Sunday, March 17, 2024

UBALOZI WA UHOLANZI, SERIKALI WAZINDUA KITABU CHA MWONGOZO WA ULIMAJI VIAZI

Kansela wa kilimo wa Ubalozi wa Uholanzi nchini , Bw Bart Pauwels (mwanzo kulia)pamoja na anayemfuata mwenye miwani ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) Dr Patrick Ngwediagi na Balozi wa Uholanzi hapa nchini , Wiebede Boer katikati na kulia kwa Balozi ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) Bw , Geoffrey Kirenga na mwisho Bw Bob Shuma mdau wa kilimo wakionyesha kitabu cha mwongozo wa kilimo cha viazi ambacho kilizunduliwa.

...................................... 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

TANZANIA kwa kushirikiana na Ubalozi wa Uholanzi wamezindua kitabu cha mwongozo wa usajili wa aina za mbegu za viazi kwa lengo la kuimarisha ustawi wa kilimo cha viazi na usalama wa chakula hapa nchini.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho wiki iliyopita jijini Dar es Salaam,Balozi wa Ufalme wa Uholanzi hapa nchini, Wiebe de Boer aliwaambia viongozi waalikwa na wageni mbalimbali kuwa hiyo ilikuwa hatua kubwa katika safari yao ya kuimarisha sekta na kilimo cha viazi hapa nchini.

"Safari ambayo imechangiwa na ushirikiano wa miaka kumi kati ya Tanzania na Uholanzi,katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, ushirikiano huu umewavutia wakulima wa viazi wa Uholanzi kusajili aina zao za viazi nchini Tanzania," aliongeza.

Alisisitiza kwamba si hivyo tu bali pia kuvutia uwekezaji kuongeza na kupanua mnyororo wa thamani wa viazi na sasa wanatambua kwamba viazi kama chakula kikuu cha kuhakikisha usalama wa chakula, kuzalisha kipato kwa wakulima na kutengeneza fursa za ajira.

Balozi Boer alisema kuwa ufanisi na tija katika kilimo cha viazi unahitaji matumizi ya mbegubora sambamba na kanuni bora za kilimo zilizochochea ukuaji wa sekta ya kilimo.

Alisema nchini Uholanzi kuna aina zaidi ya 250 za viazi zinazolimwa kwa matumizi mbalimbali,ikiwa ni pamoja na kuchemsha, kukaanga, krisps, kuoka, kuzalisha mbegu na usindikaji wa wanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania(TOSCI), Dk Patrick Ngwediagi alisema kitabu hicho kitatumika kama mwongozo kwa wagunduzi wa mbegu za viazi , wakulima na wawekezaji wa ndani na nje ya nchini wanaovutiwa kuwekeza kwenye sekta ya viazi hapa nchini.

"Kwa kweli leo ni hatua muhimu kwa sababu kitabu hiki kitasaidia wakulima kuwa na taarifa za kutosha kuhusu sera, sheria zinazosimamia sekta ya kilimo pamoja na kuangalia changamoto na fursa zilizopo nchini kwenye kilimo cha viazi," alisistiza Dr Ngwediagi.

Dk Ngwediagi alisema kuwa kitabu hicho kitawapa wakulima na wagunduzi hatua kwa hatuajinsi ya kusajili mbegu zao nchini na mchakato wa kuzalisha mbegu bora ili kuhakikisha ukuaji wa sekta hiyo.

“Jinsi hizi zote ni taratibu za hapa nchini katika kuimarisha ukuaji wa sekta na mbegu zote lazima zisajiliwe kwenye Daftari la Taifa la mbegu katika juhudi za serikali kuimarisha usalama wa vyakula kwa watanzania,” aliongeza.

Mshauri wa Kilimo wa Ubalozi wa Uholanzi, Bart Pauwels alisema kuwa Ubalozi wa Uholanzi hpa nchini utaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na sekta binafsi kwa ujumla ili kuhakikisha inakuza ukuaji wa sekta ya viazi.

“Kilimo bora ni injini ya ukuaji wa sekta, Ubalozi wa Uholanzi utaendelea kutoa msaada wasekta hii kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha kilimo kwa kuleta piateknoloji na ujuzi mwingine wa kitaalamu,” aliongeza.

Kwa miaka 10 sasa, Tanzania na Uholanzi zimekuwa na ushirikiano mzuri katika sekta ya viazi.Kupitia ushirikiano huu, jumla ya aina 16 za viazi zilisajiliwa na kati ya hizo 12 ni aina za Kiholanzi zinazotoa mavuno mengi, kustahimili ukame na wadudu.

Maendeleo haya yalivutia biashara zaidi kwenye mnyororo wa viazi kutoka kwa ufugaji, kukua hadi usindikaji. Ili kusaidia sekta hii zaidi, Ubalozi uliiwezesha TOSCI kutoa mwongozo wa hatua kwa hatua kuhusu taratibu za kuchukua iwapo mwekezaji anataka kusajili aina ya viazi nchini Tanzania kwa ajili ya biashara. Kitabu hiki kimeidhinishwa na TOSCI kwa matumizi ya Tanzania.

ujumbe wa wafugaji 30 wa viazi vya Uholanzi, watafiti, wakulima wanaojihusisha na uendelezaji wa aina za viazi hivyo wametembelea Tanzania. Lengo ni kufahamiana na mahitaji ya soko, upendeleo na kupokea maoni kutoka kwa wakulima. Taarifa hizi zitatumika katikautafiti na ukuzaji wa aina mpya kwa Tanzania.

No comments:

Post a Comment