Friday, December 16, 2022

WAANDISHI WA HABARI WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA SADAANI, HIFADHI YA KIPEKEE DUNIANI

Kamishna Msaidizi Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo (kulia) akiwa katika mstari wa pamoja na wanahabari na watumishi wengine wa hifadhi wakionesha furaha yao kwa kucheza na kuruka baada ya kufika eneo la Mafui.
Ziara ikiendelea.

Kamishna Msaidizi Uhifadhi Ephraim Mwamongo akiwa na Mwandishi Mashaka Kibaya wakiwa kwenye tabaka la ardhi Mufui.

Aliyevaa miwani na kofia kulia ni Kamshna Msaidizi Uhifadhi,Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo akiteta jambo na Mwandishi wa Global TV Ibrahim Kunoga wakati wa ziara ya waandishi wa habari walipotembelea hifadhi ya Taifa ya Saadani.

 Mwandishi wa Habari Mashaka Kibaya akiwa ndani ya boti maalumu wakati wa ziara hiyo.
Majadiliano yakifanyika katika ziara hiyo.
Waandishiwa habari wakiwa ndani ya boti wakati wa ziara hiyo.
Muonekano wa eneo la kupumzika katika hifadhi hiyo. 

Na Mashaka Kibaya, Tanga. 

HIFADHI ya Taifa ya Saadani ni Mbuga pekee ambayo mazingira yake yameungana na Bahari ikiwa na Ikolojia ya mbuga na ile ya bahari huku ikiwa imesheheni wanyama wa aina mbalimbali.

Miongoni mwa Wanyamapori wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni Chui, Nyati, Tembo, Pundamilia, Kuro na wengine wengi hivyo si jambo la ajabu kumkuta Simba akiwa anapunga upepo kwenye fukwe za Bahari ya Hindi.

Kivutio kingine kinachoipatia umaarufu mkubwa hifadhi hiyo ni uwepo wa fungu la mchanga 'Mafui'. Aina ya tabaka la ardhi linalopatikana katikati ya maji eneo ambalo ni kina kirefu, sehemu ambayo mazingira yake huvutia wageni kutembelea.

Mambo yanayopatikana ndani ya Mafui, ni viumbe hai kama vile Kasa, mawe aina ya Matumbawe yenye rangi na maumbo tofauti ambayo ni mazalia ya Samaki eneo ambalo kisheria ni sehemu rasmi ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Pia kuna mazingira rafiki yenye umbo la bakuli linalowawezesha watalii kuogelea na hata wale wasioweza wanaweza kutumia eneo hilo kujifunza mchezo huo wa kuogelea ambao umetokea kupendwa sana ulimwenguni.

Kwa wageni au watalii hawawezi kulifikia  eneo hilo la Mafui ambalo linafahamika kwa jina maarufu la 'Mwali' ambapo waatalazimika kutumia usafiri wa boti ili kwenda kujionea mambo mazuri yenye kupendeza.

Kwa nini Mafui imebeba umaarufu wa jina Mwali? Ni kwa sababu kuna wakati imekuwa ni vigumu sana kuliona tabaka hilo la ardhi lililopo kwenye kina kirefu cha Maji, hadi pale utakapofanikiwa kufuata ratiba maalum ambayo huzingatiwa na watembeza wageni 'Tour Guide.

Kwa vile Mafui inahitaji kufuata ratiba maalum pasipo kuivuruga ndipo kuiona, wale wasiozingatia kanuni zake hushindwa kuliona eneo hilo, hivyo kiasilia ama tamaduni ikafananishwa kana kwamba unataka kumuona bibi Harusi ambapo kuna taratibu maalum ili kuruhusiwa kumuona.

" Kuna wakati kumuona 'Mwali' (Mafui) ni changamoto, utaiona Mafui hadi pale maji yanapokupwa, hivyo wageni wanaotembelea wakifanikiwa kuliona tabaka hilo la ardhi hufurahi sana" anasema Ephraim Mwamongo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Hifadhi ya Taifa ya Saadani.

Anaongeza kusema Mwali anapoonekana wageni hujawa na furaha ambapo wanaweza kulitumia eneo hilo kwa kuvishana pete za uchumba, harusi na hata kupumzika tu, watu wakipiga picha na kufurahi mandhari mbalimbali yaliyopo.

Katika kumuongezea thamani Mwali (Mafui), Mwamongo alisema, upo mpango wa kujenga Dock Yard ili vyombo vya Usafiri kama boti kuegesha na kuwawezesha wageni kupanda na kusafiri kuweza kwenda kuona Mwali.

 Mwamongo anatanabaisha kuwa, Hifadhi ya Taifa ya Saadani imefanikiwa kiwa  na vijana mahiri waliobobea katika kuwaongoza na kuhudumia wageni wakiwawezesha kufurahia ziara zao wakihisi hawajapoteza kitu.

Kimsingi Hifadhi ya Taifa ya Saadani inaelezwa kuwa salama  na shirikishi kwa wananchi wanaoishi vijiji jirani ambao wamekuwa wakinufaika kwa kupatiwa  miradi mbalimbali ya maendeleo.

Manufaa mengine wanayopata wananchi wa eneo hilo kupitia uwepo wa hifadhi ya Saadani kuimarika kwa hali ya ulinzi na usalama kwenye maeneo yao, ambapo askari waliopo kwenye hifadhi wamekuwa wakihusika kuhakikisha usalama wa jamii.

Vile vile hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani imekuwa fursa adhimu ambapo wenyeji hususani wavuvi wamekuwa wakiitumia kama Soko kuu kwa ajili ya kuuzia Samaki wao kwa kuwa wageni wanaotembelea eneo hilo hushawishika kununua bidhaa hizo kwa wenyeji wao.

Ili kuiwezesha hifadhi yaTaifa ya Saadani kuendesha shughuli zake kwa tija, kazi ya uboreshaji wa miundombinu imeendelea kufanyika na kwa njia ya reli, barabara, ndege na hata maji zimefanyiwa kazi hatua ambayo imelenga kurahisisha usafiri kwa wageni kutoka sehemu tofauti.

Kamishna Msaidizi uhifadhi wa hifadhi ya Taifa ya Saadani, Ephraim Mwamongo anasema, kupitia kituo 'Station' ya reli Mvave wageni wanaweza kufika kwenye eneo la hifadhi hiyo inayoondokea kuwa  na umaarufu mkubwa duniani.

Mwamongo anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa  na Rais Samia Suluhu Hassan kuwawezesha kupata fedha zilizosaidi kufanya maboresho ya miundombinu.

Ni kupitia fedha za COVID hifadhi hiyo ya Taifa ya Saadani imeweza kunufaika ambapo kwa upande mwingine Mwamongo amemshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa hatua yake kufanya Filamu ya Royal Tour.

Kamishna Msaidizi Mwamongo anasema kwamba, Royal Tour ya Mama Samia Suluhu Hassan imekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watalii kwenye hifadhi ya Taifa ya Saadani ambapo anatoa wito kwa watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea hifadhi hiyo ya kipekee. 

Wednesday, December 14, 2022

VITUO ATAMIZI KUWA KICHOCHEO CHA MABADILIKO SEKTA YA MIFUGO NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, akizungumza na washiriki wa MafunzoRejea ya Maafisa Ugani wa Kanda ya Mashariki wakati akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Pwani jana Desemba 13, 2022. 

Na Mbaraka Kambona, Pwani 

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Wizara yake imeanzisha vituo atamizi kuwawezesha vijana kufuga kwa tija ili kujikwamua kimaisha na pia kuwa ni kichocheo kwa wafugaji wengine kujifunza kwa vitendo na kubadilika kutoka katika ufugaji wa kienyeji na kufanya ufugaji wa kisasa utakaowaletea tija zaidi na kupunguza migogoro isiyo ya lazima kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Ndaki aliyasema hayo wakati akifunga Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani jana Desemba 13, 2022.

Alisema kuwa Wizara yake imewekeza na inahamasisha Vijana kushiriki katika uzalishaji wa mifugo kupitia Vituo Atamizi ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 vijana 240 waliohitimu vyuo vya Mafunzo ya Mifugo wamedahiliwa na kuanza mafunzo ya unenepeshaji wa ng’ombe katika vituo nane (8).

“Kwa mantiki hiyo nawahimiza wadau mbalimbali kuwekeza na kuhamasisha vijana kujiunga na Vituo atamizi ambavyo vimeanzishwa na Wizara kwa sababu vijana hao wakimaliza mafunzo hayo watasaidia wafugaji wengine kubadilika na kuanza kufuga kwa tija,” alisema Ndaki.

“Mwakani tunatarajia kuwa na vijana wengi zaidi kwa sababu tutaongeza bajeti kuhusu vituo hivi ili tuweze kuwachukua vijana wengi zaidi hata kufikia 1000, kwa sababu vijana hawa wakitawanyika kote nchini wataleta mageuzi kwenye ufugaji wetu,”alifafanua 

Aidha, alisema kuwa huduma za ugani ni kiungo muhimu kati ya watafiti na wafugaji ili kupata ufugaji wenye tija hivyo ni vyema maafisa ugani wakaimarisha mahusiano mazuri ili waweze kufikia malengo tarajiwa.

“Nitoe rai kwenu kujenga ushirikiano madhubuti baina yenu na wafugaji utakaowezesha kutoa taarifa sahihi, kusambaza teknolojia, kuelimisha, kutoa ushauri wa kitaalamu na kupata mrejesho,”alisema.

Waziri Ndaki alisema kuwa wanatambua  changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya mifugo hususan katika utoaji wa huduma za Ugani hapa nchini lakini tayari Wizara kupitia Mpango wa Mabadiliko wa Sekta ya Mifugo imebainisha mikakati na afua mbalimbali za kuzipatia suluhisho changamoto hizo.

“Miongoni mwa juhudi za serikali ni pamoja na kuanza kutoa Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani Watakaowafundisha Wengine (Trainer of Trainee) ambapo jumla ya Maafisa Ugani 800 watafikiwa kwa mwaka wa fedha, 2022/2023. Aidha, Wizara inatarajia kutoa mafunzo elekezi kwa wafugaji 182,200 nchini ambapo ninyi mtatusaidia sana katika kutekeleza jukumu hilo,”alifafanua.

Aliongeza kuwa katika kutatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vya kutolea huduma za Ugani, Wizara imepanga kununua pikipiki 1,200 ambazo zitaongeza chachu kama vitendea kazi muhimu katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Vilevile Wizara imeanza matumizi ya mifumo ya TEHAMA (M-Kilimo na Digital Agricultural Service Portfolio (Ugani Kiganjani) kwa lengo la kuwafikia wafugaji wengi na kutoa mrejesho wa kila kazi ambayo Afisa Ugani atakuwa ametekeleza katika eneo lake.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(kulia) akiongea na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi. Zuwena Omary alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani muda mfupi kabla ya kwenda kufunga Mafunzo Rejea ya Maafisa Ugani Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022. 

Washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia hutuba ya ufunguzi wakati ikiwasirishwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, Mafunzo na Huduma za Ugani, Dkt. Angello Mwilawa (kulia) wakati akiagana na Mkurugenzi huyo punde baada ya kufunga Mafunzo Rejea ya Maafisa Ugani Kanda ya Mashariki yaliyofanyika mkoani Pwani Disemba 13, 2022. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Sara Msafiri.  

Sunday, December 11, 2022

WAJEDA WAACHANA NA UKAPERA BAADA YA KUFUNGA NDOA WAPEWA MANENO MAZITO

Wanajeshi (WAJEDA) Wanandoa Valentino John Tuka na Tusibwene Mustafa Juma kutoka Songea mkoani Ruvuma wakionesha tabasamu baada ya kuachana na ukapera kwa kufunga ndoa Takatifu katika Kanisa la Moravian Usharika wa Kimara  mwishoni mwa wiki Desemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam.
Mchungaji wa Kanisa hilo Usharika wa Kimara, Alamu Mwambande Kajuni akifunga ndoa hiyo.
Mchungaji wa Kanisa la Moravian Usharika wa Pugu Kajiungeni , Laiton Silumbwe akiongoza ibada ya ndoa hiyo Takatifu.
Wanandoa hao wakionesha furaha yao baada ya kuingia ukumbuni.
Brigedia Mstaafu, Cosmas Kayombo na mke wake walikuwa ni miongoni mwa wageni waalikwa walihudhuria hafla ya ndoa hiyo.
Ibada ya ndoa ikiendelea.
Mama Mzazi wa Bibi Harusi Ambwene Anyitike Kyoga (kulia) akionesha umahiri wa kuongoza Kwaya ya Kanisa hilo Usharika wa Pugu Kajiungeni wakati ikitoa burudani.
Baba Mzazi wa Bwana Harusi Mzee John Ambros Tuka (kushoto) akiwa kwenye ibada hiyo ya ndoa.
Ibada ikiendelea hao ni ndugu wa Bibi Harusi wakiwa kwenye ibada hiyo.
Kwaya ya kanisa hilo Usharika wa Kimara ikitoa burudani.
Kwaya ya kanisa hilo kutoka Pugu Kajiungeni ikitoa burudani.
Ibada ikiendelea.
Vijana walioshiba kisawasawa ndugu wa Bibi Harusi kutoka Pugu Kajiungeni wakiongozwa na Chambuso Alphan Shukuru  (kushoto) wakiwa kwenye hafla hiyo.
Bibi wa Bwana Harusi akitoa neno la kuwahusia wanandoa hao.
Mama mkubwa wa Bibi Harusi Mary Anyitike akitoa neno la shukurani kwa uongozi wa kanisa hilo.
Kwaya kutoka Pugu Kajiungeni ikitoa burudani.
Picha ya pamoja baada ya ibada hiyo ya ndoa Takatifu.

Dada wa Bibi Harusi Anna Segere Mirambo akiwa katika picha ya pamoja na Bibi Harusi, Tusibwene Mustafa Juma.

Picha ya pamoja Bibi Harusi na wadogo zake na dada yake Mbumi Donald Mwaibale (kulia)

Wanandoa wakiwa katika picha ya pamoja na mama zake Bibi Harusi  na Mjomba wao Donald Mwaibale (kulia)
Wanandoa wakiwa katika picha ya pamoja na wazazi wao wa pande zote mbili.
Wanandoa hao wakiwa katika picha ya pamoja na wazazi wa Bwana Harusi.
Wanandoa hao wakiwa katika picha ya pamoja na wazazi wa Bibi Harusi.
Picha ya pamoja.
Wajomba wa Bibi Harusi na mama zake wakiwa katika picha ya pamoja.
Baba wa Wanandoa hao wakiserebuka wakati wakiingia ukumbini.Kushoto ni Baba wa Bwana Harusi, John  Ambros Tuka na kulia ni Baba wa Bibi Harusi, Mustafa Juma.
Mama wa Wanandoa hao wakionesha umahiri wa kuserebuka wakati wakiingia ukumbuni. Kushoto ni Mama ya Bibi Harusi, Ambwene Kyoga na kulia ni Mama wa Bwana Harusi, Augusta Francis Mapunda.
Burudani zikiendelea kutolewa ukumbini.
Maharusi wakiwa katika picha ya pamoja na kamati yao ya maandalizi ya sherehe hiyo.
 

Na Dotto Mwaibale, Dar es Salaam

WANAJESHI (WAJEDA) Valentino John Ambros Tuka na Tusibwene Mustafa Juma kutoka Songea mkoani Ruvuma wameamua kuukimbia ukapera kwa kufunga ndoa Takatifu katika Kanisa la Moravian Usharika wa Kimara  jijini Dar es Salaam.

Ndoa hiyo iliyokuwa ya kuvutia na ya aina yake ambayo imefungwa Desemba 10, 2022 na kuhudhuriwa  na mamia ya watu ilikuwa na mvuto kutokana na shamrashara mbalimbali na burudani za kwaya mbili zilizokuwa zikitoa burudani ikiwepo kwaya ya kanisa hilo kutoka Pugu Kajiungeni na Kimara huku ikisindizwa na ngoma ya ya asili ya kabila la Wangoni.

Ndoa hiyo iliwahusisha ndugu jamaa na marafiki wa pande zote mbili wakiongozwa na wazazi wa wanandoa hao, Mzee John Ambros Tuka na mke wake Augusta Francis Mapunda wakiwa ni  wazazi wa bwana harusi na wazazi wa Bibi Harusi Mustafa Juma akiwa na mzazi mwenzake Ambwene Anyitike Kyoga.

Mchungaji wa Kanisa la Moravian Usharika wa Pugu Kajiungeni , Laiton Silumbwe akitoa wosia kwa wanandoa hao aliwaambia kuwa sasa wamekuwa mwili mmoja hivyo ndoa yao na iheshimiwe na watu  wote na silaha kubwa kwao ni kumtanguliza Mungu katika maisha yao,kudumisha upendo na kuomba msamaha pale watakapokoseana na si vinginevyo.

Alisema ndoa ni kusikilizana na haihitaji ubabe ni kila mmoja kumsikiliza mwenzake na kuwa na watoto ni majaliwa ya Mungu ambapo aliendelea kuwasisitiza wanandoa hao kumtumikia Mungu wakati wote wa maisha yao.

"Kutokana na kuwepo kwa utandawazi kumekuwa na changamoto nyingi kwenye ndoa nahata kufikia kupigana kwa wanandoa mambo haya nendeni mukayashinde kwani hayampendezi Mungu" alisema.

Mwinjiristi Atupele Kyomo kutoka kanisa hilo Usharika wa Msamala  mkoani Ruvuma ambaye aliwasindikiza wanandoa hao alisema sasa wamekuwa mwili mmoja hivyo watu wa nje wakiwepo ndugu, jamaa na marafiki waache kuwaingilia na mtu yeyote atakayehitaji msaada kwa wanandoa hao wanapaswa kuwahusisha wote.

"Kabla ya kufunga ndoa kuna baadhi ya ndugu walikuwa wakimpigia Bwana harusi au Bibi harusi wakiomba hela au mahitaji fulani lakini sasa nawaomba mambo hayo yaacheni ukiwa na shida washirikisheni wote" alisema Mwinjilisti huyo.

Ndoa hiyo ilifungwa na Mchungaji wa Kanisa hilo Usharika wa Kimara, Alamu Mwambande Kajuni  na baada ya hapo walifanya mapumiko mafupi Hoteli ya Temboni Garden ambapo wanandoa hao, ndugu,jamaa  na marafiki waliweza kupiga picha na kufuatia sherehe ya kukata na shoka ambayo iliambatana na kula na vinywaji iliyofanyika Ukumbi wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Ubungo Msewe.

Friday, December 9, 2022

CHANGAMOTO YA USAFIRI SIO KIKWAZO KWA MSD KUPELEKA DAWA ZAHANATI YA BAGA MKOANI MOROGORO

 Licha ya kuwepo kwa changamoto kubwa ya barabara na usafiri,  Bohari ya Dawa (MSD) imekuwa sio kikwazo kufikisha dawa na vifaa tiba katika Zahanati  ya Baga iliyopo Wilaya ya Morogoro Vijijini ambayo ipo kwenye miinuko mikubwa ya Milima ya Uruguru. Pichani wananchi wakisaidia kuzifikissha dawa katika Zahanati hiyo huku wakivuka mto.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro 

Licha ya changamoto ya miundombinu ya usafirishaji katika baadhi ya maeneo, Bohari ya Dawa (MSD) imesisitiza itaendelea kupeleka dawa na vifaa tiba kila kona ya nchi ilikutoa huduma kwa wananchi..

Changamoto ya miundombinu ya usafirishaji katika baadhi ya maeneo, inailazimu Bohari ya Dawa (MSD) kutumia gharama za ziada kufikisha huduma kwa wananchi.

Zahanati ya Baga iliyopo Mnewele mkoani Morogoro ni kielelezo cha maeneo yaliyogubikwa na changamoto hizo.

Kulingana na jiografia ya eneo hilo, ni vigumu kutumia usafiri wa gari, hivyo wanalazimika kutumia gharama za ziada kukodisha pikipiki na baadaye watu kwa ajili ya kubeba ili kufikisha dawa na vifaa tiba katika zahanati hiyo.

Akizungumza Desemba 8, 2022 katika ziara ya maofisa wa MSD mkoani Morogoro, Dereva wa MSD, Kanda ya Dar es Salaam, Said Tindwa alisema kwa hali ilivyo ni vigumu kufika na gari.

"Gari unaenda nayo kama kilometa tatu kutokea barabara kuu, unafika eneo linaitwa Mtombozi hapo ndipo gari inaishia, hadi kufika ilipo zahanati ni safari ya takriban kilometa 60," alisema.

Katika safari hiyo, alieleza baadhi ya maeneo yanapitika kwa bodaboda na mengine wanalazimika kukodi watu wabebe mzigo kichwani hadi ilipo Zahanati ya Baga.

"Safari ya pikipiki ni kama nusu saa inakufikisha mtoni hapo pikipiki haiwezi kwenda tena tunawalipa watu wabebe mzigo kwa kichwa safari ya masaa mawili hadi wanafika," alieleza.

Mfamasia wa MSD katika Kanda hiyo, Diana Kimario amesema pamoja na ugumu wa mazingira, lakini hakuna zahanati itakosa kufikishiwa huduma.

"Ni kweli baadhi ya maeneo ni magumu kufikika lakini kama MSD tunawahakikishia wananchi kwamba tutawafikishia dawa na vifaa tiba huko huko walipo," alisema.

Vijana waendesha bodaboda wakipakia maboksi ya dawa kwenye pikipiki zao tayari kwa safari ya kuzipeleka Zahanati ya Baga ambayo ipo eneo lenye changamoto ya kufikiwa kiurahisi kutokana na kuwa na changamoto ya miundombinu ya barabara.

Dawa na vifaa tiba zikishushwa kwenye gari tayari kupelekwa Zahanati ya Baga. 

Thursday, December 8, 2022

SHIRIKA LA ESTL KWA UFADHILI WA FCS WATOA MAFUNZO KWA WALEMAVU MKOA WA SINGIDA KUPINGA UKATILI

Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago akizungumza  katika mafunzo ya kuwajenge uwezo watu wenye ulemavu kutoa taarifa pale wanapofanyiwa ukatili, mafunzo  yaliyoendeshwa na ESTL leo Desemba 7, 2022 mjini hapa.

Na Dotto Mwaibale, Singida 

SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojihusisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia katika muktadha wa dhana hasi ya kuondokana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa  ufadhili wa Shirika la Foundation Civil Society (FCS)  limetoa mafunzo ya kuwajenge uwezo watu wenye ulemavu ili waweze kutoa taarifa pale wanapofanyiwa ukatili.

Mafunzo mengine yaliyotolewa ni pamoja dhana ya ujinsia na ukatili wa kijinsia na aina nyingine za ukatili wa kijinsia zinazoripotiwa katika kata,vijiji,mitaa,sheria na mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu dhana ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji. 

Pia mafunzo mengine yaliyotolewa ni fursa za kijasiriamali toka halmashauri, miongozo ya upatikanaji wa mikopo,mfumo wa upatikanaji wa mkopo wa halmashauri hasa asilimia mbili ya fedha za mkopo inayotolewa kwa kundi la watu wenye ulemavu mafunzo yaliyotolewa na Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago. 

Katika mafunzo hayo Mbago alitoa wito kwa jamii hasa wazazi kuhakikisha  wanawalinda watoto wao dhidi ya ukatili kwa kuripoti vitendo vya ukatili sehemu husika ili wanaotenda vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua. 

Afisa Mawasiliano na Vijana wa ESTL, Edna Mtui alitoa mafunzo yaliohusu dhana ya mila potofu na ndoa za utotoni, ndoa za kulazimishwa, na athari zake, dhana ya ukeketaji na athari zake na usafirishaji haramu wa binadamu. 

Mtui alisema kwa sasa kuna vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia katika jamii ambao upo wa aina tano ukiwepo ukatili wa kiuchumi ambao wakina mama wanaupitia hasa  pale baba anapouza  mazao yote licha ya mama kushiriki katika uzalishaji.

Aidha Mtui aliongeza kuwa kuna vipigo ambavyo akina mama wengi wanavipata majumbani na ukatili wa watoto wengi kuachishwa masomo yao ili waweze kuolewa.

Alisema kuna watu wengine wapo wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia pasipo wao kujua, hivyo elimu ni muhimu kwa jamii ili iweze kutambua vitendo vyote vya ukatili.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ukatili wa Kijinsia  wa ESTL  John Nzungu alisema bado kuna baadhi ya wazazi wanawaficha watoto wenye ulemavu na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupelekwa shule.

Nzungu aliongeza kuwa mila na desturi pia bado ni changamoto ambapo watoto wenye ulemavu hawapelekwi kliniki wakiona ni aibu kuwa na mtoto mwenye ulemavu, sababu hiyo inasababisha kushindwa kupata huduma za afya.

 Mwenyekiti wa Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Singida, Boniphace Kitiku alisema ukatili kwa watu wenye ulemavu ni mkubwa  licha ya kuwepo wadau wengi wanaoshughulika  kutoa elimu ya usawa kwa watu wote ili watu wa kundi hilo wasifanyiwe ukatili.

Kitiku alitoa wito kwa jamii kuwaona walemavu nao ni watu ambao wanaweza kuishi pamoja kama Mungu alivyowajaalia lakini bado kuna mitazamo hasi kutoka kwa baadhi ya watu wakiona walemavu ni mtaji wa kukuza biashara hasa zile kubwa na kuwatafutia balaa baada ya kudanganywa na waganga wa kienyeji.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameiomba serikali na wadau mbalimbali kuendelea  kutoa elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo bado baadhi ya watu wanaendelea kuvifanya.

Wamesema kuwa baadhi ya wazazi bado wanashikilia mila na desturi zilizopitwa na wakati ambazo zinasababisha vitendo hivi kuendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kusema binti kufanyiwa ukeketaji ni kutolewa mikosi.

Wameongeza kueleza kuwa  imani za kishirikina zinachangia kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutafuta  utajiri, hali inayosababisha ubakaji kwa watoto, wazee, wagonjwa wa akili kwa dhana kuwa wakitaka kufanikiwa ni lazima wafanye hivyo kama wanavyoambiwa na waganga wa kienyeji.

Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la ESTL John Nzungu (kulia) akizungumza.
Afisa Mawasiliano na Vijana wa shirika hilo Edna Mtui (kushoto) akitoa mada kwenye mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea.

Mwenyekiti wa Watu wenye ulemavu Mkoa wa Singida, Boniphace Kitiku, akizungumza kwenye mafunzo hayo.
Afisa Mawasiliano na Vijana wa shirika hilo Edna Mtui (kulia) akiteta jambo na Ofisa wa shirika hilo, Aisha Msuya.

Picha ya pamoja baada ya mafunzo hayo.