Thursday, January 19, 2023

RC SINGIDA AVITAKA VYOMBO VYA DOLA KUCHUNGUZA WATOTO KUHUSISHWA NA UHALIFU

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Puma kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Januari 19, 2023 anayoendelea kuifanya ikiwa ni muendelezo wa ziara za kutembelea kila wilaya kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi. Kushoto ni Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto na kulia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa wilaya hiyo, Mika Likapakapa. 

Na Dotto Mwaibale, Ikungi Singida

MKUU wa Mkoa  wa Singida Peter Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa ameviagiza vyombo vya dola wilayani Ikungi kuchunguza matukio ya  uhalifu yanayodaiwa kuhusisha watoto wenye umri usio zidi miaka 15.

Serukamba alitoa agizo hilo Januari 19, 2023 baada ya  kuibuliwa na wananchi wa Kijiji cha Puma  wilayani  Ikungi katika mkutano wa hadhara ikiwa ni muendelezo wa ziara za kutembelea kila wilaya kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali na kuzipatia ufumbuzi.

Kero hiyo iliibuliwa na mwananchi wa kijiji hicho Joramu Zakaria ambaye alisema vitendo hivyo vya uhalifu vimekithiri katika eneo hilo kwa kiwango cha mtu kutokuwa na uhakika wa kuamka salama.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Samwel Mbiaji alikiri kuwepo vitendo hivyo na kuwa walifanya msako kwa kushirikiana na polisi na kuwa asilimia 75 ya waliokamatwa walikuwa na umri  umri usiozidi miaka 15 ambao waliachiwa.

"Tukiwaita wazazi wao wanatuambia tufanye tunavyotaka wao wamewashinda sasa mkuu sisi tufanyeje" alisema Mbiaji.

Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ikungi, Suzana Kidiku aliahidi kulishughulikia suala hilo kwa kuwashirikisha maafisa wa ustawi, viongozi wa kijiji na kuwa wanatarajia kufanya msako wa kuwabaini wahalifu hao.

Kero nyingine iliyoibuliwa katika mkutano huo ni ile iliyotolewa mfanyabiashara wa viazi Fatuma Ramadhani ambaye aliomba kuwepo kwa soko la uhakika kwa kuwa hivi sasa wanauza bidhaa hiyo maeneo yasiyo rasmi na kusababisha kuchafua mazingira.

Pia alilalamikia utozwaji wa ushuru mara mbili unaofanyika eneo la Kintinku baada ya kutozwa wa awali wanapotoka katika kijiji hicho.

Kufuatia kero hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi alisema wanatarajia kujenga soko la kisasa katika kijiji hicho ambalo litaondoa changamoto hiyo.

Akizungumza baadaya kupokea kero hizo  Serukamba amewataka viongozi na watumishi wa Serikali wilayani humo kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii ya kutoa huduma kwa wananchi.

Alisema jambo kubwa aliloliona baada ya kusililiza kero hizo ni baadhi ya viongozi kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo na akawaomba viongozi hao kwenda katika Tarafa na Kata kufanya kazi hiyo na kuacha tabia ya kukaa ofisini.Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi (OCD), Suzana Kidiku akipiga saluti kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (Aliye kaa meza kuu kushoto) ikiwa ni kuonesha utii baada ya kutakiwa kushughulikia madai ya watoto kuhusishwa na vitendo vya uhalifu.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akisisitiza jambo kwenye mkutano huo. Kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa, akizungumza kwenye mkutano huo.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida, Msama Msama akizungumza kwenye mkutano huo.
Wakina mama wa Kijiji cha Puma wakiwa kwenye mkutano huo.
Katibu wa CCM Wilaya ya Ikungi, Stamili Dendego akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Justice Kijazi akiteta jambo na mkuu wa mkoa wakati wa mkutano huo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Winfrida Funto akizungumza kwenye mkutano huo.
Taswira ya mkutano huo.
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye mkutano huo.
Afisa Kilimo, Umwagiliaji  na Ushirika wa Wilaya ya Ikungi, Gurisha Msemo akizungumza kwenye mkutano huo.


Mfanyabiashara ya viazi vitamu, Fatuma Ramadhani akitoa kero yake kwa mkuu wa mkoa.
Mkazi wa Puma, Joramu Zakaria akitoa kero yake kwenye mkutano huo.
Afisa Ardhi wa Wilaya ya Ikungi, Ambros Ngonyani akizungumza kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea. 


Wednesday, January 18, 2023

SINGIDA WAANZA MSAKO WA WANAFUNZI AMBAO HAWAJA RIPOTI MASHULENI

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza na Maafisa elimu na wakuu wa Wilaya ili kujadili hali ya usaili wa wanafunzi  mashuleni katika kikao kilichofanyika Januari 18, 2023. Kulia ni Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Maria Lyimo

Na Mwandishi Wetu, Singida.

MAAFISA elimu na Wakuu wa Wilaya Mkoani Singida  wametakiwa kutumia muda wa Siku tatu kuanzia leo  kuhakikisha hakuna mtoto atakayebaki nyumbani wakati wengine wakiwa shuleni.

Kauli hiyo imetolewa leo na  Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba alipokutana na Maafisa elimu na wakuu wa Wilaya ili kujadili hali ya usaili wa wanafunzi  mashuleni .

Amesema idadi ya wanafunzi wa Sekondari walioripoti mashuleni ni ndogo ikilinganishwa na uwingi wa madarasa yalijengwa na Serikali hivi karibuni hivyo ni jukumu la Maafisa elimu hao kuhakisha wanasakwa popote walipo na wapelekwe shuleni.

RC Serukamba ameendelea kueleza kwamba ifikapo Siku ya jumatatu tarehe 23 January 2023 anataka taarifa ya kutoka kila kata  kuhusu wanafunzi wangapi wamesajiliwa na wangapi bado na Sababu za kutosajiliwa.

Aidha, ametoa wito kwa wazazi na walezi Mkoani Singida kuhakikisha hakuna Mtoto aliyechaguliwa kujiunga na kidato Cha kwanza atakayebaki nyumbani.

"Nimejiridhisha kwamba hali ya usaiili wa wanafunzi wa kidato Cha kwanza inasuasua Sana ,Serikali imejenga madarasa ya kutosha,imefuta Ada mashuleni lakini bado wapo wazazi hawawapeleki watoto wao shuleni hili halitakubalika" Serukamba.

Kwa upande wake DC wa Iramba Suleimani Mwenda amesema bado Katika Wilaya yake bado hali ya kujiunga na kidato Cha kwanza unaenda kwa kusuansua Jambo ambalo waliamua kuchukua hatua kwa kuwaita wazazi na wanafunzi ofsini kwake ili kuwasikiliza.

DC Mwenda anasema amebaini kwamba wapo wazazi wanaozuia watoto kwenda shule ili waweze kujiunga na Shughuli za kiuchumi za kulima kuchunga mifugo na bĂ adhi Kutafuta ajira binafsi.

Mwenda amesema wanapenda kutumia mbinu zote zikiwemo kuwashawishi kutumia Dola kuwapeleka shule na kuwachukulia hatua wazazi Watakao bainika kuwazuia watoto kwenda shule.




Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Ikungi, Margaret Kapolesya akichangia jambo kwenye kikao hicho.
Kikao kikiendelea.

Kikao kikiendelea.

MWEKEZAJI WILAYANI MKALAMA ADAIWA KUKITAPELI KIJIJI, ARDHI ALIYOPEWA KUWEKEZA SHULE AIKODISHA KWA KILIMO

 Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akizungumza Januari 18, 2023 wakati wa kikao cha kusikiliza kero za Wananchi wa Wilaya ya Mkalama katika ziara zake za kutembelea kila wilaya kwa ajili ya kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi.

Na Dotto Mwaibale, Mkalama

MWEKEZAJI aliyetaka kujenga shule ya sekondari katika moja ya kijiji  wilayani Mkalama mkoani Singida anadaiwa kufanya utapeli baada ya ardhi aliyopewa na kijiji kwa ajili ya kujenga shule  kuigeuza matumizi na kuanza kukodisha watu kuendesha shughuli za kilimo kwa zaidi ya miaka 14.

Suala hilo limeibuliwa na wananchi wa Wilaya ya Mkalama kwenye kikao na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba ambaye anaendelea na ziara yake ya kutembelea kila wilaya kwa ajili ya kusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi.

Katika ziara hiyo wilayani humo Serukamba alipokea kero 49 huku kero 43 zikihusu migogoro ya ardhi kama mashamba, viwanja na nyumba.

Akizungumza baada ya kusikiliza kero hiyo Serukamba aliagiza ardhi hiyo irudishwe kwa halmashauri ya kijiji hicho kama sheria inavyoelekeza kuwa kama ardhi haijaendelezwa kwa muda mrefu inapaswa kurejeshwa kwa walengwa.

Kero nyingine iliyoleta msisimko kwenye kikao hicho ni ya serikali ya Kijiji cha Iglansoni kudaiwa kuipora familia ya mama Melisiana mashamba zaidi ya ekari 60 na kisha kuanza kuyakodisha kwa wananchi kwa ajili ya kuendesha shughuli za kilimo huku fedha zinazopatikana zikinufaisha viongozi wa kijiji hicho.

Serukamba alimuagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Mkalama, Mkurugenzi na Afisa Ardhi wa Wilaya hiyo kwenda katika kijiji hicho na kufanya utaratibu wa kumrudishia mashamba mama huyo.

Katika hatua nyingine Maafisa ardhi, Watendaji waVijiji na Kata wilayani humo wametakiwa kuacha vitendo vinavyo sababisha migogoro ya ardhi ambayo imetajwa kama chanzo cha umaskini kwa wananchi na kuacha kushiriki vitendo vya uuzaji wa ardhi ambazo tayari zinaumiliki wa watu wengine na badala yake wajikite kuwashauri wananchi kuhusiana na mambo ya ardhi.

"Maafisa ardhi, watendaji wa kata na vijiji msiwe chanzo cha umaskini wa wananchi, watu wanataka kulima, kufanya maendeleo lakini mnawakwamisha mnaposhindwa kuwatatulia shida zao" alisema Serukamba.

Aidha Serukamba amewataka watumishi wilayani humo kutekeleza wajibu wao kikamilifu na kuwa kwa kufanya hivyo kutapunguza kero za wananchi.


Utaratibu huu ulioanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa kusikiliza kero za wananchi kila wilaya umepewa kongole na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mkalama James Mgwega ambaye alisema utasaidia kupata majawabu ya kero za muda mrefu za wananchi ambazo zilikaliwa na viongozi wa maeneo husika.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akisisitiza jambo kwenye kikao hicho.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akiteta jambo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, James Mkwega wakati wakitoka kwenye kikao cha kusikiliza kero za wananchi.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Amoni Sanga akizungumza kwenyekikao hicho.

Katibu Tawala wa wilaya hiyo, Elizabeth Rwegasira akizungumza kwenye kikao hicho.Mkuu wa Polisi wa wilaya hiyo akichangia jambo kwenye kikao hicho.

Afisa Ardhi Wilaya ya Mkalama, Imikigwe Kagubila Mwanitu, akijibu maswali kufuatia kero mbalimbali zilizokuwa zikitolewa na wananchi.
Viongozi wa Taasisi mbalimbali za Serikali na wakuu wa idara wakiwa kwenyekikao hicho.
Kero zilizokuwa zikitolewa zikiandikwa.




Kikao kikiendelea.

Baadhi ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakiwa kwenye kikao hicho. 

Tuesday, January 17, 2023

RC SINGIDA AWATAKA VIONGOZI WILAYA YA IRAMBA KUTEKELEZA WAJIBU WAO KWA WANANCHI

Mkuu wa Mkoa wa Singida. Peter Serukamba (kulia) akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Iramba ikiwa ni siku yake ya pili baada ya kuanzisha utaratibu wa kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja katika kikao kilichofanyika jana Januari 18, 2023. Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauriya Wilaya ya Iramba, .Dk. Hussein Sepoko na Mkuuwa wilaya hiyo, Suleiman Mwenda.

Na Dotto Mwaibale, Singida

MKUU wa Mkoa Singida. Peter Serukamba amewataka viongozi na watumishi wa Serikali Wilaya ya Iramba mkoani hapa kutekeleza wajibu wao kwa kufanya kazi ya kutoa huduma kwa wananchi kwa bidii na si vinginevyo.

Serukamba ameyasema hayo jana Januari 17, 2023 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Iramba ikiwa ni siku yake ya pili baada ya kuanzisha utaratibu wa kusikiliza kero zao ili kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja.

Alisema jambo kubwa aliloliona baada ya kusililiza kero hizo ni baadhi ya viongozi kushindwa kutekeleza wajibu wao ambapo aliwaomba watekeleze wajibu wao kwa kutoa huduma kwa wananchi ndio kazi yao.

“Kazi yetu ni kuwahudumia wananchi ukiwasikiliza mambo yote waliyoyasema hapa wala hayahitaji bajeti bali ni kusikilizwa na watu wanaojitoa kwa wenzao hivyo nakuomba mkurugenzi na wenzako haya yote tuliyo yabaini nendeni mkayafanyie kazi na jumanne mniletee mrejesho wa utekelezaji wake” alisema Serukamba.

Alisema hakuitisha kikao hicho kwa lengo la kusikiliza kero zao tu bali ni kuwasikiliza na kuzitatua kero hizo na kuwa zile ambazo hawatakuwa na uwezo nazo watazipeleka ngazi nyingine ya juu kwa ajili ya hatua nyingine na zile ambazo zipo ndani ya uwezo wao ni lazima wazitatue.

Serukamba alisema changamoto kubwa iliyojitokeza kutoka kwa wananchi hao ni ya migogoro ya arddhi ambapo alimuomba kamishna wa ardhi na timu yake kujipanga kwa ajili ya kutatua jambo hilo.

Alimwagiza kaimu mkurugenzi wa wilaya hiyo kusimamia haki ya wafanyakazi na alimuomba Afisa Utumishi kusimamia utekelezaji wa kazi kwa kufuata sheria na utaratibu uliowekwa wakati wa kutekeleza wajibu wao.

Alisema wananchi hao wanatarajia kusaidiwa changamoto walizo nazo ambazo sio kubwa lakini wao wamekuwa wakitumia muda mwingi  kwenda kusimamia masuala ya kujenga barabara, madarasa lakini yale yanayowahusu watu hawashughuliki nayo.

“Mimi naamini watu hawa ambao changamoto zao hamzifanyii kazi ndio waliyoiweka Serikali iliyopo madarakani hivyo wangetamani kuona inatatua matatizo yao kupitia sisi tuliopewa dhamana ya kufanya hivyo baada ya kupekwa kufanya kazi ya kuwatumikia” alisema Serukamba.

Serukamba aliwaomba viongozi na watumishi wa wilaya hiyo kubadilisha mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea badala yake uwe mfumo wa kutatua changamoto za wananchi ambapo alimtaka mkuu wa wilaya hiyo kwenda kwenye Tarafa, Kata na maeneo mengine kusikiliza changamoto za wananchi na kuwa ile tabia ya kufanya kazi bora iende wakati wake umepita.

Aliwatka wafanyakazi wa halmashauri hiyo kujiuliza wanapokwenda kazini kuanzia jumatatu hadi ijumaa kujiuliza wamefanya nini na wamewahudumia wakina nani na akaomba wawe na lugha nzuri kwa wanaowatumikia.

Aidha Serukamba aliagiza Halmashauri ya Wilaya ya Iramba kuhakikisha inaondoa takataka zote zilizopo kwenye maguba yaliyopo kwenye makazi ya watu na maeneo mengine ambapo alitoa ahadi ya kurudi kukagua maeneo hayo na wasije wakaelewana vibaya pindi atakapozikuta takataka hizo.

Baadhi ya kero zilizotolewa katika kikao hicho ni jinsi gani ya kulipwa fidia kwa mtu aliyeshambuliwa na tembo kero iliyotolewa na Hamphrey Philemon, Walimu wa Wilaya za Mkalama na Iramba ambao wana kidai chama cha akiba na mikopo cha Chamwai fedha zao waliochangia ili ziweze kuwasasidia baada ya kustaafu kero iliyowasilishwa na Mwalimu Zefania Makala, Uharibifu wa mazingira iliyotolewa na Janeth Mwendo, kutolipwa fidia kwa mmiliki wa eneo ilipojengwa Shule ya Sekondari ya New Kiomboi iliyotolewa na Stephano Juma.

Kero zingine ilikuwa ni malalamiko yaliyotolewa na Paul Alphonce aliyedai kulipia kupata huduma ya maji akiwa na wenzake  ambao walitoa Sh.150,000 kila mmoja lakini hadi leo hii bado hawajafkishiwa huduma hiyo, kero nyingine ilitolewa na Mjasiriamali Anna Kizinga ambaye aliomba kupunguzwa kwa ushuru katika minada kutokana na biashara zao kuto nunuliwa, kero nyingine ilikuwa ni kukithiri kwa uchafu katika baadhi ya maguba yaliyopo mjini Kiomboi iliyotolewa na Zabron Malecela, kero ya kupelekewa mbolea ya ruzuku ambayo wakulima hawajaizoea iliyotolewa na Elia Zefania.

Kero nyingine iliyotolewa ni iliyowahusu watu wenye ulemavu wilayani humo ambao wanaidai halmashauri ya wilaya hiyo fedha za kujikimu walipokwenda kwenye maadhimishoya siku ya watu wenye ulemavu.

Kero nyingine iliyotolewa ilitolewa na Frank Nkundi ambaye anadai fidia ya kupata ajali akiwa kazini na Michael Juma ambaye anaidai halmashauri hiyo Sh, Milioni 1.3 kama kiinua mgongo baada ya kustaafu.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Taasisi za Serikali mkoani hapa, pamoja na wakuu wa idara ili kuzisikiliza na kuzitafutia ufumbuzi ambapo kikao kama hicho kitafanyika katika wilaya zote ambapo leo Januari 18, 2023  kitafanyika Wilaya ya Mkalama.

Mkuu wa Wilaya ya Iramba,Suleiman Mwenda, akizungumzia malalamiko ya walimu 162 wanao kidai Chama cha kuweka na kukopa cha Chamwai.
Taswira ya kikao cha kupokea kero za wananchi kilichoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba.
Elizabeth Msengi akitoa kero yake inayohusu ardhi.
Afisa Ardhi Wilaya ya Iramba Bwana Magesa akitoa maelezo baada ya kutolewa kwa kero za migogoro ya ardhi kwa mkuu wa mkoa.
Mwalimu Zefania Makala akielezea kero ya madai ya fedha zao dhidi ya chama cha Chamwai.
Kero za wananchi zikiandikwa.
Baadhi ya walimu wanaokidai chama cha Chamwai wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kueleza kero yao kwa mkuu wa mkoa.
Beatrice Jonathan akitoa kero yake.
Agustino Makute akitoa kero zake mbele ya mkuu wa mkoa.
Paul Alphonce akielezea kero yake ya kutopelekewa huduma ya maji licha ya yeyena wenzake 19 kulipia Sh.150,000.
Philemon Hamphrey akiomba kujua malipo ya fidia kwa mtu aliyejeruhiwa na tembo.
Mjasiriamali Anna Kizinga akiomba ushuru upunguzwe.
Zabron Malecela akizungumzia kero ya kukithiri kwa takataka katika maguba.
Elia Zefania akizungumzia changamoto mbalimbali.
Mwenyekiti wa Watu wenye ulemavu Wilaya ya Iramba, Athuman Kingu akizungumzia malipo ya fedha zao za kujikimu baada ya kwenda kwenye maadhimisho ya siku ya walemavu duniani.