Thursday, April 22, 2021

BRELA WATAKIWA KUWATAFUTA WAVUMBUZI NA WABUNIFU WALIOPO NCHINI

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa (katikati) akizungumza  na Wafanyabiasha wa mkoa huo jana wakati akifungua mafunzo ya  siku mbili ya kutoa elimu kwa wakazi wa mkoa huo kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)


Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa (katikati) akisisitiza wakati akifungua mafunzo hayo.  


 Wakazi wa Mkoa wa Morogoro wakiwa kwenye mafunzo hayo.



Na Mwandishi Wetu, Morogoro


MKUU wa Wilaya ya Morogoro, Bakari Msulwa ametoa wito kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuweka mkakati wa kuwafikia wagunduzi na wabunifu mbalimbali katika maeneo yao ili kuweza kuwapa elimu ya usajili.

Msulwa aliyasema hayo jana wakati akifungua zoezi la siku mbili la kutoa elimu kwa Wakazi wa Mkoa huo kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA katika Ukumbi wa Midland Inn Hotel, Morogoro.

Alisema kwamba kuna Watanzania wengi wanafanya juhudi mbalimbali za kugundua vitu vipya ni vyema kukawa na mpango wa kuwafikia hao na kuwasaidia  katika masuala ya kulinda kazi zao.

Katika hatua nyingine Wafanyabiashara wa Mkoa wa Morogoro wameishukuru BRELA kwa kutoa elimu katika Mkoa wao ambayo imewapa mwanga na dira mpya katika urasimishaji wa biashara zao.

Paulina Mbawala ambaye ni Mfanyabiashara mkoani Morogoro amesema kwamba kabla ya mafunzo kuna vitu vingi walikua hawajui na hivyo kupata Ugumu katika urasimishaji wa biashara zao.

“Kabla ya mafunzo haya hatua za usajili wa Kiwanda tuliziona ni ngumu, lakini kupitia elimu tuliyopata hapa tumefahamu ni namna gani tunaweza kusajili Kiwanda kikubwa, cha kati au kidogo na jinsi ya kukuza biashara kutoka hatua moja kwenda nyingine kwa manufaa yetu Wajasiriamali na Taifa kwa ujumla”alisema Mbawala.

Mfanyabiashara Novatus John, aliyeshiriki mafunzo hayo kwa siku ya kwanza, amebainisha kwamba kupitia elimu hii sasa wamefahamu ni kwa jinsi gani wanaweza kuingia katika fursa nyingine ilikuweza kukuza biashara zao zaidi.

“Kupitia elimu hii tumeweza kufahamu namna ya kupata masoko, kuzitambulisha bidhaa zetu sokoni lakini pia kupitia Dirisha la Taifa la biashara (the Tanzania National Business Portal) tumejifunza kuwa Mfanyabiashara anaweza kufahamu taratibu za usafirishaji nje ya nchi, uingizaji nchini na upitishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali nchini.”  alisema John.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ufunguzi wa mafunzo hayo,  Afisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA, Abbas Cothema alisema, katika sehemu walizopita wakitoa mafunzo wamegundua wafanyabishara wengi wamekua wakitumia majina ya biashara kabla ya kuyasajili na badae yanaleta shida katika usajili.

“Mpaka sasa tumetoa elimu kwa Wafanyabiashara wa Mkoa wa Singida, Dodoma na sasa tupo hapa Morogoro changamoto inayojirudia ni kufanya biashara bila kurasimisha. Mfanyabiashara anaanzisha biashara leo anakuja kusajili miaka mitano badae, kwa wakati huo kama alikua anatumia jina la biashara mathalani lisiposajiliwa itamlazimu kubadili jina na kuanza kujitangaza upya”. alisema Cothema.


Wednesday, April 21, 2021

JIMBO KATOLIKI SINGIDA LAFUNGUA PAZIA KUSHEREHEKEA MIAKA 50

Askofu wa Jimbo Katoliki la Kondoa Mhashamu Bernadin Mfumbusa, akiongoza adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida jana.

Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waamini wengine wakishiriki kwa furaha moja ya tukio la Jubilei hiyo la kurusha ‘Njiwa wa  Amani’ hewani kama ishara ya jukumu la kitume katika mwendelezo wa kazi aliyowaachia Yesu Kristu ya kusambaza Habari Njema, Umoja, Amani na Mapendo kwa mataifa.

Askofu wa Jimbo Katoliki Singida Edward Mapunda akimkabidhi mmoja wa mapadre wa Jimbo hilo Msalaba kama ishara ya bendera ya ushindi ili akatangaze ushindi huo kwa Kristu aliyekubali kuteseka, kufa na baadaye kufufuka. 

Mapadre na Waamini wa Jimbo Katoliki Singida wakishiriki Ibada hiyo.

Maaskofu Bernadin Mfumbusa (kushoto) na Edward Mapunda (kulia) wakiwa wameshika Mshumaa wa Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki Singida.

Watawa wa kike kutoka mashirika mbalimbali yanayofanya utume jimboni humo wakishiriki adhimisho la Ibada hiyo.

Ibada ikiendelea.

Kiongozi wa Kwaya ya Shirikisho Jimbo Katoliki Singida Peter Jihango akiongoza kwaya hiyo katika adhimisho hilo.


Katibu wa Liturjia Jimbo Katoliki la Singida, Padre Paterni Mangi, akishiriki kuwasha mshumaa wa Jubilei hiyo.

Maaskofu na Mapadre wakiwa kwenye picha ya pamoja muda mfupi baada ya adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi wa sherehe za Jubilei ya miaka 50 ya Jimbo Katoliki Singida.



Dotto Mwaibale na Godwin Myovela, Singida


JIMBO Katoliki Singida limeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya uzinduzi kuelekea kilele cha Jubilei yake ya dhahabu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.

Jimbo hilo liliundwa na Baba Mtakatifu Paulo wa VI kutokana na majimbo ya Mbulu, Dodoma na Tabora mnamo Machi 25, 1972 (Sikukuu ya Kupashwa Habari Bikira Maria), ambapo kilele cha maadhimisho hayo ni ifikapo Agosti 21, 2022.

Akiongoza adhimisho la Ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, Mhashamu Bernadin Mfumbusa pamoja na mambo mengine, alisema Jubilee ni kipindi cha sala na shukrani kwa Mungu kwa wema na ukarimu, kujitathmini, kuanza upya, kuwa na matumaini na kusamehe.

Aidha, alisema Umoja na Mapendo iwe ni tunu na dira muhimu katika Jubilei hiyo katika muktadha chanya wa kutangaza na kumwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha.

"Msiogope kila kitu kinawezekana. Ni kipindi kizuri cha kujitathmini tunatoka wapi na tunaelekea wapi...Mungu akiwepo chochote kinawezekana," alisema Askofu Mfumbusa.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Jimbo, Askofu wa Jimbo Katoliki Singida, Mhashamu Edward Mapunda kupitia Jubilei hiyo yenye Kauli Mbiu isemayo  'Jubilei Singida-Umoja na Mapendo,' aliwashukuru wamisionari wote waliojisadaka na kushuhudia habari njema bila ya kujibakiza katika kipindi chote.

Hata hivyo, Askofu Mapunda alihimiza waamini kushiriki kikamilifu mpango dira wa matukio yaliyoandaliwa kuelekea kilele cha Jubilei hiyo ili kujiweka zaidi mikononi mwa Mungu na kumshukuru kwa zawadi ya Jimbo na Imani.

Baadhi ya matukio yaliyopo ndani ya mpango huo ni kusali, novena, mafungo, semina, hija, matembezi ya Msalaba, matendo ya ukarimu, kuanzisha na kuimarisha vyama vya kitume, kuhamasisha miito ya utawa na upadre, katekesi endelevu na kutolewa msamaha kwa masuala mbalimbali ya kiroho-ikiwemo ubatizo

Matukio mengine yaliyoambatana na adhimisho hilo ni pamoja na kuwasha Mshumaa wa Jubilei, kubariki Msalaba utakaotembezwa kwenye parokia zote kipindi chote cha maadhimisho kuelekea kilele, na tukio la kurusha hewani maarufu 'Njiwa wa Amani'-kama ishara ya kusambaza amani, upendo na Habari Njema kwa mataifa.

Tangu kuanzishwa kwake mpaka sasa, Jimbo Katoliki Singida limefanikiwa kuwa na Parokia 29, Waamini 186,797, Vigango zaidi ya 361, Makatekista 583, Mapadre wanajimbo waliopadrishwa 76 ambao kati yao ni Askofu wa sasa wa Jimbo hilo, Mhashamu Edward Mapunda.

Mapadre wengine waliopo ni kutoka Mashirika 32 yanayofanya kazi ndani ya Jimbo hilo, pia Maaskofu 3 (Askofu Bernard Mabula 1972-1999; Desiderius Rwoma 1999-2015, na Edward Mapunda 2015 mpaka sasa.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa Mashirika ya watawa wa Kiume na Like kufikia 30, Hospitali 4, Vituo vya afya 3, Zahanati 9, Seminari ndogo 3, Sekondari 7 na Shule za Msingi 12.

Imeelezwa, pamoja na mambo mengine, Jimbo hilo pia mpaka sasa lina Vyuo 6, Kituo cha Kichungaji 1, Vituo vya walemavu na wazee 3, watoto yatima 1 sambamba huduma nyingine za kiroho na kijamii.

Tuesday, April 20, 2021

SERIKALI YAANZISHA KITUO CHA KIMATAIFA CHA KUENDELEZA VIPAJI VYA MICHEZO.

 


 Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omari (kushoto), akiwa naa liyewahi kuwa Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na Kocha wa Timu ya Taifa Stars, Ami Ninje (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya Dkt. Richard Masika wakikagua eneo la chuo kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa chuo hicho ili kujenga Kituo cha kuendeleza vipaji vya michezo.

Timu ya wataalam mbalimbali wa michezo na ardhi ikipitia ramani ya maeneo ya ujenzi wa madarasa na hosteli.

Timu ya wataalam ikiangalia eneo la ujenzi wa madarasa wa Kituo cha kuendeleza vipaji vya Michezo

 



Na John Mapepele, Dodoma

 

Serikali inatekeleza mradi wa  kupanua eneo la  Chuo cha  Maendeleo ya Michezo Malya ikiwa ni  mkakati  maalum wa kuanzisha Kituo cha Kuendeleza Vipaji vya Michezo  ili kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamichezo hapa nchini.

 

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo Omary ameyasema haya  wakati alipokuwa na  Timu ya wataalam walipotembelea na kukagua eneo  hilo hivi karibuni ikiwa ni sehemu ya kufanya maandalizi ya ujenzi wa kituo hicho ambacho kitakuwa na hadhi ya kimataifa.

 

“Niseme tu kwamba  kukamilika kwa kituo  hiki kutaifanya  nchi yetu kusonga mbele kwenye  Sekta ya Michezo kwa kuwa  vipaji vya wanamichezo wetu vitaibuliwa na  tutaweza sasa  kushindana  na mataifa mengine duniani sasa” amefafanua Mkurugenzi Omary

 

Amesema Tanzania ina hazina kubwa ya vipaji kilichokuwa kinakosekana ni kituo maalum cha michezo cha kuwanoa wachezaji na kwamba kukamilika kwa kituo hiki ni suluhisho la kudumu la changamoto hiyo.

 

Awali, Katibu Mkuu wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema  Wizara imeendelea  kufanya mageuzi makubwa ili kutimiza ahadi  za Serikali na matarajio ya wananchi kwa ujumla.

 

Amesema Wizara  inatekeleza kwa kwa kasi  masuala yote  yaliyobainishwa kupitia Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka  2020-2025 ikiwemo ibara125(a)-(h) kwa Sekta ya Habari, ibara239 (a)-(m) kwa Sekta ya Utamaduni, ibara 249 (a)-(j) Sekta ya Sanaa na ibara 243(a)-(k) kwa Sekta ya Michezo.

 

Akihutubia kwenye kikao cha Wafanyakazi wa wa Wizara hiyo hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa amesema tayari Wizara yake imeshakamilisha agizo la Serikali la kuanzisha Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ikiwa pia ni mkakati wa kukuza sekta ya Michezo nchini.

 

“Wizara imekamilisha agizo hili kwa kuhuisha Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni ambao umetengewa shilingi bilioni 1.5. 

Mfuko  huu kwa  mwaka ujao wa fedha utajikita katika ujenzi wa miuondombinu muhimu ikiwemo jengo la SANAA HOUSE hapa Dodoma, pia utaendelea  kutengewa fedha zaidi kwa lengo la kutekeleza  majukumu mawili adhimu; kuwajengea uwezo wanatasnia hizo za Sanaa na Utamaduni kupitia mafunzo na  kuwawezesha kupata mikopo na ruzuku katika kazi zao” amesisitiza Waziri Bashungwa

Monday, April 19, 2021

DKT. NCHIMBI ATOA FUTARI YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHAN KWA WAISLAMU SINGIDA

Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahanl  (kulia) akimkabidhi viazi vitamu Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida, Alhaj  Burhan Mlau vilivyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi kwa ajili ya futari ya mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu wa mkoa huo  jana.

 Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu  Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Singida Vijijini,  Amiri Kisuda, akizungumzia msaada huo.

Sehemu ya shehena ya viazi vilivyo tolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt.Rehema Nchimbi.

Viazi vya futari vikishushwa kwenye gari.

Viazi vya futari vikishushwa kwenye gari.

Viazi vya futari vikiingizwa ndani kabla ya kugawiwa waislamu..


 Muonekano wa Ofisi na Msikiti wa Bakwata Mkoa wa Singida.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa chakula kwa waumini wakiislamu mkoa huo  kama sehemu ya futari katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Akikabidhi msaada huo wa viazi kwa Msikiti wa Kati na Mandewa kwa niaba ya mkuu wa mkoa Kaimu Afisa Maendeleo Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahanl alisema Dkt. Nchimbi ametoa chakula hicho kwa makundi yasiyojiweza ndani ya waumini wa Kiislamu Mkoa huo ili waweze kufuturu na kufanya ibada yao kuwa kamili.

Alisema mkuu wa mkoa anawapongeza Waislamu wote kwa kuwa chachu ya maendeleo na kuuombea mkoa wa Singida na nchi yote kwa ujumla na amewaomba waumini hao kupitia mfungo huo  wa Ramadhani kuendelea kumuomba mwenyezi Mungu ili atuepushe na mambo mabaya yakiwemo magonjwa na kumuombea Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambaye ana muda mfupi wa kuongoza nchi baada ya aliyekuwa Rais Hayati Dkt. John Magufuli kufariki.

"Wajibu wa viongozi wa dini ni kutuombea sisi na Taifa kama tulivyoona juzi walivyofanya kongamano kubwa la kuombea dini pamoja na Hayati Dkt. Magufuli." alisema Ndahani. 

Aidha wakati akipokea msaada huo wa viazi Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida,  Alhaj Burhan Mlau alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwajali Waislamu kwani kila mwaka anakuwa wa kwanza kutoa futari kwa waumini hao.

“Nimpongeze Mama yetu mkuu wa mkoa kila mwaka haachi kutoa futari kwa Waislamu tena mwanzoni kabisa mwa mwezi, mwaka jana alitoa msaada kama huu na hii ni kawaida yake kwa maana miaka yote huwa anatoa futari kwa kumi la kwanza na la pili na kumi la tatu huwa anatoa futari kwa kutuwezesha waislamu hasa walengwa ambao hawana uwezo,  wazee, mayatima, masikini, wajane na mafukara nichukue nafasi hii kwa niaba ya waislamu kumshukuru Dkt. Nchimbi kwa sadaka hii Mwenyezi Mungu aendelee kumlinda na familia yake na kumpa moyo huo huo kwani wapo matajiri wengi lakini hawafanyi kama anavyofanya yeye.”alisema Mlau.

Alhaj Mlau alisema atahakikisha futari hiyo inawafikia walengwa ili kwa siku hizo chache waweze kufuturu na kupunguza makali ya mfungo.

 Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu  Tanzania (BAKWATA) Wilaya ya Singida Vijijini,  Amiri Kisuda alimshukuru Dkt.Nchimbi kwa kuwatia moyo waislamu katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan na kuwataka watu wengine kuiga mfano huo.

Futari ni mojawapo ya chakula cha kidini ambacho huliwa wakati wa Ramadani na mara nyingi hufanyika na jamii, yaani watu wanakusanyika ili kufuturu pamoja. Futari inachukuliwa tu kabla ya Magharibi, yaani machweo. Waislamu wengi wanaamini kuwa kulisha mtu kamatar kama namna ya sadaka na yenye manufaa sana na kwamba hayo yalifanywa hata na Mtume Muhammad.

MANISPAA YA SINGIDA WAPATIWA MAFUNZO YA TB NA UKIMWI KWA WATOTO

Katibu wa Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (MKUTA) Mkoa wa Singida, Michael Moses (katikati) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafunzo yaliyotolewa leo kwa madiwani na wakuu wa idara wa Manispaa ya Singida   juu ya kifua kikuu (TB) na ukimwi kwa watoto. Kushoto ni Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Salim Ali na Mratibu wa asasi kwa mikoa ya Tabora na Singida, Sadam Kidera.


Mwenyekiti wa Asasi hiyo, Salim Ali, akizungumza katika mkutano huo.

Mratibu wa asasi hiyo kwa mikoa ya Tabora na Singida, Sadam Kidera.  akizungumza katika mkutano huo.


Na Dotto Mwaibale, Singida


MADIWANI na wakuu wa idara wa Manispaa ya Singida wamepatiwa mafunzo ya siku juu ya kifua kikuu (TB) na ukimwi kwa watoto,kwa ajili ya kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukimwi.

Mafunzo hayo yametolewa na Asasi ya Mapambano ya Kifua Kikuu na Ukimwi Tanzania (MKUTA) kupitia mradi wa CAP TB-Singida kwa ufadhili wa EGPAF unaohusisha mikoa ya Tabora na Singida katika kukabiliana na tatizo la TB na Ukimwi kwa watoto.

Akizungumza jana katika mafunzo hayo Mratibu wa mradi huo wa mikoa hiyo,  Sadam Kidera alisema kuwa bado kuna imani potofu miongoni mwa jamii kwamba mtoto anapougua magonjwa hayo anaonekana kuwa  amerogwa.

Kutokana na hali hiyo alisema  watoto wanapobainika kuugua maradhi hayo ni vema jamii ikachua hatua za kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya badala ya kuamini imani za kishirikina.

"Ni vema na jukumu letu kuwafikishia wananchi na jamii kwa ujumla umuhimu na kutambua kwa kina zaidi kwamba ni suala la muhimu na msingi waweze kuchukua tahadhari  na elimu kutolewa jinsi gani ya kupata matibabu." alisema Kidera.

Aidha Kidera alibainisha kwamba magonjwa hayo ni hatari, hivyo ni vema jamii ikachukua hatua ya kukabiliana nayo mapema  kwa kuwa yanatibika.

Katibu wa Mkuta Mkoa wa Singida,  Michael Moses alisema kuwa jamii inapoona dalili za watoto wao kuugua Kifua Kikuu na Ukimwi inapaswa kuwapeleka mara moja kwenye vituo vya kutolea tiba, tayari kwa ajili ya kupatiwa matibabu sahihi.

Mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja mkoani Singida kuanzia Juni,  2020 na kufikia tamati juni mwaka huu utaiwezesha jamii kuwa na uelewa wa kutosha kuhusiana na magonjwa hayo. 

Saturday, April 17, 2021

RC DODOMA AWATAKA WAKAZI WA DODOMA KUCHANGAMKIA ELIMU YA BRELA

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge akitoa hotuba ya kufungua mafuzo ya siku mbili kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa Wakazi wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto, Jijini Dodoma leo.

Mafunzo yakifunguliwa.
Msaidizi wa Ofisi Mwandamizi wa  Utawala kutoka BRELA, Saada Kilabula (kulia) akizungumza kabla ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge (wa sita kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafuzo ya siku mbili kuhusu huduma zinazotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa Wakazi wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Makao Makuu.



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


MKUU wa Mkoa wa Dodoma,  Dkt Bilinith Mahenge amewataka wakazi wa mkoa huo kuchangamkia elimu inayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kuwa ina umuhimu mkubwa katika kujikwamua kiuchumi.

Dkt. Mahenge ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Wakazi wa Dodoma katika Ukumbi wa Mikutano uliopo Makao Makuu ya Jeshi la Zimamoto, Jijini Dodoma.

Akizungumza katika ufunguzi huo Dkt. Mahenge amewaeleza washiriki kwamba, ili kuweza kufanikiwa katika biashara ni vyema biashara au kazi husika kuwa imerasimishwa na kutambulika kisheria.

“Hatua ya kwanza ya kufanikiwa katika biashara ni kuirasimisha biashara na ikwa inatambulika kwa mujibu wa sheria. Na BRELA wapo hapa Dodoma kwa siku mbili kwa hiyo hii ni fursa kubwa na adhimu.”alisema Dkt. Mahenge.

Msimamizi wa Kanda ya kati na Ofisi ya BRELA mkoani Dodoma, Gabriel Girangay alisema kwamba licha ya elimu hii kwa wote inayotolewa kwa siku mbili lakini pia ofisi zipo tayari kwa ajili ya kuwa hudumia.

“Ofisi ya BRELA mkoani Dodoma ipo tayari kuwahudumia na inafanya maandalizi ya kufika katika wilaya zote tisa za Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi katika maeno yao kuhusu huduma zetu.”  alisema Girangay.

Aidha Girangay amewataka wadau wa BRELA walio katika mkoa wa Dodoma na kanda nzima ya kati, wasipate shida ya kwenda ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam na badala yake wafike katika Ofisi za BRELA mkoani Dodoma zilizopo katika Jengo la PSSSF eneo la Makole, Ghorofa ya 10.

Msaidizi wa Ofisi Mwandamizi wa  Utawala kutoka BRELA, Saada Kilabula amemshukuru Mkuu wa Mkoa Dkt. Mahenge kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu,  Godfrey Nyaisa kwa kuthamini uwepo wao ndani ya Dodoma na kuja kufungua mafunzo hayo.

BRELA inaendelea na mpango wa kutoa elimu kwa umma, ambapo kwa awamu ya kwanza mikoa sita itafikiwa ambayo ni Ruvuma, Njombe, Iringa, Singida, Dodoma na Morogoro.


SHIRIKA LA ESTL, UBALOZI WA FINLAND WANAENDELEA KUFUTA UKATILI MKOANI SINGIDA

Mtendaji Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la  Empower Society Transform Lives (ESTL), Joshua Ntandu Lissu, akizungumza katika kikao  kazi cha Kamati ya Ulinzi wa Mwanamke na Mtoto ngazi ya mkoa (MTAKUWWA) kilichoketi jana mkoani hapa.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Deogratius Hinza ambaye alikuwa mgeni rasmi akiwa katika kikao hicho na viongozi wengine. Kutoka  kulia ni  Mtendaji  Mkuu wa shirika hilo,  Joshua  Ntandu Lisu na Afisa Ustawi wa Jamii  Mkoa  wa Singida, Shukran Mbago.


Wajumbe wa MTAKUWWA wakiwa kwenye kikao hicho.
Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida, Shukuru Mbago, akizungumzia majukumu ya Mtakuwwa. kwenye kikao hicho.

Mratibu wa mradi kutoka shirika hilo , Annamaria Mashaka akitoa mada katika kikao hicho.

Kikao kikiendelea.
Mwezeshaji kutoka ESTL, Hawa Hussein akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana  Kata ya Kisaki wa kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkazi wa Kata ya Kisaki Debora James akichangia jambo  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana wa kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia.
Mkutano ukiendelea.
Afisa Maendeleo ya Jamii  Manispaa ya Singida, Tumaini Christopha, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana wa kuelimisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia.



Na Dotto Mwaibale,Singida.

SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojishughulisha na utoaji wa huduma ya uelimishaji jamii kuondokana na Ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukeketaji, na mila potofu katika Mkoa wa Singida kwa ufadhili wa Ubalozi wa Finland limewakutanisha kwa pamoja wajumbe wa kamati ya ulinzi wa mwanamke na mtoto (MTAKUWWA) ngazi ya mkoa kuangalia namna bora ya kupambana na ukatili.

Wajumbe hao ambao ni viongozi wa sekta na idara mbalimbali za serikali, Ngo's,viongozi wa dini na wawakilishi wa makundi ya watu wenye ulemavu na mwenyekiti wake ambaye ni katibu tawala mkoa wamekutana jana kwenye kikao kazi kujadili mbinu za  kukabiliana na ukatili.

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine imetoka na mapendekezo kadhaa ikiwemo kuiomba serikali kuanzisha mitaala ya elimu ya masuala ya ukatili wa kijinsia kwenye shule,na kuitaka sekretarieti ya kamati hiyo kuandaa utaratibu mzuri wa utoaji elimu ya ukatili kwa sekta na idara za serikali ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na ukatili.

Aidha wajumbe hao wameiomba serikali kutenga fedha ili kugharamikia vipimo vya vinasaba (DNA) inapotokea kesi za ukatili na kuhitajika vipimo kama ilivyo kwa sampuli zingine kwani mara nyingi hatua hizo zinashindwa kuchukuliwa kutokana na gharama.

Mtendaji Mkuu wa shirika hilo,  Joshua Ntandu Lisu aliomba ushirikiano zaidi kwenye kamati hiyo ili hatua za kukabiliana na ukatili ziendelee kusonga mbele na lengo hasa ni kupinga ukatili.

"Sisi kama shirika tutaendelea kuiwezesha kamati hii ya MTAKUWWA ili tuendelee kusonga mbele katika harakati za kupinga ukatili."alisema Lisu.

Wakati huo huo ESTL pia ilikutana na wananchi wa Kata ya Kisaki Manispaa ya Singida na kufanyanao mkutano wa hadhara wenye lengo la kutoa elimu ya ukatili na kutanabaisha madhara yatokanayo na ukatili hususani ukeketaji ambapo awali kabla ya mkutano huo shirika hilo liliendesha mafunzo kwa makundi ya vijana, viongozi wa dini na mangariba wastaafu pamoja na watu maarufu katika kata hiyo.