Thursday, July 22, 2021

RC SINGIDA AWATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA KUTOKA TAASISI YA PASS

Mkoa Singida Dkt.Binilith Mahenge, akizungumza na wadau wa kilimo wakati akifungua mkutano wa wadau hao jana ulioandaliwa na Taasisi ya mikopo ya Pass inayojishughulisha na utoaji wa mikopo na udhamini kwa wakulima.
Meneja Maendeleo ya Biashara wa Taasisi hiyo,  Hamisi Mmomi akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Taasisi hiyo kwenye mkutano huo.
Meneja wa Kanda ya Kati wa Taasisi hiyo,  Hadija Seif  akizungumza kwenye mkutano huo.
Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Wadau wa kilimo wakiwa kwenye mkutano huo.
 



Na Dotto Mwaibale, Singida 


MKUU wa Mkoa Singida Dkt.Binilith Mahenge amewataka wananchi wa mkoa huo kuchangamkia ujio wa Taasisi ya mikopo ya Pass inayojishughulisha na utoaji wa mikopo na udhamini kwa wakulima kama fursa kwao katika kilimo cha alizeti.

Dkt. Mahenge aliyasema hayo mjini hapa jana wakati akifungua mkutano wa wadau wa kilimo cha zao la alizeti ulioandaliwa na taasisi hiyo.

"Nawahasa wananchi wangu wa  Singida muichukulie taasisi ya Pass kuwa ni fursa moja wapo itakayowawezesha kuharakisha kuwaletea maendeleo," alisema Mahenge.

Alisema Serikali mkoani hapa itawapa Pass ushirikiano wa kutosha ili wananchi wapate huduma hizo muhimu zitakazo wainua kiuchumi kupitia kilimo cha alizeti.

Mahenge aliitaka  taasisi hiyo kupanua wigo wa kujenga uelewa kwa kufanya mikutano mbalimbali kuanzia ngazi ya wilaya jambo litakalosaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma bora kwa kutumia fursa ya uwepo wa Taasisi hiyo na mabenki kwa ufanisi zaidi.

Pia alisema itawezesha kutengeneza mazingira mazuri ya kuibua changamoto nyingi na kuendelea kuweka mazingira rafiki ya kukabiliana nazo ili kuyafikia mapinduzi ya kilimo.

Alisema wakulima wengi ni wadogo na bado wanatumia teknolojia duni lakini kupitia taasisi  kama hiyo wataweza kuweka mazingira rafiki ya kuwafikia wadau wengi wa sekta ya kilimo kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa haliwezi kuzifikia taasisi za kifedha kwa ufanisi.

Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa Taasisi hiyo Hamisi Mmomi akizungumza kwa niaba ya mkurugenzi wa Taasisi hiyo alisema tangu taasisi hiyo ianzishwe hadi kufikia mwezi Desemba mwaka jana tayari wamekwisha wakopesha wakopaji zaidi ya 46,000 na kudhamini mikopo ya Trioni 1.08.

Alisema katika wakopaji hao 46,000 wanufaika wa moja kwa moja ni zaidi ya milioni 1.6 kwa sababu wakopaji wengine kama vyama vya ushirika kuna wanachama kuanzia 50, 100 hadi 200 hivyo kufikisha idadi hiyo.

Alisema mikopo hiyo imetengeneza ajira zaidi ya milioni 2.5 kutokana na wakulima kuajiri wakulima na kuwa mikopo hiyo wakopaji wamekuwa wakiirejesha kwa wakati kutokana na utaratibu mzuri waliouweka wa kuipitia  miradi walioikopea fedha hizo.

MUME AUA MKE SINGIDA AKIOMBWA HELA YA ADA YA MTOTO


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya jeshi hilo mkoani hapa leo hii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa, akiwaonesha  waandishi wa habari (hawapo pichani) misokoto ya bangi iliyokamatwa na jeshi hilo.
 


Na Dotto Mwaibale, Singida

MWANAMKE mmoja Moshi Mkimbu (40)  mkazi wa Kijiji cha Ndulungu Tarafa ya Ndago Wilaya ya Iramba  mkoani Singida ameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali  na mume wake aitwaye Juma Shabani.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi (ACP) Stella Mutabihirwa akizungumza na waandishi wa habari leo  aamethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo lilitokea Julai 18, 2021 katika  kitongoji cha Misughaa na kuwa  mtuhumiwa  alikamatwa na atafikishwa mahakamani  kujibu shitaka  lake. 

Mutabihirwa alisema kuwa uchunguzi  wa  awali wa Jeshi la polisi  umebaini kuwa chanzo kikubwa cha mauaji  hayo  ni  ugomvi  wa  kifamilia  pamoja  na ulevi  baada ya  marehemu  kudai  pesa za  mahindi  yaliyouzwa  kwa  ajili ya ada ya mtoto shuleni, ndipo mume wake  huyo alianza  kumshambulia kwa kumpiga na fimbo na kitu  chenye  ncha kali na kusababisha kifo cha mke wake. 

Katika tukio lingine alisema jeshi hilo mkoani hapa linaendelea na misako mbalimbali ya kubaini uhalifu kutokana na mikakati iliyojiwekea ya kuweka mkoa wa singida salama ambapo kwa kipindi cha miezi mitatu Aprili hadi Julai 2021, Jeshi la polisi limefanya misako na kufanikiwa kukakamata dawa aina bhangi misokoto 757 watuhumiwa tisa (9), watuhumiwa saba kesi zipo mahakamani hatua ya kusikilizwa na watuhumiwa wawili wametiwa hatiana.

Alisema mtuhumiwa mmoja wa dawa za kulevya  aina heroine kete moja alikamatwa  na kesi ipo mahakamani na  Pombe ya moshi (gongo) lita 113 zilikamatwa na watuhumiwa  24   ambapo watuhumiwa walifikishwa  mahakamani.  

"Kesi 16 watuhumiwa walitiwa hatiani na watuhumiwa 8 kesi bado zinaendelea mahakamani hatua ya kusikilizwa na pia pikipiki moja aina ya SANLG ilikamatwa baada ya pikipiki hiyo kuporwa  na mtuhumiwa mmoja ambaye alikamatwa na alifikishwa mahakamani na tayari  amehukumiwa kutumikia jela mwaka mmoja," alisema.

Mutabihirwa  ametoa shukrani kwa wananchi na raia wema kwa kutoa ushirikiano na kupata mafanikio hayo hivyo  wito wa jeshi hilo kwa  wananchi  wote hususani  wanandoa  kuacha tabia na vitendo  vya  ukatili wa kijinsia katika  familia zinazo wazunguka na kuwatengemea kwani vitendo hivi hupelekea madhara makubwa  na  kusababisha  vifo  katika jamii. 

Aidha Mutabihirwa amewataka wananchi kuacha tabia ya ulevi uliopindukia na matumizi ya dawa kulevya bali waishi  kwa amani, furaha na  kufuata sheria za nchi na pindi matatizo ya kifamilia yanapotokea wafike kwenye vituo vya Polisi kwenye madawati maalumu ya kushughulikia  masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto na si kujichukulia sheria 
mkononi.

Wednesday, July 21, 2021

MWENGE WA UHURU WAPITISHA MIRADI YOTE WILAYANI IRAMBA, DC AMWAGIWA SIFA

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru  Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi akizindua mradi mkubwa wa maji uliopo katika Kijiji cha Kyalosangi Kata ya Kinampanda wilayani Iramba jana.
Mwonekano wa Tanki la maji la mradi huo.
Baadhi ya mabanda yaliyotembelewa na Mwenge wa Uhuru.



Mkuu wa wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda akipanda mti wakati Mwenge wa Uhuru ukiwa katika wilaya hiyo.
 Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Luteni Josephine Mwambash akipanda mti wakati Mwenge huo  ukiwa katika wilaya hiyo.


 

Na Dotto Mwaibale, Iramba.


MWENGE wa Uhuru ambao umemaliza mbio zake za kukagua miradi ya maendeleo wilayani Iramba mkoani Singida leo na kukabidhiwa Wilaya ya Mkalama umeridhishwa na miradi yote huku Mkuu wa wilaya hiyo akimwagiwa sifa.

Baadhi ya miradi iliyopitishwa ni mradi mkubwa wa maji uliopo katika Kijiji cha Kyalosangi Kata ya Kinampanda ambao ulizinduliwa na Mkimbiza Mwenge wa Uhuru  Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi ambaye aliongozana na Mkuu wa wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda na viongozi wengine.

Mradi huo mkubwa wenye tanki la lita 50,000 kwenye mnara wa mita 6, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 5 umegharimu Sh. Milioni 150, 589, 732.72 na umeongeza upatikanaji wa maji kwa asilimia 1.98 na kufikia asilimia 61 wilayani Iramba. 

Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa Luteni Josephine Mwambashi alitembelea pia chanzo cha mradi huo na kuridhishwa na mradi huo na kuufungua  "Tumeona kuna kisima na tumepanda kwenye tanki tumeshuhudia kuna maji, tumeona pia nyaraka  ziko vizuri  na tumeona mabomba na vituo vya kuchotea maji na wananchi wanapata huduma ya maji hivyo nauzindua mradi huu na sasa nakata utepe " alisema Mwambashi.

Mwambashi alimpongeza Mkuu wa Wilaya hiyo Suleiman Mwenda kwa kusimamia vizuri fedha za Serikali katika kutekeleza miradi hiyo yote yenye manufaa makubwa kwa wananchi.

ANSWAR SUNNA SINGIDA WAFANYA IBADA YA EID EL HAJJ


Waumini wa dini ya Kiislamu dhehebu la Answar Sunna mkoani hapa wakiadhimisha ibada ya Idd Al Adha iliyofanyika jana.

Ibada ikiendelea.

Wanawake wakiwa kwenye ibada hiyo.
Swala ikifanyika.
Swala ikifanyika.
Swala ikifanyika.
 


Na Mwandishi Wetu, Singida 

MAMIA ya waumini wa dini ya Kiislamu dhehebu la Answar Sunna mkoani hapa wameadhimisha ibada ya Idd Al Adha huku ujumbe mkubwa ukiwakumbusha kutowasahau masikini.

Akiongoza ibada hiyo iliyofanyika jana kwenye viwanja vya msikiti wa Al Omary jirani na stendi kuu ya mabasi Misuna, Shekhe Yaqin Said Nkokoo alisema Mwenyezi Mungu hatazami mwili wala  umaarufu wa mwanadamu bali hutazama nyoyo zilizopambwa matendo mema na ucha-Mungu.

Alisema hata mwanadamu awe na umbo zuri, sura nzuri au maarufu kwa kiwango cha juu cha kidunia haina maana yoyote kama matendo yake ni chukizo mbele ya mola wake.

"Tunapokufa kinachochukuliwa ni roho pekee na sio mwili. Hata kama ulikuwa maarufu, una cheo kikubwa au mzuri wa sura na mwili kiasi gani vyote hivyo vitafukiwa ardhini na kuliwa na wadudu," alisema Sheikh Nkokoo.

Alisema kujizuia kutowataja watu kwa mabaya, kumcha Mungu, kuepuka kufanya maasi na kuwajali wahitaji na masikini ni wajibu kwa kila muumini wa dini ya kiislamu na ndio hasa msingi wa sunna za ibada ya Eid el Hajj.

Alisisitiza katika ibada kamilifu ya swala hiyo watu hutakiwa kuchinja mnyama kama kondoo, mbuzi au ng'ombe na kisha kuwapatia masikini, ndugu na majirani na kisha familia ili kujiongezea thawabu mbele ya Mwenyezi Mungu.

Aliongeza kuwa chimbuko la sikukuu hiyo ambayo huheshimiwa kama miongoni mwa sikukuu kubwa kwa waislamu duniani kote linapaswa kuchagiza imani ya kila muumini wa dini hiyo kwa tathmini ya matendo ya moyo wake angali yu hai kwa mfano halisi wa utii wa Ibrahim kwa mola wake dhidi ya jaribio la kiimani la kutaka kumchinja mwanawe.

Sheikh Nkokoo alisema uchinjaji huo ambao hufanyika baada ya swala ya Idd ni kumbukumbu ya sadaka ya Nabii Ibrahim ambaye anatajwa kwenye Kurani kuwa alikuwa tayari kumchinja mwanawe wa pekee Ismail kama sadaka kwa Mwenyezi Mungu, lakini hata hivyo, Mungu alimzuia asimchinje na akampatia mnyama kondoo amchinje badala yake.

"Sikukuu hii ambayo hupatikana katika mwezi huu wa Dhul Hijjah ni sunna iliyosisitizwa kuwa ni wajibu kwa kila aliye na uwezo, na thawabu yake ni kubwa," alisema.

Tuesday, July 20, 2021

MAANDALIZI IBADA YA CHINJA YAMEKAMILIKA KIJIJI CHA MSIU MKALAMA SINGIDA

Wadau kutoka Uturuki wakiwaangalia ng'ombe watakao chinjwa kesho kwenye ibada ya chinja itakayofanyika Kijiji cha Msiu wilayani Mkalama mkoani Singida. Ng'ombe hao wametolewa na Taasisi ya International Humanitarian Education of Torkey kutoka nchini Uturuki.
Baadhi ya Wazee wa Kijiji cha Msiu wakiwakaribisha wageni.
Ng'ombe watakao chinjwa kesho.
Sheikh wa Wilaya ya Mkalama Miraji Ibrahim akizungumzia ibada hiyo.
 Wazee wa Kijiji cha Msiu na wageni wao wakiwaangalia ng'ombe hao watakaochinjwa kesho.
Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro akitoa maelezo na taratibu za ibada hiyo.
 



Boniphace Jilili na Dotto Mwaibale, Singida


TAASISI za kiislamu zinazohusika na ibada ya kuchinja zimetakiwa kutekeleza ibada hiyo kwanza kwa walengwa badala ya kuwaweka nyuma.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Singida Issa Nassoro wakati wakikagua na Taasisi iliyotoa sadaka ya wanyama watakao chinjwa eneo litakalo tumika kwa ajili ya kuchinja ambalo lipo katika kijiji cha Msiu Wilayani Mkalama.

Sheikh Nassoro alisema ibada hiyo inalenga kuwasaidia watu wasiojiweza lakini mara nyingi walengwa huo huwekwa nyuma jambalo linaondoa maana halisi ya ibada hiyo.

Katika ibada hiyo inayotarajiwa kufanyika siku ya jumatano wiki hii zaidi ya ng'ombe 2,000 na Kondoo 4,000 watachinjwa ambapo wanyama hao wametolewa na Taasisi ya International Humanitarian Education of Torkey kutoka nchini Uturuki.

Aidha Sheikh Nassoro aliwashukuru wadau hao na kuwaomba pamoja na Taasisi zingine kupana wigo katika misaada wanayoitoa kwa kusaidia hata katika masuala ya Elimu,Maji na mambo mengine kwani bado jamii inahitaji misaada yao mbali na kupatiwa nyama.

Naye Mkurugenzi wa kanda ya kati kutoka Taasisi ya Education Gauge Growth Tanzania (EGG TZ) Abeid Husen al maarufu Bin Skinen alisema kuchinja ni sehemu muhimu ya ibada kwa mwiislamu hivyo walichokifanya hao waturuki ni zaidi ya Ibada.

Alisema watalisimamia zoezi hilo ili liweze kufanyika kwa utaratibu mzuri na kila mtu atakaye fika atapata nyama bila kujali itikadi wala nafasi ya mtu.

Kwa upande wake Sheikh wa Wilaya Miraji Ibrahim alishukuru ibada hiyo kufanyika kwenye wilaya yake na tayari maandalizi yanaendelea kufanyika.

MWENGE WA UHURU WAWASILI SINGIDA KUZINDUA MIRADI YA ZAIDI YA SH. 8 BILIONI

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Dk. Balozi Batilda Buriani akimkabidhi Mwenge wa Uhuru 2021 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba baada ya kuhitimisha mbio zake mkoani humo leo. Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani hapa unatarajiwa kupitia miradi mbalimbali yenye thamani ya Sh.8,182,219,653.99.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge, akisoma taarifa ya mkoa wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Binilith Mahenge akimkabidhi Mwenge wa Uhuru 2021 Mkuu wa Wilaya ya Iramba Selemani Mwenda kwa ajili ya kuanza mbio zake wilayani humo
    Mwenge wa Uhuru ukipokelewa.
Mwenge wa Uhuru ukipokelewa.
Viongozi mbalimbali wakiwa katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Viongozi mbalimbali wakipiga makofi kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Utambulisho ukifanyika


Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACAF) Ivo Ombella aliwa ameushika Mwenge wa Uhuru.


Askari wakiwa wameuzunguka Mwenge wa Uhuru kwa ajili ya usalama..



Mkuu wa Wilaya ya Iramba Selemani Mwenda, akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru.


Watumishi wa Idara  mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba wakiwa  kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru.
Wananchi na Vijana wa Skauti mapokezi wa Mwenge wa Uhuru.
Vijana wa Skauti wakimvika Skafu mmoja wa wakimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa.
Vijana wa Skauti wakiimarisha ulinzi wakati wa kuupokea Mwenge baada ya kuwasili wilayani Iramba katika Kijiji cha Mseko.
Vijana wa Skauti  wakiwa imara wakati wa mapokezi wa Mwenge wa Uhuru.
 Mkuu wa Wilaya ya Iramba Selemani Mwenda , akikabidhiwa Mwenge wa Uhuru.
Mwenge wa Uhuru ukikabidhiwa kwa Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kabla ya kuanzwa kukimbizwa katika wilaya hiyo.


Ulinzi ukiimarishwa kwenye mapokezi hayo

 



Na Dotto Mwaibale, Iramba Singida.


SERIKALI Mkoa wa Singida kwa kushirikiana na wananchi mapema leo asubuhi wameupokea Mwenge wa Uhuru ukitokea mkoani Tabora.

Miradi  yenye  thamani ya Sh. 8,182,219,653.99 inatarajiwa kupitiwa na Mwenge wa Uhuru 2021, mkoani hapa ambao mbio zake zimeanza katika Wilaya ya Iramba.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa Mwenge huo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk.Balozi Batilda Buriani katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk.Binilith Mahenge alisema  Mwenge huo utakimbizwa kwa muda wa siku tano  katika wilaya tano kwa kuanzia na Wilaya ya Iramba na utahitimisha mbio zake Julai 24/2021 ambapo utakabidhiwa Mkoa wa Dodoma.

Alisema Mwenge wa Uhuru utakapokuwa Mkoani hapa  utakimbizwa jumla ya kilometa 642.3, utapitia jumla ya miradi 55 inayohusu TEHAMA, Elimu, Afya, Mazingira, Maji, Biashara, Barabara na Programu za Rushwa, Malaria, mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya,VVU/UKIMWI na Lishe.Miradi 9 itazinduliwa, miradi 2 itafanyiwa ufunguzi, miradi 6 itawekwa jiwe la msingi, miradi 36 itakaguliwa na Miradi 2 itatembelewa. 

Alisema miradi yote itakayopitiwa na mwenge huo itakuwa na thamani ya Sh. 8,182,219,653.99 ambapo alitoa mchanganuo wake kuwa nguvu za wananchi ni Sh. 1,957,623,652.58, Halmashauri Sh. 69,630,194.42, Serikali Kuu Sh.4,627,922,247.27 na Wahisani sh.1,527,043,559.72.

Alisema  ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka2021 ambao utatolewa maeneo mbalimbali ya Wilaya za Mkoa wa Singida ni “Matumizi Sahihi ya TEHAMA” chini ya Kauli Mbiu inayosema  TEHAMA ni Msingi wa Taifa Endelevu;Itumike kwa Usahihi na Uwajibikaji.

Dk. Mahenge alisema Mkoa wa Singida umekuwa ukiamini kuwa TEHAMA ni msingi wa maendeleo endelevu, kwani matumizi sahihi ya miundombinu na mifumo ya TEHAMA yamewezesha kurahisisha mawasiliano, ukusanyaji na kuongeza mapato ya Serikali, kudhibiti matumizi ya Fedha za Umma, kuongeza uwazi na uwajibikaji katika kuwatumikia Wananchi, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi,kurahisisha taratibu za manunuzi ya Umma na kuondoa mianya ya rushwa na ubadhilifu, urahisi kwa wananchi kulipia ankara mbalimbali, kurahisisha na kuwezesha upatikanaji wa Takwimu mbalimbali kwa usahihi na kwa wakati.

" Kwa kutambua faida hizi zitokanazo na matumizi sahihi ya TEHAMA, Mkoa wa Singida umeendelea kusimamia mifumo ya TEHAMA zaidi ya 30 inayotumika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekretarieti ya Mkoa pamoja na Taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa wa Singida," Mahenge.

Alitaja baadhi  ya Mifumo ya TEHAMA inayotumika katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine ni pamoja na mifumo ya fedha ya ukusanyaji wa mapato na matumizi ambayo ni ‘Local Government Revenue Collection Information System (LGRCIS)’, ‘e-Revenue Management System’ unaotumiwa na TARURA.  Mifumo ya uhasibu Serikalini (MUSE)naFFARS. 

Aidha Dk. Mahenge alitaja mfumo mwingine kuwa ni wa TEHAMA wa TANEPs unahusika na Manunuzi ya Umma, Mfumo GoTHOMIS unatumika kudhibiti makusanyo ya vituo vya kutolea huduma za Afya pamoja na upotevu wa dawa na vifaa tiba, mfumo waTEHAMA wa ukusanyaji wa takwimu za Kilimo (ARDS), mifumoya PREM, PREMs, School Information System (SIS) na Annual School Sensor (ASC) kwaajili ya kupata takwimu sahihi za elimu na mfumo wa (HCMIS)) kwaajili ya Taarifa za kiutumishi na Mishahara.


Monday, July 19, 2021

MTATURU ACHANGISHA MILIONI 10 UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI KIJIJI CHA MATONGO IKUNGI

Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Matongo  wakati akiongoza harambee ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Matongo iliyofanyika Kata ya  Ikungi mkoani Singida juzi.
Wanafunzi wakiongoza  msafara wa Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu wakati alipofika kukagua ujenzi wa madarasa ya Shule ya Msingi ya  Kitongoji cha Mwau.
Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu akizungumza na Wananchi wa Kitongoji cha Mwau.
Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, akikagua ujenzi wa Shule ya Msingi ya Mbughantigha.


Harambee ikiendelea.
Wananchi wakiwa kwenye harambee hiyo.
Wananchi wakiwa kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea.
 Diwani wa Kata ya Ikungi itakapojengwa shule hiyo, Abel Nkuwi akizungumza kwenye harambee hiyo.
Mwalimu Yesaya Benjamin  akizungumza kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Matongo, Abubakari Selemani, akizungumza kwenye harambee hiyo.
Burudani zikitolewa kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea.
Diwani wa Viti Maalumu, Magreth Philemon akizungumza kwenye harambee hiyo wakati akichangia.
Askari Polisi Justine Dominic kutoka Kituo cha Polisi cha Kijiji cha Matongo akichangia Sh.50,000 kwenye harambee hiyo.
Harambee ikiendelea.
Harambee ikiendelea.
Mbunge wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu, akipokea saruji iliyotolewa na vikundi mbalimbali.


Dotto Mwaibale Singida


MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu ameendesha harambee ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kijiji cha Matongo iliyopo  wilayani Ikungi mkoani Singida ambapo zaidi ya Sh..10 milioni zilipatikana.

Mtaturu ambaye alikuwa mgeni rasmi alitoa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya kuanza kufyatua matofali ili ujenzi huo uanze mara moja.

Katika harambe hiyo  wananchi na wadau mbalimbali wa elimu walishirikishwa ambapo licha ya kupatikana fedha hizo pia ilipatikana mifuko ya saruji 259, malori ya mchanga 15, bati bando mbili, matofali 1000 na matela ya mchanga 10.

Fedha na michango hiyo inakwenda kuanza kujenga madarasa  na kutatua adha ya wanafunzi wa kijiji hicho ambao wanatembea umbali wa kilometa 13 kwenda kusoma  Shule ya Sekondari ya Ikungi Mchanganyiko jambo linalowasababishia  kushindwa kuhudhuria vizuri masomo yao.

Akizungumza juzi katika harambe hiyo Mtaturu aliwaambia wananchi  wa kijiji  hicho kuwa elimu ndio mkombozi na kila mtu anawajibu wa kuchangia ambapo aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya shule na kutoa elimu bure bila malipo kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.

Alisema Serikali itaendelea kujenga miundombinu ya elimu, kuongeza idadi ya walimu na kujali maslahi yao hivyo aliwaomba wafanye kazi kwa bidii kwani Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda watumishi wote hapa nchini.

Mtaturu alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi hao kuwa Serikali imepanga kuboresha miundombinu ya barabara katika jimbo hilo la Singida Mashariki ambapo nje ya bajeti yake ya mwaka huu imetoa Sh 1.5 Bilioni kwa kazi hiyo.

Akizungumzia sekta ya afya alisema  Serikali  katika bajeti yake ya mwaka huu imeongeza fedha ukilinganisha na ya mwaka wa fedha uliopita.

Alisema serikali mbali ya kuboresha miundombinu ya barabara itapeleka umeme na maji katika maeneo yote ya jimbo hilo kikiwemo kijiji hicho cha Matongo.

Katika hatua nyingine Mitaturu amechangia mabati 200 kwa ajili ya kupaua madarasa mawili ya shule shikizi ya kitongoji cha Mwau ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi.

 Kukamilika kwa madarasa hayo kutawapunguzia changamoto watoto wa eneo hilo kutembea umbali wa kilometa saba kila siku kwenda Matongo kwa ajili ya kupata elimu.

Akizungumza na wananchi wa Kitongoji cha Mbughantigha wakati akikagua ujenzi wa madarasa mawili yaliyojengwa kwa nguvu zao aliwataka wajenge madarasa mengine mawili na nyumba ya mwalimu ili shule hiyo iweze kupata usajili.

Mtaturu alisema wametoka kwenye Bajeti ya Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imelenga kuwaletea wananchi maendeleo. 

"Tunamshukuru sana Rais kwa kuonyesha upendo mkubwa kwa watanzania tumuunge mkono," alisema Mtaturu.

Diwani wa Kata ya Ikungi Abel Nkuwi alisema wanadhamira ya kujenga shule hiyo ya sekondari katika kijiji hicho ili kuwasaidia watoto ambao wanatembea umbali mrefu kwenda Ikungi kupata elimu.

Alisema kwa utangulizi ujenzi wa shule hiyo utagharimu sh.72 milioni na kuwa wamepanga kila mwananchi mwenye uwezo katika eneo hilo achangie sh.15,000 ambapo wanatarajia kupata Sh. Milioni 48 hivyo kuanza mara moja kazi ya ujenzi huku fedha zingine zikitokana na harambee hiyo na vyanzo vingine.

Mwanafunzi Nani Aley wa kidato cha pili anayetoka katika kijiji hicho kwenda kusoma Sekondari ya Ikungi Mchanganyiko alisema kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo kutawaondolea changamoto ya kutembea kila siku kwenda shuleni na kuwapunguzia mzigo wa gharama wazazi wao kwa kuwapangia nyumba za kuishi wakiwa shuleni Ikungi.

Aley alitumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa elimu bure pasipo malipo pamoja na Mbunge wao Mtaturu, Diwani wa Kata hiyo na viongozi wote na wananchi kwa kuanza mchakato wa ujenzi wa sekondari katika kijiji hicho.