Tuesday, November 23, 2021

REA YAMUAHIDI MATOKEO CHANYA MKUU WA MKOA WA RUVUMA

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (katikati), akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia) wakati viongozi hao walipokuwa katika ziara ya kazi mkoani Ruvuma jana.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge akisisitiza jambo wakati alipokuwa akizungumza na Ujumbe wa Viongozi Wakuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (hawapo pichani), walipomtembelea ofisini kwake wakiwa katika ziara ya kazi mkoani humo jana. Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto), akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (kulia). Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy. Viongozi hao walimtembelea Mkuu wa Mkoa ofisini kwake, wakiwa katika ziara ya kazi mkoani humo jana.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Ruvuma, Oddo Kilian Mwisho (kulia) akizungumza wakati wa kikao baina ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto) aliyefuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Mhandisi Hassan Saidy (wa kwanza kushoto), jana.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (kulia) akifafanua jambo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto) na Ujumbe wake, wakati wa ziara ya viongozi hao mkoani Ruvuma, kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini jana.
Msimamizi wa miradi ya REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Daniel Mwandupe, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (hayupo pichani), wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini, Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Hassan Saidy (hawapo pichani)
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge (wa tatu-kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo (wa pili-kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy (wa pili-kulia) pamoja na Ujumbe waliofuatana nao katika ziara ya kazi mkoani humo jana. Wa tatu kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Oddo Kilian Mwisho.
Kazi ya kufunga miundombinu ya umeme katika kijiji cha Namatui, Songea ikiendelea wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy mkoani Ruvuma.


 Na Veronica Simba - REA  

Uongozi wa Juu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umetoa ahadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge kuwa miradi ya nishati vijijini inayotekelezwa katika mkoa huo itasimamiwa kikamilifu na kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao na Mkuu wa Mkoa ofisini kwake, Novemba 22 mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy walisema kuwa Wakala umejipanga kushughulikia changamoto zote zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali, Mkuu wa Mkoa aliwaeleza viongozi hao uwepo wa changamoto ya Mkandarasi Namis Corporate Ltd kutotekeleza kwa kasi inayotakiwa, Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza.

Akieleza mkakati uliowekwa kutatua changamoto hiyo, Wakili Kalolo alieleza kuwa, Bodi imemtaka Mkandarasi husika kuhakikisha anakamilisha Mradi huo, siyo zaidi ya Desemba 31, 2021 vinginevyo atachukuliwa hatua za kimkataba.

Vilevile, Mkandarasi huyo ameagizwa kutengeneza Mpango-Kazi wa kila wiki ukionesha kazi atakayoifanya, atawasha umeme katika kijiji gani na muda gani na kuuwasilisha kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ambako kazi inafanyika pamoja na Diwani wa eneo husika ili waweze pia kufuatilia utekelezaji wake.

Aidha, alisema kuwa Bodi imemwagiza Mkandarasi kuongeza magenge ya kazi na kuhakikisha hayapungui matano pamoja na kuongeza wafanyakazi wenye ujuzi na kujituma ili kazi iweze kukamilishwa kwa wakati.

Akieleza zaidi, Mwenyekiti wa Bodi alisema imebainika kuwa Mshauri Mwelekezi wa Mradi amechangia pia katika ucheleweshwaji wa Mradi kutokana na kutotekeleza wajibu wake ipasavyo, hivyo Bodi imemwagiza kubadilika mara moja na kutimiza wajibu wake kikamilifu.

“Yeye ndiye anapaswa kututaarifu sisi kuhusu utendaji kazi wa Mkandarasi lakini hakuna ripoti yoyote aliyoileta rasmi kueleza matatizo ya Mkandarasi.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa REA alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuwa Serikali haitatoa muda wa nyongeza wa kukamilisha miradi hiyo.

Pia, aliwasisitiza kuhakikisha wanafanya kazi kwa kadri ya michoro ilivyo na endapo kutakuwa na tofauti yoyote basi ni lazima kwanza wapitie TANESCO na kwa Mshauri Mwelekezi kabla hawajabadilisha mchoro wowote.

Vilevile, aliwataka kuhakikisha wanawadhibiti wafanyakazi wao kutojihusisha na vitendo vyovyote vya rushwa na matumizi ya lugha zisizofaa pamoja na kuwazuia wafanyakazi hao kujihusisha. 

na kazi za kufanya ‘wiring’ katika nyumba za wananchi na majengo mbalimbali kwani ni kinyume cha mkataba.

“Hii ni miradi ya serikali hivyo ni lazima itekelezwe kwa kuzingatia taratibu,” alisisitiza Mhandisi Saidy.

Aidha, aliwataka wakandarasi kuhakikisha wanaagiza na kutumia vifaa vyenye ubora huku akisisitiza kuwa mkandarasi atakayetumia vifaa visivyo na ubora ajue kuwa anafanya hivyo kwa gharama zake binafsi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza na wa Pili mkoa wa Ruvuma, Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Kusini, Mhandisi Daniel Mwandupe alieleza kuwa, mzunguko wa kwanza wa mradi hadi kukamilika kwake, utagharimu shilingi za kitanzania 43,869,003,071.89 na fedha za kimarekani dola 7,483,076.98.

Alisema kuwa, katika mzunguko wa kwanza wa mradi, vijiji 144 vimepatiwa umeme kati ya vijiji 177 sawa na asilimia 81.4. Aidha, wateja 7,004 wa awali wameunganishwa kati ya lengo la kuunganisha wateja 9,778 mradi utakapokamilika.

Kwa upande wa mzunguko wa pili wa mradi, Mhandisi Mwandupe alieleza kuwa jumla ya vijiji 265 vya mkoa wa Ruvuma ambavyo havijafikiwa na umeme kati ya 554 vilivyopo, vitapelekewa umeme na kuunganisha wateja wa awali 5,170. Mradi utagharimu shilingi za kitanzania bilioni 71.95.

Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa aliushukuru Uongozi wa REA na wa Wizara ya Nishati kwa ujumla wake, kwa ushirikiano mzuri ambao wamekuwa wakiutoa kwa Ofisi yake katika kusimamia utekelezaji wa miradi ya nishati vijijini.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini na Mkurugenzi Mkuu wa REA, wako katika ziara kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati vijijini katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani.


KANISA LA ABC LAFANYA MAOMBI MAALUMU YA KULIOMBEA TAIFA

Askofu Kiongozi wa Kanisa la Abundant Blessing Center (ABC) la Tabata jijini Dar es Salaam,  Flaston Ndabila akiliombea Taifa kwa kuishika bendera ya Taifa katika maombi hayo maalumu.

Askofu Ndabila akiwa kwenye maombi hayo.
Mchungaji Lois Malali wa Kanisa la ABC Kibaha, akiwa katika maombi hayo.
Mke wa Askofu Ndabila Janeth Ndabila akifanya maombi ya kuliombea Taifa.
Maombi yakiendelea.
Maombi yakifanyika.
Askofu Ndabila (kushoto) akiwa kwenye maombi hayo.
Waumini na viongozi mbalimbali wa kanisa hilo wakiwa katika maombi.
Maombi yakifanyika.
Wanakwaya wa Kanisa hilo wakiwa kwenye maombi.
Maombi ya kuliombea Bara la Afika yakifanyika.
Picha ya pamoja baada ya kufanyika maombi hayo.




Na Dotto Mwaibale


KANISA la Abundant Blessing Center (ABC) la Tabata jijini Dar es Salaam limefanya maombi maalumu ya kuliombea Taifa na  kumshukuru Mungu kwa kumpa ulinzi Rais Samia Suluhu Hassan.

Maombi hayo yaliongozwa na Askofu Kiongozi wa Kanisa hilo Flaston Ndabila kwa kushirikiana na 
wakristo yalifanyika mwishoni mwa wiki.

Akizungumza katika maombi  hayo Askofu Ndabila aliwasisitiza  viongozi wa kikristo na wakiristo wote kushiriki maombi ya kushukuru na kuitamkia nchi yetu mema kila jumamosi ya tatu ya mwezi kwa kushirikiana na wakristo wote dunia ambapo pia aliishukuru huduma ya IGO Africa For Jesus Prayer Movement kwa kuwaunganisha wakriso  ulimwenguni kote kufanya maombi hayo.

"Nimpongeza  Dkt. Nicku Kyungu Mordi mtanzania aishie Marekani kwa kuiongoza huduma hii ya Igo Africa For Jesus Prayer Movement kwa miaka 28" alisema Ndabila.
   Aidha Ndabila alimshukuru Mungu kwa kuliwezesha taifa letu kuwa na amani na utulivu na kutekeleza miradi yote ya maendeleo.
 Ndabila alimuomba Mungu aliepushe taifa letu na Afrika kwa ujumla na vitendo vya ugaidi na 
kuilinda mipaka yetu ili amani iendelee kutamalaki nchini.

Pia Ndabila alimuomba Mungu atuepushe na vitendo vya ushoga, usagaji, ulawiti, utumiaji wa dawa za
kulevya, ulevi, rushwa na maovu mengine.

Ndabila alivitaka vyombo vinavyosimamia sheria, polisi, mahakama, usalama wa taifa kutenda haki 
na akamuomba Mungu awape hekima waliopewa dhamana hiyo wafanye kazi zao kwa hofu ya Mungu.

Mchungaji wa Kanisa la ABC Kibaha, Lois Malali akiongoza maombi ya kumshukuru Mungu kumpa ulinzi Rais Samia alisema kama kanisa wanaamini Mungu ataendelea kumlinda dhidi ya maadui wa nchi yetu.

“Tumuombee Rais wetu Samia Suluhu Hassan moyo wa hekima, busara na ustahimilivu wa kuweza 
kupambanua mema na mabaya kwa ajili ya nchi yetu,” alisema Malali.

 Mchungaji Msaidizi wa Uamusho wa Kanisa la Pentekosti la Shekilango jijini Dar es Salaam, Mupana 
Venuster alimshukuru Mungu kwa ajili ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, baraza la mawaziri, majaji, 
mahakimu, Spika wa Bunge Job Ndugai na wabunge kwa kuiongoza vyema nchi yetu.

Venuster alimuomba Mungu awajalie hekima ya kulipenda taifa letu na kuwa na nia ya kulijenga.

“Mungu awape ulinzi maalumu kwa wanaofanya mambo ya kuwasaidia wananchi iwe kwenye idara za
serikali, mahakama, bunge awajalie kukataa mikataba na maamuzi mabaya ya kuliangamiza taifa 
letu,” alisema Venuster.

Mchungaji Jema Fungo wa Huduma ya Maombi Kibaha alimshukuru Mungu kwa kutupatia mvua za masika na vuli tangu nchi yetu ilipopata uhuru miaka 60 iliyopita na kumsihi afanye hivyo katika kipindi hiki na azibariki kazi za mikono yetu.

Fungo alimuomba Mungu atupe mvua ya neema isiyokuwa na madhara na amani itawale kwenye mipaka yetu na nchi yetu isikumbwe na njaa.

Mke wa Askofu Ndabila, Janeth Ndabila akiongoza maombi ya kuiombea jamii alimsihi Mungu awaondoe watu wabaya wanaotaka kuiharibu jamii ya kitanzania hususan vijana wanaotumia vibaya mitandao ya 
kijamii.

“Tunaikataa hali inayoendelea sasa katika mitandao ya kijamii na familia, maneno yasiyofaa ya 
kujipendekeza bila kujali madhara yake na maneno ya unafiki,” alisema Ndabila.

Lyidia Mcharo wa Huduma ya Maombi alimuomba Mungu awainue vijana ili waamini katika kumtumikia.

Wengine walioshiriki kwenye maombi hayo ni Mchungaji Imani Shukurani,  Askofu Price Twail,
Mchungaji Joel Juma na Dickson Malali wote kutoka katika Kanisa la ABC. 

Monday, November 22, 2021

KAYA 700 IKUNGI MKOANI SINGIDA HUJISAIDIA VICHAKANI KWA KUKOSA VYOO

Muonekano wa vyoo bora.

 Mtoto huyu akiwa anatokea kwenye choo ambacho sio bora lakini mbaya zaidi akiwa hajavaa viatu _ hivyo kujiweka katika hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa mbalimbali.


Na Abby Nkungu, Singida


JUMLA ya kaya 745 katika halmashauri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, hazina vyoo hali inayosababisha wakazi wake kujisaidia kwa majirani, mashambani na vichakani hivyo  kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko; hasa watoto wenye umri chini ya miaka nane.

Takwimu  hizo zimetolewa na Mkurugenzi  Mtendaji wa  halmshauri hiyo, Justice Kijazi katika kipindi hiki ambapo Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kote wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya choo Duniani ambayo hufanyika Novemba 19 kila mwaka.

Kijazi alisema kuwa kati ya kaya zaidi ya 69,900 zilizopo katika halmashauri hiyo, 38,544 ndizo zenye vyoo bora, 30,681 zina vyoo vya kawaida visivyokubalika kiafya wakati zingine 745 hazina vyoo.

“Baadhi ya kaya ambazo hazina vyoo na zile zenye vyoo visivyokubalika kulingana na kanuni za afya, kunachangia kuwepo kwa magonjwa mbalimbali ya mlipuko kikiwemo kipindupindu, kuhara, kuhara damu pamoja na homa ya matumbo” alisema na kuongeza;

Waathirika wakubwa wa changamoto hizo ni kundi la watoto ambapo takwimu zinaonesha kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, jumla ya watu 10,091 waliugua magonjwa hayo kati yao 5,819 yaani zaidi ya nusu wakiwa ni watoto walio chini ya umri wa miaka nane”.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Kijazi alisema kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kuwa na vyoo bora na kutumia Sheria Ndogo za halmashauri kuwabana wanaokaidi.

Alisema kuwa hatua hiyo itaenda pamoja na kusimamia miongozo ya Wizara ya Elimu na Afya ili kuhakikisha kuwa shule zote zinakuwa na vyoo bora kwa ajili ya kulinda afya za watoto wawapo shuleni.

Daktari bingwa Mshauri wa magonjwa ya wanawake na watoto katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Singida, Dk Suleiman Muttani alisema kuwa vyoo bora shuleni na nyumbani ni muhimu zaidi katika kulinda afya za watoto na jamii kwa ujumla..

“Mtu mzima akibanwa atakwenda kwa jirani au kichani lakini mtoto kama hujamjengea choo, yeye atajisaidia hapo hapo kwenye uwanja nyumbani au kama ni shuleni basi nyuma ya madarasa na ni hatari kwa kuathiri shule nzima au kaya yote kwa magonjwa ya mlipuko” alieleza Dk Muttani.

 Hata  hivyo baadhi ya wadau wanasema kuwa tatizo ni elimu duni juu ya umuhimu wa vyoo bora, mila potofu na ukosefu wa teknojia rahisi ya ujenzi wa vyoo bora  bila kutumia gharama kubwa hasa vijijini.

“Kuna wengine kwa mila na desturi zao wanachukulia choo kuwa ni kitu cha anasa. Yaani atoe 200,000/- au zaidi kujenga choo wakati vichaka vipo, hawawezi…. anaona bora akanywee pombe hiyo hela. Lazima elimu itolewe, watu wajue kinagaubaga kuwa iwapo hawana choo wapo kwenye hatari” alisema Patrick Mdachi Ofisa Maendeleo ya Jamii Mstaafu na mtafiti wa mila na desturi za kabila la Wanyaturu.

Novemba 19 kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Choo Duniani ili kutoa fursa kwa wanajamii kutathimini juu ya hali ya vyoo, kuhamasisha ujenzi wa vyoo bora, kuvitumia na kuzungumzia usafi wa mazingira kwa ujumla. Ujumbe wa mwaka huu ukiwa “Tuthamini Vyoo”

Aidha, siku hii huchagiza uchukuaji hatua madhubuti katika kushughulikia janga la Usafi wa Mazingira duniani ili kusaidia kufikia lengo namba 6 la Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG 6) linalohimiza Usafi wa Mazingira kwa wote ifikapo mwaka 2030.

Sunday, November 21, 2021

MBUNGE MATTEMBE ATOA MBEGU ZA ALIZETI TANI 10 KWA VIKUNDI VYA WANAWAKE WAKULIMA MKOA WA SINGIDA


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida  Mhe.Aysharose Mattembe (wa pili kushoto) akikabidhi  mbegu za alizeti  kwa  vikundi vya wanawake mkoani hapa  ikiwa ni jitihada za  kuunga mkono juhudi za Serikali kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida  Mhe.Aysharose Mattembe (wa pili kushoto) na akina mama wakionesha mifuko ya mbegu alizowakabidhi.

Hafla ya makabidhiano ya mbegu hizo ikiendelea.


Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida  Mhe.Aysharose Mattembe (katikati) akiwa amevikwa vazi la kimila katika hafla hiyo.

TIA YAFANYA MABORESHO MAKUBWA KWENYE MITAALA, MIUNDOMBINU

 Mgeni rasmi wa Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Uhasibu Tanzania Kampasi za Singida, Mwanza na Kigoma, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu wa pili kushoto,  akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Dk. Momole Kasambala (wa kwanza kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara ya Fedha na Mipango, Wakili Said Chiguma muda mfupi kabla ya kuanza kwa mahafali hayo yaliyojumuisha Kampasi za Taasisi hiyo kwenye mikoa ya Singida, Mwanza na Kigoma mkoani Singida jana.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu (katikati) aliyemwakilisha Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Mwigulu Nchemba, akifuatilia matukio mbalimbali wakati wa mahafali hayo.

WANANCHI RUANGWA WAYAPONGEZA MASHIRIKA YA KUHIFADHI MISITU KWA KUMALIZA MGOGORO WA ARDHI


Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)  ambao wapo katika ziara ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu wilayani humo mkoani Lindi katika mkutano uliofanyika jana.

Afisa Ufuatiliaji na Utafiti wa Shirika la TFCG, Edward Emil akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari na Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hassan Ngoma.


Waandishi wa habari wakiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa wilaya.

Afisa Sera na Majadiliano wa TFCG Elida Fundi  akizungumza kwenye mkutano huo. Kulia ni Afisa Uhusiano wa TFCG Bettie Luwuge.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Nolasco Kitumile akizungumza na waandishi wa habari.

Wajumbe wa kamati mbalimbali wa Kijiji cha Malolo wakiserebuka kabla ya kuanza mkutano huo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Malolo Wilbert Mwambe akizungumza kwenye mkutano uliofanyika kwenye kijiji hicho wakati wakitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa waandishi wa habari..

Afisa Misitu wa Wilaya ya Ruangwa James Kabuta akizungumza kwenye mkutano huo.
Afisa Uhusiano wa TFCG Bettie Luwuge akizungumza kwenye mkutano huo.
Diwani wa Viti Maalumu wa Kata hiyo Ansila Lukanga akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Kikao kikiendelea.
Kikao kikiendelea.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Mwalimu Mohamed Abdallah akiendesha kikao hicho.
Mkazi wa kijiji hicho Gerald Mwambe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mzee Maarufu wa kijiji hicho Mohamed Abdallah akichangia jambo kuhusu utunzaji wa misitu.
Mkutano ukiendelea.
Mjumbe wa Kamati ya Maliasili Hilda Mwambe akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Malolo, Abdallah Said akizungumza kwenye mkutano huo.
Picha ya pamoja.



Na Dotto Mwaibale, Ruangwa Lindi.


WANANCHI wa Kata ya Malolo wilayani Ruangwa mkoani Lindi wameyapongeza Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu (MJUMITA) yanayo fadhiliwa na Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Uswis (SDC) kwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa ardhi uliyohusisha Kijiji cha Malolo na Kijiji jirani cha Ng'au.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya waandishi wa habari ambao wapo katika ziara ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu wilayani Ruangwa mkoani hapa walisema mashirika hayo yalifanikiwa kuumaliza mgogoro huo kwa amani na utulivu.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Wilbert  Mwambe alisema kumalizika kwa mgogoro huo kumesaidia kufungua fursa za matumizi bora ya ardhi na shughuli za uzalishaji endelevu wa mazao ya misitu kama, mbao, mkaa na kilimo.

"Hivi sasa hatuna ugomvi na wananchi wenzetu wa kijiji hicho ambao tulikuwa tukigombea eneo la ekta zaidi ya 2000 ambapo tulirudishiwa" alisema Mwambe.

Diwani wa Viti Maalumu wa Kata hiyo Ansila Lukanga aliyashukuru mashirika hayo kwa kutoa elimu kwa Wananchi wa Kijiji hicho ambao sasa wameanza kujua thamani ya misitu.

Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Mwalimu Mohamed Abdallah alisema hivi sasa wananchi wa eneo hilo wanahamasa kubwa ya kuinuka kiuchumi baada ya kujua thamani na matumizi bora ya ardhi na tayari wamekwisha tenga maeneo ya makazi, kilimo na ufugaji baada ya kupatiwa elimu hiyo.

Wazalishaji wa mbao na mkaa katika kijiji hicho wameyaomba mashirika hayo kuwatafutia masoko ya bidhaa hizo ambayo hayapo licha ya kuwa na mkaa magunia 40 ambayo wameyavuna kutoka katika misitu msitu wao kwa kufuata sheria.

Wananchi hao wamesema kabla ya kupelekewa mradi huo na mashirika hayo
 hatukuwa na matumizi bora ya ardhi kwani walikuwa wakikata miti kiholela jambo lililokuwa likichangia kwa kiasi kikubwa kuhalibu mazingira na misitu.

Awali akizungumza na waaandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hassan Ngoma alisema misitu ni lazima ilindwe na akatumia nafasi hiyo kuyashukuru mashirika hayo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuisaidia Serikali kutunza misitu ya asili katika wilaya hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Nolasco Kitumile alisema halmashauri hiyo imetenga sh.12 milioni kwa ajili ya kusaidia utunzaji wa misitu katika vijiji viwili vya Nangulugai na Nalung'ombe na kuwa Halmashauri hiyo ina misitu sita iliyosajiliwa huku miwili ikifanyiwa mchakato wa kusajiliwa ambapo itakuwa na misitu 8 ukiwepo na wa halmashauri.

Mashirika hayo yanatekeleza mradi huo katika wilaya ya Kilosa, Mvomero, Morogoro, Liwale, Nachingwea na Ruangwa katika Kata ya Malolo. 

Saturday, November 20, 2021

MAKUMBUSHO YA TAIFA NA TAMUFO KUSHIRIKIANA KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 ZA UHURU

Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Elimu Viumbe Arusha Dkt. Christina Ngereza.
Katibu Mkuu wa TAMUFO Stella Joel.

Mlezi wa TAMUFO Dkt. Frank Richard.

Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Lake Manyara Dkt.Noelia Myonga.
 


Na Dotto Mwaibale


KATIKA Maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na Umoja  wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) wameandaa Kongamano la Fursa katika Sekta ya Muziki.

Kongamano hilo litakuwa la siku tatu na kufanyika katika makumbusho ya Taifa ya Elimu Viumbe Arusha kuanzia Desemba 7, 2021 hadi Desemba  9, 2021.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi wa Makumbusho ya Taifa ya Elimu Viumbe Arusha Dkt. Christina Ngereza alisema wameandaa kongamano hilo ili kutoa elimu na fursa mbalimbali zilizopo katika urithi wa muziki wa Tanzania ambao umebadilika sana katika miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania.

Katibu Mkuu wa TAMUFO Stella Joel alisema maandalizi yote yamekamilika na kuwa wanamuziki wataimba nyimbo mbalimbali za zamani na za sasa uliotumika katika kipindi cha miaka 60 ya Uhuru ambao ulichangia kuhamasisha maendeleo.

Mlezi wa TAMUFO Dkt. Frank Richard alitaja fursa zitakazo patikana siku hiyo kuwa ni kutolewa Bima ya Afya NHIF kwa gharama nafuu kwa ajili ya vipimo na matibabu kwa wanamuziki ambavyo vitatolewa kwenye Hospitali za Serikali na za binafsi.

Alisema kutakuwa na fursa lukuki kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na fursa za kibenki na nyingine nyingi.

Richard alisema Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na   COSOTA watakuwepo kutoa elimu na usajili wa wanamuziki.

Joel alitumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali wa muziki kufika kwenye kongamano hilo na kuwa huduma ya chakula na vinywaji itapatika kwa gharama nafuu.

Wadau wengine walioalikwa kwenye kongamano hilo ni pamoja na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Lake Manyara Dkt.Noelia Myonga.