaki kuwa chini.